Balisidya
(1987) anaeleza kuwa fasihi ya Kiswahili ni fasihi yoyote ambayo imeelezwa kwa
Kiswahili ikiwa na lengo la kuwasilisha yasemwayo katika hadhira kubwa zaidi
kuliko familia, koo, au kabila fulani na imeandikwa na wale wanaozungumza
Kiswahili iwe ni lugha yao ya awali au lugha ya pili.
Mulokozi
(1996) akimnukuu Mazrui na Syambo (1992) wanaeleza kuwa fasihi ya Kiswahili ni
ile iliyoandikwa kwa Kiswahili tu, iwapo inazungumzia utamaduni wa Kiswahili au
utamaduni mwingineo. Maadamu fasihi hiyo imetumia lugha ya Kiswahili na
imefuata mbinu za ufasaha wa lugha hiyo.
Kwa
ujumla fasihi ya Kiswahili ni fasihi ambayo imeandikwa kwa lugha ya Kiswahili
na inazungumzia utamaduni wa waswahili na mwingineo na inaweza kuandikwa na
wazawa wa lugha ya Kiswahili au mtu yeyote mwenye ujuzi wa lugha ya kiswahili.
Pia fasihi linganishi imefasiliwa na wataalamu mbalimbali kama ifauatavyo;
Remak
(1971) anafasili fasihi linganishi kuwa ni uwanja wa kifasihi unaohusika na
uchunguzi na mahusiano ya kifasihi nje ya mipaka ya nchi moja, pia kati ya
fasihi na fani nyinginezo. Katika fasili hii huonyesha kuwa fasihi linganishi
hujishughulisha na fasihi na fani nyingine kama tafsiri, sosholojia na
saikolojia.
Wamitila
(2003) anaeleza kuwa fasihi linganishi inahusu uchambuzi wa maandishi ya wakati
mmoja na aina moja na katika lugha mbalimbali kwa nia ya kumiliki sifa
zinazoyahusisha kama athari, vyanzo, sifa zinazofanana na tofauti za
kiutamaduni. Anaendelea kueleza kuwa inawezekana kufanya hivi kwa nia ya
kuangalia matapo mbalimbali, maendeleo hata nadharia za kiuhakiki.
Kwa
ujumla fasihi linganishi ni taaluma ya usomaji wa matini za tamaduni tofauti au
utamaduni wa aina moja ili kubaini mazingira ambayo kazi hizo huingiliana na
kutofautiana. Vilevile nadharia imefasiliwa na wataalam mbalimbali kama vile;
Massamba
(2009) anafasili nadharia kuwa ni taratibu, kanuni na misingi ambayo imejengwa
katika muundo wa kimawazo kwa madhumuni
ya kutumiwa kama kielelezo cha kuelezea jambo. Fasili hii inathibitisha kuwa
nadharia inahusisha mawazo ambayo huwekwa kwa mpangilio maalumu ili kuelezea
jambo fulani.
Amini
(2005) anaeleza kuwa nadharia ni jumla ya mambo yote ambayo mtafiti amekusudia
kuelezea, kuchambua, kuelewa au hata kutabiri jambo fulani kwa utaratibu
maalumu.
Kwa
ujumla nadharia ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza,
kutatua au kutekeleza jambo fulani. Vilevile dhana za historia, itikadi na
utamaduni zimefasiliwa kama ifuatavyo;
Ndallu
na wenzake (2014) wanafasili historia kuwa ni elimu ya mambo yaliyopita. Katika
fasili hii wamejikita kueleza kuwa historia hujishughulisha na mambo mbalimbali
ya kale au yaliyopita. Hivyo basi historia ni kujifunza mambo yaliyopita,
yaliyopo na kutabiri yajayo.
Ndallu
na wenzake (2014) wanafasili utamaduni kuwa ni desturi fulani za maisha
zilizotolewa; mila na ustaarabu. Katika fasili hii wanadai kuwa utamaduni ni
lazima uhusishe desturi, mila na ustaarabu. Hivyo basi utamaduni ni jinsi binadamu
anavyokabili maisha katika mazingira yake. Hiyo hujumuisha ujuzi, imani Sanaa,
maadili sheria na desturi ambavyo mtu anajipatia kama mwanajamii.
Ndallu
na wenzake (2014) wanafasili itikadi kuwa ni mambo ya kidini ambayo muumini
anapaswa kuyakubali na kuyaheshimu kuwa ni kweli. Katika fasili hii
wanasisitiza kuwa itikadi hujishughulisha zaidi na masuala ya kidini yaani
imani ya mtu ambayo anaamini. Hivyobasi itikadi ni mkusanyiko wa imani
unaoshirikiwa na kikundi cha watu fulani. Baada ya kufafanu dhana muhimu
zilizojitokeza kwenye swali letu, zifuatazo ni nadharia za fasihi linganishi na
namna zilivyoathiriwa na mielekeo ya kihistoria, kitamaduni na kiitikadi.
Nadharia
ya ubadilikaji taratibu, ni nadharia ya kiutandawzi iliyoasisiwa na Charles Darwin
(1809-1914) katika andiko lake la Orgin
of species lililochapishwa mwaka 1959. Charles Darwin ni mwana baiolojia
ambaye alifanya utafiti kuhusu mabadiliko ya viumbe hai ambao waliishi miaka ya
mamillioni iliyopita. Katika utafiti wake aliona njia rahisi ya kubaini
chimbuko la binadamu ni kulinganisha sifa za kibiolojia baina ya viumbe hai hao.
Aligundua kwamba, kama viumbe hai wanasifa zinazofanana basi viumbe hai hao
wanatoka katika asili moja na wakapitia mabadiliko mbali mbali hadi kufikia
hali walionayo sasa. Pia anaeleza kuwa viumbe wanaoendelea kuishi ni kwasababu
wameweza kumudu mapambano dhidi ya mazingira na jambo hili aliliita Survival for the fittest. Mawazo ya utafiti wa Darwin yalishadidiwa na wanazuoni mbalimbali
kama vile Edward Burnet Taylor, James Cierge Frazer, John Roscoe, Edward Smith,
watafiti hawa walikuwa wanachunguza utamaduni wa binadamu. Katika utafiti wao
walikusanya simulizi kutoka katika jamii mbalimbali za Afrika, Asia na America
ambapo baada ya ukusanyaji wa simulizi hizo waligundua kuwa zilikuwa na ufanano
wa kimaudhui. Wanaubadilikaji taratibu wanaamini kuwa masimulizi tuliyonayo
sasa yanaasili moja isipokuwa yamekuwa yakibadilika kutokana na wakati, pia wanaamini
kuwa viumbe wote wametoka kwenye asili moja hivyo wanaakili sawa.
Ubora
wa nadharia hii ni kuwa msingi wa nadharia nyingine zilizofuatia lakini pia
imesaidia kueleza asili ya masimulizi tulionayo sasa, mfano ngano. Udhaifu wa
nadharia hii nikudai kuwa fasihi ya kiafrika ni masalia ya fasihi
zilizotangula, pia walizingatia kipengele cha maudhui na kupuuza kipengele cha
fani lakini pia walikita zaidi kueleza kufanana kwa maudhui ya masimulizi bila
kuchunguza tofauti. Nadharia hii imethiriwa na mielekeo ya kihistoria, na
kiitikadi. Kwa kuanza na mwelekeo wa kihistoria;
Nadharia
hii imeathiriwa na mwelekeo wa kihistoria kwani historia ya viumbe hai
inahusiana na mabadiliko mbalimbali ambayo wanyama wanayapitia na kuihusianisha
na fasihi. Kwani kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kihistoria yanayopatikana
katika jamii vivyohivyo fasihi nayo imekuwa ikipitia vipindi mbalimbali vya
mabadiliko ya kihistoria. Mathalani kazi mbalimbali za kipindi cha ujima ni
tofauti na fasihi ya kipindi cha utumwa na ubepari.
Pia
nadharia hii imeathiriwa na mwelekeo wa kiitikadi kwani waasisi wa nadharia hii
walikuwa wakiamini kuwa bara la Afrika ni giza na halina maendeleo kabisa na
ndio maana walidai kuwa fasihi ilitoka kwao na kuja kwa waafrika. Hivyo basi
itikadi hii waliyokuwa nayo si ya kweli kwani Afrika walikuwa na fasihi hata
kabla ya ujio wa wageni.
Nadharia
ya msambao, nadharia hii imeasisiwa na Jacob na Wilhem Grimm, baadae mawazo yao
yaliendelezwa na Maxmuller pamoja na Stere Thompson kutoka marekani. Wataalam
hawa wanaamini kuwa chimbuko la fasihi ni moja lakini kutokana na maingiliano
ya kijamii ndio yaliyosababisha kusambaa kwa ngano hasa kutoka jamii
zilizostaraabika (Ulaya) kuja katika jamii zisizostaarabika (Afrika). Okpewho
(1992) anadai kuwa wanamsambao walijishughulisha na kuhusisha ngano za jamii
mbalimbali na kugundua kuwa ngano hizo zinaufanano unaokaribiana sana.
Uhusiano
huu unahusishwa na kipindi cha kihistoria ambacho kulikuwa na mawasiliano baina
ya jamii moja na nyingine. Katika utafiti wao wanamsambao waligawanyika katika
makundi mawili, kundi la kwanza ni wale waliotoka katika shule ya India, kundi
hili liliongozwa na Jacob na Wilhelm ambapo walikusanya hadithi mbalimbali
katoka Ujerumani na barani Ulaya na kugundua kuwa ngano hizi zinafanana. Walihitimisha
kuwa ngano za ulaya zimeonekana na rangi ya nasaba bora iliyopata kuishi huko
kati ya Kaskazini na Asia rangi ya nasaba bora ni lugha zote za ulaya
zinazohusishwa na rangi hiyo. Hivyo waligundua kuwa ngano zilikuwa zinasambaa
na makundi ya wahamiaji. Kundi la pili ni la shule ya kifini shule hii
ilianzishwa na Elias Lonnrot ambaye mwaka 1825 alianza kukusanya ngano za
mashujaa katika nchi ya Fineland, akapitia maudhui yanayohusiana na akaziweka
pamoja. Ubora wa nadharia hii ni;
Kuathiriana
kwa jamii kunatokana na mwingiliano baina ya jamii hizo, ambapo zimeingiliana
katika shughuli mbalimbali kama vile biashara, ufugaji, kilimo, uwindaji na
kazi mbalimbali za kijamii.
Vilevile
nadharia hii inaudhaifu ufuatao, kwanza wanamsambao wanaona kuwa fasihi ya
kiafrika ni duni kutokana na kuiga kutoka fasihi ya kiulaya lakini pia walizingatia
ufananano na kupuuza utofauti wa jamii na umuhimu wa tofauti hizo.
Nadharia
hii imeathiriwa na mwelekeo wa kiutamaduni, kiitikadi na kihistoria, kwa kuanza
na mwelekeo wa kiutamaduni nadharia hii imeathiriwa na mwelekeo huu kwani jamii
mbili zinapoingiliana jamii moja huiga baadhi ya utamaduni wa jamii nyingine ka.
Lakini pia nadharia hii imeathiriwa na mwelekeo wa kiitikadi kwani waasisi wa
nadharia hii wanadai kuwa ngano tulizo nazo sasa zimetoka kwenye jamii
zilizostarabika kuja katika jamii ambazo hazijastarabika. Walitoa madai hayo
kulingana na itikadi zao walizokuwa nazo kuhusu bara la Afrika kuwa ni bara
ambalo halijastarabika vilevile nadharia hii imeathiriwa na mwelekeo wa
kihistoria kwani wanaeleza kuwa jamii za Afrika na Ulaya ziliwahi kuingilia na
kupelekea utamaduni wa Ulaya kusambaa katika jamii za Afrika kutokana na
uhamiaji.
Nadharia
ya kisosholojia, TUKI (2004) wanaeleza kuwa sosholojia ni taaluma ya kisayansi
inayohusu asili na maendeleo ya jamii pamoja na tabia zake. Nadharia hii
imegawanyika katika mihimili mikuu miwili ambayo ni umahususi na mkazo katika
utendaji.
Kwa kuanza na umahususi nadharia hii ilikuwa mahususi zaidi kuliko
nadharia zilizotangulia badala ya kujikita katika taaluma ya Sanaa jadi kwa
ujumla (maumbile ya mwanadamu na utamaduni wake) kama walivyofanya wananadharia
wa zamani. Nadharia hii ilijikita katika jamii pekeake baada ya kugundua dosari
zilizofanywa hapo kabla, dosari hizo ni kama kutoa matamko ya juu juu na
kijumla zaidi. Kwa hiyo wanasosholojia waliazimia kuchunguza kila jamii kwa
wakati na nafasi yake kwa kurekodi kila kilichopatikana katika jamii husika.
Miongoni mwa wataalamu waliochunguza nadharia hii ni kama Brownslow Malinowisky
na Radcliffe – Brown (uingereza), walichunguza jamii mbalimbali katika visiwa
vya Trobriand na Andaman. Mtalam mwingine ni Franz Boas (Marekani) alichunguza
jamii za wenyeji wa Marekani.
Wataalam wengine kutoka Afrika ni pamoja na E.E.
Evans-Pritchard alifanya utafiti katika katika jamii ya Nuer (Sudan), William
Boscom katika jamii ya Yoruba (Nigeria) na Marcel Griaule katika jamii ya Dogon
(Burkina Faso) watalamu hawa waaliongozwa na mawazo ya kiubadilikaji taratibu.
Muhimili wa pili ni mkazo katika utendaji, Tofauti na ilivyokuwa kwa
wananadharia wa mwanzo ambao hawakupendelea kuangalia utendekaji wa fasihi
simulizi, wanasosholojia waliweka msisitizo katika kuchunguza utendaji wa fani
mbalimbali za fasihi simulizi. Kutokana na msisitizo huo imebainika kuwa fanani
wa kazi ya fasihi wanaujuzi na ustadi wa kiutendaji katika sanaa husika na jambo
hili limetuwezesha kuelewa kuwa katika fasihi simulizi kuna kipengele cha
utendaji vilevile wamedokeza sifa za ndani za fasihi simulizi ya Kiafrika, na
hiyo wao wanaona kuwa ili kujua fasihi ya kiafrika ni vyema kuangalia jamii na utendaji
wa kazi husika.
Ubora
wa nadharia hii ni kuona upekee wa fasihi simulizi ya kiafrika na kuona ilikuwa
na dhima katika jamii mahususi. Upungufu wake ni kuwa wameshindwa kuchambua sanaa
kubwa iliyomo kwenye matini chanzi nyingi za fasihi simulizi walizochunguza.
Nadharia
hii imeathiriwa na mielekeo ya kiitikadi, kiutamaduni na kihistoria. Kwa kuanza
na mwelekeo wa kiitikadi, nadharia hii imeathiriwa na itikadi ambapo waasisi wa
nadharia hii wanaamini kuwa kila jamii ni vema ikachunguzwa pekeake ili kuweza
kujua mambo mbalimbali ambayo yanapatikana katika jamii hiyo na kuitofautisha
na jamii nyingine. Vilevile kwa upande wa mwelekeo wa kiutamaduni waasisi wa
nadharia hii wanaona kuwa jamii zinatofautiana kiutamaduni hivyo basi hata
utendaji wake ni tofauti baina ya jamii moja na jamii nyingine. Pia katika
historia wanadai kuwa jamii zinapochunguzwa kwa wakati tofautitofauti huonyesha
utofauti uliopo baina ya jamii hizo katikq kipindi fulani cha historia na
kipindi kingine.
Nadharia
ya utaifa, nadharia hii iliasisiwa na S. Adeboye, Baborola, Daniel P. Kunene na
J. P Clark, ilizuka kwenye vuguvugu la kudai uhuru barani Afrika, wanautaifa
wadai kuwa wananadharia wa nadharia ya ulimwengu hawakuwa na uelewa wa kutosha
kuhusu lugha za kiafrika, kwa kiwango kikubwa waliathiriwa na dhana za kikoloni
na upendeleo wa kibepari kuwa Afrika ni bara la giza na washenzi wasiokuwa na
aina yoyote ya ustaarabu na walistahili kustarabishwa na wazungu kupitia mlango
wa ukoloni. Waasisi wa nadharia hii wanadai kuwa ni kosa kubwa kufanya utafiti
bila kuwahusisha wahusika wa eneo la utafiti hivyo ili kufahamu vyema historia
ya fasihi simulizi ya kiafrika ni lazima kuhusisha wataalamu na wanazuoni wa
taifa au jamii hiyo kwasababu wataalam hawa ndio wenye ujuzi wa lugha,
utamaduni na historia ya jamii hiyo. Kwa ujumla wanautaifa wanamini kuwa
chimbuko la fasihi simulizi ya kiafrika inapatikana ndani ya jamii ya kiafrika na
ili kuchunguza fasihi ya jamii husika ni sharti watalaamu na wanazuoni wajamii
hiyo wahusishwe. Ubora wa nadharia ni kuhusisha wazawa wa jamii husika.
Nadharia
hii imeathiriwa na mielekeo ya kiitikadi, kiutamaduni na kihistoria. Kwa kuanza
na mwelekeo wa kiitikadi waasisi wa nadharia hii wanadai kuwa wakoloni walipokuja
Afrika walikuwa na itikadi yao ya kibepari hivyo ilipelekea wao kutoa mawazo kuwa
Afrika ni bara duni. Kwa upande wa kiutamaduni waasisi wa nadharia hii
walisisitiza kuwa ni vema kuwashirikisha wataalamu na wanazuoni wa jamii husika
kwani wao ndio wanajua lugha husika kwa ufasaha zaidi. Vilevile katika upande
wa historia waasisi wanadai kuwa ni vema kuwa husisha wataalamu ili kuweza
kufahamu vizuri historia ya jamii husika.
Nadharia
hulutishi, nadharia hii iliasisiwa na wanazuoni wa kiafrika wenye mtazamo kuwa
hata wageni wamechangia sana kukuza taaluma ya fasihi ya kiafrika. Wananadharia
hawa wanaona kuwa fasihi ya kigeni na kijadi zimeathiriana na kuingiliana.
Miongoni mwa waasisi na watetezi wa nadharia hii ni pamoja na M.M Mulokozi,
Johnson, Ngugi Wa Thiong’o, Chinua Achebe, Frantz Fanon, Abiola Irele. Hivyo
historia ya fasihi simulizi ya kiafrika inaweza kujadiliwa kwa kuhusisha au
kuchanganya mawazo ya wataalamu wote wa kigeni na kijadi. Wao walianza kuandika
kazi ya fasihi ambazo zinajaribu kuhusianisha ujadi wa waafrika na usasa
unaotokana na ujio wa wageni. Mathalani Chinua Achebe katika vitabu vyake vya Things Fall Apart na No Longer at Ease na Ngugi Wa Thiong’o katika The Grain of Wheat. Mtazamo huu umekuwa maarufu na kwa kiasi
kikubwa na kwa kiasi kikubwa unatumika.
Nadharia
hii imeathiriwa na mielekeo ya kiitikadi, kiutamaduni na kihistoria. Kwa kuanza
na mwelekeo wa kiitikadi waasisi wa nadharia hii wanaamini kuwa wataalamu wote
yaani wageni na wenyeji wanamchango mkubwa katika kuiendeleza fasihi. Pia
katika utamaduni wanaeleza kuwa fasihi ya kigeni na fasihi ya kijadi zimeathiriana,
hivyo jamii mbili zinapoingiliana jamii moja huchota vipengele vya kiutamaduni
kutoka katika jamii nyingine. Vilevile katika historia wanaeleza kuwa historia
inaweza kuelezewa kwa kuzingatia mwingiliano wa jamii hizi.
Kwa
ujumla nadharia za fasihi linganishi zinamchango mkubwa katika maendeleo ya
fasihi ya Kiswahili kwani husaidia kujua historia ya fasihi tuliyonayo sasa,
pia huwaongoza watafiti wakazi mbalimbali za fasihi pindi wanapofanya utafiti
unaohusiana na fasihi simulizi na fasihi andishi, vilevile vigumu kuelezea
nadharia za fasihi linganishi bila kuhusianisha na mielekeo ya kihistoria,
kiitikadi na kiutamaduni kwani mielekeo hii imeathiri mno nadharia za fasihi
linganishi.
MAREJELEO.
Balisidya, N. M. “Adopted or adapted to Neo Swahili Oral Literature in
Tanzania” katika Kiswahili Vol. 54/1 na
54/2 (1987), Dar es Salaam: TUKI.
Massamba, D. P. D (2009) Kamusi
ya Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.
Mulokozi, M. M. (1996). Fasihi
ya Kiswahili. Dar es salaam. DUP.
Ndallu,
A. E, Babusa, H na Mirikau, S.A (2014). Kamusi
teule ya Kiswahili. Nairobi- Kenya:
Prinywell Industries Limited.
Okpewho,
I. (1992). African Oral Literature. Backgrounds,
Character and Contiunity. USA:
Indiana
University Press.
Remak,
H. H. (1971). Comperative Literature: Its
definition and F unction. Carbondale: Southern
Illinois.
TUKI, (2004) “Kamusi ya Kiswahili sanifu”. Dar es
salaam; Oxford University Press.
Wamitila,
K. W. (2003), Kamusi ya Fasihi na Nadharia. Focus Publications Ltd.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com