Flower
Flower

Sunday, January 26, 2020

Uhakiki wa Utenzi wa Mwanakupona


Kwasababu utenzi wa Mwana Kupona unabainisha vile ambavyo fasihi huwa katika jamii ya Kimwinyi, inatubidi tuanze na maelezo ya jumla kuhusu fasihi ilivyo katika mfumo huo wa jamii ili  maelezo hayo yatusaidie katika kuupa utenzi huu uzito  wa kiuchambuzi.

FASIHI KATIKA MFUMO WA KIMWINYI
Mfumo wa Kimwinyi unabainishwa na mahusiano ya jamii ambayo ni ya kiutawala na ubaguzi ambayo yamefikia hatua mpya  ya juu zaidi ya tabaka tawala (la Umwinyi) ambalo hutawala nyanja zote za kiuchumi,kisiasa na kiutamaduni. Senkoro (1988: 12-26) akimnukuu Mulokozi katika makala yake  ya ''Ushairi wa Kiswahili ni nini''  anasema;
Uozo na ubaradhuli wa maisha ya Kimwinyi hasa wakati mfumo huu unapoanza kutetereka kutokana na nguvu za jamii na za uchumi, huwafanya mamwinyi, katika maisha yao ya kizembe na kifasiki wapendelee sana mambo ya kuvutia macho na kuliwaza pia kama vile mapambo aina aina, wanawake wazuri, nakshi na marembo ya rangi za kuvutia katika makazi yao, marashi, manukato, udi, ubani na kadhalika.

Maisha ya namna hii aliyoyaeleza Mulokozi vilevile hujitokeza katika fasihi itokanayo na mfumo huu, sio katika utenzi wa Mwana Kupona tu bali pia katika kazi nyingine kama vile utenzi wa Al-Inkshafi, unasadifu maudhui ya kipindi hiki cha Umwinyi.
Kabla ya kuchunguza ni kwa vipi mambo yote hayo na mengineyo ya Kimwinyi yamejitokeza katika utenzi wa Mwana Kupona, ni muhimu kupitia  historia ya utenzi huu kwa ufupi.

HISTORIA FUPI YA  MTUNZI WA UTENZI WA MWANA KUPONA
Mwana Kupona ni utenzi maarufu sana ambao  mwanzoni ulitungwa na mwanamke mmoja aliyejulikana kama Mwana Kupona. Baada ya kutungwa ulisambazwa kwa masimulizi, huku ukizidishwa au kupunguzwa kwa jumla ya beti kufuatana na kumbukumbu za moyoni za wapokezi na wasambazaji (Senkoro,1988:139)

Inasemekana Nana ni jina la utani la Mwana Kupona binti Mshamu Nabhany ambaye alizaliwa Pate mwaka 1810. Mwaka 1836 aliolewa na Bwana Muhammad Is-Haq bin Mbarak ( k. 1799 -1856 ) aliyejulikana zaidi kwa jina la Shee Mataka katika ndoa ya mitala iliyokuwa na wake wengine. Mwana Kupona alizaa na Shee Mataka watoto wawili: Mwana Hashima bint Shee Mataka ( 1841- 1930) aliyetungiwa utenzi huu, na Muhammad bin Shee Mataka (Muhammad mdogo) aliyezaliwa kati ya mwaka 1856 na 1858
Mwana Kupona aliondoka Siu na kuhamia Lamu ambako ndiko alikotungia utenzi huu mwaka 1858. Yasemekana kwamba  Bwana Shee Mataka alikuwa mtawala wa Siu na alipigana vita vya msituni kwa muda wa miaka 20 akipinga utawala wa  sultani wa Zanzibar , Seyyid Said.

Mwana Kupona aliutunga utenzi huu akiwa mgonjwa (inasemekana aliugua maradhi ya tumbo la uzazi) na akahisi asingepona hivyo akaamua kutunga utenzi huu ili uwe ni wosia kwa binti yake ambaye angebaki bila uongozi wa mama. Katika ubeti wa pili anasema;

Maradhi yamenishika
hata yametimu mwaka
sikupata kutamka
neno lema kukwambia 

Hata hivyo Mwana Kupona hakupona, alifariki miaka miwili baada ya kutunga utenzi wake, yaani mwaka 1860.

USULI WA UTENZI HUU

Kipindi cha utawala wa Omani (1730 – 1890) katika upwa wa Afrika Mashariki kiliambatana na migogoro ya kisiasa, iliyozua tungo za upinzani kama zile za Muyaka bin Haji ( k.1776- 1840 ), na pia ustawi wa tabaka la juu la watawala wenyeji na Waarabu lililoiga mambo mengi ya utamaduni wa Kiarabu na kusisitiza uzingativu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu katika masuala mengi ya kimaisha. Tabaka hilo lililokuwa na wasomi wengi wa elimu ya dini, ndilo lililozua tungo nyingi za tenzi za kidini zilizorejea katika historia ya kuasisiwa kwa Uislamu huko Arabuni (kama Mgeni bin Faqihi; Utendi wa Ras LGhuli  na pia tungo za falsafa, mawaidha na utamaduni kama Sayyid Abdalah Inkishafi )   

Utenzi wa Mwana Kupona unaingia katika fungu la tungo za mawaidha na utamaduni. Utenzi huu ulitungwa na Mwana Kupona  binti Mshamu kwa ajili ya binti yake aliyeitwa Mwana Hashima binti Mataka mwaka 1275 H ( 1858 M). Mtunzi aliwataka pia vijana wengine wa kike wausome pia na tunaona jamii ya wanawake wa Uswahilini ilivyoitikia vizuri wito huu na kuugeuza utungo huu kuwa asasi ya kale ya unyago ambayo ilikuwa inaanza kutoweka, na jambo hili limeudumisha utenzi huu katika mila na mapokezi ya Waswahili hadi leo.

MUHTASARI WA UTENZI WA MWANA KUPONA
Mwana Kupona ni utenzi wa mawaidha kwa msichana kuhusu unyumba na maisha kwa ujumla katika jamii ya Waswahili wa tabaka la juu. Una jumla ya beti 102 kama mtunzi mwenyewe anavyoeleza katika ubeti wa 100. Anasema;

Na baitize idadi
                   ni miati maadudi
                   na mbili za mazidadi
                   ndizo zimezozidia

Mtunzi anaanza kwa kumwita binti yake akaribie akiwa na wino na karatasi ili asikilize wosia. Anamwambia kuwa yeye ni mgonjwa na alikuwa hajapata nafasi ya kumpa mawaidha na kumtaka aanze kwa kumtukuza Mungu na kumwomba rehema zake. Anamwambia binti yake kuwa anataka kumpa hirizi iwe kinga yake, na kidani cha kujipambia akiwa na maana kwamba anampa utungo wa thamani kwake. Katika sehemu ya kwanza ya utungo huu, mwandishi anaanza kwa kutoa maaso na maelekezo kuhusu namna ya kuishi. Baadhi ya maelekezo hayo ni ;
  • kushika dini
  • kuwa na adabu
  • kuwa mwaminifu na mpenda haki
  • kujinyenyekeza mbele za wakubwa na kuwachangamkia
  • kuepuka umbea
  • kutochanganyika na watumwa ila tu wakati wa kazi
  • kuepuka wajinga wasiojichunga
  • kuheshimu Mungu na mtumewe
  • kuheshimu wazazi
  • kuheshimu mu me
Katika sehemu ya pili, utenzi unaeleza namna mwanamke anapaswa kumhudumia na kuishi na mumewe. Na baadhi ya mambo ambayo mke anapaswa kumfanyia mumewe ni;
  • kutojibizana naye
  • kumpa kila analotaka
  • kumuaga vizuri kila anapotoka na kumpokea kwa furaha anaporejea
  • kumpapasa na kumpepea usiku
  • kumkanda mwili
  • kumtukuza na kumsifia kwa watu
  • kumwandalia chakula
  • kumnyoa ndevu na kumfukiza udi
  • kumfanya mazingira yake yawe safi

Sehemu inayofuata ya utenzi huu (kuanzia ubt 37-56)  inahusu mwenendo binafsi wa mwanamke aliyeolewa  anatakiwa;
  • awe safi kimwili
  • avae na kujipamba vizuri kila siku
  • aombe ruhusa ya mumewe kabla ya kutoka na akitoka asikawie kurejea
  • anapotembea asijifunue buibui lake wala kunena na mtu njiani
  • aridhike na kile anachopewa na mumewe

 Kuanzia ubeti wa  57 mtunzi anamuasa binti yake namna ya kuishi na watu kwa jumla,  anatakiwa;
  • ashirikiane na wanandugu, marafiki na watu wengine.
  • awapende watu wote, matajiri na maskini.
  • awasaidie wale wenye kuhitaji msaada.

Sehemu ya mwisho ya utenzi huu ( kuanzia ubt 67 na kuendelea) ni dua ndefu ambayo mtunzi anawaombea walio wake, wakiwemo watoto wake, anajiombea yeye mwenyewe, na anawaombea waislamu kwa jumla, na mwishoni anawaomba wanawake wote wausome utenzi huu ili wanufaike. Anamalizia kwa kutaja jina lake na idadi ya beti alizotunga.

MJADALA KUHUSU UTENZI WA MWANA KUPONA KWA MUJIBU WA WATAALAMU  MBALIMBALI
Utenzi huu umehakikiwa na wataalamu mbalimbali kama vile Khatib (1985), Njozi (1990), Senkoro ( 1988) na Mulokozi (1993) na kuzua mjadala mkali miongoni mwa wanataaluma wa Kiswahili. Mjadala huu umejikita katika itikadi ya Mwana Kupona ya kijinsia ya kuutazama uhusiano wa mke na mume katika ndoa. Mjadala huu una matapo matatu;

Tapo la kwanza ni lile linaloongozwa na Senkoro 1988:140 ambapo anatoa mtazamo wake kuhusiana na utenzi huu. Ameweka hoja zake kwa msingi wa utawala wa Kimwinyi uliokuwepo katika ukanda wa pwani ya Afrika ya Mashariki. Senkoro anamnukuu Mulokozi(1982) kuwa wakati huo ulikuwa kipindi cha kuanza kutetereka kwa uchumi na mamwinyi walipenda anasa sana, nakshi mbalimbali, marembo ya rangi za kuvutia katika makazi yao, marashi, manukato, udi nakadhalika. Walipenda kuliwazwa. Hapa Senkoro anafikiri mwanamke wa kipindi hiki alidhalilishwa na utawala na hali halisi ya Umwinyi. Wanawake walifanywa kama mapambo na watumishi kwa wanaume. ( ubeti wa 38-41) Utenzi huu kwa mujibu wa Senkoro uliendeleza utawala wa kimwinyi na utawala dume. Msisitizo huu unajitokeza waziwazi ambapo Mwana Kupona anamtaka binti yake ajipambe na kuendana na mfumo wa kimwinyi, kwani anasisitiza juu ya mambo ya kuvutia macho. Katika wa 39 anasema;

                     nawe jipambe libasi
                     ukae kama arusi
                     maguu tia kugesi
                     na mikononi makoa

Katika kiwango hiki mwanamke anaonekana kama pambo tu.

Tapo la pili linasimamiwa na Njozi (1990). Yeye anafikiri kuwa mambo yote katika utenzi wa Mwana Kupona ni matokeo ya dini. Ameona kuwa utenzi huu unaeleza tu utamaduni wa ndoa na malezi ya Kiswahili, yaani ya Uislamu.

Kinyume na mtazamo wa awali uliochukulia kuwa mwanamke alidhalilishwa, mtazamo huu unachukulia kila kitu kama sehemu ya maisha, hususan dini (imani) na si kumdhalilisha mwanamke. Na kila jambo lililosemwa katika Mwana Kupona lilichukuliwa kuwa sahihi na wajibu kwa kila Mswahili mwenye mapenzi mema na jamii yake kufuata mafundisho hayo.

Tapo la tatu ni lile linalosimamiwa na Mbele (1985).  Yeye anasema wale wanaopinga utenzi wa Mwana Kupona hawajauelewa wosia wake vizuri kwa sababu kwa kuangalia na kutathmini vizuri utenzi huu, unawadhalilisha wanaume kwa sababu unaonesha  wanaume ni viumbe dhaifu na wapumbavu wenye kupenda kuengwa engwa. Mwanamke aliye na akili timamu anaweza kuwashinda na kuwamudu wanaume kwa kutumia udhaifu wao. Pia kuwatawala wanaume hao. Katika ubeti wa  36 anasema;

Mpumbaze apumbae
               amriye sikatae
               maovu kieta yeye
               mngu atakulipia

Msimamo wetu kama kikundi kuhusu matapo hayo tunamuunga mkono Mbele kwamba, wanaume ni viumbe dhaifu sana, ndio maana wanahitaji msaada wa kutunzwa na wake zao, hasa katika shughuli mbalimbali za kijamii ambazo wao wanajiona hawawezi kushiriki kwa sababu ya udhaifu wao na wala sio swala la kijinsia, hata katika vitabu vya dini wanaume wanaaswa kuishi na wanawake kwa akili, kwani wao hawana akili na uwezo wa kuamua mambo bila ya wake zao . Pia ni watu wenye kutegwa na mambo madogo madogo tu kama ya kupepewa, kupewa maneno matamu, kupapaswa na kuandaliwa chakula, yote haya yanawapumbaza na kuwafanya waendelee kuwa duni.

Hili lipo katika jamii yetu ya sasa ambapo wanaume wanaharibu ndoa, wanatafuta nyumba ndogo ili kufanyiwa mambo madogo madogo ambayo huenda wake zao kwa kuzidiwa na majukumu wanashindwa kuwafanyia kwa kiasi kinachoridhisha. Mambo hayo ni kama kupapaswa, kuambiwa maneno matamu, kufuliwa nguo, kupikiwa, na mengineyo mengi, hivyo wanaonesha jinsi gani walivyo dhaifu.

MAUDHUI KATIKA UTENZI HUU
Mjadala wa wataalamu hao unadhihirisha utata wa maudhui ya Mwana Kupona  hasa katika mazingira ya leo. Hata hivyo ikumbukwe kuwe maudhui hayo si mawazo ya Mwana Kupona binafsi bali ni mawazo yanayotokana na vyanzo vikuu vinne ambavyo ni mafundisho ya dini ya kiislamu, mila, desturi na imani za jadi za Waswahili na baadhi ya Waafrika wa maeneo ya pwani,  mila na desturi za Waarabu zinazofuatwa na baadhi ya wenyeji wa pwani waliosilimu, na imani, desturi, mtazamo na  uzoefu wa tabaka tawala la pwani.

Khatib (1985: 46) anasema tungo hii ya Mwana Kupona ni zao la fasihi ya kimwambao iliyoathiriwa na kupata utomvu wa uhai wake kutokana na utamaduni wa kimwambao ulioghoshiwa na maadili ya Kiislamu katika karne ya 19.  Hivyo basi maudhui katika utenzi huu yanajitokeza kama ifuatavyo;

·         Nafasi ya dini ya Kiislamu
Sehemu kubwa ya maudhui ya utenzi huu inasisitiza haja ya kuzingatia mafunzo ya dini ya  kiislamu, kumtii Mungu na mtume, kupenda na kutenda haki na kumtii mume (ubeti 12, 22, 23)
Katika ubeti wa 12 anasema;

La kwanda kamata dini
faradhi usiikhini
na sunna ikimkini
ni wajibu kuitia

  • Mapenzi, ndoa na malezi katika ndoa
Suala la ndoa limepewa umuhimu na mtunzi, na tunaona mtunzi akimpa mafunzo binti yake na namna anavyotakiwa kuishi na mumewe ili awe na  maisha mazuri ya ndoa. Kuhusu mapenzi, Mwana Kupona   anampa binti yake mbinu zitakazomsaidia katika kuimarisha penzi lake kwa mumewe, na mwanamke hapa anaonekana kuwa ndiye mwenye kazi kubwa katika kuimarisha penzi. Jambo hili linajitokeza pia katika vitabu vya dini. Kwa mfano  Biblia Takatifu inasema mwanamke mjinga huibomoa nyumba yake  kwa mikono yake mwenyewe (mithali 31:1) Katika utenzi huu wa Mwana Kupona, mawaidha haya tunaweza kuyapata katika ubeti wa 24-52

  • Nafasi ya mwanamke katika jamii
Mwanamke amechorwa kwa namna tofauti tofauti kutokana na mjadala uliozua mitazamo tofauti kuhusu utenzi huu. Tukiangalia tapo linaloona kuwa utenzi huu unamdhalilisha mwanamke, mwanamke anaonekana kuchorwa kama kiumbe duni na dhaifu na kwamba anatakiwa kumtegemea mumewe kwa kila kitu na kumtii. Katika ubeti wa 28 anasema;

Keti naye kwa adabu
usimtie ghadhabu
akinena simjibu
itahidi kunyamaa

Pia tunaweza kuona kuwa mwanamke amechorwa kama mlezi. Mwana Kupona katika kumlea binti yake anatunga utungo huu ili umsaidie, si yeye tu bali na mabinti wengine wa Kiafrika.  Katika ubeti wa 9 mshororo wa kwanza anamwambia binti yake ' nikutungie kidani' na pia katika ubeti wa 92 anasema;



     Na sababu ya kutunga,
     si shairi si malenga,
     nina kijana muinga,
     napenda kumuusia

  • Nafasi ya mwanaume katika jamii
Mwanaume amechorwa kama mwenye mamlaka na madaraka katika jamii. Anaonekana kummiliki mwanamke na ndiyo maana hata siku ya kiyama itakapofika, ndiye mwenye uamuzi juu ya mke wake kwamba aende motoni au peponi. Hili tunaliona katika ubeti wa 26 na 27. Mtunzi anasema;

       Siku ufufuliwa
       nadhari ni ya mumeo
       taulizwa atakao
       ndilo tkalotendewa

    Kipenda wende peponi
    utakwenda dalhini
    kinena wende motoni
    huna budi utatiwa

  • Matabaka
Katika mfumo wa Kimwinyi, kuna tabaka tawala na tawaliwa (wenye nacho na wasionacho). Mwana Kupona alikuwa katika tabaka tawala, na hili tunaliona katika ubeti wa 20 na 21 anapomwasa binti yake kutochangamana na watumwa na wajinga  walio katika tabaka la chini. Anasema;

      Sitangane na watumwa
      ila mwida wa khuduma
      watakuvutia tama
      la buda nimekwambia

     Sandamane na wainga
     wasoyua kuitunga
     viumbe wasio tanga
     wata kuwaquru

Suala hili ni la muhimu sana katika jamii zetu kwani katika kujishughulisha ndipo tunapoweza kujikomboa kutoka katika utumwa na utegemezi wa ndugu na jamaa zetu.

  • Kupenda kazi
Mtunzi anamuasa binti yake kuepuka tabia ya uvivu na uzembe, na anamtaka kuonyesha bidii na juhudi katika kazi, na  haswa pindi awapo na mumewe. Katika ubeti wa 37 anasema;

Mwanangu siwe mkoo
tenda kama uonao
kupea na kosha choo
sidharau mara moya

  • Kujiheshimu
Dhamira hii inajitokeza pale Mwana Kupona alipotoa maadili mbalimbali kwa binti yake, kwa mfano katika ubeti wa 13 anasema;

            pili uwe na adabu
            na ulimi wa thawabu
            uwe mtu mahabubu
            kula utakapongia .

Hapa anamtaka binti yake awe na heshima na kutumia ulimi wake vizuri pale anapokuwa na watu, na kwa njia hiyo atajijengea heshima kwa watu wote.

  • Mila, desturi na jadi ya Waswahili/ Waafrika
Waafrika wanazo mila na desturi zao za jadi kuhusu mahusiano ya watu katika ndoa na maisha kwa ujumla ambazo huwafundisha watoto wao. Mafunzo hayo kijadi yalikuwa yakitolewa katika unyago, ngano na masimulizi mengine, na katika matendo ya kimila ya kila siku. Adabu na heshima, kuepuka umbea na fitina, kujiheshimu, kupenda kazi, uzazi na  kuishi ndani ya nyumba bila makwazo ni  baadhi ya mambo yaliyofungamana na utamaduni wa Waswahili.

  • Athari ya mila na desturi za Waarabu  katika utamaduni wa Waswahili
Tunaziona athari hizi katika lafudhi ya baadhi ya watu wanapozungumza, katika mavazi, katika kutawisha wanawake na kuwafunika gubigubi wanapotoka nje, kuhesabu nasaba na kurithisha watoto kuumeni ( Waswahili kwa asili walihesabu nasaba kukeni kama yafanyavyo makabila mengi ya pwani- rejea Chiraghdin 1974 : 39). Katika ubeti wa 46 mwanamke anaambiwa;

Wala sinene ndiani
sifunue shiraani
mato angalia tini
na uso utie haya

Hizi ni mila za Kiarabu zilizoachwa mwambao wa pwani na hata sasa tunaona athari zake katika jamii yetu ya leo kwani tunawaona Waislamu wanavyovaa na kuishi kwa  kufuata tamaduni  za Waarabu.

  • Mahusiano mazuri katika jamii
Mtunzi anataka mwanae aishi vyema na watu wote kwa kushirikiana na wanadandugu, marafiki, na watu wengine. Pia anatakiwa awasaidie wale wenye uhitaji wa msaada kwake.

FANI
Katika sehemu hii, vitachambuliwa baadhi ya vipengele muhimu vya fani vinavyojitokeza katika utenzi huu. Kwa ujumla sanaa ya Mwana Kupona ni ya kawaida, lugha yake ni ya wastani, haina msamiati mgumu, sitiari wala taswira  zenye kutatiza.

  • Bahari
Utungo wa Mwanakupona unaingia katika bahari ya Utenzi ambapo kila ubeti unakuwa na vipande vinne na mizani 8 katika kila mshororo
Mtunzi anaumudu vizuri ushairi wa bahari ya utenzi na vina anavipatia vizuri. Kwa mfano katika  ubeti wa 29  tunaweza kuona mpangilio  wa vina na mizani ulivyo. Mtunzi anasema;

Enda naye kwa imani,
Atakalo simkhini,
we naye sikindaneni
ukindani huumia.

  • Mtindo
Mtindo uliotumika ni wa mwongozo – kwa lugha rasmi, nzuri na rahisi bila madoido wala utatanishi. Lengo la mtunzi lilikuwa kutoa mafunzo kwa mwanae na kwa vijana wengine, hivyo kutumia lugha ngumu ya kishairi iliyojaa picha, ishara, taswira na tamathali za semi kungeweza kufanya utenzi huu kutoeleweka kwa urahisi.

  • Nadharia ya Ujumi wa Kimapokeo katika utenzi huu
Kwa kuzingatia vipengele vinavyounda nadharia ya ujumi wa kimapokeo, tunaona kuwa vipengele vijenzi vya nadharia hii vinajitokeza katika utenzi huu. Vipengele hivyo ni pamoja na;

-maneno ya hekima
Mnyampala anasema shairi liwe na maneno ya hekima, na hili tunaliona katika utenzi huu. Anatumia maneno ya hekima ya hali ya juu katika kumuasa binti yake juu ya namna ya kuishi na watu pamoja na mume wake na hili ndilo linalofanya utenzi huu uzidi kupendwa.

-Lugha
Mwanakupona katumia lahaja ya Kiamu, na msamiati aliotumia ni mwepesi. Lugha ya picha imetumika kwa kiasi kidogo sana. Kwa mfano picha ya hirizi, koja na kidani/ kifungo (ubt 8-10) imewekwa vizuri ili kutupa picha ya utenzi kama kinga ya kumlinda aliyetungiwa dhidi ya matatizo. Tunaweza kuona mfano wa lugha ya Kiamu kama ifuatavyo;

                  nagema     wangu binti - (nagema inamaanisha nikaribie)
                   mchachefu  wa sanati   -(mchachefu inamaanisha machache)

-Hisia
Utenzi huu umegusia sana hisia za watu mbalimbali ambao kwa kuguswa kwao mioyo yao watu wamepata mitazamo mbalimbali juu ya utenzi huu  na kuuona utenzi huu kama wenye kumnyanyasa mwanamke, kumuona kama pambo, kama aliye duni na wengine pia wanaona kama ni utenzi ambao umechukua nafasi kubwa sana kwa wanawake wa pwani ambapo unaendelea kutumiwa kuwafunda sana wanawake au wasichana wa mwambao wa Pwani.

-Urari wa Vina na Mizani. 
Karibu washairi wote wa kijadi wanakubaliana kuhusu urari wa vina na mizani kuwa ni kipengele muhimu. Chiraghdin (keshatajwa) anasema ile raha ipatikanayo katika ushairi inatokana na kulingana kwa vina na mizani. Utenzi huu umefuata urari wa vina na mizani, kwa mfano katika ubeti wa 23 tunaona kuna vina vya mwisho vinavyoishia na  'e'. Vilevile vina vya mwisho vinabadilika kutoka ubeti hadi ubeti, isipokuwa vina katika mshororo wa mwisho wa beti zote havibadiliki. “a”
Kila kipande kina mizani 8, na hivyo kuufanya ubeti mmoja kuwa na jumla ya mizani 32.


-Utoshelevu
Katika kipengele hiki cha ujumi wa kimapokeo  tunaangalia suala la utoshelevu wa mawazo na maana katika utungo mzima. Kwa kiasi fulani  utenzi huu una utoshelevu katika ubeti kwani unaweza kupata maana pale tu unaposoma ubeti mmoja kwa mfano ubeti wa 31 mtunzi anasema;
  
kilala siikukuse
mwegeme umpapase
na upepo asikose
mtu wa kumpepea.
Katika ubeti huu tunapata wazo kamili linalijitosheleza. Mwana Hashima anaambiwa ahakikishe anampapasa na kumpepea mumewe pindi alalapo usiku. 

-Muwala
Ni ule mpandilio na mtiririko wa mawazo na kushonana kwa mawazo hayo tangu mwanzo hadi mwisho. Katika utenzi huu suala la muunganiko wa mawazo halijawekwa wazi sana kwani mawazo mengine yamerudiwa rudiwa sana. Kadhalika hakuna mpangilio mzuri wa beti kutokana na kwamba kuna baadhi ya beti zilizopaswa kuwa mwishoni au mwanzoni lakini hazikupangiliwa hivyo. Kwa mfano ubeti wa 22 na 23 zingeweza kuwa kati ya ubeti wa 11 na 13, kadhalika ubeti wa  42 na  43 zingeweza kuwa kati ya ubeti wa 36 na 37.  Pia ubeti wa 92 na 93 zimebeba mawazo ambayo yangefaa kuwapo mwanzoni.

-Muundo
Utenzi huu umeandikwa katika muundo wa kishairi kwa kutumia bahari ya utenzi. Ni utenzi uliopangiliwa katika beti tangu mwanzo hadi mwisho (ubeti wa 1- 102).  Pia kuna urari wa vina na mizani na matumizi ya lugha ya mkato ya kishairi.

MCHANGO WA UTENZI WA MWANA KUPONA
Kutokana na nafasi ya Utenzi huu katika jamii ya Waswahili, mchango wake unajidhihirisha kama ifuatavyo;

Kwanza kabisa utenzi huu umechukua nafasi kubwa na umepewa umuhimu mkubwa  katika jamii ya Waswahili hasa katika malezi ya vijana wa kike. Utenzi huu umetumika kutoa elimu iliyokuwa ikitolewa katika unyago na miviga ambapo mawaidha waliyopewa yanaendana kabisa na yale ya Mwana Kupona kwa binti yake.

Pia jamii yetu ya leo imemomonyoka sana kwa suala zina la kujisitiri, kijiheshimu, kuwa na ushirikiano na kufanyanya kazi kwa bidii. Utenzi huu ni hazina bora kwani kila unaposomwa unakuwa ni kumbukumbu ya kutukumbusha wanajamii, japokuwa wengine hawafuati mawaidha haya kwani sikio  la kufa halisikii dawa. Sio hivyo tu bali pia suala la malezi na masikilizano katika ndoa. Ndoa ni taasisi muhihu sana katika jamii na pale inapotokea mafarakano katika ndoa inakuwa ni chanzo cha uharibifu wa jamii yote kwa ujumla.

Utenzi huu umekuwa na athari pia katika fasihi. Watunzi kadha wa  “wosia “ kama vile Semghanga “ Kidani cha Huba” na “ Ewe Mwana “ katika diwani yake ya “Teuzi za Nafsi” (1971), Said Karama “ Wasia wa Baba”, Zainab binti Hamud “ Howani  Mwana  Howani “(1983) na Shaaban Robert katika “Utenzi wa Hati” na “Utenzi wa Adili” wamemuiga Mwana Kupona katika mawazo na hata mtindo.
Kwa mfano katika tungo hizo za Shaaban Robert, Shaaban Robert anampa mawaidha binti yake ambayo yanafanana na yale ya Mwana Kupona.  Shaaban Robert anamwambia binti yake ashike dini, awapende na kuwaheshimu watu wote, matajiri na maskini, aishi vyema na watu, awe na kauli nzuri, ajue kazi za nyumbani kama kupika, ajiheshimu na asishindane na mumewe. Yote haya tunayapata pia katika Mwana Kupona.  Shaaban Robert alitunga tenzi zake miaka mia moja baada ya Mwana Kupona. Anachokiongeza Shaaban Robert ni mawazo machache mapya kulingana na wakati wake, mathalan yale yanayohusu elimu na kujitegemea.

Vile vile tukiangalia mtindo wa utenzi huu tunaona athari zake katika kazi za watunzi waliofuata. Kwa  mfano watunzi wengi wanatunga kwa kuanza na dua kama alivyoanza Mwana Kupona, pia wanawaita watu kuja kusikiliza kama alivyofanya Mwana Kupona kwa binti yake, sawa ma alivyofanya Shaban Robert kwa mfano katika utenzi wa  Hati aliomtungia binti yake. Anasema :

leo nataka binti,
ukae juu ya kiti,
ili uandike hati,
ndogo ya wasia.

Mchango mwingine tunaoupata kutokana na utenzi huu ni athari ya mtunzi kwa watunzi wengine wanawake. Akiwa kama mwanamke wa kwanza kutunga kazi za kishairi alichochea hari ya utunzi kwa wanawake wengine na kuwaonesha kwamba wanaweza nao kuingia katika kazi ya utunzi wa mashairi kwa mfano Zainabu bint Humud katika utungo wake wa “Howani Mwana Howani”.

Kuhitimisha kuwa tunaweza kusema kuwa utenzi Mwana Kuopona ni kati ya kazi maarufu zilizoacha athari kubwa na ambazo bado zinaendelea kutumiwa katika jamii, hususani na jamii wa Waswahili wa Pwani. Kazi hii kama tulivyoona imeathiri kazi mbaimbali za kifasihi pamoja na kuamsha ari miongoni mwa watunzi wanawake, ambapo katika kutunnga kwao wameweza kuhifadhi na kuendeleza mila na desturi za Kiafrika. Hivyo basi utenzi huu ni hazina kubwa ambayo kwa hakika inapaswa kupewa nafasi na umuhimu  wake kutokana na mchango wake katika fasihi na jamii kwa ujumla.


 MAREJEO
Khatib, M. S. (1985), “Uhakiki wa Mwana Kupona” katika Mulika na. 17

Mulikozi M. M (1999) Tenzi tatu za kale (TUKI) Dar es salaam.

Senkoro F.E.M.K (1988) Ushairi; Nadharia na Tahakiki. Inter press of Tanzania Limited,

                        Tanzania                                  

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny