Wamitila
(2004) anaeleza kuwa fasihi ni sanaa
inayotumia lugha na ambayo hujishughulisha na binadamu pamoja na maisha yake na
huathiri, hugusa, na huacha athari fulani na hupatikana katika mbo ambalo
linamtambulisha kwa jamii fulani.
TUKI
(2004) wanaeleza kuwa dhana ya fasihi inamaana nyingi, kama vile enye kutumia
lugha safi na nzuri, somo linalohusiana na tungo za Sanaa kama vile ushairi,
riwaya, tamthiliya, tenzi, semi vitendawili, hadithi na ngano.
Kwa
ujumla fasihi ni sanaa inayotumia lugha kiufundi ili kufikisha ujumbe kwa
hahira iliyokusudiwa. Fasihi imegawanyika katika makundi mawili ambayo ni
fasihi simulizi na fasihi andishi. Pia dhana ya mtindo imefasiliwa na wataalamu
mbalimbali kama ifuatavyo;
Wamitila
(2003) amefasili mtindo kuwa ni jumla ya mbinu au sifa zinazomwezesha mwandishi
kuwasilisha ujumbe wake. Anaendelea kusema dhana ya mtindo hurejelea sifa
maalumu za mwandishi ndio humpambanua mwandishi huyu na mwenzake
Wamitila (2010), anasema mtindo ni elementi
muhimu sana katika kazi ya kifasihi ili kuweza kubainisha sifa za kimtindo za
kazi ya kifasihi. Sifa hizo ni kama uchanganuzi wa matini au kazi ya kifasihi
au kazi inayohusika kama uteuzi wa msamiatai wa mtunzi, miundo na mpangilio wa
sentensi, uteuzi wa matumizi ya tamathali za semi na jazanda, usawiri wa
wahusika, motifu na dhamira zinazokaririwa katika kazi ya watunzi, usimulizi na
mbinu za usimulizi wenyewe hata sifa za uakifishi hasa zinazoelekea kukiuka
njia za kawaida za kuakifisha.
Kwa
ujumla mtindo ni upekee wa mwandishi, au nile namna ambayo mwandishi wa kazi ya
fashi hujieleza katika kazi yake. Ni kweli kwamba “mtindo ndio kipengele pekee
cha fasihi ambacho huweza kumtofautisha mwandishi mmoja wa kazi ya fasihi na
mwandishi mwingine kwa sababu kila msanii anauwezo wake wa kuteua na kutumia
vipengele vya fani na maudhui vinavyojenga mtindo tofauti na msanii mwingine.
Zifuatazo ni hoja zinazothibitisha kuwa mtindo ni kipengele pekee cha kifasihi kinachoweza
kumtofautisha mtunzi mmoja wa kazi ya fasihi na mwingine.
Mandhari
ni kipengele kinachomtofautisha mtunzi mmoja na mwingine, Wamitila (2003)
anaeleza kwamba mandhari hutumiwa kuelezea mahali ambapo tendo fulani
hutendeka. Watunzi wa kazi za fasihi hutumia mandhari tofauti tofauti katika
kuwasilisha kazi zao. Matumizi ya mandhari fulani yanauwezo mkubwa wa
kumtofautisha mtunzi mmoja na mwingine. Mathalani mtunzi Shaaban Robert kwa
kiwango kikubwa sana katika kazi zake anatumia mandhari isiyo halisi mfano
katika vitabu vyake vya “KUFIKIRIKA na KUSADIKIKA” ametumia mandhari isiyo
halisi yaani haiwezi kupatikana ulimwenguni. Ukimlinganisha na mtunzi Emmanuel
Mbogo katika kazi zake za “WATOTO WA MAMA NTILIE na
MALKIA BIBI TITI MOHHAMED” ametumia mandhari halisi ambayo inapatikana katika
mazingira tunayoishi. Hivyo basi mandhari ni kipengele muhimu sana cha mtindo
kinachomtofautisha mtunzi mmoja na mwingine.
Falsafa
ya mwandishi kama kipengele cha mtindo kinachomtofautisha mtunzi mmoja na
mwingine, Madummulla (2009) anaeleza kuwa falsafa ni wazo ambalo anaamini
linaukweli fulani unaotawala maisha yake pamoja na maisha ya jamii. Kila mtunzi
wa kazi ya fasihi huweza kuwa na falsafa yake inayoweza kumuongoza na
kumpambanua kukamilisha kipengele cha mtindo. Mathalani mtunzi Shaaban Robert
kazi zake mbalimbali falsafa inayojitokeza ni “wema kushinda ubaya”. Lakini
mwandishi Euphraz Kezilahabi falsafa anayoitumia katika kazi zake nyingi ni
“maisha hayana maana”. Hivyo basi kila mtunzi ameonekana kuwa na falsafa yake
ambayo inampambanua katika kipengele cha mtindo.
Wahusika
ni kipengele kingine kinachomtofautisha mtunzi mmoja na mtunzi mwingine,
Senkoro (2011) anaeleza kuwa wahusika ni watu ama viumbe waliokusudiwa
wawakilishe dhana, mawazo, au tabia za watu katika kazi za fasihi huweza
kutofautiana katika kupambanua na kutumia wahusika fulani. Tunaposoma kazi za
Euphrazi Kezilahabi za “NAGONA na MZINGILE” anatumia wahusika ambao si rahisi
kupatikana katika mazingira halisi kama vile wahusika majoka, mizimu, majini,
ambao ni wahusika waliochorwa kuibua taswira fulani wakati katika kazi nyingi
za Penina Mhando anatumia wahusika halisi yaani ambao hupatikana na mazingira
tunayoishi kama mhusika “chizi” kama ni mtu ambaye hathaminiwi katika jamii
lakini anamchango mkubwa. Hivyo kila mtunzi ameonekana kujieleza na kuonyesha
upekee wake kupitia mazoea ya kutumia wahusika fulani kukamilisha dhana ya
mtindo.
Motifu
kama kipengele cha mtindo kinachomtofautisha mtunzi mmoja na mwingine, Mulokozi
(1996) anaeleza kuwa motifu ni kipengele cha kijamii kinachohusu kurudiwa
rudiwa kwa wazo au dhamira katika sehemu kubwa ya kazi ya fasihi. Watunzi wa
kazi za fasihi huweza kujieleza na kuonesha wake kupitia kurudia rudia baadhi
ya vipengele vya fani na maudhui. Mfano Euphraz Kezilahabi katika kazi za
“NAGONA na MZINGILE” ameonekana kutumia sana “motifu ya safari” lakini katika
utunzi wa hadithi nyingi za kijadi zinatumia “motifu ya bibi kizee”. Hivyobasi
motifu imetofautisha kujieleza kwa kazi zao na kukamilisha mtindo baina ya
utunzi wa kazi hizo za kifasihi.
Uteuzi
wa msamiati kama kipengele kinachomtofautisha mtunzi mmoja na mwingine. Watunzi
wa kazi za fasihi huweza kuonyesha utofauti au upekee katika mazoea ya kuteua
msamiati fulani katika lugha. Mathalani Mohamed Ahmed katika kazi zake nyingi
za kishairi mara nyingi anatumia misamiati ya kiarabu, hali hii humtofautisha
mtunzi huyu na mtunzi mwingine lakini pia msanii Mrisho Mpoto katika kazi zake
za fasihi anatumia misamiati ya mafumbo ambayo ni vigumu kueleweka kwa hali ya
kawaida. Hivyo uteuzi wa msamiati katika mtindo huonyesha utofauti mkubwa katika
kazi za fasihi.
Taswira
kama kipengele kinachomtofautisha msanii mmoja na mwingine, Taswira ni lugha
inayochora picha ya vitu au mahali kwa kutumia ishara. Jilala (2016) anasema
taswira ni kipengele kinachoweza kutumika katika ulinganishaji wa kazi mbili za
fasihi. Mfano Euphraz Kezilahabi katika kazi zake za “ROSA MSTIKA, NAGONA na
MZINGILE” ameonekana kupendelea kutumia taswira sana katika kujitofautisha na
watunzi wengine tofauti na watunzi wengine wanaopendelea kutumia lugha ya wazi
ambayo haimpi shida msomaji kuelewa na hivyo kuonekana kujitofautisha na msanii
mwingine.
Dhamira
ni kipengele kingine kinachomtofautisha mtunzi mmoja na mwingine, dhamira ni
wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi za fasihi. Watunzi
mbalimbali hutunga kazi zao ambazo zina maudhui tofauti. Mathalani Diamond kazi
zake nyingi zinz maudhui ya mapenzi wakati Roma Mkatoliki kazi zake nyingi huwa
na maudhui ya ukombozi wa kisiasa na kijamii.
Hivyobasi
dhamira ni kipengele muhimu katika mtindo na huwatofautisha watunzi.Kwa ujumla
mtindo ni kipengele muhimu katika fasihi ambacho kinapaswa kuangaliwa kwa
mawanda mapana sana kwani ndicho kipengele pekee kinachompambanua msanii mmoja
na mwingine katika fani na maudhui kwa ujumla. Pia kulingana na mawanda mapana
ya mtindo tuliyoyaona inatosha kudhihirisha kwamba mtindo si kipengele cha
kifani tu bali huweza kuwa cha maudhui pia.
MAREJELEO.
Jilala, H. (2016)
Misingi ya Fasihi Linganishi.
Madumulla, J. (2009). Riwaya ya Kiswahili Nadharia na Misingi ya Uchambuzi.
Dar es salaam.
Mture
Educational Publishers.
Mulokozi, M. M. (1996).
Fasihi ya Kiswahili. Dar es salaam. DUP.
Senkoro, F. (2011) Fasihi: Dar es salaam. Kauttu Limited.
Wamitila,
K. W. (2003), Kamusi ya Fasihi na Nadharia. Focus Publications Ltd.
Wamitila K.
W. (2010), Kanzi ya Fasihi Misingi ya
Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi. Vide – Muwa
Publishers.
Wamitila,
K.W. (2004), Kichocheo cha Fasihi
Simulizi na Andishi. Nairobi
English Press.
TUKI, (2004)
“Kamusi ya Kiswahili sanifu”. Dar es
salaam; Oxford University Press.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com