Flower
Flower

Tuesday, December 18, 2018

FALSAFA ZA KIAFRIKA

Katika kujibu swali hili, kazi hii imegawanywa katika sehemu mbalimbali. Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambayo inaelezea maana ya Falsafa, Falsafa ya Kiafrika, maana ya Riwaya na maelezo mafupi kuhusu Riwaya ya BW. MYOMBEKERE NA BI.BUGONOKA kilichoandikwa na ANICETI KITEREZA. Sehemu ya pili ni kiini cha swali ambayo inaelezea Falsafa mbalimbali za Kiafrika zilizopo kwenye Riwaya na sehemu ya mwisho ni hitimisho.
Kwa mujibu wa Odera (1990) anasema Falsafa ni taaluma ambayo kanuni za msingi kuhusu asili, binadamu na jamii huchunguzwa na kujadiliwa. Odera anazungumzia taaluma ambayo mtu anapaswa kuwa nayo ili kuchunguza jambo fulani na kanuni zake bila kuzitaja kanuni hizo ni zipi hasa ambazo kimsingi inawezekana kuwa hizo kanuni zenyewe ndizo Falsafa. Kwa maana hiyo, hizo kanuni zinapaswa kuwa ndizo Falsafa yenyewe kwa kuwa ndiyo inayomwongoza binadamu kuishi.
Papineau (1993) anaeleza Falsafa ni fikra za ndani kabisa kuhusu maswali magumu ambayo yapo. Mara nyingine unaweza ukadhani kama wanasayansi wanaweza kuyajibu kwa ushahidi lakini hata ushahidi huo ukakosa ukweli wa uwepo wake. Hivyo tunaona kuwa suala la msisitizo katika fasili hii ni fikra za ndani kwa mujibu wa Papineau akimaanisha kuwa hizi ni fikra tu na ikiwa ni fikra tu za ndani basi ni vigumu kujua kama huyu mtu anawaza kuhusu jambo fulani. Kwa maneno mengine ni kuwa, maswali hayawezi kupata majibu kwa kuwa majibu yamebaki kuwa fikra tu za mtu binafsi ambazo watu wengine hawawezi kuziona labda hoja ya msingi ibaki kuwa fikra lakini fikra hizo ziwasilishwe na muhusika kwa ajili ya kupata majibu ya maswali mbalimbali.
Blackburn (1994) anafafanua Falsafa kuwa ni mchakato wa kutengeneza mawazo yaliyo katika utaratibu maalumu yanayotoa tafakuri juu ya ulimwengu, kile kinachofanya uwe vile tunavyoona. Hujaribu kutazama sababu, muda, hiyari, anga na mengine mengi. Mwanafalsafa huyu anaeleza kuwa ni mawazo yaliyo katika utaratibu maalumu kitu ambacho ni sahihi lakini hajafafanua zaidi kuwa nini kifanyike baada ya kuzifahamu sababu hizo na kuna ukweli gani kuhusu sababu hizo. Kwa hiyo ingekuwa vyema zaidi kama mawazo na sababu hizo ambazo zimepatikana kama anavyosema Blackburn zingepimwa kama kuna ukweli wa sababu hizo ndipo mawazo hayo yawe Falsafa ikiwa hicho hasa ndicho alicholenga kukisema.  
Snowden (2014) anafasili dhana ya Falsafa kuwa ni jumla ya majibu yote yanayotolewa juu ya maswali mbalimbali yanayohoji uhalisia wa ulimwengu na maarifa yake kwa kutafuta ushahidi. Snowdon anajikita zaidi katika majibu kitu ambacho ni sahihi kwamba majibu ndiyo yanayofanya watu wafahamu vitu mbalimba. Pamoja na hayo, mwandishi huyu hakutazama upande mwingine wa sarafu kwani hakuchunguza hata ni nini kimetumika kuleta majibu hayo. Vilevile sio majibu pekee ndiyo yanahitajika katika ulimwengu, muda mwingine hata mafunzo tu yanahitajika juu ya ulimwengu. Hivyo alipaswa kujua kuwa hata majibu hayo yalitumia mawazo na maarifa fulani kupatikana ambayo nayo yanaweza kuwa Falsafa.
Hivyo kutokana na fasili za wataalamu mbalimbali tunaweza kusema kuwa Falsafa ni maarifa, miongozo yenye hekima na mawazo ambayo jamii au mtu huamini kuwa ni kweli na kufanya kuwa moja ya misingi katika maisha yake. Vilevile kupitia maarifa hayo ndipo tunaweza kupata utatuzi wa maswali na changamoto mbalimbali zinazohusu jamii na ulimwengu kwa ujumla. Changamoto hizi zinaweza kuwa ni za kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni.
Kuhusu suala la Falsafa ya Kiafrika wataalamu mbalimbali wanasigana, wapo wanaodai kuwa Falsafa ya Kiafrika ipo na wapo wanadai kuwa hakuna Falsafa ya Kiafrika. Kwa mujibu wa Hegel (1837) anaona hakuna Falsafa ya Kiafrika na hategemei kuona ustaarabu wowote kutoka Afrika, Waafrika hawatambui utu wao wala utamaduni wao. Katika mitazamo yake Hegel anasema kuwa Mwafrika hana dini, hana maadili, Mwafrika ni mtu dhalimu na katili. Pia anaendelea kusema kuwa Mwafrika ni mtu anayekula nyama za watu na Afrika ni tofauti na maeneo mengine. Kwa ujumla Hegel anapingana na kuwepo na Falsafa ya Kiafrika.
Tempels (1945) ni mwanafalsafa ambaye anatetea kuwapo kwa Falsafa ya Kiafrika. Anadai kuwa Falsafa ya Kiafrika hujidhihirisha katika Fasihi simulizi, mila na desturi na mifumo mbalimbali ya kijamii. Katika kitabu chake cha La Philosophie Bantu anaeleza kuwa, Falsafa ya Kiafrika hujipambanua katika Fasihi simulizi. Pia mtaalamu mwingine anayeunga mkono kuwapo kwa Falsafa ya Kiafrika ni Mbiti (1960) anadai kuwa Falsafa ya Kiafrika ni uelewa wa maisha ya Kiafrika unaotegemea maadili ambayo Waafrika wanayawaza, wanayatenda katika mazingira tofauti ya maisha yao. Anaendelea kusema kuwa Falsafa ya Kiafrika hujidhihirisha zaidi katika itikeli na maadili yanayohusiana na Waafrika wenyewe.
Kwa ujumla falsafa ya Kiafrika ni ile Falsafa inayosawiri maisha ya Waafrika na kuelezea kwa undani jinsi Waafrika wanavyoishi kwa kuzingatia mila na desturi, kanuni na sheria ambazo wanazifuata kama moja ya misingi ya maisha yao. Pia Falsafa ya Kiafrika hudhiirika katika kazi mbalimbali za kifasihi kwani mwandishi huandika yale mambo ambayo yanaihusu jamii fulani kwa ujumla. Mfano wa Falsafa za Kiafrika ni kama vile ndoa, uchawi na uganga, nguvu uhai, kifo, uduara na kadharika.
Wataalamu mbalimbali wanazungumzia kuhusu dhana ya riwaya. Nkwera (1978) anasema riwaya ni hadithi iliyo ndefu kuweza kutosha kufanya kitabu kimoja au zaidi. Ni hadithi ya kubuniwa iliyojengwa juu ya tukio la kihistoria na kuandikwa kwa mtindo wa ushairi iendayo mfululizo kwa kinaganaga katika kuelezea maisha ya mtu au watu na hata taifa, anaendelea kusema kuwa riwaya ina muhusika mmoja au hata wawili.
Mulokozi (1996) anaeleza kuwa chimbuko la riwaya ya Kiswahili lipo katika mambo makuu mawili ambayo ni fani za kijadi na fasihi pamoja mazingira ya kijamii. Mulokozi anaeleza kuwa riwaya haizuki hivihivi bali ilitokana na fani za masimulizi yaani hadithi na ndipo zikapatwa kuigwa na watunzi wa riwaya wa mwanzo. Fani hizo zilizopata kuchipuza riwaya za mwanzo ni kama vile riwaya za kingano. Hivyo inaonesha kuwa ili kujua maana ya riwaya ni vyema kuzingatia mambo kadhaa ambayo ndiyo ya msingi na mambo hayo ni lazima riwaya iwe na lugha ya kinathari, isawiri maisha ya jamii, iwe na masimulizi ya kubuni na visa virefu, wahusika zaidi ya mmoja, iwe na mpangilio wa msuko na matukio na ifungamane na wakati yaani visa na matukio lazima viendane na matukio.
Riwaya ya Kiswahili ni ile inafungamana na utamaduni wa jamii ya Waswahili katika lugha ya Kiswahili ambao hupatikana katika nchi ya Afrika mashariki na huwahusu Waswahili wenyewe. Muhando na wenzake (1997) wanasema riwaya ni kazi ya kubuni, ni hadithi ambayo hutungwa kufuatana na uwezo wa fanani kuibusha mambo kutokana na mazoea au mazingira yake, wanaendelea kusema kuwa riwaya yaweza kuanzia maneno 35000 na kuendelea.
Wamitila (2003) anasema riwaya ni kazi ya kinathari au kibunilizi ambayo huwa na urefu wa kutosha, msuko uliojengeka vizuri, wahusika wengi walioendelezwa kwa kina yenye kuchukua muda mwingi katika mandalizi na kuhusisha mandhari maalumu.
Madumulla (2009) anaeleza kuwa riwaya ilitokana na nathari bunifu simulizi kama vile hadithi, hekaya na ngano inayosimuliwa kwa mdomo. Anaendelea kusema kuwa fasihi ilitokana na mazumgumzo ya fanani ya ushairi na tendi za Kiswahili katika hati za kiarabu kwa sababu ndio maandishi yaliyotamba katika pwani ya Afrika Mashariki. Kwa ujumla Riwaya ni kazi ya fasihi andishi ambayo kwa kawaida ni ndefu kuliko hadithi fupi yenye wahusika wengi na msuko wa matukio mengi na msuko huo umejengeka vizuri na mada zake ni nzito na pana kiasi.
Kwa ufupi riwaya ya Bw. Myombekele na Bi Bugonoka ni Riwaya ambayo imeandikwa na Aniceti Kitereza mwaka (1980). Ni riwaya inayoelezea kuhusu maisha ya Bw. Myombekele na mkewe Bi. Bugonoka. Hawa ni wanandoa ambao walikuwa na tatizo la kutopata mtoto, hii ni kutokana na Bi. Bugonoka kuwa na tatizo la uzazi. Tatizo la uzazi linapelekea ndoa yao kuingia kwenye mgogoro mkubwa kupelekea ndugu wa Myombekele kumtaka amfukuze mke wake. Tatizo hilo linapelekea wazazi wa Bugonoka kumchukua Bugonoka kutokana na kusikia maneno mengi anayotukanwa na ndugu wa Myombekele. Kutokana na upendo aliokuwa nao  Myombekele inampelekea kwenda kwa wazazi wa Bugonoka ili kuomba radhi ili arudishiwe mke wake. Katika kuomba radhi anapewa masharti na anayatimiza na kuweza kurudishiwa mke wake. Harakati za maisha zinaendelea na kutokana na upendo wa Myombekele kwa mkewe anaamua kutafuta waganga ili waweze kutatua tatizo lao la uzazi. Katika riwaya hii kuna vipengele vingi vya Kifalsafa vinavyojitokeza.
Kwa mifano bayana Vifuatavyo ni vipengele vya Falsafa ya Kiafrika vinavyojitokeza katika riwaya ya Bw. Myombekele na Bi. Bugonoka.
Falsafa ya ndoa
Hiki ni kipengele kimojawapo cha Falsafa ya Kiafrika kinachojitokeza katika riwaya hii. Temples (1945) anafafanua kuwa katika maisha ya Waafrika ndoa na mimba ni vyanzo vya uhai na hudumishwa kwa kuwa na mtoto au watoto. Hivyo anadai kuwa ili maisha ya wanandoa yaendelee na yazidi kuwa ya amani na upendo lazima suala la mimba na watoto lihusike kwa kiasi kikubwa. Hivyo katika riwaya hii tunaona jinsi ndoa ya Myombekele na Bugonoka inavyoingia kwenye mgogoro baada ya Bugonoka kuwa na tatizo la uzazi. Hii ilipelekea ndugu wa Myombekele kutaka Bugonoka afukuzwe na aweze kuoa mke mwingine. Wazazi wa Bugonoka waliposikia habari hizo walichukizwa na kitendo hicho wakaenda kumchukua. Mwandishi anasema;
                      “jamaa zake wakanena, sisi tunataka umkatae mke wako huyu upose
                        mwingine, ukaoe. Sababu kama ukikaa na huyu tu hutafanikiwa kupata
                        mtoto kamwe! Maneno yalizidi kuendelea kwa mfululizo hata yakafika kwa
                        wakwe zake Myombekele, walikasirika sana wakakata shauri
                        kwenda kumchukua wamrudishe nyumbani kwao”. (Uk1)                  
Pia katika maisha ya Kiafrika tunaona kuwa kwenye jamii mbalimbali suala la ndoa huweza kupata migogoro mbalimbali kutokana na wanandoa kushindwa kupata mtoto. Jamii nyingi za Kiafrika hutegemea kuwa pindi watu wanapooana kazi iliyobaki ni kuzaa na kulea watoto, lakini wanandoa hao wakichelewa kupata mtoto hupelekea jamii na ndugu kujiuliza maswali mengi. Ndoa nyingi zimeingia kwenye mgogoro katika jamii za kiafrika kutokana na mwanamke kushindwa kupata mtoto.
Falsafa ya Kifo
Wanafalsafa mbalimbali wamefasili dhana ya kifo. Kwa mujibu wa Mbiti (1990) anafasili dhana hiyo kuwa kifo humuondoa mtu taratibu kutoka sasa na kumpeleka zamani. Kwa Waafrika kifo husababishwa na uchawi, roho za wafu, laana na kifo cha asili, Anadai kuwa mtu hufa taratibu mpaka watu wanaomkumbuka waishe. Pia Wilson (1957) anafafanua dhana ya kifo kuwa kuna majukumu amabayo huendelea kati ya watu waliohai na waliokufa. Anaendelea kusema kuwa kwa Waafrika watu walio hai kiroho na kimwili jukumu la walio baki ni kuwakumbuka waliokufa, kuwaheshimu, kuwaabudu na kutunza imani zao. Katika riwaya hii mwandishi anatuonyesha jinsi dhana ya kifo ilivyojitokeza. Anaelezea kwa kuonesha jinsi mtoto wa kike wa Bugonoka alivyofariki siku chache tu baada ya mtoto huyo kuzaliwa. Mwandishi anasema;
                      “Baada ya siku chache, mwanamke akapata tena mimba ya pili
                        na hiyo alidumu nayo kwa muda wa miezi sita na mwezi wa saba
                        akaavya tena, akatoka mtoto wa kike; kitoto kiliishi siku moja tu,
                        siku ya pili yake kikaaga dunia”. (Uk1)
Hivyo tunaona jinsi binadamu na Waafrika kwa ujumla wanavyokuwa na hofu ya kifo. Katika jamii zetu za Kiafrika katika msiba watu huweza kulia na hata kuzimia pale ambapo humpoteza mtu ambaye walikuwa wanampenda au alikuwa na umuhimu katika jamii.
Falsafa ya Uduara
Temples (1945) anafafanua dhana ya uduara kuwa, utamaduni wa Mwafrika uko katika uduara. Anaendelea kueleza kuwa vitu vingi anavyotumia Mwafrika viko katika uduara, mfano ngoma, vigoda, nyumba, umoja na ushirikiano. Katika riwaya hii tunaona dhana ya uduara inavyojitokeza. Mwandishi anatuonesha umoja na ushirikiano baina ya Myombekele na Nkwesi pale Myombekele alipokuwa anatengeneza ndizi ili aweze kupika pombe ya kupeleka ukweni. Alitakiwa kutengeneza pombe kama adhabu ili aweze kumchukua mke wake aliyempenda baada ya wazazi wake kumchukua. Nkwesi pamoja na wake zake na ndugu zake watatu  kwa umoja wao waliamua kumsaidia Myombekele bila hata ya kuwalipa kitu chochote ili aweze kutengeneza pombe. Mwandishi anasema;
                      “Walipofika kule, wakazikuta ndizi madhubuti hasa. Basi
                        wakajitutumua kuzichukua, wanaume kwa wanawake na watoto
                        wao. Yule mtoto mdogo mwanaume pamoja na wanawake
                        wakachaguliwa ndizi zinazoweza kuchukuliwa mojamoja.
                        wakatengeneza kata zao na kujitwika. Vijana wakubwa wakafunga
                        ndizi sita katikati ya mti wao, wakazipeleka kwa uchovu
                        mwingi, wakitokwa jasho, hadi penye embiso.” (Uk 70)
Pia katika jamii za Kiafrika, watu huwa na umoja na ushirikiano katika matukio mbalimbali ambapo huweza kutuonesha dhana ya uduara. Mfano katika sherehe mbalimbali watu hukusanyika na kusaidiana katika kufanikisha sherehe hizo kwa kufanya kazi mbalimbali. Vijijini pia watu husaidiana katika shughuli za kilimo, wakulima hukusanyika na kuweza kumsaidia jamaa yao kulima shamba lake bila hata ya malipo, hivyo kuonesha dhana ya uduara Kwenye jamii zetu. Dhana ya uduara ina umuhimu kwani huweza kuleta maendeleo katika jamii zetu.

Falsafa ya Uganga na Uchawi
Kwa mujibu wa Samweli (2015) anafafanua kuwa jamii nyingi zinatofautisha dhana ya uganga na uchawi. Uganga unachukuliwa kuwa ni ile hali ya kupata tiba asilia juu ya matatizo ambayo yameshindwa kupata tiba kitaalamu. Anaendelea kusema kuwa waganga katika jamii mbalimbali za Kiafrika kwa kawaida hutumia mitishamba, mizimu, miungu na mengine yanayofanana na hayo ili kutoa tiba. Uchawi anaufafanua kuwa ni ujuzi katika mambo ya kimila yanayompa uwezo mtu kumdhuru mwingine, hivyo wakati ambapo uganga huonekana kama dhana chanya, uchawi huonekana kama dhana hasi.
Katika riwaya hii mwandishi anatuonesha jinsi uganga na uchawi unavyojitokeza. Kwa kuanza na uganga mwandishi anatueleza kuwa katika jamii ya Abakerebe mganga huitwa Omufumu. Myombekele alikwenda kwa mganga anayeitwa Kibuguma ili aweze kumtibu mke wake aweze kuzaa. Bugonoka alikuwa na tatizo la uzazi hivyo kupelekea kutafuta mganga wa kumtibu baada ya kukubaliana na mume wake kuwa watafute mganga ili waweze kupata tiba ya tatizo hilo. Walikubaliana na kwenda kwa mganga, walipofika mganga aliwaeleza matatizo yanayomfanya Bugonoka asizae. Mwandishi anasema;
                      “Kibuguma naye alifurahi sana kuwaganga, akisema, “Mwanamke
                        huyu ana bahati kubwa sana kwa sababu ramli yake imependeza sana,
                        hata nimeona sababu yenyewe kweli iliyowauwa watoto wake.
                        Yeye ana mchango tumboni mwake uitwao enzoka y’ihuzi ndiyo
                        hata wewe mwanaume huna kitu cha ubaya wa mzimu”. (Uk 154)
Pia katika suala la uchawi mwandishi anatuonesha jinsi Omukama alivyoingiliwa na mchawi nyumbani kwake. Mwandishi anasema;
                      “Basi kwa kujitakia maovu, siku moja usiku alikwenda kuloga
                        wanawake wa Omukama katika makao makuu uwanjani hasa,
                        tena alikuwa uchi wa mnyama! Mnajua siri zote ya kama Abakama
                        wote hapa nchini wanao uwezo wa kuona kila kitu japo mtu akijigeuza
                        kuwa mnyama, yote hayo ni bure hakuna mchawi wa
                        kumshinda Omukama”. (Uk 182)
Katika jamii zetu za Kiafrika pia masuala ya uganga na uchawi yapo kawa kiasi kikubwa. Katika suala la uganga, wapo wanaoamini waganga wa jadi ndio watu wa muhimu sana pale wanapopata matatizo mbalimbali lakini pia wapo ambao hawaamini katika uganga kutokana na imani zao. Pia suala la uchawi katika jamii za Kiafrika lipo kwa kiasi kikubwa kwani tunashuhudia baadhi ya wanajamii wakiwaua vikongwe ambao wanamacho mekundu kutokana na imani za kishirikina. Uchawi pia huweza kuleta migogoro na mafarakano katika jamii.
Falsafa ya Uhusiano wa Mwanamke na Mwanaume.
Victoria (1997) anafafanu kuwa nafasi ya mwanaume na mwanamke imegawanyika kutokana na mambo kama vile ubinafsi, na mila na desturi. Anaeleza na kutoa pendekezo kuwa kikwazo kikubwa katika matatizo ya kijamii ni ubinafsi baina ya wanawake na wanaume, ubinafsi huo sio mzuri kwani katika kuleta maendeleo ya jamii nzima mwanamke na mwanaume wanatakiwa kuwa na umoja na ushirikiano mzuri. Hali ya kuwepo kwa ubinafsi na utengano kati ya mwanaume na mwanamke hurudisha maendeleo nyuma. Naye Chaligha (2011) alitafiti kuhusu mgawanyo wa majukumu na kuona kuwa mgawanyo wa majukumu kwenye jamii mbalimbali kati ya mwanamke na mwanaume hauko sawa kwani wanawake kwa kiasi kikubwa ndio hupewa majukumu mengi na mazito kwenye jamii zao.
Mwandishi anatuonesha jinsi mwanamke alivyokuwa akitegemewa katika kufanya kazi nyingi za nyumbani na shambani. Mwandishi anatuonesha jinsi mke wa Kibuguma alivyokuwa akilalamika kuwa mme wake anajua kula tu huku kufanya kazi ni mvivu hasa katika kulima. Mwandishi anaelezea jinsi Bugonoka alipokuwa akimwambia mume wake jinsi Weroba ambaye ni mke wa Mganga alivyomuambia kuhusu uvivu wa mume wake. Mwandishi anasema;
                      “Yeye mume wangu huyu, niseme hivyo, anahimiza juu ya
                        chakula hivyo, kwanza yeye halimi, hata usimuone vile dada
                        ukadhani kwamba analima. Ee! ni mimi tu hapa ninalima peke
                        yangu na vitoto vyangu hivi. Yeye ni mvivu sana wa kupindukia,
                        akinifuata shambani.” (Uk 215)
Pia mwanamke ameonekana kama mtu wa muhimu kwenye mji. Hii imejidhihirisha baada ya mke wa Myombekele kuchukuliwa na wazazi wake. Mwandishi anatuonesha jinsi Myombekele alivyopata taabu katika kufanya kazi na hata kupika chakula. Mwandishi anasema;
                      “Bwana Myombekele alisumbuka kabisa sababu ya kukosa mwanamke;        
                        wakati mwingine alikuwa anatembea tembea ovyo mijini mwa jamaa
                        zake na za watu wengine akitafuta chakula. Taabu ya mtu mzima
                        ikawa mzigo mzito kwake. Mara nyingine alishinda na njaa mchana
                        Siku zingine alikuwa akikoka moto nje na kuchoma viazi na Mihogo.    
                        Wakati mwingine akilala na njaa usiku hata na maziwa ya ng’ombe
                        zake nayo kusema kweli yalimchachia kwa ajili ya kunyang’anywa
                        mke wake, sababu katika mila za Bukerebe, wanawake ndiyo
                        wajengaji na waezekaji wa mji hasa. Mtu kama alikwisha kuoa halafu
                        akafarakana na mkewe , mji wake hauwi wa hali ya kupendeza”. (Uk 10)
Hivyo tunaona kuwa katika jamii za Kiafrika wanawake wamekuwa wakifanya kazi sana huku wanaume wao wakiwa wamestarehe na wengine wakinywa pombe bila ya kuwasaidia wake zao. Waafrika wengi katika jamii wanadhana potofu kuwa kuna kazi za wanaume na kazi za wanawake hii kupelekea kuwepo na matabaka na mpasuko mkubwa katika jamii.
Falsafa ya Nguvu uhai.
Kwa mujibu wa Temples (1945) anafasili Falsafa hii kuwa nguvu uhai inahusisha tabia, ontolojia, hekima na maadili. Mungu ndiye mwenye nguvu uhai kubwa kuliko viumbe wengine wote. Tunaona jinsi Myombekele alivyokuwa akimuamini Mungu kuwa ni muweza wa yote. Falsafa hii imejitokeza pale Myombekele alipokuwa akiomba radhi na kusema kuwa mpango wa kuzaa ni Mungu ndiye anayepanga. Mwandishi anasema;
                       “mimi ndimi mwenye laana ya maulana, ambaye labda amekwisha
                         kutamka: “wewe hutazaa mtoto maishani
                         mwako, mpaka kufa!” ijapo nikioa wanawake
                         wengi, nisipojaliwa na Mungu yote hayo ni ya bure”.(Uk 16)
Hivyo tunaona kuwa Myombekele anaamini kuwa suala la kuzaa kwa mke wake ni mipango ya Mungu ndiye anayeamua. Katika jamii zetu za Kiafrika watu mbalimbali wana imani tofautitofauti juu ya Mungu, lakini wengi humuamini Mungu na kumuomba kwa kusali ili aweze kutatua matatizo yao. Waafrika huamini pia kuwa Mungu ndiye mwenye nguvu uhai kubwa kuliko watu wote.
Kwa kuhitimisha, tunaweza sema kuwa Falsafa ya Kiafrika imejikita hasa kuelezea mfumo mzima wa maisha anayoishi Mwafrika na ukweli kuhusu fikra, mila, utamaduni, na mienendo yake katika jamii. Kwa sasa Falsafa ya Kiafrika imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na Falsafa ya kimagharibi hususani suala zima la utandawazi. Kuna mambo mbalimbali kama vile, mavazi, vyakula, dini, mfumo wa elimu na afya, vyote vimebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuzuka kwa utandawazi. Pia maendeleo ya sayansi na teknolojia yamesababisha Falsafa ya Kiafrika kwa kiasi kikubwa kupotea, mfano ngoma za jadi katika kizazi hiki zinazidi kupotea kutokana na kuibuka kwa taaluma ya muziki kutoka katika jamii za kimagharibi.
Kuna Falsafa ambazo zina umuhimu katika jamii na Falsafa ambazo hazifai kuendelea kutumika katika jamii zote za Kiafrika. Waafrika inabidi tufuate imani, misingi na kanuni ambazo zinaleta mafanikio na maendeleo katika jamii zetu na sio kufuata mambo ambayo yanagandamiza na kuegemea upande mmoja. Kuna umuhimu wa kujifunza Falsafa mbalimbali kwani, Falsafa inaweza kuelimisha, kuonya, kuasa na kuweza kusaidia katika kujenga na kuleta maendeleo katika jamii zetu.









MAREJELEO
Blackburn, S. (1994). The Oxford Dictionary of Philosophy. British: Oxford University Press.
Chaligha, E. N. (2011). “Usawiri wa Mwanamke na Mgawanyo wa Majukumu Kinjinsia katika 
                 Fasihi Picha ya Katuni Mnato za Kiswahili” Tasnifu ya M. A Kiswahili, Chuo Kikuu                                 
                 cha Dar es Salaam.                                                           
Hegel, G. W. F. (1945). Introduction to the Philosophy of History. Cambridge: Hacket                                                                                       
                Publishing.
Kitereza, K. (1980). Bw. Myombekele na Bi. Bugonoka. Dar es Salaam: Tanzania Publishing                                           
               House.

Madumulla, J. S. (2009). Riwaya ya Kiswahili, Historia na Misingi ya Uchambuzi. Nairobi:
                    Sitima Printer and Station Ltd.

Mbiti, J. (1990). African Religion and Philosophy. New York: Praeger Publisher.
Muhando, P., & Balisidya. (1976). Fasihi na Sanaa za Maonyesho. Dar es Salaam: Tanzania    
                Publishing House.
Mulokozi, M, M. (1996). Fasihi ya Kiswahili. Dar es salaam: The Open University of Tanzania.

Nkwera, F. (1978). Sarufi na Fasihi Sekondari na vyuo. Dar es salaam: Tanzania Publish House.

Odera, H. (1990). Trends in Contemporary African Philosophy. Nairobi: Shirikon Publishers.
Papineau, D. (2009). Philosophy. Duean Barid Publisher.
Samwel, M. (2015). Umahiri katika Fasihi ya Kiswahili. Dar es Saalaam: Meveli Publishers.
Snowden, J. (2014). Phylosophy & Social critics. Newyork: Routedge.
Tempels, P. (1945). Bantu Philosophy. Paris: Presence Africaine Publishers.
Victoria, H, P. F. (1997). Preventing Violence before it Occurs: Victorian Health Foundation.

Wamitila, K. Y. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Publication Ltd.

Wilson, C. (1957). Religion and the Rebel. England: Aristeria Press.




No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny