Dhana
ya falsafa imefasiliwa na wataalam mbalimbali kama vile Njoroge na Bennaars
(1986) wanafasili falsafa kuwa ni jaribio lolote la watu kufikia jibu au itiko
la masuala muhimu ya maisha. Hivyo wao huona kuwa falsafa hupuuza visakale na
mazingaombwe.
Odera
(1990) anafasili falsafa kuwa ni taaluma ambayo kanuni za msingi kuhusu asili,
binadamu, na jamii huchunguzwa na kujadiliwa. Mtaalam huyu alitazama falsafa
kwa mtazamo wa kitaaluma pekee wakati falsafa huweza kutazamwa kwa mtazamo
ambao falsafa ni kama mtazamo.
Kwa
ujumla falsafa ni mawazo yaliyopo katika mwendo yakitaka kujua tumetoka wapi na
tunaelekea wapi.
Falsafa
ya kiafrika imekuwa ikizua mjadala mkubwa miongoni mwa wanataaluma ambapo kuna
baadhi ya wataalam ambao huamini kuwa Afrika hakuna falsafa hasa wataalam wenye
mtazamo wa kimagharibi. Wataalam hawa hupingana na kauli kwamba, Afrika kuna
falsafa ambayo huweza kwatofautisha waafrika na watu wa maeneo mengine mfano wa
wataalam hao ni kama George Friedrich Willhelm Hegel, ambaye alikuwa ni
mwanafalsafa wa kimagharibi. Mtazamo mwingine ni ule ambao wanafalsafa
wanakubaliana kuwa Afrika kuna falsafa wanasema ilianza mnamo karne ya 20 yaani
kuandikwa na kusomwa. Pia katika kipindi cha nyuma falsafa ilikuepo hasa kwa
kupitia fasihi simulizi. Wanafalsafa ambao wanathibitisha hoja hii ni kama
wafuatao.
Temples
(1945) ambaye hakuwa mwafrika lakini alithibitisha uwepo wa falsafa ya kiafrika,
anasema falsafa ya waafrika inajidhihirisha katika mifumo mbalimbali ya
kijamii, mila, desturi na fasihi. Anaendelea kueleza kuwa falsafa ya kiafrika
hufasiliwa katika vipengele vya dini asilia, ngoma, matambiko fasihi simulizi
na itikeli.
Odera
(1990) anasema falsafa ya kiafrika ni mkururo wa mawazo na mjadala wa kifikra
halisi za kiafrika inayoendelezwa na waafrika wenyewe ndani ya miktadha halisi
ya kiafrika. Hivyo basi fasili yake imejiegemeza zaidi katika kuangalia fikra
mbalimbali ambazo huonyeshwa na waafrika wenyewe juu ya mambo mbalimbali.
Mbiti
(1960) anaeleza kuwa Falsafa ya Kiafrika ni uelewa wa maisha ya Kiafrika,
mtazamo, mantiki na uchukulizi wa mambo unaotegemea maadili ambayo Waafrika
wanayawaza, wanayatenda na kuyafanya katika mazingira tofauti ya maisha yao.
Falsafa hii hujidhihirisha kwa kupitia dini, itikeli na maadili waliyonayo
wenyewe. Hivyo basi maelezo haya yanajiegemeza katika hoja ya kuyafahamu maisha
na mazingira ya Waafrika kupitia mitazamo ya kimaisha na kile wanachokiamini.
Hivyo
basi waafrika wana falsafa yao ambayo huweza kuwatambulisha miongoni mwa jamii
zingine zinazowazunguka.
Bwana
Myombekere na Bi Bugonoka ni riwaya ambayo imetungwa na Aniceti Kitereza mnamo
1945 kwa lugha ya kikerewe, katika kipindi hiki mswada huu haukufanikishwa
kuchapishwa. Mnamo mwaka 1969 ndipo alipoamua kuufasili mswada huu kwa lugha ya
Kiswahili japokuwa alikuwa anaumwa, na ukachapishwa mwaka 1980. Riwaya hii huzungumzia
kwa ujumla mila na desturi mbalimbali ambazo hupatikana katika jamii ya
wakerewe ambao hupatikana katika kisiwa cha Ukerewe. Mila na desturi hizo zimejadiliwa
katika riwaya hii, hupatikana pia katika jamii mbalimbali za kiafrika, pia yamesaidia
kuibua falsafa mbalimbali za kiafrika.
Vifuatavyo
ni vipengele mbalimbali vya falsafa ya kiafrika ambavyo vimejitokeza katika
riwaya ya Bwana Myombekere na Bi Bugonoka.
Falsafa
ya ubuntu, kwa mujibu wa Samweli (2015) anafafanua falsafa hii kuwa ni ile hali
ya kumjali mtu au kumsaidia binadamu mwingine kama nafsi yako, anaendelea
kusema mtu mwenye utu hawezi kumfanyia mtu mwingine jambo ambalo yeye
asingependa kufanyiwa. Falsafa hii imejitokeza pale ambapo Bwana Myombekere
alipokwenda kutafuta ndizi kwa ajili ya kutengeneza pombe aina ya empahe ambayo alitakiwa aipeleke kwa
wakwe zake ili kulipa adhabu aliyokuwa amepewa. Baada ya kufika kwa rafiki yake
aitwaye Nkwesi na kumweleza alionyesha utu, kwani alikubali kumpa Myombokere
ndizi pasipo malipo yoyote yale. Mwandishi analithibitisha hili pale anaposema
“ … Nkwesi
akamwambia hivi, “Kama wamekwambia pombe tu,
usiwe na
udhia, ndugu yangu migomba ipo. Labda kama
wamesema kitu kingine, lakini
kama ni hiyo pombe tu
uliyosema tutaipata uwapelekee, wanywe.” …Ukurasa 69.
Hivyo
basi hali hii ambayo imejitokeza kati ya Nkwesi na Myombokere inadhihirisha utu
kwani Nkwesi alichukulia tatizo alilokuwa nalo Myombokere kama ni la kwake
ndiyo maana aliamua kumpa ndizi bila kudai au kuomba ujira wowote ule. Pia utu
unajidhirisha pale wake wa Nkwesi wote wanne walipojitolea kwenda kumsaidia
kwenda kubeba ndizi alizokua amezinunua kwa ajili ya kutengenezea pombe
iliyokuwa ikihitajika kwa wakwe zake. Aghalabu falsafa hii imejidhihirisha pale
ambapo shemeji wa Myombekere yaani mume wa dada yake alikubali kwenda
kuwasaidia kupalilia mtama na mawele. Mwandishi anathibitisha pale anaposema,
… “hayo si kitu, yasikusumbue, mke wangu,
kwasababu
huwa tunawaona watu kila mara wanasaidiana,
hata
wakiwa watu tu wasio
na ukoo hata kidogo, sembuse
yeye aliye nipa kujenga niache kumsaidia?
Nikiacha
kumsaidia hiyo ni
fedheha kubwa mno kwangu…” (ukurasa 237)
Kutokana
na hali hii huonyesha kuwa falsafa ya Ubuntu ni vema ikatiliwa mkazo miongoni
mwa jamii kwani kutokana na utu huweza kupelekea mendeleo miongoni mwa
wanajamii na jamii kwa ujumla.
Vilevile
falsafa ya uzazi, kwa mujibu wa Samweli (keshatajwa) anaeleza kuwa katika jamii
za kiafrika suala la uzazi limekuwa likitiliwa msisitizo sana kwasababu, uzazi
ndiyo muhimu sana katika familia nyingi za kiafrika. Kutokana na hali hii mwanamke ambaye hana
uwezo wa kuzaa huwa hathaminiwi sana miongoni mwa familia nyingi za kiafrika.
Hali hii pia imejitokeza katika riwaya tajwa pale ambapo dada wa Myombokere
walipokuwa wakimtukana Bugonoka kutokana na hali ya kutozaa. Mwandishi
anathibitisha hili pale anaposema;
“… .Wewe ni mwanamke gani,usiyezaa! Kisha
hustahili
kuolewa na ndugu yetu Myombekere
na uzuri wake,
usije ukamwambukiza ugumba
wako kefule!’ …Ukurasa 8.
Suala
la uzazi limekuwa likithaminiwa sana kwa mwanamke ambaye anauwezo wa kuzaa,
katika riwaya hii inajidhihirisha pale ambapo Myombekere anatoa utofauti kati
ya familia yenye mtoto na ambayo haina mtoto, hili hudhihirika pale anaposema;
“...Myombekere akajibu,
“Hapana shemeji, kuzaa ndiyo bora,
tena ndiyo kuzuri kabisa,
kushinda vyote, sababu wahenga wetu
walisema hivi: asiyekuwa na
mtoto hutuma mguu wake. Mwenye
huwa na heshima miongoni mwa
watu kuliko wewe mwenye kutuma
mguu wako; japo ukiwa na mingi
kuliko kiasi, vilevile huwa kazi
bure. Tazama,
sasa kitoto hicho ulichonacho nacho hicho, kinapolia
nyumbani humu,
hutuchangamsha sote waliomo…” (ukurasa 225)
Hivyo
basi katika falsafa za kiafrika suala la uzazi hupewa kipaumbele sana na
kukitokea tatizo la uzazi mwanamke ndiye hulaumiwa sana. Pia hutumia njia
mbalimbali ili aweze kupata mtoto kwasababu kuwa na mtoto ndiyo utajiri mkubwa.
Vilevile suala la uzazi limejitokeza katika ukurasa wa 227.
Fauka
ya hayo falsafa nyingine ni uduara, kwa mujibu wa Tempels (1945) anasema
utamaduni wa mwafrika upo katika uduara kwani uduara huu huweza kuonekana
katika nyumba, vyombo vya kulia chakula yaani sahani, bakuli, mitungi na
urithishaji wa majina. Falsafa hii imejitokeza katika riwaya tajwa pale ambapo
Myombekere ametoka kumchukua Bugonoka kwa wazazi wake mwandishi anasema
“… Mgawaji pombe akaichota, akampa, Myombekere
akaipokea akainywa kefu, iliyobaki
akaigawa mke wake
Bugonoka na Binti Kanwaketwa, na
mwanamke mzee,
wakainywa,
wakaimaliza…”
(ukurasa 110)
Katika
sehemu hii uduara umejitokeza pale ambapo watu mbalimbali walitumia chombo kimoja
kunywea pombe ambayo walikuwa wamepewa. Hali hii ya kutumia chombo kimoja
imejidhihirisha tena katika ukurasa wa 240 pale ambapo wakulima wa umoja na
watu waliosaidia kupika walipo kuwa wakinywa empahe kwa kutumia chombo kimoja. Kwahiyo hali hii huonyesha uduara
miongoni mwa jamii mbalimbali za kiafrika. Pia falsafa hii imejidhihirisha pale
ambapo walikuwa wakicheza ngoma. Mwandishi anasema;
“…
Hapo sauti ya ngoma hizo yaani emilango
zikapasua hewa. Katika mji wa Omukama
wa
wanaume kikawa kivumbi; mlio wa ngoma
ulipochanganyikana na mvumo wa
makelele
ya watu wengi kukawa na sauti kama ya ngurumo
ya radi…” (ukurasa 201)
Pia hali hii ya kucheza ngoma imejitokeza pia
katika Omukamazi wa wanawake pale katika ukurasa wa 192. Hivyo basi halihii
huonyesha uduara au umoja na ushirikiano ambao hujitokeza katika jamii
mbalimbali za kiafrika na hupelekea maendeleo miongoni mwa jamii na nchi kwa
ujumla.
Kadhalika
falsafa ya nguvu uhai, kwa mujibu wa Tempels (1945) anaeleza kuwa nguvu uhai ni
msingi wa vitu vyote duniani. Anaendelea kueleza kuwa Mungu ndiye mwenye nguvu
uhai kubwa kuliko viumbe wengine wote. Pia katika riwaya hii huonyesha kuwa
jamii huamini uwepo wa Mungu na kila kitu ni mali yake pia ndiye mwenye maamuzi
na vitu vyote. Mwandishi analithibitisha hili pale ambapo Myombekere anasema
“…Sasa sisi hapa tulipo, tu watu wa nani hasa?
Bugonoka hakuchelewa kumjibu,
alitamka upesi
akasema, Tu watu wa Mungu hasa…” (ukurasa 128)
Katika
falsafa ya nguvu uhai hunyesha kuwa wanajamii wa ukerewe huamini katika uwepo
wa Mungu kwani yeye ndiye mwenye mamlaka juu ya kila kitu ambacho hupatikana
ulimwenguni hii pia inathibitika katika ukurasa wa 274 wakati Myombekere
anasema Manani ndiye mwenye kuruhusu
wapate mtoto au la. Hivyo basi falsafa hii huonyesha kuwa waafrika huamini
katika Mungu ambaye huabudiwa tofauti tofauti katika jamii za kiafrika.
Aghalabu
falsafa ya uchawi, kwa mujibu wa Samweli (keshatajwa) anaeleza kuwa uchawi upo
na uwezo wa kuwadhuru watu. Hivyo basi jamii nyingi za kiafrika hutumia uchawi
ikiwa ni njia moja wapo ya kuweza kuwasaidia katika mambo mbalimbali ambayo
yanawazunguka katika jamii zao. Katika riwaya tajwa uchawi umejidhihirisha pale
ambapo mwandishi anasema
“… Baba na ndugu yangu wakapata uchungu
sana wakanena, Ondoka twende pamoja,
huwezi
tena
kukaa hapa, sababu wachawi hawa wameanza
tangu siku nyingi,
tazama jinsi wameharibu utumbo
(kikazi) wako, tumeshuhudia wazi…” (ukurasa 21)
Katika
sehemu hii wake wenza wa bibi huyu walimdhuru mwenzao na kupelekea kupata
tatizo la kutoka mimba. Pia uchawi kama falsafa ya mwafrika imejitokeza tena
katika ukurasa wa 103 pale ambapo Nakutuga anasema “alivaa hirizi ili kujilinda na ugonjwa uliyonipa kwenda
chopi”. Jamii nyingi za kiafrika zimekuwa zikitumia uchawi kama ni moja
wapo ya njia ya kuonyesha fahari pia wametumia njia hii kuwadhuru watu wengine.
Aidha
falsafa ya uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke, kwa mujibu wa Samweli
(keshatajwa) anasema mwanamke ni kiumbe dhalili ya mwanaume. Hivyo huwa
hakwezwi katika falsafa ya kiafrika huwa na jukumu la uzazi na ulezi. Falsafa
hii imejitokeza katika riwaya tajwa mwandishi analithibitisha hili pale
anaposema
“…kwani mwanamke huolewa ili akae
pamoja na mumewe
kumpikia chakula, kumtandikia
kitanda, na kumlimia chakula
na hasa kabisa kumzalia watoto na
kuwalea basi…”(ukurasa 228)
Hivyobasi falsafa hii
huonyesha uhusiano ambao huchukuliwa miongoni mwa wanawake na wanaume, katika
falsafa hii mwanamke anaonekana kuwa dhalili au kiumbe dhaifu juu ya mwanaume.
Kutokana na hali hii imepelekea wanawake wengi wa kiafrika kutokuwa na uamizi
juu ya masuala mbalimbali yanayo wazunguka.
Aghalabu
falsafa ya uganga, kwa mujibu wa Samweli (keshatajwa) anasema uganga huweza
kutoa ufumbuzi wa matatizo yaliyoshindikana katika jamii. Hivyo basi kupitia
uganga watu mbalimbali wamekuwa wakitatuliwa matatizo yao. Falsafa hii
imejitokeza kama ifuatavyo;
“…leo safari hii usimtazame tu; utamtafuatia
kwa
waganga dawa au hirizi za kumkinga maovu
yanayomharibia mimba, uovu ulio kwa
mke wako
au labda kwako mwenyewe mjini mwako
humu.” (ukurasa 225)
Pia
uganga ulisaidia kufukuza ndege waliokuwa wakila mawele kule shambani. Katika
jamii za kiafrika uganga umesaidia
familia mbalimbali kuweza kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ambayo
yalikuwa yakiwakabili.
Aghalabu
falsafa ya kifo, kwa mujibu wa Mbiti (1960) anasema kifo humuondoa mtu taratibu
kutoka sasa na kumpeleka zamani. Anaendelea kusema kwamba mtu hufa taratibu
mpaka watu wanaomkumbuka waishe. Pia anaendelea kusema kwamba watu mbalimbali
katika jamii huogopa na kukwepa kifo. Kuwapo kwa falsafa ya kifo kunajitokeza
pale ambapo mhusikaMyombekere na Bugonoka wanapata taarifa juu ya tanzia ya
shangazi yake Bugonoka. Mwandishi anasema;
“…wametuletea tanzia ya kama shangazi ya mke
wangu
amekufa, lakini amepigwa na radi…Lakini
kisa ni kilicho
nileta kwako hapa, nimekuja kwa ajili ya
kukuuliza: Sasa
mke wangu, amekwisha kuwa mjamzito hivi,
anaweza kuwalilia
wafu na kukaa matangani?”
(ukurasa 234)
Kupitia
riwaya tajwa mwandishi anaonyesha jinsi wanajamii wanavyoogopa kifo, na athari
zake miongoni mwa jamii.
Falsafa
ya kazi, kwa mujibu wa Samweli (keshatajwa) anaeleza kuwa kazi ni jambo
linalothaminiwa sana katika jamii za kiafrika. Katika jamii za kiafrika mtu
ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kujishughulisha na kazi mbalimbali aliweza
kufanikiwa katika shughuli hizo, pia haikuwa rahisi kuweza kupata janga la njaa
katika nyumba au familia yake. Anasema
“…Nitengenezee jembe
mimi nipate kulima viazi, kwa sababu
naona mwaka wa kulima mawele umepunguka,
sitasumbukia
bure kulima chakula
cha kupata hasara tu, maana matembele
(mbegu ya viazi) ni tele
kwa wakulima.” (Ukurasa 133)
Hivyo
basi kutokana na ukulima wa Bugonoka wa mazao mengi ulimsaidie kuweza kuepukana
na janga kubwa la njaa. Vilevile falsafa hii imejitokeza katika ukurasa wa 237,
katika jamii za kiafrika kuna jamii ambazo hujikita katika kufanya kazi
mbalimbali ambazo zilipelekea maendeleo na kuepukana na hali ya utegemezi.
Kwa
ujumla riwaya ya Bw Myombekere na Bi Bugonoka imesaidia kuonyesha falsafa
mbalimbali ambazo hupatikana miongoni mwa jamii mbalimbali za kiafrika. Falsafa
hizi zimeonekana kuwa ni mwongozo muhimu kwa waafrika hawa kwani kutokana na
uwepo wa falsafa hizi. Jamii mbalimbali za kiafrika zimefanikiwa kujua miiko na
tamaduni ambazo ni muhimu zikafuatwa miongoni mwa jamii husika. Hivyo basi
kutokana na uwepo wa wa falsafa hizi huonyesha kuwa waafrika wana falsafa yao
ambayo huwaongoza na kuwatofautisha na jamii nyingine.
Kitereza,
A. (1980). Bw. Myombekere na Bi. Bugonoka
na Ntulanalwo na Bulihwalo: Juzuu ya
Kwanza. Dar es
Salaam: Tanzania Publishing House.
Mbiti,
J. (1960). African Religions and
Phylosophy. New York: Praeger Publisher.
Njoroge
na Bennars. (1986). Philosophy and
education in Africa.Nairobi Transafrica
Odera,
H. O. (1990). Trends in Contemporary African
Phylosophy. Nairobi. Shirikon Publisher.
Samwel,
M. (2015). Umahiri katika Fasihi ya
Kiswahili. Dar es Salaam: Mevel Publisher.
Temples,
P. F. (1945). Bantu Phylosophy.
London: Presence African Publishers.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com