1.0 UTANGULIZI
sehemu ya kwanza ni
utangulizi, sehemu ya pili ni fasili ya dhana, sehemu ya tatu ni sifa za vikoa
vya maana, sehemu ya nne ni umuhimu wa vikoa vya maana, sehemu ya tano ni
changamoto na mwisho ni hitimisho la swali.
- Fasili ya Dhana ya Vikoa vya Maana
Ufafanuzi
kuhusu dhana ya vikoa vya maana kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali umeelezwa
kama ifuatavyo;
Briton
(2000) anaihusisha dhana ya vikoa vya maana na dhana ya haiponimia. Haiponimia
ni uhusiano wa ki-uwima ambapo fahiwa ya neno moja hujumuishwa katika fahiwa ya
neno jingine. Hii inamaana kuwa maana ya neno moja ni sehemu ya maana kubwa ya
neno. Neno lenye maana kubwa huitwa “neno jumuishi” na maneno yenye maana
ndogondogo huitwa “haiponimu”. Kwa mfano, mmea (neno jumuishi) lina haiponimu
kama mgomba, mahindi, na maharage. Tunaona mtaalamu huyu haweki wazi maana ya
vikoa vya maana ingawa anajikita Zaidi katika kuhusisha vikoa vya maana na
haiponimia.
Dirk
(2010) anaeleza kuwa, vikoa vya maana ni jozi za maneno yenye maana
zinazohusiana ambazo maana zake zinategemeana, na kwa pamoja zinatoa dhana ya
kimuundo yenye uhalisia ndani yake. Hii humaanisha kwamba, maana ya haiponimu
zinazotokana na kikoa kimoja hujumuishwa katika maana pana au jumuishi moja.
2.0 Sifa za Vikoa vya
Maana
Baada
ya kufasili vikoa vya maana kwa mujibu wa wataalaamu mbalimbali, zifuatazo ni
sifa za vikoa vya maana.
Dirk
(2010) anafafanua kuwa vikoa vya maana huwa na sifa kuu mbili; kila kikoa
kinaweza kuzaa vikoa vingine vidogovidogo. Kwa mfano 1 Matunda
- Papai
- Embe
- Chungwa
- Nanasi
- Parachichi
Mfano 2. Wanyama
- Chui
- Simba
- Mbwa
- Mbuzi
- Kifaru
Pia
hakuna kanuni ya upangaji wa hivyo vikoa yaani kipi kiwe cha kwanza na kipi
kiwe cha mwisho. Katika vikoa hakuna mpangilio maalumu wa mfuatano wa vikoa
hivyo chochote kinaweza kuanza au kuwa cha mwisho.
Kwa mfano;
Matunda
4.
nanasi
3. Chungwa
1.
Papai
2.
Embe
Halikadhalika
katika sifa hiyo ya kutokuwa na kanuni ya upangaji wa vikoa vya maana ina
vighairi, kwani kuna baadhi ya vikoa hufuata kanuni na utaratibu maalumu wa
mpangilio wa kinamba. Kwa mfano katika vikoa vya siku, miezi, miaka au namba,
hivi ni vikoa vyenye kufuata utaratibu maalumu wa mfuatano wa namba.
Mfano;
Siku
- Jumamosi
- Jumapili
- Jumatatu
- Jumanne
Mfano
2; Namba
- Moja
- Mbili
- Tatu
Vikoa
hivi vya maana hufuata utaratibu maalumu ambapo maneno huorodheshwa kwa kufuata
mpangilio wa kinamba.
3.0 Umuhimu wa Vikoa vya
Maana
Baada
ya kuangalia sifa za vikoa vya maana, ufuatao ni umuhimu wa vikoa vya maana na
ufafanuzi wake.
Vikoa
vya maana husaidia kuonesha uhusiano wa maneno yenye sifa sawa au
zinazoelekeana kimaana. Vikoa vya maana humsaidia mwanaisimu kutambua sifa za
maana mbalimbali zinazohusiana kimaana. Hii humaanisha kuwa, huwezi kuweka neno
fulani katika kikoa fulani bila kujua sifa zinazotawala neno hilo. Hivyo basi,
haiponimu zote zinazotokana na neno moja pana huwa na sifa ama zinazofanana au
zinazoelekeana. Habwe na Karanja (2004) wanafafanua kuwa neon lenye maana kubwa
huitwa neon jumuishi na lile lenye maana ndogo huitwa haiponimu. Wanaeleza kuwa
neon mnyama katika lugha ya Kiswahili ambalo ni neno kuu, lina mahusiano ya kihaiponimia
na maneno mbuzi, ng’ombe, simba, duma, nguchiro na mengineyo. Hivyo ukisema
mnyama sio lazima uwe umemaanisha mbuzi au ng’ombe lakini ukisema mbuzi au
ng’ombe kwa naman Fulani utakuwa umemaanisha mnyama.
Hurahisisha
mchakato wa ujifunzaji lugha. Vikoa vya maana husaidia kumuelekeza mtu
anayejifunza lugha fulani mahususi ili kujua vitu mbalimbali vilivyowekwa
katika kundi Fulani husika. Kwa mfano, mtu mgeni wa lugha fulani huweza
kujifunza kuwa, dhana ya neno “matunda”, hurejelea ndizi, maembe, parachichi,
zabibu na machungwa. Kwa mantiki hii, mgeni wa lugha fulani anapotajiwa moja ya
vitu vilivyoorodheshwa hapo juu, mfano ndizi, maembe au zabibu, ataelewa kuwa
kinachomaanishwa au kinachorejelewa ni matunda.
Hurahisisha
mawasiliano baina ya watumiaji wa lugha. Katika mawasiliano, matumizi ya neno
moja pana linalorejelea maana nyingine ndogondogo husaidia kuokoa muda baina ya
wazungumzaji. Kwa mfano, mtu anapokwenda sokoni, badala ya kutaja kitu kimoja
kimoja, huweza kutaja kwa ujumla wake endapo vinahusiana. Mtu akienda sokoni
huweza kuuliza; “una mboga za majani?” Atajibiwa; “kuna mchicha, chainizi,
spinachi, na matembele”. Hivyo basi vikoa vya maana vitakuwa vimesaidia katika
kurahisisha mawasiliano baina ya wazungumzaji, kwani baada ya kutaji kitu
kimoja huweza kutaja kwa ujumla wake kama vinahusiana.
Vikoa
vya maana husaidia katika shughuli za utunzi wa leksikografia. Mdee (2010),
akimnukuu Wiegand, anaeleza kuwa, leksikografia kazi ya kisanaa
inayojishughulisha na utunzi wa kamusi. Leksikografia hiyo hujishughulisha na
ukusanyajin wa misamiati mbalimbali ya lugha na ndiyo inayosaidia kutungiwa
kamusi. Kamusi ni kipengele cha kisemantiki kwa kuwa hutoa maneno yenye maana
kwa watumiaji wa lugha. Maneno hayo huweza kutumika kama vikoa vya maneno vyenye
maana. Mifano ya kamusi zenye vikoa vya maana ni kama vile; kamusi ya wanyama,
Kamusi ya mavazi, Kamusi ya tiba ya magonjwa, Kamusi za misuko ya nywele, Kamusi
za vyakula.
Kikoa
kimoja huweza kusaidia kujua na kufafanua vikoa vidogovidogo vilivyomo ndani ya
kikoa kikubwa. Kwa mfano, mtu anapokwenda hotelini na kusema; “naomba chakula”,
ataulizwa, “unahitaji ugali, ndizi, viazi, au wali?”. Kisemantiki, hii
humsaidia mtumiaji wa lugha kuteua kikoa mahususi kwa ajili ya matumizi yake
kwa wakati huo. Kwa mfano, mtu atasema; “nahitaji ndizi”.
Husaidia
kuonesha umbo la wingi ambalo lina umuhimu kisemantiki hasa katika upatanisho
wa kisarufi. Kwa mfano, badala ya mtu kusema “kikoa cha mmea” husema “kikoa cha
mimea”, badala ya kusema “kikoa cha ua” atasema “kikoa cha maua”. Vikoa hivyo
vinapotumika kwenye sentensi huwa mimea imeota badala ya kusema mmea imeota, ua
limechanuza badala ya kusema maua limechanuza
Vikoa
vya maana vina sifa ya kuwa na maana ya kileksimu na kufanya kikoa kimoja
kichanuze zaidi na kuweza kupata maneno mengine yenye maana kisemantiki. Kwa
mfano, kuna kikoa cha masomo ya sayansi, baiolojia, fizikia, kemia, kilimo.
Kikoa cha baiolojia kinaweza kufasiliwa kuwa ni somo la kisayansi linalohusiana
na viumbe hai na visivyo hai. Hivyo tunaona kuwa kikoa cha baiolojia
kimechanuza zaidi na kuleta maana ya kikoa hicho.
4.0 Changamoto za Vikoa
vya Maana
Baada
ya kuangalia sifa pamoja na umuhimu wa vikoa vya maan, vilevile vikoa vya maana
vinakumbwa na changamoto mbalimbali katika kuelezea maana ya maana
inayorejelewa. Zifuatazo ni baadhi ya changamoto hizo ambazo ni;
Kuna
baadhi ya vikoa ni changamani. Hii ni kutokana na dhana kuwa, baadhi ya vikoa
vya maana vinawakilisha dhana zaidi ya moja na hivyo kumfanya mtumiaji wa lugha
apate utata wakati wa uainishaji wake. Mfano: ndege kama mnyama, na ndege kama
kifaa cha usafiri. Katika muktadha huu, mkanganyiko wa kinachomaanishwa huweza
kujitokeza ikiwa muktadha wa mazungumzo hautakuwa wazi.
Hakuna
nadharia ya jumla inayohusika na upangaji wa vikoa hivi. Hii inatokana na
ukweli kwamba, dhana hizi zipo vichwani mwa watumiaji wa lugha na huandikwa
kutokana na matumizi yake kimaana. Kaitka kuorodhesha, mtumiaji wa lugha
anaweza kuanza na kikoa chochote akipendacho. Kwa mfano, katika kikoa cha
“mtu”, mtumiaji wa kwanza wa lugha anaweza kutaja mwanaume na mwanamke, na
mwingine akataja kwa kuanza na mwanamke kisha mwanaume.
Uainishaji
wa vikoa vya maana unahitaji umakini zaidi katika upangaji wa vikoa kwani kuna
uchomozi wa vikoa vingine. Hii hutokea pale ambapo dhana moja mahususi huwa na
dhana ndogondogo ndani yake ambazo nazo huweza kusimama peke yake na kuwa na
vikoa vyake. Kwa mfano, kikoa cha binadamu tunapata wanaume na wanawake. Katika
kikoa hiki, kuna vikoa viwili pia; kikoa cha wanawake chenye haiponimu kama
vile bibi kizee, shangazi, mama, na msichana. Kikoa cha mwanaume kina haiponimu
kama vile babu, mjomba, na mvulana.
Vikoa
vya maana hutofautiana kutokana na eneo na utamadunihusika. Kila jamii ina
utamaduni na utamaduni huo huwa na vikoa vitumikavyo katika mazungumzo yao
ambavyo vinaweza kutofautiana na utamaduni wa jamii nyingine kutokana na aina
na idadi ya vitu hivyo katika jamii husika. Mfano, kikoa cha ndizi katika
utamaduni wa Wanyakyusa, kuna vikoa vya majina ya ndizi kama vile; malinda,
matoki, mkono wa tembo, haradoni, kaambani na ndyali, lakini katika jamii ya
Wahaya kuna vikoa vya majina ya ndizi kama vile; shubili, majivu. Hivyo tunaona
kuwa vikoa vya maana huweza kutofautiana kati ya jamii moja na nyingine.
5.0 Hitimisho
Hivyo
tunaweza kusema kuwa, ingawa kunachangamoto zinazokabili vikoa vya maana, vikoa
hivyo vina umuhimu na mchango mkubwa katika kuendeleza na kukuza lugha. Hii ni
sababu, wanajamii hufanya uteuzi mzuri wa maneno yenye maana kutoka akilini na
kuyatumia maneno hayo katika mazungumzo na hivyo kufanya suala la mawasiliano
liendelee kufanikiwa zaidi.
MAREJELEO
Brinton
L. J. (2000). The Structure of Modern
English. A Linguistic intro Illustrated Edition.
John Benjamini
Publishing Company.
Dirk,
G. (2010). Theories of Lexico Semantics.
Oxford University Press: New York.
Habwe,
J. na Karanja, P. (2004). Misingi ya
Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publisher
Mdee,
J, S (2011). Nadharia na historia ya
leksikografia. TUKI: Dares salaam.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com