0.1
Utangulizi
Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo tumejadili dhana ya matini,
tafsiri na matini za tafsiri, sehemu ya pili ni kiini cha swali ambapo
tumejadili vigezo anuai na umuhimu wa uanishaji wa matini za tafsiri, sehemu ya
tatu ni hitimisho na ya nne ni marejeleo.
2.0
FASILI YA MATINI, TAFSIRI NA MATINI ZA TAFSIRI
Katika sehemu hii tumetoa
fasili ya matini, tafsiri na matini za tafsiri kama ilivyofasiliwa na wataalamu
mbalimbali:
2.1
Dhana ya Tafsiri
Wataalamu mbalimbali
wamefasili dhana ya tafsiri kama ifuatavyo;
Catford (1965:20)
anafasili tafsiri ni kuchukuwa mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja
(lugha chanzo/ LC) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana na hayo kutoka
lugha nyingine (lugha lengwa/ LL).
Nida na Taber (1969)
tafsiri ni uzalisha upya ujumbe wa lugha chanzo kwa kutumia visawe asili vya
lugha lengwa (LL) vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi, kwanza kimaana pili
kimtindo.
TUKI (2002) tafsiri ni
kutoa mawazo kutoka katika lugha moja kwenda lugha nyingine bila kubadilisha
maana.
Kwa ujumla, tafsiri ni
uhawilishaji wa mawazo au ujumbe au taarifa iliyopo katika maandishi kutoka
lugha chanzo kwenda lugha lengwa bila kupoteza maana ya matini asilia.
2.2
Dhana ya Matini
Mwansoko (1996) anafasili
matini ni wazo au mfululizo wa mawazo wenye utoshelevu wa kimaana ambao
unahitaji kutafsiriwa. Mfano matini yaweza kuwa neno, kirai,kishazi, sentensi,
aya au tungo.
Massamba (2009) amefasili
matini kuwa ni maelezo ya kitu ambayo ama yameandikwa na mtu au yamenukuliwa na
ambavyo yamekusudiwa kutumiwa kwa madhumuni maalumu.
TUKI (2013) matini ni
kifungu cha habari kilichoandikwa. Fasili hii inaweka bayana juu ya habari
ambayo ipo katika maandishi, hivyo maelezo yaliyo katika maandishi ni matini
ambayo yanaweza kuwa ni ya aina mbalimbali kama vile matini ya kisiasa.
Kwa ujumla matini ni wazo
au mawazo yenye utoshelevu kimaana yaweza kuwa katika maandishi au yasiwe
katika maandishi bali matini inayotafsiriwa lazima iwe katika maandishi.
2.3
Dhana ya Uainishaji wa Matini za Tafsiri
Florence (2014:24)
anaeleza kuainisha matini ni kuzigawa au kuziweka matini katika makundi
mabalimbali kwa kuzingatia kufanana kwake kwa sifa kadhaa, anaendelea kueleza
kuwa sababu za kuanisha matini za tafsiri ili kupata aina au makundi kadhaa
yatakayo tuongoza kuchagua njia au mbinu ya kutafsiri.
3.0
vigezo vya uanishaji wa matini za tafsiri
Florence (2014:24) ameainisha
vigezo vitatu vya uainishaji wa matini za tafsiri ambavyo ni kigezo cha mada,
kigezo cha istilahi na kigezo cha dhima kuu za lugha.
3.1 Kigezo cha Mada/ Maudhui
Katika kigezo hiki
kinachoangaliwa ni kwamba matini inaongelea nini au inahusu nini kwa mtazamo wa
kijumla. Kwa kutumia kigezo hiki cha mada tunapata aina tatu za matini ambazo
ni matini za kifasihi, matini za kiasasi na matini za kisayansi.
3.1.1
Matini za Kifasihi
Ni matini zinazohusu
maandiko ya kifasihi kama hadithi fupi na riwaya, tamthiliya, ushairi na
kuendelea. Mfano tamthiliya ya Mfalme Edipode
iliyotafsiriwa na Samwel Mushi na Mabepari
wa Venusi iliyotafsiriwa na Mwl. J. K Nyerere.
3.1.2
Matini za Kiasasi
Ni matini zinazohusu
siasa, biashara, fedha, sheria, serikali na asasi zinginezo. Kwa mfano matini
hizi za kimamlaka ni kama vile matini za kisiasa na serikali (hotuba, risala,
mikataba na vyeti).
3.1.3
Matini za Kisayansi
Ni matini zinazojumuisha
nyanja zote za sayansi na teknolojia. Mfano maelekezo ya matumizi ya vifaa
mbalimbali vya kielektroniki. Mfano matini za Kamusi za Sayansi kama vile
baiolojia, fizikia na kadhalika.
3.2
Kigezo cha Matumizi ya Istilahi
Florence (2014) Kigezo
hiki huangalia kiwango cha matumizi ya istilahi za uwanja fulani. Hivyo matini
huainishwa kwa kuangalia wingi au idadi za istilahi au msamiati maalumu kwa
ajili ya taaluma husika. Kwa kuangalia idadi ya istilahi tunapata aina tatu za
tafsiri ambazo ni matini za kiufundi,
nusu ufundi na matini zisizo za kiufundi.
3.2.1
Matini za Kiufundi
Hizi ni matini ambazo
huwa na idadi au matumizi makubwa ya istilahi.
3.2.2
Matini za Nusu Ufundi
Ni aina ya matini ambazo
huwa na kiwango cha kati cha matumizi ya istilahi.
3.2.3
Matini Zisizo za Kiufundi
Matini hizi zinakuwa
hazina matumizi ya istilahi na hivyo hutumia msamiati wa kawaida.
3.3
Kigezo cha Dhima Kuu za Lugha
Bulher (1965),
akinukuliwa na Mwansoko (2013:11), ameainisha dhima kuu za lugha tatu ambazo ni
dhima elezi (expressive function), dhima arifu (informative function) na dhima
amili (Persuasive function).
3.3.1
Dhima Elezi
Dhima elezi, amabapo
lugha hutumiwa kwa madhumuni kueleza hisia za mtu binafsi bila kujali hadhira.
Kiini cha dhima elezi ni mwandishi.
3.3.2
Dhima Arifu
Dhima arifu, ambapo lugha
hutumiwa kama nyenzo ya kutolea taarifa. Kiini cha dhima arifu ni ukweli.
3.3.3
Dhima Amili
Dhima amili, hapa lugha
hutumiwa kwa madhumuni ya kuibua au kuchochea hisia za hadhira. Kiini cha dhima
amili ni hadhira.
4.0
UMUHIMU WA UAINISHAJI WA MATINI ZA TAFSIRI
Ufuatao ni umuhimu wa
uainishaji wa matini za tafsiri kama ulivyo jadiliwa na wataalamu mbalimbali.
4.1 Mahususi ya Matini ndiyo Inayoukilia Mbinu Mwafaka
ya Tafsiri
Mwansoko (1996:15)
anaelezea kwa kutoa mfano kuwa, mahususi ya matini ndiyo inayoukilia mbinu
mwaka ya tafsiri mfano matini amili huwa na muelekeo wa kutafsiri zaidi kwa
kutumia tafsiri ya kimawasiliano(tafsiri huru). Hivyo uanishaji wa matini za
tafsiri ni muhimu kwani mfasiri huweza kukilia mbinu mbalimbali kutokana na
matini husika.
4.2 Urahisisha Upangaji wa Gharama
Mwansoko (1996:15)
anaendelea kwa kutoa umuhimu mwingine wa uanishaji wa matini za tafsiri kuwa
uanishaji wa matini za tafsiri humsaidia mfasiri kupanga gharama za matini
mbalimbali, mfano bei za matini za kisayansi hutofautiana na bei za matini za
kisheria hivyo gharama za kufasiri matini hupangwa kulingana na aina ya matini
inayofasiliwa. Pia humsaidia mfasiri kujua atatumia muda gani katika kufasili
matini.
4.3 Hurahisisha kazi ya kufasiri Matini
Mwanjala (2011:177)
anaelezea pia umuhimu mwingine wa kuanisha matini za tafsiri kuwa, uanishaji wa
matini za tafsiri humsaidia mfasiri kurahisisha kazi ya kufasiri kulingana na
aina ya matini, mfano tafsiri zinazohusisha matini zisizo za kiufundi ambazo
huwa hazina matumizi ya istilai na hivyo kutumia msamiati wa kawaida urahisi wa
kutafsiri ni tofauti na urahisi wa kufasiri matini nyingine mfano matini za
kisayansi.
4.4 Uainishaji Unamsaidia Mfasiri Kuandaa Zana
za Kufasiri
Mwanjala (2011:177)
anaendelea kwa kueleza umuhimu mwingine wa uanishaji wa matini za tafsiri kwa
kusema uanishaji huu humsaidia mfasiri kuandaa zana mbalimbali zinazotumika
katika kazi ya kutafsiri. Mfano wa zana ni kamusi, karatasi, kalamu na rula
hivyo umuhimu huu msaidia mfasiri kutafuta zana kabla ya kuanza kufasiri mfano
mfasiri anataka kufasiri matini za kisanyansi hapa mfasiri hana budi kutafuta
kamusi mbalimbali za kisanyansi ili aweze kifanikiwa katika kazi yake.
4.5 Uainishaji Humsaidia Mfasiri Kuteua Mbinu
ya Kufasiri Pamoja na Nadharia Faafu kwa Mujibu wa Aina ya Matini
Mwanjala (2011:177)
anaeleza umuhimu mwingine wa uanishaji
wa matini kuwa matini kama vile matini za kisanyansi hufasiliwa vyema zaidi kwa
kutumia tafsiri maana ilihali matini amili hufasiliwa zaidi kwa kutumia tafsiri
mawasiliano, utofauti huu umetoka na umuhimu wa uanishaji ambapo humsaidia
mfasiri kuteua mbinu na nadharia mbalimbali zitakazo muongoza katika kazi yake
ya kutafsiri.
4.6 Uainishaji Matini Hutoa Muongozo Kuhusu
Kiwango cha Ugumu wa Kufasiri kwa Mujibu wa Matini Husika.
Mwanjala (2011:177) kwa
upande mwingine Mwanjala anamalizia kwa kuelezea umuhimu mwingine wa uanishaji
wa matini ambapo, uanishaji huu wa matini za tafsiri humsaidia mfasiri kujua
kiwango cha ugumu ambapo huweza kusababishwa na muda pamoja na gharama
atakazozihitaji katika kufasiri kila aina ya matini kwani matini. Mfano za
kisanyansi muda na gharama ni tofauti na muda na gharama zitakazotumika katika kufasiri matini nyingine mfano matini
zisizo za kiufundi na hivyo viwango vya ugumu baina ya matini moja na nyingine
hutofautiana.
5.0
Hitimisho
Kwa kuhitimisha uanishaji
wa matini za tafsiri ni muhimu kwa mfasiri yeyote katika kukamilisha kazi za
tafsiri kwani vigezo anuai vya uanishaji wa matini ndio msingi matini bora kwa
mfasiri. Pia mfasiri huweza kutumia kigezo zaidi ya kimoja katika kutafsiri
matini lengo ni kufanya kazi bora. Hivyo haina budi kuzingatiwa katika kazi ya
kufasiri.
6.0
Marejelo
Catford, J.C. (1965). A linguistic Theory of Translation.
London: OUP
Florence, A.M (2014). Tafsiri na Ukalimani ( Hakijachapishwa).
Nida, E.A na Taber, C. R
(1969). The Theory and Parctice of
Translation. Prentice Hall: London
Massamba, D.P.B. (2009. Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar
es Salaam: TUKI
Mwansoko na wenzake
(2013). Kitangulizi cha Tafsiri. Nadharia
na Mbinu, Dar es Salaam:
TUKI
Mwansoko, H.J.M. (1996). Kitangulizi cha Tafsiri. Nadharia na Mbinu.
Dar es Salaam: TUKI
TUKI (2013). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es
salaam: TUKI
Wanjala, F.S, (2011). Misingi ya Ukalimani na Tafsiri. Mwanza: Serengeti Educational
Publishers LTD
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com