Odera,
(1990) anasema, Falsafa ni taaluma ambayo kanuni za msingi kuhusu asili, binadamu
na jamii huchunguzwa na kujadiliwa. Pia, Sodipo, (1993)
anasema kuwa, Falsafa ni udadisi unaohusu dhana na kanuni zinazotuongoza kuhusu
uzoefu au mazoea kuhusiana na maadili, dini, sharia, saikolojia, hisroria,
sayansi za jamii na siasa. Hivyo, Falsafa ni mawazo ambayo watu katika jamii
wanaamini kuwa ni kweli na yanafanya mawazo hayo kuendelea kutawala misingi ya
maisha toka kizazi kimoja adi kingine.
Kuhusu
Falsafa ya Kiafrika wataalamu kama vile Placide Temples (1959), Oruka (1990) na
Mbiti (1990), wameifafanua dhana hii ya Falsafa ya Kiafrika kuwa ni fikra au
mitazamo wanayoishughulikia waafrika
wenyewe na watu wengine ambao sio waafrika lakini wanakubaliana naa mila na
tamaduni za waafrika na fasihi simulizi za Kiafrika. Hivyo Falsafa ya Kiafrika ni
ile ambayo imejikita katika mifumo ya kijamii, mila, desturi na fasihi simulizi
za Kiafrika. Kwa ujumla Falsafa ya Kiafrika ni mawazo ya Waafrika wenyewe juu
ya mambo mbalimbali wanayofanya kama
vile imani juu ya maisha, mila, desturi na jinsi ya kushirikiana katika jamii
na kutafuta suluhisho juu ya matatizo au changamoto zinazowakabili.
Placide
Temples alizaliwa tarehe 18/10/1906, katika mji wa Barcal huko Ubeligiji na
alifariki 9/10/1977 akiwa na miaka sabini (70). Katika kipindi cha uhai wake
aliishi Kongo kwa miaka 29. Aliwachunguza Waafrika walioishi Kongo hususani
kabila la Waruba na akabaini kuwa Waafrika wana tamaduni zao zinazojikita
katika fasihi simulizi. Hivyo aliandika kitabu chake kilichoitwa “The Bantu
Philosophy” mwaka (1945). Katika kitabu hicho anapinga mawazo ya wazungu kwa kusema kuwa “Waafrikaa wana falsafa yao”.
Temples alitumia hoja kadhaa katika kutetea mawazo yake, kama vile imani ya
kichawi, hofu ya uhai na kifo, nguvu uhai, suala la ndoa na dhana ya uduara.
Katika
kujibu swali hili riwaya ya “Marimba ya
Majaliwa” ndio iliyotumika. Riwaya hii imeandikwa na Edwin Semzaba, mwaka
(2015). Riwaya hii inamuelezea mhusika Majaliwa mtoto mdogo akiwa na umri wa miaka 13 pekee. Majaliwa
alizunguka Tanzania nzima akisaka Marimba yake ya nyuzi ishirini. Katika safari
zake alitumia ungo na fagio huku akisaidiwa na bibi yake ambaye alikuwa ni mzimu
katika kuyapata Marimba yake. Mwandishi amemuonyesha mhusika Majaliwa
akikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo upinzani mkali kutoka kwa mzimu wa
babu yake lakini kwa juhudi za Majaliwa akisaidiwa na mzimu wa bibi yake
alifanikiwa kuipata Marimba yake kutoka kwa Kongoti Nachienga na kufanikiwa
kushinda shindano la kumtafuta bigwa wa marimba Tanzania. Yafuatayo ni mawazo
ya Temples kuhusu Falsafa ya Kiafrika yanayojitokeza katika riwaya hii na jinsi
yanavyohalisika katika jamii ya Waafrika wa leo.
Falsafa
ya Uchawi, Temples anaamini kwamba Waafrika wanategemea sana nguvu za kichawi
na wanaona kwamba wanapopata matatizo hutegemea imani za kichawi ili kupata
masuluhisho ya matatizo yao. Katika riwaya hii suala la uchawi limejitokeza
mara nyingi. Mfano mwandishi amemuonyesha mhusika Majaliwa na Bibi yake
wakisafiri mikoa mbalimbali kwa kutumia ungo na fagio. Vilevile Majaliwa
alitumia jiwe la kichawi la “Rubi” alilopewa na bibi yake kwa ajili ya kupata
chakula. Na Majaliwa alishiba bila ya chakula kupita kinywani. Kudhihirisha
haya mwandishi anasema;
“….mara Bibi aliukalia ule ufagio
akiwa ameushika kwa mikono miwili. “Panda”, akamwambia Majaliwa. Alipokwisha
kupanda, ule ufagio ukaruka juu kwa kasi. Kufumba na kufumbua, Majaliwa
alijikuta yuko angani, mji wa Zanzibar ukionekana mdogo mfano wa ramani kubwa …(UK
20).”
“…. Nilipokwambia shika iyo Rubin a
kukariri yale maneno basi chakula cha wale watu wawili hakikuingia kwenye
matumbo yao, bali kiliingia kwenye tumbo lako. Chakula chote, pamoja na soda na
maji waliyokunywa… (UK21).”
Hivyo
hata katika jamii za Waafrika wa leo, suala la uchawi linajitokeza katika jamii
mbalimbali. Mfano katika jamii za Wafipa, Wakamba, Wajaluo, Waibo, Waluba na
Wasukuma ni miongoni mwa jamii za Waafrika wanaotumia uchawi katika shughuli
mbalimbali kama vile kusafiria, kuwasiliana na kinga dhidi ya mifugo yao.
Falsafa
ya Uduara, Temples anasema kuwa Waafrika hupenda vitu vya umbo la duara kama
vile; ngoma, nyumba, sufuria na sahani kwani huamini kuwa ni vitu vizuri. Pia
hufanya shughuli mbalimbali katika umbo la uduara kama vile, kula na kucheza ngoma.
Katika riwaya hii mwandishi ameonesha vitu kama bangili, sahani na ungo
uliokuwa ukitumika kama ni chombo cha kusafiria. Pia ameonesha utamaduni wa
watu wa kucheza ngoma katika umbo la duara wakiamini ni moja ya ishara ya umoja na upendo. Kudhihirisha dai
hili mwandishi anasema;
“….mara Bibi akasema “ ungo
unakaribia kutua katika uwanja wa ungo wa kimataifa wa Hanang katika mda mfupi
ujao….(UK 95).”
“…muhudumu wa chakula alitokea
ameshika sahani mbili za pilau ya samaki n akuziweka mbele ya wale wateja
wawili waliowakuta…(UK 19).”
“….Tumaini alianza kucheza na
wenzake kwenye duara iliyozunguka kichwa cha ng’ombe kilichokua na pembe
ndefu….. Tumaini akaanza kuzunguka duara kwa kucheza na kuruka juu…(UK 94).”
Hivyo
hata katika jamii nyingi za Kiafrika kama vile; wasukuma, wakikuyu na wamasai
hupendelea kujenga nyumba zao zenye umbo la duara. Vilevile jamii ya wangoni,
wamasai na wakisi hucheza ngoma kwa kuzunguka duara.
Falsafa
ya Ndoa, katika falsafa hii Temlpes anasema, Waafrika wanaamini sana katika
ndoa zao na ndoa hizo hudumishwa ili kupata watoto. Uhai wa binadamu unaanzia
kwenye mimba, ambayo ni matokeo ya ndoa. Temples anaendelea kusema kuwa, watu
huoana baada ya kufuata taratibu zilizowekwa kama vile kutoa posa. Katika
riwaya hii mwandishi ameonesha suala hili pale ambapo kina mama walikuwa
wakiimba wimbo unaohusu kutoa posa ili uweze kupata mke. Mfano mwandishi
anasema;
“…maliza posa chukua mwali, mikono
mitupu utakosa mwali. Maliza deni upate mwali, maliza posa chukua mwali…(UK
210).”
Katika
jamii za Kiafrika za leo, suala la ndoa hukamilika baada ya kutimiza taratibu
na sheria za jamii husika. Mfano katika jamii ya Wangoni, mtoaposa hupaswa
kulipa mbuzi watano, dume mmoja na majike wanne. Sufuria kubwa moja, mablanketi
mawili, kanga doti mbili, vitenge doti mbili, shuka mbili na majembe mawili.
Jamii hii ni moja ya mfano tu wa jamii nyingine za Kiafrika ambazo zina taratibu zao katika kutimiza suala la
ndoa.
Falsafa
ya Nguvu Uhai, hili ni wazo jingine la Temples ambapo anaona kuwa Waafrika wanaamini
katika nguvu uhai. Na wanaona kuwa chanzo kikuu cha nguvu uhai ni Mungu
mwenyewe. Nguvu hii hupitia kwa wahenga au mizimu ambao hupeleka kwa binadamu
na binadamu hupeleka kwa wanyama na mimea. Temples anasema kuwa Waafrika
wanaamini nguvu ya waganga na hivyo mganga ana uwezo mkubwa wa kupunguza na
kuongeza nguvu uhai kwa binadamu. Temples anajiuliza maswali kadhaa kuhusiana
na suala la waganga mfano, dawa zawezaje kuponya?, dawa inawezaje kuua mtu
aliye mbali?. Ni vipi mtu aliyekufa anaweza kuzaliwa upya?. Na anasema kitendo
cha kupungukiwa nguvu huitwa “kufwa” na “kufudwilika” kaika “The Bantu
Philosophy” (UK 22). Hivyo Temples anasema kuwa majibu ya maswali yote matatu,
ili uweze kujibu maswali hayo ni lazima uwe mshirika wa mambo hayo. Katika
suala hili mwandishi ameonesha kuwa Mungu ndiye mwenye nguvu uhai kubwa kwa
sababu ndiye mwenye uwezo wa kuumba vitu vyote. Mfano mwandishi anasema;
“…Hapo kale Mungu aliumba Ng’ombe,
akamwambia wewe Ng’ombe, nimekuumba ili umpe binadamu maziwa na nyama, ili
apate kuishi…(UK 121).”
Vilevile
mwandishi ameonesha jinsi binadamu wanavyoweza kupata masuluhisho ya matatizo
yao kutoka kwa mizimu. Kwa sababu huamini kwamba mizimu huwa karibu sana na
Mungu kuliko binadamu wa kawaida. Mfano mwandishi amemtumia mhusika Lodwaa
ambaye alihangaika kwa muda mrefu kupata mtoto wa kiume na baadaye alifanikiwa
kupata mtoto wa kiume baada ya kusaidiwa na mzimu. Mathalani mwandishi anasema;
“…Aliwaona waganga wote wa Nchi ya
Wamasai wamsaidie lakini hakufanikiwa. Siku moja alopokuwa akichunga Ng’ombe
wake alitokewa na mbilikimo. Alikuwa hajapata kumuona mbilikimo katika maisha
yake. Akaogopa sana. Akaamini kuwa ule ni mzimu uliomshukia. Akapiga magoti
huku akitetemeka……sikiliza Lodwaa utapata mtoto wa kiume katika miezi tisa
ijayo…(UK 92-93).”
Hata
katika jamii nyingi za leo za Kiafrika, suala la nguvu uhai lipo. Na wanaamini
kuwa Mungu ndiye mwenye nguvu uhai kubwa kwasababu ndiye chanzo cha mambo yote
akifuatiwa na wahenga na mizimu inayotumika kama masuluhisho ya matatizo yao.
Falsafa
ya Hofu ya Uhai na Kifo, hii ni hoja
nyingine ya Temples, kwani anaamini kuwa Waafrika wana hofu ya uhai na kifo.
Kwa kudhihirisha hili unaweza kuangalia salamu zao na pia mtu anapopatwa na
ugonjwa huhofu kuwa hawezi kupona na
kifo kinamsogelea. Katika riwaya hii mwandishi amemtumia mhusika Lodwaa ambaye
alimlea mtoto wake wa kiume na wa pekee katika ulinzi na uangalizi mkali,
akihofia asije akafariki kabla ya kutimiza miaka kumi na nane. Mfano mwandishi
anasema;
“…Lodwaa akaagiza kuwa wakati wote,
yule mtoto alelewe ndani ya manyata. Kila wakati kulikuwa na mtu wa
kumuangalia. Si mchana si usiku. Mtoto akaendelea kukua. Siku zikapita. Majuma
yakapita. Miezi ikapita na miaka pia ikapita. Mwaka wa kumi na nane ukakaribia.
Mwaka ambao kama Tumaini angeufikia tu basi, hangekufa hadi awe kikongwe…(UK
93).”
Vilevile
mwandishi ameonesha wahusika wanafunzi wakiwa na hofu ya kifo baada ya dereva
kuendesha gari kwa kasi bila kujali usalama wao. Mfano mwandishi anasema;
“…Dereva aliendesha gari kwa hasira
bila ya kujali usalama. Waliosali walisali na waliotambika walitambika. Baada
ya muda wakaanza kupiga kelele, punguza mwendo unatuua! Jamani unatuua! Dereva
ndio kwanza akazidi kuchochea moto…(UK 183).”
Hivyo
hata katika jamii nyingi za Kiafrika za leo, watu wengi wana hofu juu ya uhai
na kifo, hasa pale mtu anapoumwa humwombea dua ili aweze kupona.
Kwa
ujumla Placide, Temples ametoa mchango mkubwa sana juu ya Falsafa ya Kiafrika,
kwani alifanya uchunguzi na kubaini kuwa Waafrika wana falsafa yao. Mawazo yake
yana uhalisia katika jamii ya Waafrika wa leo. Pia yamepelekea kuibuka kwa
Wanafalsafa wengine wanoizungumzia Falsafa ya Kiafrika kama vile Kwame
Nkurumah, J.K. Nyerere na Kenneth Kaunda.
MAREJELEO
Mbiti, J. (1990). African Religion and Philosophy. New
York: Praeger Publisher.
Odera,
H. O. (1990). Trends in Contemporary
African Philosophy. Nairobi: Shirikon Publishers.
Semzaba, E. (2015). Marimba ya Majaliwa. Dar es salaam: E
& D Vision Publishing.
Sodipo,
J. O. (1993). Foundation of African
Philosophy. Ibadan: Ibadan University Press.
Temples, P. (1959). “The Bantu Philosophy”. Paris: Presence
Africane.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com