Flower
Flower

Monday, January 29, 2018

WATAALAMU WANAODAI KUWA KISWAHILI NI LUGHA CHOTARA

Kazi hii tumeigawa katika sehemu tatu ambazo ni utangulizi, kiini na hitimisho. Katika utangulizi istilahi mbalimbali zilizojitokeza katika swali zitafafanuliwakwa mujibu wa wataalamu mbalimbali. Katika kiini tutaangalia jinsi ambavyo dhana ya kukioana Kiswahili kama lugha chotara ilivyo jadiliwa kwa kina na wataalamu mbalimbali kwa mitazamo na mawanda tofauti na mwisho tutahitisha.

TUKI (2004) wanasema lugha ni mpangilio wa sauti na maneno unaoleta maana. Ambao hutumiwa na watu wa taifa au kabila fulani kwa ajili ya kuwasiliana. Udhaifu wa fasili hii ni kwamba TUKI wamejikita zaidi katika swala la sauti na maneno na kusahau matumizi ya ishara.

Sapir (1921) anaeleza kuwa lugha ni mfumo ambao mwanadamu hujifunza ili autumie kuwasilishia mawazo, maoni na mahitaji. Mfumo huu hutumia ishara ambazo hutolewa kwa hiari.Mtaalamu huyu anaelekea kusema kwamba ili binadamu waweze kuwasiliana iliwabidi wabuni mfumo fulani wa ki-ishara ambao wangeutumia kuwasiliana miongoni mwao katika jamii. Udhaifu wafasili hii ni kwamba imeegemea zaidi kwenye ishara na hivyo kuonyesha kwamba suala la sauti halikutiliwa maanani ilihali sauti hasa ndio msingi wa lugha.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa lugha ni mfumo wa ishara na sauti za nasibu ambazo zimekubaliwa na jamii ya watu fulani ilizitumike katika kukidhi mawasiliano yao ya kila siku katika nyanja mbalimbali za maisha mfano siasa, uchumi na utamaduni.

TUKI (2004) wanasema chotara ni mtu aliyezaliwa na wazazi wa rangi mbalimbali. Udhaifu wa fasili hii ni kuwa kigezo cha rangi hakijitoshelezi katika kufasili dhana ya chotara mfano mama albino na baba mweusi wa taifa moja wakizaa mtoto je, huyu ndiye chotara? Jibu ni hapana. Vilevile fasili hii imehusisha dhana yauchotara na mtu pekee na kusahau kuwa hata vitu vingine huweza kuwa chotara mfano wanyama, miti na lugha.

Hivyo chotara ni kitu chochote kinachoweza kuwa kiumbe hai au kisicho hai kinachotokana na viumbe viwili au vitu viwili vyenye asili mbili tofauti.

Lugha chotara kwa mujibu Massamba (2008) anaeleza kuwa lugha chotara ni lugha ambayo hutokana na mchanganyiko wa lugha mbili au zaidi.

                                                          
Kwa ujumla lugha chotara ni lugha ambayo hutokana na mchanganyiko wa lugha mbili au zaidi mfano lugha ya Kingereza ikiungana na lugha ya Kijerumani tunapata lugha chotara vilevile lugha za Kibantu zikiungana na lugha ya Kiarabu huzaliwa lugha chotara.

Dhana ya kuwa Kiswahili ni lugha chotara imezua mjadala mrefu wa kitaaluma kwani hata baadhi ya wazawa wamejinasibisha na Uarabu au Ushirazi kwa sura na lugha yao. Wanaona fasili ya Kiswahili ni lugha chotara na wanadai kuwa Kiswahili kimetokana na mchanganyiko wa lugha ya Kiarabu na lugha za Kibantu. Hivyo waswahili ni watu waliotokana na wanaume wa Kiarabu na wanawake wa Kibantu. Mfano wataalamu waliojinasilbisha na Uarabu au Ushirazi ni spamoja Alamin Mazrui na Ibrahim Noor Sharif.

Wataalamu mbalimbali wamejadili dhana ya kukiona Kiswahili kama lugha chotara kwa kugawanyika katika makundi mawili. Kwanza ni wale wanaoona kuwa Kiswahili kilianza kama lugha chotara iliyotokana na wanaume wa Kiarabu na wanawake wa pwani baada ya muingiliano kati yao. Kundi la pili wanaamini kuwa Kiswahili kilianza kama pijini ya Kiarabu kwa kiasi kikubwa na lugha ya Kibantu kwa kiasi kidogo. Miongoni mwa wataalamu wanaoamini kuwa Kiswahili ni lugha chotara kwa kutokana na muingiliano kati ya wanaume wa Kiarabu na wanawake wa pwani ya Afrika Mashariki ni hawa wafuatao: Freeman Grenville (1959), Gray (1962) na Homo Sasson (1980).

Freeman Grenville (1959) aliandika makala iitwayo Medieval Evidence for Swahili. Kwa kiasi kikubwa mawazo yaliyopo katika Makala hiyo aliyachota katika kitabu kiitwacho Periplus of the Eritrean Sea. Freeman anaelezea kuhusu watu wa Rhapta ambao wanapatikana karibu na mto Pangani. Anasema “Watu wa Muza huwatoza ushuru na kupeleka huko meli ndogo. Meli ndogo nyingi zilikua na manahodha wa Kiarabu na mawakala wao, hawa wanawafahamu vizuri wakazi wa maeneo haya ya Muza na wanaishi na kuoana nao, na wanaijua lugha yao yote…” Katika maelezo haya tunaona kwamba Kiswahili ni lugha chotara ambayo ilianza mara baada ya ujio wa Waarabu katika maeneo ya pwani na kuingiliana na wanawake wa maeneo hayo. Hata hivyo mtazamo wa mtaalamu huyu una madhaifu mengi. Kwanza kama hao Waarabu waliifahamu lugha ya watu wa pwani, kwanini tena ilizaliwa lugha chotara? Pili hiyo lugha ya watu wa pwani waliyoifahamu ni ipi?

Mtaalamu mwingine niGray (1962) katika Makala yake naye alichota mawazo mengi kutoka kwenye Periplus of the Sea mtazamo wake unapishana kidogo na ule wa Freeman. Yeye anaona kwamba mswahili na lugha yake ni matokeo ya muingiliano kati ya Waarabu na watu wa pwani. Anasema “Yaelekea wafanya biashara na mabaharia wa Kiarabu walikua na mazoea ya kuweka makazi ya muda au ya kudumu katika sehemu mbalimbali za pwani na visiwa vinavyokaribiana navyo…” Kutokana na kauli hii anaeleza kwamba lugha ya Kiswahili ni mchanganyiko wa lugha mbili yaani ya baba ambaye ni Muarabu na mama ambaye ni makabila ya pwani.Mtanzamo huu unamapungufu kwani Mswahili si lazima awe mtu aliyezaliwa na baba mwarabu na mama aliyetokea maeneo ya pwani.

Matalamu mwingine ni Homo Sassoon (1980) katika makala yake anaeleza kwamba “Pepo za kaskazi huvuma baina ya mwenzi wa 9 na 3, ambazo ndizo Waarabu walizozitumia kuja huku Afrika. Pepo za kusi ambazo ndizo walizozitumia kurudi kwao. Wafanyabiashara waliochelewa pepo za Kusi iliwarazimu wakae pwani kwa miezi 6. Katika kipindi hicho iliwalazimu kuwaoa wanawake wa Kibantu na hapo ndipo Kiswahili kikaanza…” Kwa maelezo haya tunaona kuwa Kisawahili ni lugha chotara iliyotokana na Wafanya biashara wa Kiarabu waliowaoa wanawake wa Kibantu. Sassoon anafafanua kuhusu swala la kuoana anasema kwamba “Ardhi ya pwani ina rutuba nyingi na maisha yake yanavutia haikuwa taabu kwa Waarabu kukaa pwani kwa miaka michache hasa kama wangepata wasichana wa Kibantu ambao ndio walikuwa wenyeji wao. Bila shaka lugha ya Kiswahili ilianza kutokana na muingiliano wa aina hii.” Hata hivyo jina lenyewe linatokana na neno la Kiarabu “Sahil” (umoja) na wingi wake ni”Sawahil” ikiwa na maana ya pwani.

Hivyo anahitimisha kwa kusema kuwa asilimia 80 ya maneno ya Kiswahili yanatokana na lugha za Kibantu ambayo ndiyo lugha ya mama na watoto, asilimia 20 inatokana na lugha ya Kiarabu ambayo ni lugha ya baba na ya biashara ikiwa inajaza mapengo pale ambapo maneno ya Kibantu hayatoshelezi au hayakuwepo kabisa. Udhaifu wa matazamo huu ni kwamba kama lugha ya Kibantu ina asilimia 80 na Kiarabu 20, kwahiyo lugha ya Kiswahili haina msamiati wowote wa Lugha nyingine? Pia wakati wa ujio wa Waarabu lugha ya mawasilisiliano ilikua lugha gani chotara au Kiarabu?

Waumini wanaoamini kuwa Kiswahili kilianza kama pijini ya Kiarabu kwa kiasi kikubwa na lugha za Kibantu kwa kiasi kidogo hudai kuwa Kiswahili ni pijini ambayo huzaliwa kutokana na kukutanika kwa makundi mawili tofauti yanayo tumia lugha mbili tofauti. Ili makundi haya yaweze kuwasiliana kunaundwa lugha ambayo kitabia ni tofauti na zile zinazozungumzwa na makundi yanayohusika.  Lugha hii inaweza kuwa na msamiati mwingi kutoka lugha kati ya zile mbili au inaweza kuwa na msamiati wenye uzito sawa. Lugha hiyo ndiyo inaitwa pijini, mazingira yanayosababisha kuwepo kwa pijini nikama vile biashara, utumwa, na ukoloni, kwa mantiki ya nadharia hii, waumini hawa hukiona Kiswahili kuwa kilianza kama pijini kwani ni tokeo la mwingiliano baina ya wenyeji wa pwani ya Afrika Mashariki na Waarabu. Aidha husisitiza kuwa lugha ya Kiswahili haikuwepo kabla ya hapo.

Udhaifu wa nadhalia hii ni kwamba, hutumia kigezo cha msamiati tu bila kuzingatia vipemgele vingine vya lugha kama vile matamshi, maumbo ya maneno, au muundo wa sentensi. Vilevile wanadai kwamba Kiswahili hakikuwepo kabla ya hapo ila hawajaonesha ni lugha gani ilizungumzwa kabla ya ujio wao.

Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kwamba Kiswahili sio lugha chotara bali asili yake ni lugha za Kibantu, kutokana na vipengele mbalimbali vinavyotumika katika kuthibitishakuwa Kiswahili asili yake ni lugha za Kibantu, ambavyo ni ushaidi wa kiisimu na ushahidi wa kihistoria.













MAREJELEO
Freeman. G. (1959) Medieval Evidences for Swahili
Gray (1962) History of Zanzibar from Middle Age
Homo. S (1980) The Coastal Town of Jumba la Mtwana
Massamba, P. B. (2008). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha: Dar es salaam TUKI.
Sapir,E. (1921:7) Language: An Introduction to the study of Speech, New 
 York; Harcout Brace a Company Publishers 1921.
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu,Dar es Salaam:Oxford University   Press

Www.petermwiza.blogsport.co.id/ 2014 Nadharia mbalimbali kuhusu historia ya Kiswahili.

1 comment:

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny