Samsoni (2017) akiwanukuu
Luvenduski & Randall (1993) anaeleza
kuwa, ufeministi ni neno la Kilatini ‘femina’
yaani wa ‘kike’ au mwanamke.
Wanaendelea kwa kusema kuwa, katika lugha ya Kifaransa ‘feminisme’ linamaanisha harakati za ukombozi wa wanawake. Ni jina
linalojumuisha aina nyingi za misimamo, itikadi na matapo tofautitofauti
yanayochangia lengo kuu la kutetea haki za wanawake dhidi ya ubaguzi wa
kijinsia uliotawala dunia kwa muda mrefu sana katika upande kisiasa, kiuchumi,
kiutamaduni, kidini na kijamii kwa ujumla.
Miongoni mwa wadau waliochangia
kuendelea kwa kasi ya ufeministi ni Andew Dworkin mwaka 1976 huko London
Uingereza, alitoa mapendekezo makali katika kukomesha utawala wa mwanaume dhidi
mwanamke, kwa madai kuwa, “ili kufanikisha, tunahitaji kubomoa kabisa muundo wa
mihimili ya utamaduni wa jamii kama vile sanaa, kanisa, sharia, kaya
zinazodhibitiwa na baba, jamii na taswira zote za asasi, mila na desturi
zilizomwona mwanamke kama mtu hovyo.”. Ithibati za kimaandishi za kifeministi
zenye utaratibu na zilizoweka misingi ya nadharia ya ufeministi ni andiko la
Mary la Mary Wollstonecraft linaloitwa ‘A vindication of the Right of
Women’ la mwaka (1792), andiko la Woolf liitwalo ‘A Room of
One’s Own’ la mwaka (1929). Mary Wollstonecraft ndiye mwandishi aliyeasisi
mazungumzo kuhusu masuala ya wanawake na kulalama kuhusu hali waliyokuwa
wanapitia wanawake katika jamii. Katika miaka ya 1960, ufeministi ulishika
kasi. Kwa mfano mwandishi wa kifaransa, Simone de Beauvoir katika andiko lake
la ‘The Second Sex’ la mwaka 1952, anaonesha harakati za kushambulia na kukosoa
baadhi ya asasi zinazochangia kumdhalilisha na kumdunisha mwanamke kama vile
dini, ndoa na utamaduni.
Semone de Beauvior, anaeleza
kuwa, asasi ya ndoa inamgandamiza mwanamke kwa kumuona kama chombo cha kukidhi
haja ya mwanaume na kutoa suhuhisho la kuipa kisogo asasi hii. Pia, anaeleza
katika utamaduni kuwa, ni asasi inayomgandamiza mwanamke na ndiyo inayomkuza
mwanamke. Kwa kuwa utamaduni ndiyo unaomkuza mwanamke, ndiyo ulioweka misingi
ya kumfanya mwanamke kuwa ni kiumbe duni, na kumfanya akiukubali mfumo huu
hasi.
Mwanaitifaki wengine ni Milet katika kitabu chake cha ‘Sexual
Politics’ anawakosoa vikali baadhi ya waandishi wa kiume wanaoandika kazi zao
zinazowasawili wanawake katika hali hasi. Alienda mbali zaidi mpaka kwa
kuwashambulia wanaitifaki wa nadharia ya Saikolojia Changanuzi, ambao muasisi
wake ni Freud Sigmund, wanaodai kuwa mwanamke huanza kujichukia pale anapoona
kuwa yeye si wa jinsi ya kiume ambapo wao waliona kuwa ni wivu wa zuba.
Wamitila (2003:253) anaeleza kuwa, ufeministi ni msingi na
msukumo mkubwa pamoja na nia ya kupigania ukombozi wa mwanamke kutokana na
pingu za kiutamaduni, kidini, kijamii, kisiasa na kiuchumi. Fasili hii
inadadisi itikadi ya kiume ambayo imekuwepo katika jamii kwa kipindi kirefu
pamoja na mikabala ya kiubabe dume.
Njogu na Chimerah (2008:18) anaeleza kuwa, ufeministi au
mtazamo kike ni nadharia inayokinzana na mikabala ya kiumeni inayoonekana
kupendelea wanaume na kuwanyanyasa wanawakae. Mtazamo huu unaonesha namna
wanaume wanavyowakandamiza wanawake na kuwasahau kuwa wote wanahitaji kupata
haki sawa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.
Cambridge Dictionary (1995) wanaeleza kuwa ufeministi ni
mtazamo wa kiimani ambao wanawake wanatakiwa wawe na haki sawa, nguvu na nafasi
kama ilivyo kwa wanaume na kutazamwa kwa usawa. Katika fasili hii hailezi kuwa,
njia gani zitumike kuwapa wanawake haki sawa kama walizonazo wanaume.
Mulokozi (2017:368) anaeleza kuwa, ufeministi ni vugu vugu
na itikadi ya mapambano ya mwanamke ya kujikomboa kutoka katika mikakati ya
kunyonywa, kukandamilzwa na kubaguliwa ndani ya jamii, pamoja na itikadi za
ubaguzi zinazoambatana na hali hiyo.
Kwa ujumla, ufeministi ni michakato ya itikadi ambayo
inalenga kutafuta na kufikia usawa kati ya wanawake na wanaume katika nyanja
zote za kimaisha kama vile kisiasa, kielimu, kijamii kiutamaduni na kiuchumi.
Hivyo ufeministi ni itikadi ambayo inapigania usawa kwa jinsi zote.
Wamitila (2003) anaeleza kuwa, historia ya ufeministi inadai
kwamba, mapambano ya wanawake dhidi ya wanaume (ufeministi) yalianza karne ya
19. Mapambano haya yalichukuliwa kama harakati za kudai haki za wanawake
yaliyoanzia Ulaya. Miongoni mwa haki hizo, ni pamoja na haki ya kupiga kura
kwenye chaguzi za siasa, haki ya kumiliki na kupata elimu. Wakati, Mulokozi
(2017:368)) anaeleza kuwa, ufeministi ulianza Ulaya na Marekani mnamo karne ya
18, wafeministi na watetezi wengine wa wanawake walibainisha baadhi ya mambo na
asasi zinazomkandamiza mwanamke, zikiwemo mila na desturi, ndoa, dini na mifumo
ya kiuchumi na kisiasa. Kwani haki za binadamu zilipoanza kufanya kazi hapo
awali zilijadiliwa kwa wanaume pekee.
Hivyo, baada ya harakati za kumkomboa mwanamke kutoka katika
ugandamizwaji na unyonyaji dhidi ya mwanaume, ndipo yalipozuka makundi ya
ufeministi kama ifuatavyo;
Wafeministi wanamapokeo (ki marx), kundi hili linaangalia
kwamba, uhusiano wa kisiasa kati ya mwanamke na mwanaume si sawa ingawa,
wanawake hawapaswi kuvuruga mfumo uliopo (wa kiugandamizaji). Miongoni mwa
waasisi wa kundi hili ni pamoja na Selma Jems, Angela Davis, Crala Fraser, Raya
Dunayevisk Shulamith Firestone na Heidi Hartmann.
Wanamapokeo ni tapo linalodai kuwa ugandamizaji wa mwanamke
umetokana na mfumo wa unyonyaji wa kibepari, mfumo ambao umeigawa jamii katika
makundi makuu mawili, tabaka la wasionacho na walionacho. Kwa mujibu wa
wanaitifaki hawa, asilimia kubwa ya tabaka la wasionacho ni wanawake ambao wapo
chini ya wanaume kutokana na mfumo dume unaowapa hadhi wanaume. Mfumo huu wa
kibepari unawapa fursa watu wachache kumiliki mali ambao waliowengi ni
wanawake.
Kundi hili linadai kuwa, ili mwanamke aweze kukombolewa na
awe na uhuru wa kutokugandamizwa, ni lazima ubepari utokomezwe, ili kutoa fursa
kwa jinsi zote mbili katika jamii. Kwa mujibu wa Malenya (2012) Karl Marx na
Engels walikuwa wakiamini kuwa, familia ndiyo taasisi ya kwanza ya kijamii
ambako hakuna usawa kati ya mwanamke na mwanaume na kwamba mfumo huo unapaswa
kuangamizwa na badala yake zianzishwe taasisi za ushirika au ujima ili kazi za
nyumbani zifanywe na jinsi zote mbili kwa usawa.
Hivyo
wafeministi wanamapokeo wanapigania haki sawa ambazo zimekosekana kutokana na
mfumo kibepari wa unyonyaji na ukandamizaji unaofanywa na tabaka tawala ambalo
wahusika wengi ni wanaume dhidi ya tabaka tawaliwa ambao walio wengi ni
wanawake, ili kuleta usawa kati ya wanaume na wanawake katika nyanja zote za kijamii
kuanzia ngazi ya familia, kijamii hadi kitafa kwa maendeleleo endelevu yasiyo
na ubaguzi.
Wafeministi huru (Liberal feminism), ni kundi lililoanzia
mwishoni mwa karne 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 katika harakati za kupigania
uhuru wa mwanamke katika kufanya maamuzi bila kuingiliwa na mwanaume. Waasisi
wa kundi hili ni pamoja na Marry Wollstonecraft, Judith Surgent
Murray, Frances
Wright. Wanafalsafa wa kundi hili wanatetea usawa kati ya mwanamke na mwanaume
katika nyanja za kisiasa, kielimu, kiuchumi na kiutamaduni ambao ulishika kasi
miaka ya 1960 katika harakati za makundi ya kudai haki dhidi ya ubaguzi wa
rangi na ubaguzi wa kijinsia.
Waitifaki hawa, wanadai kuwa, binadamu wote ni sawa wake kwa
waume, hivyo, wanawake nao wana haki ya kuwa huru katika kuyatekeleza majukumu
na malengo yao, yaani kupewa fursa ya kuamua ni wakati gani wa kuwa na watoto
bila shinikizo la wanaume zao, pia wanatilia mkazo katika suala la malezi kuwa
ni la wote mwanamume na mwanamke. Wanaitifaki hawa wanaangalia kuwa, mgawanyo
wa kazi kutokana na hali ya kijinsi kati ya mwanamke na mwamume si sawa, hivyo
unapaswa kubadilishwa na kwamba, kama mwanamke anafanya kazi za ndani azifanye,
lakini kama atamua kufanya shughuli nyingine za kijamii nazo afanye, na ana
uhuru wa kutoa mimba na kuzaa.
Misingi ya wafeministi huru ni kwamba, mfumo
uliopo unapasawa kubadilishwa.
Pia kundi hili linatoa mwongozo kwa jamii kuwa, mwanamke
anapaswa kuwa huru katika nyanja zote za uzalishaji mali ili kuwe na usawa kati
ya mwaume na mwanamke, kuliko kumwacha mwanaume atawale katika nyanja zote na
kunyima mwanamke fursa ya uzalishaji mali katika jamii. Mfumo gandamizi wa
kibepari ndiyo unaowapa nafasi wanaume kuwakandamiza wanawake, hivyo unapaswa
kuondolewa ili kuleta usawa kawa jinsi zote mbili katika uhuru wa kufanya
mambo.
Wanamapinduzi (Radical feminism) hili ni kundi la
kimapinduzi, linalopinga mfumo dume na kudai kwamba, unapaswa kutupiliwa mbali.
Kundi hili linahusisha makundi mbalimbali ya kudai haki ambayo yalishika kasi
zaidi miaka ya 1960. Miongoni mwa waasisi wa kundi hili ni Ellen Wills,
Ti-
Grace Atkson, Carol Hanisch, Judith Brown na Shulamith Firestone. Waitifaki
hawa wanadai kuwa huu ni mfumo wa kibepari unaoendeleza unyonyaji na
ugandamizaji wa mwanamke katika nyanja za kisiasa, kiuchumi. kiutamaduni na
kielimu.
Kundi hili linadai haki sawa katika masuala ya uongozi kwa
jinsi zote mbili, kiume na kike. Kwa kuwa jamii nyingi zimemnyima mwanamke
kushiriki kufanya maamuzi kuanzia ngazi ya familia, kijamii na kitaifa, hapo
ndipo kundi hili lilisimama kidete katika kudai usawa katika suala la maamuzi.
Jitihada hizi za kuitaka jamii impe fursa mwanamke katika kufanya maamuzi,
zilizaa matunda katika mkutano wa Beijing wa mwaka 1995 wakati huo Balozi
Getrude Mongela, ukihudhuriwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Katika mkutano huu, maazimio kadha wa kadha yalipitishwa
ikiwa ni pamoja na wanawake kutengewa viti maalumu bungeni, msukumo ambao
uliwafanya wanawake kuwa na fursa katika kufanya maamuzi, hatua ambayo ilizaa
matunda kwa wanawake kupata nyazifa katika mashirika ya kiserikali na yasiyo ya
kiserikali hivyo kuleta usawa kwa kuwa na uhuru wa maamuzi kwa wanawake na
wanaume katika jamii.
Wafeministi wa kijamaa (socialist feminism), hili ni kundi
lililoshika kasi miaka ya 1960 na 1970, ambalo linaeleza kuwa, uhusiano baina
ya wanawake na wamaume unaotokana na muundo wa kijamii na kiuchumi na mageuzi
makubwa katika jamii, na kwamba kuwepo kwa haki sawa kati ya wanawake na
wanaume kupo katika usawa wa kijamii na kufutwa kwa dhulma ya kijinsia na
kitabaka katika jamii. Miongoni mwa waasisi wa kundi hili ni pamoja na Heather
Booth, Day Creamer, Susan Davis, na Tobey Klass. Wafeministi wasoshalisti
wanakubaliana na uchambuzi wa wenzao wa kimaksi kuhusu uhusiano wa kitabaka wa
ubepari ambao umekuwa gandamizi kwenye jamii kwa kuifanya jinsi ya kike kuwa
ndiyo inayoathirika kwa kiasi kikubwa.
Gabriel (2010) anaeleza kuwa, wafeministi wa kijamaa wanadai
kuwa, ili kuwe na usawa kati ya mwanamke na mwanamume, ni lazima kuwe na
mapambano dhidi ya mfumo dume na ubepari, na mapambano hayo yanapaswa kuanzia
sehemu za viwandani hadi kazi zote za umma na binafsi, kiutamaduni ambako ndiko
wanawake wanabaguliwa ili kuleta usawa
wa kijinsia kwa wanaume na wanawake. Wanadai kuwa kuleta usawa wa kijamii kati
ya wanawake na wanaume, mfumo dume unapaswa kuondolewa ili kuwe na mgawanyo
sawa kimajukumu na njia za uzalishaji mali na kushika nafasi mbali mbali ambazo
wanawake na wanaume watanufaika kwa pamoja.
Ufeministi wa kiutamaduni, hili ni kundi ambalo linautizama
utamaduni kama nyenzo kubwa katika kumfanya mwanamke aamini hali aliyonayo. Kwa
mfano; kukandamizwa, kudhalilishwa na kukosa uhuru wakutoa maoni. Ni kundi
ambalo linatoa wito kwa wanawake wote kuona umuhimu na wajibu wa kushiriki
katika ukombozi wa mwanamke dhidi ya mila na desturi zinazowagandamiza.
Wanaharakati wa kundi hili ni kuwakomboa wanawake kutoka katika minyororo ya
utamaduni unaowanyima fursa za kufanya maamuzi, kuotoa maoni na kutoshiriki
badhi ya shughuri ambazo jamii huwaona wao ni kama chombo tu ambacho hakina
nafasi yoyote isipokuwa kumsikiliza mwanaume nah ii ni kutokana na mfumo uliopo
katika jamii nyingi.
Wafeministi wasagaji, ni wanaharakati walioibuka miaka ya
2000 na kuendelea. Wafuasi wa kundi hili wanamchukulia mwanaume kuwa ndiye adui
namba moja kwa mwanamke, hivyo mwanaume hawezi kushiriki katika harakati za
kumkomboa mwanamke. Waitifaki wa kundi hili, pia hudai kuwa wanaume hutumia
asasi ya ndoa kumkandamiza mwanamke, asasi ambayo mwanamke huchukuliwa kama
chombo tu katika familia, ni mtu ambaye hana majukumu mengine Zaidi ya kulea
familia, ni mtu ambaye thamani yake haionekani Zaidi ya kuwa chini ya mamlaka
ya mwaume katika maamuzi na kumiliki nyanja zote za uzalishaji mali. Aidha
kundi hili linadai kuwa, uhuru wa mwanamke utapatikana pale atakapoacha
kujamiiana na mwanamume badala yake washirikiane wao kwa wao hata katika
masuala ya kimapenzi.
Kwa kuhitimisha, wafeministi wanaamini kuwa mtazamo wa jamii
nyingi dhidi ya wana nb wake ni kudunisha na kuwafanya watu wa daraja la pili.
Kwa msingi huo wanasistiza juu ya kubadilishwa mtazamo wa jamii kuhusu wanawake
na kufuta ubaguzi dhidi yao, mtazamo ambao umesababisha kupatikana kwa baadhi
ya mafanikio makubwa kwa maslahi ya wanawake wa nchi za magharibi, ingawa Irib (2014)
anadai kuwa, suala la kupambana na ubaguzi huo halipaswi kuwa kisingizio cha
kutokomeza na kuua maana ya maisha, kumdumisha mwanamume katika jamii na
kulazimisha haki na majukumu sawa na yanayofanana licha ya tofauti za
kimaumbile.
MAREJELEO
Cambridge
(1995) Andvanced Leaners English
Dictionary: London. Cambridge University Press
Gabriel,
G. (2015) Ufeministi, Itikadi na Misingi
yake. Mwanza: Serengeti Publishers.
Irib,
World Service (2014) Matatizo ya Wanawake
katika Ulimwengu wa Magharibi.
http://www.kiswahili.irib.ir/38823
Malenya, M. M. (2012) Matumizi
ya Lugha katika Fasihi Simulizi. Mwanza. Inland press.
Mulokozi, M.M. (2017) Utangulizi
wa Fasihi ya Kiswahili: Dar es Salaam: Moccony Press.
Njogu K &
Chimerah. (1999) Ufundishaji wa Fasihi.
Nadharia na Mbinu. Nairobi: Jomo
Kenyatta Foundation.
Samson, M. K. (2017) Nadharia
ya Ufemisti Katika Jamii: St. Augustine of Tanzania. Mwanza
TUKI (2012) Kamusi ya
Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam. TUKI.
Wamitila,
K.W. (2003). Kichocheo cha Fasihi
Simulizi na Fasihi Andishi. Nairobi: Focus
Publication Limited.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com