Katika
kujibu swali hili, tumeligawa katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni
utangulizi ambapo tumeelezea istilahi mbalimbali zilizopo katika swali letu ,
sehemu ya pili ni kiini na sehemu ya mwisho ni hitimisho.
Kwa
mujibu wa Sengo (2009) anafasili nadharia kuwa ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo
mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani kwa sababu fulani. Naye Mdee (2011)
anaelezea nadharia kuwa ni mpango wa mawazo uliotungwa ili kueleza jinsi ya
kufanya au kutekeleza jambo. TUKI (2004) wanasema nadharia
ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au
kutekeleza jambo fulani.
Kwa
ujumla nadharia ni mawazo, dhana au maelezo yanayotolewa kuelezea hali fulani: chanzo
chake, muundo wake, utenda kazi wake na mwingiliano wake wa ndani na nje.
Baada
ya kuangalia maana ya nadharia pia wataalamu mbalimbali wamezungumzia maana ya
nadharia ya tafsiri kama ifuatavyo.
Halikadharika
Newmark (1982) anasema kuwa kuna maana finyu na maana pana ya nadharia ya
tafsiri. Katika maana finyu anafasiri kuwa ni mbinu inayofaa kutumika kutafsili
matini ya aina fulani mahususi. Aidha katika kufasili maana pana anafasili kuwa
ni jumla ya maarifa yanayopatikana na yatakayopatikana katika mchakato wa
kutafsiri kuanzia msingi na kanuni za jumla hadi miongozo na mapendekezo muhimu.
Anaendelea kusema kuwa kuna sababu za kuanzishwa kwa nadharia ya tafsiri ambazo
ni wingi wa makosa katika tafsiri zilizochapishwa awali. Kuwepo kwa idadi kubwa
ya mashirika na asasi zinazojishughulisha na kutafsiri matini mbalimbali na mfumuko
wa istilahi katika taaluma mbalimbali hususani sayansi na teknolojia. Tunaona
kuwa katika fasili ya Newmark haweki wazi ni matini gani hizo zinazopaswa
kushughulikiwa.
Kwa
mujibu wa Wanjara (2011) anasema kuwa nadharia ya tafsiri huchunguza mbinu mwafaka
za kutumika katika mchakato wa kutafsiri kwa ufanisi matini ya aina fulani
mahususi. Ni jumla ya mawazo au maarifa katika mchakato wa kufasiri misingi na
kanuni za jumla na miongozo, mapendekezo na vidokezo muhimu. Wanjara pia katika
fasili yake haweki wazi mbinu hizo zinatumika katika kutafsiri matini ipi na
kanuni na miongozo inatumikaje kwenye hiyo matini.
Halikadhalika
Mwansoko (2013) anasema kuwa nadharia ya tafsiri ni nguzo au muhimili wa nguzo
ya tafsiri. Ni msingi wa kazi zote za tafsiri. Anaendelea kusema kuwa nadharia
ya tafsiri ni maelezo kuntu ya vipengele vinavyopaswa kuzingatiwa na kila
mfasiri kila akabiliwapo na kazi ya kufasiri. Mwansoko katika fasili yake
haweki wazi misingi na vipengele vinatumika kwenye matini ipi katika kutafsiri.
Kwa
ujumla tunaona kuwa nadharia ya tafsiri ni mawazo au muhimili unaomwongoza
mfasiri juu ya vipengele muhimu anavyopaswa kuvishughulikia katika mchakato
wakufasili kutoka matini chanzi kwenda matini lengwa. Au ni maelezo muhimu
kuhusu vipengele mbalimbali vya kifasiri ambavyo vinapaswa kufuatwa au
kuzingatiwa na kila mfasiri pindi anapokabiliwa na kazi ya kufasiri.
Wataalamu
mbalimbali wanafasili maana ya tafsiri kama ifuatavyo. Nida na Taber (1969) wanaelezea
tafsiri kuwa ni uzalishaji upya wa ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe asili
vya lugha lengwa vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi, kwanza kimaana na pili
kimtindo. Nida na Tiber wanaona kuwa
katika tafsiri kitu muhimu ni kuzingatia maana na mtindo.
Cartford
(1995) anasema tafsiri ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha
moja ( lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana na hayo kwenda
lugha nyingine (lugha lengwa). Catford anajikita katika ulinganifu wa mawazo
katika kazi ya kutafsiri kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
Kwa
mujibu wa TUKI (2002) wanaeleza kuwa tafsiri ni kutoa mawazo kutoka lugha moja
kwenda lugha nyingine bila ya kubadilisha maana. Fasili ya TUKI imejikita katika maana yaani unapotafsiri
hutakiwi kubadili maana iliyoko kwenye lugha moja.
Mshindo
(2010) anasema kufasili ni kufafanua maana ya matini moja na kutayarisha baadae
matini nyingine inayowiana nayo ambayo huitwa tafsiri na ambayo inawakilisha
ujumbe uleule uliomo katika matini ya awali kwa kutumia lugha nyingine. Fasili hii pia inajikita katika ujumbe na maana
uwiane kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine. Kwa ujumla tafsiri ni
uhawilishaji wa mawazo, taarifa au ujumbe kutoka lugha chanzi kwenda lugha
lengwa.
Baada
ya kuangalia istilahi mbalimbali zilizopo kwenye swali kama zilivyofafanuliwa
na wataalamu, ufuatao ni umuhimu wa nadharia ya tafsiri katika taaluma ya
tafsiri.
tunaona
kuwa nadharia ya tafsiri inajumuisha nadharia mbalimbali ambazo hutumika katika
kazi ya tafsiri. Nadharia ya Usawe wa Kimuundo, nadharia hii inatetewa na
mtaalam Cartford (1995) anasema tunapofanya kazi ya kutafsiri tunatakiwa
kuzingatia ulinganifu wa kimuundo kati ya matini chanzi na matini lengwa, maana
yake ni kwamba muundo wa matini chanzi ujitokeze katika matini lengwa. Pia
nadharia hii hutumika zaidi katika kutafsiri maandiko ya kidini hasa Biblia.
Nadharia
nyingine ni nadharia ya Usawe wa Kidhima, watetezi wa nadharia hii ni pamoja na
Nida na Taber (1969) wanaona kuwa usawe wa kidhima ni muhimu zaidi kuliko usawe
wa kimuundo. Wafasiri wanapaswa kuhakikisha kwamba dhima ya matini chanzi
pamoja na athari zake zinajitokeza katika matini lengwa. Yaani kama matini
chanzi inawalenga watoto inapaswa iandikwe. Pia Nadharia ya Usawe wa
Aina-matini, matini yoyote ile ifasiriwe kwa kuzingatia aina yake. Hii inamaana
kwamba kazi itakayotokea itafanana na matini chanzi, kama matini chanzi ni ya
kisheria itakapotafsiriwa matini lengwa nayo itaonekana kuwa ya kisheria. Nadharia
Changamani hii ni nadharia tete inadai kwamba huwezi kufanya tafsiri kwa
kutumia nadharia moja tu, kwa sababu hakuna nadharia inayojitosheleza yenyewe.
Baada
ya kuangalia dhana mbalimbali za nadharia ya tafsiri kwa mujibu wa wataalamu,
ufuatao ni umihumu wa nadharia ya tafsiri.
Wanjara
(2011) anaelezea kuwa nadharia ya tafsiri husaidia kuonesha mbinu ambazo
zinazofaa kutumiwa kufasilia aina mbalimbali za matini. Anaendelea kusema kuwa
nadharia hizi za tafsiri husaidia au humpa mwosngozo mfasiri kujua mbinu muhimu
ambazo hazina buni kufuatwa wakati wa kutafsiri matini yoyote.
Mfano: mbinu hizo ni pamoja na
tafsiri ya neno kwa neno, tafsiri sisisi, tafsiri ya kisemantiki na tafsiri ya kimawasiliano.
Hii
ni kwa sababu mbinu hizi ndizo zinakidhi malengo makuu ya tafsiri, malengo hayo
ni kutoa taarifa kuhusu mambo mbalimbali kwa kutumia lugha.
Newmark
(1982) anasema kuwa nadharia ya tafsiri husaidia kutoa misingi, kanuni, sheria
na vidokezo vya kufasiri matini na kuhakiki tafsiri, yaani matini zilizokwisha
tafsiriwa.
Mfano: mambo muhimu ambayo
hayana budi kuzingatiwa wakati wa mchakato wa uchambuzi wa matini ni kusoma
matini nzima na katika usomaji wa matini nzima dhumuni lake ni kubaini lengo la
matini, kubaini lengo la mfasiri, kubaini wasomaji lengwa, umbo la matini lengwa
na kubaini mtindo wa matini chanzi. Pia kusoma matini kwa mara ya mwisho.
Anaendelea kusema kuwa kuna hatua muhimu za kufuata kama vie maandalizi,
uchambuzi, uhawilishaji, kusawidi rasimu ya kwanza, kudurusu rasimu ya kwanza
ili kupata rasimu ya pili, kusoma rasimu ya pili na mtu mwingine na kusawidi
rasimu ya mwisho.
Mwansoko
(2013) anaelezea kuwa nadharia ya tafsiri husaidia kueleza jinsi ya
kuvishughulikia vipengele vidogovidogo katika tafsiri kama vile maana na
umuhimu wa vistari, nukta, mkato, italiki, makosa ya uchapaji na mambo mengine
kwa ujumla.
Mfano: maana na nguvu za taarifa
zinazobebwa na sitisri, uwasilishaji katika matini ya maudhui na fani yote,
haya yana uzito sawa na mazingatio mengine ya zoezi la tafsiri. Mfano asiyejua
utu si mtu. Katika mfano huu neno utu litatiliwa mkazo katika mchakato wa
tafsiri tofauti na maneno mengine yaliyo katika matini hiyo.
Nadharia
husaidia kupata visawe vya maneno katika lugha lengwa. Nider na Taber (1969)
wanafafanua kwa kutumia nadharia ya usawe wa kidhima ambapo wanasema wafasiri
wanapaswa kuhakikisha kwamba dhima ya matini chanzi pamoja na athari zake
zinajitokeza katika matini lengwa. Yaani kama matini chanzi inawalenga watoto inapaswa ipatiwe visawe vya
maneno yanayoendana na watoto katika lugha lengwa.
Kwa
kuhitimisha tunaona kuwa Kuna changamoto mbalimbali zinazoikumba kazi ya
tafsiri kama vile uelewa mdogo watu wanaofanya kazi ya kutafsiri, kukiuka taratibu
na kanuni za kazi za tafsiri kwa wafasiri mbalimbali na upotoshaji wa mawazo
yaliyopo kwenye matini chanzi pale yanapohaulishwa kwenda kwenye matini lengwa
kutokana na kutoelewa lugha vizuri.
MAREJELEO
Cartford,
J. C. (1995). A Linguistic Theory of
Translation. London: Heinmann.
Mdee, S, J.
(2011). Kamusi ya Karne ya 21; Kaamusi ya
Kiswahili yenye Uketo zaidi katika
Karne Hii.
Nairobi: Longman Publisher LTD.
Mshindo,
H. B. (2010). Kufasiri na Tafsiri.
Zanzibar: Chuo Kikuu cha Chukwan.
Mwansoko,
H, J. (2013). Kitangulizi cha Tafsiri; Nadharia
na Mbinu. Dar es Salaam.
TUKI
(2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
Dar es salaam: TUKI.
Newmark,
P. (1982). Approaches to Transslation. Oxford: Pergamon Press.
Nida,
E, & Taber, C. (1969). The Theory and
Practice of Translation. London: Prentice Hall.
Sengo,
T, S, Y, M. (2009). Fasihi za Kinchi,
The registered.
TUKI.
(2002). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
Dar es Salaam. TUKI.
Wanjara,
S. F. (2011). Misingi ya Ukalimani na
Tafsiri. Dar es salaam: Serengeti Education
Publisher LTD.
🙏
ReplyDelete