Dhana
ya falsafa imefasiliwa na wataalamu mbali mbali kama vile Njoroge na Bennaars
, wanafasili falsafa kuwa ni jaribio
lolote la watu kufikia jibu au itiko la masuala muhimu ya maisha. Falsafa ni
sayansi inayopuuza visakale na mazingaombwe na kuzingatia ukweli na urazini wa
kimawazo. Si kweli kwamba falsafa ni sayansi inayopuuza visakale na
mazingaombwe, kwasababu falsafa ya Kiafrika hujidhihilisha pia katika fasihi
simulizi.
Pia
Odera
, anafasili falsafa kuwa ni taaluma
ambayo kanuni za msingi kuhusu asili, binadamu na jamii kuchunguzwa na
kujadiliwa. Mtaalamu huyu aliitazama falsafa kwa mtazamo wa kitaaluma pekee
bila kuangalia na kwa mtazamo wa falsafa kama mtazamo.
Kwa
ujumla, falsafa ni jumla ya mawazo yanayohusiana na asili, maana na sababu za
kutokea kwa vitu au mambo katika jamii husika.
Georg
Wilhem Friedrick Hegel ni mwanafalsafa wa Kijerumani aliyezaliwa tarehe
27/8/1770 huko Duchy Muittermberg na kufaliki mwaka 1831. Mwanafalsafa huyu
alipinga kuwapo kwa falsafa ya kiafrika kwa kusema hawezi kuijadili Afrika na
kuiweka katika historia ya ulimwengu. Afrka anayoizungumzia hapa ni ile ya
kusini mwa Jangwa la Sahara, na ndiyo anayodai kuwa ndo Afrika halisi,
anaendelea kusema Afrika imefahamika kwasababu ya biashara ya utumwa na
ukoloni. Hegel anasema Mwafrika hana akili, maendeleo, utamaduni, wala hana
historia, Mwafrika anaitambua nafsi yake tu, Mwafrika hana dini, ni mtu dhalimu
na mtu katili, ni mtu ambaye hajastaarabika.
Falsafa
ya Kiafrika ni jumla ya mawazo yanayohusiana na asili, maana na sababu za
kutokea kwa vitu au mambo katika jamii ya waafrika, Samwel (2012). Anaendelea
kwa kusema kuwa mawazo haya hutupatia maarifa yenye hekima katika kuishi kwenye
dunia. Samweli (keshatajwa) anazidi kufafanua kwamba fasihi simulizi ya
Kiafrika inabeba falsafa ya kiafrika, fasihi simulizi ya Kiswahili inabeba falsafa
ya Waswahili.
Kagame
(1956) na Ngugi (1996) wakinukuliwa na Samweli (keshatajwa), wanasema kuwa
Waafrika wana falsafa yao inayoongoza
maisha yao ya kila siku sawa na falsafa za jamii nyingine duniani kote.
Wanaendelea kusema falsafa hii inadhihikika katika tanzu mbali mbali za fasihi
simulizi kama vile, visa kale, nahau, miviga, matambiko, vitendawili na
methali.
Methali
imefasiliwa na wataalamu mbali mbali kama vile Samweli (2012), anasema methali
ni semo fupi fupi za kimapokeo ambazo hubeba mafunzo mazito na busara za wazee.
Anaendelea kusema methali hubeba falsafa
na mtazamo wa jamii juu ya masuala mbali mbali na ndiyo nyenzo inayotumika
zaidi katika kutolea mafunzo. Kutokana na ufupi wake na busara iliyomo ndani
yake huaminika kuwa methali ni njia bora zaidi ya kuwasilisha mafunzo na
kuikanya jamii. Mano `Asiyesikia la mkuu huvunjika guu´ Inawafunza watoto na
vijana kuwasikiliza wazazi wao na wakubwa wao na kama wakikaidi wataharibikiwa
katika maisha yao.
Pia
Mulokozi (2017), kwa kusema methali ni usemi mfupi wa kimapokeo unaodokeza kwa
muhutasari fikra au mafunzo mazito yanayotokana na tajiriba (uzoefu wa maisha)
ya jamii inayohusika. Anaendelea kwa kusema kuwa istilahi methali inatokana
neon la kiarabu lenye maana ya `mfano´. Hivyo methali kauli inayoadilisha kwa
mifano au ufananisho.
Katika
mtazamo wa Kiafrika wanapingana na madai ya Hegel kuhusu kutokuwapo kwa falsafa
ya Kiafrika, mtazamo huu unaeleza kwamba falsafa ya kiafrika inajidhihilisha
sana katika fasihi simulizi. Kwa kutumia methali tunathibitisha kauli hii kama
ifuatavyo.
Kidole
kimoja, hakivunji chawa. Kwa mujibu wa Samweli (2012), anafafanua kuwa methali
hii inasisitiza mahusiano, kusaidiana na ushirikiano wa jamii kama msingi wa
maisha bora na amani katika jamii. Methali hii inadhihilisha kuwepo kwa falsafa
ya Kiafrika ya utu au Ubuntu, ambapo ni ile hali ya kumjali na
kumsaidiabinadamu mwingine kama nafsi yake, anaendelea kusema mtu mwenye utu
hawezi kumfanyia mwingine jambo ambalo yeye asingependa kufanyiwa, Samweli (keshatajwa).
Pia methali kama ´utu ni watu´ na ´umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu´,
zinashadadia kuwapo kwa swala la kushirikiana na kusaidiana miongoni mwa
wanajamii ambao ndo utu wenyewe. Hivyo basi, methali hizi zinapingana na
mtazamo wa Hegel ambao anaona Mwafrika ni mtu anayeitambua nafsi yake tu.
Mungu
kasema, niombe nikupe. Kwa mujibu wa Kitula na King´ei (2008), wanafafanua
methali hii kuwa mtu anapopata shida hapana mwingine wa kumuomba faraji
isipokuwa Manani, wanaedelea kusema ukimwomba Mungu bila shaka atakufanikisha.
Hivyo, methali tajwa inathibitisha uwepo wa falsafa ya kiafrika ambayo ni imani
ya uwepo wa Mungu na nguvu zake. Samweli (keshatajwa) anaeleza kuwa falsafa hii
inabainisha kuwa Waafrika wanaamini katika dini kwamba Mungu ndiye mwenye uwezo
wa yote na huchukia maovu, hivyo yeyote anayefanya maovu huadhibiwa na Mungu.
Mfano, katika jamii ya Wahaya kuna Miungu iliyoheshimika na kuabudiwa kama
Kagoro, Lyangombe, Mugasha na Nyakarembe. Kwahiyo, methali hii inaunga mkono
mtazamo wa Kiafrika na kupinga mtazamo wa Hegel kwamba Waafrika hawana dini.
Asiyefunzwa
na mamaye, hufunzwa na ulimwengu. Kitula na King´ei (washatajwa), wanafafanua
methali hii kwamba, malezi na mafunzo bora ni yale ya mama au wazazi, bila
hivyo atapata shida kuishi katika ulimwengu. Wanaendelea kusema mama humlea na kumfunza
mwanae ili akabiliane na changamoto za ulimwengu. Katika methali hii inaibuka
falsafa ya uzazi na malezi, ambapo mama ndiye anayeonekana kubeba au kubebeshwa
majukumu hayo katika jamii nyingi za Kiafrika, hatakama ikitokea ndoa fulani
haina mototo, mwanamke ndiye aliyelaumiwa. Pia methali kama ´Kinyesi cha mtoto
hakinuki kwa mama´ na ´Mama kwa mwanae, mtoto kwa mamae´, zinashadadia uwepo wa
falsafa ya uzazi na malezi. Kwa maelezo hayo inaonyesha kuwa Waafrika
walikuwanazo na wanazo mila, desturi na tamaduni zao, hivyo si sahihi kauli ya
Hegel kwamba Mwafrika hana utamaduni.
Kufa
si kuisha. Methali hii inamaana kuwa na imani ya maisha baada ya kifo,
wanaendelea kusema mtu anapokufa maisha yake hayaishii hapo. Methali hii
inadhihilisha uwepo wa falsafa ya kifo sio mwisho wa kuwapo. Tempels (1959)
anasema binadamu anasifa ya umilele, kifo kinapotokea hubadili mfumo wa maisha
ya mtu kutoka binadamu aliyehai mwenye mwili
na kuingia maisha mengine yanayoambatana na roho. Roho hizo huitwa
mizimu na zikikaa kwa muda mrefu huitwa wahenga na zinabaki kuwa sehemu ya
jamii. Binadamu huendeleza mawasiliano na Wahenga kupitia matambiko,ndoto au
kutokewa katika hali ya kawida. Methali nyingine inayodhihilisha uwepo wa
falsafa ya kifo si mwisho wa kuwapo ni `Kilichokufa, kiliishi´. Hivyo si kweli
kwamba Afrika haina historia, wala haina falsafa.
Achanikaye
kwenye mpini hafi njaa. Maana ya methali hii ni mtu anayejibidisha katika kazi
hawezi kupata tabu au kukosa chochote. Methali hii inathibitisha uwepo wa falsafa
ya kazi na umuhimu wake, Koponen (1988) akinukuliwa na Samweli (keshatajwa)
anaeleza kuwa kazi ni jambo linalothaminiwa sana katika jamii za Kiafrika.
Jamii ya jadi ya Kiafrika ilikuwa na mgawanyo wa majukumu na kila mwanajamii
alitakiwa kutimiza majukumu yake katiak kuendeleza jamii yao. Methali nyingine
zinazothibitisha madai haya ya mtazamo wa Kiafrika ni ´Asiyefanya kazi na
asile´ na ´Mchumia juani hulia kivulini´. Hivyo basi, Wafrika waliona umuhimu
wa kufanya kazi ili kufikia maendeleo.
Mke
ni nguo, mume ni kazi. Ina maana kuwa Mume ndiye mwenye majukumu ya kugharamia
mambo yote katika familia ni ya mume au baba, mke ni wa shughuli za nyumbani. Falsafa
ya uhusiano kati ya mwanamke na mwanaume inadhihilika katika methali hii,
ambapo katika jamii za Kiafrika mwanamke ni kiumbe dhaifu na mwanaume ni
jasiri, kwamba mwanamke anatakiwa kumueshimu na kumnyenyekea mume wake na hata
kama akikosa hatakiwi kumuuliza mume wake. Methali nyingine zinazodhihilisha
uwepo wa falsafa hii ni, ´Mtu nyumbani mwake hatiiwi na mkewe, haonwi kuwa
mume, asipompiga twa´. Hivyo methali hii inapinga madai ya Hegeli kwamba
Mwafrika hana falsafa, wala hana historia na wala hatakiwi kuweka katika
historia ya jamii.
Akufanyiaye
ubaya, mlipe wema. Inamaana kwamba usilipize kisasi kwa mtu aliye kutenda
vibaya kwani unaweza kuzua ugomvi mkubwa au vita. Methali hii inaibua falsafa
ya wema dhidi ya ubaya, ambapo jamii za kiafrika huamini kwamba mara nyingi
wema huushinda ubaya, hivyo walihimiza kutenda wema katika jamii zao ili kukuza
amani na upendo miongoni mwao. Falsafa ya wema dhidi ya ubaya inadhihilika pia
katika methali ya ´Wema hauozi´. Hivyo basi, Waafrika wana imani, miongozo
wanayoiishi, hivvo inapinga ntazamo hasi wa Hegeli kwamba Waafrika hawana
falsafa wala historian a ni mtu katili na dhalimu.
Kwaa
ujumla, mtazamo wa Kiafrika una unaupinga ule mtazamo wa Kimagharibi, unaoona
kwamba Waafrika hawana Falsafa. Wataalamu wa mtazamo huu wanaendelea kusema
falsafa hujidhihilisha kupitia fasihi simulizi kama vile methali, lakini pia
katika tanzu nyingine au vipera vingine hudhihilika. Mfano, matambiko
yanadhihilisha uwepo wa falsafa ya uwepo
wa Mugu au Miungu na nguvu zake. Utendi wa Mwanakupona unaodhihilisha falsafa
ya uhusiano na nafasi anayopewa mwanamke na mwanaume katika jamii za Kiafrika.
Pia visa kale, mfano kisa kale cha Ng’wanamarundi kinachoibua falsafa ya uganga
na uchawi.
MAREJELEO
Hegel, G. W. F.Introdduction to the Philosophy of History.
Cambridge: Hacket Publishing.
Kitula na King’ei
(2008). Kamusi ya Methali. Nirobi:
E.A.E.P.
Mulokozi, M. M (2017). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar
es salaam: TUKI
Njoroge, R. J. na
Bennaars, G. A. (1986). Pilosophy of
Education in Africa. Nairobi: Transafrica
Press
Odera, O. (1990). Trends in Conteporary African Philosophy.
Nairobi: Shirikon Publishers.
Samwel, M. (2012). Umahili katika Fasihi ya Kiswahili. Dar
es salaam: Mervel Publishers
Tempels, P. F. (1959). Bantu Philosophy. Paris: Presence
Africaine Publishers.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com