Bassnett
(1993), anaeleza fasihi linganishi ni taaluma ya usomaji wa matini za tamaduni
tofauti ili kubaini mazingira ambayo kazi hizo zinapokutana na zinapoachana.
Fasili hii inagusia tu usomaji wa matini, japokuwa ulinganishi pia hufanyika
katika kazi za fasihi za tamaduni tofauti.
Wamitila
(2003) anaeleza dhana ya ulinganishi kuwa ni mbinu ya kuchunguza, kuchambua na
kuelezea sifa za mfanano wa matini za kifasihi. Dhana hii huenda pamoja na
dhana ya ulinganuzi ambapo uhusisha kuchambua sifa zinazofanana na kutofautiana
kwa matini moja na nyingine.
Kwa
ujumla, ulinganishi ni taaluma inayojishughulisha na ulinganishaji wa kazi za
fasihi. Taaluma hii inashughulikia utofauti na kufanana kwa fasihi ya makundi
mawili au zaidi ya kijamii, kiisimu, kiutamaduni, kihistoria, kiitikadi na
kiuchumi.
Jilala
(2016) anaelezaa kuwa vipengele vya kiulinganishi vinaweza kuwa katika makundi
matatu ambayo ni fani, maudhui na utamaduni. Kupitia vipengele hivyo vikubwa
vinaweza kuzaa misingi mingine midogo midogo ambayo inaweza kutumika katika ulinganishi
wa kazi mbalimbali za kifasihi. Mathalani, mtindo, falsafa, motifu, historia,
dhamira na utamaduni. Ufuatao ni ufafanuzi wa misingi ya ulinganishi.
Historia,
ni taaluma inayohusisha matukio mbalimbali ya wakati uliopita, uliopo na ujao
ili kujua wapi jamii ilipotoka na wapi inapoelekea. Kupitia historia,
mlinganishi wa kazi za kifasihi anaweza kulinganisha historia za kazi hizo za
jamii tofauti tofauti na kwa kipindi tofauti tofauti cha maisha ya jamii fulani
na kubaini ni wapi kazi hizo zinapoachana na kutofautiana. Mathalani
ulinganishi unapofanyika katika Utenzi wa
Nyakiru Kibi na Tamthiliya ya Mfalme
Edipode ni mfano mzuri wa kazi zafasihi zinazotoka katika jamii mbili
toauti amapo ni jamii ya Kitanzania na jamii ya Kimagharibi lakini katika
uelezaji wa kisa kuna ufanano wa kazi hizo ambapo zote zilieleza namna
Kanyamaishwa alivyomuua babaye na Edipode alivyomuua babaye kwa mikono yake na
mwisho wanajutia kosa la kumwaga damu ya baba zao.
Falsafa ni imani aliyonayo mtu au jamii yake
kuhusiana na kuwepo kwake na vitu vingine vinavyomzunguka, kuwepo kwao huelezea
ukweli halisi wa mambo ya kiulimwengu. Wanafasihi linganishi wanaweza kutumia
kipengele hiki kama msingi wa ulinganishi, kwa kubaini falsafa za jamii tofauti
tofauti. Mathalani katika kazi ya Hekaya
za Abubuasi katika hadithi ya Karamu ya Abunuasi, falsafa ya kifo si mwisho
wa kuishi imetokea pale ambapo mjomba wa Abunuasi alipomuijia ndotoni na
kuongea naye kuhusu mipango ya karamu vilevile katika kazi za fasihi ya
Kiswahili falsafa hii inajitokeza mfano katika Hadithi ya mtoto wa kambo alipokuwa akiongea na mama yake na
kumtimizia haja zake japo angali amekufa. Vilevile falsafa ya uganga nayo ipo
katika jamii za kimagharibi na za Kiafrika kwa kuangalia kazi za kifasihi kama Marimba ya Majaliwa na Hekaya za Abunuwasi.
Dhamira,
katika kazi za kifasihi dhamira ni wazo kuu linalobebwa na kazi yoyote ya
kifasihi. Wanaulinganisi pia huweza kutumia dhamira kama msingi wa ulinganisho,
hii ni kwasababu kuna dhamira za kiulimwenngu ambazo hugusa sehemu kubwa ya
watu ulimwenguni. Kwa mfano kifo, umaskini, utawala, ufisadi na imani potofu,
hivyo mlinganishi anaweza kuhusianisha dhamira katika jamii tofauti, katika
kipindi fulani cha maisha. Mathalani, riwaya ya Firauni iliyosheheni dhamira kama mapenzi, usaiti, uongo, imani na
potofu vilevile na kazi za kimagharini kama Alufu
Lela U Lela, tunapata dhamira kama kifo, masengenyo, manunguniko, kufanya
kazi kwa bidii, ubaguzi na usaliti. Japokuwa dhamira hizi zinafanana kwa kiasi
kikubwa lakini kuna dhamira zingine huigusa jamii kwa sehemu ndogo kabisa pia hubadilika kulingana na maendeleo ya
jamii.
Motifu,
ambacho ni kipengele radidi cha kifani na kimaudhui kinachojitokeza katika kazi
mbalimbali za kifasihi, katika kufanya ulinganishi wa kazi za kifasihi matifu
ni msingi unaoweza kutumiwa na kulinganisha kazi mbili tofauti. Motifu
zinazojitokeza ni kama: motifu ya safari, motifu ya bibi kizee, motifu ya mama
wa kambo, motifu ya mwanamke mshawishi. Katika kazi za fasihi za kimagharibi
motifu ya safari inajitokeza kwa wingi mfano katika tamthiliya ya Mfalme Edipode, Edipode alikuwa akisafiri kutoka Korintho kwenda Thebe,
vilevile katika Marimba ya Majaliwa,
Majaliwa alivyokuwa akimsaka kongoti ili aweze kurejesha marimba na alimsaka
nchi nzima pia katika Utenzi wa Nyakiru
Kibi, Nyakiru alitoka Bunyoro mpaka
Kiziba kwa lengo la kutawala na kupanua himaya.
Utamaduni
pia ni msingi wa ulinganishaji, hujumuisha mila desturi, lugha, mavazi na
chakula. Katika msingi huu mlinganishi anaweza kutumia kazi za jamii tofauti
tofauti kubaini ni wapi jamii hizo zinapo kutana katika utamaduni na kuachana
kwa sehemu ipi. Mathalani katika suala la kurithi mke baada ya mumewe kufariki,
lipo katika jamii za kimagharibi pamoja na jamii za Kiafrika mathalani katika
tamthiliya ya Mfalme Edipode, Edipode
alimrithi mke wa mfalme baada ya mfalme kufariki pia katika fasihi ya Kiswahili
katika Utenzi wa Nyakiru Kibi, Mukama
Bike anawauwa wanaume wenye wake wazuri na kisha kurithi wake zao. Vilevile
utofauti wa chakula katika jamii za kiafrika kazi za fasiihi zinzeleza aina ya
chakua kinachopikwa na kuandaliwa ni kama, ndizi, senene, viazi vitamu nyama za
mawindoni kama ilivyo oneshwa katika riwaya ya Bwana Myombokere na Bibi Bugonoka pamoja na Utenzi wa Nyakiru Kibi lakini katika kazi za fasihi za kimagharibi
aina ya vyakula ni kama mikate ya kumimina, samaki wa kukaangwa, divai kama
ilivyoelezwa katika Alufu Lela U
Lela.
Kwa
kuhitimisha, ulinganishi katika kazi za kifasihi huweza kufanywa kwa kuzingatia misingi mingi ya ulinganisho kwani
katika kazi hizo kuna vipengele vingi ambavyo kila kimoja kinahitaji kufanyiwa
ulinganishi.
MAREJELEO
Bassnet,
S (1993). Comparative Literature: A
Critical Introduction. Oxford: Blackwell
Jilala,
H. (2016) Misingi ya Fasihi Linganishi:
Nadharia Mbinu na Matumizi:
Dar es Salaam: Daudi
Publishing Company.
Mulokozi,
M. M (1998) Utenzi wa Nnyakiru Kibi.
Dar es Salaam: ECO Publishers
Wamitila,
K. W (2003). Kichocheo cha Fasihi
Istilahi na Nadharia:
Nairobi: Focus
Publication Ltd.
Sophocles:
Mushi, S. S (1939) Mfalme Edipode.
Nairobi: Oxford Universty Press
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com