Flower
Flower

Wednesday, January 29, 2020

Utendi wa Hamziyyah

UTANGULIZI
Wataalam mbalimbali wamefasili dhana ya utendi kama ifuatavyo:
Mulokozi (1983:13, 1996:85) anasema utendi ni ushairi wa matendo. Ni utungo mrefu wenye kusimulia matukio ya kishujaa yenye uzito wa kijamii au kitaifa. Matukio haya huweza kuwa ya kihistoria lakini tendi nyingi huchanganya historian a visakale au visasili
Wamitila (2003:333) yeye anasema utendi huelezea shairi refu la masimulizi kwa mapana linalohusu matendo ya mashujaa. Utendi unahusisha hadithi za kishujaa, visasili na hata chimbuko la taifa Fulani. Ameendelea kubainisha aina mbili za utendi simulizi na utendi andishi
Fasili ya Wamitila na Mulokozi kuhusu dhana ya utendi zinafanana kwa kuwa wote  wanaihusisha na matendo, matukio ya kishujaa na utaifa, bali kilichoongezwa ni kubainisha aina za tendi ambazo ni tendi simulizi na andishi.
Kwahiyo utendi ni kama makavazi ya jadi ya historia ya jamii Fulani ambayo kupitia tendi mbalimbali jamii inajitambua kuhusu historia yake katika vipindi mbalimbali ilimopitia chimbuko lake, mashujaa wao na kujua mila na desturi zao. Baadhi ya tendi zijulikanazo ulimwenguni ni Utendi wa Fumo Liyongo, Kachwenyanja, Rukiza, Mugasha, NyakiiruKibi (Afrika Mashariki), Sundiata (Mandingo-Afrika ya kati), Gilgamesh(wa-kisumeri), Nibelungenlied(Ujerumani), Ramayana na Mahabarata(India), Jumong(Korea), Kalevalaa(Ufini) na Hamziyyah(Misri). Kazi hii itajikita zaidi kuelezea utendi wa Hamziyya.
Utenzi wa Hamziyya ni utungo wenye asili ya kiarabu, uliotungwa na Muhammad bin Said Al-Busiri na kutafsiriwa kwa Lugha ya Kiswahili na Sharrif Aidarus. Utendi huu ni tafsiri ya zamani sana katika lugha ya Kiswahili ingawa kitarehe kuna kazi zilizoitangulia katika kutungwa kwake kama vile utenzi wa Tambuka (Chuo Cha Herikali)
Kwa asili utendi huu ni kiarabu iliyotungwa na al-Busiri inayoitwa Kasidatul’l Hamziyyah fi ‘l-mada’ihi’ n Nabawiya yaani Kasida ya kumsifu Mtume Muhammad. Katika Kiswahili utendi huu hujulikana kama Chuo cha Hamziyyah au Maulid ya Hamziyyah au Hamziyyah tu.
Utungo huu ni wa aina ya ukawafi amabao kiasilia ulikua na beti 456 na jumla ya mizani 15 kwa kila mshororo. Ambapo katika Kiswahili kuna beti 481, beti 8 za mwanzo na 10 za mwisho zimeongezwa na mtarjumi wa kasida hii, Sharrif Aidarus.
Utenzi huu ni maarufu sana katika ulimwengu wa fasihi, dini ya kiislamu na waswahili. Umaarufu wake unatkana na kuimbwa kwake wakati wa sherehe za maulidi ya kumsifu Mtume Muhammad kama ukumbusho wa kuzaliwa kwake kama asemavyo Lubis (1983) alivyonukuliwa na Mutiso (2005:5) kwamba Hamziyyah kama kazi ya kisanaa inakaribia kwa umashuhuri zaidi kuliko al-Burdah
Utendi wa Hamziyyah umeitwa hivyo kutokana na kuishia kwake kwa abjadi ya kiarabu hamza katika mshororo wa mwisho yaani kina cha mwisho cha utungo huo wa kiarabu. Fauka hiyo kuna maandishi yanayounasibisha utungo huu na swahaba wa Mtume Hamza. Wanasema, “Hamziyyah ni dhehebu moja la kiislamu lililoanzishwa na Hamzah bin Adrak. Yawezekana kwamba kasida hii ni tunu kwa dhehebu hili. Yumkini utenzi huu uliitwa hivyo kwa kutaka kuusifu mji mtakatifu wa Makka amabako hadi sasa kuna chuo kikuu kiitwacho Umm-al Qura kama kasida yenyewe inavyoitwa. Yawezekana pia kasida hii iliitwa hivyo kwa sababu ya kumkumbuka yule shujaa wa dini ya kiislamu aitwaye Hamza (Mutiso, 2005:5)
Kauli hii haina ithibati. Kwanza hakuna dhehebu katika uislamu lililoanzishwa na Hamza lijulikanalo kama Hamziyyah. Pia kuwepo kwa chuo kiitwacho Umm-al Qura huko Makka sio sababu ya utenzi huu kuitwa hivyo bali ni sifa tu mtu apendayo kutoa kwa kitu alichokithamini. Umm-al Qura maana yake ni “Mama wa Mji”. Ukiliangalia jina na yale yaliyomo katika utendi hayana uhusiano. Hali kadhalika dai la kwamba kasida hii inaimbwa kwa kumkumbuka shujaa wa kiislamu Hamza ni uzushi kwani sifa zilizomo katika utendi huu ni za shujaa Muhammad na si Hamza na hata anayetajwa ndani ya utendi ni Muhammad
Hivyo utendi huu hauna maana nyingine zaidi ya kuwa ni utungo unaoishia na Hamza  herufi mojawapo katika herufi za kiarabu. Na hii haina maana zaidi ya kuwa herufi zilivyo herufi zingine za kirumi kama a,e,i,o,u.

HISTORIA FUPI YA MTUNZI
Sharif Muhammad bin Said Hammad Al- Bussir alikua ni mshairi wa Kimisri katika fasihi ya kiislamu aliyeishi kwenye miaka ya 608-694 H (1212-1294 m). Kwa upande wa elimu alijifunzia huko Cairo kwa Sheikh Dhahir. Alijifunza usufii, fasihi ya kiislamu, kunga za lugha ya kiarabu, kukariri Quran Tukufu kwa Moyo, Historia ya Uislamu, Hadithi na Sira ya Mtume Muhammad, kunukuu miswada, uchoraji na utiaji wa nakshi
Kutokana na kuwa na taaluma mbalimbali aliweza kutunga kazi nyingi sana, baadhi ya kazi hizo ni utenzi wa Hamziyyah, Kasida ya Burudai, Kasida ya Lamiyyah, Kasida ya Lahiyyah, Kasida ya Dariyyah, Kasida ya Mimiyyah na Dhukr
HISTORIA FUPI YA MTARJUMI
Sharif Sayyid Aidarusi bin Athmani, alikua ni mwanazuoni na miongoni mwa Maulana mashuhuri wa karne ya 18 na 19 walioongoza katika usomi wa kidini na hata kifasihi katika Afrika ya Mashariki. Alitafsiri kasida ya Hamziyyah kwa Kiswahili cha Kingozi ambacho ni Kiswahili cha zamani sana kutoka katika Lugha ya Kiarabu, Aidarus aliishi Pate nchini Kenya
TAREHE YA KUTARJUMIWA UTENDI WA HAMZIYYAH
Ama tarehe ya kutarjumiwa au kuandikwa kwa utendi huu kunahitilafiana miongoni mwa wataalamu wa fasihi ya Kiswahili waliouhakiki japo wengi wao wanakubaliana kuwa yawezekana ilitarjumiwa kabla ya mwaka 1652. Miongono mwao ni Knappert (1968, 1969, 1973, 1979, 1985), Hinchess (1936), Kijumwa (1934), Mutiso (2005), Mulokozi na Sengo (1995). Kuna wanaosema kuwa ulitarjumiwa mwaka 1652 (1257 AH) (Mulokozi 1996:144), pia 1749(1162, AH) (Mkele 1976) amabpo Hinches anasema kuwa mpaka mwaka 1936 ulikuwa na miaka 144. Hivyo yawezekana kuwa utenzi huu ulitarjumiwa kabla ya mwaka 1652. Tatizo la kutokujua tarehe sahihi ya kuandikwa kwa utenzi inaweza kuwa ni asili yake ya usimulizi ambayo kuipata tarehe sahihi kunahusishwa na kutokuwepo kwa kumbukumbu mbalimbali za kihistoria zilizohifadhiwa katika jamii husika.
YALIYOANDIKWA KUHUSU UTENDI WA HAMZIYYAH
Knappert (1968) aliandika kuhusu utendi wa Hamziyyah katika mada yak eta “The Hamziyyah Deciphered” na mwaka (1979) aliandika “The Oldest Islamic Poetry: The Hamziyyah”. Naye Mkelle katika kiango (1976) aliandika “Hamziyyah-The Oldest Swahili Translation” na Abdallah (haina tarehe) aliandika “Tanzu za Ushairi wa Kiswahili na Maendeleo yake”. Ridhiwani alitafsiri Hamziyyah kwa Kiswahili rahisi japo ilionekana ni tafsiri sisisi.
Vile vile Hinches alinukuu beti 96 wakati Knappert (1968) alinukuu beti 60-70 na kuzitarjumu kwa lugha ya kiingereza. Mkelle nae katika uchunguzi wake aliishia njiani na hivyo Ridhiwan kuthibitisha kuwa kasida hii ngumu kutafsiri.
Hivyo inasadikika kuwa kasida hii ya Hamziyah haikutafsiriwa kikamilifu kwa lugha yoyote ya kimagharibi (Knappert 1968, Mutiso 2005)
MUHTASARI WA UTENDI
Utendi wa Hamziyyah unasimulia kuhusu sira ya Mtume (S.A.W). Mwandishi ameonesha kuwa Mtume (S.A.W) alizaliwa katika kabila bora kuliko zote za kiarabu na katika ukoo wa Banni Hashim ambao ni kati ya koo za kwanza zilizo tukufu kwa Makureshi.
Mtume alipozaliwa matukio tofauti yalitokea mfano, kuanguka kwa jumba kubwa la mikutano la Kisra la Mfalme wa Uajemi (Ufursi) lililoyumbayumba na kupasuka na kuporomoka kabisa. Inasemekana pia siku hiyo Mahabushia waliazimia kuuteka mji wa Makka baada ya kuwa Yamah yote imo chini ya mikono yao. Hivyo Mwenyezi Mungu aliwaletea ndui, yakaangamia majeshi yao kwa muda mfupi na inasemekana walipukutika kama kuku.
Vile vile mito na chemichemi za Mafursi zilikauka. Jambo lililopelekea huzuni majumbani mwao sababu ya kuzimika kwa mioto ya Mafursi ambayo walikuwa wakiabudu nyumbani mwao kwa miaka mingi iliyopita. Usiku alipozaliwa mtume (S.A.W) nyota zenye mianga zilikaribia chini alipokuwa na kuangaza eneo hilo na pande zote za dunia. Mwangaza uliwawezesha wakazi wa Makka kuona jumba la mfalme Kisra. Vyote vilivyomo Makka vikang’ara kutokana na nuru ya Muhammad (S.A.W). hata waliokuwa Urumi wakaweza kuyaona makasri hayo ya Kaizari na kuiona Makka vizuri
Wakati alipozaliwa alikuwa ameangalia juu mbinguni, kasha alipiga chafya na kusema “Alhamdulilah” nao malaika wakajibu “Mwenyezi Mungu akubariki”
Mama yake akiwa na ujauzito wa miezi nane, baba yake akafariki. Kama ilivyo desturi ya waarabu, wanawake (wazazi) hawanyonyeshi watoto wao bali hunyonyeshwa na mama wengine. Wanyonyeshaji walimkataa mtume sababu alikua ni yatima na maskini na kusema kuwa waingeweza kulipwa.
Hatmaye akanyonyeshwa na Halima, mwanamke ambaye baadaye maisha yake yakabadilika na kuwa mazuri zaidi kwani wanyama wake waliokuwa hawatoi maziwa wakaanza kutoa maziwa kwa wingi wakati jamii nyingine hazikuwa na hata jani bichi la kulishia wanyama.
Mtume (S.A.W) alipofikisha miaka sita, akafiwa na mama yake, hivyo kulelewa na babu yake bwana Abdul Mutalib.
Tangu alipkuwa mtoto (mwenye kuanzia miaka miwili) malaika alikuwa akimpasua kifua na kumshona ili kuhifadhi siri katika kifua chake. Alipasuliwa pia kutolewa kipande cheusi cha nyama(damu) na kukisafisha. Siri alizowekewa alizuiliwa asizitoe mpaka atakapoamriwa aeneze.
Tangu utotoni mtume alizoea kwenda pangoni Hirrah ili kumwabudu Mwenyezi Mungu. Moyo wake, miguu na viungo vyote vya mwili wake vilikuwa imara na dhati katika kumwabudu Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu alipoamua kumtuma Mtume kuja duniani alituma vimondo kuilinda njia yake kutokana na majini. Vimondo viliwafukuza majini kutoka pale walipokuwa wakisikiliza habari za siri, kwani kuzaliwa kwake kulimaanisha mwisho wa nguvu za Wahayi na Makuhani juu ya mambo ya Mbinguni.
Mtume alipopewa utume vitu vyote visivyokuwa na roho kama vile miti na mawe viliweza kumshuhudia na kumuunga mkono vikisema “Assalaam Aleikum”. Pia vitu hivyo vilisema maneno fasaha ambayo Makureshi wasingeweza kuyasema.
Katika hali ya utume alipaishwa mbinguni, mbingu ambayo hakuna mtume aliyewahi kufikishwa. Jamii yake na wote waliomzunguka walimkana, aliumizwa, kusumbuliwa na kudharauliwa zaidi kila alipowalingania katika kumcha Mwenyezi Mungu. Japokuwa wote waliokuwa hawamwamini waliangamia, vitu vilivyomtii vilikua ni pamoja na mijuzi na paa pia mtende aliokuwa anauegemea ulikua ukimtii hali iliyopelekea kukimbiwa na watu waliogopa. Mtume aliposafiri kwenda katika biashara zake Sham, baada ya kukosa kivuli na kuketi kwenye jua, wingu na mti mkubwa vilimfunika.
Siku moja baada ya mateso makubwa, Mwenyezi Mungu alimwamuru ahame mji wa Makka, akaondoka na rafiki yake aitwae Abu-Bakr. Baada ya kujua kuwa walifuatwa wakaingia katika pango amabapo njiwa wawili walitaga mayai katika mlango wa pango na buibui alitandaza tando lake hali iliyopelekea maadui kutojua walikoelekea. Baada ya hapo walitoka na kuelekea Madina, ambapo njiani watu wengi walimpenda kutokana na tabia zake nzuri na miujiza aliyokuwa anaifanya, mfano kuweza kumkamua mbuzi asiyekuwa na maziwa kutoa maziwa yaliyotosheleza watu wote waliopo hadi kubakiza mengine.
Katika utume wake alipigana vita tofauti na maadui wa Uislamu na kushinda japokuwa nguvu jeshi lake halikuwa kubwa zaidi ya maadui. Mwisho watu kutoka mataifa tofauti walimkubali na kuweza kusimamisha dola ya Kiislamu.
Mtume katika ujana wake alimwoa bi Khadija, mwanamke aliyetambua tabia nzuri ya Mtume (S.A.W) ya kumcha Mungu na kuzipa kisogo raha za dunia, baadaye alioa wake wengine kumi hivyo kufikisha jumla ya wake kumi na moja.
UCHAMBUZI WA UTENDI WA HAMZIYYAH
Finnegan 1970 alisema kuwa katika fasihi simulizi ya kiafrika hakuna tendi bali kuna tendi andishi na sifo tu. Kauli hii ilitokana na vigezo alivyovitumia vya tendi za kiyunami amabazo aliziita ni tendi halisi. Vigezo alivyotumia ni:
  1. Utendi uwe katika umbo la ushairi na si katika nathari
  2. Utendi uwe na urefu wa kutosha
  3. Uwe ni utungo mmoja usiwe ni mkusanyiko wa tungo zinazohusisha visa mbalimbali ambavyo pengine havina uhusiano ulio dhahiri.
  4. Uzungumzie mambo yahusuyo shujaa na kusawiri matukio ya kiutendi kama kuzaliwa kwa shujaa, masahibu yake, safari zake, uongozi wake kwa watu wake na kifo chake.
Kauli hii ilipingwa na wataalamu mbalimbali kama walivyoainishwa na Mulokozi (2002:2), baadhi yao ni ; Biebuyk (1972;1976;1978), Johnson(1978;1980), Mbele(1977), Okpewho (1976;1977;1979) na Mulokozi(1975;1980;1981;1983) ambao walifanya utafiti wa kina na kuibua hoja zifuatazo:
Mbele (1977) alikanusha usemi wa Finnegan kwa kutumia utendi wa Sundiata wa Afrika ya Magharibi ambao unatetea umwinyi na kulitukuza tabaka la Mamwinyi. Kwa maoni yake anaona kuwa utendi wa Sundiata unaingia katika sifa zilizotajwa
Okpewho (1977) alitumia kipengele cha muundo ili kukanusha dai la Finnegan, alitumia tendi za Mwindo na Kambili na kuzibainisha sifa za kimuundo, kisanaa na kiutunzi za tenzi hizo ukilinganisha na sifa za tenzi za mataifa mengine na kuhitimisha kuwa tungo hizo pia ni tendi. Miongoni mwa sifa hizo ni fomula, topo, uhusiano, takriri, na malumbano ya wahusika.
Biebuyk (1978) anamuunga mkono Mbele na Okpewho katika kuthibitisha kuwa Afrika kuna tendi simulizi. Yeye anaona kuwa kauli ya Finnegan imetokana na ufinyu wa data alizopata.
Mulokozi (2002) ni miongoni mwa wataalamu waliothibitisha uwepo wa tendi simulizi barani Afrika. Yeye alitumia utenzi wa Nanga ujulikanao kama Utendi wa Kachwenyanja ambao ni maarufu mkoani Kagera, Tanzania. Alisema kuwa utenzi wa Kaachwenyanja na halisi si kwa mujibu wa vigezo vya Finnegan tu, ambavyo havitoshelezi, bali pia kwa mujibu wa vigezo vingine vya kiulimwengu, ambavyo huuchukulia utendi katika dhana ya umbo lake la asili la utendaji na si katika maana finyu ya kuwa katika maandishi tu.
Ukiwachunguza wataalamu wote hawa wanaipinga kauli ya Finnegan na kutetea kuwa tendi katika Afrika zipo, tena zinaakisi mifumo mbalimbali katika jamii husika.
Makala hii inalenga kutoa mchango katika mjadala huu, hivyo tutachambua utenzi wa Hamziyyah kwa mujibu wa sifa za utendi alizozitaja Finnegan na vigezo vingine vya kilimwengu na zile alizoziongezea Mulokozi(1996:86)
A: UMBO LA USHAIRI
Hiki ni kigezo kimojawapo cha utendi ambacho Finnegan anakisisitiza. Dhana ya ushairi aliyoikususudia hapa ni ile ya nudhumu(verse) na si ushairi. Nudhumu ni utungo wowote wenye umbo la kishairi yaani wenye mpangilio wa maneno, urefu wa mistari, beti, vina n.k hata kama utungo huo hauna uzito ule wa kishairi kama matumizi ya lugha ya picha, sitiari, maudhui ya kishairi, hisi taswira n.k
Japo yeye mwenyewe katika ukurasa wa 10 anakubali kuwa si lazima utendi mzima uwe katika ushairi bali anakiri kuwa utungo mzima unaweza kuwa utendi.
Hivyo kulingana na maelezo hayo tunaweza kuthibitisha kwa  kuangalia kama kigezo hicho kinapatikana katika utendi wa Hamziyyah kwa kuziangalia sifa pambanuzi za ushairi wa utendi ambazo yawezekana Finnegan ndizo alizozikusudia japokuwa hakuzitaja
  1. Vina na Mizani
Utendi wa Hamziyyah una urari wa mizani na kina cha mwisho kinachofanana na utendi mzima. Mizani ya utendi huu ni 15 kwa kila mshororo na kina chake ni ‘ma’ kwa utendi wa Kiswahili na herufi Hamza katika utendi wa kiarabu kwa kila mstari wa mwisho, Mfano ubeti wa 37
A  li  zi  wi  li  ya     ma  mwi  sho  ni      hi  fa  dhi  ya      ke
Na  ku te u  li  wa     ta  ngu  mwa  ndo    M  tu  mi  mwe   ma
1     2   3  4  5    6      7   8      9         10     11  12  13  14      15
Hivyo kama kigezo cha urari wa vina na mizani kitachukuliwa kama uthibitisho wa utendi kisanaa basi Hamziyyah ni miongoni mwa tendi zilizomo Afrika. Ni beti mbili (33 na 164) tu ambazo kina chake ni mwa, yawezekana mwandishi hakutaka kuharibu sifa mojawapo ya Mtume yenye jina la Tumwa.
  1. Lugha
Lugha iliyotumika katika utendi huu ni ya Kiswahili kilichosheheni lahaja za Kiswahili na msamiati wa kiarabu. Lugha Y Kiswahili iliyotumika ni ngumu yenye kutumia maneno ya Kiswahili cha kale; Mfano, matumizi ya e/ili yanayowakilisha wakati uliopita; mfano ingile-aliingia, jiile-alikuja, nsomeele-nilisoma, weene-aliona. Hizi zinatuonesha mabadiliko mbalimbali ya kiisimu. Vile vile lugha hii inaonesha uhusiano na lugha nyingine za jamii mbalimbali za Tanzania, mfano katika ubeti wa 130 kuna neno kanwa, katika jamii nyingi za kibantu kanwa ni mdomo
Pia lahaja zilizopo ni za Chimwini, Kitikuu, Kipate, na Kiamu; Maneno yaliyotumika kutoka lahaja hizo ni kama; kwechu—kwetu, fungula—fungua, lokota—okota, mkila—mkia, tala—taa, tukula—chukua. Matumizi mengine ya lugha yaliyojitokeza ni kama:
  • Lugha ya Picha
Hii ni mbinu ya kishairi inayotumika kuunda taswira mbalimbali juu ya kitu kinachozungumzwa katika mawazo ya msomaji/msikilizaji. Mara nyingi hizi hugusa vionjo vya msikilizaji au msomaji kama kuona, kusikia, kuhisi, kuonja na kugusa. Hivi vyote huungana na kuleta taswira ya kile kinachokusudiwa. Taswira hizo zaweza kuwa za kimaelezo au za kiishara. Ntingi ya taswira(picha) zilizomo katika utendi wa Hamziyyah ni zile za miujiza iliyotokea katika maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W). miongoni mwa taswira (picha) hizo ni:
Ubeti wa 23-28 wakati wa kuzaliwa kwake kukiambatana na Falme na majumba kuanguka, kichwa kuelekea juu hii inaonesha ishara za kuwa daraja la juu. Katika ubeti wa 66-68 alivyojihifadhi katika pango huku akilindwa na Njiwa, Kanga na Buibui inaonesha upekee wake unaopelekea kuhifadhiwa na Mwenyezi Mungu pia ubeti wa 128 taswira ya upole wake wa kuweza kuvumilia kashfa, huonesha utakazo aliopewa na M/Mungu wa kuwa mvumilivu. Taswira zingine nyingi zimeambatana na sifa zake na vitimbwi alivyofanyiwa na maadui zake waliomkataa, mfano kumpiga mawe, kumtilia sumu na zinginezo zinazopatikana katika beti za; 28-36b, 37-43, 46-48, 53-56, 73-79, 106, 108, 113-115, 157-163 na 269-274.
  1. Sitiari
Ni tamadhali ya usemi ambayo kwayo kitu, matendo ya kitu au vitu vyenye tabia inayofanana hulinganishwa. Au ni pale kitu kimoja kinapopewa sifa na kuchukua nafasi ya kitu kingine kisichohusiana nacho. Katika ulinganisho wa vitu mtunzi hatumii vilinganishi kama vile; kama, kama vile, n.k. katika utendi wa Hamziyyah sitiari zinajitokeza katika ubeti wa 4,10,11,81,105,127,128,140,142,215,266 n.k Mfano katika ubeti wa 4
                                 Uwe ndiwe Tala ya fadhila na mayonjia
                                  Nuru hazinawiri pasipo nuru yako njema
Maana yake ni wewe ni taa ya kila tendo bora na ndio asili ya nuru zote, ndio asili ya yote yalito mema na yenye uongofu. Sitiari hii na zingine zilizotumika huonesha sifa ya Mtume zilivyomiminika kwa Waislamu na kumtukuza kuwa ni kiongozi wa kila jema.
  1. Tashbiha
Ni tamathali ya semi ambapo kitu, vitu, hali moja au mbili na zaidi hulinganishwa na kitu kingine kwa kutumia viunganishi vilinganishi kama; ja, mithili (ya), mfano (wa), kama, fanana na....., vile vile, sawasawa na......, n.k. Kufanana huku mara nyingi huwa ni ushahibiano wa hali ya utendaji au maumbile kama vile sura, umbo, nguvu, n.k . katika utendi wa Hamziyyah zipo tashbiha kadhaa baadhi yake zinapatikana katika ubeti wa 3,12,108,112,159,267,306-309,318-320, n. K Kwa mfano ubeti wa 11
                                   Napendezwa tena na uso wako ingawa Jua
Maana yake ni: Napendezwa na uso wako ulio kama jua. Usemi huu huitabanisha hadhira ubora wa Mtume (S.A.W) kwa yale ayadhihirishayo, kwamba huwatoa watu katika ujinga.
  1. Tashihsi (Uhusishaji)
Mbinu hii ni ile ya kukifanya kitu kiwe na maumbile/tabia ya nafsi ya mwanadamu. Katika mbinu hii hali na vitu visivyo na uhai hupewa sifa na hisia za binadamu. Kama vile wadudu, miti,ndege, na wanyama. Wakati mwingine vitu hivi huongea na kutenda kama binadamu. Hali hii inajitokeza katika utenzi huu, mfano:
  • Vitu visivyo hai kumsalimia na kumsujudu Mtume Muhammad (ubeti 46-47)
  • Wanyama kuwa na akili hata zaidi ya Wanadamu mfano ndovu kukataa kuiharibu al-ka’ba (ubeti wa 61-63)
  • Changarawe na mawe viliswali na kumuunga mkono Mtume Muhammad (ubeti wa 63)
  • Mijusi kusema (ubeti wa 65)
  • Panga kukataa kumuua Mtume (ubeti wa 108)
  • Nyama ya sumu kusema kuwa imetiwa sumu (ubeti wa 116-117)
  • Wingu kumkinga (ubeti wa 138)
  • Mlima kutetemeka kwa furaha (ubeti wa 156,183) na zingine kama 168,291,283,284,285-286,322-323 na 453. Tashihsi hizi na zingine huthibitisha miujiza iliyotokea katika maisha ya Mtume (S.A.W) ambayo iliaminika kuwa ujio wake ni tishio kwa kila kitu au kiumbe.
  1. Taashira/Ishara
Kuna matumizi makubwa ya mbinu hii. Taashira ni neno, kitu au tukio linaloficha maana au hisia. Ishara hutumiwa kuwakilisha kitu ambacho hatungetaka kukitaja moja kwa moja. Miongoni mwazo ni:
  • Ishara za wakati wa kuzaliwa Mtume Muhamad zinatuonesha upekee wa mtume Muhammad kama shujaa anayezaliwa tofauti na mitume wengine (ubeti wa 15)
  • Hii ni ishara ya ushindi wa uislamu duniani kote. Mito na chemchem za Mafursi zilikauka kuonesha ushindi wa uislamu juu ya dini nyingine duniani (ubeti wa 17)
  • Kuzaliwa Muhammad kichwa kimeelekea juu ni ishara kwamba atapandishwa daraja la kifalme (ubeti wa 24-25)
  • Ishara ya kutolewa kipande cha nyama nyeusi (ubeti wa 41) ni taashira ya kutolewa nyongo kifuani mwake ili aondokane na hasira pindi awalinganiapo watu wake. Ishara hii ni alama ya kutakaswa kwa Mtume Muhammad.
  • Mutwazi/ukaya (ubeti wa 54) ni ishara la vazi takatifu ambalo mwanamke wa kiislamu aliloruhusiwa kulivaa.
  1. Matumizi ya Semi
  • Kuipa nyongo dunia ikiwa na maana ya kuachana na mambo ya dunia na kuwa waumini thabiti (ubeti wa 34)
  • Kupewa mkono mweupe yenye maana ya kutakiwa heri na Mtume Muhammad(ubeti wa 366)
  • Njia nyeupe ni njia nyoofu isiyokuwa na shaka, shida au hatari yoyote
  1. Matumizi ya Balagha/Tashtiti
Hii ni mbinu ya kuuliza maswali ambayo majibu yake mtunzi anayafahamu, lengo huwa ni kusisitiza ujumbe anaotaka kuufikisha kwa aliowakusudia. Nia ya mtunzi huwa ni kufahamu zaidi wazo husika na vile vile kutoa msimamo wake pamoja na kumtazamisha msomaji. Mara nyingi maswali haya lengo lake ni kuamsha ari ya msomaji na kumfanya atafakari zaidi juu ya kinachozungumzwa. Mtunzi kupitia balagha huwachochea wasomaji wake ili wawaze kufikiria zaidi juu ya jambo analolielezea, baadhi ya maswali ya balagha yanapatikana katika beti zifuatazo:
  • Ubeti wa 1, 20, 102, 106 na 108 zinaonesha uwezo wa shujaa Muhammad dhidi ya maadui zake. Lengo la maswali haya ni kuwakejeli maadui na wapinzani wa Mtume Muhammad na kuonesha kuwa wasingeweza kumdhuru kwa sababu alikuwa na uwezo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
  • Pia ubeti wa 200-268 ametumia balagha kuonyesha tofauti baina ya Manasara, Mayahudi na Waislamu. Mtunzi amewaonesha wasomaji kwa kulinganisha makundi hayo matatu lengo likiwa ni kuzibeba dini za Manasara na Mayahudi na kuonesha kuwa dini ya uislamu ndiyo inayopaswa kufuatwa ulimwenguni kote. Ameonesha namna ambayo manasara na mayahudi wasivyoweza kutii na kufuata yaliyomo katika vitabu vyao vay Taurati n biblia (Injili)
  1. Kejeli
Ni mbinu ambayo mtunzi anaitumia ili kumtweza au kumdunisha mtu kwa kupewa sifa ambazo hazimstahili. Mara nyingi maneno yatumiwayo huwa ni ya kuumiza, kuchoma, kukatisha tama na kutia uchungu. Mbinu hii imetumika sana hasa pale mwandishi alipozikejeli dini za Ukristo na Uyahudi kwani kwa maoni yake Uislamu ndio dini bora na inapaswa kufuatwa na watu wote na kuwahimiza Waislamu wabakie katika Uislamu. Mfani ni katika ubeti wa 218 mwandishi anasema;
                                   Enyi wenye Zuo tuyuzeni kula zilipo
                                   Kuthalithi au kudhihiri walo wa nyuma
Maana ya kejeli hii ni kwamba enyi msio amini tuelezeni sababu za kuwa na utatu au kudhibitika kwake kwa waliotangulia? Kejeli hii imetumika kama changamoto ya kutathmini kila unachoamua kukifuata.
Na ubeti wa 231;
         Mwamba liwuwiwa ni Yahudi mzumuwo
          Wali na fufuo wenu kwayo dawamu?
Maana yake ni kuwa wasema aliuliwa na Mayahudi. Hii inaonyesha kuwa mwandishi amekusudia kuwafahamisha wanaoamini kuwa Yesu aliuliwa, kwamba Mayahudi waliwekewe mtu mfano wa Yesu na wakamuua hali ya kuwa Yesu alipaishwa mbinguni.
  1. Majina ya Lakabu
Lakabu ni neno la kiarabu lakab lenye maana ya sifa ajipayo au apewayo mtu kutokana na tabia Fulani aliyonayo ya kipekee. Ni jina la sifa ya kubandikwa apewayo mtu au mhusika kwa sababu ya tabia Fulani ya kipekee (uwezo wa kuwa na sifa ya kitu kingine) Mfano:
  • Mtume Muhammad ana majina ya kalabu chungu nzima, Abdul Qarim, Buhari,Tumwa, Mtume, Jua, Kifungo, Kifunuo, Mjuzi, Kipenzi/Mpenzi, Mtengwa, Muharamu, Mustafa, Muungwana, Mwema, Mwongozi, Nuru, Nyota ya Jaha, Sayyid, Taa. Majina yote haya yanabshiria tabia njema za Mtume Muhammad.
  • Abu Jahli maana yake ni baba wa wajinga (ubeti wa 109)
  1. Ritifaa
Hii ni mbinu ambayo mshairi huonyesha kuwa anaongea na kuhutubia mtu au kitu ambacho hakipo. Katika mbinu hii kitu kisicho na uhai kusifiwa na kusimuliwa kama kipo. Mbinu hii imetumika sana katika kasida hii. Mtunzi anazungumza na kuhutubia maswala yamuhusuyo Mtume Muhammad, familia yake, mswahaba (Makhalifa) na walioahidiwa kuingia peponi baada ya kufa ingawa watu hawa wote tayari wameshafariki. (ubeti wa 355-447). Hii ni kutaka kuthibitisha kuwa Mtume Muhammad alikuwa shujaa. Mfano ubeti 433;
                           
                   We una umati mbawo kwamba watamaniye
                   Kwawe ambia upewepo sawu umama
  1. Chuku
Mbinu hii imetumiwa kwa kiasi kikubwa katika kasida hii ya Hamziyyah. Kutia chuku ni kukuza jambo Fulani kupita kiasi au kutia tungo chumvi. Matumizi ya mbinu hii si kwamba mtunzi huwa na nia mbaya, bali anakuwa na lengo la kusisituza ujumbe unaowasilishwa na kukamilisha sifa za shujaa. Mbinu hii imetumika sana katika utendi huu wa Hamziyyah, mfano:
  • Katika sifa za mtume si za kawaida kuwa kwa mwanadamu kama alivyokuwa yeye. Mfano wa ubeti 127
  • Katika baadhi ya miujiza yake.
  • Na sifa nyingine zilizomkweza tofauti na uhalisia wake ambazo ni sifa za Mwenyezi Mungu. Mfano ubeti wa 336-337 Mtume alimponya Ali hata kuona kuliko mwewe.
  • Mtume kuzaliwa kichwa kikielekea juu.
  1. Takriri/urudiaji
Mbinu hii husisitiza ama hushadadia ujumbe unaohusika ili msomaji apate athari ya msisitizo huo. Kwa mfano mapigo ya muziki katika ushairi. Mtunzi hutumia mbinu hii kwa lengo la kusisitiza jambo Fulani. Mfano katika ubeti wa 151;
               Na kula shurutiwa sharutiwe jazaa kwima;
Pia neno thama limejitokeza mara nyingi katika beti mbalimbali, mfano ubeti 26 na 30.
  1. Mazida
Ni mbinu ya urefushaji wa maneno ili kuleta urari wa mizani katika mshoshoro. Mtunzi wa mashairi hufanya hivyo kwa nia ya kusawazisha mizani ya mishororo yote katika ubeti 214, 221,263,271,274,339 kwa mfano ubeti 274 neno kulolani badala ya kulola; ubeti 271 neno mipotofu badala ya potofu.
  1. Inkisari
Hii ni mbinu ya ufupishaji wa maneno ambayo mtunzi huitumia kwa lengo la kuleta urari wa mizani katika mshororo. Hapa silabi au mizani katika neno hufupishwa. Katika utenzi huu kuna matumizi makubwa ya mbinu hii, aghalabu utenzi mzima umesheni mbinu hii. Mfano ubeti 21: neno apokeo badala ya alipopata ubeti wa 24 neno atukule badala ya alichukua.
  1. Tabdila
Ni mbinu katika ushairi ambayo mshairi hubadilisha sauti Fulani katika neno ili kuleta uwiano Fulani, hususani mwishoni mwa kipande cha mshororo. Lengo ni kupata kina kifaacho. Mfano ubeti wa 5, 30, 41, 42, 200 na 216. Katika ubeti 5; neno Adama kutoka neno Adam, ubeti 42; neno dama kutoka neno damu.
Mbinu nyingine ni:
  • Fomula na Topo:
Fomula ni kigezo cha usimulizi wa tungo yoyote. Utendi simulizi hutungwa papo kwa hapo mtunzi anaimba kwa kutumia vipande vya sentensi vilivyomo katika jadi ya ushairi huo ambao huitwa fomula huku akipanga upya mawazo na matukio ya kijadi yaitwayo topos. Hivyo haimpasi mtunzi kukariri maneno ya utenzi wote, bali hujifunza tu fomula na topo za jadi zilizomo katika hazina ya fasihi ya jamii yake na kuzitumia kutunga utenzi wake wakati akiteza. Hii hupelekea hadi mtendi akaimba hata zaidi ya maneno 10,000 kwa mfululizo bila kuishiwa au kusahau.
Hii inaashiria kuwa msingi wake ni kanuni ya kurudiarudia vina mizani na usambamba. Katika kasida hii pia tumeona huo urudiajirudiaji mkubwa wa fomula na topo. Mfano sifa zinazorudiwarudiwa za Mtume Muhammad. Hali kadhalika topo kadhaa au vituko vina marudiorudio, kwa mfano
Ø  Usambamba
Ni mbinu ya kurudiarudia na kuambatanisha mistari, vipande vya mstari au sentensi zenye kufanana au kukinzana kimuundo au kimaana, mtunzi hutumia dhana mbili ambazo zinakinzana kimaana, lengo kuu ni kusisitiza ujumbe. Katika utendi huu mbinu hii imetumika sana, mfano kuna usambamba wa kimaana,kidhamira,kiusawe na kisintaksia.
Mathalani katika ubeti wa 1 katika utangulizi kuna usambamba wa kimaana wa majina ya Mwenyezi Mungu: ar-Rahaman na ar-Rahima
                       Naanza kwa jinale Bismillahi lenye adhama
                       Na ar-Rahamani Muwawazi na ar-Rahima
                    (Maana yake ni kuwa M/Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu)
Usambamba mwingine ni wa kimuundo unapatikana katika beti zifuatazo:
  • 154      Likabubujisha vula kuu siku sabaa
            Wingu shushizalo pambiloza waliko ama
  • 155      Kalomba iwingu ikandoka kisa kulomba
                         Na pa wenye nyocha papishapo ziriba thama
  • 156       Na watu wakaja kushitaki shida ya wingu
                         Na mivula kuu shida lake laudhi anama
  • 157       Kalomba iwingu ikandoka kisa kulomba
                         Vula ya kulomba kunukakwe swifu alima
  • 158       Vula kakasati ikakata mato kutola
                          Zitongoji zote na kabila fufiwa vyema
Usambamba huu unawez kutupatia kisa au ngano inayoweza kusimuliza hivi:
Paliondokea mwarabu mmoja katika mji wa Madina aliyemwomba Mtume(S.A.W) aombe kwa ajili ya kupata mvua katika mji huo wa Madina ambao ulikumbwa na ukame kwa muda mrefu. Mtume aliomba sana na sala yake ikajibiwa na Mwenyezi Mungu. Mvua kubwa ilinyesha kwa muda wa siku saba, kama ilivyo tabia ya mwanadamu ya kutokuridhika wakaona mvua ile inawakera sana hivyo basi Mtume Muhammad akaomba tena mvua ikaisha. Baada ya mvua kuisha nchi yote na vitongoji vyake vikawa vinavutia kwa madhari nzuri ya chanikiwiti na uhai ukarejea tena, wakaishi kwa raha mustarehe.”

B: KIGEZO CHA UREFU
Hiki ni miongoni mwa vigezo alivyovitumia Finnegan kupambanua tendi. Anasema utendi ni lazima uwe na urefu lakini hajasema kiwango hicho cha urefu ama kuwe na beti kiasi gani na idadi ya mistari katika utendi mzima. Kwa kutumia kigezo hiki, tunaona kuwa utendi wa Hamziyyah una urefu wa kutosha kwani una beti 449.

C: KISA
Finnegan anasema utendi lazima uwe ni utungo mmoja. Usiwe ni mkusanyiko wa tungo unohusu visa mbalimbali ambavyo yawezekana havihusiani. Katika utendi huu kisa kinachosimuliwa ni cha Mtume Muhammad kuanzia kuzaliwa kwake, utoto wake, kupewa utume, harakati za kueneza uislamu hadi kifo chake. Kwa maana hiyo basi, ni kisa kinachojitosheleza na matukio yake yote yanawiana.

D: KUHUSU SHUJAA
Utendi wa Hamziyyah unatimiza kigezo hiki sababu kisa kinachosimuliwa kinahusu kuzaliwa shujaa Mtume Muhammad. Kuzaliwa kwake kuliambatana na miujiza mingi mfano ubeti wa 13-18 na 58-61. Tunaoneshwa masahibu aliyokumbana nayo katika kueneza uislamu Makka mfano ubeti wa 82-96 na 104-119. Halikadhalika tunaoneshwa safari zake za kwenda Israa na Miraji: mfano ubeti 75-81, kutoka Makka kwenda Madina ubeti 68-74. Vile vile tunaoneshwa uongozi wake ulivyokuwa mfano ubeti wa 58-61. Hatimaye tunaoneshwa kifo chake.
Kutokana na vidokezo hivyo ni wazi kuwa yaliyomo katika utendi huu ni mambo yanayomuhusu shujaa Muhammad. Hivyo utendi huu umekidhi kigezo cha Finnegan kwamba utendi ueleze mambo yanayohusu shujaa.

Ruwaza ya Shujaa
Shujaa wa utendi huu ni Mtume Muhammad ambaye anaingia katika ruwaza ya shujaa ya Campbell ya mwaka 1956, ambapo shujaa wa utendi huu anakuwa na sifa zifuatazo;
  • Shujaa ni wa tabaka la juu
  • Kuzaliwa kwa shujaa kunaambatana na matatizo na misukisuko kwa mfano ubeti 12-17.
  • Kuzaliwa kwake inakua ni tishio kwa jamii iliyokuwepo kabla ya kuzaliwa kwake.
  • Shujaa ananyonyeshwa na mwanamke wa hali ya chini mfano katika ubeti wa 32-33
  • Shujaa anakuwa na kuwatafuta wazazi wake.
  • Shujaa anaanza harakati za kutetea dini y a Uislamu.
  • Mwishoni anafanikiwa na kushika nafasi ya juu, mfano beti 252-281

Fomula ya Bowra ya e=m+ms (U=V+M)
Fomula hii nayo imejitokeza katika utendi huu
U=utendi, vigezo vyote vya kiutendi vimejitokeza katika utendi huu
M=muziki, utendi wenyewe unaimbika moja kwa moja kwani ni kasida.
V=vita, masuala ya vita yamezungumzwa katika kutetea dini ya Uislamu mfano ubeti 262-276 Mtume ameonekana akipigana vita vya Badri na Hunaini.

Fomula simulizi
Pia hii imejitokeza katika utendi huu. Hii ni kuthibitisha kuwa utendi huu umetokana na usimulizi, unaanza kwa dua ya ufunguzi na kufunga kwa dua. Pia urudiaji rudiaji wa maneno kama tulivyoonyesha katika takriri ni uthibitisho kuwa ni utendi uliotokana na simulizi.
Kwa kuwa utendi huu ni utendi wa Kiswahili shujaa wa utendi huu anafuata sifa za shujaa wa waswahili ambazo ni:
  • Shujaa anatoka tabaka la juu
  • Ni jasiri
  • Ana uwongofu ‘baraka’
  • Ana jaala ya Mwenyezi Mungu
  • Anapata msaada wa Allah
  • Anaungwa mkono na watu
Kwa mtazamo wetu tumeona kwamba sifa ya sihiri na udhaifu wa shujaa havijajitokeza katika utendi huu.
Utendi na historia
Halikadhalika utendi wa Hamziyyah unaweza kuwa wa kihistoria kwa sababu ya kumuelezea Mtume Muhammad  na kuasisiwa kwa dini ya kiislamu ambaye anasadikika kihistoria alipata kuishi.
Utendi na utaifa
Vile vile unaweza kuwa ni utendi wa utaifa kwa sababu maudhui mengi katika utendi huu yamejikita katika kuelezea kanuni, mila na desturi za kuanzishwa kwa dola ya kiislamu huko Makka na Madina.
Dini na kiyama
Pia utendi huu wa Hamziyyah unahusu maswala ya dini na kiama mfano safari ya Mtume Muhammad kwenda Miraji (Mbinguni) na watu walioahidiwa kuingia peponi yanadhihirisha athari ya dini ya waislamu katika utendi huu.
Kuchanganya Tanzu
Tumeona katika utenzi huu mwandishi amechanganya tanzu mbali mbali. Kuna hadithi na baadhi ya aya za kurani alizotumia katika utendi huu. Mfano:
  • Kisa cha Isra na Miraji katika ubeti wa 68 -74 kimechukuliwa katika kurani tukufu 17:1, 2:144, 149, 150, 191 na 217.
  • Vita vya Badri na Hunaini vinapatikana katika kurani tukufu sura ya 26:18, 30-31, 63 na 40:33
  • Kupasuliwa kwa kifua na moyo sura ya 50: 14
Pia utendi huu ni wa kisira unatoa wasifu wa mtume tangu kuzaliwa kwake, misukosuko aliyoipata hadi kifo chake.
Muktadha wa utendi huu ni kati ya mwaka 1500-1750 BK kilikua ni kipindi cha misuko suko ya mapambano kati ya wenyeji(waislamu) na wavamizi wa kireno (wakristo). Hivyo utendi huu ulilenga kuhamasisha jamii ya waswahili kupambana na uvamizi wa kireno ambao ulisadikika kumiliki misingi ya uzalishaji mali.

MAUDHUI
Kwa ujumla maudhui yanayopatikana katika utenzi huu ni haya yafuatayo:
Falsafa ya maisha- Maisha ni mapambano, sifa za mtume Muhammad kabla hajazaliwa, baada ya kuzaliwa na misuko suko aliyoipata hadi kufa kwake ni dhahiri kuwa maisha ndivyo yalivyo hasa kwa mashujaa wengi.
Utetezi na ufafanuzi wa dini ya kiislamu- Dini ya kiislamu imeelezwa kwa kiasi kikubwa katika utenzi huu. Mtunzi amelibainisha hilo kwa kumsawiri shujaa Muhammad akipambana na wote waliokuwa wakiipinga na kwenda kinyume na dini ya kiislamu mfano Manasara na Mayahudi waliokuwa na dhana potofu ya utatu katika umoja. Kwa hiyo utendi umeonyesha dharau kwa dini hizo na kuwahimiza waislamu wabakie katika uislamu wao. Ndio maana kulikuwa na mapambano ya mtume dhidi ya maadui zake, shida na mateso vilitokea na baadae uislamu ulishinda.
Pia utenzi huu unatuonyesha imani kubwa katika dini ya kiislamu kutokana na miujiza mbali mbali aliyokuwa anaionyesha Mtume Muhammad. Miujiza mingine ilihusisha uwezo wa wanyama kuwa na akili na kusema na kutenda zaidi ya binadamu mfano ndovu, ngamia, mijusi. Kwa kawaida wanyama kama hawa hutumika katika utendi ili kumjenga shujaa.

Matumizi ya namba
Katika utendi huu kuna matumizi ya namba tano na namba saba, mfano;
  • Maadui watano wa mfalme waliokufa kutokana na maradhi yasiyotibika ubeti wa 88-94
  • Waislamu wema watano ubeti wa 95-99
  • Mvua kubwa ilinyesha kwa muda wa siku saba ubeti wa 154-159
Namba hizi kwa jamii ya waswahili zina maana, namba tano ina maana ya swala tano zinazotekelezwa na waislamu kila siku na namba saba maana yake ni mbingu saba.
Aidha kuna kufanana kwa maudhui ya utendi huu na tendi nyingine au vitabu vingine mfano;
  • Kurani tukufu
  • Tendi zilizoandikwa zenye maudhui kama hayo ni pamoja na Utenzi wa Tambuka, Siri’I asilali, Ras’I Ghul na Inkishafi.
  • Vile vile utendi huu umepelekea kuibuka kwa utendi nyingine kimaudhui na kifani mfano Utenzi wa Inkishafi.
MOTIFU
Hiki ni kipengele kingine kinachojitokeza katika utendi huu. Motifu ni kipengele cha kifani na kimaudhui kinachojirudia rudia tungo mbali mbali. Motifu zilizojitokeza katika utendi huu ni hizi zifuatazo;
Motifu ya kuteseka kwa mitume na manabii. Motifu hii inaonekana kujitokeza sana kwa mitume katika harakati za kueneza dini, mfano Muhammad katika utendi huu ameteswa, amepigwa, na hata kupingwa na makureshi wakati wa kueneza dini ya kiislamu. Hali hii imeendana na mateso waliyoyapata Manabii na Mitume wengine katika historia kama Mussa, Yesu (Issa), Nuhu na wengineo.
Motifu ya watoto kunyonyeshwa na wazazi wasio wao. Katika utendi huu shujaa Muhammad amenyonyeshwa na Bi Halima mwanamke wa shamba, kwa waarabu hii ilikua ndiyo desturi yao lakini kiutendi hali hii huijenga ruwaza ya shujaa.
Motifu ya safari. Hii ni motifu nyingine inayojitokeza katika utenzi huu. Muhammad anasafiri kwanza kutoka Makka kwenda Yerusalem na Mbinguni. Pili anasafiri kutoka Makka kwenda Madina.
Motifu ya ukarimu yaani shujaa kupewa mali au nyumba. Katika utendi huu Muhammad anakirimiwa na waislamu wa Madina pindi alipohama kutoka Makka kwenda Madina kama ilivyojitokeza katika tendi za Ras’IGhul na Nyakiiru Kibi.
Motifu ya ukatili wa wanawake waliokataa kumnyonyesha mtume, mwanamke mbeba kuni na mwanamke aliyeweka sumu katika nyama ya mtume.
Motifu ya mtoto wa ajabu. Nayo inajitokeza katika utendi huu. Miujiza iliyojitokeza kabla na baada ya kuzaliwa kwake inadhihirisha ushujaa wa Muhammad kutokana na uajabu alioambatana nao.

Mchango wa Wanawake katika kumjenga shujaa wa utendi;
  • Amina huyu ni mama yake ambaye (siku za uhai wake) alikuwa naye sambamba tangu kuzaliwa.
  • Khadija na wake wenza walimpa moyo na kumliwaza dhidi ya maswahiba aliyokuwa akiyapata, pia walikuwa tayari kuvumilia ugumu wa maisha aliokumbana nao shujaa Muhammad (S.A.W)
  • Wengine ni Zainab Bint Ali-Harith beti 116-117, Umm Ma Abad beti 167 na Ummy Jamil ubeti 113-115.
Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kwamba utenzi wa hamziyyah licha ya kutoa maadili ya dini ya kiislamu una mchango mkubwa katika ushairi wa Kiswahili kwani ni mojawapo ya utenzi wa awali unaohusu matukio ya Uarabuni na Mashariki ya Kati wakati wa kuasisiwa kwa uislamu na ni miongoni mwa kazi za mwanzo zilizotafsiriwa katika lugha ya Kiswahili, pia uthibitisho kuwa Afrika ina tendi toka zamani na ni hifadhi ya lugha ya kale. Vile vileumepelekea kupatikana kwa bahari ya Hamziyyah katika ushairi na hivyo kuonesha uhusiano wa ukaribu uliokuwepi kati ya Afrika Mashariki na Afrika ya Kaskazini.
 


                                                                 MAREJELEO

Finnegan, R (1970). Oral Literature in Africa. The Clarendon Press. Oxford.
Mkelle, M.B (1976). “Hamziyya, the oldest Swahili Translation,” Kiswahili Vol.A6/1, kur                                  
                      71-75.
Mulokozi M.M (1989). ‘Tanzu za Fasihi Simulizi’ katika Mulika na. 21, Dar es Salaam. 
                        TUKI
Mulokozi, M. M. na T S Y Sengo (1995). History of Kiswahili Poetry: A.D 1000-2000.
                        I.K.R, University of Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M (1996) Fasihi ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania.
Mulokozi, M.M (2002) The African Epic Contoversy:Historical, Philosophical and Aesthetic
                          Persipectives on Epic Poetry and Performance, Dar es Salaam. Mkuki na    
                          Nyota Publishers.
Mutiso, K (2005). Utenzi wa Hamziyya. Dar es Salaam: TUKI
Sengo,T.S.Y (1976). Shabaan Robert: Uhakiki na Maandishi yake. Longman, Dar es Salaam.
Wamitila, K.W (2003) Kamusi ya Fasihi:Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Publications
                        Ltd.




No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny