Flower
Flower

Wednesday, July 10, 2019

MATINI ZA KIFASIHI NA MATINI ZA KISAYANSI

1.1 Fasili ya dhana matini, matini ya kifasihi na matini ya kisayansi
Dhana ya matini, matini ya kifasihi na matini ya kisayansi zimefasiliwa na wataalamu tofauti tofauti kama ifuatavyo;

1.2 Dhana ya matini.
Kamusi Teule ya Kiswahili (2013) matini ni maelezo kuhusu jambo lolote lile ambalo limeandikwa au kunakiliwa. Mfano, hotuba na gazeti. Kwa mujibu wa Massamba (2009), anaeleza matini ni maelezo ya kitu ambayo ama yameandikwa na mtu au yamenukuliwa na ambayo yamekusudiwa kutumiwa kwa makusudi maalumu. Kulingana na maana hii ni wazi kwamba matini lazima iwe imeandikwa na iwe na makusudi maalumu.
Kwa ujumla matini ni wazo au mfululizo wa mawazo ambao hujitosheleza kimaana na ambao unahitaji kutafsiriwa. Hivyo basi katika tafsiri matini yaweza kuwa neno, kirai, kishazi, sentensi aya au kifungu cha habari. Katika uanishwaji wa matini, matini zimeainishwa kulingana na vigezo vitatu ambavyo ni kigezo cha matumizi ya istilahi, kigezo dhima kuu za lugha, na kigezo cha mada.
Kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (1996) matini huweza kuainishwa kwa kufuatana na mada, kwa kutumia kigezo hiki tunapata aina kuu tatu za matini, ambazo ni matini za kifasihi, matini za kisiasa na matini za kisayansi au kiufundi.


1.3 Maana ya matini za kifasihi
Mwansoko na wenzake (2013:42) anasema matini ya kifasihi ni matiniambazo huandikwa kwa lengo la kumnufaisha nafsi ya msomaji kwa kutumia sanaa ya lugha na Mfasili anabudi kuwa sehemu ya mwanalugha husika kama atahitaji kuifasili matini ya kifasihi.
Kwa ujumla matini ya kifasihi ni aina ya matini ambayo huwa  na sanaa ya lugha ambayo mwandishi huwa na wazo fulani katika hisia zake au kutokuwa na hisia ila anakuwa na hamu ya kukonga moyo wake kuiandikia hadhira anayoikusudia. 

1.4 Dhana ya matini ya kisayansi
Mwansoko na wenzake (2013:37) wanasema matini ya kisayansi ni aina ya matini inayoegemea utafiti na uchunguzi wa kina juu ya shughuli za kisayansi wenye uvumbuzi na ubunifu kutoka kwenye nchi zenye lugha zilizoendelea kwenda kwenye nchi changa. Mfano, Uhandisi, tiba, elektroniki, sayansi ya nyuklia,sayansi ya kompyuta,sayansi menyu zote (hisabati, biolojia,fizikia na kemia).
Kwa ujumla matini ya kisayansi ni aina ya  matini ambayo uegemea katika ugunduzi, uchunguzi na uchambuzi wa kisayansi ambayo inaweza kuhusu sayansi ya nyuklia, sayansi ya viumbe hai, sayansi ya mimea na masuala mengine yanayohusiana na sayansi na teknolojia.

2.0Tofauti za kiisimu na zisizo za kiisimu katika nduni ya matini ya kifasihi na matini ya kisayansi
Upo utofauti unaojitokeza katika nduni za matini za kifasihi na kisayansi ambao unajitokeza katika kigezo cha kisimu na kisicho cha kisimu. Utofauti huo ni kama ifuatavyo;

2.1 Tofauti za kiisimu
2.1.1 Matumizi ya michoro, grafu, vielelezo, picha, takwimu, fomula, marejeleo, majedwali, bibliografia.
Kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2013)anasema katika matini za kisayansi kuna matumizi ya vielelezo, takwimu na majedwali, vielelezo hivi inaonyesha namna kitu kinavyoongezeka au kupungua. Kwa mfano, uongezekaji wa joto katika mazingira. Pia katika hisabati na fizikia kuna grafu na michoro ya maumbo mbalimbali. Lakini katika matini za kifasihi kuna matumizi ya picha na taswira ambazo zinaficha ujumbe kwa hadhira. Mfano, katika ushairi kuna taswira ambazo mwandishi hutumia ili kujiweka tofauti na wengine. Vilevile katika riwaya kuna matumizi ya picha ambazo huwa na mvuto hususani riwaya za watoto. Hivyo, utofauti wa matini hizi ni katika utumizi wa vielelezo ambapo riwaya hazitumii grafu, bibliografia, majedwali, takwimu na matini za kisayansi zinatumia vielelezo hivyo.

2.1.2Utofauti katika mada
Kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2013) utofauti wa matini za kifasihi na kisayansi upo katika mada. Matini za kisayansi huwa na mada tofauti tofauti ambazo huusiana na sayansi na teknolojia. Kwa mfano, mada kuhusu umeme,maabara, ufuaji wa vyuma, katika fizikia, ukuaji, lishe, ubadilikaji katika baiolojia na mada ya maada katika kemia. Lakini katika matini za kifasihi mtunzi wa kazi ya kifasihi anaweza kuwa na wazo kuu na mawazo madogo madogo katika kubuni kazi ambayo inahusika na uhalisia wa kugusa hadhira fulani. Mfano, katika riwaya mtunzi anaweza kuelezea ukosefu wa ajira kwa vijana lakini ndani yake akaelezea umaskini, rushwa, wizi, unyanyasaji, wivu na uchu wa madaraka.Mfano, riwaya ya “Usiku Utakapokwisha’’. Hivyo utofauti wa matini ya kifasihi unaegemea wazo kuu ambalo ubeba kazi nzima ya fasihi kwa lengo la kuelimisha na mawazo mengine madogo madogo lakini matini ya kisayansi inakuwa na mada tofauti tofauti.

2.1.3Utofauti katikaMatumizi makubwa ya Istilahi
Katika matini ya kisayansi kuna kuwa na istilahi zinazoibuka baada ya ugunduzi wa kitu fulani cha kisayansi, istilahi hizo zinaweza kuchukua 5% hadi 10% katika kurudiwa kwake katika tafiti za matini ya sayansi na teknolojia kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2013). Baada ya ugunduzi wa teknolojia istilahi mpya hutokea. Mfano, digital decoder - visimbuzi. Flash- kinyonyi,Lakini matini ya kifasihi huwa hakuna matumizi makubwa ya istilahi bali huwa kuna  tamathali za semi kama vile sitiari, matumizi ya lugha ya taswira na picha, Matumizi ya lugha ya kifasihi huwa yanaburudisha sababu huwa na vionjo na kufikisha ujumbe kwa hadhira lengwa. Mfasiri inampasa kuelewa vionjo hivyo na kuvitafsiri vema katika lugha lengwa kwa kutafuta visawe vinavyoendana navyo. Kwa mfano, Gervas ni shupavu mithili ya Simba. Hivyo matini za kisayansi ndizo huwa na istilahi zenye kuendana na wakati wa teknolojia mpya kugundulika na uenea katika mazingira ya watumiaji tofauti na matini za kifasihi ambazo huwa na tamathali za semi, taswira na picha ambazo huwa na lengo kuu la utumikaji katika kazi ya kifasihi ya mwandishi.

2.1.4 Utofauti katika mtindo wa lugha
Mtindo wa lugha katika matini ya kisayansi huwa hazina mihemko na inamsimamo. Matini hizi  kiisimu huwa na sarufi ambayo katika matumizi yake ipo kauli ya kutendwa kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2013). Kwa mfano, Uchunguzi ulifanywa na daktari Leakey kuhusu binadamu wa kwanza, lakini mtindo wa lugha katika matini za kifasihi huwa na lugha ya kisanaa yenye mihemuko, ubunifu fulani na huweza kumtofautisha na msanii mwingine.   

2.1.5Matumizi makubwa ya nafsi ya kwanza wingi mahali pa nafsi ya kwanza umoja.Matini za kisayansi huwa na matumizi ya nafsi ya kwanza wingi mahali ambapo ilitakiwa itumike nafsi ya kwanza umoja kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2013). Mfano, tunakusudia – ninakusudia, lakini katika matini za fasihi kuna matumizi ya nafdi ya pili na nafsi ya tatu ambazo huwa zinamuelezea mhusika mkuu. 

2.1.6 Matumizi ya  kauli zisizoonyesha nafsi ya mtendaji.
Katika matini ya kisayansi kuna matumizi ya kauli zisizoonyesha nafsi ya mtendaji kwani hutumia kauli za pamoja  kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2013). Kwa mfano, inafikiriwa kuwa au ilipendekezwa na, lakini katika matini za kifasihi kuna matumizi ya kauli ya nafsi ya mtendaji ambayo inamuelezea mtendaji wa jambo fulani.

2.1.7 Matumizi ya umbo la ripoti ya kitaaluma
Matini za kisayansi zinakuwa na umbo la ripoti ya kitaalamu ambayo inaweza kujumuisha vitabu vya rejelea, maelekezo au notisi zinazoandikwa na kufuata mtindo wa kitaalamu, lakini katika  matini za kifasihi maranyingi hutumia nafsi ya pili kwa sababu mwandishi huwa anaelezea matukio ya mhusika mkuu anafanya nini na matendo yake ni mazuri au mabaya kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2013).

2.1.8Utumiaji wa vitenzi vya kidhahania. 
Matini za kisayansi huwa na vitenzi vya kidhahania katika uwasilishwaji wake. Mara nyingi ugunduzi ukikamilika huwa kuna na uwasilishwaji wa teknolojia na sayansi ambapo wawasilishaji hutumia vitenzi vya kidhahania kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2013).  Kwa mfano,chukua hatua, lakini katika matini za kifasihi kuna matumizi ya vitenzi vya kawaida na vitenzi vya kidhahania huwa havitumiki.

2.2 Tofauti zisizo za  kiisimu
2.2.1Utofauti katika Utamaduni
Matini ya kisayansi haiegemei utamaduni wowote sababu inaegemea kuwalenga watu wote. Matini ya kisayansi huwa na lengo la kuweka bayana ugunduzi wa teknolojia mpya ambayo huwa gumzo duniani kote ili kuchochea ununuzi wa kifaa kipya kilichogunduliwa kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2013). Mfano, ugunduzi wa dawa,katika masuala ya tiba na sayansi ya nyuklia. Lakini matini za kifasihi huwa inaegemea utamaduni wa jamii fulani. Mwandishi katika matini ya kifasihi huwa na wazo ambalo linaendana na tamaduni husika au anaweza akaandika kazi ya kifasihi kama nafsi ya kujilizisha yeye. Mfano, katika riwaya za watoto zinamlenga mhusika ambaye ni mtoto, ndani ya kazi Mwandishi anaweza kuelezea elimu ya kijinsia, manyanyaso na adha za watoto wa mitaani.Hivyo, matini za kifasihi huwa zinaelezea ujumbe kulingana na utamaduni wa nchi au jamii fulani kwa sababu ya muktadha husika. Fasihi ni zao la utamaduni wa jamii lakini ndani ya matini ya kisayansi utamaduni wake huwa ni wa ulimwengu wote. Kama kuna teknolojia mpya itahusu dunia nzima.

3.0 Hitimisho
Kwa ujumla matini zote za kifasihi na kisayansi utofautiana. Matini ya kifasihi huwa na ugumu katika kuitafsiri sababu Mfasiri anaweza akapewa kazi fulani ya kifasihi lakini asielewe mguso wa Mwandishi,hii ni kwasababu Mwandishi anaweza akaandika kazi bila mguso wowote yani akawa anajiburudisha. Katika matini ya kisayansi ina wepesi wa kuifasili sababu istilahi inayoibuka inaweza kupatiwa kisawe chake. Lakini matini hizi zote lazima Mfasili afuate mchakato na mikakati. Pia achague mbinu ambazo zitamsaidia kuifasili vema kazi yake ili iwe bora na kumpatia kipato.

MAREJELEO.
Massamba, D.P.B. (2009). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.
Mwansoko, H. J. M. (1996). Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu. Dar es Salaam: TUKI
Mwansoko, H.J.M. Mekacha, R.D.K. Masoko, D.L.W. Mtesigwa, P.C.K. (2013).Kitangulizi 
                  cha Tafsiri Nadharia na Mbinu. Dar es salam: TUKI.
TUKI, (2013). Kamusi Teule ya Kiswahili. Nairobi: East African Educational Publishers.

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny