Flower
Flower

Saturday, June 15, 2019

MAANA NA AINA ZAKE

Katika sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo dhana ya maana imefasiliwa kwa mujibu wa wataalam mbalimbali. Sehemu ya pili ni kiini cha swali ambapo aina mbalimbali za maana zimefasiliwa kwa mujibu wa Leach (1981), na sehemu ya mwisho ni hitimisho ambapo tutahitimisha swali.
Ni vigumu kuwa na maana ya maana kwasababu maana huweza kupatikana  kutokana na vigezo mbalimbali kama vile mtazamo wa msomaji au msikilizaji. Hivyo basi wataalam mbalimbali wamefasili maana kama ifuatavyo;
 Habwe na Karanja (2007), Matinde (2012), Ogden na Richard (1923) wanakubaliana kuwa neno maana lina tafsiri nyingi, linaweza kudokeza sababu, kusudi, ishara, urejeleo, maelezo, ufafanuzi kufaa, ukweli na faida.
i.                    Unamaana gani kufika umechelewa?
      Chanzo au sababu
ii.                  Yale mawingu meusi yana maana mvua itanyesha sasa.
          Ishara
iii. Hana maana yoyote.
            Umuhimu au faida.
Kwa ujumla maana huweza kudokeza mambombalimbali kulingana na lengo au dhumuni la mzungumzaji. Dhumuni hilo linaweza kuwa sababu, kusudi, ishara urejeleo na umuhimu. Zifuatazo ni aina mbalimbali za maana kama zinavyopendekezwa na Leach (1981);
Maana ya msingi, hii ndiyo maana kuu ya neno ambayo haibadiliki badiliki kutokana na muktadha au mazingira na historia ya watu. Hivyo basi maana hii ndiyo ambayo inapatikana katika kamusi na huangaliwa na kufafanuliwa kwa kigezo cha kuwapo au kutokuwapo kwa nduni bainifu zinazokibainisha kitu hicho. Mfano
i.        Kijana
       Mtu wa makamo mwenye nguvu.
ii.        Oa
                                                                          Kufanya muungano na mwanamke ili kukaa
                                                                         pamoja kama mume na mke
                                    
iii.    Kasuku
                                                                        Ndege mkubwa mwenye rangi nyingi anayeweza
                                                                        kusema kama binadamu na mara nyingi hufugwa              
                                                                        majumbani.
Maana ya msingi pia huweza kuelezewa kwa kutumia sifa au nduni za kisemantiki vilevile ni msingi wa aina nyingine za maana, yaani kutokana na maana ya msingi hutusaidia kupata aina nyingine za maana ambazo hupatikana katika lugha mbalimbali.
Maana dokezi, ni aina ya maana ya ziada ambayo hudokezwa kutokana na sifa  ya ziada ya kitu ambacho kimetajwa au kuelezewa na mzungumzaji. Yaani maana hii ni zaidi ya maana ya msingi ambapo sifa za ziada ndizo hutumika kupata maana ya maneno au kitu ambacho kinazungumziwa na wazungumzaji. Vilevile maana hii hujishughulisha sana na tajiriba halisi ya ulimwengu ambayo mtu au watu huhusisha na taaluma ya lugha, kutokana na anachokiona au kukisikia. Mambo ambayo yanadhihirisha maana hii ni kama vile mtazamo, sifa za kisaikolojia na sifa za kiumbo. Mfano;
i.                    Mtazamo
       neno mwanaume   maana yake ni     - jasiri
                                                                   -nguvu
                                                 
ii.                  Sifa za kisaikolojia
      Neno mwanamke maana yake ni    -huruma
                                                      -upendo
                                                      
iii.                Sifa za kiumbo
                                                                 Neno mwanamke maana yake ni     -matiti
                                                                                                                          -ujauzito
 Katika mifano tajwa huthibitisha jinsi ambavyo maana dokezi huwezwa kuwasilishwa kutokana na mambo mbalimbali ambayo hupelekea kupata maana dokezi katika jamii. Vilevile maana hizi hubadilika badilika kutokana na jamii.
Maana ya kimtindo au kijamii, ni maana ambayo huzalishwa kutokana na muktadha ambamo sentensi au neno hutamkwa. Katika jamii kuna mitindo mbalimbali ambayo hutumiwa na wanajamii husika. Vilevile mitindo hii hutofautiana katika jamii moja na jamii nyingine. Misingi ya maana za kimtindo ni pamoja na lahaja na wakati, kwani kutokana na mambo haya matumizi ya lugha hutofautiana katika jamii moja na jamii nyingine. Mathalani
i.                     Bara hutumia neno bomba wakati Zanzibar hutumia mfereji.
ii.                  Bara hutumia kanzu kama ni vazi la wanaume pekee wakati Zanzibar hutumia kanzu kwa jinsi zote mbili yaani wanaume na wanawake.
iii.                Tanzania tunatumia daladala wakati Kenya wanatumia matatu.
Kutokana na mifano tajwa huthibitisha jinsi ambavyo mitindo ya lugha hutofautiana baina ya jamii moja na jamii nyingine.
Maana hisia, ni aina ya maana ambayo hupatikana kutokana na hisia za msemaji au mwandishi. Hivyo basi hisia alizonazo mtu husababisha matumizi ya maneno ambayo hubebeshwa hisia hizo. Maana hisia huweza kudhihirika kwa kutumia maana msingi au dokezi. Kwa mfano: Acha kulialia kama mwanamke (hapa msemaji anaibua hisia ya dharau kwa mwanamke, kwamba tabia ya kulialia sio ya mwanaume bali mwanamke). Aidha, maana hisia huweza kuwasilishwa kwa kutumia maana ya moja kwa moja. Mathalani, Naona na leo umependeza tena (huku akimaanisha mchafu). Vilevile, maana hisia huweza kuwasilishwa kwa kutumia kiimbo, kwa mfano: Mpole (kejeli, swali au mshangao na taarifa)
Maana akisi hujulikana pia kama maana mwangwi. Katika taaluma ya semantiki maana mwangwi ni aina ya maana ambayo hupatikana kutokana na neno moja kuwa na fahiwa nyingi ambazo zinashindana kimatumizi. Yaani maana moja hukonyeza maana nyingine. Kutokana na hali hii husababisha msikilizaji afikirie maana nyingine ambayo ni akisi si ile ambayo inamaanishwa na mzungumzaji au mwandishi. Mathalani
i.                    Safisha Mtaro.
ii.                  Tia nyuma
iii.                Weka polepole.
Katika mifano tajwa ina fahiwa nyingi kutokana na hali hii hupelekea fahiwa moja iliyozoeleka kuchukua nafasi ya fahiwa nyingine za neno hilo kama inavyodhihirishwa katika maneno tajwa. Katika neno (i) humaanisha kuingiliana kinyume na maumbile (ii) Pia humaanisha kuingiliwa kinyuma na maumbile (iii) huakisi tendo la ndoa. Aina hii ya maana hutumia zaidi tafsida ili kupunguza ukali wa maneno baina ya wazungumzaji.
Maana tangamani au ambatani, ni aina ya maana ambayo inapatikana kutegemeana na muktadha wa matumizi kwa kuzingatia maneno mawili au zaidi yanayotangamana, yaani yanayokubali kutumiwa pamoja ili yalete maana moja kwa maeneo mengine hayo yanayokamilishana. Hivyo basi maneno haya yanakuwa ni ambatani lakini maneno yote huwa na maana moja kutokana na ukaribu wake. Mfano;
i.                    Kiti changu
          Inamaanisha nilichokalia.
ii.                  Kiti wangu
            Inamaanisha pepo au mashetani.
Maana dhamira, ni maana ambayo hutokana na kile ambacho mtoa ujumbe anakipa umuhimu. Maranyingi kinachopewa umuhimu hujitokeza mwanzoni mwa sentensi. Hivyo maana inayojengwa ni ile inayositiriwa ndani ya sentensi. Hivyo basi kutokana na jinsi ambavyo mzungumzaji au mwandishi amepangilia ujumbe tunaweza kupata dhamira ya ujumbe huo kwa kusikiliza au kusoma sentensi ya kwanza. Mathalani
i.                    Juma amekula chakula (hapa msisitizo umewekwa kwa JUMA)
ii.                  Chakula kimeliwa na Juma (hapa msisitizo umetiwa katika chakula)
Hivyo basi dhamira au dhima ya mzungumzaji au mwandishi huweza kujidhihirishwa kwa sentensi ya kwanza katika sentensi husika.

Kwa kuhitimisha tunaweza kueleza kuwa, tukizitazama aina za maana kwa mujibu wa mtaalamu leech (1981) tunaweza kuzigawa aina hizi katika makundi mawili, yaani maana za msingi na maana za ziada. Hata hivyo, uelewekaji wa aina zote za maana hutegemea na maana ya msingi ya kiyambo husika. Hivyo tunaweza kueleza kuwa, suala lauanishaji wa aina za maana bado linasailika.
        
                                                
                                                               MAREJELEO.
Habwe, J. na Karanja, P. (2007). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix publishers LTD.
Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia, kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na
                                     Vyuo Vikuu.  Mwanza: Serengeti Education publishers (T) LTD.
Leach, G. N. (1981). Semantics. Hardsworth: Penguin.
Ogden, C. K & Richards, I. A (1923). The Meaning of Meaning. London: Routledge.

                                

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny