Flower
Flower

Sunday, October 13, 2019

NADHARIA YA UMUUNDO KATIKA FASIHI

Nadharia ya umuundo (structuralism)
Umuundo ni nadharia inayojibainisha kwa kuangalia Ujumla wa uhusiano wa sehemu moja kwa nyingine katika kufanya kitu kizima. Kwa mfano muungano wa maneno hufanya sentensi na sentensi zikiungana zinaunda aya au onesho na onesho kuunda tamthiliya.
Ntarangwi (2004) anasema kuwa umuundo waweza kuelezwa kama mtizamo wa kitathimini ambao huzingatia zaidi miundo inayojenga kazi binafsi.
Mwasisi anayetajwa sana katika nadharia hii ni Ferdinard De saussure aliyependekeza mtizamo mpya kuhusu lugha. Kinyume na wataalamu wengine walioshughulikia historia na sura maalum za lugha fulani, Saussure alivutiwa na miundo inayohimili lugha zote, huku akijaribu kuonyesha kwamba lugha zote za ulimwengu zaweza kutathiminiwa kwa kaida maalum za umuundo. Alizua istilahi `parole' na `langue' kueleza maoni yake: `Parole' au uzungumzi ni lugha katika matumizi na hiki ndicho walichokizingatia wanaisimu wa awali, lakini Saussure alivutiwa na mfumo wa kinadharia unaounda lugha zote au `Langue' - yaani masharti au kaida zinazoiwezesha lugha kuwepo na kuweza kufanya kazi.
Hata hivyo, kazi ya Saussure ilikuwa imetengewa wanaisimu peke yao. Katika miaka ya 1950, mtizamo huo wa Saussure ulianza kusambaa katika masomo mengine hasa wakati mawazo yake yalipozingatiwa na Mwanaanthropolojia Claude Levi-strauss. Kwa kuchukua maoni ya isimu ya Saussure na kuyaingiza katika sayansi ya kijamii . Hasa alichotaka kuendeleza kidhana ni kwamba pana viwango viwili katika kuelewa maisha ya jamii, isimu, lugha na chochote kingine kile. Viwango hivi ni cha juu juu (surface) na cha ndani (deep).
Mkondo huu wa mawazo ya umuundo kuhusu sayansi za jamii ulianzia ulaya na kuathiri mtazamo wa elimu mbalimbali (duniani) kama vile: Falsafa, Anthropolojia, Historia, Uhakiki wa kifasihi na Sasiolojia.
Kwa hivyo twaweza kuangalia jamii katika muundo wake wa kijuu juu na kuielewa lakini tukitaka kupata maana mwafaka lazima tuchunguze muundo wake wa ndani ambao hupatikana katika kila jamii ya wanadamu. Kwa hiyo hata katika kuielewa fasihi lazima tuifahamu lugha yake.
Katika kupata maana lazima kuwe na uhusiano wa kipembetatu yaani kuna DHANA, ALAMA na KITAJWA.
UMUUNDO NA FASIHI
Kama vile muundo wa lugha ulivyo mfumo, muundo wa fasihi pia una vipengele vinavyotegemeana na vinavyoelezwa katika muktadha wa vipengele vingine. Katika kazi ya fasihi kuna kitengo cha kisanaa kama vile maudhui, ploti, wahusika, muktadha na lugha. Hakuna kipengele cha fasihi kati ya hivi kitakachoelezwa katika upekee wake. Lazima kielezwe kwa kuzingatia kuwepo kwa jukumu la vipengele vingine. Kwa mfano katika kueleza au kuzungumzia ploti, wahusika watashirikishwa na lugha yao kuzingatiwa.
Kwa hiyo nadharia ya umuundo husisitiza vipengele vya kazi ya sanaa, jinsi vinavyohusiana hadi kuikamilisha kazi hiyo. Huangalia namna sehemu mbalimbali za kazi za sanaa zilivyofungamana. Yaani Neno halihitaji urejelezi ili lipate maana, na Kazi yenyewe ilivyoundwa ndivyo hutoa maana. Yaani maana inavyoumbwa ina dhima kubwa kuliko maana yenyewe.
Wafula na Njogu (2007) wanasema kuwa Umuundo unapinga wazo la kijadi linalodai kwamba fasihi ni tokeo la mchango wa maudhui na fani. Dhana ya kimapokeo kuhusu fasihi inadai kwamba fasihi ni umbo lenye viungo viwili, maudhui na fani na kwamba viungo hivi vyaweza kutenganishwa.
Wahakiki wanoegemea mkondo wa Saussure huzingatia kwamba matini husika ni mfumo unaojisimamia na hivyo basi huwa hamna haja ya kutumia mambo ya nje ili kuhakiki kazi ya fasihi. Wahakiki huzingatia matini kama kiungo kamili kinachoweza kuhakikwa kivyake. Hivyo basi mhakiki wa umuundo hujaribu kuweka sarufi ya matini pamoja na sheria za jinsi matini hiyo hufanya kazi.

Mhakiki anayezingatia zaidi muundo wa lugha ya matini bila shaka hupuuza dhana ya jadi kuhusu kile matini hiyo huweza kutueleza kuhusu maisha; na hivyo basi hufanya mtindo wa kazi yenyewe kiini cha uhakiki wake. Kwa hivyo wahakiki wanaotumia nadharia ya umuundo hujaribu kuzingatia matini peke yake huku wakiepuka kuifasiri kazi ile kulingana na kaida zilizowekwa kuhusu jinsi matini hufanya kazi.
Hata hivyo, huenda njia hii isiwe ya kufaa sana kwa sababu huwa inachukulia kwamba kila kitu kimeundwa katika mpangilio halisi usiotatanika na usiotegemea mambo mengine yaliyo nje yake. Ama kwa hakika, hata lugha yenyewe haiwezi kabisa kufanya kazi bila kuathiriwa na mambo mengine kama vile mazingira yake (Ntarangwi 2004).

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny