1.0.Utangulizi
Riwaya
ya Kufikirika ni riwaya iliyotungwa
na mwandishi mashughuli Shaabani Robert mwaka 1967. Katika riwaya hii mwandishi
anaeleza juu ya mila na desturi zilizopitwa na wakati kuwa hazina nafasi katika
kipindi cha sasa. Mwandishi anaeleza kuwa jamii ya watu wakufikirika ilikuwa inaamini
juu ya uganga na mambo ya kijadi. Hivyo kupitia muhusika Utu busara alikuwa anaelimu
kubwa ya dunia. Utu busara alijiingiza katika kundi la utabiri ili aweze kuleta
mabadiliko katika nchi ya Kufikirika. Kutokana na utabiri wake mfalme na malkia
wanafanikiwa kupata mtoto na baadae Utu busara tena anakuwa mwalimu wa mtoto wa
mfalme na kuanza kumfundisha elimu ya dunia ambayo ni kinyume na matakwa ya
mfalme, baada ya kufukuzwa na mfalme, Utu busara anaamua kujiingiza katika
kilimo ambapo ikapelekea kukamatwa kwa kudhaniwa kuwa ni mjinga. Kutokana na
elimu na weledi alionao Utu busara anafanikiwa kumponya mtoto wa mfalme kwa
kutoa ushauri kuwa apelekwe hospitali. Mwisho mtoto wa mfalme anapona na
kufanya Utu busara kufanikiwa katika nia yake ya kuleta mabadiliko katika nchi
ya kufikirika.
Katika
kuhakiki na kuchambua riwaya hii ya Kufikirika
tutazingatia vipengele vya fani na maudhui. Hivyo tutaanza kwa kuchambua
vipengele vya maudhui ambavyo hujumuisha dhamira, ujumbe, migogoro, mtazamo, na
falsafa na kisha tutatalii kwa kina juu ya fani na vipengele vyake.
2.0.
Dhamira
TUKI
(2013) anafasi dhamira kuwa ni kiini cha jambo au habari iliyosimuliwa ama
kuandikwa, hasa katika fasihi. Katika riwaya ya Kufikirika mwandishi Shabaan Robert ameonesha dhamira kuu ni
ukombozi wa kiutamaduni. Kiujumla riwaya ya Kufikirika inajadili harakati
zinazofanywa na Utu busara za kupambana na tamaduni zilizopitwa na wakati.
Kupitia mhusika Utu busara mwandishi anaonesha kuwa mila na tamaduni
zilizopitwa na wakati hazina budi kutupiliwa mbali hasa katika kipindi hiki cha
sayansi na teknolojia.
Licha
ya dhamira kuu, pia mwandishi amejadili dhamira ndogondogo kupitia wahusika
lukuki ambao amewatumia katika riwaya hii, dhamira hizo ni kama zifuatazo:
2.1. Suala la uongozi
Mwandishi
Shaban Robert hakupuuzia suala la uongozi katika riwaya hii, anaonesha kuwa
viongozi wa nchi ni lazima wawe mstari wa mbele katika kuhakikisha maslahi ya
nchi yanalindwa na wananchi wanaishi kwa amani. Mwandishi anabainisha suala
hili kwa kumtumia mhusika mfalme (uk: 1-2)
“nimejaliwa kupata ufalme kuliko
wafalme wengine walio majirani zangu. Binafsi yangu
nimepigana vita vingi kulinda nchi
isitekwe na adui. Ushindi wa kila vita umenipa
utukufuwa namna ya pekee yake. Milki
yangu pana imeenea kaskazini, kusini, mashariki
na magharibi.”
2.2. Suala la ugumba na utasa
Mwandishi Shaban Robert hakusita kulieleza
suala la ugumba na utasa katika riwaya hii ambalo ndio lilipelekea kuibua
dhamira mbalimbali. Mwandishi anatumia mhusika mfalme na malkia katia kuonehsa
tatizo hili. Mwandishi anaonesha kuwa licha ya ujasili, uzalendo na furaha yote
aliyokuwa nayo Mfalme na Malkia lakini walijiona sio kitu kutokana na kukosa
mtoto, ambaye angekuja kurithi madaraka mara baada ya kufa mfalme. (uk 1)
“Alitazama huku
na huku na akawaza kuwa kama mahali pa juu hushikwa na mwezi au
nyota juu ya mbingu, na mahali pa joto kuwa
baridi, lakini nani atashinda mahali pake
akifariki”
Kutokana
na tatizo hili mfalme akatafuta kila njia ili aweze kupata mtoto. Hapa ndipo
mfalme alipoamua kuweka bayana tatizo lake ili aweze kusaidiwa.
2.3. Suala la Imani potofu
Mwandishi
ameonesha juu ya dhana potofu zilizojengeka katika vichwa vya watu wa
kufikirika juu ya mtu mwerevu na mjinga. Wanaona kuwa mjinga na mwelevu
hujulikana kutokana na kazi anayoifanya mtu, Utu busara alionekana kama mtu
mjinga kutokana na shunguli za kilimo aliyokuwa anaifanya halikadhalika
mfanyabiashara alionekana mwerevu kutokana na kazi yake. (uk 39)
“……… mtu wa kwanza alikuwa na umbo
kuza. Kazi yake ilikuwa ni biashara mjini. Ajali ya
kukamatwa ilimkuta akiwa amekaa kitako dukani
pake, Yeye alihesabiwa kuwa mwerevu. Mtu wa pili alikuwa na umbo la wastani.
Amali yake ilikuwa ni ukulima. Ajali ya kufanywa mahabusi wa kafara ilimkuta
shambani pake analima. Huyu alidhaniwa kuwa ni mjinga…...”
Kutokana
na mtazamo huu, hatimaye mwerevu aliweza kujinasua na kifo hicho, hivyo mwandishi Shaban Robert
anajaribu kutoa mwanga kwa jamii juu ya dhana potofu na kuitaka jamii kubadilika
ili kuendana na wakati.
Halikadhalika
Imani potofu imekisili katika jamii ya watu wa kufikirika kwani wanaamini juu
ya mambo ya jadi hasa uganga na kupuuzia huduma za kisasa kama vile hospitali.
Hivyo mwandishi Shaban Robert kupitia mhusika Utu busara anaitaka jamii
kuachana na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati kwani huweza kusababisha
hasara kubwa kwa jamii husika kama ilivyowapata watu wa kufikirika ambao
walipoteza vitu vingi kwa ajili ya uganga (uk 8-14).
2.4. Nafasi ya mwanamke
Mwandishi Shabaan Robert hakupuuza nafasi ya
mwanamke katika riwaya yake. Katika riwaya hii mwandishi amechora mwanamke katika
sura mbalimbali, sura hizo zimejitokeza kama ifuatavyo;
2.4.1
Mwanamke amechorwa kama mtu muhimu
katika jamii mwenye kutoa ushauri na ukakubalika.
Mwandishi
Shaaban Roberrt katika Riwaya ya Kufikirika
amemchora mwanamke kama kiumbe muhimu katika kutatua matatizo mbalimbali
yanayoikumba jamii kupitia mhusika mkuu Mfalme. Anathibitisha hili katika (uk
1) anasema;
“……. alikuwa tayari kupokea msaada
uliotolewa kwa hiyari na mwanamke lakini kulazimisha kutendewa msaada hakupenda.
Aliona kazi na faraju zitendwazo na wanamke katika maisha zilitosha kuwa mzigo
mzito juu yao……”
Hivyo
mwandishi anaonesha jinsi mwanamke anavyofanya mambo makubwa katika jamii,
hivyo anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.
2.4.2.
Mwanamke amechorwa kama mtu mvumilivu
Mwandishi
Shabaan Robert amemuonesha mwanamke kama mtu mwenye kuvumilia matatizo mbalimbali
yanayomkabili. Malkia licha ya kukumbwa na tatizo la kukosa mtoto hakuvunjika
moyo aliendeleza upendo wake kwa mfalme mpaka pale Mungu alipowajalia kupata
mtoto.
2.5.
Dhamira ya dharau na majivuno
Dhamira
hii imejitokeza pale ambapo mhusika mfanyabiashara alipokuwa gerezani alikuwa
anamdharau Utu busara. Kutokana na kazi aliyokuwanayo mfanyabiashara alijiona
kuwa anabusara kuliko mkulima (uk 40)
“……. Huwaje, wewe mvaa koja la
ushanga shingoni kama mwanamke kupata njia! Una sifa zaidi ujinga. Nashangaa kwanini hawakutakiwa
wajinga wawili kwa kafara hii………...”
2.5.
Umuhimu wa elimu
Suala la elimu ni miongoni mwa dhamira ambayo
mwandishi Shaaban Robert ameijadili katika riwaya ya Kufikirika. Mwandishi anaonesha kuwa elimu ni jambo la muhimu kwa
maisha ya mwanadam yeyote yule na kila elimu anayotolewa inakuwa na malengo
yake. Lakini elimu ikitolewa vibaya inaweza kuleta madhara kwa mhusika au jamii
kwa ujumla. Katika riwaya hii msanii anaonesha kuwa mtomto wa mfalme baada ya
kufikisha miaka saba alitafutiwa mwalimu wa kumfindisha. Mwalimu huyo alikuwa
mwalimu bora na matokeo yake mtoto alionesha usikivu, upokeaji wa mafunzo na
wapesi waakili lakini mwalimu huyu alionekana anakiuka matakwa ya mfalme na
baadae mtoto wa mfalme alitafutia mwalimu mwingine ambaye alimfundisha na kumpa
kazi bila kikomo tena bila ya mapumziko. Mwandishi anathibitisha hili (uk.28)
“Kwa akili yake kali kama wembe alielewa
pia kuwa na maarifa ya vitabu yanamanufaa
mengi
kwa wanadamu katika maisha lakini kama wembe ulivyo siku zote matumizi
mengi hufanya kuwa dafu; na kama
watoto wengine walivyo alitamani
pumziko”
Mwandishi
anasisitiza kuwa ingawa suala la elimu ni muhimu katika jamii likini ni muhimu
liende sambamba na michezo kwani mtoto wa mfalme alidhoofika kiafya kutokana na
kufundishwa mambo bila mapumziko na tiba yake alihitaji kafara ya watu wawili,
mjinga mmoja na mwerevu.
2.6
Dhamira ya matumizi mabaya ya mali
Mwandishi Shaaban Robert katika riwaya ya Kufikirika amazungumzia suala la
matumizi mabaya ya mali ambayo yalisababishwa na mfalme kukosa mtoto, waganga
walitumia sehemu kubwa ya mali ya nchi ya Kufikirika hadi ikapelekea matatizo
katika nchi ya Kufikirika lakini (uk
14).
“Nchi ambayo zamani ilikuwa ya shibe,
utajiri, nguo, tafrija na neema zote sasa ilikuwa imegeuka nchi ya njaa,
umaskini, uzito na uhitaji wa kila namna ulikuwa mbele ya watu…..”
Mwandishi
anaitaka jamii kwenda na wakati, kwani masuala ya uganga kwa kiasi kikubwa
yamepitwa na wakati na hayana faida yoyote kwa jamii zaidi ya kuleta madhara
kama yalivyo tokea katika nchi ya kufikirika.
2. Ujumbe
Kipengele
kingine ni ujumbe. Katika riwaya ya kufikirika kupitia dhamira mbalimbali
zinaweza kuibua ujumbe ufuatao.
Umoja
ni nguvu na utengano ni dhaifu. Mfano wananchi wa kufikirika walikuwa na umoja
katika kufanikisha ustawi wa nchi yao hali kadhalika watu wa kufikirika
walikuwa na umoja na ushirikiano katika kufanikisha mfalme wao anapata mtoto.
Jamii
isijiegemeze katika imani za kimila na kiutamaduni tu bali iangalie upande
mwingine. Hii inatokana na ukweli kwamba wanakufikirika walikuwa hawaamini
masuala ya hospitali badala yake walikuwa wanaamini mambo ya kimila na
kitamaduni.
Ujinga
na werevu wa mtu hupimwa kwa matendo na sio kazi anayoifanya. Hii inatokana na
watu wa kufikirika ambao walikuwa wanapima werevu na ujinga wa mtu kutokana na
kazi zao.
Ujumbe
mwingine ni kwamba viongozi lazima wadumishe sheria za nchi ili kuleta usawa na
amani katika nchi.
Hivyo
Shaaban Robert anaitaka jamii ibadilike kwa kuzingatia maonyo na maadili
yapatikanayo katika riwaya hii ya Kufikirika.
3.0 Migogoro
Kipengele
kingine ni migogoro, mgogoro ni mvutano kati ya pande mbili au zaidi. Mwandishi
Shaaban Robert katika riwaya ya Kufikirika
ameonesha migogoro mbalimbali kama vile; mgogoro wa kiuchumi, kijamii, kisiasa,
kiutamaduni na mgogoro wa nafsi.
Tukianza
na mgogoro wa kiuchumi, mwandishi ameonesha jinsi nchi ya kufikirika
ilivyoyumba kiuchumi kutokana na mali zote za nchi zilivyotumika katika kumtibu
mfalme na malkia na mwishowe shughuli za nchi zilisimama (Uk 8-12).
Pia
mgogoro wa kijamii, mwandishi ameonesha mgogoro wa mfalme na malkia kwa kukosa
mtoto, kwakua walijiona hawana umuhimu katika jamii ingawa walikua na mali
nyingi (uk 1-6).
Pia
mgogoro mwingine wa kijamii ni kati ya Mfalme na waganga kwani makundi matano
ya waganga waliokusudiwa kumtibu mfalme na malkia walishindwa kuwatibu (uk
8-13)
Mgogoro
mwingine wa kijamii ni kati ya mfalme na waliotakiwa kutolewa kafara, katika
nchi ya Kufikirika suala la mtu kutolewa kafara ni suala ambalo haliendani na
sheria za nchi ya Kufikirika hivyo mfalme alipinga swala hilo.
Vilevile
kuna mgogoro wa nafsi uliojitokeza kwa mfalme, jinsi mfalme alivyokua akiumia
juu ya kukosa mtoto kwa muda mrefu takribani miaka kumi baada ya kuoana na
malkia.
Pia
malikia alikua na mgogoro na nafsi yake juu ya kukosa mtoto kwa muda mrefu
tangu kuoana kwao.
Hali
kadhalika kuna mgogogro kati ya waziri mkuu na wajumbe juu ya kubadili mfumo wa
uongozi.
Pia
mgogoro kati ya ukale na usasa, mgogoro huu umejitokeza pale ambapo wananchi wa
kufikirika waliamini sana mambo ya ushirikina wakati Utubusara alikua akijaribu
kuwaelimisha juu ya mambo ya sayansi na teknolojia na wachane na mambo ya
zamani.
Pia
kuna mgogoro wa kisiasa, mwandishi ameonesha jinsi mfalme alivyokuwa ameegemea
kuongoza nchi yake kupitia mila na desturi, lakini tunaona jinsi Utubusara
alivyokuwa akijaribu kuishauri jamii ya kufikirika kuepukana na mila
zilizopitwa na wakati na waegeme katika sayansi na teknolojia ili waweze kuleta
mabadiliko.
4. Falsafa
Kiujumla
falsafa ni mchujo wa welekeo wa mawazo muhimu yaliyojitokeza kila mara katika
kazi mbalimbali za msanii (Senkoro 2011). Katika kazi hii mwandishi Shaaban
Robert anaamini kuwa mila na desturi zilizopitwa na wakati hazina nafasi katika
jamii ya sasa ya utandawazi.
5. Mtazamo
Mwandishi
Shaaban Robert anaonekana kuwa na mtazamo wa kimapinduzi, mwandishi anaona kuwa
jamii isiangalie mila na tamduni tu bali iangalie mambo ya sayansi na
teknolojia.
Baada
ya kuchambua vipengele vya maudhui vifuatavyo ni vipengele vya fani. Kiujumla
fani katika fasihi ni ule ufundi wa kisanaa anaotumia msanii katika kazi yake (Senkoro
2011). Katika kuchambua vipengele vya fani tutajikita katika muundo, mtindo,
wahusika, mandhari na matumimizi ya lugha.
6.0 Wahusika
Wahusika
ni viumbe waliokusudiwa wawakilishe dhana, mawazo au tabia za watu, katika kazi
za fasihi. Katika riwaya ya Kufikirika
mwandishi Shaaban Robert ametumia wahusika mbalimbali katika kuibua dhamira.
Badhi ya wahusika aliowatumia ni kama wafuatao;
6.1. Mfalme
Huyu
alikuwa ndiye kiongozi au mfalme wa nchi ya Kufikirika ambaye aliongoza vyema
na alikuwa mtu wa huruma na upendo na watu wake, alikuwa jasiri na mzalendo
aliyepigania haki za raia wake na kuzilinda sheria za nchi ya kufikirika, licha
ya mali na furaha yote aliyokuwa nayo mfalme lakini kwa kipindi kirefu cha
maisha yake alisumbuliwa na tatizo la kukosa mtoto.
6.
2. Malkia
Alikuwa
ni mke wa mfalme ambaye pia alikuwa anasumbuliwa na tatizo la utasa, ni
mwanamke mvumilivu na mwenye subira hivyo anapaswa kuigwa na jamii.
6.3.
Utu busara ujinga hasara
Alikuwa
ni mtu makini na mwenye upeo mkubwa katika kufikiria mambo, alitabiri kuzaliwa kwa
mtomto wa mfalme, baadaye akawa mwalimu wa mtoto wa mfalme na baadae tena
akajiingiza katika suala la ukulima. Anafaa kuigwa na jamii kutokana na hekima
na uelewa uliomsaidia kujikomboa kutoka kwenye vikwazo vyote alivyokumbana
navyo.
6.4.
Mwerevu
Huyu
alikuwa ni mfanyabiashara ambaye alionekana ni mwerevu kutokana na kazi yake,
ni mhusika aliyejaa dharau na majivuno. Kulingana na tabia ya dharau na
majivuno mhusika huyu hafai kuigwa katika jamii.
6.5.
Waziri mkuu
Ni
mhusika ambaye alitumia vitisho na nguvu katika kushawishi wajumbe kukubaliana
na ubadilishaji wa sheria za nchi ya Kufikirika.
7.0. Muundo
Senkoro
(2011) anaeleza kuwa katika kazi ya fasihi muundo ni mpango na mtiririko wa
visa na matukio. Katika riwaya ya Kufikirika
mwandishi ametumia muundo wa moja kwa moja ambapo amesimulia kitabu mwanzo hadi
mwisho. Katika kuipamba kazi yake mwandishi ameigawa riwaya katika sehemu
ndogondogo, kila sura inakichwa cha habari. Sura hizo ni kama vile Mfalme,
Waganga, Matokeo ya utabiri, Mtoto wa Mfalme na Kafara. Pia sura ya tano
ameigawa katika sehemu mbili ambazo ni Baraza na gereza.
7.1. Mtindo
Senkoro
(2011) aneeleza kuwa mtindo katika kazi ya fasihi ni namna ambayo msanii
hutunga kazi na kuipa sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha kanuni
zilizofuatwa kama ni za kimapokeo au kipekee. Katika Riwaya ya Kufikirika mwandishi ametumia mtindo wa
masimilizi yaani amesimulia matukio yote katika mtiririko unaofaa. Pia nafsi
zote zimetumika lakini pia ametumia mtindo wa ushairi katika (uk. 18-19).
7.2. Mandari
TUKI
(2013) wanafasili mandhari kuwa ni sura ya mahali. Katika riwaya hii mwandishi
ametumia mandari ya kufikirika, kwani hata nchi anayozungumzia ni ya
kufikirika, pia nchi zilizopakana na nchi ya Kufikirika ni za kufikirika kama
vile nchi ya majaribu na nchi ya anasa. Pia mwandishi ametumia mandhari halisi
kama vile gerezani, nyumbani kwa mfalme na bustanini (uk.1)
7.3.
Matumizi ya lugha
Shaabani
Robert katika riwaya ya Kufikirika
ametumia misemo nahau, misemo, nahau, metahali na tamathali za semi.
7.3.1. Methali
Baadhi ya methali ambazo mwandishi ametumia
katika riwaya hizi ni Nyumba ya mgumba haina matanga (uk.5), mwenye haya hazai (uk.6).
7.3.2
Misemo
Misemo
iliyotumika katika riwaya hii ni Dunia
haifichi siri (uk.6), maisha ni kma
kuwa katika bahari (uk. 24).
7.3.3 Tamathali za semi
Haya
ni maneno ambayo hutumiwa na wasanii wa kazi za fasihi ili kutia nguvu katika
maana na mtindo. Pia tamathali za semi hutumika ili kupamba lugha au
mazungumzo. Katika riwaya ya Kufikirika mwandishi
ametumia tamathali mbalimbali kama vile;
7.3.3.1
Tashibiha
TUKI
(2013) wanafasili tashibiha kuwa ni ufananisho au mlinganisho wa vitu viwili au
zaidi kwa kutumia maneno kama vile kama.
Katika riwaya hii mwandishi ametumia tashibiha kama vile kichwa chake kilishindiliwa kama gunia (uk.29), sauti ya waafrika ni kali
kama ile ya radi (uk.6), waliweza kunusa kama mbwa mwitu (uk.8)
7.3.3.2.
Tashihisi
Tashihisi ni kuvipa vitu sifa alizonazo binadamu.
Katika riwaya hii mwandishi amebainisha tashihisi zifuatazo, sauti ya ndege waliokuwa wakiimba matawini kwa kuagana na mchana ilikuwa na
simanzi masikioni (uk.1)
7.3.3.3
Sitiari
Hii
ni tamathali ambayo hulinganisha vitu bila kutumia viunganishi. Mwandishi wa
riwaya hii ametumia sitiari kama vile, mjinga
ni mnyama (uk. 41) na wanawake ni malaika (uk. 40).
7.3.3.4
Mubalagha
Ni
tamathali ya semi ambayo hukuza jambo au kutia chumvi. Katika riwaya ya Kufikirika mwandishi ametumia mbinu hii
katika (uk.11) siku hiyo kuni, mkaa, na
mafuta yote yalikwisha kwa kuchoma
hirisi hizo, moshi mwingi uliruka juu ukatanda kama wingu kubwa la mvua.
8.0.
Jina la kitabu
Jina
la kitabu Kufikirika linasadifu
yaliyomo, kwanza nchi yenyewe ya kufikirika ni nchi ambayo haipo hata katika
ramani ya dunia, mwandishi anaeleza kuwa hata mfalme mwenyewe haijui mipaka
yake na hata nchi zinazopakana nayo ni za kufikirika tu, pia hata katika mambo
ya kafara ni ya kufikirika tu kwani hata katika jamii zetu hayapo.
Kwa
kuhitimisha tunaweza kusema kuwa mwandishi Shaaban Robert katika riwaya ya
kufikirika kwa kiasi kikubwa ameonesha matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii
ya sasa na kuyatolea ufumbuzi.
MAREJELEO
Robert,
S. (1991). Kufikirika. Dar es Salaam:
Mkuki na Nyota Publishers.
Senkoro,
F.E.M.K (2011). Fasihi. Dar es Salaam: KAUTTU.
TUKI, (2013). Kamusi
ya Kiswahili Sanifu. Nairobi Kenya: Oxford University Press
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com