Flower
Flower
Showing posts with label KISWAHILI. Show all posts
Showing posts with label KISWAHILI. Show all posts

Monday, April 29, 2019

Dhana ya vitenzi imeelezwa na wanazuoni tofautitofauti kama ifuatavyo: TUKI (1990) wanafafanua kitenzi kuwa ni neno ambalo hutokea kama sehemu muhimu ya kiarifu. Hii ina maana kuwa kitenzi ndio kijenzi kikuu cha kiarifu katika muundo wa sentensi. Matinde (2012) anasema kitenzi ni neno linalotoa taarifa kuhusu tendo linalofanyika, lililofanyika na litakalofanyika.

Richard na wenzake (1985) wanasema kuwa kitenzi ni neno ambalo hutokea kama sehemu muhimu ya kiarifu na ambalo huambishwa mofu za njeo, hali, nafsi, idadi na dhamira. Aidha, vitenzi hueleza juu ya tendo au hali. Naye Nkwera (2003) anasema kuwa vitenzi ni maneno yanayoarifu jambo ambalo hufanywa na jina au kufanyiwa jina. Pia, Nkwera anaeleza kuwa kitenzi kinaweza kuwa kiwakilishi au kivumishi kisimamapo peke yake kama jina. Vitenzi hutaja matendo, matukio, hali au mabadiliko. Kitenzi ni neno ambalo limebebeshwa vitu vingi ndani yake suala linalowafanya wanasarufi wengi kupendelea kuliita neno hilo kifungutenzi badala ya kitenzi.

Naye Mdee (2007) anatoa maana ya kitenzi kuwa ni neno linaloeleza jambo linalotendwa na lililotendeka. Kitenzi huarifu tendo lililofanywa au litakalofanywa na mnyama, mtu, au kiumbe chochote kinachoweza kutenda jambo. Mdee anaendelea kufafanua kuwa vitenzi vya Kiswahili havisimami pekee vinapotumiwa katika tungo, bali huambatana na viambishi vingine vyenye kuwakilisha mtenda wa tendo au mtendewa wa jambo. Kitenzi huambatishiwa pia viambishi vyenye kuonesha wakati tendo linapofanyika, kama mfano ufuatao unavyoonesha: Mfano Dada a-na-soma, watoto wa-na-ruka, baba a-ta-fika.

Mgullu (2010) anasema kuwa vitenzi ni aina ya maneno ambayo hutumika kama sehemu muhimu sana ya kiarifu cha sentensi ambayo hueleza jambo fulani linalohusu kiima cha sentensi. Katika lugha ya Kiswahili vitenzi ni maneno pekee ambayo ni lazima yawepo katika sentensi ndipo kifungu cha maneno kiweze kuwa sentensi, kwa mfano katika sentensi: Mtoto anakula. Aidha, Matinde (2012) anaeleza kuwa kitenzi ni neno linalotoa taarifa kuhusu tendo lililofanyika, linalofanyika au litakalofanyika. Katika muundo msingi wa tungo za Kiswahili kitenzi ndilo neno kuu katika sehemu ya kiarifu au kirai tenzi. Kitenzi kinapoondolewa katika sentensi bila shaka kifungu hicho cha maneno hukosa maana. Matinde anafafanua kuwa vitenzi huweza kusimama bila msaada wa aina zingine za maneno na sentensi ikawa kamilifu na yenye uarifishaji mkamilifu.

Kwa mujibu wa Massamba (2012), anafasili dhana ya Uarifu kuwa ni uhusiano wa kiima na kiarifu kwa namna ambayo kiarifu kinakuwa na neno linalovumisha kiima.  Kwa kutumia mifano ya kutosha kutoka katika lugha ya Kiswahili ufuatao ni ufafanuzi wa uarifu wa kitenzi.
Kitenzi huarifu kuhusu njeo. Habwe na Karanja (2007) wanasema kuwa kuna aina tatu za njeo, nazo ni njeo ya wakati wa sasa, wakati uliopita, na wakati ujao. Waihiga (2010) anaeleza kuwa kuna nyakati za aina tatu zinazowakilishwa na viambishi mbalimbali katika Kiswahili yaani, wakati uliopo, wakati uliopita na wakati ujao. Aidha, wanazuoni wengi wanakubaliana kuwa wakati uliopo huwakilishwa na kiambishi ‘na’, wakati uliopita huwakilishwa na kiambishi ‘li’ na wakati ujao huwakilishwa na kiambishi ‘ta’. Njeo ni miongoni mwa kategoria za kisarufi zinazosaidia kufasili dhana ya kitenzi.
                 Mfano: i) njeo ya wakati uliopo.
                              Anacheza, anapika, anasoma, analima anaimba.
                             ii) njeo ya wakati uliopita.
                              Alikula, alisoma, alioga,
                            iii) njeo ya wakati ujao.
                              Atacheza, ataimba, atalima,
Hivyo tunaona kuwa, katika mfano wa kwanza kiambishi na  katika kitenzi huarifu kuhusu wakati uliopo. Kiambishi li katika kitenzi huarifu wakati uliopita na liambishi ta, huarifu wakati ujao.
Kitenzi kinaarifu kuhusu nafsi, Kwa mujibu wa Habwe na Karanja (2007), wanafafanua nafsi kuwa ni kipahio kinachodhihirisha muhusika katika usemaji. Anaendelea kusema kuwa kuna nafsi tatu ambazo hudhihirika katika umoja na wingi. Nafsi ya kwanza huhusu yule mtu anayesema, nafsi ya pili inahusu mtu anayesemwa ilihali nafsi ya tatu inahusu anayesemwa juu yake.
                        

Mifano: i) Nafsi ya kwanza umoja inayohusu mtu anayesema  na nafsi ya kwanza wingi inahusu watu wanaosema.
Umoja                                                       wingi.
Ninakula,                                                 tunaku
                                        Ninachunga                                              tunachunga
     Nasafisha                                                tunasafisha
Katika mifano hiyo kiambishi ni katika kitenzi huarifu kuhusu mtenda na kiambishi tu huarifu kuhusu nafsi ya kwanza wingi
                   ii)  Nafsi ya pili
                                          Umoja                                                        wingi
                                          Unakula                                                   Mnakula
                                          Unachunga                                               Mnachunga
                                          Unasafisha                                               Mnasafisha
Aidha  kiambishi u katika kitenzi hutoa taarifa kuhusu nafsi ya pili umoja na kiambishi m huarifu kuhusu kitenzi cha nafsi ya pili wingi.
iii) Nafsi ya tatu
                                   Umoja                                                 Wingi
                                 Anakula                                               wanakula
                                 Analia                                                  wanalia
                                Anapiga                                                wanapiga
Katika mfano huu kiambishi a kinaarifu nafsi ya tatu umoja katika kitenzi pia kiambishi wa kinaarifu nafsi ya tatu wingi.

Kitenzi kinaarifu kuhusu kauli mbalimbali, Habwe na Karanja (2007) wanasema kauli ni umbo la kitenzi linaloonesha uhusino baina ya kiima na yambwa. Sentensi ambayo huchukua yambwa yaweza kuwa katika kauli ya kutenda au kutendwa.
Mfano: Kauli ya kutenda,  i) Mama anakula chakula
                                          ii) Mama amempiga mtoto
                                                     iii) Baba analima
Katika mifano hii kiambishi a kinaonesha kauli ya kutenda.
 Kauli ya kutendwa. 
                               Mifano: i) Mbuzi ameibwa leo
                                                        ii) Barua imeandikwa na mama.
                                                       iii) Kuku amechinjwa jana jioni.
Kauli za kutendewa.
                                          Mifano: i)  Mwanafunzi amefanyiwa mtihani
                                                       ii) Baba amepikiwa chakula.
                                                      iii) Ana ameandikiwa barua.
Kauli ya kutendesha.
                                           Mifano: i)  mama alimpigisha mtoto mswaki.
                                                        ii) Mjomba alimsomesha Ana.
                                                       iii) Napenda kuchezesha midori.
Kauli ya kutendeka.
                                            Mifano: i) Mpira umechezeka.
                                                         ii) Nguo imechanika.
                                                        iii) Chakula kimelika.
Hivyo basi katika mifano hiyo, viambishi iw, na, wa, ish, esh, ek, ik katika sentensi  vinaonesha kauli mbalimbali.
Kitenzi cha idadi, ni kategoria ya kisarufi yenye kuonesha umoja na wingi katika tungo. Idadi katika Kiswahili hudhihirika katika  ngeli  na upatanisho wake.

Mifano:   umoja                             wingi
                                 mtoto analia                     watoto wanalia
                                      mtoto anacheza                watoto wanacheza
                                    kiti kimevunjika               viti vimevunjika
                                     uzi umekatika                   nyuzi zimekatika
Hivyo katika sentensi hizo vitenzi vina arifu viambishi ngeli idadi ambapo a, ki, na u katika ngeli katika umoja na wa, vi, na zi katika wingi.
Kitenzi huarifu kuhusu hali mbalimbali kama vile hali ya mazoea na hali ya masharti.
Hali ya mazoea.
                                Mifano:  i) Mwalimu hufundisha wanafunzi.
                                              ii) Mayasa huimba kwaya kila siku.
                                             iii) Mtemi hutembelea watu wake kila siku jioni.
Hali ya masharti.
Mifano: i) Kama angeliwai kufika ningelimuona.
                                   ii) Mwalimu angelifundisha vizuri Salome angelifaulu
                              iii) Sara angelimsikiliza kiongozi wake angelikuwa
mwanafunzi bora.



Hali timilifu.                              Mifano: i) Mtoto ameimba leo.
                                                               ii)  Mwalimu amefundisha.                      
                                                              iii)  Mtoto amekula.
Hivyobasi, viambishi hu  huonesha  namna hali ya mazoea katika vitenzi vya Kiswahili  inavyo bainika  na kuarifu hali ya mazoea yaani tendo ambalo hufanyika mara kwa mara, pia viambishi ngali na ngeli vinaarifu kuwa ili jambo moja lifanyike basi lazima jambo fulani litendeke au kutokea na kiambishi me huo hali timilifu.
Matinde (2012), anafafanua kuwa kitenzi ni neno linalotoa taarifa kuhusu tendo linalofanyika, lililofanyika na litakalofanyika. Anaendelea kufafanua kuwa dhima kuu inayofanywa na kitenzi ambapo huarifu tendo. Fasili hii hailezei wazi kwani kuna baadhi ya vitenzi havielezei tendo mathalani vitenzi vishirikishi vinaarifu kuwapo au kutokuwapo kwasifa, hali au kitu Fulani.
Mfano:  i) Mwajuma ni mchafu.
     ii) Huyu si mwizi.
         iii) Watoto hawana heshima.
Hivyo basi Vitenzi ni, si na hawana vinaarifu kuwapo au kutokuwapo kwa jambo fulani haviarifu kuhusu kutendeka kwa tendo lolote.
Richards (1985) anafafanua kuwa vitenzi huarifu au hueleza mambo mbalimbali kuhusu kiima. Mambo hayo ni pamoja na:
Huarifu tendo linalofanywa au litakalofanywa.
Mifano: i) Mwabupina atacheza.
               ii) Mwabupina hatacheza.
Huarifu siku au wakati.
                                                     Mifano:  i) Leo ni jumatatu.
             ii) Kesho ni jumanne.
Huarifu cheo au kazi anayofanya mtu.
Mifano:  i) Bichwa ni mwalimu.
            ii) Kigori si mchezaji.
Huarifu hali ya kuwa au kutokuwa na kitu fulani
                                                    Mifano:  i) Nives ana kalamu.
            ii) Nives hana kalamu.
Huarifu sifa ya au za mtu.
                                                    Mifano:  i) Okwi ni mchezaji.
          ii) Okwi si mchezaji.
Huarifu hali ya kuwa au kutokuwa mahali fulani.
         Mifano:  i) Mulokozi yuko darassani.
                          ii) Mulokozi hayuko darasani.
Anaendelea kusema kuwa mifano ya vitenzi hapo juu hueleza mambo mengi na si matendo. Hii ndio inafanya tukubali kutumia istilahi ya vitenzi.
Kwa kuhitimisha urafishaji wa vitenzi unafanywa na viambajengo vya vitenzi kama vile nafsi, njeo, viambajengo vya idadi, hali za vitenzi na kauli mbalimbali za vitenzi. Viambajengo hivi vina dhima yakuarifu kuhusu kiima au vinaonesha uhusiano kati kiima na kiarifu ambapo vinataarifu anayetenda tendo.




MAREJELEO
Habwe, J. na Karanja, P. (2007). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix.
Massamba, D. P. B. (2012). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.
Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha; Isimu na Nadharia. Mwanza: Serengeti Educational              
                    Publishers.
Mdee. J. S. (2007). Nadharia na Historia ya Leksikografia. Dar es Salaam: TUKI.
Mgullu, R. S. (2010). Mtaala wa Isimu: Fonetiki Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi:
                    Longhorn Publisher.
Nkwera, F. V. (2003). Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam:                   
                    Tanzania Publishing House.
Richard, J. et. al (1985). Dictionary of Applied Linguistics. Harlow: Longman.
TUKI. (1990). Kamusi ya Sanifu ya Isimu na Lugha: Dar es Salaam. TUKI.
Waihiga, G. (2010). Sarufi Fafanuzi ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publisher.



Kwa mujibu wa Sengo (2009) anafasili nadharia kuwa ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani kwa sababu fulani. Naye Mdee (2011) anaelezea nadharia kuwa ni mpango wa mawazo uliotungwa ili kueleza jinsi ya kufanya au kutekeleza jambo.  TUKI (2004) wanasema nadharia ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au kutekeleza jambo fulani.
Kwa ujumla nadharia ni mawazo, dhana au maelezo yanayotolewa kuelezea hali fulani: chanzo chake, muundo wake, utenda kazi wake na mwingiliano wake wa ndani na nje.
Baada ya kuangalia maana ya nadharia pia wataalamu mbalimbali wamezungumzia maana ya nadharia ya tafsiri kama ifuatavyo.
Halikadharika Newmark (1982) anasema kuwa kuna maana finyu na maana pana ya nadharia ya tafsiri. Katika maana finyu anafasiri kuwa ni mbinu inayofaa kutumika kutafsili matini ya aina fulani mahususi. Aidha katika kufasili maana pana anafasili kuwa ni jumla ya maarifa yanayopatikana na yatakayopatikana katika mchakato wa kutafsiri kuanzia msingi na kanuni za jumla hadi miongozo na mapendekezo muhimu. Anaendelea kusema kuwa kuna sababu za kuanzishwa kwa nadharia ya tafsiri ambazo ni wingi wa makosa katika tafsiri zilizochapishwa awali. Kuwepo kwa idadi kubwa ya mashirika na asasi zinazojishughulisha na kutafsiri matini mbalimbali na mfumuko wa istilahi katika taaluma mbalimbali hususani sayansi na teknolojia. Tunaona kuwa katika fasili ya Newmark haweki wazi ni matini gani hizo zinazopaswa kushughulikiwa.
Kwa mujibu wa Wanjara (2011) anasema kuwa nadharia ya tafsiri huchunguza mbinu mwafaka za kutumika katika mchakato wa kutafsiri kwa ufanisi matini ya aina fulani mahususi. Ni jumla ya mawazo au maarifa katika mchakato wa kufasiri misingi na kanuni za jumla na miongozo, mapendekezo na vidokezo muhimu. Wanjara pia katika fasili yake haweki wazi mbinu hizo zinatumika katika kutafsiri matini ipi na kanuni na miongozo inatumikaje kwenye hiyo matini.
Halikadhalika Mwansoko (2013) anasema kuwa nadharia ya tafsiri ni nguzo au muhimili wa nguzo ya tafsiri. Ni msingi wa kazi zote za tafsiri. Anaendelea kusema kuwa nadharia ya tafsiri ni maelezo kuntu ya vipengele vinavyopaswa kuzingatiwa na kila mfasiri kila akabiliwapo na kazi ya kufasiri. Mwansoko katika fasili yake haweki wazi misingi na vipengele vinatumika kwenye matini  ipi katika kutafsiri.
Kwa ujumla tunaona kuwa nadharia ya tafsiri ni mawazo au muhimili unaomwongoza mfasiri juu ya vipengele muhimu anavyopaswa kuvishughulikia katika mchakato wakufasili kutoka matini chanzi kwenda matini lengwa. Au ni maelezo muhimu kuhusu vipengele mbalimbali vya kifasiri ambavyo vinapaswa kufuatwa au kuzingatiwa na kila mfasiri pindi anapokabiliwa na kazi ya kufasiri.
Wataalamu mbalimbali wanafasili maana ya tafsiri kama ifuatavyo. Nida na Taber (1969) wanaelezea tafsiri kuwa ni uzalishaji upya wa ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe asili vya lugha lengwa vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi, kwanza kimaana na pili kimtindo.  Nida na Tiber wanaona kuwa katika tafsiri kitu muhimu ni kuzingatia maana na mtindo.
Cartford (1995) anasema tafsiri ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja ( lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana na hayo kwenda lugha nyingine (lugha lengwa). Catford anajikita katika ulinganifu wa mawazo katika kazi ya kutafsiri kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
Kwa mujibu wa TUKI (2002) wanaeleza kuwa tafsiri ni kutoa mawazo kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine bila ya kubadilisha maana. Fasili ya TUKI  imejikita katika maana yaani unapotafsiri hutakiwi kubadili maana iliyoko kwenye lugha moja.
Mshindo (2010) anasema kufasili ni kufafanua maana ya matini moja na kutayarisha baadae matini nyingine inayowiana nayo ambayo huitwa tafsiri na ambayo inawakilisha ujumbe uleule uliomo katika matini ya awali kwa kutumia lugha nyingine. Fasili  hii pia inajikita katika ujumbe na maana uwiane kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine. Kwa ujumla tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo, taarifa au ujumbe kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
Baada ya kuangalia istilahi mbalimbali zilizopo kwenye swali kama zilivyofafanuliwa na wataalamu, ufuatao ni umuhimu wa nadharia ya tafsiri katika taaluma ya tafsiri.
tunaona kuwa nadharia ya tafsiri inajumuisha nadharia mbalimbali ambazo hutumika katika kazi ya tafsiri. Nadharia ya Usawe wa Kimuundo, nadharia hii inatetewa na mtaalam Cartford (1995) anasema tunapofanya kazi ya kutafsiri tunatakiwa kuzingatia ulinganifu wa kimuundo kati ya matini chanzi na matini lengwa, maana yake ni kwamba muundo wa matini chanzi ujitokeze katika matini lengwa. Pia nadharia hii hutumika zaidi katika kutafsiri maandiko ya kidini hasa Biblia.
Nadharia nyingine ni nadharia ya Usawe wa Kidhima, watetezi wa nadharia hii ni pamoja na Nida na Taber (1969) wanaona kuwa usawe wa kidhima ni muhimu zaidi kuliko usawe wa kimuundo. Wafasiri wanapaswa kuhakikisha kwamba dhima ya matini chanzi pamoja na athari zake zinajitokeza katika matini lengwa. Yaani kama matini chanzi inawalenga watoto inapaswa iandikwe. Pia Nadharia ya Usawe wa Aina-matini, matini yoyote ile ifasiriwe kwa kuzingatia aina yake. Hii inamaana kwamba kazi itakayotokea itafanana na matini chanzi, kama matini chanzi ni ya kisheria itakapotafsiriwa matini lengwa nayo itaonekana kuwa ya kisheria. Nadharia Changamani hii ni nadharia tete inadai kwamba huwezi kufanya tafsiri kwa kutumia nadharia moja tu, kwa sababu hakuna nadharia inayojitosheleza yenyewe.
Baada ya kuangalia dhana mbalimbali za nadharia ya tafsiri kwa mujibu wa wataalamu, ufuatao ni umihumu wa nadharia ya tafsiri.
Wanjara (2011) anaelezea kuwa nadharia ya tafsiri husaidia kuonesha mbinu ambazo zinazofaa kutumiwa kufasilia aina mbalimbali za matini. Anaendelea kusema kuwa nadharia hizi za tafsiri husaidia au humpa mwosngozo mfasiri kujua mbinu muhimu ambazo hazina buni kufuatwa wakati wa kutafsiri matini yoyote.
             Mfano: mbinu hizo ni pamoja na tafsiri ya neno kwa neno, tafsiri sisisi, tafsiri ya kisemantiki na tafsiri ya kimawasiliano.
Hii ni kwa sababu mbinu hizi ndizo zinakidhi malengo makuu ya tafsiri, malengo hayo ni kutoa taarifa kuhusu mambo mbalimbali kwa kutumia lugha.
Newmark (1982) anasema kuwa nadharia ya tafsiri husaidia kutoa misingi, kanuni, sheria na vidokezo vya kufasiri matini na kuhakiki tafsiri, yaani matini zilizokwisha tafsiriwa.
               Mfano: mambo muhimu ambayo hayana budi kuzingatiwa wakati wa mchakato wa uchambuzi wa matini ni kusoma matini nzima na katika usomaji wa matini nzima dhumuni lake ni kubaini lengo la matini, kubaini lengo la mfasiri, kubaini wasomaji lengwa, umbo la matini lengwa na kubaini mtindo wa matini chanzi. Pia kusoma matini kwa mara ya mwisho. Anaendelea kusema kuwa kuna hatua muhimu za kufuata kama vie maandalizi, uchambuzi, uhawilishaji, kusawidi rasimu ya kwanza, kudurusu rasimu ya kwanza ili kupata rasimu ya pili, kusoma rasimu ya pili na mtu mwingine na kusawidi rasimu ya mwisho.
Mwansoko (2013) anaelezea kuwa nadharia ya tafsiri husaidia kueleza jinsi ya kuvishughulikia vipengele vidogovidogo katika tafsiri kama vile maana na umuhimu wa vistari, nukta, mkato, italiki, makosa ya uchapaji na mambo mengine kwa ujumla.
               Mfano: maana na nguvu za taarifa zinazobebwa na sitisri, uwasilishaji katika matini ya maudhui na fani yote, haya yana uzito sawa na mazingatio mengine ya zoezi la tafsiri. Mfano asiyejua utu si mtu. Katika mfano huu neno utu litatiliwa mkazo katika mchakato wa tafsiri tofauti na maneno mengine yaliyo katika matini hiyo.
Nadharia husaidia kupata visawe vya maneno katika lugha lengwa. Nider na Taber (1969) wanafafanua kwa kutumia nadharia ya usawe wa kidhima ambapo wanasema wafasiri wanapaswa kuhakikisha kwamba dhima ya matini chanzi pamoja na athari zake zinajitokeza katika matini lengwa. Yaani kama matini chanzi  inawalenga watoto inapaswa ipatiwe visawe vya maneno yanayoendana na watoto katika lugha lengwa.
Kwa kuhitimisha tunaona kuwa Kuna changamoto mbalimbali zinazoikumba kazi ya tafsiri kama vile uelewa mdogo watu wanaofanya kazi ya kutafsiri, kukiuka taratibu na kanuni za kazi za tafsiri kwa wafasiri mbalimbali na upotoshaji wa mawazo yaliyopo kwenye matini chanzi pale yanapohaulishwa kwenda kwenye matini lengwa kutokana na kutoelewa lugha vizuri.




MAREJELEO
Cartford, J. C. (1995). A Linguistic Theory of Translation. London: Heinmann.
Mdee, S, J. (2011). Kamusi ya Karne ya 21; Kaamusi ya Kiswahili yenye Uketo zaidi  katika 
                Karne Hii. Nairobi: Longman Publisher LTD.
Mshindo, H. B. (2010). Kufasiri na Tafsiri. Zanzibar: Chuo Kikuu cha Chukwan.
Mwansoko, H, J. (2013). Kitangulizi cha Tafsiri; Nadharia na Mbinu. Dar es Salaam.
TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es salaam: TUKI.
Newmark, P. (1982). Approaches to Transslation. Oxford: Pergamon Press.
Nida, E, & Taber, C. (1969). The Theory and Practice of Translation. London: Prentice Hall.
Sengo, T, S, Y, M. (2009). Fasihi za Kinchi, The registered.
TUKI. (2002). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam. TUKI.
Wanjara, S. F. (2011). Misingi ya Ukalimani na Tafsiri. Dar es salaam: Serengeti Education  

                    Publisher LTD.

Kapinga (1983), anafafanua  neno ngeli limetoka katika lugha ya Kihaya likiwa na maana ya kitu au vitu.
TUKI (1990), wanafafanua ngeli za nomino ni kundi moja la majina yaliyo na upatanisho wa kisarufi unaofanana na viambishi vya umoja na wingi vinavyofanana.
Mgullu (1999) anasema istilahi ngeli imechukuliwa kutoka lugha ya Kihaya. Katika lugha ya Kihaya, neno “Ngeli” lina maana ya aina ya kitu, anaendelea kusema kuwa ngeli ni utaratibu wa taaluma ya sarufi ya lugha katika kupanga aina za majina.
Massamba na wenzake (2012), wanafafanua  ngeli ni mgawanyiko wa aina mbalimbali za nomino katika mtazamo wa kisarufi katika fikra ya viashiria vya nomino katika aina nyingine za maneno zinazoambatana nazo.
Kwa ujumla, ngeli ni utaratibu au namna ya kuweka nomino katika makundi yanayofanana au kuwiana. Utaratibu huu unaweza kuwa ni ule unaoangalia upatanisho wa kisarufi wa viambishi awali vya umoja na wingi au ule unaoangalia viambishi awali vya umoja na wingi wa nomino. Aidha uainishaji wa ngeli za nomino ni utaratibu wa kupanga aina za majina katika makundi kwa kuzingatia kuwiana au kufanana kisifa.
Baada ya kuona fasihi ya ngeli kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali ufuatao ni upungufu wa uainishaji ngeli kwa kigezo cha kimofolojia na kisintakisia. Kwa kuanza na kigezo cha kimofolojia.
Kigezo cha kimofolojia; Obuch (2015), anaeleza kuwa hiki ni kigezo kikongwe zaidi ya vyote na kimetumika kwa muda mrefu katika uainishaji wa ngeli za Kiswahili. Katika kutumia kigezo hiki nomino hutumika katika ngeli kwa kuzingatia kufanana kwa viambishi vya mwanzo vya nomino husika. Yaani viambishi awali vya nomino vya umoja na wingi vinavyofanana huwekwa katika kundi moja la ngeli za nomino. Katika kigezo cha kimofolojia tunapata makundi tisa (09) ya ngeli za nomino kwa mujibu wa Obuchi (keshatajwa).
Ubora wa uainishaji ngeli kwa kigezo hiki ni kama ifuatavyo:- Obuchi (2015), kwanza kigezo cha kimofolojia ndiyo kimekuwa msingi au chimbuko la vigezo vingine vya uainishaji wa ngeli za nomino za Kiswahili.  Mfano uainishaji ngeli kisintakisa na kisemantiki, kwa mujibu wa Obuchi (keshatajwa), anaeleza hiki ndicho kigezo kikongwe katika uainishaji wa ngeli za nomino, vilevile  ndicho kigezo cha kwanza kuzipanga au kuziainisha  nomino za Kiswahili katika makundi.  Hivyo kuwawezesha wanafunzi wa lugha ya Kiswahili na watu wote wanaozifuatilia kwa ukaribu lugha hii kuweza kubaini makundi ya nomino.
Unatusaidia kujua uhusiano iliopo baina ya Kiswahili na lugha za kibantu. Uainishaji ngeli kimofolojia unadhihirisha uhusiano wa moja kwa moja kati ya kiswahili na kibantu ambapo nomino nyingi za kibantu zinaingia katika uainishaji huu.Upungufu wa uainishaji ngeli kwa kigezo cha kimofolojia ni kama ifuatavyo:
Kutozingatia hadhi ya nomino, uainishaji wa nomino katika kigezo hiki cha kimofolojia haujazingatia kabisa hadhi ya nomino zenyewe. Mgullu (1999), ngeli ya KI-VI ina nomino zenye hadhi tofauti lakini zimewekwa katika kundi moja la nomino. Mfano ngeli ya KI-VI
Umoja
Wingi
kiti
Viti
kikombe
Vikombe
kipofu
Vipofu
kijana
Vijana
kiongozi
Viongozi

Hivyo nomino kikombe, kiti, kipofu, kijana na kiongozi hazina hadhi sawa lakini zimechanganywa katika ngeli moja na hivyo kuonyesha udhaifu mkubwa katika kigezo hiki cha kimofolojia.
Baadhi ya ngeli hazina viambishi vya umoja na wingi; kigezo hiki kwa mujibu wa Obuchi (2015), kinaangalia viambishi awali vya umoja na wingi vya nomino. Udhaifu unaodhihirika ni badhi ya ngeli kutokuwa na viambishi vya umoja na wingi. Mfano ngeli ya 7,8 hazina kabisa viambishi vya umoja na wingi. Vlevile baadhi ya ngeli viambishi vya umoja au wingi  havipo dhahiri. Mfano ngeli ya 5



Ngeli ya 5
Umoja
Wingi
5
U/N
Ukucha
ø Kucha
Ukuta
ø Kuta
Unywele
ø Nyele
7
N/N
Nyundo
Nyundo
Kuku
Kuku
Samaki
Samaki
Kalamu
Kalamu
Nyumba
Nyumba
8
K/U
kuimba
kuimba
kusoma
kusoma
kucheza
kucheza

Hivyo kutokana na udhaifu tuliouona na dhahiri kigezo hiki kinahitaji marekebisho.
Upungufu mwingine ni baadhi ya ngeli zinatumia viambishi vinavyofanana. Kuna baadhi ya ngeli viambishi awali vya umoja vinafanana, mfano ngeli ya 1 na 2. Na baadhi ya ngeli viambishi vya wingi vinafanana mfano ngeli ya 3 na 6.
Mfano

Ngeli
Umoja
Wingi
1
M/Mu-wa
Mtoto
Watoto
Mtu
Watu
2
M/Mi
Mti
Miti
Mchungwa
Michungwa
Mkoba
Mikoba
3
Ji/ma
Jicho
Macho
Jina
Majina
6
U/m/ ø
ugonjwa
magonjwa

Uasi
maasi

Hivyo kiambishi ‘M’ umoja katika ngeli ya kwanza na ya pili vinafanana na kiambishi ‘ma’ wingi katika ngeli ya 3 na 6 pia vinafanana kutokana na kufanana kwa viambishi katika baadhi ya ngeli kunaashiria upungufu.Kwa kumalizia , kigezo cha kisintaksia kama ifuatavyo.
Mgullu (1999), anafafanua Uainishaji wa ngeli kwa kigezo cha kisintaksia huziainisha ngeli za nomino kwa kuzingatia uhusiano wa nomino na maneno mengine katika tungo.Obuchi (keshatajwa), anafafanua kuwa uainishaji wa ngeli kisintaksia umelenga kutatua baadhi ya matatizo yaliyoainishwa na kigezo cha kimofolojia kilichozingatia viambishi awali vya nomino.
Iribemwangi (2008), anasisitiza kwamba matataizo mengi ya kiuainishaji huenda yakashughulikiwa kwasababu uainishaji huu hutilia mkazo suala zima la uamilifu badala ya umbo au muundo wa nomino husika.
Ufuatayo ni ubora na upungufu wa uainishaji wa ngeli kwa kigezo cha kisintaksia kwa kuanza na ubora kama ifuatavyo.
Obuchi (2015), kigezo hiki cha uainishaji wa ngeli kisintaksia ulilenga kutatua matatizo ya nomino zote zinazowahusu wanadamu na wanyama kuekwa katika kundi moja la nomino kinyume na zilivyowekwa awali kwa mfano katika uainishaji wa kimofolojia viumbe hai na vitu vilikuwa vinaingia katka ngeli ya nne lakini katika uainishaji wa kisintaksia viumbe hai vyote vinaingia katika ngeli ya kwanza
Ngeli yu-a-wa
Mfano
(a)  Kipofu anakuja
Vipofu wanakuja
(b)  Kiongozi anahutubia
Viongozi wanahutubia.
Hivyo basi huu pia ni ubora wa kigezo cha kisintaksia kwasbabu uainishaji huu  umetofautisha viumbe hai na visivyo hai katika ngeli tofauti.
Obuchi (2015), kigezo hiki husaidia kujua/kutambua uhusiano uliopo baina ya nomino na maneno mengine kwa mfano nomino na vitenzi
Mfano;  (i) Uzi umekatika
                   Nyuzi zimekatika
                (ii) Mtoto mzuri anacheza
                   Watoto wazuri anacheza
Katika mfano (i) tunaona namna nomino ilivyo na uhusiano na kitenzi na katika mfano (ii) tunaona namana nomino ilivyo na uhusiano na kivumishi na kitenzi hivyo basi huu pia ni ubora wa uainshaji wa ngeli kwa kigezo cha kisintaksia kwa kumalizia na upungufu wa kigezo cha kisintaksia kama ifuatavyo;
Obuchi (2015), anafafanua kuwa upungufu wa kigezo cha kisintaksia ni  kutokugusia nomino zenyewe moja kwa moja. Kwa mfano kutumia vipatanishi vyake ambavyo vipatanishi hivyo huwekwa katika vitenzi, vivumishi na viwakilishi mfano ngeli ya tatu LI-Ya
 Mfano   Linauma
              yanauma

Hapa tunaona namna ambavyo nomino haijatajwa moja kwa moja na badala yake kipatanishi kimewekwa katika kitenzi. Hivyo basi huo ni upungufu mmoja wapo.
Vilevile kufanana kwa viambishi ngeli hua pia ni upungufu mmoja wapo kwa mfano.

Ngeli
Mifano ya sentensi
ii
U - I
Umeanguka
Imeanguka
vi
U
 Ulimponza
vii
U – YA
Umeenea
Yameenea
viii
U – ZI
Umeibiwa
Zimeibiwa

Hivyo basi hapa tunaona viambishi ngeli ya 2,6,7 na ya 8 vinafanana hivyo basi huu pia ni upungufu wa kigezo cha kisintakisia.
Mgullu (1999), anabainisha upungufu wa kigezo cha kisintaksia kuwa baadhi ya ngeli vina viambishi viwili na ni vya kilahaja zaidi si Kiswahili sanifu kwa mfano.


Ngeli
Umoja
Wingi
1
YU – A – WA
Mtoto yu aja
Mtoto anakuja
Watoto wanakuja

Hivyo basi huu pia ni upungufu wa kigezo cha kisintaksia ngeli ya kwanza yu-a-wa kiambishi yu hakitumiki katika kiswahlili sanifu.
Kwa ujumla uainishaji wa ngeli kwa kigezo cha kimofolojia na kisintaksia una ubora wake na una upungufu wake, hivyo basi wataalamu hawana budi kufanya utafiti zaidi ili kupata kigezo bora zaidi ambacho kitatumika katika uainishaji wa ngeli.



MAREJEO
Kapinga, C (1983). Sarufi maumbo ya Kiswahili sanifu. Dar es salaam: TUKI.
Mgull, R.S (1999). Mtaala wa Isimu, Fonetiki, fonolojia na mofolojia ya Kiswahili:                                           Nairobi, Longhom Publishers.
Massamba, D.P.B et al (2012) Sarufi Miundo ya Kiswahili sanifu (SAMIKISA).                                                                     Sarufi Miundo ya Kiswahili sanifu Sekondari  na
                                                    vyuo. Dar es salaam: TUKI.
Obuchi,S.M na Mlikhwana, A (2015). Muundo wa Kiswahili ngazi na vipengele.                                                                                Nairobi Kenya : Printing services Ltd.
TUKI (1990). Kamusi ya Kiswahili sanifu. Dar es salaam: TUKI.


AddToAny