Flower
Flower

Monday, April 29, 2019

NADHARIA KATIKA TAFSIRI NA UMUHIMU WAKE

Kwa mujibu wa Sengo (2009) anafasili nadharia kuwa ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani kwa sababu fulani. Naye Mdee (2011) anaelezea nadharia kuwa ni mpango wa mawazo uliotungwa ili kueleza jinsi ya kufanya au kutekeleza jambo.  TUKI (2004) wanasema nadharia ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au kutekeleza jambo fulani.
Kwa ujumla nadharia ni mawazo, dhana au maelezo yanayotolewa kuelezea hali fulani: chanzo chake, muundo wake, utenda kazi wake na mwingiliano wake wa ndani na nje.
Baada ya kuangalia maana ya nadharia pia wataalamu mbalimbali wamezungumzia maana ya nadharia ya tafsiri kama ifuatavyo.
Halikadharika Newmark (1982) anasema kuwa kuna maana finyu na maana pana ya nadharia ya tafsiri. Katika maana finyu anafasiri kuwa ni mbinu inayofaa kutumika kutafsili matini ya aina fulani mahususi. Aidha katika kufasili maana pana anafasili kuwa ni jumla ya maarifa yanayopatikana na yatakayopatikana katika mchakato wa kutafsiri kuanzia msingi na kanuni za jumla hadi miongozo na mapendekezo muhimu. Anaendelea kusema kuwa kuna sababu za kuanzishwa kwa nadharia ya tafsiri ambazo ni wingi wa makosa katika tafsiri zilizochapishwa awali. Kuwepo kwa idadi kubwa ya mashirika na asasi zinazojishughulisha na kutafsiri matini mbalimbali na mfumuko wa istilahi katika taaluma mbalimbali hususani sayansi na teknolojia. Tunaona kuwa katika fasili ya Newmark haweki wazi ni matini gani hizo zinazopaswa kushughulikiwa.
Kwa mujibu wa Wanjara (2011) anasema kuwa nadharia ya tafsiri huchunguza mbinu mwafaka za kutumika katika mchakato wa kutafsiri kwa ufanisi matini ya aina fulani mahususi. Ni jumla ya mawazo au maarifa katika mchakato wa kufasiri misingi na kanuni za jumla na miongozo, mapendekezo na vidokezo muhimu. Wanjara pia katika fasili yake haweki wazi mbinu hizo zinatumika katika kutafsiri matini ipi na kanuni na miongozo inatumikaje kwenye hiyo matini.
Halikadhalika Mwansoko (2013) anasema kuwa nadharia ya tafsiri ni nguzo au muhimili wa nguzo ya tafsiri. Ni msingi wa kazi zote za tafsiri. Anaendelea kusema kuwa nadharia ya tafsiri ni maelezo kuntu ya vipengele vinavyopaswa kuzingatiwa na kila mfasiri kila akabiliwapo na kazi ya kufasiri. Mwansoko katika fasili yake haweki wazi misingi na vipengele vinatumika kwenye matini  ipi katika kutafsiri.
Kwa ujumla tunaona kuwa nadharia ya tafsiri ni mawazo au muhimili unaomwongoza mfasiri juu ya vipengele muhimu anavyopaswa kuvishughulikia katika mchakato wakufasili kutoka matini chanzi kwenda matini lengwa. Au ni maelezo muhimu kuhusu vipengele mbalimbali vya kifasiri ambavyo vinapaswa kufuatwa au kuzingatiwa na kila mfasiri pindi anapokabiliwa na kazi ya kufasiri.
Wataalamu mbalimbali wanafasili maana ya tafsiri kama ifuatavyo. Nida na Taber (1969) wanaelezea tafsiri kuwa ni uzalishaji upya wa ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe asili vya lugha lengwa vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi, kwanza kimaana na pili kimtindo.  Nida na Tiber wanaona kuwa katika tafsiri kitu muhimu ni kuzingatia maana na mtindo.
Cartford (1995) anasema tafsiri ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja ( lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana na hayo kwenda lugha nyingine (lugha lengwa). Catford anajikita katika ulinganifu wa mawazo katika kazi ya kutafsiri kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
Kwa mujibu wa TUKI (2002) wanaeleza kuwa tafsiri ni kutoa mawazo kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine bila ya kubadilisha maana. Fasili ya TUKI  imejikita katika maana yaani unapotafsiri hutakiwi kubadili maana iliyoko kwenye lugha moja.
Mshindo (2010) anasema kufasili ni kufafanua maana ya matini moja na kutayarisha baadae matini nyingine inayowiana nayo ambayo huitwa tafsiri na ambayo inawakilisha ujumbe uleule uliomo katika matini ya awali kwa kutumia lugha nyingine. Fasili  hii pia inajikita katika ujumbe na maana uwiane kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine. Kwa ujumla tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo, taarifa au ujumbe kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
Baada ya kuangalia istilahi mbalimbali zilizopo kwenye swali kama zilivyofafanuliwa na wataalamu, ufuatao ni umuhimu wa nadharia ya tafsiri katika taaluma ya tafsiri.
tunaona kuwa nadharia ya tafsiri inajumuisha nadharia mbalimbali ambazo hutumika katika kazi ya tafsiri. Nadharia ya Usawe wa Kimuundo, nadharia hii inatetewa na mtaalam Cartford (1995) anasema tunapofanya kazi ya kutafsiri tunatakiwa kuzingatia ulinganifu wa kimuundo kati ya matini chanzi na matini lengwa, maana yake ni kwamba muundo wa matini chanzi ujitokeze katika matini lengwa. Pia nadharia hii hutumika zaidi katika kutafsiri maandiko ya kidini hasa Biblia.
Nadharia nyingine ni nadharia ya Usawe wa Kidhima, watetezi wa nadharia hii ni pamoja na Nida na Taber (1969) wanaona kuwa usawe wa kidhima ni muhimu zaidi kuliko usawe wa kimuundo. Wafasiri wanapaswa kuhakikisha kwamba dhima ya matini chanzi pamoja na athari zake zinajitokeza katika matini lengwa. Yaani kama matini chanzi inawalenga watoto inapaswa iandikwe. Pia Nadharia ya Usawe wa Aina-matini, matini yoyote ile ifasiriwe kwa kuzingatia aina yake. Hii inamaana kwamba kazi itakayotokea itafanana na matini chanzi, kama matini chanzi ni ya kisheria itakapotafsiriwa matini lengwa nayo itaonekana kuwa ya kisheria. Nadharia Changamani hii ni nadharia tete inadai kwamba huwezi kufanya tafsiri kwa kutumia nadharia moja tu, kwa sababu hakuna nadharia inayojitosheleza yenyewe.
Baada ya kuangalia dhana mbalimbali za nadharia ya tafsiri kwa mujibu wa wataalamu, ufuatao ni umihumu wa nadharia ya tafsiri.
Wanjara (2011) anaelezea kuwa nadharia ya tafsiri husaidia kuonesha mbinu ambazo zinazofaa kutumiwa kufasilia aina mbalimbali za matini. Anaendelea kusema kuwa nadharia hizi za tafsiri husaidia au humpa mwosngozo mfasiri kujua mbinu muhimu ambazo hazina buni kufuatwa wakati wa kutafsiri matini yoyote.
             Mfano: mbinu hizo ni pamoja na tafsiri ya neno kwa neno, tafsiri sisisi, tafsiri ya kisemantiki na tafsiri ya kimawasiliano.
Hii ni kwa sababu mbinu hizi ndizo zinakidhi malengo makuu ya tafsiri, malengo hayo ni kutoa taarifa kuhusu mambo mbalimbali kwa kutumia lugha.
Newmark (1982) anasema kuwa nadharia ya tafsiri husaidia kutoa misingi, kanuni, sheria na vidokezo vya kufasiri matini na kuhakiki tafsiri, yaani matini zilizokwisha tafsiriwa.
               Mfano: mambo muhimu ambayo hayana budi kuzingatiwa wakati wa mchakato wa uchambuzi wa matini ni kusoma matini nzima na katika usomaji wa matini nzima dhumuni lake ni kubaini lengo la matini, kubaini lengo la mfasiri, kubaini wasomaji lengwa, umbo la matini lengwa na kubaini mtindo wa matini chanzi. Pia kusoma matini kwa mara ya mwisho. Anaendelea kusema kuwa kuna hatua muhimu za kufuata kama vie maandalizi, uchambuzi, uhawilishaji, kusawidi rasimu ya kwanza, kudurusu rasimu ya kwanza ili kupata rasimu ya pili, kusoma rasimu ya pili na mtu mwingine na kusawidi rasimu ya mwisho.
Mwansoko (2013) anaelezea kuwa nadharia ya tafsiri husaidia kueleza jinsi ya kuvishughulikia vipengele vidogovidogo katika tafsiri kama vile maana na umuhimu wa vistari, nukta, mkato, italiki, makosa ya uchapaji na mambo mengine kwa ujumla.
               Mfano: maana na nguvu za taarifa zinazobebwa na sitisri, uwasilishaji katika matini ya maudhui na fani yote, haya yana uzito sawa na mazingatio mengine ya zoezi la tafsiri. Mfano asiyejua utu si mtu. Katika mfano huu neno utu litatiliwa mkazo katika mchakato wa tafsiri tofauti na maneno mengine yaliyo katika matini hiyo.
Nadharia husaidia kupata visawe vya maneno katika lugha lengwa. Nider na Taber (1969) wanafafanua kwa kutumia nadharia ya usawe wa kidhima ambapo wanasema wafasiri wanapaswa kuhakikisha kwamba dhima ya matini chanzi pamoja na athari zake zinajitokeza katika matini lengwa. Yaani kama matini chanzi  inawalenga watoto inapaswa ipatiwe visawe vya maneno yanayoendana na watoto katika lugha lengwa.
Kwa kuhitimisha tunaona kuwa Kuna changamoto mbalimbali zinazoikumba kazi ya tafsiri kama vile uelewa mdogo watu wanaofanya kazi ya kutafsiri, kukiuka taratibu na kanuni za kazi za tafsiri kwa wafasiri mbalimbali na upotoshaji wa mawazo yaliyopo kwenye matini chanzi pale yanapohaulishwa kwenda kwenye matini lengwa kutokana na kutoelewa lugha vizuri.




MAREJELEO
Cartford, J. C. (1995). A Linguistic Theory of Translation. London: Heinmann.
Mdee, S, J. (2011). Kamusi ya Karne ya 21; Kaamusi ya Kiswahili yenye Uketo zaidi  katika 
                Karne Hii. Nairobi: Longman Publisher LTD.
Mshindo, H. B. (2010). Kufasiri na Tafsiri. Zanzibar: Chuo Kikuu cha Chukwan.
Mwansoko, H, J. (2013). Kitangulizi cha Tafsiri; Nadharia na Mbinu. Dar es Salaam.
TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es salaam: TUKI.
Newmark, P. (1982). Approaches to Transslation. Oxford: Pergamon Press.
Nida, E, & Taber, C. (1969). The Theory and Practice of Translation. London: Prentice Hall.
Sengo, T, S, Y, M. (2009). Fasihi za Kinchi, The registered.
TUKI. (2002). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam. TUKI.
Wanjara, S. F. (2011). Misingi ya Ukalimani na Tafsiri. Dar es salaam: Serengeti Education  

                    Publisher LTD.

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny