Flower
Flower

Thursday, May 30, 2019

UCHAPISHAJI NA IDARA ZAKE


Mulokozi (2003) anasema uchapishaji ni mbinu ya usambazaji wa habari, maarifa au fasihi kwa maandishi yaliyopigwa chapa au kunakiliwa katika nakala nyingi.

TUKI (2013), wanasema Uchapishaji ni kazi ya kushughulika na utoaji wa vitabu na kutawanya kwa kuviuza kwa watu.

Kamusi Teule ya Kiswahili (2014) wanaeleza kuwa uchapishaji ni utoaji wa nakala za maandishi kwa kutumia mtambo maalum. Hivyo basi uchapishaji ni mchakato wa utoaji na usambazaji au uenezaji wa taarifa kwa watu wengi katika umbo mahsusi. Sababu ambazo zilipelekea kuzuka kwa uchapishaji ni uandishi na kisomo, dini, siasa, biashara, ugunduzi wa karatasi na ugunduzi wa uchapaji.

Kampuni ya uchapishaji hujumuisha idara na vitengo mbalimbali kama vile, idara ya utawala, idara ya uhariri, idara ya usanifu na utoaji, idara ya uhasibu, idara ya uhifadhi na idara ya TEHAMA au kompyuta. Mfano wa makampuni ya uchapishaji ya Afrika Mashariki ni Mkuki na Nyota, TUKI, Mture, Macmillan Aidan, Vide Muwa, Phoenix, Focus Books na Crane Publishers. Ufuatao ni umuhimu wa idara na vitengo hivi katika kampuni ya uchapishaji.

Idara ya Utawala, ni idara ambayo hujumuisha mameneja pamoja na wakuu wa vitengo, ambao ndio wasimamizi na waendeshaji wa kampuni. Idara hii huwa na umuhimu ufuatayo, kusimamia uendeshaji wa shughuli zote za kampuni ikiwemo, kuajili na kuwalipa mishahara wafanyakazi na mrabaha kwa waandishi wa vitabu, ikiwa ni sehemu ya malipo yao ya mauzo ya vitabu. Pia kulipa kodi kwa serikali, na kuhakikisha suala la mawasiliano.

Idara ya uhariri.TUKI (2013) wanasema Uhariri ni kazi ya kusoma kusahihisha na kusanifu miswada ya makala au vitabu. Katika idara hii kuna muhariri wa jumla na muhariri wa matini. Muhariri wa jumla majukumu yake ni kubainisha maeneo yanayofaa kuandikwa au kutolea kitabu na kutafuta miswada inayofaa au waandishi wanaoweza kuandika miswada hiyo. Pia kutathimini miswada inayoletwa kwaajili ya uchapishaji. Kuandaa pendekezo la uchapishaji wa mswada anaona unafaa kuwa kitabu. Kuandaa mkataba wa uchapishaji kati ya kampuni yake na mwandishi, baada ya kujadiliana na kukubaliana na mwandishi na wakuu wa kampuni yake. Kupendekeza kutoa au kutokutoa chapa mpya za kitabu zinapomalizika. Majukumu ya muhariri wa matini ni kunyoosha au kusahihisha maelezo katika mswada ili kuboresha na kurahisisha mawasiliano kati ya mwandishi na msomaji wake. Hivyo hujaribu kuufanya ujumbe wa mwandishi uwafikie walengwa kwa njia bora, wazi na yenye kuvutia Zaidi, kwa kuboresha matumizi ya lugha, kuangalia uwiano mzuri kati ya fani na maudhui katika mwsada kulingana na walengwa, kupendekeza aina ya vielelezo vinavyohitajika katika kitabu na kunyoosha mpangilio wa mawazo wa uwasilishaji wa mawazo hayo.

Idara ya Usanifu. Feather (2003) Usanifu ni Sanaa ya kuoanisha vipengele vyote ya kitabu, katika maudhui, mtindo, michoro, vielelezo na muundo katika umbo nadhifu, ili kuwasilisha ujumbe katika muundo unaovutia. TUKI (keshatajwa), wanasema Usanifu ni ufundi au ustadi wa uchoraji maumbo yanayoonesha jinsi kitu chenyewe kitakavyokuwa.  Idara hii hufanya kazi karibu na idara ya uhariri, pia hupangilia namna ya kitabu kuwa. Usanifu hufanywa kwa kuzingatia teknolojia itakayotumika, kuchapa, gharama, walengwa, matumizi ya kitabu hicho, na biashara au soko. Pia suala la ukubwa au udogo wa kitabu, rangi na mandishi hupangwa na idara hii.

Idara ya Uhasibu, ni idara ambayo hufanya kazi kwa karibu sana na idara ya utawala pamoja na uhariri. Majukumu ya idara hii ni kurekodi mahesabu ya kampuni ikiwa ni pamoja na mapato na matumizi. Uhusiano wa karibu wa idara hii na idara ya utawala ni pale ambapo, muhasibu huusika na mahesabu ya mapato na matumizi na hupeleka ripoti katika idara ya utawala kwani yenyewe ndiyo huusika na uratibu wa matumizi na mapato hayo. Uhusiano wa karibu wa idara ya uhasibu na uhariri ni pale ambapo muhariri wa jumla huitaji pesa kutoka kwa muhasibu zinazo msaidia kushughulikia menejimenti ya kukamisheni, kutafuta miswada na kuratibu kazi zote za uaandaji wa kitaabu.

Idara ya Uhifadhi, kwa mujibu wa TUKI (keshatajwa) wanasema ni tendo au hali ya kuweka kitu mahali fulani kwa usalama. Katika idara hii huwa na majukumu ya uhifadhi, masoko, uuzaji, na usambazaji. Katika uhifadhi, huhusisha utunzaji wa vitabu, majalada ya kumbukumbu mbalimbali zinazohusu kampuni ya uchapishaji. Uuzaji na usambazaji huhusisha namna au jinsi vitabu ambavyo huweza kuuzwa na kusambazwa ili kuwafikia watumiaji husika, kwa njia ya mtandao au kwa njia ya usambazaji katika maduka mbalimbali ya vitabu.



Kwa ujumla uchapishaji ulianza kwa njia ya kunena ambao ulihusisha au walitumia fasihi simulizi, ngoma, ngomezi, na ala mbalimbali za sauti. Ulifuatiwa na maandishi katika kipindi hiki nchi mbalimbali walitumia maandishi ili kufikisha ujumbe kwa jamii iliyo kusudiwa. Mfano misri walitumia michoro ya hierographics, na wasumeria walitumia cuneiform na baadae uchapishaji.                                                              
                                            MAREJELEO

Feather, J (2003. “Communication knowledge” Berlin: Walter de Gruyter.

Mulokozi, M. (2003). “Uandishi na Uchapishaji” Dar es salaam; TUKI.

Ndallu, A. E (2014). Kamusi teule ya Kiswahili. Nairobi- Kenya: Prinywell Industries Limited

TUKI, (2013) “Kamusi ya Kiswahili sanifu”. Dar es salaam; Oxford University Press.







































                                      














                            

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny