Dhana
ya vitenzi imeelezwa na wanazuoni tofautitofauti kama ifuatavyo: TUKI (1990)
wanafafanua kitenzi kuwa ni neno ambalo hutokea kama sehemu muhimu ya kiarifu.
Hii ina maana kuwa kitenzi ndio kijenzi kikuu cha kiarifu katika muundo wa
sentensi. Matinde (2012) anasema kitenzi ni neno linalotoa taarifa kuhusu tendo
linalofanyika, lililofanyika na litakalofanyika.
Richard
na wenzake (1985) wanasema kuwa kitenzi ni neno ambalo hutokea kama sehemu
muhimu ya kiarifu na ambalo huambishwa mofu za njeo, hali, nafsi, idadi na
dhamira. Aidha, vitenzi hueleza juu ya tendo au hali. Naye Nkwera (2003)
anasema kuwa vitenzi ni maneno yanayoarifu jambo ambalo hufanywa na jina au
kufanyiwa jina. Pia, Nkwera anaeleza kuwa kitenzi kinaweza kuwa kiwakilishi au
kivumishi kisimamapo peke yake kama jina. Vitenzi hutaja matendo, matukio, hali
au mabadiliko. Kitenzi ni neno ambalo limebebeshwa vitu vingi ndani yake suala
linalowafanya wanasarufi wengi kupendelea kuliita neno hilo kifungutenzi badala
ya kitenzi.
Naye
Mdee (2007) anatoa maana ya kitenzi kuwa ni neno linaloeleza jambo linalotendwa
na lililotendeka. Kitenzi huarifu tendo lililofanywa au litakalofanywa na
mnyama, mtu, au kiumbe chochote kinachoweza kutenda jambo. Mdee anaendelea
kufafanua kuwa vitenzi vya Kiswahili havisimami pekee vinapotumiwa katika
tungo, bali huambatana na viambishi vingine vyenye kuwakilisha mtenda wa tendo
au mtendewa wa jambo. Kitenzi huambatishiwa pia viambishi vyenye kuonesha
wakati tendo linapofanyika, kama mfano ufuatao unavyoonesha: Mfano Dada
a-na-soma, watoto wa-na-ruka, baba a-ta-fika.
Mgullu
(2010) anasema kuwa vitenzi ni aina ya maneno ambayo hutumika kama sehemu
muhimu sana ya kiarifu cha sentensi ambayo hueleza jambo fulani linalohusu
kiima cha sentensi. Katika lugha ya Kiswahili vitenzi ni maneno pekee ambayo ni
lazima yawepo katika sentensi ndipo kifungu cha maneno kiweze kuwa sentensi, kwa
mfano katika sentensi: Mtoto anakula. Aidha, Matinde (2012) anaeleza kuwa
kitenzi ni neno linalotoa taarifa kuhusu tendo lililofanyika, linalofanyika au
litakalofanyika. Katika muundo msingi wa tungo za Kiswahili kitenzi ndilo neno
kuu katika sehemu ya kiarifu au kirai tenzi. Kitenzi kinapoondolewa katika
sentensi bila shaka kifungu hicho cha maneno hukosa maana. Matinde anafafanua
kuwa vitenzi huweza kusimama bila msaada wa aina zingine za maneno na sentensi
ikawa kamilifu na yenye uarifishaji mkamilifu.
Kwa
mujibu wa Massamba (2012), anafasili dhana ya Uarifu kuwa ni uhusiano wa kiima
na kiarifu kwa namna ambayo kiarifu kinakuwa na neno linalovumisha kiima. Kwa kutumia mifano ya kutosha kutoka katika
lugha ya Kiswahili ufuatao ni ufafanuzi wa uarifu wa kitenzi.
Kitenzi
huarifu kuhusu njeo. Habwe na Karanja (2007) wanasema kuwa kuna aina tatu za
njeo, nazo ni njeo ya wakati wa sasa, wakati uliopita, na wakati ujao. Waihiga (2010)
anaeleza kuwa kuna nyakati za aina tatu zinazowakilishwa na viambishi
mbalimbali katika Kiswahili yaani, wakati uliopo, wakati uliopita na wakati
ujao. Aidha, wanazuoni wengi wanakubaliana kuwa wakati uliopo huwakilishwa na
kiambishi ‘na’, wakati uliopita huwakilishwa na kiambishi ‘li’ na wakati ujao
huwakilishwa na kiambishi ‘ta’. Njeo ni miongoni mwa kategoria za kisarufi
zinazosaidia kufasili dhana ya kitenzi.
Mfano: i) njeo ya wakati
uliopo.
Anacheza,
anapika, anasoma, analima anaimba.
ii) njeo ya wakati
uliopita.
Alikula, alisoma,
alioga,
iii) njeo ya wakati
ujao.
Atacheza, ataimba, atalima,
Hivyo
tunaona kuwa, katika mfano wa kwanza kiambishi na katika kitenzi huarifu kuhusu wakati uliopo.
Kiambishi li katika kitenzi huarifu wakati uliopita na liambishi ta, huarifu
wakati ujao.
Kitenzi
kinaarifu kuhusu nafsi, Kwa mujibu wa Habwe na Karanja (2007), wanafafanua
nafsi kuwa ni kipahio kinachodhihirisha muhusika katika usemaji. Anaendelea
kusema kuwa kuna nafsi tatu ambazo hudhihirika katika umoja na wingi. Nafsi ya
kwanza huhusu yule mtu anayesema, nafsi ya pili inahusu mtu anayesemwa ilihali
nafsi ya tatu inahusu anayesemwa juu yake.
Mifano:
i) Nafsi ya kwanza umoja inayohusu mtu anayesema na nafsi ya kwanza wingi inahusu watu
wanaosema.
Umoja wingi.
Ninakula, tunaku
Ninachunga tunachunga
Nasafisha tunasafisha
Katika
mifano hiyo kiambishi ni katika kitenzi huarifu kuhusu mtenda na kiambishi tu
huarifu kuhusu nafsi ya kwanza wingi
ii) Nafsi ya pili
Umoja wingi
Unakula Mnakula
Unachunga Mnachunga
Unasafisha Mnasafisha
Aidha kiambishi u
katika kitenzi hutoa taarifa kuhusu nafsi ya pili umoja na kiambishi m huarifu kuhusu kitenzi cha nafsi ya
pili wingi.
iii) Nafsi ya tatu
Umoja
Wingi
Anakula wanakula
Analia
wanalia
Anapiga wanapiga
Katika
mfano huu kiambishi a kinaarifu nafsi
ya tatu umoja katika kitenzi pia kiambishi wa
kinaarifu nafsi ya tatu wingi.
Kitenzi
kinaarifu kuhusu kauli mbalimbali, Habwe na Karanja (2007) wanasema kauli ni
umbo la kitenzi linaloonesha uhusino baina ya kiima na yambwa. Sentensi ambayo
huchukua yambwa yaweza kuwa katika kauli ya kutenda au kutendwa.
Mfano: Kauli ya kutenda,
i) Mama anakula chakula
ii) Mama amempiga mtoto
iii) Baba analima
Katika mifano hii kiambishi a kinaonesha kauli ya kutenda.
Kauli ya
kutendwa.
Mifano: i) Mbuzi
ameibwa leo
ii) Barua
imeandikwa na mama.
iii) Kuku amechinjwa jana jioni.
Kauli za kutendewa.
Mifano: i)
Mwanafunzi amefanyiwa mtihani
ii)
Baba amepikiwa chakula.
iii)
Ana ameandikiwa barua.
Kauli ya kutendesha.
Mifano: i) mama alimpigisha
mtoto mswaki.
ii) Mjomba alimsomesha Ana.
iii) Napenda kuchezesha midori.
Kauli ya kutendeka.
Mifano: i) Mpira umechezeka.
ii) Nguo imechanika.
iii) Chakula kimelika.
Hivyo basi katika
mifano hiyo, viambishi iw, na, wa,
ish, esh, ek, ik katika sentensi
vinaonesha kauli mbalimbali.
Kitenzi cha idadi, ni
kategoria ya kisarufi yenye kuonesha umoja na wingi katika tungo. Idadi katika
Kiswahili hudhihirika katika ngeli na upatanisho wake.
Mifano:
umoja wingi
mtoto analia watoto wanalia
mtoto anacheza watoto wanacheza
kiti kimevunjika viti vimevunjika
uzi umekatika nyuzi zimekatika
Hivyo katika sentensi
hizo vitenzi vina arifu viambishi ngeli idadi ambapo a, ki, na u katika ngeli katika umoja na wa, vi,
na zi katika wingi.
Kitenzi huarifu kuhusu
hali mbalimbali kama vile hali ya mazoea na hali ya masharti.
Hali
ya mazoea.
Mifano: i) Mwalimu hufundisha wanafunzi.
ii) Mayasa huimba kwaya kila siku.
iii) Mtemi hutembelea watu wake kila siku jioni.
Hali
ya masharti.
Mifano: i) Kama
angeliwai kufika ningelimuona.
ii) Mwalimu
angelifundisha vizuri Salome angelifaulu
iii) Sara angelimsikiliza
kiongozi wake angelikuwa
mwanafunzi bora.
Hali
timilifu.
Mifano: i) Mtoto ameimba leo.
ii) Mwalimu amefundisha.
iii) Mtoto amekula.
Hivyobasi,
viambishi hu huonesha
namna hali ya mazoea katika vitenzi vya Kiswahili inavyo bainika na kuarifu hali ya mazoea yaani tendo ambalo hufanyika
mara kwa mara, pia viambishi ngali na
ngeli vinaarifu kuwa ili jambo moja
lifanyike basi lazima jambo fulani litendeke au kutokea na kiambishi me huo hali timilifu.
Matinde
(2012), anafafanua kuwa kitenzi ni neno linalotoa taarifa kuhusu tendo linalofanyika,
lililofanyika na litakalofanyika. Anaendelea kufafanua kuwa dhima kuu inayofanywa
na kitenzi ambapo huarifu tendo. Fasili hii hailezei wazi kwani kuna baadhi ya
vitenzi havielezei tendo mathalani vitenzi vishirikishi vinaarifu kuwapo au
kutokuwapo kwasifa, hali au kitu Fulani.
Mfano: i) Mwajuma ni mchafu.
ii) Huyu si mwizi.
iii) Watoto
hawana heshima.
Hivyo
basi Vitenzi ni, si na hawana vinaarifu kuwapo
au kutokuwapo kwa jambo fulani haviarifu kuhusu kutendeka kwa tendo lolote.
Richards
(1985) anafafanua kuwa vitenzi huarifu au hueleza mambo mbalimbali kuhusu
kiima. Mambo hayo ni pamoja na:
Huarifu
tendo linalofanywa au litakalofanywa.
Mifano:
i) Mwabupina atacheza.
ii) Mwabupina hatacheza.
Huarifu
siku au wakati.
Mifano: i) Leo ni jumatatu.
ii) Kesho ni jumanne.
Huarifu
cheo au kazi anayofanya mtu.
Mifano: i) Bichwa ni mwalimu.
ii) Kigori si mchezaji.
Huarifu
hali ya kuwa au kutokuwa na kitu fulani
Mifano: i) Nives ana kalamu.
ii) Nives hana kalamu.
Huarifu
sifa ya au za mtu.
Mifano: i) Okwi ni mchezaji.
ii) Okwi si mchezaji.
Huarifu
hali ya kuwa au kutokuwa mahali fulani.
Mifano: i) Mulokozi yuko darassani.
ii) Mulokozi hayuko darasani.
Anaendelea
kusema kuwa mifano ya vitenzi hapo juu hueleza mambo mengi na si matendo. Hii
ndio inafanya tukubali kutumia istilahi ya vitenzi.
Kwa
kuhitimisha urafishaji wa vitenzi unafanywa na viambajengo vya vitenzi kama
vile nafsi, njeo, viambajengo vya idadi, hali za vitenzi na kauli mbalimbali za
vitenzi. Viambajengo hivi vina dhima yakuarifu kuhusu kiima au vinaonesha
uhusiano kati kiima na kiarifu ambapo vinataarifu anayetenda tendo.
MAREJELEO
Habwe,
J. na Karanja, P. (2007). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi:
Phoenix.
Massamba,
D. P. B. (2012). Kamusi ya Isimu na Falsafa
ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.
Matinde, R. S.
(2012). Dafina ya Lugha; Isimu na
Nadharia. Mwanza: Serengeti Educational
Publishers.
Mdee.
J. S. (2007). Nadharia na Historia ya
Leksikografia. Dar es Salaam: TUKI.
Mgullu, R. S.
(2010). Mtaala wa Isimu: Fonetiki Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi:
Longhorn Publisher.
Nkwera,
F. V. (2003). Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu Sekondari na Vyuo.
Dar es Salaam:
Tanzania Publishing House.
Richard,
J. et. al (1985). Dictionary of Applied Linguistics.
Harlow: Longman.
TUKI.
(1990). Kamusi ya Sanifu ya Isimu na
Lugha: Dar es Salaam. TUKI.
Waihiga, G. (2010). Sarufi Fafanuzi ya Kiswahili. Nairobi:
Longhorn Publisher.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com