Sehemu ya utangulizi imesheheni ufafanuzi wa dhana ya Fasihi ya Watoto pamoja na mkabala. Katika kiini cha swali, mikabala mitatu ya kufafanua Fasihi ya Watoto imebainishwa huku mapungufu na ubora wa mikabala hiyo ikielezwa pia pamoja na kueleza mkabala ambao ni faafu katika kufafanua Fasihi ya Watoto. Sehemu ya nne ni marejeleo, ambapo vyanzo na taarifa muhimu za kazi hii zimewekwa.
Mtesigwa (2009), akimnukuu Stem (1983), ameeleza kuwa, Mkabala ni mtazamo au jumla ya mitazamo inayofungamana na kupangiliwa kwa mantiki ndani ya mkondo wenye mwelekeo wa mawazo yanayofanana. Fasili hii inamaanisha kuwa, mkabala humtangulia mfasili katika kueleza jambo fulani. Hii inajidhihirisha katika fasili zifuatazo;-
Herman (2012), ameeleza kuwa Fasihi ya Watoto ni ile ambayo inawahusu watu walio chini ya umri wa miaka kumi nane. Fasili hii imejikita katika mkabala / kigezo cha umri pekee, jambo ambalo linachagiza utata kwani, Mwandishi hakueleza watoto hawa ni wale wanaoipika na kuiandaa kazi hiyo ya fasihi ama ni hadhira.
Naye Wamitila (2002), amefasili Fasihi ya Watoto kuwa, ni fasihi ambayo imekusudiwa kuelezwa kwa watoto. Kwa maana hiyo ili kuhakikisha kuwa, fasihi hii imekuwa na mvuto kwa watoto, ni lazima fasihi hiyo iweze kufanikisha kuiteka saikolojia ya watoto. Anaendelea kusema kuwa, fasihi ya watoto ni fasihi maalumu, kwa ajili ya watoto. Fasili hii imeegemea katika mkabala wa maudhui.
Kwa ujumla kuna mikabala mikuu mitatu ya kufafanua dhana ya Fasihi ya Watoto. Mikabala hiyo imejadiliwa katika sehemu ifuatayo, ikiwa imesheheni mifano mbalimbali pamoja na ubora na udhaifu wa mikabala hiyo. Kisha kubaini mkabala faafu katika kufafanua dhana ya Fasihi ya Watoto.
Wamitila (2016), amefasili dhana ya Fasihi ya Mtoto kwa kutumia mikabala miwili, kama inavyoonyeshwa katika sehemu ifuatayo;-
Mosi, Mkabala wa kihadhira, katika mkabala huu, inaelezwa kuwa Fasihi ya Watoto ni ile ambayo hadhira yake lengwa ni yake ni watoto. Mkabala huu unaiona ni Fasihi ya Watoto kama kazi ambayo huandaliwa kwa ajili ya watu maalumu tu, ambao ni watoto. Ubora wa mkabala huu ni kwamba, unamhusisha Mtoto moja kwa moja kama hadhira hivyo kuweka mipaka ya kiyakinifu kati ya Fasihi ya Wakubwa na Watoto. Mbali na ubora, mkabala huu una udhaifu kwani, haujaeleza fasihi hii inatungwa na nani. Jambo la kusisitiza hapa ni kwamba ili dhana ya Fasihi ya Watoto iwe bora lazima kutazama Nyanja zote kuanzia inapoandaliwa mpaka kumfikia mhusika ambaye ni mtoto.
Pili, mkabala wa kimaudhui na dhamira. Mkabala huu unaiona Fasihi ya Watoto kuwa, ni utanzu ambao maudhui na dhamira zake, zinawahusu watoto pekee. Kwa kiwango fulani mkabala huu unashabihiana na mkabala wa kihadhira kwani maudhui na dhamira siku zote humlenga hadhira, ambaye ni mtoto kulingana na maelezo yam kabala wa kidhamira na maudhui. Ubora wa mkabala huu ni kwamba, fasihi yoyote inajengwa kwa fani na maudhui. Hivyo kutumia kigezo hiki ni sahihi na kinajipambanua kwa urahisi zaidi.
Herman (keshatajwa:124), ameongeza mkabala wa tatu, ambao ni mkabala wa kiuandaaji. Katika mkabala huu, Fasihi ya Watoto inafasiliwa kuwa ni ile ambayo inatungwa na kuandaliwa na mtoto mwenyewe. Hii ina maana kuwa mtoto ndiye muumbaji halisi wa aina ya fasihi hii. Kwa kiwango kikubwa, mkabala huu una mashiko kwani unampa mtoto dhima ya kuiandaa kazi mwenyewe pasipo kuingiliwa na kitu kingine, hivyo tunategemea zao la kazi hiyo itawagusa watoto moja kwa moja.
Kwa ujumla, mikaba yote ina mashiko kwani kila mmoja unasimama katika wakati wake na wakati mwingine kuingiliana, ingawa kwa maoni yetu ni kwamba, mkabala ambao ni faafu zaidi ni ule wa kiuandishi kwasababu, Fasihi ya Watoto ikitungwa na kusimuliwa na mtoto itatumia lugha rahisi na inayoeleweka kwani hiyo ndiyo sifa yake kuu. Waandishi wengi wa leo wa kazi za Fasihi ya Watoto wanajaribu kutumia lugha nyepesi lakini si kwa kiwango ambacho kingepaswa kuwa kwani kuna uchanganyaji wa lugha za picha na urejeshi kama ilivyo katika riwaya ya Marimba ya Majaliwa.
Pia mkabala huu ni bora zaidi kwa sababu Fasihi ya Watoto ikitungwa na mtoto itakuwa fupi, hivyo haitapoteza uhalisia wake, tofauti na Fasihi nyingi za watoto ambazo kwa sasa zinaelekea kupoteza sifa yake kwani waandishi wanatunga ndefu na kusahahu uwezo wa mtoto kiakili na kimawanda. Mathalani riwaya ya Safari ya Prospa ina kurasa 166. Kwa watoto, kazi hii ni ndefu sana.
Pia, mkabala huu ni faafu kwani unaepuka masuala ya udhibiti. Kazi nyingi zinazoandaliwa kwa ajili ya watoto, aidha kutokana na kuhusianishwa na kuchangamanishwa na masuala fulani katika jamii, hufanya kupata vikwazo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kugusa tabaka tawala, hivyo ni vyema fasihi hiyo akaachiwa mtoto aiandae kutokana na uelewa wake. Ni imani kuwa atatumia lugha rahisi, kazi yake itakuwa fupi lakini pia si rahisi kuzungumzia mada ambazo ziko nje ya uwezo wake
Kwa kuhitimisha, mikabala ya kufafanua dhana ya Fasihi ya Watoto, haikinzani kwa kiwango kikubwa. Hii inatokana na sababu kuwa, ziko kazi nyingine hazijaundwa na watoto lakini zina kila sifa ya kuitwa Fasihi ya Watoto, ni pendekezo kuwa, jitihada zifanyike katika kumfikishia mtoto maana ya Fasihi ya Watoto kisha kumtengenezea yeye mwenyewe mazingira ya kuiandaa kazi hiyo pasi na kumwingilia. Hiyo itakuwa kazi bora kwani maudhui na fani atakazotumia mtoto huyo ni zile ambazo ziko ndani ya uwezo wake.
MAREJELEO
Herman, L. (2012). “Fantasia katika Fasihi ya Kiswahili kwa Watoto.” Katika P.S.
Malangwa & L.H. Bakize (wah) Kioo Cha Lugha. Jarida la Taasisi ya
Taaluma za Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Dar es Salaam.
122-134.
Lema, E na Dahl, E (2004). Safari ya Prospa. Dar es Salaam: E&D Vision Publishing
Mtesigwa P. C. K (2009). “Utayarishaji wa Vitabu vya Kufundishia Kiswahili kama Lugha ya
Kigeni”: Haja ya Kuzingatia Mkabala wa Mawasiliano. Dar es Salaam: TUKI.
Semzaba, E. (2008). Marimba ya Majaliwa. Dar es Salaam: E&D Vision Publishing.
Wamitila, K.W (2016) Kamusi Pevu ya Kiswahili. Dar ea salaam; Vide-Muwa Publishers L.td.
Wamitila, K. W. (2002). Uhakiki wa Fasihi, Misingi na Vipengele Vyake, Mombasa:
Phoenix Publishers Ltd.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com