Flower
Flower

Sunday, January 26, 2020

Umuhimu wa Muktadha katika mawasiliano


                             
Dhana ya mawasiliano ni pana zaidi ya lugha, ingawa lugha ndio msingi wa mawasiliano katika jamii, King`ei (2010:72). Mtaalamu huyu anafafanua kuwa mawasiliano yanaweza kufanyika kwa kutumia lugha lakini kuna njia mbalimbali ambazo jamii hutumia kufanya mawasiliano kama vile ishara. Aidha Matinde (2012:3), akifafanua dhima ya lugha kuwa ni kuwasilisha dhana au mawazo yaliyo akilini, vilevile humsaidia mtu kuuliza, kueleza mabo fulani na hata kubadilisha mawazo. 

Aidha Luhmann (2008), anafafanua mawasiliano kuwa ni njia ambayo huusisha mfumo wa jamii. Anaendelea kusema kuwa mawasiliano huusisha ujumbe, taarifa na uelewa wa mtu katika kufasili ujumbe huo. Hivyo katika fasili ya Luhman tunaona kwa fasili hii haijaweka bayana mifumo hiyo ambayo inahusika katika mawasiliano.

Hivyo basi mawasiliano ni hali ya kufikisha ujumbe, mawazo, mtazamo, fikra, hisia na kupashana habari mbalimbali kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa njia mbalimbali kama vile mazungumzo, maandishi, ishara, na kadhalika.

Muktadha ni ile hali inayotawala na kuelekeza kitendo cha matumiazi ya lugha, King`ei (2010:77). Aidha anaendelea kusema kuwa mahali, wakati, hadhira, matakwa na hata sifa nyinginezo za kimazingira, hali ya unenaji na kadhalika. Sambamba na fasili hii, muktadha kwa ujumla ni dhana pana ambayo inazingatia mambo mengi kama vile hadhira, muda, eneo, mtindo na mengine ambayo hupatikana wakati wa utumiaji wa lugha katika mawasiliano.
Ni kweli kuwa, muktadha ni kipengele muhimu sana kinachoathiri matumizi ya lugha, vilevile muktadha ni muhimu kwani ndio unaomlazimisha mzungumzaji kuteua lugha mwafaka ili kukidhi haja ya mawasiliano yake, King`ei (2010:18,78).  Akimaanisha kwamba, mtu huteua namna fulani ya uzungumzaji ama utumiaji wa lugha kulingana na muktadha aliyopo. Kwa mfano mtu huteua maneno ama msamiati kulingana na mada, uhusiano, umri, mazingira, wakati, hadhira na kadhalika. Endapo mtu asipozingatia muktadha husababisha mawasiliano yasiwe thabiti au asieleweke vyema.

Aidha Habwe na wenzake (2016:71), wakifafanua suala la sajili kuwa ni mtindo  kutumia lugha ambao hukubalika kimatumizi na ambao huonyesha sura mbalimbali za muktadha wake wa matumizi kama vile wahusika, matilaba na mandhari/ ama ni mtindo wa lugha ambao hutumika katika muktadha mahususi.

Mawazo ya wataalamu hao yanawiana sana na mawazo ya King`ei (2010:71,72) na Matinde (2012:3), ambao wanadhihirisha kuwa utumizi ya lugha kama nyenzo mojawapo inayotumika katika mawasiliano ya wanajamii katika kufikisha habari, mawazo, mitazamo, ujumbe miongoni mwao ni sharti au muhimu uzingatie muktadha wa utumikaji. Hivyo basi, ni dhahiri kuwa, mawasiliano baina ya mtu na mtu, jamii ama kundi fulani la jamii hutawaliwa kwa kiasi kikubwa na muktadha na usipozingatiwa mawasiliano hayaweza kufanikiwa ama kuwa thabiti.

Baada ya utangulizi huo, ufuatao ni ufafanuzi wa namna gani kipengele cha muktadha kikizingatiwa hufanikisha mawasiliano na kwa namna gani usipozingatiwa hushindwa kufanikisha mawasiliano.  

Muktadha ukizingatiwa husaidia kuteua mtindo wa kuwasilisha taarifa au ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira, jamii au mtu husika. Mtindo ni jinsi mtu ambavyo hutumia lugha kujieleza, Habwe na wenzake (2016:4). Anaendelea kusema kuwa “Mtu huweza kubadilisha mtindo wa lugha kulingana na hadhira, aina ya matini, uhusiano,tabaka, hali, mada na matilaba”. Pia Mwansoko (1994:22), akifafanua muktadha katika kipengele cha taaluma ya uandishi wa marejeleo, kuwa mtu hufuata utaratibu maalumu wa uadishi kulingana na muktadha husika, vivyo hivyo katika lugha ya mazungumzo mtu hufuata namna fulani ya kuwasilisha ujumbe ama taarifa kwa jamii kulingana na hadhira inayohusika. Kwa mfano;
i)                   Bibi: Hadithi hadithi!
Wajukuu: Hadithi njoo, uongo njoo, utamu koleaa!
Bibi: Hapo zama za kale…..!
Katika mfano huo, tunaona kwamba “Bibi” ameteua mtindo wa masimulizi ili kufikisha ujumbe kwa hadhira ambayo ni “Watoto”, ni mbinu au mtindo ambao hautawachosha watoto na kuwafanya waelewe ujumbe uliokusudiwa ni suala ambalo lingetofautiana na “Bibi” kuwasilisha ujumbe kwa watu wazima.

Vilevile muktadha ukizingatiwa vyema huimarisha uhusiano uliopo miongoni mwa jamii kulingana na namna ambavyo wanajamii wanaitumia lugha kuwasiliana. Matumizi ya lugha, hasa pale watu wanapokutana ana kwa ana ni chombo mahususi cha maingiliano katika jamii kama vile mazungumzo, mafunzo, maamkizi, mijadala, kupongeza, mahojiano, kutongoza na hata kutambulisha, King`ei (2010:71). Mawazo haya yanashadidiwa na mawazo ya Matinde (2012:4), kuwa watu wanapozungumza lugha moja huweza kuwasiliana, hali ambayo hubainisha maelewano baina ya watu hao. Anaendelea kusema kuwa lugha huwafanya watu wajihisi wako pamoja na wenzao, kwa mfano maamkizi ya asubuhi, adhuhuri na jioni ambayo tumezoea ni hali ambayo husaidia kuendeleza na kudumisha mahusiano mema baina ya wanajamii. Kwa mfano;
i)                   Baba: Umeamkaje mwanangu?
Mtoto: Nimeamka salama, shkamoo baba!

ii)                 Ramadhani: Ndugu yangu, habari ya wakati huu!
Rashidi: Salama kabisa, habari za huko utokako!
Ramadhani: Ewalaa! Huko ni njema!
Rashidi: Familia nayo?
Ramadhani: Familia ni njema kabisa, ya kwako je!
Rashidi: Tunamshukuru Mwenyezi Mungu tuwazima!
Ramadhani: Basi vyema ndugu, kawasalimie sana!
Katika mifano hiyo, tunaona ni namna ya maamkizi yanayotumiwa sana katika jamii ya Waswahili. Matumizi hayo hutumiwa na jamii lengo likiwa ni kujuliana hali na kupitia matumizi hayo watu hudumisha upendo miongoni mwao. Vilevile matumizi kama ya mfano wa kwanza (i) huzingatia heshima, adabu, au nidhamu inayotegemewa katika jamii ya Waswahili, King`ei (2010:72). Hivyo ni dhahiri mtu akizingatia muktadha hasa katika uhusiano wa mtu na mtu uhusiano wao hudumu na kuimarika, vilevile mawasiliano yao huwa thabiti.

Pia, muktadha ukizingatiwa husaidia katika uteuzi mzuri wa maneno na utumizi wa lugha bora ya mawasiliano miongoni mwa wanajamii,  kama vile matumizi ya tafsida badala ya maneno ambayo kwa namna moja ama nyingine si faafu katika muktadha fulani wa matumizi ya lugha katika mawasiliano, kwa mfano;
i)                   A: Nani Kongoro?
B: Mimi hapa!
ii)                 A: Nani Ngurume wali?
B:Mimi Nguruwe wali!               King`ei (2010:98).

iii)               A: Unakwenda wapi?
B: Nakwenda Msalani!
A: Mh  kila mara!
B: Ile ilikuwa haja ndogo, hii haja kubwa!

Katika matumizi hayo ya maneno au lugha kulingana na mazingira, uteuzi huo ni sahihi na hautegemewi kukutwa katika mazingira mengine. Aidha ni dhahiri utumiaji huo katika muktadha huo mawasiliano hayo huwa thabiti na ujumbe hufika kama ilivyotarajiwa na kila mmoja huelewa, lakini endapo uteuzi huo utatumika sehemu ama mazingira tofauti kama vile ofisini si rahisi kueleweka na mawasiliano huvunjika. Pia, maneno kama msalani, haja kubwa na haja ndogo ni maneno ambayo huteuliwa lengo kuondoa ukali wa maneno ili kulinda heshima na nidhamu, kutokana na muktadha na wahusika waliopo katika mazingira hayo.

Muktadha ukizingatiwa husaidia ujumbe kufika kiurahisi na kueleweka kwa haraka katika jamii.  Wazungumzaji na wasikilizaji wa lugha huelewana kwa kufahamu kaida za matumzi ya lugha au uteuzi wa lugha inayofaa kulingana na mazingira/ muktadha, Mekacha (2011:57). Mtaalamu huyu amejaribu kufafanua kwa namna gani muktadha humsaidia mtu kufikisha ujumbe kwa haraka endapo akizingatia muktadha hasa kipengele cha mazingira, kwa mfano Mchungaji wa Kanisa akitumia muktadha usio sahihi kuhubiri basi ujumbe wake hautafika haraka endapo akitumia muktadha sahihi kama vile kanisani au viwanja maalumu. Kama vile;
A)    Katika chombo cha Usafiri.
i)                   Mchungaji: Tusimame tumsifu Bwana!
Abiria: Kimya!
ii)                 Utingo: Dereva kula Kichwa!
Dereva: Mwepesi huyo fanya chap!
Katika mazungumzo hayo, tunaona mfano wa (i) Mchungaji hajazingatia muktadha na ujumbe wake si rahisi kueleweka na kutekelezeka kwani muktadha huu hauwaruhusu watu kutekeleza agizo kama wanavyofanya waumini wakiwa kanisani, lakini katika mfano wa pili mazungunmzo kati ya dereva na utingo ni rahisi kueleweka na kutekelezeka kwani mazingira hayo huwaruhusu kutumia namna hiyo ya uzungumzaji na kuelewana yaani “Mwepesi ni abiria asiyekuwa na mzigo wowote ule” na “Kichwa ni abiria”. Hivyo basi mawasiliano haya huweza kuwa thabiti pale ambapo ujumbe ukifika kwa hadhira kama ilivyokusudiwa.

Vilevile muktadha ukizingatiwa husaidia kujua ama kuteua mada gani ya kuzungumza kulingana na hadhira, muda, uhusiano na kadhalika. Mada ni kiini cha habari katika mazungumzo, TUKI (2004). Kwa kawaida mada inayozungumzwa hutegemea ursmi wa mazungumzo na muktadha, Hamad (2015:15-16). Anaendelea kusema kuwa mada rasmi huzungumzwa katika muktadha rasmi na mada zisizo rasmi huzungumza katika muktadha usio rasmi. Hivyo basi katika utumizi wa lugha katika suala la mawasiliano muktadha ni muhimu kuzingatiwa ili kusaidia namna gani ya kuwasilisha mada fulani au mada ipi ya kuzungumza na wakati gani, kwa mfano;
A: SARUFI YA KISWAHILI. (MADA)
i)                   Mwalimu Majura: Fonimu kama tukio la Kisaikolojia ni……tunaelewana?
Kidato cha nne: Hapana!
Katika mfano huu, mwalimu hakuzingatia hadhira yake katika uwasilishaji wa mada yake kwani ni hadhira ambayo haiwiani na namna ambavyo mwalimu ameiwasilisha kulingana na kiwango chao cha elimu. Hivyo basi mawasiliano baina ya mwalimu na mwanafunzi ni magumu.

Halikadhalika muktadha ukizingatiwa husaidia kubaini utambulisho wa mtu na uhusiano miongoni mwa wanajamii. Lugha siyo tu kipengele muhimu katika utambulisho bali pia lugha ina utambulisho umefungamana na jamii ambamo mzungumzaji ni sehemu yake, Msanjila (2011:48). Hivyo kupitia mazungumzo ni rahisi kumtambua mtu kijinsi, kitabia, hadhi, cheo, dini, umri na kadhalika. Suala hili husaidia kujua namna, nini, wapi na lini uzungumze na mwanajamii fulani ambaye tayari kutokana na mazungumzo yake ya awali yaliyomtambulisha.
i)                   Hamisi: Muheshimiwa, vipi umekwisha andaa ripoti?
Ezekieli: Ndiyo, na sasa naepeleka makao makuu!
Mazungumzo hayo huweza kuwatambulisha kuwa hawa watu (Ezekieli na Hamisi) ni viongozi, hivyo mtu mwingine ama msikilizaji anyehitaji kuzungumza na hawa atateua namna ya utumiaji wa lugha ambao utamsaidia kuwasiliana kutokana na hadhi wa walengwa wake. Hali hii hufanya mawasiliano kuwa thabiti kwani mtumiaji wa lugha atazingatia utambulisho maalumu wa walengwa wake.

MAREJELEO
Habwe, J.A na wenzake (2010). Darubini ya Isimujamii kwa Shule na Vyuo.   
                                 Nairobi : Phoenix Publisher Ltd.
Hamad, K. J. (2015). Tofauti za Matumizi ya Lugha katika Miktadha mbalimbali ya                                                  Mazungumzo. Kioo cha Lugha Juzuu 14, 15-16.
King’ei, K. (2010). Misingi ya Isimu jamii. Dar es Salaam: TUKI.
Luhmann,N. (2008). Theory of Society. Vol. 1. Stanford University Press.
Matinde, R. S.  (2012). Dafina ya Lugha, Mwanza: Serengeti Publisher`s Limited.
Mekacha, D. K. (2011). Isimujamii: Nadharia na Muktadha wa Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI.
Msanjila  Y.P. na wenzake (2011). Isimujamii: Sekondari na vyuo; Dar es Salaam, TUKI.
Mwansoko, H. J. (1994). Mitindo ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam:
TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.










                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                   













No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny