Flower
Flower

Thursday, May 30, 2019


Mulokozi (2003) anasema uchapishaji ni mbinu ya usambazaji wa habari, maarifa au fasihi kwa maandishi yaliyopigwa chapa au kunakiliwa katika nakala nyingi.

TUKI (2013), wanasema Uchapishaji ni kazi ya kushughulika na utoaji wa vitabu na kutawanya kwa kuviuza kwa watu.

Kamusi Teule ya Kiswahili (2014) wanaeleza kuwa uchapishaji ni utoaji wa nakala za maandishi kwa kutumia mtambo maalum. Hivyo basi uchapishaji ni mchakato wa utoaji na usambazaji au uenezaji wa taarifa kwa watu wengi katika umbo mahsusi. Sababu ambazo zilipelekea kuzuka kwa uchapishaji ni uandishi na kisomo, dini, siasa, biashara, ugunduzi wa karatasi na ugunduzi wa uchapaji.

Kampuni ya uchapishaji hujumuisha idara na vitengo mbalimbali kama vile, idara ya utawala, idara ya uhariri, idara ya usanifu na utoaji, idara ya uhasibu, idara ya uhifadhi na idara ya TEHAMA au kompyuta. Mfano wa makampuni ya uchapishaji ya Afrika Mashariki ni Mkuki na Nyota, TUKI, Mture, Macmillan Aidan, Vide Muwa, Phoenix, Focus Books na Crane Publishers. Ufuatao ni umuhimu wa idara na vitengo hivi katika kampuni ya uchapishaji.

Idara ya Utawala, ni idara ambayo hujumuisha mameneja pamoja na wakuu wa vitengo, ambao ndio wasimamizi na waendeshaji wa kampuni. Idara hii huwa na umuhimu ufuatayo, kusimamia uendeshaji wa shughuli zote za kampuni ikiwemo, kuajili na kuwalipa mishahara wafanyakazi na mrabaha kwa waandishi wa vitabu, ikiwa ni sehemu ya malipo yao ya mauzo ya vitabu. Pia kulipa kodi kwa serikali, na kuhakikisha suala la mawasiliano.

Idara ya uhariri.TUKI (2013) wanasema Uhariri ni kazi ya kusoma kusahihisha na kusanifu miswada ya makala au vitabu. Katika idara hii kuna muhariri wa jumla na muhariri wa matini. Muhariri wa jumla majukumu yake ni kubainisha maeneo yanayofaa kuandikwa au kutolea kitabu na kutafuta miswada inayofaa au waandishi wanaoweza kuandika miswada hiyo. Pia kutathimini miswada inayoletwa kwaajili ya uchapishaji. Kuandaa pendekezo la uchapishaji wa mswada anaona unafaa kuwa kitabu. Kuandaa mkataba wa uchapishaji kati ya kampuni yake na mwandishi, baada ya kujadiliana na kukubaliana na mwandishi na wakuu wa kampuni yake. Kupendekeza kutoa au kutokutoa chapa mpya za kitabu zinapomalizika. Majukumu ya muhariri wa matini ni kunyoosha au kusahihisha maelezo katika mswada ili kuboresha na kurahisisha mawasiliano kati ya mwandishi na msomaji wake. Hivyo hujaribu kuufanya ujumbe wa mwandishi uwafikie walengwa kwa njia bora, wazi na yenye kuvutia Zaidi, kwa kuboresha matumizi ya lugha, kuangalia uwiano mzuri kati ya fani na maudhui katika mwsada kulingana na walengwa, kupendekeza aina ya vielelezo vinavyohitajika katika kitabu na kunyoosha mpangilio wa mawazo wa uwasilishaji wa mawazo hayo.

Idara ya Usanifu. Feather (2003) Usanifu ni Sanaa ya kuoanisha vipengele vyote ya kitabu, katika maudhui, mtindo, michoro, vielelezo na muundo katika umbo nadhifu, ili kuwasilisha ujumbe katika muundo unaovutia. TUKI (keshatajwa), wanasema Usanifu ni ufundi au ustadi wa uchoraji maumbo yanayoonesha jinsi kitu chenyewe kitakavyokuwa.  Idara hii hufanya kazi karibu na idara ya uhariri, pia hupangilia namna ya kitabu kuwa. Usanifu hufanywa kwa kuzingatia teknolojia itakayotumika, kuchapa, gharama, walengwa, matumizi ya kitabu hicho, na biashara au soko. Pia suala la ukubwa au udogo wa kitabu, rangi na mandishi hupangwa na idara hii.

Idara ya Uhasibu, ni idara ambayo hufanya kazi kwa karibu sana na idara ya utawala pamoja na uhariri. Majukumu ya idara hii ni kurekodi mahesabu ya kampuni ikiwa ni pamoja na mapato na matumizi. Uhusiano wa karibu wa idara hii na idara ya utawala ni pale ambapo, muhasibu huusika na mahesabu ya mapato na matumizi na hupeleka ripoti katika idara ya utawala kwani yenyewe ndiyo huusika na uratibu wa matumizi na mapato hayo. Uhusiano wa karibu wa idara ya uhasibu na uhariri ni pale ambapo muhariri wa jumla huitaji pesa kutoka kwa muhasibu zinazo msaidia kushughulikia menejimenti ya kukamisheni, kutafuta miswada na kuratibu kazi zote za uaandaji wa kitaabu.

Idara ya Uhifadhi, kwa mujibu wa TUKI (keshatajwa) wanasema ni tendo au hali ya kuweka kitu mahali fulani kwa usalama. Katika idara hii huwa na majukumu ya uhifadhi, masoko, uuzaji, na usambazaji. Katika uhifadhi, huhusisha utunzaji wa vitabu, majalada ya kumbukumbu mbalimbali zinazohusu kampuni ya uchapishaji. Uuzaji na usambazaji huhusisha namna au jinsi vitabu ambavyo huweza kuuzwa na kusambazwa ili kuwafikia watumiaji husika, kwa njia ya mtandao au kwa njia ya usambazaji katika maduka mbalimbali ya vitabu.



Kwa ujumla uchapishaji ulianza kwa njia ya kunena ambao ulihusisha au walitumia fasihi simulizi, ngoma, ngomezi, na ala mbalimbali za sauti. Ulifuatiwa na maandishi katika kipindi hiki nchi mbalimbali walitumia maandishi ili kufikisha ujumbe kwa jamii iliyo kusudiwa. Mfano misri walitumia michoro ya hierographics, na wasumeria walitumia cuneiform na baadae uchapishaji.                                                              
                                            MAREJELEO

Feather, J (2003. “Communication knowledge” Berlin: Walter de Gruyter.

Mulokozi, M. (2003). “Uandishi na Uchapishaji” Dar es salaam; TUKI.

Ndallu, A. E (2014). Kamusi teule ya Kiswahili. Nairobi- Kenya: Prinywell Industries Limited

TUKI, (2013) “Kamusi ya Kiswahili sanifu”. Dar es salaam; Oxford University Press.







































                                      














                            


  1. UTANGULIZI
Swali hili limegawanywa katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambao unajumuisha fasili za dhana zilizojitokeza katika swali na ufafanuzi mfupi wa riwaya ya Ua la Faraja, sehemu ya pili ni kiini cha swali ambapo kinahusu athari za majina ya wahusika wa kazi ya fasihi tuliyoichagua na sehemu ya tatu ni hitimisho.
1.1 Fasili ya Dhana zilizojitokeza Katika Swali
Zifuatazo ni fasili mbalimbali zilizojitokeza katika swali.
1.1.1 Fasili ya Fasihi
Kwa mujibu wa Nkwera (2003), Fasihi ni sanaa yaani mkusanyiko wa kazi mbalimbali zilizosanifiwa kwa kutumia lugha itumiayo zaidi maneno na kujishughulisha na jinsi binadamu anavyojitambua mwenyewe binafsi, Pia anavyoathiriwa na binadamu wenzake aidha na viumbe vingine aina kwa aina katika mazingira mbalimbali ya maisha. Tunaona fasili hii imejikita zaidi katika maneno kuelezea maana ya fasihi na kazi zilizosanifiwa.
Nae, Wamitila (2004), anafasili fasihi ni sanaa ya lugha inayoshughulikia masuala yanayomuhusu binadamu matatizo yake, ndoto zake, matumaini yake, migogoro yake na jinsi anavyoingiliana na mazingira yake fasihi; ni sanaa itoayo maudhui yake kwa kutumia lugha ya maneno ambayo hutamkwa ama kuandikwa.
Kwa mtazamo wetu kutokana na maana za waandishi tofautitofauti ambao wamejitahidi kutoa maana ya fasihi tunaona kuwa fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha katika njia masimulizi au maandishi katika kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa jamii husika katika kuikabili mazingira yake katika nyanja mbalimbali za maisha kama vile siasa, uchumi, na utamaduni.
1.1.2 Ufafanuzi kuhusu Majina ya Wahusika
Kenan (2007), anaona  kwamba majina ya wahusika yanaweza kujitokeza kwa kuzingatia tabia zao zinazoweza kujitokeza katika matendo, maneno na muonekano wa nje ya mazingira.
Nae, Mlama (2003), anasema wahusika huteuliwa na hujengwa kutokana na matukio na uwezo wa kisanaa alionao mwandishi. Mwandishi huwapa maneno, matendo na mawazo wahusika wake kutokana na matukio ili kuonyesha uhalisia na uhusika wa kuaminika katika hali wanamotokea. Anaendelea kusema kuwa uteuzi wa majina ya wahusika katika riwaya si kitu rahisi. Ugumu uko katika kuchagua na kuumba majina ya wahusika na kuwaonyesha kimawazo, kimatendo na kimaneno ili kukidhi na kuwakilisha dhana mbalimbali za maisha  katika jamii.
1.1.3 Riwaya ya Ua la Faraja
Ni riwaya iliyoandikwa na Makufya na imejadili dhamira ya mapenzi kama dhamira kuu. Mapenzi yanayojadiliwa kwa kiasi kikubwa ni mapenzi ya ndoa na uaminifu wake na mapenzi kati ya mtu na mtu, mtu nan chi pamoja na mapenzi ya mtu na familia. Halikadharika dhamira zingine kama ulevi, uhujumu uchumi, umuhimu wa kufanya kazi, magonjwa, umasikini na nyingine nyingi. Riwaya hii imetumia wahusika kama vile Omolo, Pendo, Chiku, Msafiri, Asha, Queen, Juma, Dk Hans nakadhalika.
2.0 Kiini cha Swali
Hussein (2003), anafafanua kuwa wahusika katika kazi za fasihi huwa na athari kubwa sana kwa hadhira au wasomaji kutokana na kwamba ndiyo wanaobeba matukio yote yanayotakiwa kuwasilishwa katika jamii. Zifuatazo ni athari za wahusika wa kazi ya fasihi kwa wasomaji kwa kutumia riwaya ya Ua la Faraja.
Majina ya wahusika husaidia kuonyesha umoja na mshikamano kwa wasomaji. Mwandishi katika riwaya hii ametumia jina Juma kama muhusika ambaye alikuwa na umoja na upendo katika familia yake. Juma ni jina linalotokana na siku ya Ijumaa katika Kiswahili, yenye kumaanisha siku ya Sala kwa dini ya Kiislamu ambapo waislamu wote hukutana pamoja kuonesha umoja miongoni mwao, na kusaidiana na jina hili hupewa watoto wa Kiume. Hivyo jina Juma katika riwaya hii humaanisha uwezo wa kuwakusanya watu kwa pamoja na kusaidiana. Halikadhalika tunaona jinsi juma alivyokuwa na upendo na mshikamano kwa familia yake na jinsi alivyokuwa akimsaidia mama yake na wadogo zake katika shida na raha. Tunamuona anavyohakikisha na kuwaweka wadogo zake katika hali ya umoja na upendo. Mwandishi anaonesha Juma akisema;
                               “mama usiondoke. Unajua hali ya hapa nyumbani. Nuru na Rahma watabaki
                                 na nani sisi tukienda shule” (uk 37)
Hivyo tunaona jinsi gani jina la muhusika huyu linvyotoa funzo kwa wasomaji kuwa na umoja na mshikamano katika jamii zetu tunamoishi. Jamii zinapaswa kuwa na umoja na mshikamano katika kusaidiana katika mambo mbalimbali ili kuleta maendeleo katika jamii.
Majina ya wahusika husaidia kuonyesha hekima, akili na shupavu katika mapambano ya kimwili na kiroho ili kufanikisha jambo fulani. Mwandishi katika riwaya hii amemtumia Grace kama muhusika mwenye hekima na akili ya kupambanua mambo. neno Grace asili yake ni kutoka katika lugha ya kiingereza lenye maana ya hali na tabia za mungu kama upole, uvumilivu, utu, wema. Mwandishi anamuonesha Grace jinsi anavyoishi kwa amani, upendo na furaha na dada yake Tabu na Omolo, amekuwa mshauri mzuri kwa Tabu, Omolo na Ngoma, amewauguza Tabu na Ngoma hadi kufa kwao. Anawalea watoto wa Tabu kama mama yao, anamkomboa Omolo katika giza la maisha alimokuwa na kumuweka katika mwanga wa maisha ya ndoa kama ambavyo Grace mwenyewe anasema;
                 “…alijiona mwenye wajibu wa kulitatua pingamizi lile, wajibuu wa    
                                kumwokoa   Omolo kutoka kwenye upweke ulimwandama na kumwathiri.            
                Hakujua ataanzaje, lakini alijipa Imani ya mafanikio” (uk. 271)
Maelezo haya ni ya makusudi kabisa yanayomwonesha Grace kuwa ni shupavu, jasiri na mvumilivu katika mapambano ya kumkomboa Omolo kwenye matatizo yake na hata katika kuwasaidia watu wengi. Hivyo tunaona kuwa msomaji na jamii kwa ujumla kupitia muhusika Grace tunaweza kujifunza kuwa na ushupavu katika kukabili mambo mbalimbali yanayojitokeza.
Majina ya wahusihusika huonyesha hali mbalimbali zinazomkabili mtu, kitu au vitu. TUKI (2009), imefasili neno Tabu kama hali ya kutokuwa na raha, kuwa na adha, usumbufu, shida, mashaka na kero. Halikadhalika katika riwaya hii tunaona jinsi muhusika Tabu alivyoishi maisha yasiyo ya raha, yenye usumbufu, kero, mashaka, udhia na shida mbalimbali toka kuolewa kwake. Hii inajidhirisha pale ambapo mwandishi anasema:
                               “…Akaeleza habari za mapenzi ya siku nyingi baina ya mwanamke aliyeitwa  
                                 Queen na mumewe Ngoma. Akaeleza mizozo ya huko nyuma baina yake na
                                 mumewe kuhusu huyo mwanamke. Kisha akamalizia kwa habari  alizozipata   
                              kwamba mwanamke huyo tayari anadalili zinazojulikana kama ni za
UKIMWI” (uk. 59).
Kupitia jina la Tabu tunaona  msomajia anaweza kujua hali mbalimbali zinazomkabili mtu katika jamii na jinsi ya kuzikabili hali hizo kama jinsi Tabu alivyokabiliana na hali hizo, mathalani kuambukizwa UKIMWI na mumewe, kutotimiziwa mahitaji mbalimbali ya kifamilia nakadhalika. Inatubidi kujua hali tulizonazo, kuzikubali na kutafuta namna ya kuzikabili.
Majina ya wahusika husaidia kuonyesha upendo na uthamini wa kitu au kazi unayoifanya. Mwandishi amemtumia muhusika pendo kuonyesha upendo na uthamini katika kazi aliyokuwa akiifanya. Jina Pendo linatokana na neno penda, kwa mujibu wa TUKI (2009), penda ni kutaka shauri kufanya jambo kwa kuridhika mwenyewe. Hivyo pendo ni jina la mtu lenye maana penda. Katika riwaya hii mwandishi amemuonyesha pendo kama kama muhudumu wa bar aliyekuwa akiipenda kazi yake na kuithamini pamoja na kuwahudumia wateja na hata kucheza mziki pamoja. Tunaona pendo aliithamini na kuifurahia kazi yake ya kuwahudumia watu. Mwandishi anasema;
                              “aliendelea kulisakata rumba, pendo akamwendea. Wakawa wanacheza
                               pamoja huku ngoma akizidisha mbwembwe baada ya kupata mwenza.” (uk 7)
Hivyo kupitia muhusika huyu wasomaji wanajifunza kuthamini kazi au majukumu mbalimbali wanayoyapata katika jamii zao. Matahalani kazi ya ualimu, mwalimu anatakiwa kuifanya kazi hiyo vizuri na kuithamini kazi hiyo bila kujali changamoto anazokabiliana nazo.
Pia majina ya wahusika husaidia kuonyesha kazi mbalimbali. Hapa mwandishi amemtumia muhusika Msafiri, kama aliyekuwa anafanya kazi ya  kusafirisha mafuta kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Msafiri ni jina linalotokana na neno Safiri. TUKI (2009), imefasili neno safari kama ni kutoka mahali fulani na kwenda mahali pengine, mathalani kutoka mji mmoja kwenda mji mwingine na kadhalika. Katika riwaya hii tunaona msafiri alikuwa kazi ya kusafirisha mafuta kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Kigali. Mwandishi anasema;
                                “msafiri alikuwa dereva wa gali la mafuta. Alisafirisha mafuta toka bandari
                                  ya Dar es Salaam hadi Kigali. Inasemekana gari la mafuta alilolitumia
                                  lilikuwa mali yake.” (uk 89 -90)
tuaona kuwa majina ya wahusika katika kazi ya fasihi, mwandishi huwapa uhusika huo kutokana na kazi wanazofanya, hivyo kusaidia wasomaji kujua kazi mbalimbali katika jamii. Halikadhalika katika jamii zetu baadhi ya watu hupewa majina kutokana na mambo, tukio au siku fulani ambalo litabaki kuwa kumbukumbu. Mathalani majina kama Tabu, Shida nakadhalika.
Halikadhalika majina ya wahusika husaidia kuonyesha uzuri wa kitu, mtu au jambo na matatizo yake. Tunaona mwandishi amemtumia muhusika Queen kuonyesha dhana ya uzuri. Queen ni jina la kingereza lenye maana ya malkia katika lugha ya Kiswahili. Jina malkia linafasiliwa kama mtu mzuri sana na anayevutia. Queen alikuwa mwanamke mzuri, mrembo na msomi na aliyevutia kwa kila mwanaume aliyeonana nae. Kutokana na uzuri wake, aliutumia vibaya kwa kuwa na wanaume wengi hadi kupelekea kupata maradhi ya UKIMWI. Katika riwaya hii mwandishi anasema kuwa:
                       “Queen alikuwa mashuhuri mtaani kwa urembo wake, na pia kwamba
                        alikuwa mwanamke pekee msomi na menye cheo kikubwa kazini kwake .Hivyo
                       habari za kuuguwa kwake zilichukuliwa na wengi, hasa wanawake, kwa hisia za
                       furaha iliyotokana na wivu na chuki dhidi yake” (uk 36)
Tunaona kuwa msomaji huweza kuelewa dhana ya uzuri na changamoto zake zinazojitokeza kutokana na uzuri huo. Hivyo, wasomaji wataelimika na kuweza kujua kuwa uzuri wa kitu, mtu huweza kuwa na matatizo mbalimbali pindi unapotumika vibaya.
3.0 Hitimisho
Kutokana na majina ya wahusika yaliweza kutumika katika riwaya ya Ua la Faraja msomaji ameweza kupata athari mbalimbali kwa jinsi mwandishi alivyoweza kuwatumia wahusika hao na majukumu aliyowapa kutokana na sifa za majina ya wahusika. Mwandishi huweza kuunda wahusika wa kazi ya fasihi kulingana na mambo na majukumu ambayo anataka kuwapa, ambayo huendana na sifa za majina yao.
                                                                     MAREJELEO
Kenan, S. R (2007). Narrative Fiction. New York: Routledge.
Hussein, E. (2003). Hatua mbalimbali za Kubuni na Kutunga Tamthiliya kufuatana na Misingi
                ya Ki – Aristotle. Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III.
                Dar es Salaam. TUKI.
Mlama, P. O. (2003). Utunzi wa Tamthiliya katika Mazingira ya Tanzania. Makala za Semina ya
Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III. Fasihi. Dar es Salaam: TUKI.
Nkwera, F. V. (2003). Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu: Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam:
                   Creative Prints Ltd.
TUKI. (2009). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.
Wamitila, K.W. (2010). Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi. Nairobi Kenya: Vide-Muwa.


1.0 UTANGULIZI

sehemu ya kwanza ni utangulizi, sehemu ya pili ni fasili ya dhana, sehemu ya tatu ni sifa za vikoa vya maana, sehemu ya nne ni umuhimu wa vikoa vya maana, sehemu ya tano ni changamoto na mwisho ni hitimisho la swali.

    1. Fasili ya Dhana ya Vikoa vya Maana

Ufafanuzi kuhusu dhana ya vikoa vya maana kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali umeelezwa kama ifuatavyo;

Briton (2000) anaihusisha dhana ya vikoa vya maana na dhana ya haiponimia. Haiponimia ni uhusiano wa ki-uwima ambapo fahiwa ya neno moja hujumuishwa katika fahiwa ya neno jingine. Hii inamaana kuwa maana ya neno moja ni sehemu ya maana kubwa ya neno. Neno lenye maana kubwa huitwa “neno jumuishi” na maneno yenye maana ndogondogo huitwa “haiponimu”. Kwa mfano, mmea (neno jumuishi) lina haiponimu kama mgomba, mahindi, na maharage. Tunaona mtaalamu huyu haweki wazi maana ya vikoa vya maana ingawa anajikita Zaidi katika kuhusisha vikoa vya maana na haiponimia.

Dirk (2010) anaeleza kuwa, vikoa vya maana ni jozi za maneno yenye maana zinazohusiana ambazo maana zake zinategemeana, na kwa pamoja zinatoa dhana ya kimuundo yenye uhalisia ndani yake. Hii humaanisha kwamba, maana ya haiponimu zinazotokana na kikoa kimoja hujumuishwa katika maana pana au jumuishi moja.

2.0 Sifa za Vikoa vya Maana

Baada ya kufasili vikoa vya maana kwa mujibu wa wataalaamu mbalimbali, zifuatazo ni sifa za vikoa vya maana.

Dirk (2010) anafafanua kuwa vikoa vya maana huwa na sifa kuu mbili; kila kikoa kinaweza kuzaa vikoa vingine vidogovidogo. Kwa mfano 1 Matunda

  1. Papai
  2. Embe
  3. Chungwa
  4. Nanasi
  5. Parachichi

Mfano 2. Wanyama

  1. Chui
  2. Simba
  3. Mbwa
  4. Mbuzi
  5. Kifaru

Pia hakuna kanuni ya upangaji wa hivyo vikoa yaani kipi kiwe cha kwanza na kipi kiwe cha mwisho. Katika vikoa hakuna mpangilio maalumu wa mfuatano wa vikoa hivyo chochote kinaweza kuanza au kuwa cha mwisho.

                                                                 Kwa mfano; Matunda

4. nanasi

      3. Chungwa

1. Papai

2. Embe

Halikadhalika katika sifa hiyo ya kutokuwa na kanuni ya upangaji wa vikoa vya maana ina vighairi, kwani kuna baadhi ya vikoa hufuata kanuni na utaratibu maalumu wa mpangilio wa kinamba. Kwa mfano katika vikoa vya siku, miezi, miaka au namba, hivi ni vikoa vyenye kufuata utaratibu maalumu wa mfuatano wa namba.

Mfano; Siku   

  1. Jumamosi
  2. Jumapili
  3. Jumatatu
  4. Jumanne

Mfano 2; Namba

  1. Moja
  2. Mbili
  3. Tatu

Vikoa hivi vya maana hufuata utaratibu maalumu ambapo maneno huorodheshwa kwa kufuata mpangilio wa kinamba.

3.0 Umuhimu wa Vikoa vya Maana

Baada ya kuangalia sifa za vikoa vya maana, ufuatao ni umuhimu wa vikoa vya maana na ufafanuzi wake.

Vikoa vya maana husaidia kuonesha uhusiano wa maneno yenye sifa sawa au zinazoelekeana kimaana. Vikoa vya maana humsaidia mwanaisimu kutambua sifa za maana mbalimbali zinazohusiana kimaana. Hii humaanisha kuwa, huwezi kuweka neno fulani katika kikoa fulani bila kujua sifa zinazotawala neno hilo. Hivyo basi, haiponimu zote zinazotokana na neno moja pana huwa na sifa ama zinazofanana au zinazoelekeana. Habwe na Karanja (2004) wanafafanua kuwa neon lenye maana kubwa huitwa neon jumuishi na lile lenye maana ndogo huitwa haiponimu. Wanaeleza kuwa neon mnyama katika lugha ya Kiswahili ambalo ni neno kuu, lina mahusiano ya kihaiponimia na maneno mbuzi, ng’ombe, simba, duma, nguchiro na mengineyo. Hivyo ukisema mnyama sio lazima uwe umemaanisha mbuzi au ng’ombe lakini ukisema mbuzi au ng’ombe kwa naman Fulani utakuwa umemaanisha mnyama.

Hurahisisha mchakato wa ujifunzaji lugha. Vikoa vya maana husaidia kumuelekeza mtu anayejifunza lugha fulani mahususi ili kujua vitu mbalimbali vilivyowekwa katika kundi Fulani husika. Kwa mfano, mtu mgeni wa lugha fulani huweza kujifunza kuwa, dhana ya neno “matunda”, hurejelea ndizi, maembe, parachichi, zabibu na machungwa. Kwa mantiki hii, mgeni wa lugha fulani anapotajiwa moja ya vitu vilivyoorodheshwa hapo juu, mfano ndizi, maembe au zabibu, ataelewa kuwa kinachomaanishwa au kinachorejelewa ni matunda.

Hurahisisha mawasiliano baina ya watumiaji wa lugha. Katika mawasiliano, matumizi ya neno moja pana linalorejelea maana nyingine ndogondogo husaidia kuokoa muda baina ya wazungumzaji. Kwa mfano, mtu anapokwenda sokoni, badala ya kutaja kitu kimoja kimoja, huweza kutaja kwa ujumla wake endapo vinahusiana. Mtu akienda sokoni huweza kuuliza; “una mboga za majani?” Atajibiwa; “kuna mchicha, chainizi, spinachi, na matembele”. Hivyo basi vikoa vya maana vitakuwa vimesaidia katika kurahisisha mawasiliano baina ya wazungumzaji, kwani baada ya kutaji kitu kimoja huweza kutaja kwa ujumla wake kama vinahusiana.

Vikoa vya maana husaidia katika shughuli za utunzi wa leksikografia. Mdee (2010), akimnukuu Wiegand, anaeleza kuwa, leksikografia kazi ya kisanaa inayojishughulisha na utunzi wa kamusi. Leksikografia hiyo hujishughulisha na ukusanyajin wa misamiati mbalimbali ya lugha na ndiyo inayosaidia kutungiwa kamusi. Kamusi ni kipengele cha kisemantiki kwa kuwa hutoa maneno yenye maana kwa watumiaji wa lugha. Maneno hayo huweza kutumika kama vikoa vya maneno vyenye maana. Mifano ya kamusi zenye vikoa vya maana ni kama vile; kamusi ya wanyama, Kamusi ya mavazi, Kamusi ya tiba ya magonjwa, Kamusi za misuko ya nywele, Kamusi za vyakula.

Kikoa kimoja huweza kusaidia kujua na kufafanua vikoa vidogovidogo vilivyomo ndani ya kikoa kikubwa. Kwa mfano, mtu anapokwenda hotelini na kusema; “naomba chakula”, ataulizwa, “unahitaji ugali, ndizi, viazi, au wali?”. Kisemantiki, hii humsaidia mtumiaji wa lugha kuteua kikoa mahususi kwa ajili ya matumizi yake kwa wakati huo. Kwa mfano, mtu atasema; “nahitaji ndizi”.

Husaidia kuonesha umbo la wingi ambalo lina umuhimu kisemantiki hasa katika upatanisho wa kisarufi. Kwa mfano, badala ya mtu kusema “kikoa cha mmea” husema “kikoa cha mimea”, badala ya kusema “kikoa cha ua” atasema “kikoa cha maua”. Vikoa hivyo vinapotumika kwenye sentensi huwa mimea imeota badala ya kusema mmea imeota, ua limechanuza badala ya kusema maua limechanuza

Vikoa vya maana vina sifa ya kuwa na maana ya kileksimu na kufanya kikoa kimoja kichanuze zaidi na kuweza kupata maneno mengine yenye maana kisemantiki. Kwa mfano, kuna kikoa cha masomo ya sayansi, baiolojia, fizikia, kemia, kilimo. Kikoa cha baiolojia kinaweza kufasiliwa kuwa ni somo la kisayansi linalohusiana na viumbe hai na visivyo hai. Hivyo tunaona kuwa kikoa cha baiolojia kimechanuza zaidi na kuleta maana ya kikoa hicho.

4.0 Changamoto za Vikoa vya Maana

Baada ya kuangalia sifa pamoja na umuhimu wa vikoa vya maan, vilevile vikoa vya maana vinakumbwa na changamoto mbalimbali katika kuelezea maana ya maana inayorejelewa. Zifuatazo ni baadhi ya changamoto hizo ambazo ni;

Kuna baadhi ya vikoa ni changamani. Hii ni kutokana na dhana kuwa, baadhi ya vikoa vya maana vinawakilisha dhana zaidi ya moja na hivyo kumfanya mtumiaji wa lugha apate utata wakati wa uainishaji wake. Mfano: ndege kama mnyama, na ndege kama kifaa cha usafiri. Katika muktadha huu, mkanganyiko wa kinachomaanishwa huweza kujitokeza ikiwa muktadha wa mazungumzo hautakuwa wazi.

Hakuna nadharia ya jumla inayohusika na upangaji wa vikoa hivi. Hii inatokana na ukweli kwamba, dhana hizi zipo vichwani mwa watumiaji wa lugha na huandikwa kutokana na matumizi yake kimaana. Kaitka kuorodhesha, mtumiaji wa lugha anaweza kuanza na kikoa chochote akipendacho. Kwa mfano, katika kikoa cha “mtu”, mtumiaji wa kwanza wa lugha anaweza kutaja mwanaume na mwanamke, na mwingine akataja kwa kuanza na mwanamke kisha mwanaume.

Uainishaji wa vikoa vya maana unahitaji umakini zaidi katika upangaji wa vikoa kwani kuna uchomozi wa vikoa vingine. Hii hutokea pale ambapo dhana moja mahususi huwa na dhana ndogondogo ndani yake ambazo nazo huweza kusimama peke yake na kuwa na vikoa vyake. Kwa mfano, kikoa cha binadamu tunapata wanaume na wanawake. Katika kikoa hiki, kuna vikoa viwili pia; kikoa cha wanawake chenye haiponimu kama vile bibi kizee, shangazi, mama, na msichana. Kikoa cha mwanaume kina haiponimu kama vile babu, mjomba, na mvulana.

Vikoa vya maana hutofautiana kutokana na eneo na utamadunihusika. Kila jamii ina utamaduni na utamaduni huo huwa na vikoa vitumikavyo katika mazungumzo yao ambavyo vinaweza kutofautiana na utamaduni wa jamii nyingine kutokana na aina na idadi ya vitu hivyo katika jamii husika. Mfano, kikoa cha ndizi katika utamaduni wa Wanyakyusa, kuna vikoa vya majina ya ndizi kama vile; malinda, matoki, mkono wa tembo, haradoni, kaambani na ndyali, lakini katika jamii ya Wahaya kuna vikoa vya majina ya ndizi kama vile; shubili, majivu. Hivyo tunaona kuwa vikoa vya maana huweza kutofautiana kati ya jamii moja na nyingine.

5.0 Hitimisho

Hivyo tunaweza kusema kuwa, ingawa kunachangamoto zinazokabili vikoa vya maana, vikoa hivyo vina umuhimu na mchango mkubwa katika kuendeleza na kukuza lugha. Hii ni sababu, wanajamii hufanya uteuzi mzuri wa maneno yenye maana kutoka akilini na kuyatumia maneno hayo katika mazungumzo na hivyo kufanya suala la mawasiliano liendelee kufanikiwa zaidi.






MAREJELEO

Brinton L. J. (2000). The Structure of Modern English. A Linguistic intro Illustrated Edition.

 John Benjamini Publishing Company.

Dirk, G. (2010). Theories of Lexico Semantics. Oxford University Press: New York.

Habwe, J. na Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publisher

Mdee, J, S (2011). Nadharia na historia ya leksikografia. TUKI: Dares salaam.

Saturday, May 18, 2019

Dhana ya mofolojia imefasiliwa na wataalam mbalimbali kama vile
Tuki (1990), wanafasili kuwa mofolojia ni tawi la isimu ambalo huchunguza maneno na aina zake. Hivyo basi tawi hili husaidia kujua aina mbalimbali za maneno ambazo hutumika katika lugha mbalimbali.
Besha (2007) anafasili mofolojia kuwa ni taaluma inayojishughulisha na kuchambua muundo wa maneno katika lugha. Mfano katika lugha ya Kiswahili kitenzi cheza kinaweza kuunda nomino mchezaji, katika mfano huu mwandishi ametumia njia ya unominishaji kuunda nomino.

Obuchi na Mukhwana (2015) wamefasili mofolojia kuwa ni taaluma inayohusu maneno. Wanaendelea kufafanua kwamba taaluma hii hudhihirisha muundo wa maneno kwa kurejelea mofu mbalimbali zenye kazi za kisarufi.
Kwa ujumla mofolojia ni taaluma inayoshughulikia vipashio vya lugha katika kuunda maneno.  Yaani inachunguza na, kupambanua maumbo ya maneno ambayo ni umbo la ndani na umbo la nje mfano
                 Umbo la ndani                                                     umbo la nje
                 Mu+alimu                                                                  mwalimu
                 Ki+ungu                                                                       kyungu

Dhana ya fonolojia imefasiliwa na wataalam mbalimbali kama vile
Massamba na wenzake (2001) wamefasili fonolojia kuwa ni taaluma inayoshughulikia uchambuzi wa mfumo wa sauti katika lugha. Yaani jinsi vipashio hivyo vinavyofuatana na kuathiriana.
Fudge (1973) anasema fonolojia ni kiwango kimoja wapo cha lugha fulani kilicho na vipashio vidogo zaidi kuliko vipashio vingine vyote vya lugha. Vipashio vya kifonolojia ni fonimu na alofoni.

Kwa ujumla fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchambuzi wa mfumo wa sauti katika lugha inayohusika.  Na kipashio kidogo cha fonolojia kinachobadili maana ya neno ni fonimu.
Vilevile dhana ya sintaksia imefasiliwa na wataalam mbalimbali kama ifuatavyo:
Obuchi na Mukhwana (2015) wanafasili sintaksia kuwa ni tawi la isimu linaloshughulikia uchanganuzi, mpangilio na uhusiano wa vipashio katika kuunda sentensi. Wanaendelea kusema kuwa katika taaluma hii tunahakiki namna maneno yanayopangwa ili kuunda tungo na sentensi zenye maana.

Habwe na karanja (2004) wanasema sintaksia ni utanzu wa isimu unaoshughulikia muundo wa sentensi, na elementi nyingine zinazounda sentensi kama vile kategoria za maneno, virai  na vishazi.
Kwa ujumla sintaksia ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchambuzi wa maneno mbalimbali katika lugha jinsi yanavyoungana na kuunda sentensi.
Dhana ya semantiki imefesiliwa na wataalam mbalimbali kama vile
Crystal (1987) anasema semantiki ni utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha. Anaendelea kusema kuwa taaluma ya semantiki ni taaluma ambayo hujishughulisha na uchunguzi wa maana katika viwango vyote vya lugha.

Massamba (2004) anafasili semantiki kuwa ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa maana za maneno na tungo katika lugha. Anaendelea kusema kuwa semantiki imegawanyika katika makundi manne ambayo ni leksika, mantiki, muundo na nadharia.
Kwa ujumla semantiki ni utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha ya mwanadamu.

Taaluma ya mofolojia inahusiana na kusigana na taaluma nyingine za kiisimu kama vile fonolojia, sintaksia na semantiki. Kama ifuatavyo kwa kuanza na uhusiano na kusigana kwa mofolojia na fonolojia:
Ufuatao ni uhusiano wa mofolojia na fonolojia:
Taaluma zote mbili hutegemeana katika mchakato wa uundaji wa maneno katika lugha fulani, Massamba na wenzake (2013) wanashadidia hoja hii kwa kusema kuwa, maneno huundwa na mofimu vilevile mofimu huundwa na sauti au vitamkwa. Aidha uundaji wa mofimu hufuata taratibu maalum za mfuatano wa sauti za lugha husika. Kwa mfano:
                                          SAUTI                        MOFIMU                       MANENO
                                           /p/ +/a/+/t/+/a/                  pat-a                                     pata
                                         /k/+/a/+/b/+/a/                    kab-a                                    katkaba
                                        /l/+/i/+/m/+/a/                      lim-a                                     lima.
Mfano huo hapo juu umeonyesha jinsi ambavyo sauti huungana na kuunda mofimu katika lugha ya Kiswahili.

Fonolojia na mofolojia huhusiana katika kuunda michakato ya kimofofonolojia, Michakato hii hupelekea kuundwa kwa kanuni ambazo husaidia kuunda maneno katika lugha ya Kiswahili.maelezo haya yanashadadiwa na Massamba (2004) anaeleza kuwa mofofonolojia ni taaluma ya isimu inayohusu uhusiano baina ya fonolojia na mofolojia katika kuunda maneno. Miongoni mwa michakato ya kimofofonolojia ni kama vile uyeyushaji, udondoshaji, muungano wa sauti. Kwa mfano muungano wa sauti kanuni hii hutokea pale ambapo irabu ya mofimu moja inapokaribiana na irabu ya mofimu nyingine katika mpaka wa mofimu. Irabu hizo huungana na kuzaa irabu moja.
                                             UMBO LA NDANI                                  UMBO LA NJE.
                                                       / wa+enye/                                                   wenye
                                                        /ma+ino/                                                         meno
                                                       /wa+izi/                                                           wezi
Uundaji wa Mofimu za lugha ambao ni sehemu ya mofolojia hufuata taratibu maalum za fonolojia ya lugha husika, ndio sababu kunauhusiano wa moja kati ya mofolojia na fonolojia. Mfano mfuatano wa sauti ufuatao haukubaliki katika lugha ya Kiswahili na kupelekea maandishi yasiyo maana katika lugha hii. Hoja hii inashadidiwa na Massamba na wenzake 2013. Miongoni mwa sauti hizo ni kama zifuatazo:
                               

                              SAUTI ZENYE MPANGILIO                    UMBO LISILOKUBALIKA
                                     LISILOKUBALIKA
                                           /g/, /d/, /k/, /a/                                                         gdka
                                         /m/, /m/, /y/, /u/                                                         mmyu.
Mpangilio huu haukubaliki na hauleti maana katika lugha ya Kiswahili, hivyo basi haukubaliki.
Mofolojia na fonolojia husigana kama ifuatavyo:
Maana, dhana hizi zina maana tofauti, vilevile utendaji wake kazi ni tofauti kwa kuanza na mofolojia 

kwa mujibu wa Besha (2007) anafasili mofolojia kuwa ni taaluma inayojishughulisha na kuchambua muundo wa maneno katika lugha. Mfano katika lugha ya Kiswahili kitenzi cheza kinaweza kuunda nomino mchezaji, katika mfano huu mwandishi ametumia njia ya unominishaji kuunda nomino. Hivyo basi mofolojia hujihusha na uchunguzi wa maumbo mbalimbali ya maneno jinsi yanavyopaswa kuwa na yanavyotumika katika lugha husika. Vilevile fonolojia Massamba na wenzake (2001) wanafasilikuwa fonolojia ni taaluma inayoshughulikia uchambuzi wa mfumo wa sauti katika lugha. Yaani jinsi vipashio hivyo vinavyofuatana na kuathiriana. Katika fonolojia sauti mbalimbali hupangwa katika mpngilio unaokubalika katika lugha inayohusika. Mpangilio huu wa sauti ni lazima ulete maana inayokubalika katika lugha husika.

Taaluma hizi hutofautian katika Ukongwe, Taaluma ya fonolojia ilianza hata kabla ya mofolojia  kwa sababu sauti ndiyo iliyoanza, hivyobasi fonolojia ni kongwe yaani sauti zilianza ndipo maumbo ya maneno yakafuatia. Kutokana na hali hii mofolojia  imeibuka baada ya kuwapo kwa sauti mbalimbali ambazo zinatumiwa  katika lugha ambapo sauti hizi hutumika katika mchakato wa uundaji wa maneno.
Mofolojia na fonolojia husigana katika vipashio, kuna utofauti wa vipashio vya dhana hizi, mofolojia kipashio chake kikuu ni mofu. TUKI (1990) wanafasili mofu kuwa ni kipashio cha kimofolojia ambacho huwakilisha mofimu. Kwa hiyo mofu hutumika kuwakilisha mofimu. Kipashio cha fonolojia ni fonimu, fonimu ni kipashio kidogo cha kimofolojia kinachojihusisha na lugha mahususi. Vilevile kipashio hiki hufanya kazi katika  lugha mahususi na utendaj kazi wake hutofautiana katika lugha moja na lugha nyingine. Mathalani
                                       MOFU ZA KISWAHILI                         FONIMU ZA KISWAHILI
                                              m-toto                                                                /m/, /n/, /t/ na /k/
                                               wa-toto
Katika mfano tajwa m ni mofu funge ya umoja na wa ni mofu funge ya wingi. Vilevile /m/, /n/, /t/ na /k/ ni mofimu za Kiswahili.
Ufuatao ni uhusiano baina ya mofolojia na sintaksia:
Maumbo ya kimofolojia huathiri vipengele vingine vya kisintaksia  Rubanza (1996)anashadadia kwa kusema kuwa vipengele ambavyo huathirika mara kwa mara ni umoja na wingi kwa sababu kutokana na mabadiliko ya umbo kutoka umoja kwenda wingi hivyo vipengele vingine ambavyo hupatikana katika tungo hiyo huathiriwa na mabadiliko hayo. Mathalani
                                           UMOJA                                                            WINGI
                    i.         Mwalimu anafundisha                                   walimu wanafundisha
                  ii.        Gauni limeibiwa                                             magauni yameibiwa
Katika mifano tajwa viambishi “m na “w” katika kiima kwenye mfano wa kwanza vimeathiri utokeaji wa viambishi “a” na “wa” katika kiarifu. Vivyo hivyo katika mfano wa pili viambishi “g” na “m” katika kiima vimeathiri utokeaji wa viambishi cha “li” na “ya” katika kiarifu.
Taaluma hizi huhusiana katika uundaji wa sentensi, kwani sentensi huundwa na maneno vilevile maneno huundwa na mofu. Hivyo huwezi kupata sentensi bila muunganiko wa mofu unaotupatia maneno ambayo hutusaidia kuunda sentensi.
Ufuatao ni utofauti baina ya mofolojia na sintaksia.
Hutofautiana katika maana, Mofolojia na sintaksia hutofautiana katika maana kwani Obuchi na 

Mukhwana (2015) wanasema mofolojia ni taaluma inayohusu maneno. Wanaendelea kufafanua kwamba taaluma hii hudhihirisha muundo wa maneno kwa kurejelea mofu mbalimbali zenye kazi za kisarufi. Hivyo maneno ni lazima yawe na muundo ambao unakubalika na unaoleta maana miongoni mwa watumiaji wakati   sintaksia ni utanzu wa isimu unaoshughulikia muundo wa sentensi, na elementi nyingine zinazounda sentensi kama vile kategoria za maneno, vikundi na vishazi. Vilevile ni lazima iwe na muundo ambao unakubalika na kuleta maana katika lugha inayohusika. Mfano katika lugha ya Kiswahili hutumia muundo wa kiima + kitenzi + yambwa (KTY) muundo huu ndiyo unaokubalika na kuleta maana miundo mingine kama kitenzi + yambwa + kiima (TYK) haukubaliki. Mathalani
i.          Mwalimu anafundisha darasani
                                               kiima       kitenzi      yambwa.
ii.          Anafundisha darasani mwalimu.
Kitenzi        yambwa    kiima.
 Katika mfano wa kwanza muundo uliotumika ndio unaokubalika katika lugha ya Kiswahili na muundo uliotumika katika mfano wa pili haukubaliki na hauleti maana iliyokusudiwa.
 Pia hutofautiana katika suala la utendaji dhana hizi hutofautiana katika utendaji kwani mofolojia hujihusisha na maumbo ya maneno kwa ujumla ambayo hutumika katika lugha ya Kiswahili. Miundo ya maneno hayo ni lazima ilete maana miongoni mwa watumiaji wake wakati sintaksia huchunguza muundo mzima wa sentensi yaani muundo wa sentensi hiyo ni lazima ukubalike miongoni mwa watumiaji wa lugha hiyo.
Ufuatao ni uhusiano wa mofolojia na semantiki:
Maneno yanayoundwa na mofolojia lazima yalete maana ambayo huwasilisha semantiki, katika mofolojia maneno yanayoundwa ni lazima yawe katika mpangilio ambao unaeleweka. Kutokana na muundo sahili wa maneno husaidia kupata neno au sentensi ambayo imejikamilisha kimuundo na kimaana.

Utofauti kati ya mofolojia na semantiki.
Maana,  Tuki (1990) wanasema mofolojia ni tawi la isimu ambalo huchunguza maneno na aina zake. Hivyo basi tawi hili husaidia kujua aina mbalimbali za maneno ambazo hutumika katika lugha mbalimbali mfano Kiswahili. Aina za mneno hizo ni kama nomino, kitenzi, kivumishi na zinginezo wakati semantiki ni taaluma inayochunguza maana  katika lugha fulani naye  Crystal (1987) ameifafanua semantiki kuwa ni utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha. Anaendelea kusema kuwa taaluma ya semantiki ni taaluma ambayo hujishughulisha na uchunguzi wa maana katika viwango vyote vya lugha. Hivyo basi ili sentensi ilete maana ni lazima muundo wake uwe unaokubalika miongoni mwa watumiaji wa lugha husika.

Zinatofautiana katika aina au matawi, Massamba (2004) anafafanua kuwa taaluma hizi zinatofautiana katika aina au tanzu ambazo hutumika, kwa kuanza na mofolojia ina tanzu mbili ambazo ni mofolojia ya mnyumbuliko wa maneno na mofolojia ya uundaji wa maneno. Matawi haya hushirikiana katika utendaji kazi wake ili kuleta muundo unaoeleweka. Semantiki ina matawi manne ambayo ni leksika, mantiki muundo na nadharia. Vilevile tanzu hizi hushirikiana ili kuunda maneno yenye maana.

Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa ingawa taaluma ya mofolojia inahusiana na kusigana na taaluma nyingine za kiisimu kama vile fonolojia, sintaksia na semantiki lakini pia hakuna taaluma inayoweza kusimama peke yake na kukamilisha sarufi ya lugha husika, taaluma zote hutegemeana, huathiriana na kukamilishana katika isimu. Vilevile taaluma  ya mofolojia inamchango mkubwa katika isimu kama vile, husaidia kuainisha lugha mbalimbali, ,huunda maneno mbalimbali  na kueleza kanuni za maathiliano ya vipashio katika maumbo ya maneno. 







                                                             MAREJELEO.
Besha, R.M. (2007). Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es salaam: Macmillan Aidan.
Crystal, D. (1987). The Cambridge Encyclopedia of Language. New York: Oxford University
                               Press.
Fudge, E.C (1973). Phonology, Selected Readings. London: Cambridge University.
Habwe, J na P, Karanja. (2004).  Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers
                                                     Limited.
Massamba, D. (2004) Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha Dar es Salaam. TUKI-UNESCO-SIDA.
Massamba, D. P.B. na Wenzake (2001). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu: Sekondari na Vyuo.  
                                                               Dar es Salaam. TUKI.
Massamba D.P.B. na Wenzake (2013) Fonolojia ya Kiswahili Sanifu. Sekondari na Vyuo.Dar es
                               Salaam: TUKI.  
Obuchi, M.O, na Mukhwana A. (2015) Muundo wa Kiswahili. Ngazi na Vipengele. Nairobi The
                                                        Jomo Kenyatta Foundation.
Rubanza, Y.I (1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar es salaam: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
TUKI (1990). Kamusi ya Isimu na Lugha. Dar es salaam: TUKI.

























AddToAny