Swali
hili tumeligawa katika sehemu kuu tatu, ambapo sehemu ya kwanza ni utangulizi,
sehemu ya pili ni kiini na sehemu ya tatu ni hitimisho. Ambapo katika
utangulizi tutaeleza nini maana ya dhana telezi, katika kiini tutaeleza utata
au utelezi unaojitokeza katika dhana ya sintaksia na mwisho tutahitimisha.
Dhana
telezi kwa mujibu wa Kamusi Pevu ya Kiswahili (2016), wanasema “telezi”
imetokana na neno teleza ambayo ina maana ya taka kuanguka hasa baada ya
kukanyaga au kupita mahali panya utelezi. Mfano Sakafu hii inateleza. Pili wanasema teleza ni fanya kosa au kutenda
bahati mbaya. Mfano Yule si mwanafunzi jeuri aliteleza tu. Aidha katika mawanda ya taaluma
tunapozungumzia dhana telezi tunamaanisha kwamba ni dhana ambayo inamkanganyiko
miongoni mwa wataalamu yaani mpishano wa wataalamu katika kufasili au kuielewa dhana
hiyo. Utelezi katika taaluma unajitokeza katika dhana mbalimbali ikiwemo tawi
la sintaksia kama tutakavyo liangalia katika swali letu.
Aidha,
katika kufasili dhana ya sintaksia kumekuwepo na utata mkubwa sana, utata huu
unasababishwa na mambo yafuatayo;
Mosi,
sintaksia ni taaluma ya isimu ianayojishughulisha na nini? Kwa mujibu wa Kamusi Sanifu ya Isimu (1990), wanaeleza
kwamba sintaksia ni tawi la sarufi linalojishughulisha na mpangilio na uhusiano
wa vipashio katika sentensi. Pia Kamusi
ya Webster New Collegiate (1979),
wanaeleza kwamba sintaksia ni namna ambavyo maneno huungwa pamoja kuunda
vikundi virai, vishazi au sentensi. Wakati Richard na wenzake (1985), anasema
ni taaluma inayohusu namna maneno yanavyoungana ili kuunda sentensi na vilevile
sheria ambazo husimamia uundaji wa sentensi. Katika fasili hizi kwa mfano
fasili ya kamusi sanifu ya isimu (keshatajwa), na Kamusi ya Webster New
Collegiate (keshatajwa) wanatilia mkazo kwamba sintaksia inajihusisha na
kuchunguza mpangilio na uhusiano wa maneno katika sentensi, wakati tunaona
kwamba Richard na wenzake (keshatajwa)
wanatilia mkazo kwamba Sintaksia ni tawi la isimu linalojishughulisha na mpangilio wa
maneno pamoja na sheria. Mtaalamu mwingine mwenye mtazamo kama huu ni Carnie
(2006), nae anasema kuwa sintaksia inajihusisha na mpangilio pamoja na kanuni
au sheria. Hivyo tunaona utelezi wa dhana ya sintaksia unajitokeza kuhusu nini
hasa Sintaksia inachojishughulisha nacho ambacho kwayo ndiyo cha msingi.
Pili,
Asili ya neno lenyewe sintaksia, kwa mujibu wa Graffi (2001), anasema kwamba
sintaksia ni neno la kigiriki lenye maana ya mpangilio wa vitu pamoja. Katika
asili ya neno lenyewe sintaksia lina maana ya mpangilio ya vitu pamoja, asili
ya neno hilo linaleta utelezi kwani wataalamu wanapofasili dhana yenyewe kuna
vitu wanaviongezea amabvyo ni zaidi ya asili ya neno lenyewe sintaksia.Kwa mfano Massamba ma Wenzake (1999), anafasili
sintaksia kama ni utanzu wa sarufi unaojishughulisha na uchunguzi wa mpangilio
wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipashio vyake. Wanaendelea kusema,
utanzu huu uchunguza sheria au kanuni zinazofatwa katika kuyapanga maneno ili
yalete maana inayokubalika katika lugha husika. Hivyo utaona fasili ya massamba
na wenzake inavuka mipaka ya asili ya neno lenyewe sintaksia. Jambo ambalo
linazua utelezi sana katika kufasili dhana hiyo.
Tatu,
Sheria na kanuni ambazo zinapaswa kufwata ni zipi? Wataalamu kadhaa katika
fasili zao wanadai kwamba sintaksia inajishughulisha na Kanuni au sheria zinazofatwa
katika kuyapanga maneno ili yalete maana. Kwa mfano Massamba na Wenzake
(keshatajwa) wanafasili utanzu kwamba huu unachunguza sheria au kanuni
zinazofatwa katika kuyapanga maneno ili yalete maana inayokubalika katika lugha
husika. Pia Carnie (keshatajwa) sintaksia inajihusisha na mpangilio pamoja na
kanuni au sheria.
Kwa mfano; a) Juma jana alienda
kutembea - Hii inafata kanuni zote hivyo inakubalika
b) Halima amekwenda
shule – Hii inakubalika
a) Alienda
juma jana kutembea - Hii haikubaliki kwani haijafata mpangilio
b) Shule
Halima amekwenda – Hii haikubaliki
Wataalamu
hawa hawatuambii kwamba hizo sheria na kanuni zenyewe zinaitwaje, na ni zipi,
jambo kama hili ndilo linalochangia kuleta utelezi kwenye dhana ya sintaksia.
Nne,
Je sintaksia inatazama mpangilio wa maneno au vipashio katika sentensi? Katika
kufasili dhana ya sintaksia wanatofautiana juu ya nikipi hasa kinachoungana na
kingine ili kuunda sentensi. Kwa mujibu
wa Kamusi Sanifu ya Isimu (1990),
wanaeleza kwamba sintaksia ni tawi la sarufi linalojishughulisha na mpangilio
na uhusiano wa vipashio katika sentensi. Pia Besha (2007), anafasili sintaksia
kama taaluma inayojishughulisha na uchambuzi wa muundo wa sentensi za lugha.
Aidha Habwe na karanja (2004), wanafasili sintaksia kama ni utanzu wa isimu
unaoshughulikia muundo wa sentensi na elementi zinazonda sentensi kama vile
kategoria za maneno, vikundi (virai) na vishazi. Katika fasili hizo zilizotajwa
na wataalamu hao zinaleta mkanganyiko kwani wataalamu wanashindwa kuweka bayana
kama sintaksia inatazama muundo wa maneno katika sentensi? Au vipashio vingine
kama muunganiko wa virai au vishazi. Mikanganyiko hiyo ndio inayoleta utata au
utelezi katika kufasili dhana ya sintaksia.
Tano,
mawanda ya sintaksia yanaanzia kwenye kipashio kipi? Kuna baadhi ya wataalamu
katika kufasili dhana ya sintaksia hawaweki bayana wapi sintaksia inapoanzia
ingawa wengi wanakubaliana sintaksia inaishia kwenye kiwango cha sentensi. Kwa
mfano Besha (2007), hatuambii kuwa sintaksia wapi inaanzia ingawa anatuambia
kuwa wapi sintaksia inapoishia. Pia Kamusi
Sanifu ya Isimu (1990), wanaeleza
kwamba sintaksia ni tawi la sarufi linalojishughulisha na mpangilio na uhusiano
wa vipashio katika sentensi. Ukichunguza fasili za wataalamu hawa hawabainishi
wapi ambapo sintaksia inaanzia, jambo ambalo linaendelea kuibua utata au
utelezi katika dhana hiyo.
Kwa
ujumla, licha ya kuwa dhana ya Sintaksia ni telezi lakini bado inaweza
kufasilika endapo mfasili atazingatia na kuweka bayana baadhi ya mambo katika
fasili yake; Mosi Sintaksia inajishughulisha na nini, pili ni kipashio kipi cha
msingi katika sintaksia ili kuunda sentensi, tatu sheria za sintaksia zinalenga
nini hasa. Kwa kutumia vigezo hivyo tunaweza kufasili sintaksia kama ni tawi la
isimu linalojishughulisha na mpangilio wa maneno katika sentensi ili yalete
sentensi ilete maana.
MAREJELEO
Besha,
R.M (2007) Utangulizi wa Lugha na Isimu.
Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.
Carnie,
A. (2006) Syntax: A generative Introduction (2nd
ed).Oxford; Wiley – Blackwell.
Graffi,G
(2001) 200 years of syntax. A Critical
survey. Amsterdam.
Habwe,
J na karanja, P (2004) Misingi ya
Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publisher.
Massamba,
D na Wenzake. (1999) Sarufi Miundo ya
Kiswahili Sanifu,Sekondari na vyuo. Dar es Salaam: TUKI.
Richard
et al (1985) Dictionary of Applied Linguistics.
Harlow: Longman.
TUKI
(1990) Kamusi sanifu ya Isimu. Dar es
Salaam: TUKI& Philadelphia: Benjamins.
Wamitila,
K.W (2016) Kamusi Pevu ya Kiswahili.
Nairobi: Vide-Muwa Publisher.
Webster
New Collegiate (1979) Webster New
Collegiate Dictionary. Springfield, Mass: G&C Merriam Co.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com