Dhana ya mazungumzo imefasiliwa na
wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo; TUKI (2014) wanaeleza mazungumzo ni jambo
linalojadiliwa na watu au kikindi cha watu kwa lengo fulani. Pia Kamusi Pevu ya
Kiswahili () inaeleza mazungumzo kuwa ni hali ya kubadilishana maoni au maneno
kuhusu jambo au suala fulani.
Vilevile BAKITA (2015) wanatoa fasili
mbili kuhusu mazungumzo kwa kusema kuwa ni mkutaniko wa watu wawili au zaidi
wanaongelea jambo fulani. Au mazungumzo ni jambo linaloongelewa na watu wawili
au zaidi kuhusu suala fulani. Matei (2011) anaeleza kuwa mazungumzo ni maelezo
ya mdomo kwa lugha ya kawaida kuhusu suala lolote. Kwa maana hiyo yanaweza kuwa
rasmi au siyo rasmi.
Kwa ujumla mazungumzo ni jambo au maelezo
yanayojadiliwa na watukwa lugha yanayohusisha pande mbili au zaidi kwa lengo
fulaniama huhusu suala lolote. Mazungumzo yanaweza kuwa rasmi au siyo rasmi.
Pia utanzu wa mazungumzo umejadiliwa na
wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo; Mulokozi (1996) anaeleza, mazungumzo ni
maongezi au maelezo ya mdomo, katika lugha ya kawaida juu ya jambo lolote lile.
Si kila mazungumzo ni fasihi. Ili mazungumzo yaitwe fasihi, lazima yawe na
usanii wa aina fulani, yaumithilishe uhalisi badala ya kunakili. Anaendelea
kusema kuwa hali hii hujidhihirisha katika lugha, katika muundo na mtirirko na
mazungumzo yenyewe na katika namna yanavyotolewa kwa mfano, maongezi ya wazee
katika baraza, hotuba zinazotolewa katika mazingira rasmi ya kimila ( wakati wa
kuposa ) na malumbano ya watani.
Matei (2011) anaeleza kuwa mazungumzo huwa
fasihi pale ambapo yanadhihirisha usanii wa aina fulani; pale ambapo yanaeleza
ukweli kwa namna ambavyo hayaunukuu tu moja kwa moja, bali yanaueleza kwa
ubunifu. Katika kuzungumzia tukio la kawaida, mtu anaweza kufinyanga lugha kwa
njia isiyo ya kawaida. Mazungumzo ya aina hii huwekwa katika fasihi simulizi.
Kwa ujumla utanzu wa mazungumzo ni aina ya
sanaa inayotumia lugha yenye ubunifu na kuwasilishwa kwa njia ya mdomo baina ya watu au kikundi cha watu
fulani kuhusu jambo lolote. Mfano hotuba, mawaidha na malumbano ya watani.
Baada ya kuangalia namna dhana ya
mazungumzo na utanzu wa mazungumzo zilivyojadiliwa na wataalamu mbalimbali,
turejee kwenye kiini cha swali hili kwa kuonesha namna Mulokozi (1996) na Matei
(2001)walivyozianisha tanzu hizo kisha tutaonesha namna walivyotofautiana na
kufanana katika kuzianisha.
Mulokozi (2017:56) akimnukuu Kobia (2006)
ameainisha utanzu wa mazungumzo na vipera vyake kama vile, malumbano, ulumbi,
soga na mawaidha. Aidha Mulokozi (1996) ameainisha utanzu wa mazungumzo kama
kundi lenye nui ya hotuba yenye tanzu na mikondo mbalimbali. Uainishaji huo ni
kama ifuatavyo;
Utanzu wa hotuba; Ni mazungumo rasmi
ambayo huwasilishwa kwenye vikao rasmi vya kimila, kisiasa na kidini. Hotuba
rasmi hutolewa na watu maalumu wenye uzoefu na umilisi mkubwa wa lugha. Hotuba
hizo hupangiliwa kimantiki na hutolewa kisanaa kama vile, matumizi ya methali. Kwa
mfano hotuba za Rais au hotuba yw kiongozi yeyote kuhusu jambo fulani.
Utanzu wa malumbano ya watani; Mulokozi
anafafanua kuwa mila ya utani imeenea sana katika makabila mengi ya Afrika
Mashariki. Aghalabu watani wanapokutana hutaniana kwa maneno na hata kwa
vitendo, huku wakizingatia masharti yanayotawala uhusiano wao wa kiutani kwa
mfano utani wa Wahaya na Wakurya, Wachaga na Wapare, Wasukuma na Wagogo
vilevile kuna utani wa mababu au mabibi na wajukuu, utani wa mashemeji, utani
wa makabila au kiukoo, utani wa wanarika na utani wa marafiki. Mifano ya utani
ni kama vile;
(i)
yeye ni mrefu mpaka
anauza njugu karanga kwenye ndege
(ii)
yeye ni mweusi mpaka
haumwi na mbu usiku.
Vilevile kuna utani baina ya kabila na
kabila kwa mfano utani wa Wahaya kwa Wakurya wakati wa msiba
Tweija kubalaba inywe abataina kantu, mwelizaliza
mwine njala. Kutuije tubatekele obujini obugali shana enjala kelewa mlalekeka
kulila. Waleba mwabulwa amahela gukugala enyama mwabanza kwita ente. Mbwenu
tulebe mkelatugola.
Katugende kushenya enku tubage ente yangu
eyomwaita tubatekele mulye mlekele kulila enjala. Katulaluga kushanaya enku
tuije kubatahila amanzi mwije mwoge, kumulamala mujwalege mulekele kwelizaliza.
Ente yomwaita itwe tutwikugyenda, ntuija kubabegila enzidi kuluya umuhigo,
enkoko ne mbata ne mbuzi mulye mugute olwokube ienjala niyo elikubaliza.
Tafsiri
Tumekuja kuwaona msio na kitu, mnalia tu
kwasababu ya njaa zenu. Ebu tuwapikie uji na ugali labda njaa zenu zikiisha
mtaacha kujiliza. Mmekosa hela ya kununua nyama sasa mmeuza tu ng’ombe, sasa
ngoja tuone kama atatutosha. Ngojeni twende tukachanje kuni tuje tuwachinje ng’ombe
wenu mliomnunua tuwapikie mle muache kulia njaa.
Tukimaliza kutafuta kuni twende kuwachotea
maji muoge na mkimaliza mvae nguo vizuri muache kulialia. Ng’ombe mliyemuua sisi
hatumhitaji, tutawachinjia kwengine toka zizini, kuku, bata na mbuzi mle mshibe
kwasababu njaa ndiyo inawaliza.
Kabila la Wakurya, Wahaya hujitokeza na
kuanza kutaniana na kumuita marehemu ng’ombe aliyeuwawa kwasbabu ya kukosa pesa
ya kununua nyama, hivyo matani yao huendelea hadi kufikia hatua ya kufanya
uharibifu vitu vingine kama kuchinja kuku mbuzi nk.
Utanzu wa ulumbi; ni uhodari wa kuzungumza
ambao huwa ni wa kifasaha na madoido. Kigezo kilichotumika katika kuainisha
utanzu huu ni kigezo cha kifani ambapo lugha iliyotumika ni ya kimadoido na
kiufasaha. Katika utanzu huu kuna ushawishi fulani ili kufanikisha jambo fulani
au unalotaka kupitisha. Kwa mfano habari zenu ndugu zangu wa damu, mimi ni
mjori wenu na nawapenda sana naomba mnikubalie niwe kiongozi wenu. Hii
inaonesha namna mzungumzaji anavyotumia vyema uhodari wake wa kushawishi ili kuwaaminisha
jamii yake kuwa yeye anaweza kuwa kiongozi.
Utanzu wa mizaha; Ni masimulizi mafupi ya
kuchekesha ambayo aghalabu hufanywa kupitishia wakati. Baadhi ya mizaha huwa ni
ya matusi. Baadhi ni kejeli au kebehi zenye kusaili tabia au matendo ya watu
fulani, hasa viongozi. Dhima ya mizaha ni kufurahisha na kuchekesha wahusika
hasa wawapo katika vikao visivyo rasmi na kukoleza mazungumzo.
Utanzu wa sala; Haya ni maombi ya msaada
wa kiungu katika utatuzi wa matatizo ya kimaisha ambayo muombaji kashindwa
kuyafumbua kwa uwezo wake mwenyewe. Mara nyingi maombi hayo huwa katika lugha
ya kisanaa yenye kutumia sana fomula na sitiari. Wakati mwingine hata nyimbo na
ushairi hutumiwa sala huweza kuwekwa katika mikondo mbalimbali kama vile dua,
maapizo na tabano.
Kwa upande wa mtaalamu Matei (2011),
amefafanua utanzu wa mazungumzo kupitia vipera vyake kama ifuatavyo;
Malumbano ya watani; Ni majibizano kati ya
watu wawili au makundi mawili ya watu kwa nia ya kutaniana. Ni mazungumzo
yanayofanywa kwa kutumia maneno ya mzaha ili kuleta ucheshi. Watu hutaniana kwa
kutumia lugha kwa ufundi na mtiririko maalumu. Kuna aina mbalimbali za utani
kama vile, utani wa mababu/ mabibi na wajukuu, utani wa marafiki, utani wa koo,
makabila au mbari, utani wa mawifi na mashemeji, utani wa marika na utani wa
maumbu.
Ulumbi; Huu ni uhodari wa kutumia lugha
kwa ufundi wa kipekee. Ni utumiaji wa lugha kwa mvuto na ufasaha. Ulumbi
humuwezesha mtu kulielezea jambo la kawaida kwa namna ambavyo linaonekana kuwa
kigeni kabisa na kuwashawishi watu kulikubali au kulipenda. Ulumbi umegawanyika
katika aina mbili ambazo ni ulumbi rasmi na ulumbi usio rasmi.
Hotuba; Ni maelezo au taarifa ambayo
hutolewa mbele ya hadhira kuhusu mada fulani. Kwakawaida, hotuba ni mazungumzo
rasmi na hutolewa katika vikao rasmi kama vile hafla za kisiasa, kanisani,
tamasha za muziki na kwenye mazishi, sherehe za kitamaduni, kortini(kabla jaji
hajatoa hukumu, anaweza kutanguliza hotuba) na kwenye harusi.
Mawaidha, Haya ni mazungumzo ambayo hutolewa
ili kumpa mtu ushauri au nasaha kuhusu jambo
fulani. Mawaidha hutoa muongozo na maelekezo ya kukubaliana na
changamoto katika maisha na jinsi ya kuhusiana na wanajamii. Mfano mawaidha ya
mama kwa mwanae, “kaa hapa mwanangu, ningependa tuzungumze”wakati huo mtoto
hufahamu fika kuwa hili ni jukwaa lingine, hali hubadilika sauti ya mama huwa
si ile ya kawaida. Hivyo haya ni baadhi mawaidha ambayo hutolewa katika
mazungumzo.
Soga: Ni mazungumzo yanayonuiwa kupitisha
wakati. Mazungumzo haya huchukuliwa kama fasihi yanapotolewa kwa usanii fulani
yakimithinisha uhalisia na badala ya kunakili. Katika soga, jambo la kawaida
linalozungumziwa hupigwa chuku na kufanywa lionekane kana kwamba halina
uhalisia. Aidha kimsingi soga hutumiwa kwa ajili ya kuchekesha, kuejeli,
kuchochea au kuumbua, kukebehi, kufanyia dhihaka nk. Kwa mfano,
Basi kizito Mtakuro alipewa cheo kikubwa
kazini kutokana na uchapakazi wake. Shirika alilokuwa akilifanya likawa na
matumaini makubwa, Kizito naye badala ya kuchapa kazi akawa anatamba na kujitapa
mtaani. “ukubwa ninaujua miye. Mimi ndiye Kizito hapa, Kizito mzito mimi,
akaringa. Akawadharau akina Wanjiku, Amina na Shikuku. Akajitosa kwenye raha bila
kujali akavaa suti nzito nzito alizoagiza kwa fedha za shirika.
Muda si muda shirika likaingia hasara.
Mwishowe ametimuliwa kazi na wazito wenyewe. Ameondoka na mkoba mzito wa madeni
na fedheha, nguo sasa anavaa matambara mazito. Jamaa uzito unakowapeleka wazito!
Hii ni soga jnayojidhihirisha katika utanzu wa mazungumzo kama Matei alivyoianisha
tanzu hii.
Maapizo; Ni maombi maalumu ya kumtaka
Mungu/miungu/mizimu kumwadhibu mhusika
hasidi, mkinzani au mwovu. Hivyo, maapizo ni dua ya laana au maombi
mabaya kutoka kwa mtu ambaye anahisi ametendewa wovu au amesalitiwa na
mwingine.
Baada ya kufafanua uanishaji wa Utanzu wa
Mazungumzo kwa mujibu wa wataalamu tajwa, hivyo swali linahitaji tubainishe
utofauti na ufanano wa Utanzu wa Mazungumzo kwa kuwarejelea wataalamu ambao ni
Mulokozi (1996) na Matei (2011). Kwa kuanza na utofauti wataalamu hawa
wametofautiana kama ifuatavyo;
Utofauti katika matumizi ya istilahi;
Mulokozi (1996:229-230) ametumia istilahi ya kundi la mazungumzo akimaanisha
utanzu wa mazungumzo ambapo ndani ya kundi hilo ameweka hotuba kama nui, ndani
ya hotuba ameainisha tanzu za mazungumzo kama vile hotuba, malumbano ya watani,
ulumbi, mizaha na sala, vilevile Mulokozi ametumia istilahi sala. Pia ametumia
istilahi ya mikondo iliyotumika katika tanzu ya malumbano ya watani na sala.
Lakini Matei (2011:135-144) ametumia istilahi utanzu wa mazungumzo na vipera
vya mazungumzo pia ametumia istilahi ya maapizo badala ya sala.
Utofauti wa idadi ya tanzu zilizoainishwa;
Mulokozi (1996:229-230) ameanisha tanzu tano ambazo ni hotuba, malumbano ya
watani, ulumbi, mizaha na sala. Kwa upande wa Matei (2011:135-144) ameanisha
vipera sita ambavyo ni malumbano ya utani, ulumbi hotuba, mawaidha, soga na
maapizo. Hivyo hii inaonesha kuwa Mulokozi yeye kwa upande wake hajataja soga.
Utofauti katika ubainishaji wa sifa za
vipera vya mazungumzo, Mulokozi (1996) hakuweza kubainisha sifa za kila tanzu
alizozianisha. Lakini Matei (2011) amefanikiwa kueleza na kubainisha sifa
za vipera vya mazungumzo
alivyoviainisha.
Ufuatao ni ufanano wa uainishaji wa utanzu wa
mazungumzo kwa mujibu wa Mulokozi (1996) na Matei (2011) katika kuanisha kwao;
Ufanano katika ufasili wa dhana; Katika
kufasili dhana ya utanzu wa mazungumzo wataalamu tajwa wote wamehusisha suala
la sanaa na ubunifu. Ili mazungumzo yawe fasihi ni lazima kuwepo na lugha yenye
ubunifu wa kisanaa kwa mfano matumizi ya ulumbi, nyimbo na methali mbalimbali.
Ufanano katika uainishaji wa baadhi ya
tanzu; Mulokozi (1996) ameainisha tanzu ya hotuba, malumbano ya watani na
ulumbi. Pia Matei (2011) ameainisha vipera ambavyo ni hotuba, malumbano ya
watani na ulumbi. Hivyo wamefanana katika uanishaji wa vipera au tanzu hizi.
Ufanano katika kuainisha aina za malumbano
ya watani; Mulokozi (1996) na Matei (2011) wote wamefanikiwa kuainisha aina za
malumbano ya watani kama vile utani wa mababu na mabibi na wajukuu, utani wa
mashemeji, utani wa kikabila na utani wa marafiki.
Kwa ujumla wataalamu tajwa wameelezea
utanzu wa mazungumzo lakini wanatofautiana katika uanishaji wa utanzu huo
kutokana na kukosekana kwa vigezo mahususi vya uainishaji wa utanzu wa
mazungumzo. Kukosekana kwa vigezo vya uainishaji imesababisha kila mtaalamu
kuwa na istilahi tofauti na mtaalamu mwengine kama vile Mulokozi ametumia neno
utanzu katika kufafanua aina za mazungumzo ya kifasihi na Matei ametumia
istilahi vipera. Hivyo kunatakiwa kuundwa kigezo mahususi cha uainishaji wa
mazungumzo ili kuepuka utofauti wa uainishaji wa utanzu huu.
MAREJELEO
BAKITA (2015). Kamusi Kuu ya Kiswahili.
Longhorn Publishers.Dar es Salaam.
Matei, Assumpt. K (2011). Fani ya Fasihi Simulizi kwa shule za Upili
Nairobi Kenya:Oxford Uversity Press.
Mulokozi, M. M (1996). Fasihi ya Kiswahili. Dar es salam: OUT
Mulokozi, M.M (2017). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: Moccony Printing
Press.
TUKI (2014). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.Oxford
University Press East Africa Limited. Nairobi, Kenya.
Wamitila, K.W. (2011). Kamusi pevu ya Kiswahili. Vide-Muwa
Publishers Limited. Nairobi, Kenya.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com