Flower
Flower

Friday, April 19, 2019

UHARIRI NA MAJUKUMU YA MHARIRI

Kwa mujibu wa Omari (1995), anaeleza uhariri ni utengenezaji wa maandishi yoyote yale kwa kuyasahihisha, kuyalekebisha, na kuyapanga ili hatimaye yaweze kuchapishwa katika gazeti, au kitabu, au makala katika majarida. Kazi hii ya uhariri inafanyika katika viwango mbalimbali kutegemeana na aina ya kazi inayohusika. Pia, TUKI (2013), wanafasili kuwa uhariri ni kazi ya kusoma, kusahihisha na kusanifu miswada ya makala, vitabu.

Mulokozi (1982), anaeleza uhariri ni mchakato wa kugundua, kupata, kuteua, kurekebisha na kuunda mswada kwajili ya uchapishaji kwa niaba ya mwandishi au mchapishaji. Uhariri unahusisha kupanga, kukamisheni, kuanda mikataba, kuanda matini, sanjari na wandishi, wachapishaji na wachoraji.
Mhariri wa jumla ni Yule mhariri anayeshughulika na menejimenti au kuratibu shughuli uchapishaji, kuandaa vitabu, kukamisheni waandi wa miswada na utoji wa vitabu.  Pia, mhariri wa matini ana jukumu la kuhakikisha kuwa maudhui ya mwandishi yanamfikia msomaji kwa njia inayoridhisha.

TUKI (2013), wanafasili dhana ya mhariri kuwa ni mtu anayefanya kazi ya kusoma, kusahihisha, na kusanifu miswada kama vile makala au vitabu.

Kwa mujibu Einsohn (2006), anabainisha masharti ambayo anatakiwa kuzingatia mhariri wakati wa kuhariri; Anatakiwa asiharibu mantiki ya mswada, asionyeshe makosa ambayo hayapo katika mswada, pia asiharibu maana ya mswada ambayo imekusudiwa na mwandishi, na pia asiwe nje ya muda ambao anatakiwa kufanya kazi yake.

Kwa mujibu wa Mallya (1993), ameeleza majukumu ya mhariri wa jumla anavyoweza kuufanya mswada kuwa kitabu kama ifuatavyo.

Mhariri wa jumla ana jukumu la kuufanya mswada kuwa kitabu kwa kutathmini mswada, mhariri wa jumla wanaweza kutathmini mswada yeye mwenyewe au akawapata wasomaji wengine mswada na kupokea ushauri kwa wasomaji wake.  Kwahiyo mhariri wa jumla huweza kuwapa wasomaji wengine wa mswada ambao ni wataalamu wanaoweza kutathmini mswada huo na kutoa tathmini ya kutosha juu ya mswada huo, kama unaweza kufaa kuwa kitabu au la. Mhariri wa jumla huweza kuwapa mswada wasomaji ambao wanauelewa na kile kinachohusiana na ule mswada, na wasomaji hao wanaweza kuwa wa ndani ya kampuni au nje ya kampuni, lengo kuu la kuwapa wasomaji hao mswada ni kuweza kutoa tathmini au mapendekezo juu ya huo mswada kama unafaa kuwa kitabu au la.
Mhariri wa jumla ana jukumu la kuufanya mswada kuwa kitabu kwa kufanya uhariri wa undani, hii inahusika na kukata au kuongeza mambo mengi katika mswada, kupanga upya mtiririko wa mswada, na kuhakikisha kuwa mambo yameelezwa katika lugha ya wazi na fasaha. Ni kama kuandika kitabu upya. Hivyo basi mhariri wa jumla anatakiwa kuangalia sintaksia, maumbo ya maneno, na usahihi kiujumla katika mswada wake.

Mhariri wa jumla ana jukumu la kuufanya mswada kuwa kitabu kwa kutayarisha mswada kwa uchapaji, hapa mhariri huchambua na kumuonyesha mchapaji sehemu kadhaa za mswada na namna anavyota zionekane katika maandishi kutokana na umuhumu wake. Miongoni mwa vitu anavyohitaji vionekane katika uchapaji yaweza kuwa ni picha, jalada, fonti kulingana na walengwa au wasomaji wa kitabu.  Kwahiyo mhariri wa jumla anakuwa ni kiungo kati ya mchapishaji, msanifu na mchapaji.

Kwa mujibu wa Einsohn (2006), pia mhariri wa matini ana jukumu la kuufanya mswada kuwa kitabu kama ifuatavyo, kwa

Mhariri wa matini ana jukumu la kuufanya mswada kuwa kitabu kwa kunyoosha lugha iliyo katika mswada, hasa pale mwandishi asipotumia lugha ya mvuto na inayoendana na wasomaji. Mhariri ana jukumu hilo la kunyoosha lugha ili iendane na wasomaji waliokusudiwa au walengwa, pia mhariri ana jukumu la kurekebisha mswada pale mwandishi anapokuwa ametumia ujuzi mkubwa katika kazi yake kuliko wasomaji lengwa. Mhariri ana jukumu la kuhariri kazi hiyo ili iendane na wasomaji. Vilevile mhariri anatakiwa kusoma neno bada ya neno heri baada ya heri katika kuhariri mswada ili ujekuwa kitabu.

Mhariri wa matini ana jukumu la kuufanya mswada kuwa kitabu kwa kuhusianisha na kuangalia uwiano wa vipengele vilivyopo katika mswada, mathalani mswada unaweza kuwa ni mfupi na mwepesi lakini mhariri anatakiwa aangalie uwiano wa vipengele vilivyopo katika mswada huo, hasa kwa kuzingatia vipengele kama vile kupendekeza vielelezo vikae mahali gani, kuangalia vielelezo kama vinaendana na maudhui, na pia kuangalia kile kilichopo katika yaliyomo kama kinaendana na mswada.

Mhariri wa matini ana jukumu la kuufanya mswada kuwa kitabu kwa kuangalia ushikamani mzuri kati ya fani na maudhui katika mswada kulingana na walengwa, kwahiyo mhariri ana kazi ya kuangalia yale maudhui yaliyokusudiwa na mwandishi yanaendana na walengwa walio kusudiwa kuwafikia, na kuangalia fani iliyotumika ina kiwango sawa na walengwa au la. Kwa mfano fani na maudhui ya vitabu vya watoto ni tofauti na vitabu vya wanafunzi wa chuo kikuu.
Pia, mhariri wa matini ana jukumu la kuufanya mswada kuwa kitabu kwa kumkumbusha mwandishi kufatilia ruhusa ya kunakili kile ambacho amekichukua kutika kwa waandishi wengine, kama bado kipo chini ya hakimiliki. Kwa mfano mwandishi akiwa amerejelea majedwali, michoro au nukuu kutoka kwa mwandishi mwingine. Hivyo mhariri hufanya kazi ya kumkumbusha mwandishi mara kwa mara kuweza kufuatilia ruhusa kutoka kwa mwandishi mwingine ambaye ametumia katika kazi yake, au mhariri kufanya jukumu hilo la kufuatilia ruhusa kwa matalaamu ambaye mwandishi amemtumia katika kazi yake.

Kwa ujumla, wahariri wana jukumu kubwa katika kuufanya mswada kuwa kitabu, kutokana na majukumu yao yanawawezesha kufanikisha kazi hiyo ya uhariri. Hivyo wahariri ni kiungo muhimu sana katika kuhakikisha mswada unakuwa kitabu, kwani wana majukumu mazito katika kukamilisha mchakato huo wa kutengeneza kitabu mpaka kufikia hatua ya kuchapwa na kutolewa kwa wasomaji. Tunaweza kuona uhariri si kazi rahisi, ni jukumu zito katika kumsaidia mwandishi kufikisha ujumbe wake kwa walengwa. 






MAREJELEO
Einsohn, A. (2006). The Copyeditor’s Handbook. London: University of California Press
Mallya, J. M. K. (1993) “Uandishi wa Matatizo ya Uchapishaji Tanzania” katika Makala ya
                                    Semina ya Umoja wa Waandishi Vitabu Tanzania. Vol 1 (Uk214)
Mulokozi, M.M (1982). Maendeleo na Matatizo ya Uchapishaji wa Vitabu vya Kiswahili. Dar-
                                    es-Salaam: TUKI
Omari, B. (1995) “Uhariri wa Kamusi ya Kiswahili” katika Makala ya Tahakiki na Uchapishaji
                                    wa Kamusi. Vol 1 (Uk70)
TUKI (2013). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press East African

                                    Limited

3 comments:

  1. Kazi hii imenifaidi mno kufanikisha swali langu la mhula la uhariri.Mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa nne, chuoni Nairobi katika taaluma ya Kiswahili na mawasiliano.Natoa mkono wa tahania.

    ReplyDelete
  2. Je mhariri anaweza husiana vipi na wafanyikazi wengine katika shirika la uchapishaji

    ReplyDelete
  3. Hello am very much appreciative to the content you have provided, furthermore I would like you to offer a discussion on the kategoria ya virai, thank you and God bless you.. keep good work going

    ReplyDelete

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny