Flower
Flower

Friday, March 9, 2018

USHAIRI NI NINI

Wanamapokeo wanafasili maana ya Ushairi kama ifuatavyo.

Aberatif Abdalah (2003) anafasili ushairi kuwa ni utungo unaofaa kupewa jina la ushairi sio utungo wowote ni utungo wenye ulinganifu wa vina vitukufu. Utungo huu ni ule wenye vipand e wenye mizani zisizopungufu wala zilizozidi. Vipande hivyo viwe vimepandwa na maneno ya mkato maalumu na yenye lugha nyoofu, tamu, laini, lugha ambayo ni telezi kwa ulimi kuitamka. Lugha ambayo ina uzito wa fikra, ni tumbuizi kwa masikio ya kusikia na yenye kuathiri moyo. Lazima umuathiri mtu kama alivyokusudiwa.

Abeid (1996) anafasili kuwa Ushairi ni wimbo, hivyo kama shairi haliimbiki halina maana.
Mnyampala (2003) anasai kuwa Ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale na ndicho kitu kilicho bora sana katika maongozi ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato ya lugha nzito yenye kunata iliyopambwa kwa urari na mizani.

Shaban Robert anafasili Ushairi kuwa ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa sanaa ya vina ushairi una ufasaa wa maneno machache. Wimbo ni shairi dogo, shairi ni wimbo mkubwa na utenzi ni upeo wa ushairi.
Kina na ufasaha waweza kuwa nini?
Kina ni mlingano wa sauti za herufi, ulinganifu kwa maneno mengine kina huitwa mizani ya sauti. Lugha fasaha hufata sarufi ya lugha husika, lugha sanifu ni lugha iliyosanifiwa na kukabiliwa katika matumizi.

Wanausasa wanafasili maana ya Ushairi kama ifuatavyo.

Kezilahabi (1976) anafafanua maana ya Ushairi kuwa ni tukio, hali au wazo ambalo linaoneshwa kwetu kutokana na upangaji mzuri wa maneno fasaha yenye mizani kwa kifupi ili kuonesha ukweli fulani wa maisha.

Njogu (2008) Ushairi ni sanaa ya lugha inayoeleza jambo kwa uwazi, kwa njia ya mkato na kwa namna inayoteka hisia za msomaji au msikilizaji.

Mulokozi na Kahigi (1996) Ushairi ni sanaa iliyopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa maneno fasaha yenye muwala kwa lugha ya mkato, picha, sitiari au ishara. Sanaa hii inaweza kuwa katika usemi, maandishi ya wimbo ili kuleta wazo au mawazo kwa njia inayogusa moyo.

Kwa ujumla Ushairi, fani na maudhui ni vipengele muhimu katika ushairi. Mawazo, fikra nzito au hisi za ndani ni vya muhimu katika ushairi. Ushairi ni utungo maalumu, si kila utungo unapaswa kuwa ushairi, ushairi hauna budi kuvuta hisia, ushairi hauna budi kutumia lugha ya mkato.

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny