1.1 Historia ya Kabila la Kiikoma
Kiikoma ni kabila miongoni mwa makabila ya kibantu yanayopatikana mkoa wa Mara wilaya ya Serengeti. katika kabila la waikoma suala la mgawanyomu wa unazingatia jinsi ya mtu na umri. Waikoma ni miongoni mwa wanajamii wenye taratibu zao kwani wamekuwa wakiendeleza mila na desturi zao kwa kurithishana kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.
1.2 Dhana ya Kabila
TUKI (2004:187) wanafasili dhana ya kabila kuwa ni kikundi cha watu wanaohusiana kwa lugha, mila desturi na tamaduni, au ni jamii ya watu au vitu vya aina moja. Hivyo kabila ni kikundi cha watu katika jamii ambacho kinahusiana katika masuala ya lugha, historia, mila, desturi na tamaduni zinazowazunguka. Pia dhana ya nyimbo imefasiliwa na wataalamu kama ifuatavyo;
Wamitila (2003:107) anafasili nyimbo ni tungo zenye mahadhi ya sauti ya kupanda na kushuka. Pia anaongeza kuwa tungo hizo huundwa kwa lugha ya mkato, matumizi ya picha na mapigo ambazo zimepangika katika utaratibu fulani na muwala wenye mapigo ya kimuziki. Fasili hii inaelekeana na
TUKI (2012) wanaoleza kuwa wimbo ni maneno yanayotamkwa kwa sauti zilizopangiliwa kimuziki ambazo wakati mwingine huambatana na mapigo ya vyombo vya ala za sauti.
Mulokozi (2017:118) anafasili wimbo ni utungo wa kisanaa unaowasilishwa kimuziki kwa kutumia sauti iliyo katika mpangilio fulani wa mahadhi ya melodia, yenye mapigo ya kiurari.
Hivyo mtalaamu huyu ametofautiana na wengine kwani ameeleza kuwa wimbo ni utungo wa kisanaa pia kaongeza kuwa, wimbo ni dhana pana inayojumuisha tanzu nyingi maana kila kinachoimbwa huweza kuitwa wimbo. Hivyo baadhi ya tanzu za kinathari zinaweza kuwa miongoni mwa sehemu ya wimbo. Mfano misemo, nahau, vitendawili, wakati mwingine simulizi ndani ya wimbo au wimbo wenyewe kuwa simulizi.
Mulokozi (2017) anaendelea kueleza mambo muhimu yanayotambulisha wimbo ni pamoja na muziki wa sauti ya mwimbaji au waimbaji wenye mapigo, mahadhi na melodia yake, matini au maneno yanayoimbwa, hadhira inayoimbiwa na muktadha unaofungamana na wimbo huo. Pia katika jamii nyingi za kiafrika, nyimbo zinadhima nyingi kama vile kuburudisha wakati wa mapumziko, kuonya, kuarifu, kuelimisha, kunogesha hadhira, kuomboleza, kubembeleza, kutia hamasa na kuchapuza kazi.
Kamusi elezi huru (2019), wanaeleza kuwa wimbo au nyimbo ni tungo zenye kufuata mapigo fulani ya kimuziki yenye maadhi ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti (urali wa sauti) na mpangilio maalumu wa maneno. Wanaendelea kusema, nyimbo huundwa kwa lugha ya mkato pamoja na matumizi ya lugha ya picha (taswira). Muundo wa nyimbo huwa ni wa kuimbika na mizani ya kila mstari mara nyingi huungana aghalabu nyimbo huambatana na ala za muziki kama vile ngoma, zeze, marimba, makofi, vigelegele. Hivyo mujibu wa maelezo hayo yafuatayo ni maelezo namna taswira zinazosawili mwanamke na mwanamume katika nyimbo za jamii ya waikoma.
2. Taswira ya Mwanamke na Mwanamume
Mwanamke na mwanamume wameweza kuchorwa katika taswira mbalimbali katika jamii fulani. Mfano katika jamii ya waikoma kumekuwa na mgawanyo wa kimajukumu kulingana na umri na jinsi ya mtu. Kwa kuanza na taswira ya mwanamke, katika wimbo ufuatao
Wimbo wa kiikoma
Tigha kwembele Maghori omisi x2
Nomisi monawito, Nyagwishenge naghire,
Ghutema eghesinge moritororo, nakucha atabhori,
Otamisi inchera, olamisi inchera anchera yeghoghughota,
Tigha anchera nimbe, anchera yehita, yitiri Yima na maye,
Yitiri Tata naabhasiri bhose,
Nyako wose nagire, ghutema eghesinge, molitororo,
Otighe korera, nyako nakucha atabhori,
Hamwabhe nakucha, alacha noghughoka,
Tigha kwembele Maghori omisi x2
Nomisi mona wito, nookire omona eee!.
Tafsiri katika Kiswahili
Acha nikuimbie Maghori ili ulale,
Ulale mtoto wetu, shangazi yako ameenda kuvunja visiki shambani,
Atakuja asubuhi, ila chunga usilale njaa,
Hata njaa ikikushika usilale njaa, njaa ni mbaya ilimuua mama,
Ilimuua baba, iliwauwa wafu wengine,
Mama yako pia ameenda shambani, kusafisha visiki huko,
Nyamaza uache kulia, atarudi asubuhi,
Ikitokea bahati nzuri, mama yako akija utanyonya,
Acha nikuimbie Maghori ili ulale x2
Nyamaza mtoto uache kulia, nyamaza eeeee! ,
5
2.1 Taswira ya mwanamke katika kabila la waikoma
Katika wimbo huu mwanamke amechorwa katika taswira mbalimbali kama vile,
Taswira ya mwanamke kama mlezi wa familia, katika jamii ya kabila la waikoma mwanamke ndiye anaonekana kuwa tegemeo kwa familia kwani ndiye anasubiriwa arudi kutoka shamba kisha aandae chakula kwa ajili ya watoto. Japo mwanzoni mwandishi amemtumia mhusika shangazi alikuwa akimrejelea mwanamke.
Taswira ya mwanamke kama mfanyakazi, kwa mujibu wa wimbo wa wanajamii wa kabila la kiikoma mwanamke amechorwa, unaeleza kuwa mwanamke ndiye anafanya kazi kama kwenda shamba, mfano kusafisha shamba na kulima.
Pia amechorwa kama mtu anayefanya kazi bila mapumziko, kwani wimbo unaeleza kuwa endapo mama atakuwa amerudi kwa nyumbani atakuwa amerudi kwa bahati tu, hivyo elimu ya kijinsia inatakiwa itolewe katika jamii ili kuachana na mitazamo ya kumkandamiza mwanmke na kumbeba mwanamume.
Mbali na kuwapo nyimbo zinazotumia taswira katika kumueleza mwanamke katika jamii ya waikoma, kuna baadhi ya misemo iliyobeba taswira ya mwanamke.
Kiikoma - Ntere mouchi oohano, kwibhora kundetiri
Kiswahili - Mwanamke sio mhusika ni kuzaa kumempeleka ukweni
Mwanamke hawezi kufanya kitu chochote tofauti na kuzaa, mwanamke amechorwa kama mtu asiyeweza kufanya kitu chochote ukweni, bali kuzaa tu ndiyo kazi yake. Hivyo mwanamke hapewi thamani kabisa kuwa nayeye anaweza kuwa na mchango katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa pia kiutamaduni.
Mwanamke ameoneshwa kuwa kama mtu asiye na uamuzi binafsi, katika msemo huo wakati mwingine unakuwa na maana kuwa mwanamke hana uamuzi wa aina yoyote pindi anapoolewa. Hivyo anaoneshwa kuwa yeye ni mtu wa kuzaa tu na hata idadi ya watoto hapangi yeye isipokuwa mumewe
2.3 taswira ya mwanamume katika kabila la waikoma
Pia mwanamume amejengwa kutumia taswira mbalimbali katika jamii ya waikoma japokuwa mara nyingi humuonesha mwanamume kuwa mmiliki wa mali,
Wimbo wa kiikoma
Ooooh! nimbeeee ooooh! Hiyeee! x2
Chang’ombe nimbe oooh nimbee Hiyeee!
Hano chekucha na bhamula chekulee x2
Hiyeeee bhamura oooh heee! Hiyooo x2
Hano chekucha na bhamula chekulee x2
Tafsiri kwa Kiswahili
Ng’ombe ni kitu cha thamani x2
Zinawahusu vijana wa kiume tu x2
Mwanamume ameoneshwa kuwa mmiliki wa mali, mfano wametumia mnyama Ng’ombe kueleza kuwa mali inamhusu kijana wa kiume pekee. Kwa namna hiyo mwanamke haruhusiwi kuwa mmiliki wa mali bali mwanamume pekee.
Mwanamume anachorwa kama kiongozi, mtu asiyepaswa kuongozwa na mwanamke, mwanamume amechorwa kama kiongozi kwani katika umiliki wa hutegemeana na uongozi, hivyo mali zinamilikiwa na kiongozi na sharti awe mwanamume.
Pia kuna baadhi ya misemo inayotumia taswira kueleza kuwa mwanamume ndiye mwenye nguvu. Hivyo mwanamume ndiye mwenye nguvu katika jamii na anauwezo wa kufanyia mwanamke jambo lolote naye asimjibu kitu. Mfano
Kiikoma - Aheri nebhighoti
Kiswahili - Ng’ombe dume anasifiwa shingo
Hapa wametumia taswira ya ng’ombe dume ila lengo ni kuifahamisha jamii kuuwa mwanamume ndiye kila kitu na ndiye mwenye nguvu katika jamii.
Pia mwanamume anaonekana ndiye mwenye thamani na mrithi, katika jamii ya waikoma mwanamume amechorwa kuwa mwenye thamani na hupongezwa pindi anapofanya jambo fulani na kulifanikisha sambamba na urithi wa mali anahusika mwanamume. Mfano katika wimbo ufuatao
Kiikoma
Heee bhuchama x2
Lelo oghakora ang’ana,
Neghwitera aserecha x2
Kiswahili
Wee kijana x2
Leo umetenda jambo,
Nitakuchinjia Jogoo x2
Hivyo mwanamume ameonekana ndiye mtu pekee katika jamii mwenye uwezo wa kuleta mabadiliko. Kwani anaambiwa kuwa leo umetenda jambo kubwa nitakuchinjia Jogoo. Wimbo huu huimbwa kumsifia kijana pale anapotenda jambo fuani.
3 Hitimisho
Katika jamii ya waikoma kuna mila na desturi zinazomkandamiza mwanamke, hivyo elimu lazima itolewe ili kutambua nafasi zote za wanajamii kulingana na jinsi zao kwani mwanamke hajapewa nafasi sawa na mwanamume kwa kumuona kuwa yeye ni kiumbe dhaifu, mtu asiye na uamuzi, mtu asiyeweza kumiliki wala kurithi mali katika jamii. Kwani maendeleo huletwa na jamii nzima kwa ushirikiano.
Marejeleo
Mulokozi, M.M. (2017) Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili: Dar es Salaam: Moccony Press.
TUKI (2004) Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la 2. Dar es Salaam: TUKI.
TUKI (2012) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam. TUKI.
Wamitila, K.W. (2003). Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi. Nairobi: Focus
Publication Limited.
http://www.artintanzania.org/en/about/children-songs-north-tanzania-africa
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com