Dhana
ya mofolojia imefasiliwa na wataalam mbalimbali kama vile
Tuki
(1990), wanafasili kuwa mofolojia ni tawi la isimu ambalo huchunguza maneno na
aina zake. Hivyo basi tawi hili husaidia kujua aina mbalimbali za maneno ambazo
hutumika katika lugha mbalimbali.
Besha
(2007) anafasili mofolojia kuwa ni taaluma inayojishughulisha na kuchambua
muundo wa maneno katika lugha. Mfano katika lugha ya Kiswahili kitenzi cheza kinaweza kuunda nomino mchezaji, katika mfano huu mwandishi
ametumia njia ya unominishaji kuunda nomino.
Obuchi
na Mukhwana (2015) wamefasili mofolojia kuwa ni taaluma inayohusu maneno.
Wanaendelea kufafanua kwamba taaluma hii hudhihirisha muundo wa maneno kwa
kurejelea mofu mbalimbali zenye kazi za kisarufi.
Kwa
ujumla mofolojia ni taaluma inayoshughulikia vipashio vya lugha katika kuunda
maneno. Yaani inachunguza na, kupambanua
maumbo ya maneno ambayo ni umbo la ndani na umbo la nje mfano
Umbo la ndani umbo
la nje
Mu+alimu mwalimu
Ki+ungu kyungu
Dhana
ya fonolojia imefasiliwa na wataalam mbalimbali kama vile
Massamba
na wenzake (2001) wamefasili fonolojia kuwa ni taaluma inayoshughulikia
uchambuzi wa mfumo wa sauti katika lugha. Yaani jinsi vipashio hivyo
vinavyofuatana na kuathiriana.
Fudge
(1973) anasema fonolojia ni kiwango kimoja wapo cha lugha fulani kilicho na
vipashio vidogo zaidi kuliko vipashio vingine vyote vya lugha. Vipashio vya
kifonolojia ni fonimu na alofoni.
Kwa
ujumla fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchambuzi wa mfumo
wa sauti katika lugha inayohusika. Na
kipashio kidogo cha fonolojia kinachobadili maana ya neno ni fonimu.
Vilevile
dhana ya sintaksia imefasiliwa na wataalam mbalimbali kama ifuatavyo:
Obuchi
na Mukhwana (2015) wanafasili sintaksia kuwa ni tawi la isimu linaloshughulikia
uchanganuzi, mpangilio na uhusiano wa vipashio katika kuunda sentensi.
Wanaendelea kusema kuwa katika taaluma hii tunahakiki namna maneno yanayopangwa
ili kuunda tungo na sentensi zenye maana.
Habwe
na karanja (2004) wanasema sintaksia ni utanzu wa isimu unaoshughulikia muundo
wa sentensi, na elementi nyingine zinazounda sentensi kama vile kategoria za
maneno, virai na vishazi.
Kwa
ujumla sintaksia ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchambuzi wa maneno
mbalimbali katika lugha jinsi yanavyoungana na kuunda sentensi.
Dhana
ya semantiki imefesiliwa na wataalam mbalimbali kama vile
Crystal
(1987) anasema semantiki ni utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha.
Anaendelea kusema kuwa taaluma ya semantiki ni taaluma ambayo hujishughulisha
na uchunguzi wa maana katika viwango vyote vya lugha.
Massamba
(2004) anafasili semantiki kuwa ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na uchunguzi
na uchambuzi wa maana za maneno na tungo katika lugha. Anaendelea kusema kuwa
semantiki imegawanyika katika makundi manne ambayo ni leksika, mantiki, muundo
na nadharia.
Kwa
ujumla semantiki ni utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha ya mwanadamu.
Taaluma
ya mofolojia inahusiana na kusigana na taaluma nyingine za kiisimu kama vile
fonolojia, sintaksia na semantiki. Kama ifuatavyo kwa kuanza na uhusiano na
kusigana kwa mofolojia na fonolojia:
Ufuatao
ni uhusiano wa mofolojia na fonolojia:
Taaluma
zote mbili hutegemeana katika mchakato wa uundaji wa maneno katika lugha
fulani, Massamba na wenzake (2013) wanashadidia hoja hii kwa kusema kuwa,
maneno huundwa na mofimu vilevile mofimu huundwa na sauti au vitamkwa. Aidha
uundaji wa mofimu hufuata taratibu maalum za mfuatano wa sauti za lugha husika.
Kwa mfano:
SAUTI MOFIMU MANENO
/p/
+/a/+/t/+/a/ pat-a pata
/k/+/a/+/b/+/a/ kab-a katkaba
/l/+/i/+/m/+/a/ lim-a lima.
Mfano
huo hapo juu umeonyesha jinsi ambavyo sauti huungana na kuunda mofimu katika
lugha ya Kiswahili.
Fonolojia
na mofolojia huhusiana katika kuunda michakato ya kimofofonolojia, Michakato hii
hupelekea kuundwa kwa kanuni ambazo husaidia kuunda maneno katika lugha ya
Kiswahili.maelezo haya yanashadadiwa na Massamba (2004) anaeleza kuwa
mofofonolojia ni taaluma ya isimu inayohusu uhusiano baina ya fonolojia na
mofolojia katika kuunda maneno. Miongoni mwa michakato ya kimofofonolojia ni kama
vile uyeyushaji, udondoshaji, muungano wa sauti. Kwa mfano muungano wa sauti
kanuni hii hutokea pale ambapo irabu ya mofimu moja inapokaribiana na irabu ya
mofimu nyingine katika mpaka wa mofimu. Irabu hizo huungana na kuzaa irabu moja.
UMBO
LA NDANI
UMBO LA NJE.
/ wa+enye/
wenye
/ma+ino/
meno
/wa+izi/
wezi
Uundaji
wa Mofimu za lugha ambao ni sehemu ya mofolojia hufuata taratibu maalum za
fonolojia ya lugha husika, ndio sababu kunauhusiano wa moja kati ya mofolojia
na fonolojia. Mfano mfuatano wa sauti ufuatao haukubaliki katika lugha ya
Kiswahili na kupelekea maandishi yasiyo maana katika lugha hii. Hoja hii
inashadidiwa na Massamba na wenzake 2013. Miongoni mwa sauti hizo ni kama
zifuatazo:
SAUTI ZENYE MPANGILIO UMBO LISILOKUBALIKA
LISILOKUBALIKA
/g/,
/d/, /k/, /a/
gdka
/m/,
/m/, /y/, /u/ mmyu.
Mpangilio
huu haukubaliki na hauleti maana katika lugha ya Kiswahili, hivyo basi
haukubaliki.
Mofolojia
na fonolojia husigana kama ifuatavyo:
Maana,
dhana hizi zina maana tofauti, vilevile utendaji wake kazi ni tofauti kwa
kuanza na mofolojia
kwa mujibu wa Besha (2007) anafasili mofolojia kuwa ni
taaluma inayojishughulisha na kuchambua muundo wa maneno katika lugha. Mfano
katika lugha ya Kiswahili kitenzi cheza kinaweza
kuunda nomino mchezaji, katika mfano
huu mwandishi ametumia njia ya unominishaji kuunda nomino. Hivyo basi mofolojia
hujihusha na uchunguzi wa maumbo mbalimbali ya maneno jinsi yanavyopaswa kuwa
na yanavyotumika katika lugha husika. Vilevile fonolojia Massamba na wenzake
(2001) wanafasilikuwa fonolojia ni taaluma inayoshughulikia uchambuzi wa mfumo
wa sauti katika lugha. Yaani jinsi vipashio hivyo vinavyofuatana na
kuathiriana. Katika fonolojia sauti mbalimbali hupangwa katika mpngilio
unaokubalika katika lugha inayohusika. Mpangilio huu wa sauti ni lazima ulete
maana inayokubalika katika lugha husika.
Taaluma
hizi hutofautian katika Ukongwe, Taaluma ya fonolojia ilianza hata kabla ya
mofolojia kwa sababu sauti ndiyo
iliyoanza, hivyobasi fonolojia ni kongwe yaani sauti zilianza ndipo maumbo ya
maneno yakafuatia. Kutokana na hali hii mofolojia imeibuka baada ya kuwapo kwa sauti mbalimbali
ambazo zinatumiwa katika lugha ambapo
sauti hizi hutumika katika mchakato wa uundaji wa maneno.
Mofolojia
na fonolojia husigana katika vipashio, kuna utofauti wa vipashio vya dhana
hizi, mofolojia kipashio chake kikuu ni mofu. TUKI (1990) wanafasili mofu kuwa
ni kipashio cha kimofolojia ambacho huwakilisha mofimu. Kwa hiyo mofu hutumika
kuwakilisha mofimu. Kipashio cha fonolojia ni fonimu, fonimu ni kipashio kidogo
cha kimofolojia kinachojihusisha na lugha mahususi. Vilevile kipashio hiki
hufanya kazi katika lugha mahususi na
utendaj kazi wake hutofautiana katika lugha moja na lugha nyingine. Mathalani
MOFU ZA
KISWAHILI FONIMU
ZA KISWAHILI
m-toto
/m/, /n/, /t/ na /k/
wa-toto
Katika
mfano tajwa m ni mofu funge ya umoja na wa ni mofu funge ya wingi. Vilevile /m/,
/n/, /t/ na /k/ ni mofimu za Kiswahili.
Ufuatao
ni uhusiano baina ya mofolojia na sintaksia:
Maumbo
ya kimofolojia huathiri vipengele vingine vya kisintaksia Rubanza (1996)anashadadia kwa kusema kuwa vipengele
ambavyo huathirika mara kwa mara ni umoja na wingi kwa sababu kutokana na
mabadiliko ya umbo kutoka umoja kwenda wingi hivyo vipengele vingine ambavyo hupatikana
katika tungo hiyo huathiriwa na mabadiliko hayo. Mathalani
UMOJA WINGI
i. Mwalimu anafundisha walimu wanafundisha
ii. Gauni limeibiwa
magauni yameibiwa
Katika
mifano tajwa viambishi “m na “w” katika kiima kwenye mfano wa kwanza vimeathiri
utokeaji wa viambishi “a” na “wa” katika kiarifu. Vivyo hivyo katika mfano wa
pili viambishi “g” na “m” katika kiima vimeathiri utokeaji wa viambishi cha
“li” na “ya” katika kiarifu.
Taaluma
hizi huhusiana katika uundaji wa sentensi, kwani sentensi huundwa na maneno vilevile
maneno huundwa na mofu. Hivyo huwezi kupata sentensi bila muunganiko wa mofu
unaotupatia maneno ambayo hutusaidia kuunda sentensi.
Ufuatao
ni utofauti baina ya mofolojia na sintaksia.
Hutofautiana
katika maana, Mofolojia na sintaksia hutofautiana katika maana kwani Obuchi na
Mukhwana (2015) wanasema mofolojia ni taaluma inayohusu maneno. Wanaendelea
kufafanua kwamba taaluma hii hudhihirisha muundo wa maneno kwa kurejelea mofu
mbalimbali zenye kazi za kisarufi. Hivyo maneno ni lazima yawe na muundo ambao
unakubalika na unaoleta maana miongoni mwa watumiaji wakati sintaksia ni utanzu wa isimu unaoshughulikia
muundo wa sentensi, na elementi nyingine zinazounda sentensi kama vile
kategoria za maneno, vikundi na vishazi. Vilevile ni lazima iwe na muundo ambao
unakubalika na kuleta maana katika lugha inayohusika. Mfano katika lugha ya
Kiswahili hutumia muundo wa kiima + kitenzi + yambwa (KTY) muundo huu ndiyo
unaokubalika na kuleta maana miundo mingine kama kitenzi + yambwa + kiima (TYK)
haukubaliki. Mathalani
i.
Mwalimu anafundisha darasani
kiima kitenzi yambwa.
ii.
Anafundisha darasani mwalimu.
Kitenzi yambwa kiima.
Katika mfano wa kwanza muundo uliotumika ndio
unaokubalika katika lugha ya Kiswahili na muundo uliotumika katika mfano wa
pili haukubaliki na hauleti maana iliyokusudiwa.
Pia hutofautiana katika suala la utendaji
dhana hizi hutofautiana katika utendaji kwani mofolojia hujihusisha na maumbo
ya maneno kwa ujumla ambayo hutumika katika lugha ya Kiswahili. Miundo ya
maneno hayo ni lazima ilete maana miongoni mwa watumiaji wake wakati sintaksia
huchunguza muundo mzima wa sentensi yaani muundo wa sentensi hiyo ni lazima
ukubalike miongoni mwa watumiaji wa lugha hiyo.
Ufuatao
ni uhusiano wa mofolojia na semantiki:
Maneno
yanayoundwa na mofolojia lazima yalete maana ambayo huwasilisha semantiki, katika
mofolojia maneno yanayoundwa ni lazima yawe katika mpangilio ambao unaeleweka.
Kutokana na muundo sahili wa maneno husaidia kupata neno au sentensi ambayo
imejikamilisha kimuundo na kimaana.
Utofauti
kati ya mofolojia na semantiki.
Maana,
Tuki (1990) wanasema mofolojia ni tawi
la isimu ambalo huchunguza maneno na aina zake. Hivyo basi tawi hili husaidia
kujua aina mbalimbali za maneno ambazo hutumika katika lugha mbalimbali mfano
Kiswahili. Aina za mneno hizo ni kama nomino,
kitenzi, kivumishi na zinginezo wakati semantiki ni taaluma inayochunguza
maana katika lugha fulani naye Crystal (1987) ameifafanua semantiki kuwa ni
utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha. Anaendelea kusema kuwa taaluma
ya semantiki ni taaluma ambayo hujishughulisha na uchunguzi wa maana katika
viwango vyote vya lugha. Hivyo basi ili sentensi ilete maana ni lazima muundo
wake uwe unaokubalika miongoni mwa watumiaji wa lugha husika.
Zinatofautiana
katika aina au matawi, Massamba (2004) anafafanua kuwa taaluma hizi
zinatofautiana katika aina au tanzu ambazo hutumika, kwa kuanza na mofolojia
ina tanzu mbili ambazo ni mofolojia ya mnyumbuliko wa maneno na mofolojia ya
uundaji wa maneno. Matawi haya hushirikiana katika utendaji kazi wake ili
kuleta muundo unaoeleweka. Semantiki ina matawi manne ambayo ni leksika,
mantiki muundo na nadharia. Vilevile tanzu hizi hushirikiana ili kuunda maneno
yenye maana.
Kwa
kuhitimisha tunaweza kusema kuwa ingawa taaluma ya mofolojia inahusiana na
kusigana na taaluma nyingine za kiisimu kama vile fonolojia, sintaksia na
semantiki lakini pia hakuna taaluma inayoweza kusimama peke yake na kukamilisha
sarufi ya lugha husika, taaluma zote hutegemeana, huathiriana na kukamilishana
katika isimu. Vilevile taaluma ya
mofolojia inamchango mkubwa katika isimu kama vile, husaidia kuainisha lugha
mbalimbali, ,huunda maneno mbalimbali na
kueleza kanuni za maathiliano ya vipashio katika maumbo ya maneno.
Besha,
R.M. (2007). Utangulizi wa Lugha na
Isimu. Dar es salaam: Macmillan Aidan.
Crystal,
D. (1987). The Cambridge Encyclopedia of
Language. New York: Oxford University
Press.
Fudge,
E.C (1973). Phonology, Selected Readings.
London: Cambridge University.
Habwe,
J na P, Karanja. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi:
Phoenix Publishers
Limited.
Massamba,
D. (2004) Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha
Dar es Salaam. TUKI-UNESCO-SIDA.
Massamba,
D. P.B. na Wenzake (2001). Sarufi Miundo
ya Kiswahili Sanifu: Sekondari na Vyuo.
Dar es Salaam.
TUKI.
Massamba
D.P.B. na Wenzake (2013) Fonolojia ya
Kiswahili Sanifu. Sekondari na Vyuo.Dar es
Salaam:
TUKI.
Obuchi,
M.O, na Mukhwana A. (2015) Muundo wa
Kiswahili. Ngazi na Vipengele. Nairobi The
Jomo Kenyatta
Foundation.
Rubanza,
Y.I (1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar
es salaam: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
TUKI
(1990). Kamusi ya Isimu na Lugha. Dar
es salaam: TUKI.
Ni taaluma ipi kuu kati ya zote ambayo isipokuwepo lugha haitoweza kutumika????
ReplyDelete