Kwa
kuanza na dhana ya dhamira imefasiliwa na wataalamu mbalimbali kama vile; Sengo
(2009) anasema dhamira ni sehemu ya maudhui na maudhui ni yale yasemwayo na
kazi ya fasihi. Ubora wa fasili hii ni kuwa mtaalamu huyu ameonyesha moja kwa
moja kuwa dhamira ni miongoni mwa kipengele ambacho kinapatikana katika upande
wa maudhui ambapo kutokana na hali hii humrahisishia msomaji moja kwa moja katika
usomaji wake. Udhaifu wa fasili hii ni kwamba mwandishi ameeleza fasili hii kwa
majumui baada ya kujikita moja kwa moja katika kipengele cha dhamira.
BAKIZA (2010), wanaeleza kuwa dhamira ni jambo
linalozungumzwa katika kazi ya fasihi. Ubora wa fasili hii ni kwamba
wamezingita lengo au jambo ambalo mwandishi amekusudia kulizungumzia katika
kazi yake. Udhaifu hawajaelezea kuwa dhamira zipo upande gani yaani upande wa
fani au maudhui.
Hivyo basi dhamira ni wazo kuu au mawazo
mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi na huwa sehemu tu ya maudhui,
aghalabu dhamira kuu ndio hujenga kiini cha kazi ya fasihi. Dhamira
zimegawanyika katika makundi makuuu mawili dhamira kuu na dhamira ndogo ndogo.
Dhana
ya ngomezi imefasiliwa na wataalama mbalimbali kama vile, Mng’aruthi (2008)
anafasili ngomezi kuwa ni kitengo cha maigizo ambapo ngoma hutumika kuwasilisha
ujumbe. Anaendelea kufafanua kuwa asili yake ni utamaduni wa kiafrika kabla ya
majilio ya wakoloni na miaka michahe baadae. Ubora wa fasili hii ni kuwa
mwandishi ameeleza asili ya ngomezi ni utamaduni wa waafrika wenyewe. Udhaifu
wa fasili hii ni kwamba ameiweka ngomezi kwenye kitengo cha maigizo wakati
ngomezi ni utanzu unaojitegemea.
Mulokozi (2017), anaeleza kuwa ngomezi ni
midundo fulani ya ngoma ambayo huwakilisha kauli fulani katika lugha ya kabila
hilo, anaendelea kueleza kwamba mara nyingi kauli hizo huwa ni za kishairi au
za mafumbo. Mulokozi akimnukuu Nketia (1963) anasema kuna namna tatu za upigaji
ngoma ambazo ni upigaji wa kalima, upigaji wa uashiriaji na upigaji wa
uchezaji. Ubora wa fasili hii ni kwamba, Mulokozi amezingatia suala la
kutofautisha utamaduni wa kabila moja na lingine kupitia midundo ya ngoma kwani
midundo hiyo hutofautiana baina ya kabila moja na kabila lingine. Fasili hii
inaudhaifu kwani haijaleza asili ya ngomezi.
Kwa
ujumla ngomezi ni utanzu ambao hutumia ngoma ili kufikisha ujumbe au kupashana
habari miongoni mwas jamii inayohusika midundo fulani ya ngoma huwakilisha
kauli fulani katika lugha ya kabila hilo na mara nyingi kauli hizo huwa ni za
kishairi au kimafumbo. Ngomezi inasifa mbalimbali kama vile; hutumia midundo
mbalimbali ya ngoma kufikisha ujumbe fulani, huhitaji mtaalamu wa ngoma, maana
ya midundo mbalimbali hubadilika kutoka jamii moja hadi nyingine hivyo basi ni
vigumu kwa jamii adui kutambua ujumbe wake.
Vilevile
ngano imefasiliwa na wataalam mbalimbali kama vile; Njogu na Chimerah (1999)
wanaeleza kuwa ngano ni hadithi zinazotoa mifano kadha wa kadha ya maisha ya
binadamu na matatizo anayokumbana nayo ulimwenguni. Ubora wa fasili hii ni
kwamba imezingatia mifano halisi ya mambo ambayo binadamu anakumbana nayo
kwenye ulimwengu. Lakini pia fasili hii inaudhaifu kwani haijazingatia baadhi
ya vipengele muhimu vya ngano kama vile wahusika, lugha, dhamira na ujummbe
Wamitila
(2003) anafasili ngano kuwa ni hadithi za kimapokeo ambazo hutumia wahusika wa
aina mbalimbali wakiwemo wanyama miti, au watu kusimulia tukio au kisa fulani
chenye mafunzo, anaendelea kueleza kuwa neno ngano hutumiwa katika jamii zetu
kwa maana pana sana kiasi kwamba aina nyingine ya simulizi au hadithi zinaweza
kujumuishwa kwenye kundi pana la ngano. Ubora wa fasili hii ni kwamba Wamitila
amezingatia vipengele muhimu vya ngano kama vile wahusika na ujumbe, udhaifu wa
fasili hii ni kwamba hajaeleza maana pana inayotumiwa kwenye ngano ni ipi?
Hivyo inakuwa ni vigumu kuielewa fasili hii moja kwa moja.
Kwa
ujumla ngano ni hadithi ya kimapokeo itumiayo wahusika kama wanyama, mazimwi,
miti na watu kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Ngano inavipera mbalimbali kama
ifuatavyo; Istiara ni hadithi zenye maana kuu mbili, yaani maana ya wazi na
maana fiche. Maana wazi huwakilisha maana iliyofichika, ambayo ili ieleweke
inahitaji ufahamu wamuktadha wa hadithi yenyewe. Kipera kingine ni kisasuli, ni
kipera cha ngano chenye kusimulia kuhusu chimbuko au asili ya jambo fulani.
Kipera kingine ni khurafa, hii ni ngano inayotumia wahusika wasiokuwa binadamu
hasa wanyama, mazimwi na mimea ili kuwasilisha matukio na ujumbe wake. Kipera
kingine ni mbazi hizi ni hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo wakati wa
maongezi au wakati wa kumkanya mtu. Ngano inasifa mbalimbali kama vile; huwa na
mianzo maalumu miongoni mwa mianzo hiyo ni kama
paukwa……….. pakawa,
hadithi….. hadithi.
Huwa na miisho maalum kama vile hadithi yangu inaishia hapa na
wakaishi kwa raha na mstarehe.
Huwa
na funzo fulani ambalo hutajwa mwishoni mwa ngano au hadithi husika. Husimuliwa
kwa lugha ya kinathari, hutumia mbinu nyingine za fasihi simulizi kama vile
nyimbo, methali, vitendawili na misemo. Huwa na wahusika mbalimbali kama vile
binadamu, wanyama, mazimwi, na maumbile. Huwa na muundo wa moja kwa moja na
masimulizi yake huwa ni ya wakati uliopita.
Baada
ya kufafanua dhana muhimu za kwenye swali letu zifuatazo ni dhamira za ngano na
ngomezi na nafasi yake katika jamii. Kwa kuanza na dhamira za ngano na nafasi
yake katika jamii tumejadili kama ifuatavyo;
Ngano
hubeba dhamira ya wema kuushinda ubaya, dhamira hii inapatikana katika ngano
nyingi za Kiswahili. Mulokozi (2017) anashadidia kuwa mara nyingi ngano kwa
kupitia kipera cha khurafa huwa na pande mbili upande wa wema na upande wa
uovu. Anaendelea kusema kuwa mhusika mkuu wa kila upande huwakilisha tabia
fulani inayopatikana katika jamii vivyo hivyo ngano huwa ni kielelezo cha ubaya
au uzuri wa tabia hiyo. Mara nyingi wanyama wenye nguvu ndio huwaonea wanyama
wasio na nguvu, hatimaye wanyama wanaoonewa hushinda na wenye nguvu hushindwa.
Mathalani katika ngano ifuatayo;
Sungra na Fisi
Paukwa
………….. pakawa.
Hapo zamani za kale, Sungura na
Fisi walikuwa marafiki walioshibana kwelikweli walipendana hata wakaamua
kujenga kibanda ambacho wao walikiita nyumba na wakaishi humo pamoja. Siku moja
Tembo alitembelea maeneo yao hakukuwa na dalili ya amani kutembelewa na tembo
kwani alipofika tu alipiga teke kibanda chao nacho kikakatika kwa kuvunjika
vipande vipande.
Fisi alijaribu kumzuia tembo
asiendelee kufanya uharibifu zaidi loo! Aliambulia kuvunjwa mbavu mbili za
kushoto Sungura alijaribu kuhoji kwanini Tembo alimvunja mbavu Fisi basi Tembo
aliporidhishwa na fujo zake kwa mwendo wa maringo akaondoka. Sungura na Fisi
walijizoazoa na kujiganga.
Baada ya siku tatu walikijenga
kibanda chao. Safari hii walitumia mbao imara kutoka msitu wa mukula. Fahari ya
macho kibanda kilipendeza ikavutia viumbe wote msituni ili kuepusha kuvamiwa na
tembo walitegesha utelezi katika njia ya kuja kwao. Tembo alipata taarifa za
mtego huo hivyo hakuthubutu tena kuwafuata.
Sungura na fisi wakaishi raha
mstarehe.
Hivyo
basi katika ngano tajwa inathibitisha wema unavyoushinda ubaya kwa kupitia
wahusika Sungura na Fisi ambao ni wema na mhusika Tembo ambaye ni si mwema.
Katika jamii suala la wema kushinda ubaya linanafasi kubwa kwani tunaona suala
la wema lnafaida na jinsi watu wanavyotenda wema wanawafundisha watu ambao
wanatenda mabaya kuacha tabia hizo kwani hazina faida yoyote.
Ngano
hubeba dhamira ya umoja na ushirikiano, Mulokozi (2017) anafafanua hilo kwa
kueleza kuwa khurafa hutumia wahusika wasiokuwa binadamu ili kuwasilisha
matukio au ujumbe wake. Hivyo tunaona kuwa wahusika hao wasiokuwa binadamu
mfano wanyama hushirikiana kufanya mambo mbalimbali yenye manufaa kwao. Pia kwa
upande wa kipera cha mbazi ambacho hubeba suala la umoja na ushirikiano miongoni
mwa wanajamii. Mathalani pale ambapo masimulizi yanatolewa kwa wanajamii na watu
wenye umri mkubwa, wanapotoa maonyo kwa jamii husika hasa wakati wa jioni.
Mfano wa ngano hiyo ni kama ifuatavyo:
Mama
na ndege
Hapo kale palikuwa na mwanamke mmoja
ambaye alikuwa hazai alitafuta kila njia ya kufanikiwa siku moja wakati akiwa
porini alikutana na ndege, ndege yule akamuuliza ewe mama unakosa gani? Hata
kuja kukata kuni peke yako mama akamweleza ndege ya kwamba hakukuwa na kosa
lolote ila shida yake ilikuwa mtoto – angefurahi kama ndege angeweza kumpa
maarifa ya kupata mtoto.
Ndege huyo akamsikitikia sana mama
huyo naye akajitolea kumsaidia ili apate mtoto alimpa dawa akameza. Ndege
akamwambia mama huyo ya kwamba atazaa msichana na akampa onyo ya kwamba hata
siku moja msichana huyo asije akafika kwenye pori la Matindiringoma. Mama
akaenda zake nyumbani baada ya muda si mrefu alijifunga na baadae akajifungua
mtoto wa kike. Alimlea mtoto huyo hadi akawa mkubwa akafikia umri wa kuolewa.
Siku zote mama yake alimkanya sana mtoto wake asije akathubutu kwenda poli la
Matiringoma. Mtoto aliyashika sana maneno ya mama yake.
Katika
hadithi hii suala la umoja na ushirikiano linajidhihirisha pale ambapo ndege
anampa dawa mama ambayo imemsaidia kupata mtoto. Hivyo basi dhamira hii ina dhima kubwa katika jamii kwani huonya
jamiii au wanajamii wanaopatikana katika maeneo hayo waendane na tamaduni
ambazo zinakubalika vilevile zinapatikana katika jamii husika.
Ngano
hubeba dhamira ya maadili, Mastin (2008) anasema kuwa katika jamii kuna
miongozo ambayo huiongoza jamii kuhusu lipi la kufanya na lipi si la kufanya.
Anaendelea kusema mwenendo wa mtu katika jamii ni lazima ufuate yale mambo
yanayokubalika katika jamii. Dhamira hii imejitokeza katika kipera cha mbazi
kwani kipera hiki husisitiza kuonya jamii kwa kutumia methali mathalani katika
mfano wa mbazi ifuatayo;
Asiyesikia la mkuu huvunjika guu
Mzee mwinyi alimshauri kijana wake Hamidu
asiwe na tamaa kwa kutamani vya watu. Siku zote alimuusia ya kwamba, tamaa ni
mbaya na mwisho wake ni majuto. Ilitokea siku moja, Hamidu akamuaga baba yake
juu ya safari yake ya kwenda kijiji jirani. Baba yake alimuuliza mwanae. Ni nini
alitaka kwenda kufanya huko Hamidu alijibu kulikuwa na sherehe ya rafiki yake
ambaye angepata jiko siku tatu zijazo.
Mzee Mwinyi alimruhusu Hamidu aende
katika sherhe lakini akamkumbusha kuwa asitamani cha watu. Naye Hamidu
alikubali na kuondoka zake kumbe Hamidu alidanganya, hakwenda katika sherehe
bali aliungana na marafiki zake wanne wakaenda mjini kwa lengo la kuvamia duka
la mpemba mmoja aliyependwa na watu kwa sababu ya ukarimu wake walifika mjini
wakapanga mkakati. Kisha wakapanga mkakati kisha wakavamia katika duka usiku wa
manane wakiendelea kupora mali, wapiti njia walishtuka kuona hali isiyo kuwa ya
kawaida katika duka lile. Hatimaye waligundua uwapo wa wezi ndipo wakapiga
kelele watu walijaa Hamidu na wenzake walipigwa sana. Isingekuwa uwapo wa
askari wa doria usiku ule, Hamidu na wenzake wangeuawa. Wakiendelea kuvuja damu
walichukuliwa mpaka kituo kidogo cha polisi. Askari mmoja alimsogelea Hamidu na
kumwambia, wewe ni kijana mdogo sana. Bil shaka hukusikiliza ushauri wa wazazi
wako, siku zote, “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu”
Hivyo
basi dhamira hii inamchango mkubwa katika jamii kwani husaidia kurekebisha au
kufunza jamii juu ya mambo mbalimbali ambayo yanakubalika katika jamii zao.
Mathalani kwa kupitia hadithi hizi watoto hujifunza maadili mema kupitia
wahusika ambao hupatikana katika hadithi husika.
Ngano
hubeba dhamira ya malezi, Samweli (2015) anaeleza kuwa dhamira ya malezi
inajitokeza kwenye ngano mbalimbali zilizokusudiwa kuhimiza malezi bora kwa
watoto katika ngano hizo zinasisitiza kuwa mtoto anapaswa kupewa malezi mema
kwani akisha kuwa mtu mzima itakuwa vigumu kumrekebisha. Aidha zinasisitiza mtoto
asiye lelewa vizuri dunia itamfundisha kwa kumpa adhabu mbalimbali kwa kufanya
matendo yake maovu, anafafanua kuwa katika jamii za kiafrika malezi ni jambo
lililopewa kipaumbele sana na lilikuwa jukumu la wazazi na jamii nzima. Suala
la malezi hujidhihirisha katika vipera mbalimbali vya ngano mathalani kipera
cha mbazi kifuatacho:
Asiye sikia la mkuu huvunjia guu.
Hapo zamani za kale paliondokea mtu
na mkewe. Watu hawa walikaa kwa muda mrefu bila kupata mtoto. Wakashauriana
kwenda kwa mganga ili awapatie mtoto walipofika kwa mganga akawaambia watoe
mbuzi wawili na kuku mmoja mweupe wakatoa. Yule mganga baada kupata hivyo vitu
akafinyanga udongo akaupulizia madawa yake na kuunuizia, alipomaliza kufanya
hivyo akawapa masharti wale wazee kuwa mtoto watakaye mzaa mwiko wake ni
kunyeshewa mvua. Basi siku si nyingi yule mke akashika mimba akazaa mtoto. Yule
mtoto akakua kama kawaida ya mtoto maranyingi alikuwa akienda kucheza na
wenzake. Wazazi wake walimuonya kuwa asicheze kwenye mvua. Siku moja alienda
kucheza na wenzake mbali sana kufika kule mawingu yakatanda yeye kuona vile akawaaga
wenzake ili awahi kufika nyumbani wenzake wakamwabia kuwa kama akiwaacha
watampiga basi yule mtoto ikabidi asiondoke kwani atapigwa na wenzake wakati
akisubiri mawingu yakazidi. Mwishowe wakaamua kurudi nyumbani mama yake kuona
hivyo kule nyumbani akaanza kuimba.
Mama: wewe katope ogopa hiyo mvua
Mtoto: ninakuja mama, ninakuja.
Wakati huo wote mvua ilikuwa
ikinyesha sana mwishowe yule mtoto akaanza kumong’onyoka kwanza mkono
ulidondoka wakati anakimbia kabla hajafika mbali mguu ulikatika pia, kufika mlangoni
mwili wote ulipolonyoka na akafa hapohapo. Wazazi wakabaki katika hali ileile
ya zamani. Yale masharti aliyowapa hawakuyafuata.
Dhamira
ya malezi inadhima kubwa katika jamii kwani husaidia kuwalea watoto katika
misingi inayofaa na inayokubalika katika jamii.
Ngano
hubeba dhamira ya mapenzi, suala la hili linajitokeza katika ngano mbalimbali
mathalani katika kipera cha khurafa ambacho hutumia wahusika wanyama kuelezea
mapenzi ya dhati na mapenzi yasiyo ya dhati pia kipera cha kisasuli kinaonyesha mapenzi ya dhati na mapenzi yasiyo
ya dhati kupita asili ya maumbile ya wanyama mbalimbali kama vile chanzo cha
jongoo kuwa na miguu mingi, chanzo cha nyoka kutokuwa na miguu ambapo hadithi
hizo huonyesha jinsi m mapenzi ya dhati kwa mwenzake na kumshawisihi afanye
jambo flani ambalo hupelekea mwenzake
kupata madhara. Vilevile mapenzi ya dhati yanajitokeza pale ambapo wanyama
wanashirikiana katika mambo mbalimbali. Mathalani katika kisasuli cha Mbuzi kuwa na mkia mfupi ambacho kimesimuliwa kama ifuatavyo;
Hapo zamani za kale mbuzi na kondoo
walikuwa marafiki waliishi pamoja katika nyumba yao iliyokuwa pembezoni kidogo
ya mji. Walipendana na walishirikiana kazi mbalimbali mbuzi alikua na mkia
mrefu kama wa ng’ombe. Aliupenda mkia wake kwasababu ulimsaidia kufukuza nzi na
wadudu wengine wasumbufu kondoo alikuwa na mkai mnene ulionona mafuta. Kila
walipotaka kupika wali kondoo aliweka sufuria juu ya moto, sufuria ikipata
moto, anaweka mkia wake na kutoa mafuta wakapata kupikia.
Mbuzi hakufurahia kuona kuwa rafiki
yake kila siku ndiye anayetoa mafuta akaamua kumsaidia. Siku hiyo, mbuzi
aliweka sufuria juu ya moto, sufuria lilipopata moto na kuwa jekundu mbuzi
aliweka mkia wale loo! Mkia ulinasa hapohapo mbuzi akakimbia kuelekea mtoni
ambako alitumbukia ndani ya maji na kufanikiwa kuuzima moto ule hatahivyo, mkia
wa mbuzi uliungua vibaya na kufanya kibaki kipande kidogo kama tukionacho leo.
Hiyo ndiyo sababu ya mbuzi kuwa na
mkia mfupi.
Dhamira
ya mapenzi ina dhima kubwa katika jamii kwani huwaasa wanajamii waishi kwa
upendo na kushauriana mambo mazuri ambayo yanamanufaa kwa jamii yao.
Fauka
ya dhamira za ngano na dhima zake katika jamii, zifuatazo ni dhamira za ngomezi
na dhima zake katika jamii ya leo.
Ngomezi
hubeba dhamira ya umoja na ushirikiano, hii ni dhamira ambayo inajidhihirisha
kupitia midundo ya ngoma za makabila mbalimbali. Mulokozi na Kahigi (1979)
wanasema kuwa kutoka awali waafrika walikuwa na umoja, waliishi kwa
kushirikiana na hata kufanya kazi pamoja kwa umoja. Wanaendelea kusema kuwa
umoja ulijidhihirisha kwa kupitia ngoma, kazi na mikutano ya vijiji. Kwa hiyo
kwa kupitia ngomezi au fasihi ya ngoma wanajamii wamekuwa wakishirikiana katika
mambo mbalimbali. Mathalani katika upigaji wa uashiriaji wanajamii wamekuwa
wakishirikiana katika shughuli mbalimbali kutokana na uashiriaji fulani ambao
unawasilishwa kwa kupitia ngoma au fasihi ya ngoma dhamira hii inajidhihirisaha
katika midundo ya ngoma ya kabila la wabena inayoitwa mtuli hupigwa kwa lengo la kuwaita watu wajumuike pamoja kwenye
sherehe mbalimbali kama harusi, kuzaliwa kwa mtoto, mtoto kuota meno na sherehe
nyinginezo. Hivyobasi dhamira hii inadhima kubwa katika jamii kwani husaidia
kukamilisha mambo mbalimbali kwa wakati maalumu.
Dhamira
ya vita, Mng’aruthi (2008) anashadidia hoja hii kwa kueleza kuwa, kupitia ngoma
au ngomezi tunapata dhamira ya vita ambapo midundo mbalimbali ya ngoma
huashiria kuanza au kuisha kwa vita. Mdundo wa kuanza vita hutofatiana na
mdundo wa kumaliza vita ili kuondoa utatanishi. Hivyo basi kwa kupitia ngomezi
watu wa jamii fulani wanapovamiwa wakisikia midundo ya aina ya kuanza kwa vita
hujitahadharisha kwa lengo la kupambana na adui, vivyo hivyo wakisikia midundo
ya kuisha kwa vita huendelea na shughuli zao. Mathalani katika mfano wa ngoma
ya vita kutoka kwa wa Akan wa huko Ghana ambao umetafsiriwa na Mulokozi (2017)
kama ifuatavyo:
Walinzi imara kama chuma moto umezao mataifa
Fimbo ya chuma iliyopingika
Tumeichupa bahari
Je tutashindwa na wangwa?
Je moto uwapo mkubwa utaizidi bahari
Njooni walinzi njooni walinzi. Dhamira hii inadhima
kubwa kwa jamii ya sasa kwani kuwataarifu wanajamii kujitahadharisha juu ya
vita hiyo.
Ngomezi
hubeba dhamira ya uongozi, midundo ya ngoma mbalimbali ambazo hupigwa kwenye
makabila mbalimbali yanayopatikana Afrika huwa na dhamira ya kuashiria kuwa
kiongozi wa jamii hiyo au mfalme anasimikwa, hivyo wanajamii huwasili eneo hilo
kwa lengo la kushuhudia namna kiongozi huyo anavyosimikwa au kuwasili kwa
kiongozi wa kabila lingine kwenye jamii yao. Mfano katika jamii ya wabena
hutumia midundo ya ngoma inayoitwa mtuli
kutoa taarifa za uongozi. Dhamira hii inanafasi kubwa katika jamii kwani kwa
kupitia midundo ya ngoma huwaarifu wanajamii kuhusu mambo ambayo yanatendeka
katika jamii husika.
Dhamira
ya kutunza na kurithisha amali za jamii, Katika jamii mbalimbali za Afrika watu
huweza kutunza na kurithisha amali za jamii kupitia midundo mbalimbali ya ngoma
zinazoendana na utamaduni wao, Mng’aruthi (2008) anashadadia jambo hili kwa
kutolea mfano wa midundo ya ngoma kutoka katika kabila la Wajaluo ambayo
hupigwa kwa lengo la kuwaondoa mashetani kati yao. Pia anaeleza kuwa waswahili huamini kuwa
mashetani wapo na huwakumbuka watu, jambo hili litokeapo ngoma flani huchezwa
kwa midundo ya kipekee ambayo huwasiliana na mashetani hao. Anatolea mifano ya
midundo ya ngoma ambazo hutumika kupinga mashetani kama vile kisokota, kaputa,
kibwengo, kitimiri na kumba. Dhamira hii inanafasi kubwa katika jamii kwani
husaidia kukuza mila na desturi za jamii mbalimbali, midundo
ngoma hizo hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Kwa
ujumla ngomezi na ngano hupatikana katika jamii mbalimbali za kiafrika na zina
dhima mbalimbali ambazo husaidia kuijenga na kuiimarisha jamii katika misingi
inayofaa kwani kupitia ngomezi na ngano jamii huweza kupata mafunzo ambayo yan
tija kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.
MAREJELEO.
BAKIZA (2010). Kamusi ya Kiswahili Fasasha. Oxford University Press East
Africa Limited
Kenya.
Mastin,
L. (2008). A Cultural Journey through the
English Lexicon. Harvard: Havard University
Press.
Mng’aruthi,
K.T. (2008). Fasihi simulizi na
Utamaduni. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Mulokozi,
M. M. (1989). Tanzu za Fasihi Simulizi MULIKA
21:1-24. Dar es Salaam: TUKI.
Mulokozi,
M. M. (2017). Utangulizi wa Fasihi ya
Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI.
Njogu,
K. na Chimerah, R. (1999), Ufundishaji wa
Fasihi Nadharia na Mbinu. Jomo Kenyatta:
Foundation Nairobi, Kenya.
Samwel,
M. (2015). Umahiri katika Fasihi ya
Kiswahili. Dar es Salaam: Mevel Publisher.
Sengo,
T. Y. S. M. (2009). Sengo na Fasihi za
Kinchi. Dar es salaam: AERA Kisahili Researcher
Product
Wamitila,
K. W. (2003), Kamusi ya Fasihi na Nadharia. Focus Publications Ltd.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com