Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo
tumefasili dhana mbalimbali zilizojitokeza pamoja na Historia fupi
ya Siti Binti Saad, sehemu ya pili ni
kiini cha swali ambapo tutahakiki vipengele vya fani na maudhui na mwisho ni hitimisho la swali.
TUKI
(2014), wanadai kuwa uhakiki ni uchambuzi wa ndani kabisa wa kitu au jambo liloloambatana
na fikra za mchambuzi.
Riwaya
ya kiwasifu, ni riwaya ambayo mwandishi huandika kwa lengo la kumhusu mtu fulani.
Mfano Riwaya ya Wasifu wa Siti Binti Saad.
Ifuatayo ni Historia fupi ya Siti Binti Saad tangu kuzaliwa kwake hadi umauti
wake ulipomkuta.
Siti
Binti Saad alizaliwa katika Kijiji cha Fumba, Zanzibar mwaka 1880. Alipozaliwa
alipewa jina la Mtumwa hii ni kwa
vile alizaliwa katika kipindi cha utumwa wa Kiarabu. Jina la Siti alipewa na
mkabaila mmoja wa Kiarabu.
Baba
yake bwana Saad alikuwa ni Mnyamwezi
kutoka Tabora na mama yake alikuwa ni Mzigua toka Tanga, lakini wote wawili
walizaliwa Zanzibar. Hali ya maisha ya familia yao ilikuwa ni duni sana na
walijishughulisha zaidi katika shughuli za kilimo na ufinyanzi kazi ambazo Siti alijifunza na kuzimudu vizuri pia.
Kama
Waswahili wasemavyo “kuzaliwa maskini si kufa maskini” Siti alibarikiwa kuwa na
kipaji cha pekee cha uimbaji. Kipaji hiki kilimsaidia sana tangu siku za awali
za maisha yake kwani alitumia uimbaji wake kuuza vyungu vya mama yake
alivyokuwa akimsaidia kuvitembeza. Siti alipoimba sauti yake iliweza kupaa na
kusafiri kwa umbali wa maili nyingi nah ii ndio ilikuwa ishara ya watu kujua
kwamba vyungu vya vya akina Siti vinapita leo.
Kutokana
na wakati ule elimu kwa Watoto wa kike kutotiliwa mkazo, Siti hakuwahi kwenda shule wala kuhudhuria mafunzo ya Qur-an. Hivyo
mnamo mwaka 1911 aliona ni bora ahamie mjini ili kuboresha Maisha yake Zaidi.
Ujio wake wa mjini ulikuwa wa neema kwni alikutana na bwana mmoja wa kundi la
muziki wa Taarabu la “Nadi Ikhwani Safaa”
aliyeitwa Muhsin Ali. Katika kipindi hicho
hilo ndilo lilikuwa kundi pekee la muziki wa taarabu lililoanzishwa na Sultan
mpenda starehe na anasa bwana Seyyid Barghash Said. Kundi hili lilikuwa la wanaume peke yake, wanawake hawakuruhusiwa
kujiunga na vikundi vya muziki kwa vile ilikuwa inachukuliwa kama ni uhun. Bwana
Muhsin alikiona kipaji cha pekee cha Siti
na hivyo akajitoa kumfundisha kuimba kwa kufuata vyombo vya muziki na lugha
ya kiarabu.
Baada
ya hapo alikwenda kumtambulisha kwa wanamuziki wenzie wa “Nadi Ikhwani Safaa” amabo
bila kusita wakaanza kufanya naye maonyesho mbalimbali katika jamii. Walipata
mialiko mingi hasa kutoka kwa Sultani na matajiri wengine wa Kiarabu, pia
katika maharusi na sharehe zingine mbalimbali, inasemekana ulifika wakati
ambapo sherehe ilishindwa kufana kama Siti Binti Saad hakuwepo kutumbuiza. Siti alikuwa na moto wa kuotea mbali na
jina lake lilivuma kwa haraka sana hadi nje ya mipaka ya nchi na bara la Afrika.
Mwaka
1928, Kampuni ya kurekodi muziki ya Columbia and His Master’s voice yenye
makazi yake Mumbai India ilisikia umaarufu wa Siti Binti Saad na hivyo
ikamwalika yeye pamoja na kundi lake kwenda kurekodi kwa lugha ya Kiswahili ili
kujaribu kama muziki wake utauzika. Kampuni ili haikuweza kuamini jinsi muziki
ule ulivyouzika kwa kasi kubwa kwani wastani wa santuri 900 ziliweza kuuzika
katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo, hadi kufikia 1931 santuri 72,000
zilikua zimeuzwa. Kutokana na kusambaa kwa santuri hizi, umaarufu wa Siti ulizidi mara dufu watu kutoka
sehemu mbalimbali za dunia walikuwa wakija Zanzibar kuja kumwona. Mambo yalizidi
kuwa mazuri kwa Siti hadi ikafikia
hatua kampuni ya kurekodi ya Columbia kuamua
kujenga studio ya kurekodi muziki palepale Zanzibar maalumu kwa ajili ya Siti Binti Saad.
Hatua
hiyo ya hadi kujengewa studio iliwaumiza wengi wenye wivu, hivyo wakaanza
kumtungia nyimbo za kumkejeli ili kumshusha na hasa walitumia kigezo kwamba hana
uzuri w asura, nyimbo nyingi ziliimbwa kumkashifu Siti lakini hawakuweza kufanikiwa katika hilo.
Tarehe
8 Julai 1950 Siti Binti Saad
alifariki dunia na kuacha pengo kubwa katika fani ya Taarabu. Ingawa pengo hilo
haliwezi kuzibika lakini kuna watu wengi walioweza kuibuka na umaarufu wa
kuimba taarabu kupitia kwake, mfano hai ni Bi Kudude.
Baada
ya kuangalia historia fupi ya Siti Binti
Saad, kupitia riwaya hii ya Wasifu wa
Siti Binti Saad iliyoandikwa na Shaaban Robert ufuatao ni uchambuzi wa
vipengele vya Maudhui na Fani ambavyo vimejitokeza katika kazi yetu. Kwa kuanza
na kipengele cha Maudhui ambacho huweza kubeba vipengele kama vile dhamira,
ujumbe, migogoro na Falsafa.
TUKI
(2014), wanadai kuwa dhamira ni kiini cha jambo au habari iliyosimuliwa ama
kuandikwa, hasa katika fasihi. Riwaya ya Wasifu
wa Siti Binti Saad kina dhamira ambazo kimsingi zinazungukia mambo mengi
yanayohusu maisha ya watu wa Tanzania. Kwa kutumia mbinu mbalimbali mwandishi
ameonyesha mambo mbalimbali ambayo yaliuwa yanamkubwa Siti Binti Saad
katika maisha yake yote. Zifuatazo
ni dhamira ambazo zimejitokeza katika riwaya ya Wasifu wa Siti Binti Saad.
Mosi,
suala la umaskini, katika riwaya hii mwandishi anamuelezea mhusika Siti kama
mtu ambaye amezaliwa katika familia ya wazazi maskini ambapo wazazi walikuwa
katika hali ngumu ya na kumfanya Siti alelewe katika mazingira magumu kwani
baba yake alikuwa ni mkulima na mama yake alikuwa ni mfinyazi hivyo hali hii ya
maisha ikamfanya Siti awe mtoto wa nyumbani akishinda na wazazi wake. Matahalani
kwenye ukurasa (2) mwandishi anasema;
“Mwanamke huyu alizaliwa Fumba na
wazazi waliokuwa maskini baba yake
alikuwa mkulima na mama yake alikuwa mfinyazi.”
Hivyo,
suala hili la umaskini pia lipo katika familia nyingi za Kitanzania ambazo kutokana
na hali ngumu ya maisha hupelekea kuathiri maisha ya mtoto katika ukuaji wake.
Pili,
ukosefu wa elimu, katika riwaya hii mhusika Siti ameonekana kama mtu ambaye
hakupata bahati ya kuweza kupata elimu hii ni kutokana na wazazi wake kutofahamu
umuhimu wa elimu kwa binti yao. Suala hili linajitokeza hasa katika ukurasa wa (2)
pale mwandishi anaposema;
“Wazazi
wake waliokuwa masikini
na
wajinga wa kusoma hawakushughulika
na
kuweka shajara ya vitu vidogo kama
wakati,
siku na tarehe ya uzazi wa mtoto wao”.
Hivyo,
suala hili la ukosefu wa elimu lilisababisha wazazi wake Siti kushindwa
kuandika kumbukumbu ya tarehe na mwezi ambao Siti alizaliwa pia lilipelekea wao
kutokua umuhimu wa elimu hivyo ikapelekea hata kumyima haki ya elimu binti yao.
Tatu,
suala la dini, aidha mwandishi amemuonyesha Siti kama mtu ambaye alikuwa anafuata
misingi ya dini yake ya uislam kwani alikuwa anatekeleza ibada mbalimbali za
dini yake kama vile kufunga. Suala hili linajitokeza katika ukurasa wa 17 pale
mwandishi anaposema;
“Siti
alikuwa mwanamke mcha Mungu wa sala. Alisali vipindi
vitano kila siku, akafunga faradhi na suna katika Maisha
yake yote.”
Hivyo,
licha ya kukosa elimu ya dunia, Siti aliweza kupata elimu ya dini ya Kiislam na
kuishi katika misingi ya dini yake. Hivyo hii ni kawaida kwa watu wanaoishi
maeneo ya Zanzibar kufuata maadili ya Dini ya Kiislam.
Nne,
uvumilivu, Aidha mwandishi amemchora mhusika Siti kama mtu ambaye alikuwa
mvumilivu ambaye alikuwa hapendi kukata tamaa licha ya kuwa na hali ngumu ya
kimaisha. Aidha Siti aliweza kuhangaika ili aweze kupata ridhki ili kuyafanya maisha
yake yaweze kupata afueni. Suala linajitokeza kwenye ukurasa wa (23) pale mwandishi
anaposema;
“Alikuwa
si mwanamke wa kukata tamaa, akaonyesha saburi na uvumilivu wa ajabu. Kwa desturi, mwanadamu alikuwa kiumbe wa
ajabu siku zote.”
Aidha suala hili la uvumilivu linajitokeza
tena kwenye ukurasa wa 24 pale mwandishi anaposema
“Alikuwa
na moyo mkuu. Hii si mara yake ya kwanza kujaribiwa. Dhiki kubwa na umaskini
mkali vilikuwa vimekwisha mjaribu vikamfanya imara kama mwamba”.
Hivyo
ni dhahiri kuwa katika jamii za watu hususani wanawake wapo ambao wana moyo wa
uvumilivu wa kupambana na matatizo, kejeli, changamoto mbalimbali za kimaisha.
Tano,
uwajibikaji, katika riwaya hii mwandishi amemsawiri mhusika Siti kama mtu
ambaye anawajibika na shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuweza kuendesha maisha
yake. Mwandishi anatuambia kuwa Siti alikuwa anafanya shughuli kama vile kuuza
vyungu, vikundi vya Taarabu. Suala hili la uwajibikaji linajionesha kwenye
ukurasa wa (5) pale mwandishi anaposema;
“Alizunguka
vichochoro visivyo hesabikia katika mji wa unguja akitafuta huku na huko wanunuzi
wa vyungu vyake katika kila mlango wa nyumba. Katika kila hatua moja njiani
alinadi kwa sauti kuu, Vyungu vyungu, vyungu vizuri, nunueni! Vyungu
kwa bei rahisi!”
Hivyo
hata katika jamii wapo wanawake ambao wanajishughulisha na biashara mbalimbali ili
ziwasaidie kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Sita,
Suala la kujiheshimu na kujithamini, kwa kuthibitisha dai hili mwandishi
amemtumia mhusika Siti ambaye licha ya kwamba alipata umaarufu na mali nyingi
kupitia kazi yake ya uimbaji, lakini hakutumia nafasi hiyo vibaya kwa
kujirahisisha kwa wanaume juu ya vitendo vya kingono, bali alikuwa akijitunza
na kujistahi mwili wake ili kutunza heshima yake. Vilevile wakati yupo kijijini
alikuwa akifanya kazi ya kuuza vyungu ili kujipatia riziki kuliko kuwa tegemezi
kwa kuomba kwa wanaume ambapo mwisho wa siku angeweza kujiharibia heshima yake.
Pia mwandishi anasema Siti alikuwa ni
mfano wa kuingwa kwa wanawake wote wa kisiwa cha Unguja. Suala hili
limejitokeza katika ukurasa wa (49,54 na 59). Mathalani katika (uk 59)
mwandishi anasema;
“Afrika
Mashariki ilikuwa na sababu kubwa ya kuona fahari juu yake. Mwili wa mwanamke
huyu ulikuwa wake mwenyewe, hakuuza katika wakati wowote kwa thamani yoyote ya utajiri.
Nafsi yake ilikuwa yake mwenyewe hakuiuza kwa heshima yoyote. Alikuwa mwanamke
wa mazao ya adili kubwa, si mazao ya upotevu, aibu wala ulegevu”
Hivyo
hata katika jamii ya leo kuna wanawake ambao wanajiheshimu na kujithamini kwa
kulinda utu wao.
Mtaji
wa maskini ni nguvu zake mwenyewe, jambo hili linajidhihirisha hususani katika
ukurasa wa 5 pale mwandishi anaposema
“Alizunguka
vichochoro visivyo hesabikia katika mji wa unguja akitafuta huku na huko
wanunuzi wa vyungu vyake katika kila mlango wa nyumba. Katika kila hatua moja
njiani alinadi kwa sauti kuu, Vyungu vyungu, vyungu vizuri, nunueni! Vyungu
kwa bei rahisi!”
Mvumilivu
hula mbivu, kwa kumtuia mhusika Siti mwandishi anasema kuwa, Siti alijuwa
kwamba kama anataka kufanikiwa ni lazima avumilie matusi, wivu na maneno yote
ya kashifa aliyokuwa akiambiwa na watu. Mathalani katika (uk 54) mwandishi
anasema;
“Hapana shaka
kwa matukane yale yaliyorarua kama kucha za chuma katika moyo wake, alikuwa
katika maudhi yasiyoelezeka kwa lugha ya kitabu, lakini alivumilia. Alijua
kwamba ilimpasa kupigana na wivu, masingizio, kashifa, ujinga na ulimwengu
mzima kiungwana kama alitaka kufanikiwa”
Aidha,
malezi mabaya ni chanzo cha kuwa na kizazi kisichokuwa na msaada katika jamii.
Mwandishi anasema kuwa wazazi wengi, waliwalea watoto wao kama malaika, bila ya
kuwapa mbinu na misingi ya kupambana na kipindi kigumu cha maisha katika siku
za mbeleni. Mathalani katika (uk 62) mwandishi anasema;
1.
“Baadhi ya wazazi
walikuza mabinti zao kana kwamba ni malaika. Walakini, walipofanya hivi
hawakujali kuwafundisha neno lolote la kutenda juu ya kujikimu wenyewe katika
nyakati za dhiki. Mabinti kama hao walikuwa hawawezi kusimama kwa miguu yao,
msaada wa wazazi wao ulipokosekana kwa mabadiliko ya Maisha. Hivyo jambo bora
lilikuwa kujaribu kuweka tayari kila mwanamke, katika utoto wake, kwa heri au
shari iliyoletwa na mabadiliko ya Maisha katika dunia”
Ili
kufikia mafanikio katika jamii ni lazima kujitoa mhanga. Mwandishi amemtumia
mhusika Siti ambaye licha ya kwamba watu wa jamii yake walimuona hawezi kufanya
jambo lolote la kuacha alama katika jamii yake lakini bado aliamini kwa kupitia
sauti yake ataweza kufanya jambo la maana. Kufuatia kuimba Siti alikuwa maarufu katika Unguja na hata katika
Afrika Mashariki kwa ujumla. Mathalani katika (uk 49 na 50) mwandishi anasema;
“Kama Siti alitazama sura yake mbaya akasema
kwamba hawezi kutenda neno; asingalitenda jema lolote, kama alitazama rangi
yake nyeusi akasema kwamba alistahili kuwa katika sahau; asingalikumbukwa na
mtu hata mmoja, kama alijipima akajion alikuwa duni; asingalitukuka haya
kidogo, na kama hakujaribu kufumbua tambo ya Maisha, asingalipata jawabu lake
milele.
Fauka
ya ujumbe au mafunzo yaliyopatikana katika riwaya ya Wasifu wa Siti Binti Saad Pia, kuna migogoro ambayo tumeweza kuipata
baada ya kusoma riwaya hii, migogoro hiyo ni kama ifuatayo;
Mosi,
mgogoro kati ya Siti na nafsi yake, Licha ya kujariwa ujuzi wa ususi, kushona
na kufinyanga vyungu, Siti kuna jambo lingine alilokuwa analiwaza lililomfanya aliwaze,
aliote mchana na usiku bila ya kupata majibu na mwisho ya siku akaamua kuhama
kijijini kwao na kwenda unguja kwa madhumuni ya kuanza Maisha mapya. Mathalani
katika (uk 7) mwandishi anasema;
“Alikuwa
hana starehe kwa sababu mambo mawili haya, yalikuwa yakipingana katika moyo wake
wakati wote. Alikuwa hana mashauri wa kushiriki naye siri kama ile”
Pili,
mgogoro kati ya Siti na kikundi kingine cha taarabu, kutokana na mafanikio ya Siti
ilimbidi apambane na changamoto zilizokuwa zikiibuka kutoka kwa wanajamii,
changamoto hiyo ilikuwa ni kashfa, wivu, kudharauliwa na matukano. Lakini Siti aliushinda
mgogogro huu kutokana na tabia yake ya kiungwana na hivyo alimchukulia kila
mmoja kama alivyo. Mathalani kaika (uk 22) walimtungia wimbo uliokua ukii mbwa
hivi:
“Siti Binti Saad;
Ulikuwa mtu lini?
Ulitoka shamba,
Na kaniki mbili chini,
Kama si sauti;
Ungekula nini?
Tatu, mgogoro kati Siti na Wanakijiji wa Fumba, mwandishi anaeleza kuwa wanafumba
walimuona Siti ni mtu wa kawaida sana
na asiyeweza kutenda jambo wala kuacha alama katika jamii lakini Siti alijiona ni mtu anayeweza kufanya jambo
zuri zaidi ya kushona na kufinyanga vyungu. Hivyo ndio maana aliamua kuhama
kijijini kwao na kuhamia Unguja ili kutimiza ndoto yake. Mathalani katika (uk 7)
mwandishi anasema;
“watu walioonana na Siti katika utoto wake hawakudhani
hata mara moja kwamba maumbile yalikuwa yamekusudia kumtoa katika giza la sahau
na kumtia katika nuru ya umaarufu baadaye. Hivyo siti aliondoka kwao bila kitu
kingine isipokuwa kaniki mbili zizizokuwa juu ya Ngozi yake, ili kwenda
kujaribu kutimiza ndoto yake”
Falsafa ya mwandishi, katika riwya hi
mwandishi anaamini kuwa ‘wema huushinda ubaya’. Falsafa hii imejidhihirisha
pale ambapo Siti alikuwa akizushiwa
maneno machafu ya kumfedhehesha na kumdharaulisha lakini ukweli ulibaki kuwa
alikuwa na kipaji cha kuimba na ndicho kilichomfanya kuwa maarufu katika kisiwa
cha Unguja na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Fauka ya kuangalia Maudhui na vipengele
vyake, vifuatavyo ni vipengele vya fani vilivyojitokeza katika riwaya ya Wasifu wa Siti Binti Saad.
Wamitila (2016), anaeleza kuwa fani ni ufundi
anaoweza kutumia mwandishi katika kuifinyanga kazi yake. Fani huusisha
vipengele kama vile muundo, mtindo, wahusika, mandhari. Katika riwaya ya Wasifu wa Siti Binti Saad vipengele vya
fani vilivyojitokeza ni kama vifuatavyo.
Muundo, katika riwaya hii mwandishi
ametumia muundo wa moja kwa moja. Ameanza kwa kuelezea Maisha ya Siti alipokuwa
mtoto katika kijiji cha Fumba, harakati zake za kutafuta mafanikio katika mji
wa unguja na mwisho mwandishi ameelezea mafanikio aliyoyapata pamoja na kifo
chake.
Mtindo, Mwandishi ametumia mtindo wa matumizi
ya nafsi ya tatu umoja kwa kiasi kikubwa. Aidha katika kukamilisha mtindo wake
mwandishi ametumia nyimbo ili kuweza ujumbe kwa urahisi wa walengwa husika. Uk
29, 32.
Matumizi ya Lugha, lugha aliyoitumia mwandishi
ni lugha rahisi iliyojaa misemo, methali, tamathali za semi na mbinu nyingine
za kisanaa.
Misemo
i.
Maisha ni matendo sio usingizi. Uk 49
ii.
Kusema fedha kujibu dhahabu. Uk 43
iii.
Ukidunisha mtu leo, utamwona juu ya kilele
cha utukufu kesho. Uk23
iv.
Cheka uchafu, usicheke kilema. Uk 30
Methali
i.
Chema cha jiuza kibaya chajitembeza. Uk 21
Tamathali za Semi
Tashibiha
i Imara kama mwamba. Uk 7
ii Alikuwa na moyo wa kuhifadhi mambo wepesi
kama umeme. Uk 10
iii. Jasho liliminiika kama maji mwilini
wake. Uk 5
Tashihisi
i.
Pwani ilipokuwa ikimuita, bara ilikuwa
ikimpungia nguo. Uk 48
ii.
Siti alikuwa na sauti ya kulevya kweli. Uk
46
iii.
Kwa maneno macheche nay a waziwazi aliweza
kuviringisha kipopo cha fikra kubwa. Uk43
Tabaini
i.
Sauti yake ilikuwa nzuri kama moyo wake,
na moyo wake ulikuwa mwema kama moyo wake. Uk 52
ii.
Kwa hali iwayo yote katika umaskini au
tajiri; ujinga au elimu, enzi au uraia tabia ilikuwa kitu cha maana. Uk 53
iii.
Ilikuwa zuio au pingamizi, jeuri au kiburi,
udanganyifu au ugomvi, ushenzi au utovu hayo yote yalipingwa.
Mbinu
nyingine za Kisanaa
Takriri
i.
“Vyungu Vyungu, Vyungu vizuri, nunueni!
Vyungu kwa bei rahisi”. Uk 5
ii.
Kinyume nyume, kimbele mbele. Uk 9
Mjalizo
i.
Aliwaza, akaota, aliota, akawaza mchana na
usiku. Uk 22
ii.
Hawakubuni neno, hawakusheheni neno,
hawakujaribu neno. Uk 25
Wahusika
Siti,
Huyu ndiye mhusika mkuu wa riwaya hii. Siti alikuwa na mweupe, unene kiasi, Sura
yenye mvuto kiasi na sauti nzuri, si mrefu lakini hakuwa mfupi. Kwa tabia Siti alikuwa
mwanamke aliyekuwa anapenda kujishughulisha na shughuli tofauti tofauti za maendeleo
kwani alihama kijijini kwao fumba na kwenda unguja kutafuta Maisha.
Vilevile Siti alikuwa na
moyo wa kuthubutu kila jambo, alikuwa haamini kuwa kuna kitu kinaitwa
haiwezekani kwani aliweza kujiunga na kundi la taarabu kule unguja akiwa
mwanamke peke yake kati ya wale wanaounda kundi hilo la mziki wa Taarabu.
Wahusika
wadogo
i.
Musa
na Mbaruku, hawa ni wadogo zake Siti.
ii.
Ali
Saud,
huyu ni kijana ambaye alimsaidia Siti.
iii.
Muhsin
Ali,
huyu alikuwa mpiga udi mahiri, naye ndiye aliyemfundisha Siti Kiarabu na kuimba.
iv.
Rajabu,
huyu alikuwa mume wake Siti.
v.
Mariyam,
Huyu ni mtoto wa Siti.
vi.
Subeti,
Buda, Shaaban na Mbaruku, hawa walikuwa wanakikundi cha mziki
wa Taarabu.
Mandhari
Mandhari iliyotumika kwenye riwaya hii ni
mandhari halisi, maeneo yanayotajwa ni kama vile unguja, fumba, Zanzibar, Kenya,
Tanganyika, Uganda, India.
Mtazamo
na Msimam
MAREJELEO
Robert, S. (1991). Wasifu wa Siti Binti
Saad. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers.
TUKI
(2014). Kamusi ya Kiswahili sanifu.
Nairobi: Oxford University Press.
Wamitila,
K.W. (2016). Kamusi Pevu ya Kiswahili.
Nairobi: Vide Muwa.
Indeed this is a well and good job done....Keep it up🔥🔥🔥
ReplyDeleteAsante kwa uhakiki huu ingawa mfupi lakini unaeleza yote niliyokuwa natamani kuelewa katika wasifu wa siti binti saad, umenipa mwanga wa kuchambua kazi hii.
ReplyDeletekazi nzuri umeifanya, kongole!
sarah k
Asante
Delete