Flower
Flower

Monday, April 29, 2019

NGELI ZA MAJINA

Kapinga (1983), anafafanua  neno ngeli limetoka katika lugha ya Kihaya likiwa na maana ya kitu au vitu.
TUKI (1990), wanafafanua ngeli za nomino ni kundi moja la majina yaliyo na upatanisho wa kisarufi unaofanana na viambishi vya umoja na wingi vinavyofanana.
Mgullu (1999) anasema istilahi ngeli imechukuliwa kutoka lugha ya Kihaya. Katika lugha ya Kihaya, neno “Ngeli” lina maana ya aina ya kitu, anaendelea kusema kuwa ngeli ni utaratibu wa taaluma ya sarufi ya lugha katika kupanga aina za majina.
Massamba na wenzake (2012), wanafafanua  ngeli ni mgawanyiko wa aina mbalimbali za nomino katika mtazamo wa kisarufi katika fikra ya viashiria vya nomino katika aina nyingine za maneno zinazoambatana nazo.
Kwa ujumla, ngeli ni utaratibu au namna ya kuweka nomino katika makundi yanayofanana au kuwiana. Utaratibu huu unaweza kuwa ni ule unaoangalia upatanisho wa kisarufi wa viambishi awali vya umoja na wingi au ule unaoangalia viambishi awali vya umoja na wingi wa nomino. Aidha uainishaji wa ngeli za nomino ni utaratibu wa kupanga aina za majina katika makundi kwa kuzingatia kuwiana au kufanana kisifa.
Baada ya kuona fasihi ya ngeli kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali ufuatao ni upungufu wa uainishaji ngeli kwa kigezo cha kimofolojia na kisintakisia. Kwa kuanza na kigezo cha kimofolojia.
Kigezo cha kimofolojia; Obuch (2015), anaeleza kuwa hiki ni kigezo kikongwe zaidi ya vyote na kimetumika kwa muda mrefu katika uainishaji wa ngeli za Kiswahili. Katika kutumia kigezo hiki nomino hutumika katika ngeli kwa kuzingatia kufanana kwa viambishi vya mwanzo vya nomino husika. Yaani viambishi awali vya nomino vya umoja na wingi vinavyofanana huwekwa katika kundi moja la ngeli za nomino. Katika kigezo cha kimofolojia tunapata makundi tisa (09) ya ngeli za nomino kwa mujibu wa Obuchi (keshatajwa).
Ubora wa uainishaji ngeli kwa kigezo hiki ni kama ifuatavyo:- Obuchi (2015), kwanza kigezo cha kimofolojia ndiyo kimekuwa msingi au chimbuko la vigezo vingine vya uainishaji wa ngeli za nomino za Kiswahili.  Mfano uainishaji ngeli kisintakisa na kisemantiki, kwa mujibu wa Obuchi (keshatajwa), anaeleza hiki ndicho kigezo kikongwe katika uainishaji wa ngeli za nomino, vilevile  ndicho kigezo cha kwanza kuzipanga au kuziainisha  nomino za Kiswahili katika makundi.  Hivyo kuwawezesha wanafunzi wa lugha ya Kiswahili na watu wote wanaozifuatilia kwa ukaribu lugha hii kuweza kubaini makundi ya nomino.
Unatusaidia kujua uhusiano iliopo baina ya Kiswahili na lugha za kibantu. Uainishaji ngeli kimofolojia unadhihirisha uhusiano wa moja kwa moja kati ya kiswahili na kibantu ambapo nomino nyingi za kibantu zinaingia katika uainishaji huu.Upungufu wa uainishaji ngeli kwa kigezo cha kimofolojia ni kama ifuatavyo:
Kutozingatia hadhi ya nomino, uainishaji wa nomino katika kigezo hiki cha kimofolojia haujazingatia kabisa hadhi ya nomino zenyewe. Mgullu (1999), ngeli ya KI-VI ina nomino zenye hadhi tofauti lakini zimewekwa katika kundi moja la nomino. Mfano ngeli ya KI-VI
Umoja
Wingi
kiti
Viti
kikombe
Vikombe
kipofu
Vipofu
kijana
Vijana
kiongozi
Viongozi

Hivyo nomino kikombe, kiti, kipofu, kijana na kiongozi hazina hadhi sawa lakini zimechanganywa katika ngeli moja na hivyo kuonyesha udhaifu mkubwa katika kigezo hiki cha kimofolojia.
Baadhi ya ngeli hazina viambishi vya umoja na wingi; kigezo hiki kwa mujibu wa Obuchi (2015), kinaangalia viambishi awali vya umoja na wingi vya nomino. Udhaifu unaodhihirika ni badhi ya ngeli kutokuwa na viambishi vya umoja na wingi. Mfano ngeli ya 7,8 hazina kabisa viambishi vya umoja na wingi. Vlevile baadhi ya ngeli viambishi vya umoja au wingi  havipo dhahiri. Mfano ngeli ya 5



Ngeli ya 5
Umoja
Wingi
5
U/N
Ukucha
ø Kucha
Ukuta
ø Kuta
Unywele
ø Nyele
7
N/N
Nyundo
Nyundo
Kuku
Kuku
Samaki
Samaki
Kalamu
Kalamu
Nyumba
Nyumba
8
K/U
kuimba
kuimba
kusoma
kusoma
kucheza
kucheza

Hivyo kutokana na udhaifu tuliouona na dhahiri kigezo hiki kinahitaji marekebisho.
Upungufu mwingine ni baadhi ya ngeli zinatumia viambishi vinavyofanana. Kuna baadhi ya ngeli viambishi awali vya umoja vinafanana, mfano ngeli ya 1 na 2. Na baadhi ya ngeli viambishi vya wingi vinafanana mfano ngeli ya 3 na 6.
Mfano

Ngeli
Umoja
Wingi
1
M/Mu-wa
Mtoto
Watoto
Mtu
Watu
2
M/Mi
Mti
Miti
Mchungwa
Michungwa
Mkoba
Mikoba
3
Ji/ma
Jicho
Macho
Jina
Majina
6
U/m/ ø
ugonjwa
magonjwa

Uasi
maasi

Hivyo kiambishi ‘M’ umoja katika ngeli ya kwanza na ya pili vinafanana na kiambishi ‘ma’ wingi katika ngeli ya 3 na 6 pia vinafanana kutokana na kufanana kwa viambishi katika baadhi ya ngeli kunaashiria upungufu.Kwa kumalizia , kigezo cha kisintaksia kama ifuatavyo.
Mgullu (1999), anafafanua Uainishaji wa ngeli kwa kigezo cha kisintaksia huziainisha ngeli za nomino kwa kuzingatia uhusiano wa nomino na maneno mengine katika tungo.Obuchi (keshatajwa), anafafanua kuwa uainishaji wa ngeli kisintaksia umelenga kutatua baadhi ya matatizo yaliyoainishwa na kigezo cha kimofolojia kilichozingatia viambishi awali vya nomino.
Iribemwangi (2008), anasisitiza kwamba matataizo mengi ya kiuainishaji huenda yakashughulikiwa kwasababu uainishaji huu hutilia mkazo suala zima la uamilifu badala ya umbo au muundo wa nomino husika.
Ufuatayo ni ubora na upungufu wa uainishaji wa ngeli kwa kigezo cha kisintaksia kwa kuanza na ubora kama ifuatavyo.
Obuchi (2015), kigezo hiki cha uainishaji wa ngeli kisintaksia ulilenga kutatua matatizo ya nomino zote zinazowahusu wanadamu na wanyama kuekwa katika kundi moja la nomino kinyume na zilivyowekwa awali kwa mfano katika uainishaji wa kimofolojia viumbe hai na vitu vilikuwa vinaingia katka ngeli ya nne lakini katika uainishaji wa kisintaksia viumbe hai vyote vinaingia katika ngeli ya kwanza
Ngeli yu-a-wa
Mfano
(a)  Kipofu anakuja
Vipofu wanakuja
(b)  Kiongozi anahutubia
Viongozi wanahutubia.
Hivyo basi huu pia ni ubora wa kigezo cha kisintaksia kwasbabu uainishaji huu  umetofautisha viumbe hai na visivyo hai katika ngeli tofauti.
Obuchi (2015), kigezo hiki husaidia kujua/kutambua uhusiano uliopo baina ya nomino na maneno mengine kwa mfano nomino na vitenzi
Mfano;  (i) Uzi umekatika
                   Nyuzi zimekatika
                (ii) Mtoto mzuri anacheza
                   Watoto wazuri anacheza
Katika mfano (i) tunaona namna nomino ilivyo na uhusiano na kitenzi na katika mfano (ii) tunaona namana nomino ilivyo na uhusiano na kivumishi na kitenzi hivyo basi huu pia ni ubora wa uainshaji wa ngeli kwa kigezo cha kisintaksia kwa kumalizia na upungufu wa kigezo cha kisintaksia kama ifuatavyo;
Obuchi (2015), anafafanua kuwa upungufu wa kigezo cha kisintaksia ni  kutokugusia nomino zenyewe moja kwa moja. Kwa mfano kutumia vipatanishi vyake ambavyo vipatanishi hivyo huwekwa katika vitenzi, vivumishi na viwakilishi mfano ngeli ya tatu LI-Ya
 Mfano   Linauma
              yanauma

Hapa tunaona namna ambavyo nomino haijatajwa moja kwa moja na badala yake kipatanishi kimewekwa katika kitenzi. Hivyo basi huo ni upungufu mmoja wapo.
Vilevile kufanana kwa viambishi ngeli hua pia ni upungufu mmoja wapo kwa mfano.

Ngeli
Mifano ya sentensi
ii
U - I
Umeanguka
Imeanguka
vi
U
 Ulimponza
vii
U – YA
Umeenea
Yameenea
viii
U – ZI
Umeibiwa
Zimeibiwa

Hivyo basi hapa tunaona viambishi ngeli ya 2,6,7 na ya 8 vinafanana hivyo basi huu pia ni upungufu wa kigezo cha kisintakisia.
Mgullu (1999), anabainisha upungufu wa kigezo cha kisintaksia kuwa baadhi ya ngeli vina viambishi viwili na ni vya kilahaja zaidi si Kiswahili sanifu kwa mfano.


Ngeli
Umoja
Wingi
1
YU – A – WA
Mtoto yu aja
Mtoto anakuja
Watoto wanakuja

Hivyo basi huu pia ni upungufu wa kigezo cha kisintaksia ngeli ya kwanza yu-a-wa kiambishi yu hakitumiki katika kiswahlili sanifu.
Kwa ujumla uainishaji wa ngeli kwa kigezo cha kimofolojia na kisintaksia una ubora wake na una upungufu wake, hivyo basi wataalamu hawana budi kufanya utafiti zaidi ili kupata kigezo bora zaidi ambacho kitatumika katika uainishaji wa ngeli.



MAREJEO
Kapinga, C (1983). Sarufi maumbo ya Kiswahili sanifu. Dar es salaam: TUKI.
Mgull, R.S (1999). Mtaala wa Isimu, Fonetiki, fonolojia na mofolojia ya Kiswahili:                                           Nairobi, Longhom Publishers.
Massamba, D.P.B et al (2012) Sarufi Miundo ya Kiswahili sanifu (SAMIKISA).                                                                     Sarufi Miundo ya Kiswahili sanifu Sekondari  na
                                                    vyuo. Dar es salaam: TUKI.
Obuchi,S.M na Mlikhwana, A (2015). Muundo wa Kiswahili ngazi na vipengele.                                                                                Nairobi Kenya : Printing services Ltd.
TUKI (1990). Kamusi ya Kiswahili sanifu. Dar es salaam: TUKI.


No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny