Wamitila
(2002) anaeleza kuwa fasihi simulizi ni fasihi ambayo huwasilishwa kwa njia ya
mdomo kwa kusimuliwa, kuimbwa, kutongolewa au kughanwa.
TUKI
(2004) inatoa fasili ya fasihi simulizi kuwa ni fasihi inayohifadhiwa na
kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine kwa njia ya mdomo kama
vile methali, hadithi, ngoma na vitendawili. Fasili hii ina maana kuwa nyenzo
kuu ya uwasilishwaji wa fasihi simulizi ni matumizi ya mdomo na kwamba fasihi
simulizi hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine baada ya kuhifadhiwa.
Kwa
ujumla kutokana na fasili hizi tunaweza kufasili fasihi simulizi kuwa ni sanaa
inayotumiwa lugha ya kusemwa na utendaji inayowasilishwa kwa hadhira kwa njia
ya ana kwa ana.
Wamitila
(2012) anadai kuwa ushairi simulizi ni ushairi ambao huwasilishwa kwa sauti
mbele ya hadhira, ambao hutungwa papo hapo au huwasilishwa kutokana na
kumbukumbu ya muwasilishaji wake.
Anaeleza zaidi kuwa ushairi simulizi ni sehemu ya utamaduni ambao
hurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Asili ya ushairi simulizi inahusishwa na
asili ya ushairi wenyewe hasa katika matambiko ya kijamii. Kuwepo kwa miundo
fulani, ruwaza au mpangilio maalumu wa sauti, ishara na uso. Huu ndio msingi wa
kujulikana kama ushairi simulizi. Wamitila (2012) anaendelea kusema kuwa pana
umuhimu mkubwa wa kutofautisha kati ya ushairi simulizi na tungo ambazo
zimeandikwa kwa minajili ya kuwasilishwa mbele ya hadhira.
Mulokozi
(2017) anasema kuwa ushairi simulizi na nyimbo hakuna utofaauti, yaani ni
ndugu. Anasema kuwa undugu huo unatokana na vigezo fulani vinavyobainisha fani
hizo. Mfano; Nudhumu (utanzu wa kufuata urari wa vina na mizani) matumizi ya
ala za muziki na uzito wa hisia na mkitadha wa uwasilishaji kwa hadhira.
Kwa
ujumla ushairi simulizi ni utanzu unaojumuisha tungo zote zenye mapigo ya
kimuziki, mawazo, hisia, na hoja. Aidha utanzu huu huwasilishwa kwa njia ya
mdomo kwa kutumia lugha ya mkato yenye mpangilio maalumu wa maneno katika
mishororo. Ushairi simulizi huimbwa, hughanwa, au kukaririwa, pia ni muhimu
kujua kuwa ushairi simulizi hutofautiana na mashairi ambayo huandikwa kwa lengo
la kuwasilishwa mbele ya hadhira katika mashindano ya matamasha ya muziki au
yanayowasilishwa katika hadhira maalum.
Wamitila
(2003) anaeleza kuwa tanzu ni istilahi inayotumiwa kuelezea au kurejelea aina
ya kazi mbalimbali za kifasihi. Naye Mulokozi (2017) amefasiri dhana ya tanzu
kuwa ni aina au fungu la tungo za kifasihi zenye vigezo vya tungo na mbinu za
uwasilishwaji wa aina moja au zaidi zinazofanana.
Kwa
ujumla tunaweza kusema kuwa tanzu za fasihi simulizi ni aina mbalimbali ya za
fasihi simulizi mfano hadithi, ushairi, semi na maigizo.
University
of Nairobi (1995) wanafasili dhana ya muundo katika fasihi simulizi kuwa ni
mpango na mtiririko wa kazi ya fasihi simulizi. Wanaendelea kueleza kuwa kwa upande wa visa na
matukio katika muundo huzingatia jinsi fanani anavyofuma na kuunganisha tukio
moja na jingine, pia huangalia jinsi inavyogawanyika kimpangilio, kisura na
kimaonesho.
Kwa
upande wa kipera cha methali, Samwel (2015) anaeleza kuwa ni semo fupi fupi
ambazo hubeba mafunzo mazito na busara za wazee. Pia anaeleza kuwa methali
hubeba falsafa na mtazamo wa jamii juu ya masuala mbalimbali na ndiyo nyenzo
inayotumika zaidi katika kutolea mafunzo. Kutokana na ufupi wake na busara
iliyomo ndani yake, huaminika kuwa methali ni njia bora zaidi ya kuwasilishia
mafunzo na kuikanya jamii. Kwa mfano;
“Asiyesikia
la mkuu, Huvunjika guu.
Kwamujibu
wa Mulokozi (2017) anaeleza kuwa methali ni usemi mfupi wa mapokeo unao dokeza
kwa muhtasari fikra au mafunzo mazito yanayotokana na tajiriba ya jamii
inayohusika. Kwa ujumla medhali ni semi fupi fupi za mapokeo zenye kubeba
mafunzo mazito kwa jamii.
Baada
ya kuangalia fasili hizo muhimu katika swali hili zifuatazo ni tofauti zilizopo
kati ya kipera cha shairi na kipera methali kimuundo,
Methali
na ushairi hutofautiana katika idadi ya maneno, muundo wa methali huweza kuwa
na muundo wa mshororo mmoja wenye vipande viwili. Mfano katika methali zifuatazo;
Mchumia
juani, hulia kivulini
Haba
nahaba, hujaza kibaba
Lakini
katika shairi huwa na mfululizo wa beti nyingi ili kuweza kutoa ujumbe ulio
kusudiwa hivyo huwa na maneno mengi tofauti na methali ambazo huwa na maneno
machache. Samwel (2015) anaeleza kuwa utungo wa ushairi una mishororo mine kwa
kila ubeti na vipande viwili vya mizani nanenane.Mfano katika shairi la “Ajira
za Watoto” la Mutua (2009) lililonukuliwa na Samwel (2015).
“Natunga
nikiwaasa, watoto kutowaajiri
Nawaelezea hasa,
ya mambo ya livyojiri
Ni kinyume shika
sasa, huo ukweli mukiri
Komeni tena komeni watoto
kuwaajiri…”
Kutokana
na hoja hii ni dhahiri kuwa methali na ushairi hutofautiana sana katika kigezo
cha idadi ya maneno.
Shairi huambatana na ala za muziki katika
uwasilishaji wake (sio mara zote). Wakati wa uwasilishaji wa mashairi ala kama
vile ngoma, pembe, vugo na marimba huweza kutumiwa. Tofauti na methali ambazo
katika uwasilishaji wake hazihitaji ala yoyote, hii ni kwa sababu methali
hutolewa kwa mazungumzo bila kuwa na mapigo yeyote ya kimuziki.
Muundo
wa idadi ya vipande katika mshororo mmoja. Samwel (2015) anaeleza kuwa kuna
baadhi ya mashairi yenye vipande vitatu katika mshororo mmoja na mashairi hayo
huitwa ukawafi. Anaeleza zaidi kuwa ukawafi ni bahari ya shairi yenye vipande
vitatu kila mshororo huku kila kipande kikiwa na kina chake. Katika shairi
vipande hivi vina majina, kipande cha kwanza huitwa ukwapi, kipande cha pili
huitwa utao na kipande cha tatu huitwa mwandamizi. Anatoa mfano kutoka wa
shairi la “Biashara” lililopo katika Mbarwa (2000) kama linavyonukuliwa hapa
chini;
“Biashara ni
hasara, huwaka moto, ni kujitolea
Haitaka
fikara, ila mvuto, inaweza kolea
Mbiashara
busara, impa mapato, na kuendelea…”
Lakini
methali huwa na muundo wa vipande viwili tu kwa kila mshororo. Mfano wa methali
ni kama zifuatazo;
i.
Pema usijapo pema, ukipema si pema tena
ii.
Ukiambwa jambwe, usijeamba kumbe
iii.
Hindi ndiko kwenye nguo, na wendao tupu
wako
Hivyo
muundo wa methali na shairi umetofautiana katika idadi ya vipande katika
mshororo kama ilivyofafanuliwa.
Baada
ya kuangalia tofauti zilizopo baina ya shairi na methali, zifuatazo ni hoja
zinazofafanua ufanano baina ya kipera cha shairi na kipera cha methali.
Methali
na shairi huwa na urari wa vina na
mizani, methali nyingi katika jamii za Waswahili aghalabu huwa na urari wa vina
na mizani pamoja na mpangilio mzuri wa vina.Wamitila (2012) anaeleza kuwa sifa
mojawapo ya methali ni urari wa vina na mizani.Mfano wa methali hizo ni;
i.
Hindi ndiko kwenye nguo, na wendao tupu
wako
ii.
Akwitaye kajaza, ukikawia atapunguza
iii.
Mzoea punda, hapandi farasi
Aidha,
suala la urari wa vina na mizani linajitokeza pia katika shairi ambapo Samwel
(2015) anaeleza kuwa shairi huzingatia ubeti wenye vipande viwili vya mizani
nane nane kila kipande. Pia Samwel (2015) anatoa mfano shairi lenye urari wa
vina na mizani liitwalo shairi la “Ulevi”.
“Kuna
wa pombe ulevi, na wengi wake walevi
Alobobea mlevi, aenda kama kiwavi
Atalala kwenye jamvi, jamala yake ugomvi
Hana heshima
mlevi, hakosi kuwa mchimvi…”
Hivyo
utaona kuwa katika shairi hilo la “Ulevi” kina cha kati ni “vi” na vya mwisho
ni “vi”. Pia mizani ya kipande cha kwanza cha shairi inaendana na ile ya
kipande cha pili, ambapo ipo mizani 8 kila kipande. Hivyo ni wazi kusema kuwa
miundo ya methali na ya mashairi aghalabu hufanana.
Vipera
vyote vina muundo wa takriri. Hii ni mbinu ya kisanaa ya kurudiarudia neno au
kifungu cha maneno ili kussitiza ujumbe fulani.
Wamitila (2012) anaeleza kuwa methali huwa na muundo wa takriri ili
kusistiza wazo au jambo linalokusudiwa. Kwa mfano;
i.
Bandu
bandu, humaliza gogo.
ii.
Hayawi
hayawi, yamekuwa.
iii.
Haraka
haraka, haina Baraka.
iv.
Haba
na haba, hujaza kibaba.
v.
Hauchi
hauchi, unakucha
Vilevile
katika mashairi mbinu ya takriri hutumika sana kwani neno au kifungu cha maneno
huweza kujirudia mara kadhaa kwa lengo la kuweka msisitizo juu ya jambo fulani.
Mfano katika shairi la “Nimo” lililoandikwa na Mahiri Mwita na kunukuliwa na
Samwel (2015) matumizi ya takriri yameweza kujidhihirisha kama linavyosomeka
hapa chini;
“Nimo”
“Nimo ndimo mimi nilimo, simo simostahili,
Nimo niwajibikamo,
simo mwenye ujalili,
Nimo nikusudiamo,
simo wanamodhariri,
Nimo nanitakikamo,
simo name kwa thakili,
Nimo kwa kina na
kimo, simo mwa wasokubali,
Nilimo nimo….”
Hivyo
kutokana na mifano tajwa hapo juu ni dhahiri kuwa methali na shairi huwa na muundo
wa takriri
Muundo
wa sehemu mbili, methali nyingi huwa na muundo wenye sehemu mbili, ambapo sehemu
ya kwanza huanzisha wazo fulani na sehemu ya pili hukamilisha wazo hilo. Kwa
mfano;
i.
Haraka haraka / haina Baraka
ii.
Tama mbele / mauti nyuma
iii.
Mdharau mwiba / mguu huota tende
Hivyo
katika methali hizi, wazo linalozingatiwa katika sehemu ya kwanza ya methali
linakamilishwa katika sehemu ya pili. Lakini pia muundo huohuo hutumika katika
mashairi kwani mashairi mengi aghalabu huwa na pande mbili. Kwa mfano katika
shairi la “Kifo” ambalo Samwel (2015) amelinukuu kutoka kwa Muzale (2009).
Kifo ninakukimbia,sauti
kali hewani
Kifo ninakulilia,chozi
hadi miguuni
Kifo ninakutungia,shairi lenye thamani
Kifo ninakuinamia,bila
kofia kichwani.
Hivyo
kipera cha shairi na kipera cha methali zinaufanano wa muundo kwa sababu ya
kuwa na muundo wenye pande mbili.
Kwa
ujumla kipera cha shairi na kipera cha methali hutofautiana halikadhalika
hufanana kama ilivyodhihirishwa katika hoja tajwa hapo juu. Pia methali na
shairi kidhima zote zina jukumu moja la kuelimisha jamii, kuonya jamii,
kuburudisha jamii, kuhifadhi na kutunza amali za jamii na zote hukuza lugha.
Hivyo kipera cha methali na kipera cha shairi ni muhimu kwa jamii zetu.
MAREJELEO
Mulokozi, M. M (2017). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar
es Salaam: KAUTTU
Samwel, M. (2015). Umahiri Katika Fasihi ya Kiswahili. Dar
es Salaam: Mavel
Publishers(MVP)
TUKI
(2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
Dae es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
University
of Nairobi. (1993:45). Annual Report:
Kenya.
Wamitila, K. W. (2003).
Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia.
Nairobi: Focus Publication Ltd.
Wamitila, K. W. (2012).
Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi.
Nairobi: Focus Publication
Ltd.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com