Flower
Flower

Thursday, August 23, 2018

KITENZI NI NINI NA UARIFUSHAJI WA KITENZI

Katika kujibu swali hili tumeligawa katika seheemu kuu tatu ambapo kuna utangulizi, kiini na hitimisho. Katika utangulizi tumefasili dhana ya kitenzi na kiarifu, katika kiini tumeangalia miundo mbalimbali ya kiarifu na mwisho ni hitimisho la swali letu.

Dhana ya vitenzi imeelezwa na wanazuoni tofautitofauti kama ifuatavyo: TUKI (1990) wanafafanua kitenzi kuwa ni neno ambalo hutokea kama sehemu muhimu ya kiarifu. Hii ina maana kuwa kitenzi ndio kijenzi kikuu cha kiarifu katika muundo wa sentensi. Matinde (2012) anasema kitenzi ni neno linalotoa taarifa kuhusu tendo linalofanyika, lililofanyika na litakalofanyika.

Richard na wenzake (1985) wanasema kuwa kitenzi ni neno ambalo hutokea kama sehemu muhimu ya kiarifu na ambalo huambishwa mofu za njeo, hali, nafsi, idadi na dhamira. Aidha, vitenzi hueleza juu ya tendo au hali. Naye Nkwera (2003) anasema kuwa vitenzi ni maneno yanayoarifu jambo ambalo hufanywa na jina au kufanyiwa jina. Pia, Nkwera anaeleza kuwa kitenzi kinaweza kuwa kiwakilishi au kivumishi kisimamapo peke yake kama jina. Vitenzi hutaja matendo, matukio, hali au mabadiliko. Kitenzi ni neno ambalo limebebeshwa vitu vingi ndani yake suala linalowafanya wanasarufi wengi kupendelea kuliita neno hilo kifungutenzi badala ya kitenzi.

Naye, Mdee (2007) anatoa maana ya kitenzi kuwa ni neno linaloeleza jambo linalotendwa na lililotendeka. Kitenzi huarifu tendo lililofanywa au litakalofanywa na mnyama, mtu, au kiumbe chochote kinachoweza kutenda jambo. Mdee anaendelea kufafanua kuwa vitenzi vya Kiswahili havisimami pekee vinapotumiwa katika tungo, bali huambatana na viambishi vingine vyenye kuwakilisha mtenda wa tendo au mtendewa wa jambo. Kitenzi huambatishiwa pia viambishi vyenye kuonesha wakati tendo linapofanyika, kama mfano ufuatao unavyoonesha:-
                    Mfano Dada a-na-soma, watoto wa-na-ruka, baba a-ta-fika.

Mgullu (2010) anasema kuwa vitenzi ni aina ya maneno ambayo hutumika kama sehemu muhimu sana ya kiarifu cha sentensi ambayo hueleza jambo fulani linalohusu kiima cha sentensi. Katika lugha ya Kiswahili vitenzi ni maneno pekee ambayo ni lazima yawepo katika sentensi ndipo kifungu cha maneno kiweze kuwa sentensi, kwa mfano katika sentensi: Mtoto anakula. Aidha, Matinde (2012) anaeleza kuwa kitenzi ni neno linalotoa taarifa kuhusu tendo lililofanyika, linalofanyika au litakalofanyika. Katika muundo msingi wa tungo za Kiswahili kitenzi ndilo neno kuu katika sehemu ya kiarifu au kirai tenzi. Kitenzi kinapoondolewa katika sentensi bila shaka kifungu hicho cha maneno hukosa maana. Matinde anafafanua kuwa vitenzi huweza kusimama bila msaada wa aina zingine za maneno na sentensi ikawa kamilifu na yenye uarifishaji mkamilifu.

Kwa mujibu wa Massamba (2012), anafasili dhana ya Uarifu kuwa ni uhusiano wa kiima na kiarifu kwa namna ambayo kiarifu kinakuwa na neno linalovumisha kiima.  Kwa kutumia mifano ya kutosha kutoka katika lugha ya Kiswahili ufuatao ni ufafanuzi wa uarifu wa kitenzi.
Kiarifu. Kwa mujibu wa Matei(2008 ) ni sehemu ya sentensi inayoarifu kiima. Pia, Habwe na Karanja (2014), wanafafanua kuwa kiarifu ni sehemu ya sentensi ambayo inatoa taarifa kuhusu kiima. Katika sehemu ya kiarifu hapa ndipo kitenzi kikuu huwa. Lakini kiarifu kwa mujibu wa Matei (keshatajwa ) ametaja sifa kuu mbili za kitenzi ambazo ni :-
a)      Huwa na kitenzi na pengine maneno mengine
Mfano: i) Jua limetoa mwangaza mkali.
             ii) Ugonjwa umeleta maafa makubwa.
b)      Kwa kawaida huja baada ya kiima.
Mfano: i) Mnazi umeanguka
            ii) Wanafunzi wanasoma kitabu.

Hivyo kiarifu huambatana na kiima au na maneno mengine ili kutoa taarifa kamili. Kiarifu hutoa taarifa juu ya kiima kuonesha tendo linalofanyika, litakalofanyika au lililofanyika. Kwa mujibu wa Matei (Keshatajwa). Ifuatayo ni miundo ya kiarifu inayofanya uarifishaji wa kitenzi cha Kiswahili kama ifuatavyo:-

Kiarifu huwa na muundo wa kitenzi peke yake na kuweza kutoa taarifa fulani.
Mfano: i) Mtoto anacheza.
                                  T
            ii) Baba anakula.
                               T

            iii) Manyama analima.
                                       T
             iv) Babu anaoga.
                                 T
             
              v) Kiti kimevunjika.
                                   T
Kiarifu huwa na muundo wa kitenzi na nomino moja.  kwa mujibu wa Mgullu (keshatajwa) anaeleza kuwa nomino ni maneno ambayo hutaja majina ya watu, vitu, mahali, vyeo, dhana na hata tendo.Muundo huu unaundwa na kitenzi na nomino peke yake na kuweza kutoa taarifa.
Mfano: i) Anasoma daftari.
                       T           N
            ii) Anacheza mpira.
                         T          N
           iii) Analima shamba.
                       T            N
                       
           iv) Anapiga ngoma.
                       T           N
           v) Anafagia uwanja.
                     T            N

Katika mifano hiyo tunaona kuwa muunganiko wa kitenzi na nomino moja unatoa taarifa kuhusu jambo linalofanywa.

Kiarifu huwa na muundo wa kitenzi na nomino mbili, katika muundo huu nomino inayoathiriwa na tendo huitwa yambwa na inayoathiriwa ni yambiwa.
i)         
j)        Mtoto ameweka kitabu darasani.
               T            N           N
ii)  Mama amemnunulia mtoto kalamu.
                        T               N          N
iii) Asha ameweka kitabu kabatini.
                   T           N             N
iv) Asha amewekewa fedha banki.
                      T              N       N
v)  Dutwa amempikia Amina chakula.
                        T            N           N
 Kiarifu huwa na muundo wa kitenzi na sentensi.
i)        Juma alisema kuwa atakuja kesho
            T                          S
ii)  Mwalimu alisema kuwa watoro wote wataadhibiwa.
                         T                                 S    
iii)  Waziri aliagiza kuwa makontena yote yaondolewe.
                  T                                     S
iv)  Mkurugenzi aliagiza kwamba waajiriwa wote wakusanye barua zao.
                               T                                                 S 
v)  Sara aliuza kuwa kwanini hatujaosha vyombo. 
               T                                             S
Lakini mwanazuoni mwingine Richards (1985),  akinukuliwa na Mgullu (1990), anafafanua kuwa vitenzi huarifu au hueleza mambo mbalimbali kuhusu kiima. Mambo hayo ni pamoja na:
Huarifu tendo linalofanywa au litakalofanywa.
Mifano: i) Mwabupina atacheza.
               ii) Mwabupina hatacheza.
Huarifu siku au wakati.
                                                     Mifano:  i) Leo ni jumatatu.
                                                                               t
             ii) Kesho ni jumanne.
             t
Huarifu cheo au kazi anayofanya mtu.
Mifano:  i) Bichwa ni mwalimu.
            t
            ii) Kigori si mchezaji.
            t
Huarifu hali ya kuwa au kutokuwa na kitu fulani
                                                    Mifano:  i) Nives ana kalamu.
                                                                                  T
                                                                   ii) Nives hana kalamu.
                                                                                    T
Huarifu sifa ya au za mtu.
                                                    Mifano:  i) Okwi ni mchezaji.
                                                                                 t
          ii) Okwi si mchezaji.
        t

Huarifu hali ya kuwa au kutokuwa mahali fulani.
         Mifano:  i) Mulokozi yuko darassani.
                           T
                          ii) Mulokozi hayuko darasani.
                             T
Anaendelea kusema kuwa mifano ya vitenzi hapo juu hueleza mambo mengi na si matendo. Hii ndio inafanya tukubali kutumia istilahi ya vitenzi.
Kwa kuhitimisha urafishaji wa vitenzi unafanywa ili kuonyesha kuwa vitenzi zinaeleza juu ya mambo mengi na si matendo pekee yake. Katika hali hii ndiyo huweza kutufanya tuamini na kukubaliana ili kuweza kutumia istilahi ya vitenzi badala ya ile ya matendo ambayo imekuwa ikitumiwa na baadhi ya wanazuoni wengine wa awali.




                                                  










MAREJELEO
Habwe, J. na Karanja, P. (2007). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix.
Massamba, D. P. B. (2012). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.
Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha; Isimu na Nadharia. Mwanza: Serengeti Educational              
                    Publishers.
Mdee. J. S. (2007). Nadharia na Historia ya Leksikografia. Dar es Salaam: TUKI.
Mgullu, R. S. (2010). Mtaala wa Isimu: Fonetiki Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi:
                    Longhorn Publisher.
Nkwera, F. V. (2003). Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam:                   
                    Tanzania Publishing House.
Richard, J. et. al (1985). Dictionary of Applied Linguistics. Harlow: Longman.
TUKI. (1990). Kamusi ya Sanifu ya Isimu na Lugha: Dar es Salaam. TUKI.



1 comment:

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny