Katika
kujibu swali hili, kazi hii imegawanywa katika sehemu mbalimbali. Sehemu ya
kwanza ni utangulizi ambayo inaelezea maana ya mawasiliano na muktadha . Sehemu
ya pili ni kiini cha swali ambayo inaelezea umuhimu wa kuzingatia kipengele cha
muktadha ili mawasiliano yawe thabiti na sehemu ya mwisho ni hitimisho.
Wataalamu
mbalimbali wameelezea maana ya muktadha kama ifuatavyo. Kwa mujibu wa Julia
Wood (2004), anafasili mawasiliano kuwa ni mfumo maalumu ambao viumbe hutumia
kwa kutumia ishara ili kukamilisha na
kufasili maana. Anaendelea kusema kuwa mawasiliano ni mfumo maalumu, huusisha
ishara na huwa na maana. Katika fasili ya Wood tunaona kuwa hajaweka wazi ni viumbe gani
ambao wanatumia mawasiliano na pia amejikita katika matumizi ya ishara tu
wakati mawasiliano huweza kuhusisha njia nyingine.
Kwa
mujibu wa Luhmann (2008), anafafanua mawasiliano kuwa ni njia ambayo huusisha
mfumo wa jamii. Anaendelea kusema kuwa mawasiliano huusisha ujumbe, taarifa na
uelewa wa mtu katika kufasili ujumbe huo. Hivyo katika fasili ya Luhman tunaona
kwa fasili hii haijaweka bayana mifumo hiyo ambayo inahusika katika
mawasiliano. Kwa ujumla tunaona kuwa mawasiliano ni kitendo cha kupashana habari au
kubadilishana habari, taarifa au ujumbe baina ya watu wawili au zaidi kwa kutumia
njia tofauti tofauti za mawasiliano. Mfano kwa njia ya maneno au mazungumzo,
njia ya simu au barua na vyombo vya habari, aidha mawasiliano huweza kufanywa
na watu ambao wapo karibu au sehemu tofauti tofauti.
Baada
ya kufafanua maana ya mawasiliano kama ilivyoelezewa na wataalamu mbalimbali,
ufuatao ni ufafanuzi wa maana ya Muktadha. Kwa mujibu wa King’ei (2010),
anafafanua muktadha kuwa ni ile hali inayotawala na kuelekeza matumizi ya lugha
inayozungumzwa. Kwa mfano mahali, wakati, hadhira na kusudio la msemaji.
Halikadhalika katika lugha ya mazungumzo wazungumzaji wengi hushawishika
kutumia aina fulani ya lugha kulingana na muktadha fulani ambao hutoofautiana
na muktadha mwingine. Hali hii inaonesha kuwa kuna mambo fulani ambayo
huwafanya wazungumzaji wa lugha wateue msamiati fulani katika mazungumzo yao
unaolingana na muktadha walipo wakati huo.
Hali
kadhalika Msanjila na wenzake (2011), wanasema kuwa mawasiliano yanaweza kuwa
katika muktadha wa mazungumzo au maandishi, na matumizi ya lugha katika muktadha
hubeba mawasiliano kwa wanajamii. Vilevile SwahiliHub (26/6/2016), wakimrejelea
Austin (1962), wanasema kuwa ni muhimu kuhusisha matumizi ya lugha na muktadha
wake wa kijamii kwani lugha huwa na matumizi tofauti kama vile kutoa
mapendekezo, kuahidi, kukaribisha, kuomba, kuonya, kufahamiana, kuagiza,
kukashifu, kusifu na kuapiza. Kwa ujumla tunaona kuwa muktadha ni mazingira au
hali ambamo tukio au jambo hutendeka.
Baada
ya kufafanua kwa kifupi maana ya dhana zilizojitokeza katika swali hili, tunajikita
kwenye kiini cha swali ambapo tunapaswa kueleza umuhimu wa kipengele cha muktadha katika kufanikisha mawasiliano kuwa
bora na thabiti. Zifuatazo ni baadhi ya hoja zinazoshadidia umuhimu wa
kipengele hiki:
Husaidia
kutambua mtindo unaofaa kuwasilishia ujumbe, wakati msemaji anatambua muktadha
na mazingira aliyomo, moja kwa moja atatambua ni mtindo upi autumie kuwasilisha
ujumbe wake kwa wasikilizaji au hadhira. Mwansoko (1994:22), anabainisha namna
muktadha unaweza kusaidia kutambua mtindo. Mfano, katika mtindo wa kitaaluma
msemaji anaweza kuzingatia utaratibu maalumu wa uandishi wa marejeleo ya
vitabu, makala, magazeti na majarida . Kwa mfano, uandishi wa rejeleo la kitabu
ambacho kimeandikwa na mwanaisimu Bloomfield unapaswa kuanza na jina la ubini,
jina lake, mwaka, jina la kitabu, mahali kilipochapishwa na wachapishaji.
Hivyo, hata kwa wazungumzaji wa miktadha mingine kama ya dini au siasa,
mzungumzaji atatumia mtindo unaoendana na sehemu hiyo ya ibaada au uwanja wa
siasa.
Huimarisha
ushirikiano baina ya mzungumzaji na wasikilizaji, Msanjila (2009 : 8) anaeleza
kuwa mzungumzaji anpofahamu muktadha aliopo anaweza kuzungumza lugha ambayo
itazingatia alipo na aina ya watu waliopo. Mfano, mzee akifika katika kundi la
wazee wenzake ni lazima atatumia lugha ambayo itamfanya wenzake watege sikio
kumsikiliza. Hivyo, kuzungumza kwake kwa kuzingatia muktadha kunawafanya
wenzake kuonyesha ushirikiano katika mazungumzo.
Mzee 1: Habari za asubuhi wazee
wenzangu.
Kundi la wazee: Salama mwenzetu.
Katika
mfano huo tunaona wazee wenzake wamemsikiliza na wamemjibu, ni tofauti na mzee
huyu angeenda katika kijiwe cha vijana na kutoa salamu kama ile aliyoitoa kwa
wazee wenzie.
Mfano
2: Muumini wa dini ya Kikristo asipozingatia muktadha akaenda msikitini na kuzungumza
maneno aliyotakiwa kuzungumzaji kanisani hawezi kupata ushirikiano.
Mzungumzji:
Bwana Yesu asifiwe.
Wasikilizaji:
Kimya.
Katika
mfano huo tunaona kwamba mzungumzaji huyo huyo akitambua kuwa maneno kama hayo
anapaswa kuyasema kanisani angejibiwa ama kupewa ushirikiano.
Husaidia
kubaini uhusiano uliopo baina ya wazungumzaji, kwa kuwa muktadha unahusisha
vipengele kadhaa kama vile mada, mazingira, muda, uhusiano wa wazungumzaji, ni
wazi kuwa mzungumzaji na msikilizaji wanapokuwa katika muktadha mahsusi ni
rahisi kutambua uhusiano uliopo baina yao. Msanjila ( 2009:7), anasema
mfanyakazi anapokuwa kazini na mkuu wake wa kazi mazungumzo huwa kama
ifuatavyo:
Mkuu wa
kazi: Juma, kwa nini jana hukufika kazini?
Juma:
Samahani mkuu, mimi jana sikufika kazini kwa sababu nilikuwa
naumwa.
Katika
mfano huo, tunaona wazi kuwa mtu mwingine akisikiliza mazungumzo hayo anaweza
kubaini kiurahisi kuwa mazungumzo hayo ni baina mfanyakazi na mkuu wake. Vilevile
ni rahisi pia kubaini mahusiano baina ya mwalimu na mwanafunzi wanapokuwa
katika mazingira ya shule au muktadha wa darasani.
Husaidia
kuelewa na kuchagua mada ya kuzungumza, TUKI (2004:213), wanaeleza kuwa mada ni
kiini cha habari katika mazungumzo. Kwa maelezo ya TUKI (keshatajwa) tunaweza
kufahamu kutambua na kuchagua mada ipi inazungumzwa katika muktadha husika au
mzungumzaji azungumze mada ipi kulingana na muktadha aliopo. Hamad (2015:15-16),
anasema kwa kawaida mada inayozungumzwa hutegemea urasmi wa mazungumzo na
muktadha. Anaendelea kusema kuwa mada rasmi huzungumzwa katika miktadha rasmi
na mada zisizo rasmi huzungumzwa katika miktadha isiyo rasmi.
Jaji: Kesi ya kwanza.
Karani: John
dhidi ya Abela. Mashahidi wote wa kesi hii wanaombwa
watoke nje.
Katika
mfano huo wa mazungumzo tunaona sehemu ya mazungumzo rasmi kama mahakamani kuwa
muktadha huo unataka kutumia lugha ya muktadha wa mahakamani na mtu mwingine ni
lazima azungumze au kujibu kulingana na muktadha huo kama Karani alivyomjibu
Jaji.
Kwa
maelezo ya Hamad (keshatajwa), tunaona kuwa muktadha humsaidia mzungumzaji
kufahamu ni mada ipi inazungumzwa na inafaa kuzungumzwa. Mfano, wanafunzi
wanapokuwa katika maktaba ya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili tunategemea
kuwaona wakisoma au wakizungumza mada mbalimbali zinazohusu somo la Kiswahili
na sio Hisabati, Fizikia, Kemia ama vinginevyo.
Husaidia
ujumbe kueleweka kwa urahisi, mara nyingi ujumbe uliokusudiwa unaweza
usieleweke kutokana na mzungumzaji kushindwa kuzingatia muktadha. Hata hivyo,
ukweli ni kuwa uzingatiaji wa muktadha husababisha ujumbe ufike kwa urahisi.
Mekacha (2011:57), anasema wazungumzaji na wasikilizaji wa lugha huelewana kwa
kufahamu kaida za matumizi ya lugha au uteuzi wa lugha inayofaa kulingana na
mazingira (muktadha). Mfano, katika mazungumzo ya hotelini mhudumu na mteja
huelewana kwa urahisi kwa kuwa lugha anayotumia ni ya hotelini. Vilevile
mazungumzo ya daktari na mgonjwa hayawezi kufanana na yale ya hotelini.
Hotelini,
Mhudumu: Nani ng’ombe?
Mteja: Mimi hapa.
Hospitali, Daktari: Dawa hizi
umeze 2*3
Mgonjwa: Sawa daktari, asante
sana.
Katika
mifano hiyo tunaona kuwa muhudumu wa hoteli amefikisha ujumbe kwa mteja wake na
umeeleweka kama ilivyo pia kwa daktari na mgonjwa. Hata hivyo, ingekuwa ni
vigumu ujumbe kueleweka au kufika kama ulivyokusudiwa kama muhudumu wa hoteli
angeenda hospitali na kuanza kuwauliza watu nani ng’ombe kwa kuwa sio muktadha
husika. Hivyo kipengele cha muktadha ni huhimu sana katika kuimarisha
mawasiliano.
Huonesha
tofauti za matumizi ya lugha, kwa mujibu wa Habwe na Wenzake (2010) wanasema
kuwa mazungumzo yanaweza kufanyika sehemu kama vile ofisini, darasani, nyumbani
barazani na sehemu nyingine. Wanaendelea kueleza kuwa mahali walipo waungumzaji
huathiri matumizi ya lugha yao kwa vile lugha ndio chombo ambacho hutumika
kuelezea mazingira yanayowazunguka wazungumzajia, pia lugha hiyo hiyo hutumika
kuelezea yale yaliyopo katika mazingira hayo na kuamua matumizi ya lugha kwa
kulingana na muktadha, mfano, mada moja inawaza kuzungumzwa katika sehemu mbili
tofauti lakini matumizi ya lugha yakatofautiana baina ya sehemu moja na
nyingine kulingana na mahali pa mazungumzo.
Husaidia
kuficha ujumbe kwa watu wasiohusika, Myelimu (12/06/2018,05:08) wanasema kwamba
wazungumzaji wanapozungu kwa kuzingatia muktadha hutumia lugha yao ambayo huwa
kama mafumbo kwa watu wasio husika na hivyo kuelewana bila ujumbe kutoka nje ya
wahusika. Mfano, katika rejesta za vijiwe vya watumiaji wa dawa za kulevywa
huwa na misemo kama kete, ngada na unga kiasi kwamba kama mtu si mhusika wa
maeneo yale ni vigumu kuelewa. Lakin katika mazingira tofauti na yale
mzungumzaji huyo huyo hapaswi au hawezi kutumia maneno yaleyale kwa watu
wengine kwa kuwa hawata muelewa au mtu asiyehusika akiwa katika muktadha wa
watumiaji hao hataelewa.
Husaidia
wazungumzaji kutambua kanuni zinazotawala mazungumzo katika lugha. Kwa mujibu
wa msanjila na wenzake (2011), anafafanua kuwa katika miktadha mbalimbali ya
mazungumzo kunawasaidia watumiaji wa lugha kuelewa namna ya kutumia vizuri
lugha ya jamii ikiwa ni pamoja na, kuzingatia kanuni na kaida za mazungumzo na
uteuzi sahihi wa maneno.
Mfano: mzungumzaji mzee hataweza
kutumia lugha ya vijana kuzungumza na wazee wenzake badala yake atajibidiisha
kutumia lugha inayokubalika na wazee wa lika lake katika jamii inayohusika.
Hivyo
tunaona kuwa katika mfano huo mzungumzaji atazingatia kanuni ya mahusiano kwa
kuzingatia mada inayozungumzwa na uhusiano baina ya wahusika ambao wote ni
wazee. Halikadhalika wazungumzaji wanapo kuwa katika muktadha wa kanisani
wanatakiwa wazingatie kanuni na utaratibu wa uteuzi wa maneno yanayoendana na
mazingira ya pale.
Kwa
ujumla, mzungumzaji wa lugha anapaswa kuzingatia kioenggele cha muktadha ili
mawasiliano yaweze kuwa thabiti. Muktadha ndio humuongoza mzungumzaji kutokana
na mada ya mazungumzo, lengo la mazungumzo, uhusiano baina ya wazungumzaji na
wakati. Kwa hiyo ni muhimu kuzingatia vipengele vyote tajwa ili mawasiliano
yaweze kukamilika.
MAREJELEO
Habwe,
J.A, Matei, A.K na Nyonje, J. (2010). Darubini
ya Isimujamii kwa Shule na Vyuo. Nairobi : Phoenix Publisher Ltd.
Hamad, K. J. (2015). Tofauti za Matumizi ya Lugha katika Miktadha
mbalimbali ya Mazungumzo. Kioo cha Lugha Juzuu 14, 15-16.
King’ei, K. (2010). Misingi ya Isimu jamii. Taasisi ya Taaluma za Kiswahili: Chuo Kikuu
cha
Dar es Salaam.
Luhmann,N.
(2008). Theory of Society. Vol. 1.
Stanford University Press.
Mekacha, D. K.
(2011). Isimujamii: Nadharia na Muktadha
wa Kiswahili. Taasisi ya Taaluma za
Kiswahili: Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam.
Mwansoko,
H. J. (1991). Mitindo ya Kiswahili Sanifu.
Dar es Salaam:
Msanjila, Y. P, Kihore, Y. M &
Massamba, D. P. B (2011). Isimu jamii:
Sekondari na Vyuo.
Dar es Salaam. TUKI.
TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi:
Oxford University Press.
Wood, J. T.
(2004). Communication Theories in Action:
An Introduction. Belmont: Wadsworth
Print.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com