Kwa mujibu wa Neil Fraistal
(1985), wanafafanua kuwa kitabu ni makala iliyoandikwa kisanaa na makala hii inaweza kuzalishwa na
mtu yoyote yule mwenye uwezo wa kufanya hivyo. Tunaona fasili hii inajikita
katika swala la sanaa na kufanya kitabu kiwe kipana zaidi kwani swala la sanaa
ni pan asana na mtaalamu huyu hafafanui ni sanaa ipi.
Halikadhalika, TUKI (2014),
wanafasili kitabu ni maandishi yaliyowekwa pamoja katika kurasa zilizoandikwa
kwa mkono au zilizopigwa chapa na kupangwa kwa utaratibu maalumu na kutiwa
jalada. Tunaona fasili hii inajikita katika kurasa kuelezea maana ya kitabu
huku haiweki wazi utaratibu maalumu ambao kitabu inabidi kiwe nao.
Pia Kamusi pevu ya Kiswahili
(2016) wakifafanua maana ya kitabu wanaeleza kuwa ni kurasa zenye maandishi zilizofungwa pamoja
kwa utaratibu. Pia fasili hii inajikita katika kuelezea utaratibu maalumu na
kurasa lakini pia haiweki wazi huo utaratibu maalumu ni upi.
Kwa mujibu wa Oxford Advanced
Leaners Dictionary (2012), wanafafanua kuwa kitabu ni jumla ya karatasi
zilizochapwa ambazo zimewekwa kwa pamoja ndani ya jalada ambazo zinaweza
kusomwa. Fasili hii inajikita katika kuelezea kuwa kitabu lazima kiwe kwenye
jalada na kuwa kwenye mfumo wa karatasi.
Collins na Thesaurus (2018),
wanafafanua kuwa kitabu ni idadi ya vipande vya karatasi vyenye maneno
yaliyochapishwa juu yake ambayo yanaunganishwa pamoja na kuwekwa ndani ya
jalada gumu. Pia fasili hii inajikita katika kuelezea kuwa kitabu huwa kwenye
vipande vya karatasi na huwekwa kwenye jalada.
UNESCO katika (Business
Dictionary), wanaeleza kuwa Kitabu ni chapisho lolote lenye kurasa 48 au zaidi.
Tunaona fasili hii inajikita katika idadi ya kurasa katika kuelezea maana ya
kitabu huku ikisisitiza kitabu kuanza na kurasa 48 na kuendelea.
Kwa ujumla kutokana na fasili za
wataalamu hao tunaweza kufasili dhana ya kitabu kuwa ni mkusanyiko wa mawazo,
maarifa yaliyowekwa pamoja katika utaratibu maalumu na kuhifadhiwa kwa njia
mbalimbali kama vile maandishi katika nakala ngumu au laini na njia ya sauti.
Hivyo kutokana na fasili
mbalimbali za wataalamu mbalimbali nilizozipitia, naona kuwa uchangamani katika
dhana ya kitabu unatokana na mambo mbalimbali ambayo kutokana na fasili za
wataalamu yamejitokeza kama ifuatavyo;
Uchangamani wa kitabu
unaletelezwa na namna ya uhifadhi. Katika fasili za wataalamu mbalimbali
tunaona wataalamu wanatofautiana na kukinzana kuhusu kitabu kinapaswa
kihifadhiwe wapi. mathalani kwa mujibu wa kamusi Pevu (keshatajwa) wanasema
kitabu ni kile kilichotiwa jalada, halikadhalika Collins (keshatajwa) anaunga
mkono na kudai kuwa kitabu lazima kiwe kwenye jalada. Katika swala la uhifadhi
kitabu kinawezwa kuhifadhiwa kwa namna mbalimbali na bado kikawa kitabu kama
vile njia ya sauti, nakala laini na nakala ngumu na njia ya sidii na kaseti.
Dhana ya kitabu ni changamani
kutokana na idadi ya kurasa. Mathalani UNESCO wanadai kuwa kitabu ni kile
kinachoanzia kurasa 48 na kuandelea, hivyo kama kuna kitabu ambachokina kurasa
pungufu ya 48 sio kitabu. Fauka ya hayo kuna vitavu vya watoto ambavyo huwa
vina kurasa chache pungufu ya 48 na pia wataalamu wengine hawahusishi idadi ya
kurasa katika kufasili dhana ya kitabu hivyo kuleta uchangamani kuhusu dhana ya
kitabu.
Dhana ya kitabu ni changamani
kutokana na suala la umbo la kitabu. Suala la umbo la kitabu ni lipi limeleta
utata na kuchanganya wataalamu mbalimbali. Hii ni kutokana na kushindwa kujua
umbo la kitabu ni lipi, mathalani umbo la kitabu ni mstatili, bapa, pembe tatu
au duara. Suala la umbo pia limesababisha dhana ya kitabu kutoeleweka miongoni
mwa watu mbalimbali.
Dhana ya kitabu ni changamani
kutokana na suala la muonekano wa kitabu. Mathalani Oxford Advanced Learner
(washatajwa) wanadai kuwa kitabu huwa kipo kwenye muonekano wa karatasi
zilizochapwa na kuwa ndani ya jarada. Pia TUKI (washatajwa) wanaona kuwa kitabu
huwa kwenye muonekano wa karatasi zilizoandikwa kwa mkono. Hivyo tunaona kuwa
kitabu kinaweza kuwa katika muonekano tofautitofauti kama vile kuwa katika
nakala ngumu, nakala laini na kadhalika.
Dhana ya kitabu ni changamani
kutokana na suala la sura za kitabu. Mathalani kitabu kinatakiwa kiwe na sura
ngapi? Lakini pia kuna baadhi ya waandishi huandika kitabu bila ya kuzingatia
sura za kitabu. Suala la sura za kitabu husababisha pia dhana ya kitabu kuwa na
utata miongoni mwa wataalamu.
Pia dhana ya kitabu ni changamani
kutokana na suala la ukubwa wa kitabu. Mathalani kitabu kinatakiwa kiwe na
ukubwa upi na maandishi ya kwenye kitabu yanatakiwa yatumie fonti yenye ukubwa
upi. Wapo wataalamu wanaoamni kuwa kitabu kinatakiwa kiwe kikubwa, wastani au
hata kidogo hivyo kuleta changamoto katika dhana ya kitabu.
Kwa ujumla ili kuweza kuondoa
uchangamani katika dhana ya kitabu inabidi tuweke wazi vitu vya msingi ambavyo
vinatakiwa viwepo kwenye kitabu ili dhana ya kitabu ikamilike. Mathalani kitabu
kinabidi kiwe na sehemu za kitabu kama vile, jarada la mbele, jarada la mbele
ndani, nusu anuani, anuani, ukurasa wa haki miliki, tabaruku, dibaji, yaliyomo,
matini, bibiliografia, sherehe, faharasa, jarada la nyuma ndani na nje. Kwa
kufanya hivyo kunaweza kuondoa utata juu ya dhana ya kitabu. Pia kutoa elimu
kwa waandishi, wachapishaji na wachapaji kuhusu uandishi mzuri wa kitabu na
mambo kadha wa kadha ambayo wanatakiwa kuzingatia katika uandishi wa kitabu.
MAREJELEO
Collins na Thesaurus. (2018). English
Dictionary Complete and Unbrigde: Third edition.
Faistal, N. na Flanders,
J.(1985). Textual Scholarship: Cambridge University Press.
Publisher
Kamusi Pevu ya
Kiswahili (2016). Nairobi: Vide – muwa publisher Limited.
Oxford Advanced
Learners Dictionary. (2012). Oxford University Press Elt.
TUKI (2014). Kamusi
ya Kiswahili Sanifu. TUKI: Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com