1.0 Utangulizi
Kazi
yetu imegawanyika katika sehemu kuu nne, ambazo ni utangulizi, kiini, hitimisho
na marejeleo. Katika sehemu ya kwanza ni utangulizi, ambapo tumejadili dhana ya
tafsiri kulingana na mawazo ya wataalamu mbalimbali, dhana hizo zimefuatiwa na
mawazo yetu juu ya dhana ya tafsiri, sehemu ya pili ni kiini cha swali ambapo
tumeeleza historia ya tafsri na umuhimu wake katika maendeleo ya mwanadamu,
sehemu ya tatu ni hitimisho la kazi yetu na sehemu ya nne ni marejeleo ya kazi
hii.
2.0 Fasili
ya Tafsiri na Maendeleo
Kuna
wataalamu mbalimbali walioelezea kuhusu dhana ya tafsiri na dhana ya maendeleo
kwa mawanda mapana ya fikra zao. Kwa kuanza kueleza maana ya tafsiri, kasha
itafuata maana ya maendeleo kwa mujibu wa wataalamu hao;
2.1 Dhana
ya Tafsiri
Maana
ya tafsiri imeelezwa na watalamu mbalimbali, lakini hapa tutajadili baadhi ya
wataalamu walioelezea dhana ya tafsiri kama ifuatavyo;
Catford
(1965 Uk:20) akinukuliwa na Mwansoko na wenzake (2015 Uk:01) wanaeleza kuwa
kufasiri ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja (lugha
chanzi) na kuweka badala yake mawazo yaliyolingana katika lugha nyingine (lugha
lengwa). Katika fasili hii Catford hakuweka bayana kuwa, tafsiri inahusu
uhawilishaji wa matini iliyo katika maandisha, kutoka lugha moja (lugha chanzi)
kwenda lugha nyingine (lugha lengwa), kwani kuna matini zinazoweza kuhawilishwa
kwa njia ya sauti.
Newmark
(1988 Uk:07) akinukuliwa na Mwansoko na wenzake (2015 Uk:02) wanaeleza kuwa, tafsiri
ni utoaji wa maana ya matini kwenda lugha nyingine katika namna ambayo
mwandishi aliikusudia matini hiyo. Pia hakutilia mkazo kuhusu utoaji wa maana
hizo sharti uwe katika lugha ya maandishi katika fasili ya tafsiri.
Mshindo
(2010 Uk:02) akinukuliwa na Antigon (2014 Uk:07) anaeleza kutafsiri ni
kufafanua maana ya matini moja na kutayarisha baadae matini nyingine inayowiana
nayo ambayo huitwa tafsiri, ambayo inawakilisha ujumbe uleule iliyomo katika
matini ya awali kwa kutumia lugha nyingine. Tafasili hii inadosali kwa sababu
kutafasiri sharti ihusishe matini iliyo katika maandishi.
Mwansoko
na wenzanke (2015 Uk:01) tafsiri ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika
kutoka lugha moja hadi lugha nyingine. Pia wameendelea kueleza kuwa mawazo,
ujumbe au matini ya lugha chanzi na lugha lengwa sharti iwe katika maandishi.
TUKI
(2016) wanasema tafsiri ni maandishi yaliyofasiriwa kutoka lugha moja kwenda
nyingine. Aidha kinachotazamwa katika tafsiri, sharti ujumbe au matini au maana
msingi isipotoshwe katika mchakato mzima wa kutafsiri.
Kwa
ujumla, tafsiri ni mchakato au kitendo cha kuhawilisha mawazo yaliyo katika
maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi) kwenda lugha nyingine (lugha lengwa)
pasipo kubadili maana iliyokusudiwa na mwandishi wa matini ya lugha chanzi.
Suala la msingi katika uhawilishaji wa mawazo, ujumbe au matini sharti utumie
maandishi, pia mawazo au ujumbe kati ya
lugha chanzi na lugha lengwa sharti yalingane. Mwansoko anaeleza kuwa, kwa hakika
hakuna tafsiri inayolingana kabisa, badala yake wataalamu wanatumia visawe na
maneno yanayolingana na siyo mawazo yaliyo sawa.
2.2 Dhana
ya Maendeleo
Aidha
ni kweli kwamba tafsiri ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya mwanadamu ili
kubaini hili hatunabudi kuelezea maana ya maendeleo kama ifuatavyo;
TUKI
(2016) wao wanaeleza kuwa, dhana ya maendeleo ni hali ya kutoka hatua ya chini
hadi hatua nyingine mpya na bora kisiasa, kiuchumi, na kijamii. Hivyo maendeleo
lazima iwe hatua ya kutoka hali duni kimaisha kwenda hali bora.
Kwa
ujumla maendeleo ni hali ya mabadiliko kutoka hatua ya chini kwenda hatua ya
juu, iliyo bora zaidi katika nyanja mbalimbali za kimaisha yaani kiuchumi,
kisiasa, kijamii na kiutamaduni. Baada ya kuangalia dhana ya tafsiri pamoja na
dhana ya maendeleo, ifuatayo ni historia fupi ya tafsiri kama ilivyofafanuliwa
na baadhi ya wataalamu.
3.0 Historia
Fupi ya Tafsiri Ulimwenguni
Mwansoko
na wenzake (2015: 4-6) waneeleza historia ya tafsiri kuwa, tafsiri ilianzia
Afrika huko Misri miaka elfu tatu (3000) na zaidi kabla ya kristo, ugunduzi wa
ustaarabu uliokuwa Misri uliigwa na Wayunani, hatimae kuufanya kuwa chimbuko la
ustaarabu wa ulaya katika karne ya 19, mbinu kuu iliyotumika katika kueleza
ustaarabu huu wa wamisri huko ulaya ni tafsiri. Maendeleo ya tafsiri
yametazamwa katika vipindi tofautitofauti kulingana na sehemu husika, kama
ifuatavyo;
3.1 Karne
ya 5-11
Katika
karne ya 5 hadi 11 wakati wa dola ya Warumi hasa baada ya ukristo kuenea Ulaya
nzima, elimu hiyo ya zamani ilianza kupigwa vita kwa kudaiwa kuwa ilikuwa ni ya
kipagani kwani iliigwa na wanataaluma wa Kiyunani na kuipeleka Ulaya, baada ya
elimu ya tafsiri kupigwa vita ilisababisha Ulaya kurudi katika kipindi kilichojulikana
kama zama za giza (Dark ages).
3.2 Karne
ya 12-15
Karne
ya 12 wakati wa vita ya msalaba kati ya wakristo na waislamu, wataalamu wa Ulaya
waliofika nchi za Kiarabu waligundua maendeleo makubwa ya kitaaluma na sayansi
katika nchi hizo. Wataalamu hao walibeba vitabu vya Kiarabu na kuvipeleka kwao
na kuvifanyia tasfiri katika lugha ya Kilatini na lugha nyingine za Ulaya.
Matokeo yake Ulaya ilianza kutoka zama za giza na kuingia kipindi cha ufufuko
wa elimu na maarifa yaani “Renaissance”.
3.3 Karne
ya 15-19
Tafsiri
hizo zilichangia kuitoa Ulaya katika zama za giza kipindi cha karne ya 15 na
kuingia katika kipindi cha ufufuko wa elimu na maarifa. Katika karne ya 19
ilikuwa ya mkondo mmoja ambapo vitabu vya waandishi mashuhuri katika nchi
zilizoendelea vilifasiriwa kwa ajili ya wasomaji wa nchi zinazoendelea.
Karne
ya 19 wamishionari walifasiri vitabu vingi vya kikristo ikiwemo Biblia, wakati
wa ukoloni hasa katika kipindi cha utawala wa Waingereza maandiko yanayohusu
taaluma na fasihi za ulaya, yalifasiriwa kwa Kiswahili. Mfano wa hadithi za
hekaya za Abunuasi, Alfu-lela-Ulela, Siku Elfu na Moja na hadithi za Esopo.
3.4 Karne
ya 20
Kipindi cha karne ya 20 kinajulikana kama
karne ya tafsiri, kutokana na mfumuko mkubwa wa kazi za tafsiri. Mikataba ya
kimataifa baina ya mashirika ya umma na mashirika ya binafsi, ilifasiriwa kwa
yeyote anayehitaji taarifa hizo. Uhitaji huu ulisababisha tafsiri kupata nguvu
mpya, maendeleo ya haraka ya teknolojia na haja ya kuyaendeleza maendeleo hayo
katika nchi changa yameongeza pia mahitaji ya tafsiri.
4.0 Historia
ya Tafsiri Nchini Tanzania
Hapa
nchini Tanzania taaluma ya tafsiri haina historia ndefu, ukilinganisha na nchi
zingine kama vile Misri, Hispania na mahali pengine huko ulaya. Tafsiri ya
kwanza iliyofanyika katika lugha ya Kiswahili ni ya utenzi wa kiarabu uitwao Hamziyya uliotungwa huko Misri mnamo
karne ya 19, tafsiri iliyofanywa na Aidarus bin Athumani.
Baada
ya uhuru wazalendo walifanya juhudi za kufasiri vitabu bora vya ulimwengu kwa
Kiswahili, pamoja na taasisi mbalimbali zilitafsiri matini, majalida, mikataba
na vitabu. Mfano Mwalimu J. K. Nyerere alitafsiri vitabu viwili vya William Shakespeare,
ambavyo ni Julias Kaizari (Julius Caesar 1963) na tamthiliya ya Mabepari wa
Venis (The Merchants of Venis 1969). Kwa ujumla wananchi wengi waliokuwa na
ujuzi wa lugha za kigeni walifasiri maandiko mbalimbali ya lugha hizo kwa lugha
ya Kiswahili. Baada ya kuangalia historia ya tafsiri, sehemu ifuatayo inaelezea
umuhimu na mchango wa tafsiri katika maendeleo ya mwanadamu kiuchumi, kisiasa,
kiutamaduni na kijamii.
5.0 Umuhimu na Mchango wa Tafsiri Katika
Maendeleo ya Mwanadamu.
Kutokana
na kufanya tafsiri, tafsiri imekuwa na umuhimu sana kwa binadamu, mambo mengi yamefanyika
kwa kusaidiwa na tafsiri kufanyika miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na
maendeleo ya binadamu, hivyo sehemu hii imejikita kuelezea umuhimu na mchango
wa tafsiri katika maendeleo ya mwanadamu kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na
kijamiikam ifuatayo;
5.1 Tafsiri
Husaidia Kurahisisha Ujifunzaji wa Taaluma na Teknolojia.
Katika
taaluma nyingi za sayansi kama vile taaluma ya kemia zipo baadhi ya isitilahi,
ambazo huundwa ili zieleweke kwa jamii husika ya watumiaji. Isitlahi hizo
hazinabudi kutafutiwa visawe vinavyoeleweka kwa watumiaji hao. Pia zipo baadhi
ya kamusi husika za kemia, baiolojia na fizikia, lengo likiwa ni kutaka kufanya
taaluma hizi zieleweke vema kwa jamii husika. Mitambo mingi ipatikanayo
viwandani na shambani imekuwa ikitumika vema. Licha ya kuwa na lugha za kigeni
kama vile kingereza, kichina, na lugha chanzi ambapo mitambo hiyo imekuwa ikitengenezwa.
Haya yote yanarahisishwa kutokana na kuwepo kwa tafsiri ambayo imesaidia
kufasiri lugha inayoeleweka kwa watumiaji wa jamii husika hii imekuwa chachu ya
kuogezeka kwa uzalishaji wa bidhaa na kusaidia maendeleo kwa mwanadamu.
5.2 Tafsiri
Husaidia Kuinua Kipato cha Mtu Mmoja Mmoja au Jamii Nzima.
Watu
hutumia tafsiri kama chanzo ajira ya kujipatia kipato ama kwa kuajiriwa au
pengine kwa kujiajiri wao wenyewe. Mfano katika viwanda, taasisi mbalimbali
kama vile Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), Taasisi ya Uchunguzi wa
Kiswhili (TUKI), Balaza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na kampuni nyinginezo. Hivyo
kupitia mchakato mzuri wa tafsiri umesaidia kuinua hali ya maisha ya mtu au
jamii nzima kufanya maendeleo.
5.3 Tafsiri
Husaidia Kuunganisha Jamii Mbalimbali Zinazozungumza
Lugha Tofautitofauti.
Tafsiri
ni kiini au daraja la kuunganisha jamii mbili au zaidi zenye kutumia lugha
tofautitofauti. Kupitia maingiliano haya ya jamii, yamesadia jamii kupata ujuzi
na maarifa kutoka kwenye jamii moja ama nyingine kupitia tafsiri. Mfano nchini
Tanzania kuna baadhi ya kampuni kutoka nchi mbalimbali zilizoendelea ambazo,
zimewekeza katika taasisi mbalimbali. Kupitia tafsiri wameweza kuwasiliana na
kushirikishana katika ujuzi, kwa kufanya hivyo tafsiri inachangia maendeleo ya
binadamu kwa sababu jamii hizo zinashirikiana katika uzalishaji mali. Kwani
lugha ndiyo nyenzo muhimu ya mawasiliano katika uzalishaji mali.
5.4 Tafsiri
Husaidia Mawasiliano Miongoni mwa Watumiaji wa Lugha Tofautitofauti.
Tafsiri
hutumika katika biashara katika kutolea maelekezo ya matumizi ya bidhaa ili
kufanikisha mawasiliano miongoni mwa watumiaji wa bidhaa hizo. Bidhaa
zinazouzwa nchi za nje huambatana na maelekezo ya namna ya kutumia bidhaa
husika. Hivyo tafsiri husaidia mawasiliano baina ya wauzaji na watumiaji wa bidhaa
hizo. (Newmark 1988: 7) alibaini kuwa mlipuko wa bomu la atomiki huko Hiroshima
(Japan) ulisababishwa na upotofu wa kutafsiri neno “Mokasutu” katika telegramu iliyopelekwa
Washington (Marekani) kutoka Japan neno hilo lilifasiriwa kimakosa kuwa ni “ignore”
(yaani kataa) badala ya “considered” (yaani zingatia). Hivyo ni wazi kuwa jamii
yaweza kupata matatizo iwapo fasiri haitaeleweka vema katika suala la
mawasiliano. Kwa kusaidia mawasiliano yanasaidia maendeleo ya mwanadamu.
5.5 Tafsiri
Husaidia Kueneza Utamaduni wa Jamii Moja na Nyingine.
Hii
ni wazi kwamba kupitia tafsiri jamii moja na nyingine kitaifa na kimataifa
zimejikuta zikitumia utamaduni wa jamii nyingine ambao kiasili si utamaduni wao.
Mfano kunako mwishoni mwa karne ya 19 utamaduni wa kiafrika uliiga mambo kadha
wa kadha toka katika tamaduni za Ulaya ikiwa ni pamoja na dini ya kikristo,
mifumo ya kisiasa hasa katika mfumo wa vyama vingi, mitindo ya mavazi na vyakula.
Pia wasomi wa nchi za ulaya walijifunza maarifa kwa kutumia tafsiri kutoka nchi
za kiarabu mashariki ya kati, kitu kilichowasaidia kuendeeleza jamii zao
zilizokuwa katika kipindi cha giza.
5.6 Tafsiri
Husaidia Ujifunzaji wa Lugha Katika Jamii.
Kupitia
tafsiri mwanafunzi ama mtu yeyote anayesoma kazi tofautitofauti ambazo
zimefanyiwa tafsiri huweza kujiongezea msamiati mpya ambao umefasiriwa katika
lugha yake toka lugha fulani ya kigeni, mfano School of Oriental and African
Studies (SOAS) na chuo kikuu cha London zimeonesha wanafunzi waingereza
waliokuwa wanajifunza lugha ya Kiswahili waliweza kubaini vipengele mbalimbali
vya sarufi ya Kiswahili wao wenyewe bila msaada wa mwalimu kutokana na mazoezi
ya kufasiri mashairi ya Kiswahili. Hivyo tafsiri inasaidia maendeleo katika lugha
na kuongeza maarifa na ujuzi.
5.7 Tafsiri
Husaidia Kukuza Kazi za Kifasihi.
Kupitia
tafsiri wafasiri na wasomaji wa kazi au matini zilizofasiriwa wamejikuta wakiwa
na hamu za kuandika vitabu vya kifasihi. Kwa sababu baada ya kuzisoma kazi hizo,
wasomaji wanaongeza maarifa kwa kuona kuwa na wao wanaweza kuandika kazi za
kifasihi zinazohusiana na jamii zao, kuzihimiza kufanya kazi kwa bidii,
kushirikiana na kutoa mafunzo. Mfano waandishi wa kwanza wa Afrika Mashariki
kama vile Ngugi wa Thiong’o, Shaaban Robert, James Mbotei, Whole Sonyika na wengine
walisisitiza umoja, kujikomboa, uhuru na kujikwamua kimaisha. Hivyo walijikuta
wanakuwa waandishi mahiri baada ya kuwepo kwa tafasiri. Mfano wa kazi za
kifasihi zilizotafasiriwa ni Songs of Lawino, utenzi wa Hamziyya, mabepari wa
Venis, hadithi za esopo, Hekaya za Abunuas, Alf-Lela-Ulela na kisa cha Mfalme
Edipode.
5.8 Tafsiri
ni Kiliwazo cha Nafsi ya Mfasiri.
Kwa
kufanya tafsiri na kupitia tafsiri, mfasiri wa matini kutoka lugha moja hadi
lugha nyingine ni kufurahisha na kuburudisha nafsi ya mtafsiri. Mfano Mwl J. K.
Nyerere alisema kuwa alitumia muda wake
wa kupumzika kufanya kazi ya kutafasiri kitabu cha Mabepari wa Venis na kitabu
cha Julius Kaizer, kwa kuifurahisha nafsi yake. Kwa kufanya hivyo, huongeza
ujuzi na kusambaza maarifa kwa watu ambao wasingeweza kupata funzo kama matini
husika ingebaki katika matini chanzi, hivyo tafsiri huchangia maendeleo ya
mwanadamu.
6.0 Hitimisho
Kwa
ujumla tafsiri imesaidia kwa kiwango kikubwa katika kuuleta ulimwengu pamoja,
kwa kurahisisha njia za upashanaji habari. Aidha tafsiri imekuwa chachu ya
kuuvunja wigo mpana uliokuwa ukiitenganisha jamii mbalimbali ulimwenguni. Kwani
mabadiliko makubwa yaliyopo katika jamii zetu kiini chake ni katika
uhawilishaji wa maarifa, mbinu na namna ambayo jamii moja imetumia kiuchumi,
kisiasa na kijamii kulikotolewa tafsiri na kutumiwa katika jamii lengwa.
MAREJELEO
Antigon,
F. M. (2014), “Tafsiri na Ukalimani. Utangulizi Muhimu Katika Tafsiri na Ukalimani”
Bakize,L.
H. (2013). Tafsiri na Ukalimani, Dar
es Salaam: Muccony Printing press.
Catford,
J. C. (1965), A Linguistics Theory of
Translation in English. Oxford University Press.
TUKI
(2016), Kamus Pevu ya Kisawhili, Dar
es Salaam.
Mshindo,
H. B.(2010), Kufasiri na Tafsiri,
Chuo Kikuu Cha Chukwan. Zanzibar.
Mwansoko
na wenzake (1996), Kitangulizi cha Tafsiri:
Nadharia na mbinu,
Dar es Salaam. TUKI.
Mwansoko
na wenzake (2015), Kitangulizi cha
Tafsiri: Nadharia na mbinu.
Dar es Salam. TUKI.
Newmark,
P. (1988), A Text Book of Translation.
Prentice International VUIO Ltd.
Congrats good work 🤝 hongera
ReplyDelete