Kwa
mujibu wa NOUN (2010) wanasema kwamba fasihi ya watoto ni dhana inayorejelea
utunzi unaowalenga watoto pekee. Utelezi wa fasili hii unajitokeza katika neno
watoto ambapo Noun haweki wazi watoto anaowakusudia ametumia mtazamo gani aidha
wa kidini au wa kikatiba. Pia fasili hii inaleta utelezi pale anaposema kuwa
fasihi ya watoto huwalenga watoto pekee, lakini tunaona kuwa fasihi ya watoto
huusisha na watu wazima sio watoto tu, Mfano kitabu cha Mtego Kabambe.
Naye
Wamitila (2010) anafafanua dhana ya fasihi ya watoto kuwa ni ile ambayo msingi
wa dhamira na maudhui huwarejelea watoto. Katika fasili hii tunaona kuwa
wamitila anadai kuwa dhamira na maudhui huwalenga watoto lakini kiuhalisia
hauwezi kuwaelezea watoto bila kuwepo na wazazi au walezi wa watoto hao, hivyo
tunaona kuwa dhamira na maudhui huwalenga watoto pamoja na walezi wao.
Bruno
(2011) akimnukuu Irene (2003) anasema kuwa fasihi ya watoto ni ile fasihi
iliyoandikwa hasa kwa jinsia ya kiume. Anaendelea kusema kuwa fasihi hii
inahusu masuala ya michezo, usakaji ambao uliishia na ushindi. Katika fasili
hii tunaona kuwa Bruno ameegemea katika jinsia ya kiume tu na kusahau jinsia ya
kike, pia haiweki bayana hiyo jinsia ya kiume ni ya watoto au ya watu wazima.
Kutokana
na fasili za wataalamu mbalimbali walioelezea maana ya fasihi ya watoto
tunaweza kujumuisha mawazo yao na kusema kuwa fasihi ya watoto ni fasihi ambayo
fani na maudhui yake huwalenga watoto walio na umri chini ya miaka kumi na nane
na huusisha walezi au wazazi kama sehemu mojawapo katika kukamilisha fasihi
hiyo.
Baada
ya kuangalia fasili za wataalamu na fasili ya ujumla kuhusu fasihi ya watoto na
kuonyesha utelezi, sehemu inayofuata ni kiini ambapo tunaelezea na kufafanua
maana ya fasihi ya watoto kwa kutumia vipengele vya fani na maudhui huku
tukitoa mifano kwa kutumia vitabu tulivyosoma ambavyo ni Mtego Kabambe na Kilio Chetu.
Kwa
kuanza na muhutasari wa kitabu cha Kilio
Chetu, hiki ni kitabu kilichoandikwa na Medical Aid Foundation ni
tamthiliya inayovunja ukimya uliotawala miongoni mwa jamii katika kutatua
matatizo makubwa ambayo chimbuko lake ni mahusiano ya kijinsia, Katika
tamthiliya hii vijana wanatoa sauti iliyojaa sononeko na shutuma dhidi ya
wazazi, walezi na viongozi ambao wanafumbia macho suala hili nyeti. Ndiyo maana
tamthiliya hii inasisitiza sana haja ya kuwapa vijana elimu juu ya mahusiano ya
kijinsia badala ya hofu na vitisho ambavyo vimedhihirika kupitia hali halisi
kuwa vimeshindwa. Kilio Chetu ni
tamthiliya inayojikita kuzungumzia umuhimu wa elimu ya jinsia na UKIMWI kwa
vijana, tamthiliya hii inaonesha namna ukosefu wa elimu ya jinsia na UKIMWI
kwa jamii hususani vijana inavyochangia mimba za utotoni au mimba
zisizotarajiwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa vijana.
Katika
tamthiliya hii, mwandishi anaonesha namna ambavyo jamii ikihangaika
kujielimisha kuhusu elimu hii ya jinsia na kuwaacha vijana wakiangamia kwa
kukosa elimu hiyo, hali hii inaifanya jamii kugawanyika, wapo wanaoona kuwa
suluhisho la janga hili la UKIMWI, ni jamii nzima wakiwemo na vijana kupewa
elimu hii lakini wapo wazazi wanaopinga wakiamini vijana umri wao wakupewa
elimu hii haujafika bado.
Halikadhalika
katika kitabu cha Mtego Kabambe ni
kitabu kilichoandikwa na Mehta Abeid. Kitabu hiki kinahusu mapambano dhidi ya
maambukizi ya virusi vya UKIMWI ambapo katika kitabu hiki tunaona namna
Masharubu alivyotaka kumuingiza katika mtego wa kumuambukiza Chausiki virusi
vya UKIMWI kwa makusudi lakini dhamiri ya Masharubu inagonga mwamba baada ya
Machupa na Kili kubaini mtego wa masharubu kwamba ni kumuambukiza mwenzao
virusi vya UKIMWI. Mwisho tunaona Masharubu anakamatwa na polisi na kuwekwa
jela.
Baada
ya kuangalia muhutasari wa vitabu hivyo tunaweza kuangalia namna maana ya
fasihi ya watoto inavyojidhihirisha katika kitabu cha Kilio Chetu na Mtego Kabambe
kama ifuatavyo.
Fasihi
ya watoto hutumia muundo sahili au muundo wa moja kwa moja. Kwa mujibu wa Senkoro
(2011) anafasili kuwa katika kazi ya fasihi muundo ni mpango na mtiririko wa
kazi hiyo kwa upande wa visa na matukio. Naye Wamitila (2010) anaelezea muundo
wa fasihi ya watoto ni mwepesi na hutulia maanani sana matukio na aghalabu
hukitwa kwenye muundo wa moja kwa moja wa mtiririko wa matukio yenyewe. Muundo
huu wa moja kwa moja tunauona katika kitabu cha Kilio Chetu yaani
visa vyake vimepangwa kuanzia kisa cha kwanza , kati hadi mwisho, katika
kuvipanga visa vyake, mwandishi ameigawa kazi yake katika sehemu sita, ambazo
amezipa majina, Sehemu ya kwanza, Sehemu ya Pili, ya Tatu, ya Nne, Tano na
Sehemu ya Sita.
Sehemu
ya kwanza. Mtambaji
anasimulia habari za Dubwana ambalo ni UKIMWI, anasimulia namna
wakubwa wanavyoelimishana namna ya kujilinda na ugonjwa huo, huku wakiwaacha
watoto wakiangamia kwa kukosa elimu ya jinsia na ukimwi. (Uk 1)
Sehemu ya Pili. Hapa mwandishi
anatuonesha nyumbani kwa Mama Suzi, Mama Suzi na Mama Joti wanapeana habari za
kifo cha Fausta kilichosababishwa na UKIMWI, Mama Suzi anakuta kasha la vidonge
kwenye mfuko wa sketi ya Suzi wakati akifua jambo linalozua mgogoro kati ya
Suzi na mama yake, Mjomba na Baba Anna wanamshauri Mama Suzi kuacha kutumia
ukali na badala yake anatakiwa kumpa elimu ya jinsia binti yake ili ajitambue
jambo linalopingwa vikali na Mama Suzi. (Uk 4)
Sehemu ya Tatu.
Hapa mwandishi anatuonesha
mtaani, Joti anakutana na Suzi, Suzi anaamua kuachana na Joti kwa sababu ya
vidonge vya kuzia mimba alivyopewa na Joti kumsababishia kupigwa na mama yake.
Joti anawasimulia wenzake namna alivyofanikiwa kumpata Suzi, Joti, Jumbe,
Choggo na Mwarami wanaenda mtaani kuangalia sinema za X. (Uk 17)
Sehemu ya Nne. Tukio
linatendeka njiani, Joti na Suzi wanakutana, Suzi anamlaumu Joti kwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wasichana
wengine, wanaamua kurudisha uhusiano wao, Joti anaanza kujisikia vibaya, Jumbe
anaamua kumpeleka nyumbani, Mwarami anaonekana akimshawishi Anna amkubalie ombi
lake la kuanzisha mahusiano ya kimapenzi, Anna anaonesha msimamo anamkatalia,
mwandishi pia anatuonesha namna Anna anavyoshinda vishawishi vya kingono. (Uk
21)
Sehemu ya Tano. Tukio
linatendeka chumbani kwa Suzi akiwa na Anna, Suzi anajisikia vibaya, anahisi
huenda ana mimba, anataka kuitoa, rafiki yake Anna anamshauri kuachana na
mpango huo kwani ni hatari, anaamua kwenda kwa Joti kuzungumza naye suala hilo.
( Uk 31)
Sehemu ya Sita.
Hii ni sehemu ya mwisho, mwandishi anatuonesha nyumbani
kwa baba Joti, tunaona namna baba Joti alivyoangaika kwa waganga mbalimbali
kutafuta tiba ya Joti bila mafanikio, mwisho wanaamua kumpeleka hospitali, huko
wanapata wajibu kuwa Joti amethirika na virusi vya ukimwi, Jirani anamshauri
Baba Joti kumpeleka Joti kwa mganga mwingine, Mjomba anamshauri Baba Joti
kuachana na mpango huo kwani ugonjwa alionao Joti hauna tiba wala dawa. Suzi
anawasili kwa akina Joti anagundua Joti ana ukimwi, Joti anafariki dunia, Suzi
anakuwa na wasiwasi kama naye atakuwa ameambukizwa virusi vya ukimwi, anabaki
akijutia kwa kukosa elimu ya jinsia na ukimwi. (Uk 35)
Pia
katika kitabu cha Mtego Kabambe mwandishi ametumia muundo wa moja kwa moja au
sahili, kwani visa vyake na matukio vimepangwa kwa muundo wa moja kwa moja
kwani tunaona jinsi Masharubu anavyotumia mitego mbalimbali ili kumtega
Chausiku na visa vyake na matukio yake yanaendelea huku Masharubu akibadili
mbinu mbalimbali ili ampate Chausiku na mwisho wa kitabu tunaona Masharubu
anakamatwa.
Pia fasihi
ya watoto hutumia mtindo wa vielelezo ( picha, michoro au nyimbo). Senkoro (2011) anafasili mtindo ni upekee wa uundaji wa kazi ya fasihi na hutofautiana
baina ya msanii mmoja na mwingine kulingana na hisia za msanii huyo. Utofauti
huo unaweza kujitokeza kwenye matumizi ya nafsi, uteuzi wa msamiati, mwanzo na
mwendelezo wa kazi yake, usimulizi wa mwandishi, uchanganyaji wa tanzu
mbalimbali za fasihi, kama vile kuingiza kipengele cha wimbo katika kazi ya
fasihi andishi. Ngugi (2011) anafafanua kuwa mara nyingi kazi ya fasihi ya
watoto lazima ziwe na vielelezo na vielelezo hivi huweza kuwa michoro au picha.
Anaendelea kusema kuwa hii humfanya mtoto avutiwe zaidi na kuwa makini na ile
kazi ya fasihi na kuona uhalisia wa kile anachokisoma.
Mfano: katika tamthilia ya Kilio
Chetu tunaona mwandishi ametumia michoro mbalimbali katika jarada,
Pia
vielezo vya michoro vinapatikana ukurasa wa 4, 6, 10, 13, 19, 22, 24, 30, 32 na
ukurasa wa 38. Vilevile mwandishi ametumia matumizi ya nyimbo pale walipokuwa
katika mazishi ya joti mwandishi anasema,
“Kiongozi: Joti afwite sanda salauya × 3
Wote:
Ena, ena, ena salauya × 3
Kiongozi: umwana afwite sanda saluaya ×3
Wote:
Ena, ena, ena salauya × 3”. Uk
(39)
Vilevile
katika kitabu cha mtego kabambe mwandishi ametumia michoro mbalimbali ili
kusaidia uelewa wa mtoto. Michoro hiyo imetumika katika ukurasa wa 1, 2, 3, 4,
5, 6, 7, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 19, 20, 21, 23, 24, 25, 26, 27, 28, 29
na ukurasa 30.
Pia
ukubwa wa maandishi yake hutegemea viwango vya watoto. Kazi andishi zenye
fasihi ya watoto huchapishwa kwa maandishi yenye ukubwa tofauti. Kazi
inayowalenga watoto wadogo sana hasa wale ambao kwanza ndo wanaanza kusoma kazi
zao huwa zimesheheni maandishi makubwa. Mfano
mtoto wa darasa la nne na la tano maandishi yao huwa tofauti na mtoto wa
darasa la pili na darasa la sita na darasa la saba.
Fasihi
ya watoto hutumia wahusika, amabapo wahusika wakuu huwa ni watoto. Kwa mujibu
wa Njogu na Chimerah (2008) anafasili maana ya wahusika kuwa ni sehemu ya fani
na ni viumbe wa sanaa wanaobuniwa kutokana na mazingira ya msanii. Naye
Wamitila anaeleza kwamba fasihi ya watoto haiwezi kusemwa kuwa ni ya aina hiyo
ikiwa wahusika wanaosukuma msuko wa kazi zinazousika si watoto. Anaendelea
kusema kuwa kwa mtunzi makini wa kazi za fasihi, mara nyingi huanza kwa
kumuhusisha mtoto mwenyewe kama muhusika mkuu, watoto hupenda wahusika wa fasihi
wenye umri sawa na wao.
Mfano: katika kitabu
cha Kilio Chetu mwandishi amewatumia
Joti na Suzi kama wahusika wakuu ambao ni watoto, pia ametumia wahusika wengine
watoto kama vile Ana na Mwarami, fauka ya hayo ametumia wazazi na watu
wazima kama vile mama Suzi, mjomba,
Chausiku na baba Ana. Vilevile katika kitabu cha Mtego Kabambe mwandishi amemtumia Chausiku kama muhusika mkuu
ambaye alikuwa anasoma darasa la sita, wahusika wengine watoto ni kama vile Kili,
Mosi, Machupa ambao wote walikuwa wanasoma darasa la sita. Pia alitumia
wahusika wengine ambao ni watu wazima kama vile Masharubu, Mwalimu mkuu na
wazazi wake chausiku.
Fasihi
ya watoto hutumia lugha nyepesi. Kwa mujibu wa Wamitila (2010) anaafafanua kuwa
lugha ni chombo muhimu kwa mwandishi wa fasihi yoyote yule. Anaendelea kusema
kuwa katika kazi za fasihi zinazowalenga watu wazima si lazima lugha iwe
nyepesi mara nyingi huwa ni lugha yenye kiwango sawa na walengwa, kwa kuwa watu
wazima uwezo wao ni mkubwa na urazini wao pia ni mkubwa, hivyo basi lugha yao
huwa ni pevu lakini lugha inayotumika katika fasihi ya watoto huwa ni changa na
uchanga wake unakuwa katika hadhi ya tungo kama sentensi fupi, kujiepusha na
sentensi changamani zinazoweza kuwachanganya watoto. Kwa hali hiyo lazima lugha
iwe nyepesi ili mtoto aweze kujifunza kwa urahisi na hatimaye kumjenga katika
lugha hiyo. Kwa mfano katika kitabu cha Kilio
Chetu mwandishi anasema,
“Mwarami: mshikaji Joti ee, mbona umetuanika juani hivi
Joti: kwani vipi jamani?
Choggo: Eti vipi? We
sio tulukubaliana kukutana pale kijiweni?” (Uk 18)
Vilevile
katika kitabu cha Mtego Kabambe
tunaona lugha iliyotumika miongoni mwa wahusika ni nyepesi na yenye kueleweka
ambayo inasaidia watoto kuelewa. Mfano mwandishi anasema;
“unasema kweli, Machupa
alitokwa na macho. Ni kweli tupu,
Kili alimuhakikishia si
unajua kuwa mimi nimejionea mengi
juu ya UKIMWI. Nafahamu
Machupa alisema”. (Uk 22)
Fasihi
ya watoto huwa na dhamira ambazo si changamani. Kwa mujibu wa Samweli (2015)
anafafanua dhamira kuwa ni lengo au mada, kusudi, wazo kuu linalozungumzwa na
kazi ya fasihi. Kazi ya fasihi huweza kuwa na dhamira za kisiasa, kiuchumi,
kijamii na hata kiutamaduni. Kazi za watoto mara nyingi huwa na dhamira ambazo
mara nyingi si changamani. Hii ni kumrahisishia mtoto aweze kujua kile
mwandishi anachotaka kumwambia. Kama dhamira zitajengwa kwa uchangamani mtoto
atafurahia picha tu na hataelewa kile kinachoelezwa na mwanafasihi. Hii
inadhihirika katika kitabu cha Kilio
Chetu na Mtego Kabambe ambapo
tunaona dhamira ambayo imechukua nafasi kubwa ni Ugonjwa wa UKIMWI, hivyo kuwa
lahisi kwa mtoto kuweza kuelewa nini kinachoongelewa katika kazi hizo. Mfano
katika kitabu cha Kilio Chetu
mwandishi anamuonesha mjomba alipokuwa akimsimulia dada yake. Mwandishi
anasema;
“Mjomba: Lakini dada, haya ndiyo
yale niliyokuwa nakusimulia jana juu ya
marehemu Fausta ambaye hata
madaktari wamethibitisha kwamba alikufa
kwa UKIMWI. Upepo umebadilika
sasa. Hawa vijana wetu wapewe elimu ya familia
ikiwemo hii ya jinsia”. (Uk 11)
Pia
katika kitabu cha mtego kabambe mwandishi anatuonesha dhamira hii ya UKIMWI
pale anapoeleza dalili za ugonjwa huu kwa kusema;
“ mwili hudhoofika na kupungua uzito kwa asilimia kumi au zaidi,
homa za mara kwa mara,
kuharisha kwa muda mrefu, kukohoa kwa
muda mrefu”. (Uk 29)
Pia
katika ujumbe kazi za fasihi ya watoto hulenga kuwaelimisha watoto juu ya mambo
mbalimbali. Kwa mujibu wa Samweli (2015) anafasili ujumbe kuwa ni yale mambo
ambayo msanii wa kifasihi simulizi angependa hadhira ijifunze ili kuweza
kufanikisha msimamo uliojengwa na msanii huyo, mfano kama kazi ya fasihi
inahusu mapenzi ujumbe unaweza kuwa mapenzi yanaua.
Hivyo
tunaona katika kitabu cha Kilio Chetu
kutokana na dhamira ya UKIMWI mwandishi anawasihi wazazi wawaelimishe watoto
juu ya elimu ya kijinsia. Mfano mwandishi anamuonesha mama suzi kama mzazi
ambaye alikuwa anapinga watoto kupewa elimu ya kijinsia kwa sababu bado ni
wadogo hii ikapelekea suzi kupata mimba kutokana na kutopata elimu ya kinjisia
mapema. Mwandishi anamuonesha mama suzi kama mpinga elimu ya kijinsia pale
anaposema;
“Mama suzi: Ee heri unisaidie
maana naona mie hatuelewani.
Oo aelimishwe jinsia, ajijue,
ajijue nini huyu? Wakati wa kujijua bado na atajijua
mwenyewe bila kukalishwa
kikao”. (Uk 12)
Halikadhalika
katika kitabu cha Mtego Kabambe mwandishi anatoa ujumbe kwa watoto namna ya
kujikinga na maaambukizi ya virusi vya ukimwi. Mfano mwandishi anataja njia
hizo kama
“kuwa mwaminifu katika ndoa
yako, kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu,
vijana kuacha kabisa
kujamiana hadi baada ya kuoana na mtu mwaminifu.
Kuacha kabisa kuchangia
vifaa vyenye makali kama nyembe na mkasi”. ( Uk 30)
Kwa
kuhitimisha tunaona kuwa kazi za fasihi zinaweza kuathiri watoto katika hali
nzuri au mbaya. Wasomaji au wasikilizaji wa fasihi hubadilika mara baada ya
kupitia kazi ya fasihi, mabadiliko ya wasomaji ama wasikilizaji wa fasihi
yanaweza kuwa chanya au hasi kutokana na kazi husika ya fasihi. Wito kwa
wanafasihi ni kulinda maslahi ya jamii hasa katika kuandaa kazi za watoto kwani
watoto wa leo ni watu wazima wa kesho na kama tukiwaharibu tunaweza kuharibu
taifa la kesho.
MAREJELEO
Abeid,
M. (2003). Mtego Kabambe.
Bloomington: Mathew Books and Stationary.
Bruno, B. (2001). The
Children of the Dream. New York city: Simon and Schuster.
Medical Aid Foundation.
(1995). Kilio Chetu. Dar es Salaam:
Tanzania Publishing House.
Ngugi, P. (2010). Language
and Literacy Education: The State of Children’s in Kiswahili in
Kenya. Berlin: Lambert Academic
Publishing.
Njogu, K. & Chimera, R.
(2008). Ufundishaji wa Fasihi, Nadharia
na Mbinu. Kenya, Nairobi:
Jomo Kenyatta Foundation.
NOUN. (2010). Instructional system design development
and evaluation for open and distance
learning. Presentation at NOUN
headquarters, Victoria Island: National Open
University of Nigeria.
Samwel,
M. (2015). Umahiri katika Fasihi ya
Kiswahili. Dar es Saalaam: Meveli Publishers.
Senkoro, F. E. M. K (2011). Fasihi Andishi. Dar es Salaam: Kauttu
Limited.
Wamitila, K. (2010). Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi.
Nairobi: Vide – Mua Publisher.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com