Katika kujibu swali hili, tumeligawa katika sehemu kuu tatu,
kwanza ni utangulizi ambapo tumelezea dhana ya tendouneni na kuelezea chimbuko
la nadharia ya tendouneni na kwenye kiini tutaelezea madai ya Austin (1962), na
Searle (1975) kuhusu tendo uneni na mwisho ni hitimisho. Kwa kuanza na utangulizi
ni kama ifuatavyo;
Matinde (2012:309), anaelezea maana ya tendo uneni
kuwa ni utoaji wa matamko ambayo husababisha utokeaji au utendaji wa tendo. Kwa
mfano, tamko linaweza kuhusu kushukuru, kutoa ahadi, kuamua, kuomba radhi.
Nadharia ya tendouneni imeasisiwa na John Austin (1962), katika kitabu cha “How to Do Things with Words” ambapo
alianzisha nadharia hii kupinga mawazo ya wanafalsafa na wanaisimu wa mwanzo
ambao mawazo yao yalikuwa kwamba kazi ya lugha ni kueleza, kufafanua, na
kuarifu mambo mbalimbali. Kyeu (2011)
Austin (kashatajwa) anaeleza kuwa si mara zote lugha hutumika kufafanua
mambo bali mara nyingine hutumika kutenda. Austin (1962:5). Anaendelea kueleza
kuwa, mtu anaposema madhabahuni kuwa ninamuoa au nimekubali kuolewa na mtu fulani,
huwa haelezi kuhusu ndoa wala kutoa taarifa ya ndoa bali anafanya tendo la kuoa
au kuolewa. Austin (kashatajwa) anayaita matamko haya kuwa ni (matamko tenda) ama tendo uneni kama anavyokuja kuyaita Searle (1975).
Nadharia hii ilikuja kuboreshwa na mwanaisimu mwingine ambaye ni Searle (1975)
yeye anasema kwamba kuongea ni kutenda kwa mujibu wa kanuni na kwamba vitendo
usemi ndivyo vipashio vidogo kabisa vya mawasiliano. Yafuatayo ni madai ya
msingi ya Austin (1962), kuhusu tendouneni kama ifuatavyo;
Kwa mujibu wa Austin (1962:101-107), amegawa muundo
wa kitendouneni katika sehemu kuu tatu, kwanza ni tendo la kutamka, pili
dhamira ya tamko, tatu athari za tamko. Tendo la tamko ni utoaji au
uwasilishaji wa sauti au maneno yaliyo na uamilifu ndani yake, Austin
(keshatajwa) anafafanua kuwa katika tendo la tamko kuna vipengele vitatu,
ambavyo ni kipengele cha kifonetiki, hiki kinahusu utamkaji wa sauti. Kipengele
chengine ni cha kifonolojia hiki kinahusu sauti zilizotamkwa sharti ziegemee
katika lugha fulani. Kipengele cha mwisho ni semantiki na sintaksia ambapo
sauti zinazotamkwa sharti ziwe na maana pia zihusianishwe na muktadha maalumu.
Dhamira ya tamko, tamko linapotolewa hutupa nia au
kusudio kuhusu jambo fulani, mara nyingi nia hii hubebwa na vitenzi vya
utendeshi,ambapo vitenzi hivyo kuwa vya kuahidi, kulaumu, na kuomba msamaha.
Mfano, ikitokea msemaji akiomba msamaha kutoka kwa msikilizaji bila shaka
msemaji atakuwa anaamini kwamba msikilizaji amekasirika akirejea maneno na atakavyoyasema.
Tamko lina nguvu fulani zinazolifanya tamko hili kuwa na uwezo wa kutenda.
Athari za tamko, Mara nyingi athari hiyo hujionyesha
au hujidhihirisha kwa msikilizaji. Hii hutokana na mwitiko wa msikilizaji kutokana
na tamko la msemaji. Kwa mfano, mtu anapomuomba mwenzake msamaha huwa na
uhakika kwamba mwenzake amechukizwa na jambo fulani. Hivyo, anaye ombwa msamaha
anaweza kuridhia au kutokuridhia ombi la aliyeomba msamaha. Kitendo cha
kuridhia au kutoridhia kinadhihirisha
athari ya tamko.
Aidha, Austin (1962:14,) amebainisha masharti ya
tendouneni sita na kuyagawa katika makundi matatu. Kundi la kwanza kuna masharti
mawili ambayo ni, lazima kuwapo na kaida juu ya utendaji wa tendo hilo na mwitiko
wa tendo hilo ijulikane mahari pote. Pili, mazingira na watu wanaohusika katika
uneni wa tendo husika lazima wawe muafaka.
Kundi la pili pia amebainisha masharti mawili ambayo
ni kwanza, utaratibu wa kutekeleza tendo husika lazima ufuatwe kwa usahihi.
Pili, utaratibu huo lazima ufuatwe kikamilifu.
Kundi la tatu kuna masharti mawili ambayo ni kwanza,
wahusika wawe na dhamira ya kweli ya kufanikisha tendo husika. Pili, iwapo
wajibu ambao anatakiwa kutimiza baada ya tendo uneni unafahamika kwa watu
fulani lazima wahusika watekeleze.
Vilevile, Austin (1962:152-162), yeye anadai kuwa kuna aina tano za
tendouneni ambazo ni, kitendouneni cha maamuzi, kitendouneni cha maagizo,
kitendouneni cha maagano, kitendouneni cha hisia,
kitendouneni cha maelezo na kitendouneni cha hulka.
Kitendouneni cha maamuzi, ni aina ya kiendouneni
ambacho huonesha kutoa maamuzi ambayo yanaweza kuwa maamuzi ya mwisho au yasiyo
ya mwisho. Aina hii hutumia vitenzi
kama
vile, amua, kadiria, panga
na thaminisha.
Kitendouneni cha maagano, hiki ni kitendouneni
ambacho watu huwekeana maagano ambayo sharti yatimizwe. Mfano, hutumia vitenzi
kama husisha, ahidi, hakikisha, kuapa, kubaliana, dhamiria, maanisha, na kupanga.
Mfano;
·
Nakuhakikishia kuwa nitakupa pesa zako.
·
Naapa kuwa nitakuwa mwaminifu kwa katiba
ya nchi yangu.
Kitendouneni cha hulka, ni kitendouneni kinachohusiana
na tabia za kijamii. Anaendelea kusema kwamba, aina hii ya tendouneni inahusu
mwitiko wa mtu kuendana na kitu ambacho mwengine amekifanya. Kiujumla kitendo
hiki hulenga sana hisia za watu. Kwa
mfano
- Katika kuomba radhi
maneno yanayotumika ni kama vile, naomba
radhi, niwie radhi,
naomba msamaha, samahani.
- Kwenye kushukuru
maneno yanayoweza kutumika ni kama; nashukuru,
shukrani, ahsante. Kuonesha masikitiko; pole, nakuhurumia, nimesikitishwa,
nakupa pole.
- Kwenye kupongeza
hutumia maneno kama; najivunia,
nakupongeza na hongera.
- Kwenye kumpa mtu
changamoto, maneno yanayotumika ni kama; thubutu, jaribu,
Aina nyingine ya tendouneni inayotajwa na Austin ni kitendo neni cha maelezo, ambapo ni kitendouneni kinachohusu mtu kutoa hoja kwa watu au kutoa
uthibitisho wa jambo. Mfano; nakubaliana, nakataa, nimekubali, nakutaarifu,
natoa ripoti, kudadavua, kutambua, kushuhudia, kusisitiza na kuhitimisha. Kwa mfano
·
Tunaweza kusisitiza kuwa mazingira
tutunze mazingira ili nayo yatutunze.
Baada ya kuangalia aina za tendo uneni kama
alizotaja Austin (1962), zifuatazo ni aina za tendouneni kama zilivyoboreshwa
na Searle (1975). Akitumia kigezo cha athari ya kitendo kikiwa na uhusiano
na
mazingira halisi.
Kitendouneni cha msimamo, hiki ni kitendouneni kinachoeleza jinsi msemaji anavyotekeleza aliyoyasema.
Mfano, kuamini, kutokubadili msimamo, kukubali, kukiri, kukataa, kuhitimisha,
mfano;
·
Ninaripoti kupotelewa kwa fedha zangu.
·
Sikubaliani na maamuzi ya mahakama hii.
·
Ninakiri kuwa nimefanya kosa hili.
Kitendouneni cha agizi, hivi vinahusiana na wajibu wa
mtu, haki za mtu, athari za mtu, ushauri na maonyo. Hii pia humutahadharisha
mpokea tendo juu ya athari ya kitendo anachoweza kukifanya. Mfano wa vitenzi
vinavyotumika katika aina hii yakitendouneni ni pamoja na vile vinavyo onesha
kuamuru, kusisiza, kuonya, kutisha na kushauri. Mfano;
·
Nasisitiza kwamba kila mtu afike kwa
muda muafaka.
·
Ninakushauri urudi nyumbani mapema.
·
Ninakuonya kutokurudia tena kosa hili.
Kitendouneni kuapa, hivi hujihusisha na utoaji wa
ahadi. Lengo kuu huwa ni kwamba msemaji huwa amejitolea kutekeleza jambo au
wajibu fulani. Matinde (2012:314) analezea aina hii ya kitendouneni kuwa huonesha
nia ya msemaji kutenda jambo fulani siku za usoni. Kwa mfano
·
Nitahakikisha
kuwa tunawafunga.
Kitendouneni cha vizua hisi, hivi ni vitendouneni
vinavyoonesha muelekeo wa msemaji kutokana na hali fulani ya kijamii. Hivi uhusisha
kupongeza, kuliwaza, kuomba radhi, kuomba ruhusa, kushukuru, kukaribisha, kutoa
maoni na kulaani. Mfano;
·
Nakupongeza kwa kufaulu mitihani.
·
Natoa pole kwa wote walioguswa na msiba
huu.
·
Naomba ruhusa sitoweza kuhudhuria darasani
leo.
Kitendouneni cha tamko, ni kitendouneni ambacho
kinaelezea athari ya tamko fulani kwa msemaji au anayepokea tamko hilo. Matinde
(2012:314) akielezea
kitendo hiki anasisitiza kwamba mtoa tamko ni lazima awe na dhamana juu ya athari ya tamko hilo.
Mfano padri kwa
muumini, hakimu kwa muhalifu. Mfano katika sentensi
- Ninatangaza
kuwa kuanzia
sasa ninyi ni mke na mume.
- Ninaacha kazi
rasmi kuanzia leo.
Katika sentensi
ya kwanza padri anatangaza kuwa walio mbele ni mume na mke na inakua hivyo kwa kuwa ni mwenye dhamana ya
kufungisha ndoa. Sentensi ya pili inaonesha athari kuwa baada ya kusema
ninaacha kazi Mtu huyo hatoenda ofisini tena.
Kwa ujumla, Wataalamu hawa wawili yaani Austin (1962) pamoja na
Searle (1975) wametupa nwangaza wa kuelewa nadharia ya tendo uneni lakini pia
kusaidia kuelewa umuhimu wa nadharia hii. Mathalani nadharia ya tendo uneni husaidia
kuelewa maana ya tamko katika mazingira mahususi, hurahisisha kuonesha uamilifu
wa tukio na namna ya ufikishaji wa tamko hilo, pia hutusaidia kubashiri maana
ya tamko.
MAREJELEO
Austin, J. L. (1962).
How to do things with Words. London:
Oxford University Press.
Kyeu, D. (2011).
Nadharia ya Kitendoneni na Jinsi
Kinavyoweza Kutumika
Kuchanganua Usemi:Tasnifu
ya uzamivu. Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madson.
Matinde, R. S.
(2012). Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia: Kwa sekondari, Vyuo vya kati na
vyuo vikuu.
Mwanza:
Serengeti Education Publishers Lt d.
Searle, J. R.
(1975). Speech Acts:An Essay in
Philosophy of Language.. New York: Cambridge
University Press.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com