Flower
Flower

Wednesday, January 29, 2020

Sintaksia kwa kutumia sababu za kiisimu


1.0  Utangulizi 
Katika kujadili, tumegawa kazi katika sehemu kuu tatu ambapo katika utangulizi tunaangalia fasili na ufafanuzi wa dhana muhimu, yaani isimu, kategoria na sintaksia kwa kuwarejelea wataalamu mbalimbali na sehemu ya pili ni kiini cha swali ambapo tutajadili kategoria za kisintaksia kwa ufupi na kisha kuangalia kwa undani sababu zinazothibitisha au kubainisha uwepo wa kategoria hizo kwa mujibu wa watalamu mbalimbali. Sambamba na hilo tutaonesha utoshelevu na upungufu wa sababu hizo. Sehemu ya mwisho ya kazi hii ni hitimisho ambapo tutaonesha umuhimu wa kuwa na kategoria za kisintaksia katika lugha. 

2.0: FASILI YA DHANA ZA ISIMU, SINTAKSIA, KATEGORIA, LEKSIMU NA KIRAI 

2.1 Dhana ya Isimu 
Mgullu (1999) anasema kuwa isimu ni taaluma ambayo hushughulikia uchunguzi wa lugha mbalimbali kwa kutumia misingi ya kisayansi, kutokana na huo mkabala wa kisayansi katika uchunguzi wake ndipo isimu aghalabu huitwa sayansi ya lugha.  

Ndalu na Wenzake (2014) wanaeleza kuwa isimu ni taaluma ambayo inachunguza lugha kisayansi. Wanaeleza aina za isimu ni kama vile isimu nafsi, isimu jamii, isimu uamilifu, isimu amali, isimu matumizi, na isimu historia. 

abwe na Karanja (2012) wanaeleza kuwa isimu ni taaluma inayochunguza lugha ya mwanadamu kisayansi, wanaendelea kueleza kuwa isimu ni sayansi kwa sababu hufuata mbinu za msingi za utafiti wa kisayansi mbinu hizo huhusisha sifa kama vile uchunguzi uliothibitiwa, uundaji wa haipothesia, uchunguzi ujumlishi, utabiri, majaribio na uthibitisho pamoja na urekebishaji au ukataaji wa haipothesia. 

Hivyo, isimu ni taaluma inayochunguza na kuchambua lugha kwa kutumia misingi ya kisayansi. Kwa msingi huo isimu ni sayansi ya folonojia, sintaksia, semantiki na mofolojia katika lugha. 

2.2 Dhana ya Sintaksia

Tallerman (2011) anaeleza kuwa sintaksia ina maana ya uundaji wa sentensi, yaani namma ambavyo kundi la maneno huweza kuwekwa pamoja na kuunda sentensi au tungo. Anaendelea kueleza kuwa baadhi ya wataalamu hutumia istilahi sarufi wakiamanisha sintaksia lakini yeye anakanusha dai hili kwa kuthibitisha kuwa wakati ambapo sintaksia inajishugulisha na uundaji wa sentensi au tungo sarufi yenyewe inashugulikia taaluma zaidi ya moja yaani maumbo ya maneno, uundaji wa tungo, uchunguzi wa sauti na maana za maneno kulingana na muktadha hivyo sintaksia ni sehemu tu mojawapo ya sarufi ila siyo sarufi. 

Habwe na Karanja (2012) wanaeleza kuwa sintaksia ni utanzu wa ismu unaoshughulikia muundo wa sentensi na elementi nyingine zinazounda sentensi kama vile kategoria za maneno, vikundi na vishazi. 

Massamba na Wenzake (2009) wanaeleza kuwa sintaksia ni utanzu wa sarufi unaojihusisha na uchunguzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipashio vyake. Pia, wanaendelea kusema kuwa katika utanzu huu, kinachochunguzwa ni zile sheria au kanuni ambazo hazina budi kufatwa katika kuyapanga maneno ya lugha katika mfuatano (neno moja baada ya jingine) kwa namna ambayo itafanya maneno hayo yalete maana inayokubalika na kueleweka katika lugha husika. 

Kwa ujumla, kulingana na fasili za wataalamu mbalimbali, katika Makala haya  sintaksia inafasiliwa kama taaluma inyochunguza miundo ya tungo na uundaji huo huenda sambamba na kanuni mbalimbali za lugha inayotawala miundo hiyo, tungo zinazoundwa huanzia ngazi ya neno mfano baba, kirai  mfano baba yake , kishazi kinaweza kuwa kishazi huru ambacho huwa na maana iliyokamilika mfano Juma analia au kishazi tegemezi ambacho hutawaliwa na kitenzi ambacho hakitoi maana iliyokamilika mpaka kiandamane na kishazi huru mfano binti uliyempokea jana na kiwango cha mwisho katika muundo wa tungo ni sentensi mfano Baba na Babu wanapunga upepo ufukweni mwa bahari. 

2.3 Dhana ya Kategoria 
Khamisi na Kiango (2002) wanasema kuwa dhana ya kategoria ilitumiwa na wanasarufi mapokeo kwa namna tofauti na inavyotumiwa na wanasarufi mamboleo, neno kategoria kama lilivyotumika katika sarufi mapokeo ya akina Aristolte imetokana na neno la kigiriki na kufasiliwa kama uarifu (predication). Wanamapokeo walitumia dhana ya kategoria kuwa ni sifa bainishi zinazoambatana au zinazoambikwa kwenye aina za maneno, kwa mfano nafsi, idadi, kauli, njeo, ngeli, dhamira na uhusika. Kategoria kwa mtazamo wa kisarufi mamboleo ni jamii, seti, kundi au makundi ya maneno yanayofanya kazi ya kufanana. Aidha darajia yoyote ya vipashio inayotambuliwa katika uchambuzi fulani wa lugha huitwa kategoria. 

Matinde (2012) anaeleza kuwa kategoria za kisarufi ni maumbo au vipashio vya kisarufi vinavyotumika kubainisha mahusiano ya kategoria za maneno katika sentensi. Uamilifu wa kategoria za kisarufi ni kupatanisha viambishi awali vya kitenzi, nomino, kiwakilishi na kivumishi ambavyo hutokea katika kirai, kishazi au sentensi. 

Hivyo, kategoria ni jumla ya maumbo au vipashio vingine ambavyo huchangia sifa fualani, maumbo hayo yanaweza kuwa katika kiwango kimoja cha neno au zaidi ambayo huwa na dhima Fulani katika tungo mfano, 
i. Juma anakula neno “Juma” ni nomino ambayo inafanya kazi ya kiima katika sentensi. ii. Mtoto mdogo neno “mdogo” ni kivumishi ambacho kina sifa ya kuambatanishwa na kiambishi cha upatanisho cha umoja M- pia kivumishi mdogo kina dhima ya kufafanua au kukumbusha nomino. 

3.0  Kategoria za Kisintaksia 
 Kategoria za kisintaksia zimegawanyika katika viwango au darajia mbili   ambapo kuna kategoria katika kiwango cha neno au kileksika na kategoria katika kiwango cha kikundi au kirai(O’Grady 1996). 

3.1  Kategoria za Kileksika 
Hizi ni kategoria za kiwango cha neno moja moja mfano nomino, kitenzi, kivumishi, na kiunganishi, wataalmu mbalimbali wametofautiana katika mitazamo kuhusiana na idadi na istilahi za kategoria hizi. Kuna wanaotaja kategoria nne kama O’ Grady (1996) ilihali Nkwera na Kapinga wanataja kategoria saba huku Kihore (1996) akitaja nane. Kwa kuangalia kategoria mbalimbali ambazo zimetolewa na wataalamu hawa kwa pamoja zinauunda au zinapelekea uwepo wa kategoria tisa za kileksika ambazo ni Nomino, kitenzi, kivumishi, kihusishi, kielezi, kiwakilishi, kiunganishi, kibainishi, kiingizi au kihisishi. 

3.2  Kategoria za Virai 
O’ Grady (1996) anaeleza kuwa maneno ambayo yanahusiana huwekwa pamoja ili kuunda kikundi cha maneno, mfano nomino inaweza kuhusishwa na kivumishi na ikatupatia kikundi nomino au kitenzi kinaweza kuhusishwa na nomino tukapata kikundi kitenzi, vikundi vya mneno kama hivo ndivyo hujulikana kama virai.  


Kama ilivyokuwa katika kategoria za kileksika pia katika kategoria za kirai au kikundi wataalamu hutofautiana katika idadi, fasili na istilahi ya kirai ambapo katika idadi Massamba na Wenzake (2012) wamebainisha aina tano za virai ambazo ni virai nomino, virai vitenzi, virai vivumishi, virai vielezi na virai viunganishi ilihali Matinde (2012) amebainisha aina sita za virai ambazo ni kirai nomino, kirai kivumishi, kirai kitenzi, kirai kielezi, kirai kihusishi na kirai kiunganishi. Kwa upande wa istilahi wataalamu pia wanatofautiana ambapo Nkwera (1978), Matei (2008) na Massamba na Wenzake (2009) wanaita kirai na Mdee (2007) yeye anaita kikundi. Pia, katika kufasili dhana ya kirai wataalamu wanatofautiana katika fasili zao, fasili zifuatazo zilizotolewa na wataalamu tofautitofauti zinadhihirisha utofauti huu wa fasili kama ifuatavyo, 

Matei (2014) anaeleza kuwa kirai ni fungu la maneno ambalo hufanya kazi kama neno moja na huwa na uamilifu sawa. Anaendelea kusema kuwa kirai hudokeza maana lakini maana hiyo si kamili mfano, 
Pale chini ya mti  a) Mwenyebaka jeusi usoni 
Tungo hizi bado zinahitaji kuongezewa vipashio vingine ili ziweze kutoa maana iliyokamilika. 
Massamba na Wenzake (2009) wanaeleza kuwa kirai ni kipashio cha kimuundo chenye neno moja au zaidi lakini ambacho hakina uhusiano wa kiima na kiarifu. 
Kutokana na tafsiri hizo kirai kinaweza kufasiliwa kuwa ni kipashio cha kimuundo chenye neno moja au zaidi ambacho kinaweza kuwa kiima au kiarifu pia ni kikubwa kuliko neno na kidogo kuliko kishazi au sentensi.  O’ Grady (1996) anasema kuwa kirai huundwa na sehemu kuu mbili ambazo ni neno kuu ambalo hutawala kirai chote na kijalizo ambacho hukamilisha taarifa za neno kuu mfano katika tungo: amepanda gari neno kuu ni amepanda na kijalizo ni gari. 

4.0  USHAHIDI WA KUWEPO KWA KATEGORIA ZA KILEKSIKA NA VIRAI  

4.1  Ushahidi wa Kuwepo kwa Kategoria za Kileksika 
Kipengele hiki kinajadili ushahidi wa kuwepo kwa kategoria za kileksika, ushahidi huo ni pamoja na;   
4.1.1  Ushahidi wa Kisintaksia  
Rubanza (2003) anaeleza kuwa kuna kanuni mbili zinazojipambanua ambazo ni mfuatano wa maneno kimlalo (usilisila) na kuhusiana na kutofautiana kwa maneno kiwima. Katika sentensi maneno hayafatani kiholela tu bali kuna utaratibu wa mfuatano wa maneno hayo ambayo kwayo yana aina maalum kwa mfano nomino inaweza kufuatwa na kivumishi au kionyeshi halafu kitenzi na kielezi au nomino nyingine. Hivyo basi, mfuatano wa usilisila unatuwezesha kufasili aina ya neno kwa ubayana zaidi kuliko kufasili aina ya neno hilo kwa msingi wa nadharia ya mtajo ambayo inahusisha neno (yaani lugha). Kwa mtazamo wa mfuatano wa maneno kimlalo tunaweza kufasili nomino kama neno linalofuatwa na ama kivumishi na/ au kionyeshi ambacho pia kinafuatwa na kitenzi ambacho idadi yake ina upatanisho wa kisarufi yaani inatokana na nomino tangulizi kwa mfano, 
i. Mtoto huyu anasoma vizuri. ii. N+V+T+E. 
Mfuatano uonyeshwao hapo juu ni wa nomino kufuatwa na kivumishi ambacho nacho kinafuatwa na kitenzi na mwisho kitenzi kinafuatwa na kielezi.  
O’ Grady (1996) anaeleza kuwa katika lugha ya Kingereza nomino huweza kutokea pamoja na vionyeshi pia vitenzi huweza kutokea pamoja na vitenzi visaidizi. Mfano, 
i. Nomino: a car, the wheat. ii. Kitenzi: may go, will stay. 

Utoshelevu wa ushahidi huu, unatusaidia kubaini kategoria za maneno kwa kuangalia mfuatano sahihi wa maneno katika tungo kwani maneno hayatokei kiholela holela kwa mfano, nomino kamwe haiwezi kufuatana na kiwakilishi isipokua huwa vinabadilishana nafasi (Rubanza 2003). 
Mapungufu ya ushahidi huu, ni kuwa baadhi ya mifuatano katika tungo haikubaliki. Mfano katika lugha ya Kingereza kitenzi kikuu hakiwezi kuambatana na kionyeshi (O’ Grady 1996) mfano *the destroy pia nomino haiwezi kutokea pamoja na kitenzi kisaidizi mfano *will destruction. Vivyo hivyo, hata katika lugha ya Kiswahili nomino haiwezi kutokea pamoja na kiwakilishi mfano * Vesco huyu. 

4.1.2  Ushahidi wa Kisemantiki 
 O’ Grady (1996) anasema kuwa kigezo kinachotumika hapa ni maana kwa maneno mengine tunajua kuwa neno fulani lipo katika kategoria fulani kutokana na linavyofasiliwa. Kwa mfano; 

i. Nomino ni maneno yanayo taja vitu mfano, Masatu, Neema na Tanzania. ii. Vitenzi ni maneno yanayotaja vitendo mfano, cheza na piga. iii. Kielezi ni maneno ambayo hueleza namna tendo linavyofanyika mfano, vizuri, kila siku na sana.  
Rubanza (2003) anatumia kigezo cha utata kuthibitisha uwepo wa kategoria za kileksika  ambapo anaeleza Kuwa kuna aina mbili za utata; utata wa kileksika na utata wa kimuundo. Utata wa kileksika unajibainisha katika neno kuwa na maana zaidi ya moja. Kwa mfano neno chungu, lina maana ambazo hupelekea kuwepo kwa kategoria tofautitofauti. 
a) Mdudu   nomino { N } b) Ladha    kivumishi {V} c) Kifaa    Nomino  {N} 
Utata wa muundo wa neno husika, anafafanua kuwa neno wafanyakazi na wafanya kazi linategemea  tafsiri inayopewa neno hilo husika ama kama nomino ikiwa na maana ya watu wanaofanya kazi au kama kitenzi wafanya pamoja na nomino ya kazi. Utoshelevu wa ushahidi huu, 
i. Hutusaidia kutambua kategoria Fulani ya neno kutokana na linavyo fasiliwa. Mfano neno anacheza linafasiliwa kama tendo ambalo linatupatia kategoria ya kitenzi na neno mzuri linadokeza sifa ambalo pia linatupatia kategoria ya kivumishi. ii. Suala la utata katika neno husika linatusaidia kupata kategoria zaidi ya moja kutokana na neno moja. Mfano neno ua linatupatia kategoria ya kitenzi endapo litatumika kama kitendo cha kutoa uhai na kama nomino iwapo litatumika kama mmea. 
Mapungufu ya ushahidi huu ni vigumu kubainisha kategoria kutokana na maneno yenye utata bila kuangalia nafasi ya neno hilo katika tungo au muktadha wa matumizi. Mfano katika neno pamba linaposimama peke yake linaleta utata kwani mtu huweza kujiuliza neno hili limetumika kama kitenzi au nomino lakini katika sentensi, Neema anapamba ukuta ni rahisi kusema kuwa neno pamba ni kitenzi kutokana na nafasi yake katika tungo. 

4.1.3  Ushahidi wa Kimofolojia 
Kigezo kinachotumika katika ushahidi huu ni cha uambishaji. Vivumishi fulani vya kisarufi huweza kuambikwa kwenye maneno yaliyo katika kategoria fulani tu na haviwezi kuambikwa katika maneno ya kategoria tofauti. O’ Grady (1996) anasema kuwa katika lugha ya Kingereza kiambishi cha wingi “s” huambikwa kwenye maneno ya kategoria ya nomino mfano books, cats, lakes. Kwa upande wa kiambishi cha njeo iliyopita kiambishi kama “ed” cha hali ya kuendelea huambikwa kwenye vitenzi mfano, supported, provided, na viambishi vya ukadirifu -er, -est huambikwa kwenye vivumishi mfano, taller na tallest. 

Rubanza (2003) anatumia pia kigezo cha uambatizi, yeye anaelezea zaidi kwa upande wa lugha ya Kiswahili ambapo anafafanua kuwa viambishi vya idadi na ngeli huambikwa katika nomino na vivumishi, mfano Mtoto na Watoto (M- na wa- ni viambisha vya idadi) viambishi vya njeo, kauli, na ukanushi huambikwa katika vitenzi mfano anapikia ambapo kiambishi “na” huonyesha njeo na kiambishi i kinaonesha kauli ya kutendea. Anaendelea kusema kuwa kutokana na ufafanuzi huu kategoria za maneno zinaweza kufasiliwa kwa namna tofautitofauti. Hivyo anaeleza kuwa nomino ni aina ya neno inayoambatana na ngeli ambayo nayo inadhihilika kwa mofimu idadi-umoja na wingi. Kitenzi ni aina ya neno ambalo linaambatana na viambishi vya kauli, njeo na nafsi. Kivumishi ni aina ya neno ambalo huambatana na viambishi vya ngeli na idadi (Rubanza 2003).  

Utoshelevu wa ushahidi huu ni kuwa unaonyesha mchango wa viambishi katika kuunda kategoria za kisintaksia mfano viambishi vya idadi na ngeli vinatupatia kategoria ya nomino. Katika lugha ya Kiingereza mofu ya –er na –est hutupatia kategoria za vivumishi. Na kiambishi “s” hutusaidia kupata kategoria ya nomino kama tulivyoona hapo juu. 
Mapungufu ya ushahidi huu, si kila neno linaweza kupokea viambishi katika lugha mfano katika lugha ya Kiswahili maneno kama vile na, kwa, na lakini hayawezi kuambikwa viambishi vyovyote. 

O’ Grady (1996) anathibitisha kuwa katika lugha ya Kingereza si kila vivumishi vinaweza kuambikwa viambishi vya ukamilifu kama vile *intelligenter na* beautifulest. Pia anaeleza kuwa baadhi ya nomino haziwezi kuambikwa viambishi vya ukamilifu kama vile moisture, bravery na knowledge. 

4.1.4  Ushahidi wa Kifonolojia  
Rubanza (2003) anaeleza kuwa ushahidi wa kifonolojia katika Kiswahili hauna mifano mingi lakini upo. Neno moja ambalo ni bayana ni neno barabara neno hili lina maana mbili: (a) njia ndefu na pana (b) kama inavyotakiwa, sawasawa. Maana ya kwanza kwa kutegemea namna ya utamkaji ina maana kuwa neno hilo ni nomino wakati maana ya pili inajidhihirisha kama kivumishi ama kielezi. Hivyo kigezo kinachotumika katika ushahidi huu ni uwekaji wa mkazo au shadda katika kutamka neno fulani. Neno moja linaweza kuwa katika kategoria tofauti tofauti kutokana na uwekaji wa mkazo. 

Utoshelevu wa ushahidi huu, husaidia kufahamu namna matamshi yanavyopelekea kuwepo kwa kategoria mbalimbali za maneno. Hii ina maana kuwa sauti moja inapotamkwa kwa namna tofauti huweza kuunda maana tofauti na hivyo kuwekwa katika kategoria tofauti kwa mfano katika Kingereza we need to import new knowledge, we need an import of new technology katika tungo hizo sauti zilizopigiwa mstari zimepelekea uwepo wa kategoria ya kitenzi (T) na Nomino (N) ambazo zimetokana na mabadiliko ya uwekaji wa mkazo. 
Upungufu wa ushahidi huu, ushahidi huu umejikita zaidi katika lugha ya mazungumzo tu. Ambapo neno fulani husikika kuwa limewekewa mkazo sehemu fulani kutokana na neno linavyotamkwa. 

4.2  Ushahidi wa Kuwepo kwa Kategoria za Virai 
Sehemu hii inaangazia ushahidi unaothibitisha kuwepo kwa kategoria za virai kama ifuatavyo; 

4.2.1  Ushahidi wa Kisintaksia 
Rubanza (2003) anadokeza  kuwa kigezo kinachotumika ni kigezo cha mtawanyiko pia, nae O’ Grady (1996) anaeleza kuwa kuna majaribio matatu ambayo yanaweza kuthibitisha kuwepo kwa kirai katika tungo. 

Jaribio la kwanza ni jaribio la ubadala ambapo tuaangalia uwezekano wa kibadala kujaza nafasi inayojazwa na kirai mfano katika lugha ya Kiswahili, 
i. Neema atapika chakula leo usiku endapo Jane atafanya hivyo, atafanya hivyo ni kibadala cha atapika chakula leo usiku. Pia mfano katika lugha ya Kingereza, ii. The citizens rebelled after they discovered the truth. (They = the citizens). 

Jaribio la pili ni jaribio la kuhamisha ambalo linathibitisha kuwa kirai ni kipashio cha kisintaksia kwani kinaweza kuhamishwa kama kipashio kimoja na kupelekwa pengine mfano, 

i. Mchezo wa tenesi ni maarufu sana nchini Tanzania→ Nchini Tanzania mchezo wa tenesi ni maarufu sana. Pia mfano katika lugha Kingereza, ii. They stopped (pp at the corner)→ (pp at the corner), they stopped. 

Jaribio la tatu ni jaribio la uambatanishaji hili linahusu virai viunganishi mfano katika Kiswahili; 
Utoshelevu katika kigezo hiki, jaribio la uambatanishaji hutusaidia kupata tungo ndefu zaidi kupitia uunganishaji wa tungo zenye hadhi sawa kama tulivyo bainisha kaika tungo tajwa hapo juu pia, jaribio la ubadala linatusaidia kuepuka urudiaji wa tungo ileile katika sentensi moja mfano, Neema atapika chakula leo usiku endapo Jane atafanya hivyo, atafanya hivo ni kibadala cha atapika chakula leo usiku.  

Upungufu wa kigezo hiki, si kila kundi la maneno linaweza kuhamishwa na kuleta maana. Mfano Masatu anakula ugali wa dona huwezi kusema ugali wa dona anakula Masatu isipokuwa uhamishaji wa tungo ni lazima uzingatie sarufi ya lugha husika. 

4.2.2  Ushahidi wa Kisemantiki 
Rubanza (2003) anaeleza kuwa katika kategoria za virai kigezo kinachotumika ni kigezo cha utata ambapo kirai fulani kinaweza kuwa na tafsiri zaidi ya moja kutokana na uwezekano wa kufasiliwa kuwa na kategoria tofauti mfano, siku hizi simba wanaonekana bure kabisa.  

a. Tafsiri ya kwanza ni kikundi kivumishi maana yake ni si lolote na, b. Tafsiri ya pili ni kikundi kielezi maana yake ni bila kiingilio. 
Utoshelevu wa kigezo hiki utata hutusaidia kupata kategoria zaidi ya moja kutokana na tungo moja mfano katika tungo hali halali. 
a. Tafsiri ya kwanza ni kikundi nomino maana yake ni hali ambayo si haramu na, b. Tafsiri ya pili ni kikundi kitenzi maana yake hawezi kula wala kulala. 
Upungufu wa kigezo hiki, ni vigumu kubainisha kategoria moja kwa moja bila kuzingatia muktadha maalum wa matumizi kwa mfano tunaweza kusema kuwa tungo hali halali ina maana kuwa hawezi kula wala kulala iwapo tu tupo katika mazingira ya hosipitalini au kama kuna mtu anaumwa nakadhalika. 

4.2.3  Ushahidi wa Kimofolojia  
 O’ Grady (1996) anaeleza kuwa kigezo kinachotumika katika mofolojia ni kigezo cha mofu milikishi “s” ambayo katika lugha ya Kingereza hupachikwa katika kirai nomino, ikiwa itapachikwa mahali ambapo itaitenga nomino hiyo huo muundo utakuwa haukubaliki mfano katika tungo mother’s milk tungo hii ndiyo sahihi, *Mothers milk hii haikubaliki. 

Utoshelevu wa kigezo hiki, kinaonesha mchango wa viambishi katika kuunda tungo kubwa zaidi ya neno yaani kirai kwa mfano juma’s shoes mofu ‘s’imechangia kuunda kirai nomino. 
Upungufu wa kigezo hiki, baadhi ya lugha hazina mofu bayana kwaajili ya umilikishi mfano katika Kiswahili hatuna mofu zinazobainisha umilikishi moja kwa moja isipokuwa umilikishi huoneshwa na kategoria fulani hususani kivumishi kwa mfano mtoto wangu,wangu ni kivumishi cha umilikishi.  

5.0 Hitimisho 
Kwa ujumla, kulingana na ushahidi huo tuliojadili hapo juu ni dhahiri kuwa kategoria za kileksika na viri zipo ambazo ni nomino, kivumishi, kiwakilisi, kitenzi, kielezi, kihusishi, kiunganishi, kibainishi na kiingizi au kihisishi (kategoria za kileksika), kirai nomino, kirai kivumishi, kirai kitenzi, kirai kihusishi na kirai kielezi (kategoria za virai). Pia uanishaji wa kategoria za kisintaksia una umuhimu mkubwa katika lugha kwani kategoria zinazoundwa huwa na dhima mbalimbali katika tungo kwa mfano viwakilishi vina dhima ya kufanya kazi kama kiima au kuwakilisha nomino mfano yule anaimba na nomino hubeba upatanisho wa kisarufi,yaani nomino huweza kuingizwa katika ngeli kwa umbo la umoja na wingi na ndiyo huongeza aina zingine za maneno ili kupata upatanisho wa kisarufi mfano nomino inaweza kuteua kivumishi katika tungo mtoto mzuri au watoto wembamba. 
                                     


                                                                 MAREJELEO 
Habwe, J. & Karanja.  P. (2012).  Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers. 
Khamis, A. M. na Kiango, J. G. (2002). Uchanganuzi wa Lugha ya Kiswahili. Dar es Salaam: Chuo                                   Kikuu Huria Cha Tanzania.  
Massamba, D. P. B. na Wenzake (2009). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA): Sekondari 
                                 na vyuo. Dar es Salaam: TUKI. 
Matei, A. (2014). Darubini ya Sarufi Ufafanuzi Kamili wa Kiswahili.  Nairobi: Phoenix Publisher. 
Matinde, S. R. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia. Tanzania: Serengeti Educational                                             Publisher. 
Mdee, J. S. (2007). Sarufi ya Kiswahili: Sekondari na Vyuo. Dar eS Salaam: Dar es laam University                                      Press. 
Mgullu. S. R. (1999). Mtaala wa Isimu. Kenya:  Longhorn publishers Ltd.  
Ndalu, E. na wenzake (2014). Kamusi Teule ya Kiswahili Kilele cha lugha. Nairobi Kenya: East                                            African Educational Publishers Ltd.  
Nkwera, F. V. (1978). Conditions in Kiswahili. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 
O’ Grady, William. (1996). “Syntax the Analysis of Sentence Structureˮ katika O’ Grady na wenzake (wah.) (1996) (tol.3) Contemporary Linguistics: an Introduction, London: Longman Limited, Kur. 164-167. 
Rubanza, Y. I. (2003). Sarufi, Mtazamo wa Kimuundo. Dar es Salaam: Chuo Kikuu Huria cha                                                Tanzania. 
Tallerman. M. (2011). Understanding Syntax. London: Hodder Education. 

 a

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny