- UTANGULIZI
Swali hili limegawanywa katika
sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambao unajumuisha fasili za
dhana zilizojitokeza katika swali na ufafanuzi mfupi wa riwaya ya Ua
la Faraja, sehemu
ya pili ni kiini cha swali ambapo kinahusu athari za majina ya wahusika wa kazi
ya fasihi tuliyoichagua na sehemu ya tatu ni hitimisho.
1.1 Fasili ya Dhana zilizojitokeza Katika Swali
Zifuatazo ni fasili mbalimbali
zilizojitokeza katika swali.
1.1.1 Fasili ya Fasihi
Kwa mujibu wa Nkwera (2003), Fasihi ni sanaa yaani
mkusanyiko wa kazi mbalimbali zilizosanifiwa kwa kutumia lugha itumiayo zaidi
maneno na kujishughulisha na jinsi binadamu anavyojitambua mwenyewe binafsi, Pia
anavyoathiriwa na binadamu wenzake aidha na viumbe vingine aina kwa aina katika
mazingira mbalimbali ya maisha. Tunaona fasili hii imejikita zaidi katika
maneno kuelezea maana ya fasihi na kazi zilizosanifiwa.
Nae, Wamitila (2004), anafasili fasihi ni sanaa ya lugha
inayoshughulikia masuala yanayomuhusu binadamu matatizo yake, ndoto zake, matumaini
yake, migogoro yake na jinsi anavyoingiliana na mazingira yake fasihi; ni sanaa
itoayo maudhui yake kwa kutumia lugha ya maneno ambayo hutamkwa ama kuandikwa.
Kwa mtazamo wetu kutokana na maana za waandishi
tofautitofauti ambao wamejitahidi kutoa maana ya fasihi tunaona kuwa fasihi ni
kazi ya sanaa inayotumia lugha katika njia masimulizi au maandishi katika
kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa jamii husika katika kuikabili mazingira yake
katika nyanja mbalimbali za maisha kama vile siasa, uchumi, na utamaduni.
1.1.2 Ufafanuzi kuhusu Majina ya Wahusika
Kenan (2007), anaona
kwamba majina ya wahusika yanaweza kujitokeza kwa kuzingatia tabia zao
zinazoweza kujitokeza katika matendo, maneno na muonekano wa nje ya mazingira.
Nae, Mlama (2003), anasema wahusika huteuliwa na hujengwa
kutokana na matukio na uwezo wa kisanaa alionao mwandishi. Mwandishi huwapa
maneno, matendo na mawazo wahusika wake kutokana na matukio ili kuonyesha
uhalisia na uhusika wa kuaminika katika hali wanamotokea. Anaendelea kusema
kuwa uteuzi wa majina ya wahusika katika riwaya si kitu rahisi. Ugumu uko
katika kuchagua na kuumba majina ya wahusika na kuwaonyesha kimawazo, kimatendo
na kimaneno ili kukidhi na kuwakilisha dhana mbalimbali za maisha katika jamii.
1.1.3 Riwaya ya Ua la Faraja
Ni riwaya iliyoandikwa na Makufya na imejadili dhamira ya
mapenzi kama dhamira kuu. Mapenzi yanayojadiliwa kwa kiasi kikubwa ni mapenzi
ya ndoa na uaminifu wake na mapenzi kati ya mtu na mtu, mtu nan chi pamoja na
mapenzi ya mtu na familia. Halikadharika dhamira zingine kama ulevi, uhujumu
uchumi, umuhimu wa kufanya kazi, magonjwa, umasikini na nyingine nyingi. Riwaya
hii imetumia wahusika kama vile Omolo, Pendo, Chiku, Msafiri, Asha, Queen,
Juma, Dk Hans nakadhalika.
2.0 Kiini cha Swali
Hussein (2003), anafafanua kuwa
wahusika katika kazi za fasihi huwa na athari kubwa sana kwa hadhira au
wasomaji kutokana na kwamba ndiyo wanaobeba matukio yote yanayotakiwa
kuwasilishwa katika jamii. Zifuatazo ni athari za wahusika wa kazi ya fasihi
kwa wasomaji kwa kutumia riwaya ya Ua la Faraja.
Majina ya wahusika husaidia
kuonyesha umoja na mshikamano kwa wasomaji. Mwandishi katika riwaya hii
ametumia jina Juma kama muhusika ambaye alikuwa na umoja na upendo katika
familia yake. Juma ni jina linalotokana na siku ya Ijumaa katika Kiswahili,
yenye kumaanisha siku ya Sala kwa dini ya Kiislamu ambapo waislamu wote
hukutana pamoja kuonesha umoja miongoni mwao, na kusaidiana na jina hili hupewa
watoto wa Kiume. Hivyo jina Juma katika riwaya hii humaanisha uwezo wa
kuwakusanya watu kwa pamoja na kusaidiana. Halikadhalika tunaona jinsi juma
alivyokuwa na upendo na mshikamano kwa familia yake na jinsi alivyokuwa
akimsaidia mama yake na wadogo zake katika shida na raha. Tunamuona
anavyohakikisha na kuwaweka wadogo zake katika hali ya umoja na upendo.
Mwandishi anaonesha Juma akisema;
“mama usiondoke.
Unajua hali ya hapa nyumbani. Nuru na Rahma watabaki
na nani sisi
tukienda shule” (uk 37)
Hivyo tunaona jinsi gani jina la
muhusika huyu linvyotoa funzo kwa wasomaji kuwa na umoja na mshikamano katika
jamii zetu tunamoishi. Jamii zinapaswa kuwa na umoja na mshikamano katika
kusaidiana katika mambo mbalimbali ili kuleta maendeleo katika jamii.
Majina ya wahusika husaidia kuonyesha
hekima, akili na shupavu katika mapambano ya kimwili na kiroho ili kufanikisha
jambo fulani. Mwandishi katika riwaya hii amemtumia Grace kama muhusika mwenye
hekima na akili ya kupambanua mambo. neno Grace asili yake ni kutoka katika
lugha ya kiingereza lenye maana ya hali na tabia za mungu kama upole,
uvumilivu, utu, wema. Mwandishi anamuonesha Grace jinsi anavyoishi kwa amani,
upendo na furaha na dada yake Tabu na Omolo, amekuwa mshauri mzuri kwa Tabu,
Omolo na Ngoma, amewauguza Tabu na Ngoma hadi kufa kwao. Anawalea watoto wa
Tabu kama mama yao, anamkomboa Omolo katika giza la maisha alimokuwa na
kumuweka katika mwanga wa maisha ya ndoa kama ambavyo Grace mwenyewe anasema;
“…alijiona mwenye wajibu wa
kulitatua pingamizi lile, wajibuu wa
kumwokoa Omolo kutoka kwenye upweke ulimwandama na
kumwathiri.
Hakujua ataanzaje, lakini alijipa Imani ya
mafanikio” (uk. 271)
Maelezo haya ni ya makusudi
kabisa yanayomwonesha Grace kuwa ni shupavu, jasiri na mvumilivu katika
mapambano ya kumkomboa Omolo kwenye matatizo yake na hata katika kuwasaidia
watu wengi. Hivyo tunaona kuwa msomaji na jamii kwa ujumla kupitia muhusika
Grace tunaweza kujifunza kuwa na ushupavu katika kukabili mambo mbalimbali
yanayojitokeza.
Majina ya wahusihusika huonyesha
hali mbalimbali zinazomkabili mtu, kitu au vitu. TUKI (2009), imefasili neno
Tabu kama hali ya kutokuwa na raha, kuwa na adha, usumbufu, shida, mashaka na
kero. Halikadhalika katika riwaya hii tunaona jinsi muhusika Tabu alivyoishi
maisha yasiyo ya raha, yenye usumbufu, kero, mashaka, udhia na shida mbalimbali
toka kuolewa kwake. Hii inajidhirisha pale ambapo mwandishi anasema:
“…Akaeleza
habari za mapenzi ya siku nyingi baina ya mwanamke aliyeitwa
Queen na
mumewe Ngoma. Akaeleza mizozo ya huko nyuma baina yake na
mumewe
kuhusu huyo mwanamke. Kisha akamalizia kwa habari alizozipata
kwamba
mwanamke huyo tayari anadalili zinazojulikana kama ni za
UKIMWI” (uk. 59).
Kupitia jina la Tabu tunaona msomajia anaweza kujua hali mbalimbali
zinazomkabili mtu katika jamii na jinsi ya kuzikabili hali hizo kama jinsi Tabu
alivyokabiliana na hali hizo, mathalani kuambukizwa UKIMWI na mumewe,
kutotimiziwa mahitaji mbalimbali ya kifamilia nakadhalika. Inatubidi kujua hali
tulizonazo, kuzikubali na kutafuta namna ya kuzikabili.
Majina ya wahusika husaidia
kuonyesha upendo na uthamini wa kitu au kazi unayoifanya. Mwandishi amemtumia
muhusika pendo kuonyesha upendo na uthamini katika kazi aliyokuwa akiifanya.
Jina Pendo linatokana na neno penda, kwa mujibu wa TUKI (2009), penda ni kutaka
shauri kufanya jambo kwa kuridhika mwenyewe. Hivyo pendo ni jina la mtu lenye
maana penda. Katika riwaya hii mwandishi amemuonyesha pendo kama kama muhudumu
wa bar aliyekuwa akiipenda kazi yake na kuithamini pamoja na kuwahudumia wateja
na hata kucheza mziki pamoja. Tunaona pendo aliithamini na kuifurahia kazi yake
ya kuwahudumia watu. Mwandishi anasema;
“aliendelea
kulisakata rumba, pendo akamwendea. Wakawa wanacheza
pamoja huku
ngoma akizidisha mbwembwe baada ya kupata mwenza.” (uk 7)
Hivyo kupitia muhusika huyu
wasomaji wanajifunza kuthamini kazi au majukumu mbalimbali wanayoyapata katika
jamii zao. Matahalani kazi ya ualimu, mwalimu anatakiwa kuifanya kazi hiyo
vizuri na kuithamini kazi hiyo bila kujali changamoto anazokabiliana nazo.
Pia majina ya wahusika husaidia
kuonyesha kazi mbalimbali. Hapa mwandishi amemtumia muhusika Msafiri, kama
aliyekuwa anafanya kazi ya kusafirisha
mafuta kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Msafiri ni jina linalotokana na neno
Safiri. TUKI (2009), imefasili neno safari kama ni kutoka mahali fulani na
kwenda mahali pengine, mathalani kutoka mji mmoja kwenda mji mwingine na
kadhalika. Katika riwaya hii tunaona msafiri alikuwa kazi ya kusafirisha mafuta
kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Kigali. Mwandishi anasema;
“msafiri alikuwa
dereva wa gali la mafuta. Alisafirisha mafuta toka bandari
ya Dar es
Salaam hadi Kigali. Inasemekana gari la mafuta alilolitumia
lilikuwa mali
yake.” (uk 89 -90)
tuaona kuwa majina ya wahusika
katika kazi ya fasihi, mwandishi huwapa uhusika huo kutokana na kazi
wanazofanya, hivyo kusaidia wasomaji kujua kazi mbalimbali katika jamii.
Halikadhalika katika jamii zetu baadhi ya watu hupewa majina kutokana na mambo,
tukio au siku fulani ambalo litabaki kuwa kumbukumbu. Mathalani majina kama
Tabu, Shida nakadhalika.
Halikadhalika majina ya wahusika
husaidia kuonyesha uzuri wa kitu, mtu au jambo na matatizo yake. Tunaona
mwandishi amemtumia muhusika Queen kuonyesha dhana ya uzuri. Queen ni jina la
kingereza lenye maana ya malkia katika lugha ya Kiswahili. Jina malkia
linafasiliwa kama mtu mzuri sana na anayevutia. Queen alikuwa mwanamke mzuri,
mrembo na msomi na aliyevutia kwa kila mwanaume aliyeonana nae. Kutokana na
uzuri wake, aliutumia vibaya kwa kuwa na wanaume wengi hadi kupelekea kupata
maradhi ya UKIMWI. Katika riwaya hii mwandishi anasema kuwa:
“Queen alikuwa mashuhuri
mtaani kwa urembo wake, na pia kwamba
alikuwa mwanamke pekee
msomi na menye cheo kikubwa kazini kwake .Hivyo
habari za kuuguwa kwake
zilichukuliwa na wengi, hasa wanawake, kwa hisia za
furaha iliyotokana na
wivu na chuki dhidi yake” (uk 36)
Tunaona kuwa msomaji huweza
kuelewa dhana ya uzuri na changamoto zake zinazojitokeza kutokana na uzuri huo.
Hivyo, wasomaji wataelimika na kuweza kujua kuwa uzuri wa kitu, mtu huweza kuwa
na matatizo mbalimbali pindi unapotumika vibaya.
3.0 Hitimisho
Kutokana na majina ya wahusika
yaliweza kutumika katika riwaya ya Ua la Faraja msomaji ameweza kupata athari
mbalimbali kwa jinsi mwandishi alivyoweza kuwatumia wahusika hao na majukumu
aliyowapa kutokana na sifa za majina ya wahusika. Mwandishi huweza kuunda
wahusika wa kazi ya fasihi kulingana na mambo na majukumu ambayo anataka
kuwapa, ambayo huendana na sifa za majina yao.
MAREJELEO
Kenan, S. R (2007). Narrative Fiction. New York: Routledge.
Hussein, E. (2003). Hatua mbalimbali za Kubuni na
Kutunga Tamthiliya kufuatana na Misingi
ya Ki – Aristotle. Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III.
Dar es Salaam. TUKI.
Mlama, P. O. (2003). Utunzi wa Tamthiliya katika
Mazingira ya Tanzania. Makala za Semina ya
Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III. Fasihi. Dar
es Salaam: TUKI.
Nkwera, F. V. (2003). Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu: Sekondari na
Vyuo. Dar es Salaam:
Creative Prints Ltd.
TUKI. (2009). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi:
Oxford University Press.
Wamitila, K.W. (2010). Misingi ya
Uchanganuzi wa Fasihi. Nairobi Kenya: Vide-Muwa.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com