Massamba
na wenzake (1999:1) wanasema lugha ni mfumo wa sauti zenye kubeba maana na
ambazo hutumiwa na jamii fulani ya watu kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao.
Massamba
(2004:45) anafasili lugha kuwa ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo zimebuniwa na
jamii kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao. Fasili hii imejikita katika
kufasili lugha kama sauti za nasibu ambazo hakuna uhusiano wa moja kwa moja
kati ya kitaja na kitajwa vilevile imejikita katika sauti na kusahau ishara
kama njia ya mawasiliano.
Massamba
na wenzake (1999) wanakubalina kuwa lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo
hutumiwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao. Wana maana kuwa kwa
uasili binadamu hazaliwi na lugha bali huikuta katika jamii.
Kwa
ujumla lugha ni mfumo wa sauti za nasibu na ishara zilizokubaliwa na watu
zitumike katika mawasiliano. Vilevile fonolojia imefasiliwa na wataalamu
mbalimbali kama ifuatavyo:
Massamba
(2012:32) anafasili fonolojia kuwa ni tawi la isimu linalojishughulisha na
kuchunguza mifumo ya lugha mbalimbali za binadamu anaendelea kufafanua kuwa
kila lugha ya binadamu ina mfumo wake wa sauti ambao huongoza ujenzi wa maneno
ya lugha hiyo. Hivyo amejikita katika muundo na kazi ya sauti za lugha katika
lugha mbalimbaliza binadam.
Massamba
na wenzake (1999) wanaeleza kuwa fonolojia ni tawi la isimu ambalo
hujishughulisha na uchunguzi, uchambuzi na uanishaji wa sauti pambanuzi ambazo
hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za lugha za binadamu.
Obuchi
na Mukhwana (2015:73) wanafasili fonolojia ni kitendo kimojawapo cha muundo wa
lugha ambacho hushughulika na uchambuzi wa mfumo wa sauti zinazotumika katika
lugha fulani.
Kwa
ujumla fonolojia ni tawi la isimu linalojishughulisha na ujifunzaji wa mfumo wa
sauti za lugha maalumu. Yaani huangalia jinsi sauti zinavyotumika katika maneno
ya lugha maalumu ili kuleta maana.
Massamba
(2012:13) ameeleza sifa majumui za lugha kuwa ni sifa fulani ambazo zinaelekea kuchangiwa na lugha zote asilia. Zifuatazo ni sifa majumui
za lugha katika fonolojia.
Sifa
majumui halisia za lugha, Massamba (2012:12) anaeleza kwamba ni zile sifa za
kiisimu ambazo ni za kawaida katika lugha zote za binadamu. Katika kila lugha
kunakua na sifa ambazo zinapatikana katika lugha zote za asili. Mathalani lugha
zote za binadamu huwa na irabu katika orodha za sauti zake, mfano
lugha ya Kiswahili na Kiingereza zina irabu tano ambazo ni a, e, i, o na u
wakati
Mulokozi (2014) anasema Kiarabu kina jumla ya irabu tatu ambazo ni a, i,
na u. Katika sifa hii kinachozingatiwa sio idadi ya irabu bali uwepo wa irabu.
Vilevile
katika lugha zote huwa na utaratibu wa kuwa na irabu na konsonanti katika
kuunda silabi japo idadi ya konsonanti au irabu huweza kutofautiana kati ya lugha
moja hadi nyingine kama vile Kiswahili ambacho kina konsonanti 24 wakati
Kiarabu kina konsonanti 28 wakati Kiswahili kina irabu tano na Kiarabu kina
tatu. Bila kujali tofauti hizo za idadi ya konsonti na irabu, hoja ya msingi ni
kuwekwa pamoja kwa konsonanti na irabu katika kuunda silabi ya lugha nyingi
duniani.
Sifa
majumui za lugha pana, Massamba (2012:13) anaeleza kuwa ni zile sifa ambazo
zinapatikana katika lugha nyingi ingawa si zote. Mfano lugha nyingi za binadamu
huwa na irabu tano kama Kiswahili wakati lugha nyingine huwa na irabu saba au
zaidi na kuna lugha zenye irabu tatu tu kama Kiarabu.
Vilevile
katika lugha nyingi duniani kunakuwepo na sauti yenye sifa fulani ambayo huashiria
uwepo wa sauti nyenziye yenye kupingana na sifa hiyo.
Mfano; Sauti /g/ ambayo ni ghuna na /k/ ambayo si ghuna
Sauti /ng/ ambayo ni ghuna na /y/ ambayo si
ghuna
Maelezo
haya ya kufanana kwa sifa nyingi za lugha zinatokana na ukweli kuwa sauti zote
za binadamu zinachotwa katika bohari moja la sauti.
Vilevile
Chomi (2003) anasema kukosekana kwa sauti kama /ny/ katika lugha kama
Kiingereza kumesababisha wazungumzaji wa lugha hiyo kukutana na changamoto ya
kuzungumza maneno yenye sauti hiyo wanapojifunza Kiswahili ambapo hutumia sauti
/n/.
Mfano; nyoka (nioka)
nyanya (niana)
Anachokimaanisha
Chomi ni kwamba, ni vigumu kwa mzungumzaji ambaye si mzawa wa lugha mahsusi
kuwa mahiri katika lugha fulani, sifa hii ipo katika lugha nyingi ulimwenguni.
Sifa
majumui tabirifu, sifa hii huelezea kutabiri uwepo wa sifa fulani kutokana na
uwepo wa sifa nyingine kwa kutabiri tu. Mfano, toni ambayo imefasiliwa na
Mgullu (1999:37) kuwa ni kiwango cha kidatu pamoja na mabadiliko yake ambayo
wakati mtu anapotamka silabi au maneno kwa kawaida tukishagundua kwamba lugha
fulani ina toni juu na hubadili maana ya umbo linalohusika tutabashiri kwamba
lugha hiyo pia ina toni chini. Katika hali hii lugha inaweza kuwa na sauti
fulani kutokana na kuwepo kwa sauti nyenzie ambayo ni ya msingi au ambapo
unaweza kutabiri kuwapo kwa toni nyingine kutokana na toni fulani iliyopo.
Vilevile
Chomi (ameshatajwa) ameeleza uwepo wa sauti ghuna (+ghuna) katika lugha fulani
hufanya watu kutabiri na kukisia kuwa kuna sauti inayofanana na hiyo ambayo si
ghuna (-ghuna).
Mfano ; sauti ny (+ghuna) n (-ghuna)
sauti g
(+ghuna) k (-ghuna)
sauti p (-ghuna) b (+ghuna)
Ni
dhahiri kuwa sifa tabirifu zinajikita katika zile sifa ambazo zipo wazi katika
upande mmoja na kuhisi uwepo wa upande wa pili wa sifa hiyo kama pande mbili za
sarafu.
Kwa
kuhitimisha tunaweza kusema kuwa fonolojia kama taaluma inayoshughulika na
mpangilio wa sauti za lugha mahsusi inaonyesha wazi kuwa kuna lugha nyingi
zilizo na fonolojia inayofanana hata kama kuna tofauti ndogondogo ya sauti
maadamu zinatoka katika bohari moja ya lugha. Kwa kuwa kujifunza lugha mbalimbali hasa katika
kufahamu namna ya kutumia maana ya sauti za katika lugha ya binadamu
kunategemea taaluma ya Fonolojia, basi taaluma ya fonolojia ni ya muhimu sana katika kujifunza lugha na
haina budi kutiliwa mkazo.
MAREJELEO.
Chomi,
E. W. (2003) Fonetiki Matamshi ya Kiswahili. Sebha: Chuo Kikuu cha Libya.
Massamba,
D. (1990) Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha
Dar es Salaam. TUKI-UNESCO-SIDA.
Massamba,
D. P.B. na Wenzake (1999) Sarufi Miundo
ya Kiswahili Sanifu: Sekondari na Vyuo.
Dar es Salaam.
TUKI.
Mgullu,
R.S. (1999) Mtalaa wa Isimu, Fonetiki na
Fonolojia ya Lugha ya Kiswahili.
Nairobi.Longhorn
Publishers.
Massamba
D.P.B. na Wenzake (2004) Fonolojia ya
Kiswahili Sanifu. Sekondari na Vyuo.Dar es
Salaam: TUKI.
Massamba,
D. P.B. (2012) Misingi ya Fonolojia. Dar
es Salaam. TATAKI.
Mulokozi
M.M. (2014) Utangulizi wa Uchapishaji Kwa
Kiswahili: Historia ya Uchapishaji. Dar
es Salaam: TUKI
Obuchi,
M.O, na Mukhwana A. (2015) Muundo wa
Kiswahili. Ngazi na Vipengele. Nairobi The
Jomo Kenyatta
Foundation.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com