Wataalamu mbalimbali wametoa
maana ya utendi katika mitizamo tofauti tofauti ,miongoni mwa watalaamu hao ni
kama wafuatao;
Mulokozi (1996:85) utendi ni utanzu mashuhuri
sana katika kundi la ghani-masimulizi. Utendi ni ushairi wa matendo. Ni utungo
mrefu wenye kusimulia matukio ya kishujaa yenye uzito wa kijamii au kitaifa.
Matukio haya huweza kuwa ya kihistoria na visakale/ visasili.
Wamitila (2003:333) anaelezea utendi kuwa ni
shairi refu la kisimulizi linalozungumzia kwa mapana na mtindo wa hali ya juu
matendo ya mashujaaa au shujaa mmoja. Kimsingi utendi huwa na sifa nyingi na
huweza kuleta pamoja hadithi ya kishujaa, mugani, visasili, historia pamoja na
ndoto za taifa fulani. Anaendelea kusema kwamba kuna aina mbili za tendi ambazo
ni tendi zinazohusisha fasihi simulizi na utendi wa kifasihi/ andishi.
Ruth Finnegan alifanya utafiti juu ya tendi
za Kiafrika akagundua kwamba Afrika hakuna tendi bali kuna sifo. Katika kitabu
chake kilichoandikwa mwaka 1970 anaeleza kuwa utanzu wa utendi hautokei sana
Afrika. Katika kuelezea sifa za utendi , Finnegan alibainisha sifa nne za tendi
simulizi ambazo ni nudhumu, urefu yaani utendi lazima uwe mrefu, sifa ya
upatanifu yaani utendi ni utungo wenye visa vilivyounganika kimantiki na
maudhui ambayo yanapaswa kusimulia maisha na matendo ya kishujaa. KARATASINI
Wataalam wengine waliona sifa alizotoa Finegan
hazijajitoshereza na hivyo wakaongeza sifa nyingine za utendi,wataalamu hao ni
Okpewho (1979), Jonhson (1986) Mulokozi (1987) wamethibitisha kuwa utendi ni fani iliyoonea
sana Afrika na wameongeza sifa za utendi. Sifa hizo ni kama zifuatazo: Utendi
lazima uwe ni masimulizi, hutolewa kishairi, huhusu matukio muhimu ya
kihistoria au kijamii, huelezea habari za ushujaa na mashujaa, huwasilishwa kwa
kughanwa au kuimbwa pamoja na ala za muziki, hutungwa papo kwa papo yaani
hautungwi kabla na kuhifadhiwa kichwani na hutawaliwa na muktadha wa utungaji
na uwasilishaji kwa jamii.
Muhtasari wa Utendi
Utendi wa Rukiza (Enanga ya Rukiza) ni
miongoni mwa tendi simulizi mashuhuri za
Wahaya na Wanyambo mkoani Kagera nchini Tanzania.
Utendi wa Rukiza uliimba na Yeli (manju wa tendi) aitwaye Habibu Suleiman ambaye alizaliwa mwaka 1929 na kufariki mwaka 1993. Utendi huu
ulirekodiwa na M.M. Mulokozi mwaka 1974.
Utendi wa Rukiza ni utendi wa Kisira (Kiwasifu) unaosimulia hadithi ya maisha ya Nguli
au shujaa Rukiza kabla ya kuzaliwa hadi
kifo chake matukio yanayojitokeza katika utendi huu yanapelekea kupata ruwaza
ya shujaa kama ilivyoelezwa na wataalamu wa utendi na hivyo kumnasibisha Rukiza
na mashujaa wa Kiutendi
Fomula zilizotumika
katika wa Utendi wa Rukiza.
Utendi wa Rukiza huweza kuelezwa kwa fomula
zifuatazo:
Ushujaa = Ushakii + sihiri + watu
Utendi
huu umefuata fomula hii kwa sababu ni miongoni mwa tendi za kiafrika ambazo
nguvu za ushujaa hutegemea ushakii, sihiri na watu.
Hapa
tunaona kuwa Rukiza ana nguvu zaidi za sihiri kuliko Ruhinda. Ruhinda anajaribu
kumpiga Rukiza lakini anashindwa. Kushinda kwa Rukiza. hakutokani na ubora wa
majeshi ya Rukiza bali kunatokana na nguvu za ziada za sihiri. Ili Kumshinda
Rukiza inabidi Ruhinda naye atafute nguvu za ziada kwa waganga ambapo baadaye
anafanikiwa kumshinda Rukiza kwa kugundua asili ya nguvu zake kwa kupitia kwa
waganga/wabashiri.
Hivyo
mapambano katika utendi huu na tendi nyingi za Kiafrika ni silaha, sihiri na
watu na sihiri hushindwa kwa sihiri bora zaidi. Hapa ina maana kuwa shujaa hufanikiwa anapokuwa na
nguvu na ujasiri (ushakii), msaada wa uganga na ushirikiano na watu (Mulokozi
2002:7).
Fomula Simulizi
Wamitila (2003:50) aneleza kuwa fomula
simulizi hutumiwa kuelezea tungo ambazo hurudiwarudiwa katika usimulizi wake.
Sifa hii yaweza kupatikana katika fasihi andishi na fasihi simulizi. Katika
fomula simulizi mtunzi hana muda wa kupangilia yaani anatunga papo kwa papo
Jadi anayotumia mtunzi imeshinikiza vipashio fulani vya lugha ambavyo mtunzi
anavitumia katika utunzi wa utendi/ shairi. Kitu cha muhimu kwa mtunzi ni
kuwasilisha kwa kutumia sifa za kijadi na siyo ubunifu binafsi. Hapa
kinachozingatiwa ni kuimba kwa kufuata ala za muziki. Fomula simulizi ina sifa
za uradidi/ urudiaji wa maneno/ sentensi, ujazaji wa nafasi wazi na uhusishi.
Katika ujazaji wa nafasi mtunzi anaingiza vitu vipya na shairi linaendelea.KARATASINI
Kwa kifupi ni kwamba utendi wa Rukiza umetumia fomula simulizi kwa sababu kuna urudiaji
mwingi umefanyika . Kwa mfano mishororo ifuatayo:
175:
Kutokea mlimani huonekana kama madimbwi ya mvua za masika!
343
Ukiwa mlimani yaonekana kama madimbwi ya mvua za masika!.
Matumizi
ya takriri katika utendi huu ni kipengele ambacho kinafanya fomula simulizi
ijitokeze au itumike kwani huonyesha urudiaji wa maneno, sentensi na vifungu
vingine vya maneno kwa lengo la kuimbika.
Matumizi ya Topo
Fomula
simulizi katika utendi huu iliongezewa Topo ambayo ni vitushi radidi. Topo
zizonazojitokeza katika utendi huu ni kama zifuatazo:
Mtoto
kuongea kabla hajazaliwa, orodha ya Baganga ambao wamekuwa wakiitwa mara nyingi, topo ya mtoto
kuonyesha maajabu baada ya kuzaliwa. Vipengele hivyo huonyesha uradidi wa
vitushi yaani vipengele ambavyo vimerudiwarudiwa.
Ruwaza ya shujaa
Utendi huu wa Rukiza unaingia katika ruwaza ya
shujaa kwa kuwa unamuelezea Rukiza kama shujaa kutokana na hatua muhimu alizozipitia
toka kuzaliwa hadi kifo chake. Matukio
haya ni kama yafuatayo: Kuzaliwa kwa Rukiza kimiujiza na mama yake akiwa
ugenini, utoto wa Rukiza na maajabu anayoyatenda, kurejea kwa Baganga Byantanzi
na vituko zaidi vya Rukiza na maajabu anayoyatenda, kurejea kwa Baganga
Byantanzi na vituko zaidi vya Rukiza
njiani kustawi kwa Baganga Byantazi, ujio wa Kilokote (Kalondano) na
kukaribishwa kwake katika ukoo wa Baganda, usaliti wa Kilokote, pambano la
kwanza kati ya Ruhinda na Rukiza na kushindwa kwa jeshi la Ruhinda. Juhudi za
Ruhinda ya kutafuta ushindi kwa njia ya sihiri kuolewa kwa binti Rukiza na
Ruhinda, kufichuliwa kwa siri ya uwezo wa Rukiza na binti yake kutokana na
athari ya sihiri. Pambano la pili kati ya Ruhinda na Rukiza kifo cha Rukiza na
mwishoni ni kifo cha Ruhinda kwa mkono wa mkewe aliyelipiza kisasi.
Fani na maudhui katika Utendi
wa Rukiza
Fani
Hiki
ni kipengele muhimu sana katika kuchambua kazi yoyote ya fasihi. Katika fani
tutaangalia vipengele vifuatavyo.
i)
Mtindo, (ii) Lugha (iii) Wahusika (iv)
mandhari
Mizani
Kwa kiasi kikubwa utendi huu hauna mizani
ndefu lakini kuna baadhi ya mistari michache imejitokeza kuliko mingine amabayo
ina mizani ndefu. Kwa kutumia muundo wa mizani ndefu kuliko mizani ya
kawaida, kumeleta mchomozo katika utendi
huu. Pia mtunzi alikuwa na nia ya kusisitiza jambo fulani kwani mishororo
iliyoelezwa hapa chini:
92: Jamani mtoto gani huzungumza akiwa
tumboni mwa mama yake!
111: Nikaona dume huyo anaanguka mweleka
karibu na muoto
115: Waliporudi walikuta kimekwisha mchinja
dume kwa vidole vyake.
254: Kikajibu, Nimetokea katika nchi ya
Wasiovaa na Wasiojifunika
343: Ukiwa mlimani yanaonekana kama madimbwi
ya ya mvua za masika!
Mtindo
Katika
mtindo wa utendi huu kuna matumizi ya majigambo, sitiari, usambamba, takriri,
tashbiha na matumizi ya chuku.
Majigambo
Katika
utendi huu mtunzi ametumia mtindo wa majigambo katika usimulizi wake kwa mfano
katika mishoro 23-36 akasema “Nilizaliwa ndimi Rukiza. Hapa Rukiza anaanza
masimulizi kwa kujigamba kama yeye ni shina la mgomba lililooza. Hapa
inamanisha mfumo anaouwakilisha umeoza lakini hataanguka peke yake utamwangusha
na yule atakayeuchokoza. Pia anajigamba kwamba yeye ndiye Rukiza mkombozi wa
kaya ya Baganga ambaye ndiye msingi na mleta ngoma na asali.
Matumizi ya Sitiari
Sitiari
hutumika kufananisha vitu viwili kwa kutumia neno “ni”. Katika utendi huu
mtunzi amaetumia sitiari pana. Kwa mfano katika mishororo ifuatayo kuna
matumizi ya sitiari
Mshororo
wa 34-37 pale Rukiza anapojifananisha na shina la mgomba kwa kusema
“Mimi shina la mgomba nilioza zamani
Nilikataa kuanguka bila kutikiswa
atakayenitikisa nitaanguka naye”
Pia katika mishororo ifuatayo kuna
matumizi ya sitiari
89: Wakasema, “Huyu si mtoto, labda ni kioja,
ni ndumba
504: Hawa ni njiwa tu, nitawatumia
Katika
sitiari hiyo ya shina la mgomba, Rukiza anaonyesha jinsi anavyojiamini na nguvu alizonazo. Yeye hapa anatabiri kifo
chake kwani alijua siku moja atakufa na yule ambaye atamuua na yeye atakufa
naye.
Matumizi ya Tashbiha
Hii
ni tamathali ya semi ambayo vitu viwili hulinganishwa kwa kutumia neno “kama”. Katika
mshororo wa 186 hapa mtunzi alitaka kulinganisha uwezo wa pande mbili Kwa
mfano,
186:
Wanaume kadhaa kama ninyi hapa tulikuwepo
Tashbiha
nyingine ni kama zifuatazo:
200:
Sitopata tena uzao kama huu
203:
Ana roho kama jiwe
347:
Anasema yeye ni mfalme kama wewe.
Usambamba
Hii
huonyesha mfanano wa mistari miwili, mitatu na kuendelea. Mf katika mishoro
ifuatayo
608:Eeee
eeee ai maskini
609:Eeeee
ai maskini
Matumizi ya chuku
Katika utendi wa Rukiza kuna matumizi ya chuku yaani maneno yenye kutia
chumvi. Kwa mfano katika mishororo ya
172-179 tunaona kuna matumizi ya chuku. Kwa mfano:
Badanga
wakapona ufukara
Wakanywa
maziwa yakawashinda
Mengine
wakayamwaga katika ishazi kutokea mlimani huonekana kama madimbwi ya mvua za
masika!
Tukaona
samli ngumu
Nyumbani
mwa Rukiza ikichezewa na watoto
Nikaona
samli laini inakandikwa kwenye viambaza
Bagnga
wote wakatonoka
Katika
hali ya kawaida haya hayawezi kutokea kwa hiyo hapa kuna ukuzaji/kutia chumvi.
Hapa mtunz alikuwa anataka kukusisitiza jambo fulani kwamba mambo yaliyokuwa
yakitendeka hayakuwa ya kawaida.
Takriri
Kurudiarudia
kwa maneno kunaonyesha msisitizo wa
jambo fulani yaani mtunzi anataka ujumbe fulani uifikie jamii. Kwa mfano
95: Wakajaribu vyembe vya mlanzi vikateleza
96: Wakajaribu kisu cha kunyolea
hakikufaa
460: Ewe Rukiza, Rukiza, Rukiza, Rukiza,
Rukiza, mtoto wa mama
600: Nyingine ipo kwenye mgomba wa
ntundu
601: Nyingine ipo kwenye muoto wa
mtoto
Udokezi
Udokezi
hutegemea muktadha katika utendi wa Rukiza mtunzi ametumia udokezi akiamini
kuwa hadhira inaelewa kile anachokisema kwa kudokeza kwa mfano katika mshororo
wa 441. “Vipi cheupe –cha-wamala hii ina maana kuwa ng’ombe wake ni mweupe.
Hapa anadokeza kitu kingine na inawakilisha kisakale. Kwa hiyo wenye utamaduni
wa Kihaya wataelewa kinachozungumzwa.
Lugha
Lugha
katika utendi wa Rukiza imeonekana
kueleweka zaidi kwa wazee kuliko vijana/watoto. Sababu kubwa zaidi ni mtindo
wake unaotumia mbinu mbalimbali za lugha hususani tamathali za semi kama sitiari, jazanda, takriri, ishara na udokezi
katika kuwasilisha ujumbe wake.
Mwimbaji wa utendi huu amechukulia kuwa
hadhira yake inafahamu vyema matukio yanayozungumziwa.
Lugha ya Kifalme
Kuna
maneno yanayotamkwa kabla ya kutaja jina la mfalme. Kwa mfano mishororo ya
(329-
329:
Kikasalimia, Na uishi na kudumu milele ee Mfalme!
335:
Ewe mtukufu mimi nilifika kwa Rukiza
330:
Kikasujudia miguuni kwa mfalme
376:
Mfalme akajibu, Kitwana hufa hutokufa
378:
Kwa kudhubutu kubomoa uzio wa mfalme kama huu
379:
Maana ni muhali kwa uzio wa Mfalme kuvunjwa na mtwana
Kwa
hiyo lugha ya kifalme imetumika kuonesha namna utawala wa kijadi ulivyokuwa na
nguvu na pia ilitumika kuwagawa watu katika matabaka kutegemea namna walivyo
thaminiwa katika jamii.
Lugha ya ufugaji/ng’ombe
Sajili
ya ufugaji ina maneno na misemo mingi inayohusu ng’ombe mfano mzuri ni majina au maneno yanayowatambulisha ng’ombe kwa mujibu wa rangi na sifa zao
nyinginezo zinazoonekana. Kwa mfano kisa/rusa ng’ombe mwenye rangi ya maziwa au
krimu. Siina – ng’ombe mwenye rangi ya kahawia nyeusi kitale – ng’ombe mweupe
kabisa, Gaaju – ng’ombe mwenye rangi ya kahawia nyepesi, Bihogo – ng’ombe mwenye
rangi ya kahawia nyeusi, Nkungu- ng’ombe asiye an pembe
435: Milia wa ikondo – ng’ome mwenye pembe kubwa
na ndefu zilizoelekea mbele
Lugha ya kijadi
Matumizi
ya maneno ya kijadi (uchanganyaji misimbo maneno ya kiswahili na Kihaya)
Katika
utendi huu kuna maneno ya kijadi ambayo ni vigumu kuyafasiri katika lugha ya
kiswahili. Mfano muhoro – panga la kijadi
419:
kilele - kibuyu cha
kunywea pombe chenye shingo ndefu ambacho hutumiwa na wanaume hasa
wanaoheshimika.
660:
Nchweke: Pepo au mashetani
yanayompata mtu aliye karibu sana na yule aliyefariki .
87: na 89 Ekikumila: Kisifa cha mapepo/ jini au mazingaombwe
587:
Kilela - Kitovu cha mtoto
mchanga
600: Ntundu Aina ya mgomba, ndizi zake hutumika kutengenezea pombe
16-17
Eshwiga - Mboga ya majani
ambayo huliwa na pia hutumika kama dawa (mnavu)
111:
Ekome/komi - Moto unaokokwa mbele
ya nyumba wakati wa usiku na kuzungukwa na wanaume wakati wanaongea. Mara
nyingi hukokwa wakati wa msiba (matanga) au wafugaji wanapotumia kuulia wadudu.
126:
Ekigabilo: Mti mkubwa wa baraka,
ambapo watu hufanya matambiko ili kukamilisha mambo yao.
16-17 Omugobe: Majani ya kunde, omushonge: nyumba ya jadi ya
wanyambo
Eshwiga – mboga ya majani ambayo huliwa na pia hutumika kama dawa
(mnavu)
11:
Obuganga: Nchi ya Baganga
Obukhankabana: Visumba vya ndizi
Ekyanzi – Gudulia la mti la kukamulia
maziwa
Engozi – mbeleko ya ngozi
Eiyembe – kioja pembe ya uchawi au
mazingaombwe yenye vituko
251: Mkago:
ndugu wa kuchanjiana damu (kushela mkundi)
Yapo
maneno mengi sana ya kijadi ambayo yametumika katika utendi huu. Hivyo huu ni
uchanganyaji misimbo wa lugha ya Kiswahili na Kihaya ambapo baadhi ya maneno yanapaswa yatafsiriwe ili kuufanya
utendi huu ueleweke zaidi. Mhariri amefanya hivyo mwisho wa utendi huu.
Lugha ya Uganga
Lugha
hii ya uganga imetumika pale Ruhinda alipoita wabashiri ili wamfanyie dawa
binti wa Rukiza na familia yake mfano katika mishoro ifuatayo, lugha ya uganga
imetumika mfano katika mshoro wa 537-589.
537:
Wakapiga ramli, utumbo wa kuku ukawa mweusi
538:
Wakapiga ramli bila mafanikio
581: Tumetakasa Ndumba -Ahamari
582:
Kaya yote ya Rukiza ihamishwe
583:
Tumetakasa Ndumba Paramizi
584:
Kaya yote ya Rukiza iparamiwe!
586:
Mpe mwali ndumba hizi
587:
Azitundike kwenye nguzo tatu za kilele
588:
Akikuuliza unamzindika kitu gani
589:
Mjibu kuwa umemzindika dhidi ya mapepo ya mizimu ya kwao
Lugha hii inaonesha matumizi ya maneno ya uganga yanayohusiana na
sihiri.
Vilevile lugha ya dini imetumika kwa
kiasi kidogo, kwa mfano katika mishororo
ya 563 na 569; Akajibu “Mungu anipishe mbali” Hapa inaonesha imani ya kidini ya
mwali huyo. (binti Rukiza). Kwa ujumla
lugha iliyotumika katika utendi huu ni ya kawaida japokuwa kuna mchanganyiko wa
maneno ya Kihaya lakini inaeleweka.
Wahusika
Rukiza
Ni
mhusika mkuu katika utendi huu na ndiye amebeba jina la utendi. Alizaliwa ili
kuwaokoa Baganga baada ya kupata njaa kali huko Uganda na kulazimika kuhamia
Karagwe kutafuta malisho na makazi yao. Rukiza maana yake ni mkombozi na kweli
amewakomboa Bananga japo alizaliwa kimaajabu sana. Alikuwa na nguvu za ajabu
zilizotokana na sihiri, kiasi kwamba alivyokuwa akichomwa mkuki hafi na badala
yake anaua watu wengi sana alipopigana na Ruhinda. Binti yake aliolewa na Ruhinda na baadaye
alikuwa chanzo cha kifo cha baba yake. Kuzaliwa kwake kulionekana kioja kwa
watu wote. Hii ni kutokana na matendo
aliyokuwa akiyafanya akiwa tumboni na mara baada ya kuzaliwa.
Vilevile
Rukiza anaamini sana imani ya jadi hasa kufanya matambiko na mambo mengine ya mila na desturi. Aliweza kufanya
mambo ya ajabu ambayo waheshimiwa wengine na wafalme walikuwa hawayafanyi kwa
mfano kuishi na Kilokote (Kalondano) ambaye alikuwa ni mtwana. Hata hivyo kilokote ndiye aliyekuwa chanzo
cha mapigano kati ya Rukiza na Ruhinda na hatimaye wote wakafa. Hii ilitokana
na maneno aliyoyasema Rukiza mwenyewe kuwa atakayemtikisa ataanguka naye. Hata
hivyo Rukiza anaonekana ni tu mwenye busara kwani alipanga kwenda kwa mfalme
Ruhinda kuuliza juu ya maneno ya uchonganishi aliyoletewa na Kilokote. Kabla
hajafanya hivyo alivyokusudia ndipo usiku huo huo akavamiwa na Ruhinda na vita
ikaanza.
Ruhinda
Alikuwa
mfalme wa Karagwe ambaye aliwapokea Baganga walipohamia kutoka Uganda
wakitafuta makazi na malisho ya ng’ombe. Mwanzo alikuwa mtu wa karibu sana na
Rukiza na walikuwa wakishirikishana mambo mbalimbali kama marafiki ila anakosa
busara anapoletewa maneno ya uchochezi na Kilokote. Alipaswa kumwuliza Rukiza
juu ya yote aliyoambiwa na Kilokote, badala yake anaenda kuvamia kwa Rukiza kwa
mapigano na anapigwa vibaya sana na Rukiza na watu wake aliambatana nao wengi
walikuwa mfano katika mishororo (451-427).
Alimwoa
binti Rukiza kama mbinu ya kujua asili ya nguvu za Rukiza baada ya kuambiwa na
wabashiri wake (wafumu). Baada ya kumwoa binti Rukiza aliendelea kuwatumia hadi wakafanikiwa kumfanya huyo
binti Rukiza aseme asili ya nguvu za baba yake na ndipo alipopigwa na
Ruhinda na jeshi lake na kumuua. Hapo
walichukua ng’ombe wote wa Rukiza na kuja nao. Binti yake naye akamchoma kisu
Rihinda naye akafa kwa kujikata shingo. Mfano katika mishororo (630-683).
Kilokote
Ni
mtwana ambaye aliishi kwa Rukiza baada ya kuokotwa njiani akiwa uchi.
Alipokutwa njiani Rukiza alitaka kumwua
ila Baganga wakakataa na ndipo Rukiza akaamua kumchukua akakaa naye. Kilokote
alipendeza na kunawiri nyumbani kwa Rukiza.
-
Alikuwa chanzo cha mapigano kati
ya Rukiza na Ruhinda kwani ndiye aliyewachonganisha hadi mapigano yakaanzishwa
na Ruhinda.
-
Alivunja mihoro na kilele
alipotumwa kwa Ruhinda na Rukiza ili visionekane kule kwa Rukiza. Akiwa
anaingia kwa Ruhinda alipitia Buyondo na Wayondo wakataka kumuua, akajitetea na
ndipo alifika kwa mfalme Ruhinda na kuongea uongo ambao ulileta mgogoro. Mfano
katika mishororo (395-419).
Baada
ya kutaja mali zake zote alizodai zimeharibia huko kwa mfalme Ruhinda, Rukiza
alimpa nyingine naye Kilokote akaingia ndani akalala baada ya kula na usiku ule
vita ikaanza.
Binti Rukiza
Aliolewa
na Ruhinda baada ya Ruhinda kutumia nguvu za sihiri kwa kuwatumia watabiri
ambao walitumia dawa zilizomfanya Rukiza kukubali bintie kuolewa na Ruhinda.
Hata
hivyo sihiri hizo zilitumika pia kumfanya Binti Rukiza atoe siri ya nguvu za
baba yake.
Baada
ya baba yake kuuawa, analipiza kisasi kwa kumchoma kisu Ruhinda naye kujikata
shingo na ndipo usemi wa baba yake wa atakayenitikisa nitaanguka naye
ulipotimia mshororo wa 36).
Wahusika
wengine wametajwa na mtambaji katika kukamilisha utendi huu. Wahusika hawa ni
kama Kachenkela ambaye ni mama yake Rukiza. Wayondo ambao ni wapishi wa mfalme
Ruhinda, majeshi ya Ruhinda watoto wengine wa Rukiza na mke wa Rukiza (Luhunge
binti Nshaiga).
Mandhari
Mandhari
ya utendi huu ni katika jamii za Wahaya na Wanyambo katika mkoa wa Kagera
nchini Tanzania. Matukio yaliyomo katika Utendi wa Rukiza
yalitokea katika ufalme wa Karagwe jamii ya Baganga ambayo imehamia Karagwe
kutoka Kaskazini ya Uganda na magharibi ya Rwanda. Jamii hii ni ya wafugaji
ambao walizunguka kutafuta malisho ya mifugo yao mpaka wakafika kaskazini
Magharibi mwa Karagwe na kujenga makazi yao katika eneo la Byantanzi.
Maudhui ya Utendi Wa
Rukiza
Utendi wa Rukiza unaakisi mgogoro wa kihistoria kati ya mifumo miwili yaani mfumo wa
kijadi na mfumo wa kifalme. Amali za mfumo wa kijadi ni umoja na ushirikiano wa
watu wa damu moja, matambiko ya pamoja, umiliki wa mali kwa pamoja hususani
mifugo na ardhi, uamuzi wa pamoja wa masuala muhimu ya kiukoo na wajibu wa
kulindana na kutunziana siri za ukoo.
Katika
kuangalia maudhui ya utendi huu tutajikita katika vipengele vya motifu,
dhamira na migogoro.
Motifu
Motifu
ya mtoto wa ajabu.
Kuna
Motifu ya mtoto wa ajabu ambaye ni Rukiza. Amezaliwa katika mazingira ya ajabu.
Alikuwa anaongea akiwa tumboni mwa mama yake amemlazimisha mama yake
amtayarishie vitu fulani kabla hajazaliwa na anamlazimisha mama yake amzae. Hii
inajidhihirisha katika mishororo (20-22, 40-45 70-71). Karibu nitazaliwa,
ndimi Rukiza, Jina langu niite Rukiza
Motifu
ya mtoto wa ajabu inaelezewa pia katika mishororo ya (70-139). Kwa kuangalia mishororo hiyo
hapo juu tunaona kuwa Rukiza ni mtoto wa ajabu, kwa sababu ana matendo ya ajabu
ambayo hayatarajiwi kufanywa na mtoto wa umri wake. Hii imepelekea jamii yake
ya Baganga kusema:
87: Wakasema, Huyu si mtoto, tumeona kioja!”
Hii ni kutokana na matendo
aliyoyafanya ambayo si kawaida.
Motifu ya Safari
Hii
inajidhirisha katika utendi huu, kwa safari ya Baganga walipokuwa wakitoka
Kaskazini mwa Uganda kuja Karagwe kwa ajili ya kutafuta malisho ya ng’ombe wao.
Inaelezwa kuwa Baganga walivuka mto kuja Kaskazini mwa Karagwe.
Motifu
hii ya safari inapelekea kuwa na motifu ya msako ambapo jamii ya Baganda
inasafiri ikisaka malisho ya ng’ombe wao na makazi yao kwa sababu kule
walikotoka kulikuwa na njaa na ukame. Hii inajidhihirisha katika mishororo ya
(136-162).
136;
Akasema ,Nibebeni turudi kwetu
137:
Baganga wakambeba mtoto
138:
Siku hiyo Baganga wakambeba mtoto
139:
Tukakongozana nyianyianyia!
141:
Tukafika kwenye ziwa la chumvi
161:
Nikaona wamemvusha Rukiza
162:
Akaja kwao Byantazi
Katika
safari yao ya kusaka malisho na makazi bora, tunaona kuwa walifanikiwa kufika
Byantazi ambapo walipata neema kama inavyodhihirisha katika mishororo ya
(170-174).
170:
Wakatamalaki na kumjenge kitala
171:
Ukawa ufalme kama falme nyingine
173:
Baganga wakapona ufukara
173:
Wakanywa maziwa yakawashinda
174;Mengine
wakayamwaga katika ishazi
Dhamira
Dhamira
kuu katika utendi wa Rukiza ni mgogoro uliosababishwa na ujenzi wa himaya
mpya ambayo imeleta mgogoro wa
kihistoria na wa kitabaka kati ya mifumo miwili yaani, mfumo wa kijadi /
kiukoo na mfumo mpya wa kifalme wa dola
inayoinuka. Mgogoro huo ni wa kimfumo aamabapo kuna mapambano ya kiukoo
inayowakilishwa na Ruhinda na ule wa kifalme unaowakilishwa na Rukiza.
Dhamira nyingine ndogondogo zilizojitokeza ni kama zifuatazo:
Usaliti: Hii inajitokeza pale ambapo binti Rukiza alivyomsaliti baba yake kwa
kutoa siri kuhusu nguvu zinazomlinda baba yake. Siri hiyo anapewa mfalme
Ruhinda ambaye anapanga njama za kumwua Rukiza. Uvujaji wa siri hiyo
unasababisha kuuawa kwa Rukiza. Hii imeonekana katika mishororo (598-629).
Usaliti
mwingine unajitokeza pale ambapo Kilokote anapomsaliti mfalme Rukiza wakati
alipotumwa kupeleka salamu kwa Ruhinda alimtaka ashiriki katika ufunguzi wa
nyumba Byantanzi hapa anatoa maelezo ambayo hajatumwa. Hii imeonekana katika
mishororo ya (335-349).
335:Ewe mtukufu, mimi nilifika kwa Rukiza
336: Nikiwa na ng”ombe wangu magana sitini
337: Akaninyang”anya na kuwachukuwa
338: Ameleta halaiki ya watoto wa kwao
339: Na kuwajaza katika uwanda mzima
345: Nyumbani kwa rukiza inachezewa na watoto
346: N samli laini inakandikwa viambazani
347: Anasema yeye ni mfalme kama wewe
348:Hakutaaadhimishi bali anakuamkua
349:
Hata kigoda anakalia cha mapembe
Sihiri
Katika
utendi wa Rukiza suala la sihiri limeonyeshwa kwa kiasi kikubwa kwani kuna
matumizi ya uganga katika kuwezesha mambo fulani kufanyika. Hii
inajidhihirisha pale ambapo Ruhinda
alitaka kujua asili ya nguvu za Rukiza na Rukiza alipokataa binti yake kuolewa
na Ruhinda. Wakaona kwamba njia pekee ya
kufanya hilo lifanikwie ni kumwita mbashiri. Huu inajidhihirisha katika
mishororo ya (533-595).
533: Ruhina akasema, ‘Niiteni
mbashiri wangu”
535: Mfumu huyo alikuwa akiishi
Byantazi
536:
Wakakamata kuku Mchakuraju-Mkeshaji
537: Wakapiga ramli, utumbo wa kuku ukawa mweusi
538: Wakapiga ramli bila mafanikio
581: Tumetakasa Ndumba -Ahamari
582: Kaya yote ya Rukiza ihamishwe
583: Tumetakasa Ndumba Paramizi
584:
Kaya yote ya Rukiza iparamiwe!
586:
Mpe mwali ndumba hizi
587:
Azitundike kwenye nguzo tatu za kilele
588:
Akikuuliza unamzindika kitu gani
589:
Mjibu kuwa umemzindika dhidi ya mapepo ya mizimu ya kwao
Sihiri
au suala la uganga linatokana na imani kwamba ili kufanikisha jambo fulani ni
lazima utumie sihiri. Katika utendi huu,
ukiwa mmojawao wa tendi za Kiafrika, mashujaa wengi husaidiwa na nguvu za
sihiri pamoja na miungu yao. Mfalme Ruhinda alifanikiwa kumshinda Rukiza kwa
sababu ya kutumia sihiri ambayo ilifanya binti kutoa siri za nyumbani kwao hasa
siri ya nguvu za baba yake.
Dhamira ya kulipiza kisasi
Kulipiza
kisasi kilitokea kati ya mfalme Ruhinda na Rukiza ambao walikuwa katika mgogoro
mkali uliosababishwa na Kilokote ambaye alitoa taarifa za ugombanishi aliporudi kutoka ikulu ya
Ruhinda. Aliporudi kutoka Ikulu Rukiza akamuuliza mfano katika mishororo ya
(405-418)
Rukiza
alikasirishwa na maelezo yaliyotolewa na Kilokote akapanga kwenda Ikulu kumuona
Ruhinda. Hii inaonyeshwa katika mishororo ya 427-429
Katika
utendi huu ulipizaji wa kisasi unajitokeza pale ambao mshikamano wa kiukoo
unadai ulipizaji kisasi iwapo mwana koo mmojawapo anadhulumiwa au kuawa. Kanuni
inayotawala katika utendi huu ni jicho kwa jicho. Hii inaidhihirisha pale mfalme
Rukiza anapouawa inabidi binti yake
alipize kisasi kwa kumuua Ruhinda. Hii inajidhihirisha katika mishororo ya
679-683
Dhamira ya uzazi
Hii
imejitokeza kwenye mshororo wa 181-184 na 200-205 katika mishororo hii suala la
uzazi inaonyeshwa pale Rukiza amekua akaoa na kuwa na familia, vile vile katika
mshororo wa 200-205 baada ya Rukiza kupata watoto. Hapa inaonesha jinsi uzazi
ulivyo muhimu.
Dhamira ya utabaka
unyanyasaji na dharau
Utabaka
umeonyeshwa kwa kiasi kikubwa katika utendi huu. Kwani jamii hii ya Baganga
imegawanyika katika matabaka mawili tabaka la kifalme na tabaka la watwana
ambalo ni la watu wa chini.
Mfumo
wa kiukoo wa Rukizia ni wa kitabaka Rukiza anatamba kuwa haitwi “Rukiza” bali
huuitwa Mwinyi na kwamba yuko radhi kufa kuliko kula takataka. Hii
inajidhihirisha katika mishororo ya (462-463).
462: Ni nani wewe uniitaye “Rukiza ?”
463: Hujui kuwa mimi huitwa “Mwinyi”
Kwa
kuwa Rukiza alikuwa mfalme yaani mtu wa tabaka la juu hakuweza kuchanganyika na
watwana. Inafikia wakati chakula wanachokula watu wa tabaka la chini. Kwa mfano
katika mishororo ya (16-18). Heri nijiue kuliko kula haramu. Kula mboga za
majani ya kunde na shiviga kula takataka zisanywazo na wajakazi.
Lakini
utabaka wa jamii hii haujakoma, bado unawezekana kwa mtwana kugeuzwa mwana-ukoo
kama inavyotokea kwa Kilokote ambaye ni mtwana. Kilokote ananusurika kufa kwa
sababu ya utwana wake, kwani watwana walikuwa wakitolewa kafara katika jamii
ile. Hali hii ya utabaka kwa kulitenga tabaka la chini inajidhihirisha kwa
maneno ya mwimbaji Habibu Selemani
ambaye kila wakati anatahadharisha hadhira yake ijihadhari na watwana.
Hali hii inaonyesha jinsi utabaka ulivyokuwa wa hali ya juu. Hii inajidhihirisha katika mishoro (303-308).
Lakini ogopeni mtwana!
Mzee Yoweli, muogope mtwana!
Kweli ogopeni kitwana kama mimi hapa!
Ha! Ha! Ha! Ha!
Yarabi maskini!
Lakini ogopeni kitwana!
Kutokana
na utabaka huo watwana ambao ni wa tabaka la chini walifikia hata kuawa kwa mfano mishororo
166-169.
Nipo alaipokutana na mtwana.
Akavuta upinde asubuhi na kumwua kwa mshale.
Watu wakauliza, “Rukiza, mbona umemwua mtwana?”
Akajibu,” Hiyo ni sadaka ya kaya yetu.
Pia
katika mishororo (206-209) inaelezea jinsi watwana wanavyoendelea kunyanyaswa
na kuonewa na kudharauliwa.
Tukakuta kitwana kimoja kimeanguka kichalichali
Kimejifunika uchi wake kwa vidole
“Hebu mwueni mtwana huyo!”
Toka, Rukiza atakuua!”
Mtwana
huyu aliponea chupuchupu baada ya kusema kuwa ana uhusiano na Rukiza. Hii inaonyeshwa katika mishororo (211-215)
mbona mimi ni mchale wa Rukiza.
Pia
utabaka unyanyasaji na dharau haviishii tu kwa watwana, inaendelea hata kwa
kabila ya Wanyambo. Kwa mfano katika mishoro ya (141-158) tunaona kwamba watu
hawa wananyanyaswa na kudharauliwa. Hii
inajidhihirisha kwa kuangalia matumizi ya “ki na vi”ambayo yanaonyesha
kudhalilisha mtu au kumdharau mtu. Kwa mfano:
Tukafika kwenye ziwa la chumvi
Tukakuta vinyambo
Vimekaa vinachunga mwaro
“Vinyambo nipisheni niende zangu!”
Vinyambo vikakataa, “oya”
Enyi vinyambo, “Tokeni nipite!”
Hapa
inaonyesha utabaka na dharau kwa tabaka la chini hasa watwana na Wanyambo.
Dharau na utabaka huo unajidhihirisha kwa matumizi ya kiambishi -ki ambacho ni cha awali cha nafsi
kinachoonyesha umoja. Dhana kubwa inayopatika hapa ni udogoshaji yaani kitu
kinashushwa hadhi.
Dhamira ya Mila na desturi
Katika
utendi huu kuna baadhi ya mila na desturi ambazo zimeonyeshwa. Kwa mfano
matambiko, hii inajidhihirisha katika mishororo ay 211-214. Hapa inaonesha mila
ya kuchanjiana ili kujenga undugu mbona mimi ni mchale wa Rukiza huyo Rukiza
mnayemzungumzia tujidumiliza tulichangiana kule Byantanzi tulipokuwa wadogo
tukichunga na ndama wa kijivu.
Mbona mimi ni mchale wa Rukiza?
Huyo rukiza mnayemzungumzia tumedumiliza
Tulichanjiana kule Byantanzi
Tulipokuwa wadogo tukichunga ndama wa kijivu
Pia
katika mila na desturi ilikuwa ni mwiko kutoa siri za familia kwani waliamini
kuwa inaweza kusababisha matatizo kwenye familia.
Kwa mfano tunaona pale Binti Rukiza alivyotoa
siri ya nguvu za baba yake kwa Ruhinda tunaona kuwa ilisababisha kifo. Pia
tunaona ilikuwa mila na desturi kuheshimu nyumba ya mfalme hasa jikoni kwa
mfalme. Ilikuwa ni mwiko kwa mtu kwenda au kupitia Buyondo yaani jikoni kwa
mfalme.
Migogoro
Mgogoro
mkubwa katika utendi wa Rukiza ule kati ya Rukiza na mfalme Ruhinda, ambao
umesababishwa na migongano ya mifumo ya kijamii unaowakilishwa na Rukiza na ule
unaowakilishwa na Ruhinda. Mgogoro huu unapelea kutokea kwa vita baina yao
baada ya kuchonganishwa na kitwana (Kilokote) ambaye alitumwa na Rukiza
kupeleka salamu kwa Mfalme Ruhinda naye akabadili maneno kwa kuongea uongo, mfano katika mshororo wa
144-158.
Mgogoro
mwingine ni kati ya binti Rukiza na mfalme Ruhinda. Baada ya Rukiza kuuawa na
mfalme Ruhinda bintiye Rukiza ambaye ndiye aliyesababisha kifo cha baba yake
baada ya kutoa siri tunaona Binti Rukiza
anachukua kisu na kumuua mfalme Ruhinda
rejea katika mishoro ya (645-685).
Vilevile
katika utendi huu kuna migogoro mwingine midogo midogo kwa mfano mgogoro kati
ya Rukiza na Vinyambo, mishororo ya (144-158) pale Vinyambuo walipofushwa macho
baada ya kumzuia Rukiza kuvuka ziwa Chumvi alipokua akielekea Byantanzi.
Pia
kuna mgogoro kati ya Kitwana (Kilokote) na mfalme Ruhinda, baada ya Kilokote
aliyekuwa mtwana wa Rukiza kutumwa kwa
mfalme Ruhinda naye badala ya kupita katika lango kuu akatoboa ua na kuingia
ndani ya miliki ya mfalme na kusababisha mfalme Ruhinda kuchukia mfano
mishororo ya (369-379).
Mgogoro
mwingine uliojitokeza ni kati ya Rukiza na Kitwana Kilokote ambapo Kilokote
alipiga kelele na kuwatisha watoto wa Rukiza ambapo walitetemeka kwa hofu na
kuutisha baba yao mfano katika mishororo ya (206-239).
Kwa
hiyo migogoro iliyoibuliwa katika utendi huu ni kwa lengo la kuonesha utabaka
uliokuwemo katika jamii pamoja na ushujaa ulivyojidhihirisha kulingana na nguvu za sihiri zilizoambatana na maajabu mengi.
Uhusiano wa utendi wa
Nyakiruukibi na tendi nyinginezo
Mfalme Edipode/FUMO
LIONGO(ulijali)RUKIZA(DUMILIZA)
Hii inahusiana na utendi wa
Nyakiirukibi katika suala la mtoto wa balaa(nuksi)Edipode mwenyewe alitabiliwa
na baba yake kwamba atakuwa mtoto wa nuksi na ndio maana akaenda kutupwa
Kwa
ufupi tunaweza kusema kuwa utendi wa Rukiza una uhusiano mkubwa na tendi
nyingine za Afrika kwani inafuata ruwaza au sifa za tendi za Kiafrika ambazo ni
ruwaza ya shujaa ambaye anatoka katika tabaka la juu, mwenye ujasiri nguvu za
sihiri urijali na anayeungwa mkono na watu. Tendi hizo nyingine za kiafrika ni
kama vile Silamaka, Mwindo, Lianja na Sundiata. Mfanano huu pia unajidhihirisha katika maudhui
kwani tendi nyingi za Kiafrika zinazungumzia masuala ya migogoro, usaliti, mila
na desturi za Kiafrika na dhamira nyinginezo.
Uhusiano
huu pia unapelekea tendi nyingi za Kiafrika kufuata fomula au ruwaza ya USHUJAA
= Ushakii + Sihiri + watu.
Utendi wa Silamaka
Ukiangalia
utendi wa Silamaka, ni utendi unaoelezea mapambano makali kati ya Silamaka na
Maadui zake yaani Wasegou. Alikuwa mtoto a mfalme wa Fula na alisaidiana na
mtumishi wake Pullori ambao walikuwa pamoja. Hatimaye Silamalamaka anauawa na
albino kama ilivyotabiriwa.
Utendi wa Sundiata
Katika
utendi wa Sundiata, Sundiata alizaliwa kiwete na mwenye matatizo mengi na
alikuwa hana nguvu. Baadaye alikuja
kupata nguvu akawa askari mashuhuri aliyeongoza mapambano ya kijeshi na akashinda. Alipambana na mtu aliyeitwa Sujmunguru ambaye
anatafuta siri ya kumuua Sundiata anashindwa kuipata sihiri inafanya kazi kuba
sana katika utendi wa Sundiata. Tunaona baadaye Sundiata anashindwa na
Sumanguru baada ya siri ya nguvu zake kujulikana.
Utendi wa MwindoKARATASI/
Katika
utendi huu kunakuwa na mapambano kati ya mtoto na baba yake, Mwindo
(Kabutwakunda) ambaye ni mtoto wa ajabu aliyetembea baada ya kuzaliwa ambaye
anaongea akiwa bado tumboni mwa mama yake na anatembea mara tu alipozaliwa. .
Utendi huu wa Mwindo unahusu motifu ya mtoto wa ajabu. Huu unahusiana kwa kiasi
kikuba na Utendi wa Rukiza kwa sababu zote zinaelezea motifu ya mtoto
wa ajabu.
Utendi wa Lianja
Lianja
ni utendi wa Kongo ambao unahusu kabila
la Wamongo. Lianja anashirikiana na dada
yake kuongoza Wamongo.Lianja amezaliwa katika mazingira ya ajabu yeye anatumia
viumbe mbalimbali katika kupambana.
Baada
ya kuangalia baadhi tendi za Kiafrika, ni dhahiri kwamba tendi hizo zina
husiana kwa kiasi kikubwa sana kwani zinafuata ruwaza ya ushujaa ambayo ni
ushujaa ushakii + sihiri + watu. Ila kwa kiasi kikubwa sana Utendi wa Rukiza unafanana na
utendi wa Mwindo.
Hitimisho
Kwa
kuhitimisha tunaweza kusema kuwa utendi huu ni wa kijadi ambao unazungumzia kwa
kina tawala za kijadi za Wahaya huko Kagera
hasa wilaya ya Karagwe. Ujadi huo unaendana na ufungaji pamoja sihiri
zinazowawezesha wafalme kufanikisha mambo yanayoyapangwa ili kuweza kupata
ushujaa. Kwa vile utendi huu unahusu jamii ya Wahaya ndio maana kuna maneno ya
kijadi ya Kihaya ambayo yametafsiriwa
ili kurahisisha uelewaji kwa wasomaji.
Kimsingi,
utendi huu unahusu itikadi ya kitabaka ya kijadi ya jamii zinazohusika,
ontolojia ya jamii hizo kuhusu maisha na mipaka ya uwezo wa mwanadamu, na
mtazamo wa jumla wa jamii hizo kuhusu udugu na ushujaa. Pia unaakisi mgongano
wa kihistoria uliokuwapo kati ya mifumo ya kijamii na kati ya matabaka
yanayoiwakilisha. Utendi huu unaeleza kuwa, kwa mtazamo wa kijadi kuhusu
ushindi wa jambo lolote unategemea nguvu za sihiri. Hata hivyo nguvu za sihiri
zinazidiana ndio maana Ruhinda kwa kutumia wafumu (waganga) aliweza kumwua
Rukiza kwa vile alitegemea nguvu za mazindiko yake aliyokuwa ameyaweka katika
sehemu tofauti tofauti katika mazingira yake yaliyoishi. Mwishoni tunaweza
kusema kuwa mtu wa karibu ndani ya familia anaweza akakutenda jambo baya sana kwa
kutoa siri na kukusaliti kama ilivyo kwenye utendi huu. Kwa hiyo utendi huu
unafundisha
kwamba siyo vizuri kutoa siri za familia kwani inaweza kuleta madhara.
MAREJEO
Finnegan,
R. (1970) Oral Literature in Africa. Clarendo Press, Oxford
Mulokozi,
M.M (1996) Fasihi ya Kiswahili :Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
Wamitila
K.W (2003) Kamusi ya Fasihi Istilahi
na Nadharia : Focus Publication Ltd
Mulokozi,
M.M (2010) Utendi wa Rukiza :Tendi Simulizi na Andishi za Kswahili
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com