1.0 UTANGULIZI
Sehemu
ya kwanza ni utangulizi, sehemu ya pili ni fasili ya dhana, sehemu ya tatu ni
vigezo muhimu vya kuchambua na kuhakiki kamusi, sehemu ya nne ni ufanano na
utofauti wa kamusi, sehemu ya mwisho ni hitimisho la swali.
1.1
Fasili
ya Dhana ya Leksikografia
Kwa
mujibu wa Weigand (1984) leksikogarafia ni kazi ya kutunga kamusi.
Leksikografia hujumlisha uorodheshaji wa msamiati wa lugha inayotungiwa kamusi
pamoja na maelezo yenye kufafanua kila neno lililoorodheshwa kadri ya mahitaji
ya mtumiaji wa kamusi aliyelengwa.
1.1.1 Fasili ya Dhana ya
Kamusi
Bakiza
(2010) wanaeleza kuwa Kamusi ni kitabu chenye orodha ya manneno yaliyopangwa
kwa alfabeti na kuelezwa fasili zake, aina, matumizi na taarifa nyingine
zinazohusiana nayo. Fasili hii haiweki wazi taarifa zingne zinazohusiana nayo
ni zipi.
Matinde
(2012:273) kamusi ni kitabu chenye mkusanyiko wa maneno sanifu katika lugha
mahususi yaliyoorodheshwa kialfabeti na kutoa taarifa za kifonetiki,
kimofolojia, kifonolojia, kisintaksia na hata kisemantiki. Fasili hii
imezungumzia taarifa mbalimbali zinazo wekwa katika kamusi, lakini yafaa
kuzingatia kuwa si kamusi zote zina taarifa hizo.
Massamba
(2004:14) kamusi ni kitabu cha orodha ya maneno katika lugha yaliyopangwa kwa
utaratibu maalumu pamoja na maana au fasili zake, katika uchanganuzi wa lugha
haya ni maneno ya kileksika, yaani yasiyokuwa ya kisarufi au kifonolojia.
Fasili hii imeegemea sana maneno ya kileksika ilihali kuna kamusi zenye taarifa
za kisarufi mathalani Kamusi ya Isimu
Kwa
ujumla, kamusi ni kitabu cha marejeleo chenye msamiati uliokusanywa kutoka kwa
wazungumzaji wa jamii fulani na kupangwa kwa utaratibu wa kialfabeti, kisha
kuwekewa taarifa za kisemantiki, kifonolojia kisintaksia na hata kimofolojia,
na kufafanuliwa kwa namna ambayo msomaji anaweza kuelewa.
1.1.2 Ufafanuzi kuhusu
Kamusi la Kiswahili Fasaha
kwa
mujibu wa BAKIZA (2010) wanaeleza kuwa wazo la kuandika kamusi la Kiswahili
liliwasilishwa na kujadiliwa kwa mara ya kwanza katika kikao cha Kamati ya
Kamusi na Usanifishaji ya Baraza la Kiswahili la Zanzibar Oktoba 2002. Wazo
hilo lilipata Baraka za Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman, ambaye wakati huo
shughuli za utamaduni zilikuwa chini ya dhamana yake. Alilipa baraza nguvu,
nyenzo na kulijengea uwezo wa kutekeleza azma hiyo.
Kazi
ya utungaji wa kamusi ilianza rasmi 2003 na ilishirikisha jopo la wataalamu
walioteuliwa kwa misingi ya uwakilishi wa lahaja zinazozungumzwa Zanzibar.
Uteuzi huo ulifanywa kwa makusudi ili kupata wigo mpana zaidi wa maana na
matumizi ya maneno ya Kiswahili. Pia malengo ya kamusi hii ni kuendeleza hadhi
ya Kiswahili pamoja na utamaduni wa Mswahili, kuwaongezea wasemaji,
wazungumzaji na watumiaji wa lugha hii kutumia kwa ufasaha na usahihi miundo na
mitindo yake. Kamusi hili limechota misamiati kutoka mazingira ya wasemaji wa
Kiswahili.
Kamusi
hili limegawanywa katika sehemu kuu tatu; sehemu ya kamusi yenyewe yenye maneno
yaliyopangwa kialfabeti kuanzia A mpaka Z ambayo ni maneno Zaidi ya 15000,
matamshi, kategoria za sarufi za maneno hayo pamoja na fasili zake, sehemu ya
kurasa za kudurusu yenye ufafanuzi wa chimbuko la Kiswahili, sehemu ya picha za
rangi zenye mvuto zilizopipangwa kulingana na mada au mazingira mbalimbali.
1.1.3 Ufafanuzi kuhusu
Kamusi ya Kiswahili Sanifu
Kwa
mujibu wa TUKI (2014) wanasema hili ni toleo la tatu la Kamusi ya Kiswahili
Sanifu. Toleo la kwanza lilitolewa mwaka 1981, uandishi wa toleo hili ni
ushirikiano wa wanaleksikografia na wataalamu wa lugha na fasihi wa Taasisi ya
Taaluma za Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hili ni toleo la aina
yake kwani limesheheni msamiati wa nyanja mbalimbali kama vile sayansi na
teknolojia, kompyuta na maneno mengine yaliyoibuka kutokana na lugha kuwa na
matumizi mapana.
Katika
toleo hili picha na michoro imeboreshwa na kuvutia. Kuingizwa kwa picha hizo
kutamsaidia msomaji kuelewa vizuri zaidi maana au kile anachokitafuta kwenye
kamusi. Katika kamusi hii mambo mapya mbalimbali yameingizwa kama vile
etimolojia ya maneno, ngeli zilizoainishwa kimofolojia, kisintaksia, na rangi
kubainisha visawe, misemo, nahau na methali.
2.0 Vigezo muhimu vya
Kiuchambuzi na Kiuhakiki katika Kamusi
Baada
ya kuangalia fasili mbalimbali kwa mujibu wa wataalamu na ufafanuzi wa kamusi
hizi vifuatavyo ni vigezo muhimu vya kiuchambuzi na kiuhakiki katika kamusi.
Kwa
mujibu wa mdee (2010) akimnukuu Landau (1984) anabainisha vigezo vikuu vitatu
vya kuzingatia katika kuhakiki kamusi ambavyo ni:
i)
Wingi wa taarifa zilizoingiwa katika kamusi.
katika
kigezo hiki taarifa zinazohakikiwa ni pamoja na idadi ya vitomeo
vilivyoingizwa, idadi ya maana zilizoorodheshwa kwa kila kidahizo, idadi ya
msamiati mpya ulioingizwa katika kamusi, msimbo wenye kuashiria mitindo ya nyanja
za matumizi ya kidahizo ilioonyeshwa na taarifa ya etimolojia.
ii)
Ubora wa taarifa iliyoingizwa kwa kila kidahizo.
katika
kigezo hiki huzingatia taarifa ambazo huingizwa katika kamusi zenye usahihi,
kamilifu na wazi. Ni muhimu taarifa hizo kuelezwa kwa urahisi ili kuweza
kueleweka kwa msomaji.
iii)
namna taarifa zilivyowasilishwa katika kamusi.
Katika
kigezo hiki mambo ya kuzingatia wakati wa kuhakiki ni jinsi taarifa
zilivyoingizwa katika kamusi mfano, kuorodhesha maneno kialfabeti, jinsi
etimolojia ilivyoingizwa, mpangilio wa maana za maneno zilivoorodheshwa,
uchapaji na ukubwa wa maneno wenye hadhi tofauti. Mdee (keshatajwa) anaendelea
kusema kuwa vipengele vingine ambavyo hutumiwa katika kuhakiki kamusi ni: Mwaka
wa kuchapishwa kwa kamusi, idadi na weledi wa washauri waliohusika katika
kutunga kamusi, idadi ya kurasa za kamusi na wastani wa idadi ya maneno katika
kitomeo.
3.0 Ufanano uliopo katika
Kamusi ya Kiswahili Sanifu na Kamusi la Kiswahili Fasaha
Baada
ya ufafanuzi wa vigezo vinavyotumika katika uhakiki na uchambuzi wa kamusi, zifuatazo
ni hoja zinazoelezea ufafano wa kamusi hizi kwa kuzingatia vigezo muhimu vya kiuhakiki
na kiuchambuzi.
Kamusi
hizi zimezingatia na kutumia mfumo wa kuorodhesha maneno kialfabeti. Vidahizo
vimeingizwa na kupangwa kwa kuanza na herufi A – Z. Katika kamusi ya KKS
imeanza na kidahizo a, aa na kundelea huku ikifuata mtiririko
wa kialfabeti na kumalizia na vidahizo vyenye herufi z. Pia katika kamasi ya KAKIFA wamezingatia upangaji wa vidahizo
kialfabeti wakianza na herufi a, aa na kumaliza na herufi Z.
Kamusi
hizi zimefanana katika mpangilio wa taarifa au maana zilizoorodheshwa katika
kidahizo. Katika kamusi taarifa zilizotumika kufafanua kidahizo kwa kiasi
kikubwa zinafanana. Mathalani kamusi zote katika kufafanua kidahizo wameanza na
fonolojia (matamshi), kategoria ya neno na maana ya kidahizo.
Mfano: neno abiria lilivyoandikwa
katika kamusi hizi
abiria / abirija/ nm. a/wa
mtu anayependa chombo cha usafiri na angha (KAKIFA)
abiria/ abirija/ nm. a/wa
mtu anayesafiri kwa chombo chochote (KKS)
Hivyo
ni dhahiri kuwa kuna ufanano katika upangaji wa taarifa za vidahizo baina ya
kamusi hizi mbili.
Zote
zinafanana katika ukubwa wa maneno na ukolezwaji vidahizo. Katika kamusi hizi
vidahizo vyake vimekolezwa kwa kutumia wino au rangi ya bluu. Halikadhalika
uchapaji wake yaani ukubwa wa maneno yaliyofafanua vidahizo na vidahizo
vyenyewe ni wa aina moja.
Zote
zinafanana katika kuonesha mfumo wa matamshi ya maneno. Mfumo uliotumika katika
kamusi hizi mbili unafanana kwani zote zinaoonyesha matamshi ya vidahizo kwa
kutumia alfabeti za kifonetiki katika kuonyesha jinsi ya kuyatamka maneno. Hii
humsaidia msomaji kutamka neno kama linavyotakiwa kwa kufuata namna matamshi
yalivyoandikwa. Pia matamshi yameandikwa baada ya vidahizo kuandikwa katika
kamusi zote mbili.
Ufanano
katika lugha iliyotumika katika uandishi na ufafanuzi wa vidahizo. Kamusi hizi
zimetumia lugha ya Kiswahili katika uandishi wa vidahizo na ufafanuzi wake. Kwa
mujibu wa Mdee (2010) anaeleza kuwa kamusi ya lugha moja hutungwa kwa ajili ya
wazungumzaji wa lugha inayohusika. Haja ya kuwa na kamusi ya lugha moja
inatokea pale matumizi yanapopanuka na lugha kuwa na msamiati mwingi na mpya
kwa wazungumzaji wengine. Umuhimu wa lugha moja unaongezeka wakati lugha
inapoanza kuandikwa na kuwa na maandishi anuai.
Ufanano katika idadi ya maana zilizoorodheshwa
kwa kila kidahizo. Katika ufafanuzi wa vidahizo, kuna maneno ambayo huwa na
maana zaidi ya moja kutokana na jinsi yanavyotumiwa na jamii. Katika kamusi
hizi vidahizo vyenye maana zaidi ya moja vimetolewa maana kuanzia mbili na
kuendelea.
Mfano; neno Babu. 1 baba yake baba
au mama. 2 lakabu ya heshima kwa mwanaume mzee. 3 cheo cha juu katika mchezo wa
karata. 4 Upana wa kitambaa kwenye jora (Kamusi ya Kiswahili Fasaha)
Babu. 1 baba
mzaa baba au mama. 2 kiongozi wa kiume katika kikundi cha umoja wa ngoma za
wanawake au mshauri wa kiume katika chama cha wanawake. 3 hutumiwa na wanawake
kuitana. 4 aina ya kipimo cha kitambaa. (Kamusi ya Kiswahili Sanifu)
Matumizi
ya vifupisho kuwakilisha maneno. Kamusi hizi zimetumia vifupisho mbalimbali
katika kuwakilisha maneno. Mathalani aina mbalimbali za maneno zimebainihswa
kwa kutumia vifupisho vifuatavyo;
1.
Nomino (nm)
2.
Kitenzi (kt)
3.
Kiwakilishi (kw)
4.
Kivumishi (kv)
5.
Kiunganishi (ku)
6.
Kihusishi (kh)
Halikadhalika
vifupisho vingine vimetumika mathalani, kama vile (k.v), aghalabu (agh), kwa
mfano (k.m).
3.1
Utofauti uliopo katika Kamusi ya
Kiswahili Sanifu na Kamusi la Kiswahili Fasaha
Uingizaji
wa taarifa za kietimolojia. Kwa mujibu wa TUKI (2014) etimolojia ni uwanja
unaohusika na historia ya maneno na maana zake. Hivyo katika uingizaji wa
taarifa za kietimolojia, Kamusi ya Kiswahili Sanifu tu ndio imeingiza taarifa
za kietimolojia kwa kuonyesha asili za maneno.
Mfano; Kamusi ya hii imeonyesha
asili ya neo ethonolojia kuwa asili
yake ni kutoka katika lugha ya Kingereza, dunia
asili yake ni kutoka lugha ya Kiarabu na maneno mengine mengi.
Ukubwa
na idadi ya maneno katika kamusi. Kamusi hizi zinautofauti mkubwa katika idadi
ya maneno yaliyoko kwenye kamusi. Kamusi ya Kiswahili Sanifu ina maneno ya zaidi
ya 285000 huku ikiwa na vidahizo Zaidi ya 25000, lakini Kamusi ya Kiswahili
Fasaha ina maneno zaidi ya 15000 huku ikiwa na vidahizo zaidi ya 15000.
Kutokana na takwimu hizo ni wazi kuwa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ni kubwa
kuliko Kamusi ya Kiswahili Fasaha.
Matumizi
ya picha na michoro katika kufafanua vidahizo. Kamusi hizi zina utofauti mkubwa
katika
matumizi ya picha katika kuelezea na kufafanua kidahizo. Kamusi ya
Kiswahili Sanifu imetumia picha na michoro katika kufafanua baadhi ya vidahizo
ndani ya kamusi na mwishoni
mwa
kamusi. Mathalani picha ya ghala (uk 132), mchoro wa kumbikumbi (uk 281) na
mingine mingi ambayo imetumika kufafanua vidahizo. Lakini katika Kamusi ya
Kiswahili Fasaha haijatumia michoro na picha katika kufafanua vidahizo bali
picha hizo zimewekwa mwishoni mwa kitabu zikionyesha vitu mbalimbali.
Matumizi
ya vifupisho kuwakilisha maneno. Kwa
mujibu wa BAKIZA (2010) vifupisho ni kutumia herufi moja, mbili au tatu kwa
mazumuni ya kuwakilisha neno fulani. Kamusi hizi zimetumia baadhi ya vifupisho vinavyotofautiana
katika neno moja.
Mfano; KKS KAKIFA
Kielezi (kl) Kielezi (ke)
Idadi
na weledi wa washauri waliohusika katika utungaji wa kamusi. Kamusi ya
Kiswahili Fasaha ilitumia waandishi nane katika kutunga na kuandika kamusi hii
ambao ni Bw Hamad Bakari Mshindo, Bw Haji Suleiman Amour, Mmanga, Mjengo
Mjawiri, Hussein Ali Hussein, Amour Abdalla Khamis, Soud Mohammed Masoud, Abass
Makame Mdungi na Khatib Makame Omar. Lakini Kamusi ya Kiswahili Sanifu ilitumia
waandishi watano katika uandishi ambao ni Dkt Chiduo, Prof Khamis, Bw Hans na
Bw Hassan K said.
Idadi
ya kurasa za kamusi. Idadi ya kurasa zilizotumika katika kamusi hizi
zinatofautiana, Kamusi ya Kiswahili Fasaha imetumia kurasa 492 kufafanua
vidahizo, kurasa 32 za picha za rangi zinazovutia na kurasa 10 za kumwongoza mtumiaji.
Lakini Kamusi ya Kiswahili Sanifu imetumia kurasa 16 za michoro ya rangi kuhusu
mada mbalimbali na kurasa 656 zikiwa na vidahizo pamoja na ufafanuzi wake.
Mwaka
wa kuchapishwa kamusi. Kamusi hizi zinatofatiana katika miaka iliyochapishwa.
Kamusi ya Kiswahili Fasaha imechapishwa mwaka 2010 ilihali Kamusi ya Kiswahili
Sanifu imechapishwa mwaka 2014.
4.0 Hitimisho
Baada
ya kulinganisha na kulinganua kamusi hizi tunaona kuwa kamusi hizi zinamchango
mkubwa kwa watumiaji wake. Kamusi hizi husaidia kutafuta, kutambua, kufahamu na
kutumia maneno kwa njia sahihi, kujifunza
lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Waswahili, kusoma, kuzungumza na
kuandika kwa lugha ya Kiswahili fasaha na kupata maneno muhimuna kupanua na
kuongeza idadi ya msamiati kwa watumiaji.
MAREJELEO
BAKIZA
(2010). Kamusi la Kiswahili Fasaha.
Zanzibar: Oxford university press.
Massamba,
D. (2004). Kamusi Sanifu ya Isimu na
Lugha Dar es Salaam. TUKI.
Matinde, R. S. (2012). Dafina
ya Lugha Isimu na Nadharia, kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na
Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Education publishers Ltd.
Mdee, J. S. (2010). Nadharia na
Historia ya Leksikografia. Dar es Salaam: TUKI
TUKI
(2014). Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Toleo
la tatu). Dar es Salaam: Oxford University
Press.
Weigand,
H. F (1984). Structure and Contents of a
General theory of Lexicography. New York.
Karoma Publisher.
Sawa
ReplyDelete