Katika
kujibu swali hili nimeligawa katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni
utangulizi ambapo nimeelezea maana ya nyimbo, usawiri na dhana ya mwanamke na
ufafanuzi kuhusu lugha ya Kijita ambayo nimetumia nyimbo ya lugha hii kuonyesha
jinsi mwanamke anavyosawiriwa. Sehemu ya pili ni nyimbo ambayo zinamuelezea
mwanamke katika jamii na sehemu ya tatu ni kiini ambapo nimeelezea na kufafanua
jinsi mwanamke anavyosawiriwa katika jamii.
Kwa
mujibu wa Okpewho (1992), anaeleza kuwa nyimbo ni sanaa ya kuwasilisha ujumbe
kwa hadhira inayoambatana na mdundo wa ngoma au muziki. Katika uimbaji fulani
hutoa sauti inayoendana na mapigo ya ngoma au mziki na nyimbo hizi huweza
kuimbwa katika tukio maalumu. Hivyo tunaona kuwa fasili ya inajikita katika
vitu viwili, kuwa nyimbo huambatana na mdundo wa ngoma na mziki, lakini fasili
hii imejikita kwenye mdundo wa ngoma tu wakati kuna midundo mbalimbali ambayo
haihusishi ngoma peke yake bali kuna vitu vingine vinavyotoa mdundo.
Halikadhalika,
Wamitila (2008), anafafanua kuwa nyimbo ni sanaa ya uimbaji inayoambatana na
mdundo wa ngoma au muziki ili kufikisha ujumbe kwa hadhira. Anaendelea
kufafanua kuwa mara nyingi nyimbo hizi huwa na muktadha kulingana na ujumbe
uliolengwa, hivyo tunapata nyimbo za ndoa au harusi, hodiya, kimai, nyimbo za
mazishi, nyimbo za kidini na nyimbo za mapenzi. Hivyo tunaona kuwa Wamitila
fasili yake ya nyimbo imejikita zaidi kwenye vitu vitatu ambavyo ni mdundo wa
ngoma, muktadha na ujumbe, halikadhalika tunaona kuwa fasili hii imejikita
kwenye mdundo wa ngoma tu, wakati kuna midundo mbalimbali ambayo haihusishi
ngoma pekee.
Kwa
ujumla tunaona kuwa nyimbo ni aina ya sanaa katika fasihi ambayo hutumia lugha
teule, sauti na kiimbo ili kufikisha ujumbe kwa hadhira lengwa. Pia nyimbo
huusisha ala za muziki kama vile ngoma, gitaa, kinanda na huweza kuimbwa na mtu
mmoja au zaidi.
Wataalamu
mbalimbali wamefasili na kuelezea dhana ya mwanamke na maana ya usawiri kama
ifuatavyo.
Kwa
mujibu wa BAKITA (2015), anafafanua kuwa
usawiri ni kitendo cha kutoa sura halisi ya kitu kwa kutumia mfumo wa kisanii
kwa kalamu, rangi au mashine.
Nae,
Engels (1948), anamuelezea mwanamke kwa kusema kuwa mwanamke alianza kubaguliwa
kipindi kile ambacho jamii iligawanyika katika mfumo wa maisha hasa suala la
umiliki wa mali. Mwanamke huwa anamajukumu ya kufanya kazi zote za nyumbani na
anaonekana hana umuhumi wowote mbele ya mwanaume. Robert (1960), anaeleza
nafasi ya wahusika hususani wanawake kuwa anamwona mwanamke kuwa ni mtu
anayehitaji kusaidiwa, kuthaminiwa na
kuheshimuwa. Mwandishi anatusihii tuwaheshimu wanawake na kuwapa haki zao
wanazostahili kama vile kuwapa uongozi ili waonyeshe uwezo wao na kuacha
kuwabagua. Tunaona anasisitiza zaidi wanawake kuheshimiwa na kupewa haki zao.
Durant
(1985), anafafanua kuwa mwanamke ni binadamu mwenye jinsi ambaye ameshatimiza
umri wa mtu mzima. Anaendelea kusema kuwa kazi nyingi katika jamii hufanya
mwanamke. Anaendelea kusema kuwa kwa asili mwanamke hutaka amani na sio vita,
inaonekana kuwa katika jamii nyingi za viumbe mwanamke hana silka ya ugomvi na
ukorofi akiamua kupigana, basi ni kwa ajili ya watoto wake. Mwanamke ana subira
zaidi kuliko mwanaume ingawa mwanaume ni jasiri zaidi katika kukubaliana na
kazi za hatari na matatizo katika maisha. Mwanamke huwa na uvumilivu mkubwa
zaidi na anaweza kukabiliana na ugumu na kero ndogondogo nyingi vizuri zaidi.
Morris
(1993), anafafanua dhana ya mwanamke kwa kueleza kuwa wanawake wanabaguliwa
katika masuala ya kijamii na kitamaduni hususani kutokana na tamaduni
wanazorithi toka utotoni. Mfano katika jamii nyingi za Tanzania mtoto wa kike
kazi zake ni kumsaidia mama jikoni wakati mtoto wa kiume anasoma na kuhudumiwa
kila kitu. Anaendelea kusema kuwa tamaduni hizi zimepitwa na wakati kwani jinsi
zote zinahaki sawa katika jamii.
Vazir
haleh na wenzake (2003), wanadai kuwa kwa muda wa miongo kadhaa iliyopita,
wanawake wametokea kuwa wenye juhudi nyingi katika masuala ya jamii zao.
Lakini hadi sasa bado wangali mbali sana
na mahali ambapo wangestahili kuwa iwe ni katika sekta ya binafsi au ya umma.
Asilimia ya wanawake wanaoshikilia nafasi za juu za uongozi na usimamizi katika
kazi mbalimbali ni ndogo sana, pia kiwango cha wanawake wanaoshiriki katika
maamuzi ya kiuchumi ya ngazi za juu kimeendelea kuwa kidogo mno. Hadi sasa
serikali zilizo nyingi hazijali wala hazionyeshi nia ya kutaka kukidhi mahitaji
ya kazi za kitaaluma na uongozi kwa wanawake. Utofauti huu wa kijinsia sio
matokeo ya kipengele kimoja tu cha utaratibu wa kihistoria kama vile tabia za
kijamii, dini, mahusiano ya kiuchumi au sheria bali ni matokeo ya mchanganyiko
wa sababu zilizotofauti. Wanawake wengi wanatambua utata wa mfumo wa kijamii
ambao bila sababu za msingi huwanyanyasa na huwanyima nafasi ya kukuza na
kutumia vipaji vyao. Kwa mtazamo huo wanawake wanatambua kuwa tatizo lao kubwa
sio kushindana na wanaume tu bali pia ni
jinsi gani ya kujenga fikra mpya na kusaidia kujenga mfumo mpya wa jamii ambao
umewafunga watu wote.
Kwa hiyo ili wanawake waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo
popote pale walipo, hawana budi wajitahidi kushiriki kadri wanavyoweza katika
masuala ya jamii zao. Ni lazima uwezo na madaraka yao ya utendaji yaimarishwe.
Richard
na wenzake (2007) wanatueleza kuwa, masuala ya wanawake yalianza kuzungumziwa
katika karne ya 19 na kutia fora katika miaka ya 60 na 70 ya karne iliyopita.
Kwa mujibu wa watafiti hawa, wakati huu ndipo wanawake hususani wa Magharibi
walipoanza kuzungumzia masuala yao katika machapisho. Hata hivyo pamoja na
jitihada hizo bado wimbi kubwa la malalamiko dhidi ya dhuluma na uvunjaji wa
haki za wanawake kwa takribani nyanja zote za maisha yalizidi kuongezeka. Kwa
mujibu wa (TGNP 2001), katika bara la Afrika hususani Kusini mwa Afrika,
wanawake wameonekana kuwekwa katika kundi la wanyonge na walioachwa nyuma kiasi
kwamba, bado hawajafaidi hali ya usawa kama walivyo wanaume katika kupata
huduma mbalimbali za kijamii. Hali hii inatushawishi kufanya utafiti ili kuweka
mkakati na mapendekezo ya kumkwamua mwanamke wa Afrika.
Chaligha
(2011), anafafanua kuwa wanawake kwa kiasi kikubwa ndio hupewa majukumu mengi
na makubwa kwenye jamii zao. Anafafanua zaidi kuwa katika uongozi wanawake
hupewa nafasi za chini kuliko wanaume kwa sababu ya kutokuwepo kwa ushirikiano na
kuwaona kuwa wao ni wadhaifu.
Ifuatayo
ni historia fupi kuhusu lugha ya kijita ambayo tumetumia nyimbo za lugha hii
kuelezea jinsi mwanamke anavyosawiriwa kwenye jamii.
Kwa
mujibu wa Massamba (2006), anafafanua kuwa, Wajita ni jamii mojawapo kati ya
jamii zinazopatikana katika nchi ya Tanzania na wanaishi mkoa wa Mara. Nae
Manyama (2013), anafafanua kuwa, neno majita lilitokana na mlima “Masita” ambao ndio chimbuko la jina la
kabila la Wajita na sehemu yao wanayokaa inaitwa Majita. Hii ni kutokana na
kwamba wazungu yaani Wadachi walishindwa kutamka neno masita badala yake
wakatamka majita, hivyo kufuatia matamshi hayo watawala wa kikoloni waliweka
katika maandishi na watu wote mpaka sasa wanaita sehemu hiyo Majita.
Ufuatao
ni wimbo wa Kijita unaoitwa NDOLELA ulioandikwa na kuimbwa na Maringo.
Wimbo
huu katika kabila la wajita huibwa katika sherehe ya harusi na humuhusu
mwanamke anayeolewa, hivyo mwanamke huimbiwa wimbo huu kwenye sherehe yake ya
kuolewa. Katika wimbo huu kiitikio huimbwa kila baada ya kuimba ubeti mmoja.
Kiitikio
Ndolelaa,
ndolelaa bhabha, ndolela karukuru awe
Ndolela
chaseleleka x 2
Mabeti
Lata awe
nyabhusita gutu, ndolela bhabha, (baba mtengeneza zizi, angalia)
gega jing’a jo
omwana wao ugende ulebhe, (chukua ng’ombe za binti yako ukachunge)
Ndolela
chaseleleka. (angalia tunasherehekea)
Mai awe bhuma
ulukendi, ndolela bhabha, (mama piga vigelegele)
Omwana akuyana libhalo,
(binti au mtoto ameleta heshima na baraka)
Ndolela
chaseleleka. (angalia tunasherehekea)
Sengi awe togela
mwenga, ndolela bhabha, (shangazi mfunde au mfundishe vizuri bibi harusi)
Atalija akakinga,
nakuloga, (asije kufika ukweni akakuaibisha)
Ndolela
chaseleleka. (angalia tunasherehekea)
Sengi sengi,
omubhagi, ndolelaa bhabha, (shangazi mfundaji)
Gega manyi
tekela mwenga, (chukua maini mpikie bibi harusi)
Ndolela
chaseleleka. (angalia tunasherehekea)
Sengi awe
nyarugega Magana, ndolela bhabha, (shangazi mchukua mahali)
Nufwafye mwenga
eswe chifuwe, (mvalishe bibi harusi tutoe zawadi)
Ndolela
chaseleleka. (angalia tunasherehekea)
Lata awe nyaluge
Magana, ndolela bhabha, (baba mchukua mahali)
Labha mukwelima
wamubhwene, (kama mkwelima umepata)
Ndolela
chaseleleka. (angalia tunasherehekea)
Mai awe
nusekeseke ndolela bhabha, (mama chekelea tu)
Labha ni
mkwelima wamubhwene, (kama ni mkwelima umempata)
Ndolela
chaseleleka. (Angalia tunafurahia)
Mjomba awe siga
kwifuteta ndolela bhabha, (mjomba usihuzunike)
Gega jimbusi
genda usibhike, (chukua ng’ombe ukachunge)
Ndolela
chaseleleka. (angalia tunasherehekea)
Sengi awe nusige
lila, ndolela bhabha, (shangazi acha kulia)
Labha ni
mkwelima wamubhwene, (kama nimkwelima umepata)
Ndolela chaseleleka.
(angalia tunasherehekea)
Hivyo,
katika wimbo huu tunaona mwanamke anasawiriwa kwa namna mbalimbali kama
ifuatavyo;
Mwanamke kuolewa
ni sifa na heshima kwa familia.
Katika
wimbo huu mtunzi anatuonesha kuwa mwanamke kuolewa ni sifa na heshima kwa
familia. Mtunzi anasema;
Mai awe bhuma ulukendi, ndolela bhabha, (mama piga vigelegele)
Omwana akuyana
libhalo, (binti au mtoto ameleta heshima na baraka)
Ndolela chaseleleka.
(angalia tunasherehekea).(ubeti wa 2)
Halikadhalika
katika jamii zetu tunaona kuwa kutokana na tamaduni na fikra za jamii zetu
mbalimbali, mwanamke kuolewa ni jambo la lazima pindi anapofikia umri wa
kuolewa, ingawaje wengine huolewa wakiwa na umri mdogo. Kutokana na fikra za
jamii zetu za kiafrika mwanamke akikawia kuolewa huonekana na kusadikiwa kuwa
ana mkosi. Hivyo jamii za kiafrika zinabidi zibadilike na kuona kuwa swala la
kuolewa ni jambo la hiari na sio lazima.
Mwanamke
amesawiriwa kama mtu mwenye huzuni, mtu wa kulia kwenye matukio mbalimbali.
Katika wimbo huu tunaona kuwa mwanamke ameonyeshwa kama mtu mwenye huzuni pale
binti yake anapoolewa. Mwandishi anamuonesha shangazi kama mtu anaelia katika
sherehe ya binti yake. Mwandishi anasema;
Sengi awe nusige lila, ndolela bhabha, (shangazi acha kulia)
Labha ni mkwelima
wamubhwene, (kama nimkwelima umepata)
Ndolela chaseleleka.
(angalia tunasherehekea). (ubeti 9)
Halikadharika
katika jamii zetu pia tunaona kuwa wanawake wamekuwa watu wa kulia na kuwa na
huzuni katika matukio mbalimbali, kama vile sherehe au msiba. Mathalani katika
sherehe huweza kuwa na huzuni hasa wazazi wa kike kwa kuonelea kwamba binti wao
anaondoka na kumuacha mpweke na huenda huko anapoenda ataenda kuteseka. Hii
imepelekea kuonekana katika jamii zetu kuwa mwanamke kuwa na huzuni na kulia
katika matukio mbalimbali ni kitu cha kawaida na kuona kuwa wanawake wana mioyo
myepesi isiyoweza kuvumilia mambo mbalimbali.
Mwanamke
amesawiriwa kama mlezi na mtu mwenye majukumu.
Malezi
ni hali ya wazazi au walezi kuwaongoza watoto wao katika misingi na maadili ya
jamii yao. Katika wimbo huu tunaona kuwa mwanamke ndiye aliyeachiwa jukumu la
kuhakikisha mtoto anatabia njema, mwandishi amemuonesha shangazi kama mlezi na
anayetakiwa kuhakikisha binti anatabia njema. Mwandishi anasema;
Sengi awe togela mwenga, ndolela
bhabha, (shangazi mfunde vizuri bibi harusi)
Atalija akakinga, nakuloga, (asije kufika
ukweni akakuaibisha)
Ndolela chaseleleka. (angalia tunasherehekea).(ubeti
3)
Katika
jamii zetu tunaona kuwa jukumu la malezi kwa kiasi kikubwa wameachiwa wanawake.
Mathalani mtoto anapofanya kosa lawama huenda kwa mzazi wa kike pekee wakati
mzazi wa kuime yupo. Momanyi (2001)
anashadidia kuwa, jukumu la malezi ni la wazazi wawili (baba na mama) wa mtoto
na si mmoja peke yake. Kutokana na mfumo dume uliopo katika jamii, mama ndiye
aliyeachiwa jukumu la kulea watoto na baba akishughulika na shughuli za
uzalishaji mali na maendeleo kwa jumla. Hata hivyo, katika hali ya kushangaza
mtoto anapokuwa na tabia nzuri za kusifika katika jamii, baba ndiye hupongezwa
na kupatiwa sifa kwa malezi bora ya mtoto. Inapotokea mtoto huyo akawa na tabia
isiyo nzuri ya kuridhisha, lawama za malezi mabovu humwangukia mama.
Mwanamke
amesawiriwa kama mali ya mwanaume.
Katika
wimbo huu, tunaona kuwa mtunzi amemsawiri mwanamke kama mali ya mwanaume, kwani
kitendo cha mwanaume kutoa mahali ni kama kumnunua mwanamke. Katika wimbo huu
mtunzi anamuonesha baba mzazi wa mwanamke anaeolewa kama mpokea mahali. Mtunzi
anasema;
Lata awe nyaluge Magana, ndolela bhabha, (baba mchukua mahali)
Labha mukwelima
wamubhwene, (kama mkwelima umepata)
Ndolela chaseleleka.
(angalia tunasherehekea.(ubeti 6)
Hivyo
tunaona kuwa katika jamii zetu suala la mwanamke kuwa mali ya mwanaume lipo kwa
kiasi kikubwa. Hii ni kutokana na mwanamke kutolewa mahali jambo linalopelekea
kuonekana kama amenunuliwa na mwanaume. Mathalani migogoro inapotokea baina ya
wanandoa, moja ya jambo ambalo wanawake huambiwa ni kuwa wamelipiwa mahali,
hivyo ni mali ya mwanaume.
Mwanamke
amesawiriwa kama mpishi katika sherehe.
Katika
wimbo huu, tunaona kuwa mwandishi amemsawiri mwanamke kama mpishi. Mtunzi
amemtumia shangazi kama mpishi, ambae alimpikia binti anaeolewa mayai. Mtunzi
katika wimbo wake anasema;
Sengi
sengi, omubhagi, ndolelaa bhabha, (shangazi mfundaji)
Gega manyi tekela
mwenga, (chukua maini mpikie bibi harusi)
Ndolela chaseleleka.
(angalia tunasherehekea).(ubeti wa 4)
Katika
jamii zetu pia wanawake ndio wamekuwa mstali wa mbele katika kazi mbalimbali
ingawaje kadri siku zinavyoendelea wanaume wameanza kuwasaidia katika kazi
mbalimbali. Mathalani wanawake wamekuwa na vikundi mbalimbali kwa ajili ya
sherehe na hafla mbalimbali naa wengine hushona nguo zinazofanana kwa lengo la
kusherekea.
Kwa
kuhitimisha tunaona kuwa mwanamke katika jamii ni moja ya mtu muhimu sana,
hivyo jamii inapaswa na inatakiwa kumthamini mwanamke. Kupitia ushirikiano wa
mwanaume na mwanamke, jinsi hizi mbili zinaweza kuleta mabadiliko na maendeleo
makubwa kwenye jamii pasipo kugandamiza jinsi moja. Mambo mengi katika jamii
zetu yamekuwa kikwazo kikubwa kwa mwanamke hali inayopelekea harakati nyingi za
kimaendeleo za mwanamke kukwama. Hivyo yaipasa jamii kubadilika na kuona jinsi
zote zina haki sawa katika mambo mbalimbali yaliyoko kwenye jamii zetu.
MAREJELEO
BAKITA (2015).
Kamusi Kuu ya Kiswahili, Longhorn
Publisher Limited. Nairobi, Kenya.
Chaligha, E. N. (2011). “Usawiri wa Mwanamke na Mgawanyo wa Majukumu
Kinjinsia katika
Fasihi Picha ya Katuni Mnato
za Kiswahili”
Tasnifu ya M. A Kiswahili, Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam.
Durant, J.
(2000). Two cultures of public
understanding of science. Amsterdam: Harwood
Academic.
Massamba. D.P.B.
(2006). sssKiswahili cha Musoma: Mwanzo
wa lahaja nyingine? Katika
jarida la (TUKI). Dar es
Salaam
Manyama. S.D
(2013).Wajita Zamani mpaka Sasa.
Momanyi, C.
(2001), Nadharia ya Uchanganuzi Nafsia katika Mtazamo wa Kike na Uhakiki wa
Kifasihi: Kioo cha
lugha. Idara ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Morris,
N. (1993). Literacy and health outcomes:
A cross-sectional study in 1002 adults with
diabetes. BMC
Family Practice.
Okpewho, I.
(1992). African Oral Literature.
Bloongton: Indian University Press.
Richard na wenzake. (2007). Nadharia
za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Sai
Industries Ltd.
Richard, J.
(2007). Dictionary of Applied Linguistics.
Harlow: Longman.
Robert, S .(1960s). Kielelezo
cha Insha. Nelson London.
TGNP. (2001). Kuelekea kwenye Usawa: Taswira ya Wanawake
Tanzania. Dar es Salaam.
Vazir haleh na
wenzake (2003). Feminism and Materialism:
Women and Modes of Production. L
Wamitila. K. W (2008). Kanzi ya Fasihi 1. Nairobi: Vide-mu wa Publishers Limited.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com