Flower
Flower

Sunday, October 13, 2019

NADHARIA YA UMARX KATIKA FASIHI

Nadharia ya umarx (marxism)
Kwa maana rahisi kabisa, tunapoongelea kuhusu nadharia ya U-Marx tuna maana ya kurejelea mikabala mbalimbali ambayo misingi yake mikuu ni mawazo yanayohusishwa na Carl Marx na Friedrich Engels.  Katika kitabu cha The Germany Ideology, Marx na Engels walisema kuwa kitu cha msingi katika maisha ya binadamu ni kula na kunywa, kupata malazi na mavazi na mambo mengine. Tendo la kwanza la kihistoria kwa hiyo ni kutafuta njia ya kuyakidhi mahitaji haya ya msingi. Ili kufanikiwa katika lengo hilo, binadamu hulazimika kujiunga pamoja au kuunda umoja ili kuimarisha umoja na wepesi wa kuizalisha mali ya kukidhi mahitaji hayo. Muungano huo huwa na ugawaji wa majukumu au kazi ambayo ndiyo msingi wa kuundwa kwa matabaka katika jamii. Hatua ya juu ya mwendelezo huu ni uzukaji wa mfumo wa ubepari. Katika mfumo huu, mali inamilikiwa na idadi ndogo ya watu. Watu hao wanaipata mali yao kutokana na unyonyaji wa umma na hasa wafanya kazi (Wamitila 2002:).

Kwa mawazo ya Marx,  maendeleo ya jamii huthibitika katika vipindi vya maisha ambavyo kizazi cha binadamu kimepitia. Kutokana na Marx tabaka la jamii hutoweka na lingine huchipuka kwa sababu ya mgongano wa kitabaka. Mgongano huu hutokea kwa sababu kuna tabaka la wanyonyaji na wanaonyonywa. Hivyo, inabidi kuwa na mapinduzi dhidi ya mifumo ya kuzalisha mali inayohimili unyonyaji. Mapinduzi yanayotokea baadaye yanaongeza tumaini la ujenzi na uimarishwaji wa jamii inayozingatia usawa. Marx anamwona binadamu kuwa kiini cha historia yote na matendo yote yanayotendeka humu duniani. Umarx unamwabudu binadamu, hivyo humpa tumaini binadamu la kungoa mizizi yote ya unyonyaji na unyanyasaji na kujenga ulimwengu wa kinjozi usiokuwa na madhila (Wafula na Njogu 2007). Vidato ambavyo jamii ilipaswa kupitia kabla ya kufikia ukamilifu wa kinjozi ni vifuatavyo: Ujima, Utumwa, Umwinyi, Ubepari, Ujamaa na Ukomunisti
Kwa jumla, twaweza kusema kwamba mhakiki wa Ki-marx hukita nadharia yake kwenye itikadi za Karl Marx na Fredrick Engels, na hasa kwenye madai ya hao wawili kuwa, katika tathimini ya mwisho kabisa maendeleo ya historia ya binadamu pamoja na taasisi zake, yatakuwa ni tokeo la mabadiliko katika njia za kimsingi za uzalishaji mali. Kwamba mabadiliko kama hayo husababisha mageuko katika muundo wa matabaka ya kijamii ambayo katika kila kipindi huendeleza kung'anga'aniwa kwa uwezo wa kiuchumi, kisiasa na kijamii; na kwamba dini, fikra na utamaduni wa jumuiya yoyote (zikiwemo sanaa na fasihi kwa kiwango fulani) huwa ni `itikadi' na miundo maalum ya `kitabaka' ambayo ni zao la miundo na matabaka ya kijamii yaliyomo wakati huo.

Umarx huchukulia kwamba jamii zote za kitabaka huzalisha mkururo wa miundo ya urazini inayokinzana na kushindana. Katika jamii ya kikapitolisti, kwa mfano, aina tofauti za mitizamo kuhusu maisha huwakilisha haja tofauti za kitabaka ambazo hutegemea hasa mikinzano kati ya mapato na nguvu za kutenda kazi. Kwa hivyo Umarx huhusisha itikadi na uzalishaji mali na jukumu lake katika mivutano ya kisiasa katika jamii. Jinsi watu binafsi wanavyoelewa msingi wa maisha yao hutokea kuwa kamba ya mvutano ambapo wanaweza ama kubadilika au kuendelezwa.
HOJA ZA UMARX KWA UFUPI

i/ Katika historia ya mwanadamu, jamii na mahusiano yake, taasisi zake namna yake ya kufikiri; mambo yote hayo hutegemea mabadiliko ya mfumo wa uzalishaji mali. Yaani jinsi uchumi, uzalishaji, mgawanyo na umilikaji mali unavyoendeshwa.

ii/ Mabadiliko ya kihistoria katika msingi wa uzalishaji mali yanaathiri mabadiliko ya muundo wa matabaka ya jamii, na hivyo hutokeza (kwa kila wakati) tabaka tawala na tawaliwa ambayo huwamo katika mapambano na harakati za kugombea uchumi, siasa na faida za kijamii.

iii/ Urazini wa mwanadamu umeundwa na itikadi. Imani, thamani ya kitu, namna za kufikiri na kuhisi. Ni kupitia hivi, mwanadamu huuona ulimwengu wake, na huelezea yale yaliyomzunguka na yale anayoyaona kuwa kweli.

Kwa hiyo wazo kuu la U-Marx ni kwamba hata waandishi wa mkondo huo huandika kwa kutumia falsafa ya Marx jinsi alivyoiona historia ambapo wazo kuu ni kuwa: harakati za matabaka ndio msingi mkuu unaofanya mambo yawe kama yalivyo.


Umarx katika Fasihi

  Usanii ni uumbaji wa Ukweli katika maisha.
  Ukweli unaooneshwa katika kazi za fasihi hiyo ni usahihi wa mambo katika jamii? Kama ni Riwaya, Tamthilia, Ushairi na kadhalika inawakilishaje ukweli?
  Kazi za kisanaa zinatakiwa kuonesha mivutano iliyopo katika jamii hasa kati ya wanyonyaji na manyonywaji. 

1 comment:

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny