Flower
Flower

Thursday, August 23, 2018

UAMBATIZI NI NINI

Katika swali hili tutajadili dhana ya Uambatizi na Unyambulishaji. Kwa kuanza na fasili ya uambatizi. Kwa mujibu wa Habwe na Karanja (2014) wanafasili dhana ya Uambishaji ambao wengine huuita uambatizi ni utaratibu wa kuongeza viambishi katika mofimu na mzizi wa neno.

TUKI (2009) Uambishaji katika taaluma ya mofolojia huu ni utaratibu wa kuweka viambishi kabla, katikati na baada ya mzizi wa neno. Massamba na wenzake (2012) wanasema uambishaji katika lugha ni uwekaji pamoja viambishi na mzizi kwa namna mbalimbali, kutilia maanani suala la aina ya maumbo yanayopatikana ilimradi miunganiko inayotokea ikubalike katika lugha. Uambishaji wengine huita uambatizi.

Kwa mujibu wa Rubeza (1996) anafasili uambatizi kuwa ameuita kuwa ndio uambishaji ambao huonesha upatanisho wa kisarufi wa vipashio vingine vya sentensi. Kwa ujumla uambatizi ni upachikaji wa viambishi au mofu katika mzizi wenye uamilifu wa kisarufi yaani kuongeza maana ya msingi ya neno. Katika lugha ya Kiswahili viambishi vingi vya uambatizi hupachikwa mwanzoni mwa mzizi.

Baada ya kuangalia dhana ya uambatizi kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali tuangalie maana ya Unyambulishaji.
Kwa mujibu wa Matinde (2012) anafasili unyambulishaji kuwa ni mbinu ya uundaji wa maneno, kwamba viambishi mbalimbali huambikwa kwenye mzizi husika ili kuunda neno jipya. Pia Massamba (2009) anasema unyambulishaji ni utaratibu wa kupachika viambishi kwenye mzizi ili kuunda maneno mapya. Halikadharika Kamusi ya Isimu ya lugha (1990) wanafasili unyambulishaji kuwa ni tendo la kupachika vipashio kwenye kiini ili kujenga neno jipya au maneno mapya.

Kwa ujumla unyambulishaji ni upachikaji wa viambishi au mofu ambavyo vina uamilifu wa kubadili kategoria ya neno au maana wakati viambishi hivi vinapoongezwa katika mzizi wa neno. Neno linalopatikana huwa ni neno jipya au huleta maana mpya.

Dhana ya uambatizi na unyambulishaji ni dhana mbili zinazitofautiana na kufanana. Kwa kuanza na mfanano kati ya uambatizi na unyambulishaji.
Zote zinahusu kuambika viambishi, yaani uambishaji huitwa hivyo kwa kuwa kuna mchakato wa kupachika au kuambika viambishi. Hivyo basi yaweza kusema kuwa viambishi ndio nguzo kubwa na tegemeo la uwepo wa michakato hiyo na nisawa na kusema bila viambishi hakuna uambishaji wala unyambulishaji.
                      Mifano: i)  a – na – som – a  viambishi vyake ni (a, na)
                                   ii)  tu – li – u – chez – a  viambishi vyake ni (tu, li, u)
                                   iii)  som – ew - a  viambishi ni (ew,  )
                                   iv) som – esh – a viambishi ni (esh, a)
Zote zinaweza kuunda neno jipya; kwa kutumia mifano (i, iv) inadhihirisha ya kuwa waweza kunyumbulisha neno kitenzi katika  (i, ii) na kuunda nomino ambayo ni neno jipya kwa kutumia viambishi vinominishi. Katika (iii, iv) inadhihirisha ya kuwa maneno ambayo awali yalikuwa vivumishi baada ya uambishaji kinominishi yamebadilika na kuwa nomino.
                       Mifano: i) som – a → som – o
                                    ii) chez – a → chez – o
                                   iii) bora → ubora
Pamoja na ufanano huo pia kuna utofauti kati ya uamatizi na unyambulishaji kama ifuatavyo.
Sehemu ya utokeaji ya mchakato wenyewe; viambishi vya uambatizi mara nyingi hutokea kabla ya mzizi au shina la neno.
                        Mifano: i)  a – na – nicheka
                                       ii) a – na – ku - sema
                                      iii) a- li – m – saidia
Wakati viambishi vya unyambulishaji mara nyingi hutokea baada ya mzizi au shina la neno. Kinachosisitizwa hapa ni baada ya mzizi au shina kwa msingi huu bila kujali matokeo ya uongezaji au upachikaji wa mofu au viambishi. Uambishaji ukifanyika baada ya mzizi huitwa unyambuklishaji.
                         
                              Mifano: i) som – o
                                            ii) som – e – an – a
                                           iii) som – w – a
Kwa upande mwingine uambatizi hufanya kazi ya kisarufi yaani maana za viambishi vinavyowekwa katika mzizi wa neno huwa na maana ya kisarufi tu, lakini maneno yanayozalishwa baada ya kunyambulishwa huwa na maana ya kikamusi.
                        Mifano:
                                 Uambatizi                                                    unyambulishaji   
                                Tu – na – wasilish – a                                   shindano
                                Wa – na – tu- elewa                                      waimbaji

Katika neno tunawakilisha kuna viambishi ambavyo vina maana kisarufi. Kwa mfano neno tu linawakilisha nafsi ya kwanza wingi na wakati uliopo, pia neno wasilish ni mzizi na a ni kiambishi tamati. Pia neno muimbaji lina maana mtu anayeimba.
Uambatizi hauna mabadiliko yeyote ya kategoria za maneno au maana ya kileksimu, wakati unyambulishi hubadili maana ya kategoria ya maneno yanapopachikiwa viambishi nyambulishi.
                        Mifano:  uambatizi                        unyambulishi
                                       Alimpigia                          mwimbaji
                                       Anamchezesha                   refusha

Katika mifano hiyo viambishi vilivyowekwa kwenye – pig – na – chez – havijabadili maana wala kategoria za maneno lakini viambishi vilivyopachikwa kwenye mzizi – imb – na – ref – vimebadili aina ya maneno. Vilevile viambishi huweza kubadili aina ya neno kuwa kitenzi.
   Mifano:  Nomino                                     kitenzi
                     Maana                                     maanisha
                      safari                                       safirisha
               kivumishi                                      kitenzi
               zee                                                zeesha
               refu                                               refusha
viambishi vya uambatizi hufanana sana kimaana vinapopachikwa katika mizizi mbalimbali ya maneno wakati viambishi nyambulishi hutofautiana kimaana vinapopachikwa katika mizizi au mashina ya maneno.
    Mifano
               Uambatizi                                      unyambulishi
            Lima, limisha, limiana                     (lim) kilimo, mkulima
            Soma, somana                                  (som) msomi, msomaji

Uambatizi hauolozeshwi kama leksimu au msamiati katika kamusi wakati maneno yote yanayotokana na dhana ya unyambulishi huolozeshwa kama leksimu au msamiati katika kamusi.
   Mifano:
               Uambatizi                                       unyambulishi
             Amekula                                           mlo, mlaji
             Ameimba                                          mchujo
             Atacheza                                           uchovu, uchofu

Kwa kuhitimisha tunaona kuwa uambishaji na unyambulishaji kila nomino inakubali uambishaji au unyambulishaji majina hasa ya kipekee mengine hayakubali kuambikwa. Hili linaweza kuwa moja ya tatizo la uambikaji kama njia ya uundaji wa maneno ya Kiswahili. Pia uambikaji ni njia ambayo inamsaidia mkubwa katika kuongeza msamiati wa lugha na kupanua maana ili kukidhi mahitaji ya kimawasiliano.


MAREJELEO
Habwe, J & Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publisher
Kipacha, A. (2005). Uchanganuzi wa lugha na Isimu. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Dar es      
                 Salaam.
Massamba, D. P. B. (2012). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es salaam: TUKI.
Massamba, D. P. B. (2012). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu: Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam.
Matinde, S. ( 2012). Dafina ya Lugha, Isimu na Nadharia kwa Sekondari, Vyuo vya kati na
                Vyuo. Dar es Salaam.
Rubanza, Y. I. (1996). Mofolojia  ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Dar es Salaam.


No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny