Flower
Flower

Monday, January 29, 2018

MUINGILIANO WA FONIMU NA UJOZI PEKEE

Katika kujibu swali hili tumeligawa katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza tumefafanua istilahi muhimu zinazojitokeza katika swali, sehemu ya pili kiini cha swali ambapo tumefafanua dhana mbalimbali na mwisho ni hitimisho.

Kwa mujibu wa Hartman (1972) akinukuliwa na Mgullu anafasili fonolojia kuwa ni mtaala wa sauti zinazotumiwa katika lugha fulani na uamilifu wao ndani ya mfumo wa lugha inayohusika.
Nae Fudge (1973) anafasili fonolojia kuwa ni kiwango kimoja wapo cha lugha Fulani kilicho na vipashio vidogo zaidi kuliko vipashio vingine vyote vya lugha. Anaendelea kusema kuwa vipashio vya kifonolojia ni fonimu na alofoni zake.

TUKI (2013) wanafasili fonolojia kuwa ni tawi la isimu ambalo hushughulikia uchunguzi, uchambuzi, na uainishaji wa mfumo wa sauti pambanuzi katika lugha mahususi.
Halikadhalika Massamba (2012) anafasili fonolojia kuwa ni tawi laisimu linalojishughulisha na kuchunguza mifumo ya lugha mbalimbali za binadamu. Anaendelea kusema kuwa maelezo haya yana maana kwamba kila lugha ya binadamu ina mfumo wake wa sauti ambao huongoza ujenzi wa maneno ya lugha hiyo.

Kwa ujumla fonolojia ni tawi la Isimu linalojishughulisha na ujifunzaji wa mfumo wa sauti za lugha maalumu asilia. Huangalia jinsi sauti zinavyotumika katika maneno ya lugha maalumu ili kuleta maana. Hivyo huangalia muundo na uamilifu wa sauti hizo katika mfumo wa lugha maalumu kwani kila lugha ina mfuatano wake wa sauti katika kuunda maneno yake. Kwa hiyo, kila lugha ina fonolojia yake ingawa kuna sifa chache zinazofanana, na hii hutokana na kwamba lugha zote huchota sauti toka bohari moja la sauti.

Wataalamu mbalimbali wamejadili maana ya fonimu, Trubertzkoy (1939) kama anavyonukuliwa na Massamba anasema fonimu ni jumla ya sifa za sauti zilizo na umuhimu wa kifonolojia. Yaani upambanuzi wake wa kutofautisha maana katika lugha au mfumo husika.

De Courtney (1952) akinukuliwa na Mgullu (1952:53) anasema fonimu ni kipande sauti ambacho picha yake huwa akilini mwa mtu ambayo hukusudia aitoe wakati anaongea.
Massamba (2004) fonimu ni kipande kidogo kabisa katika mfumo wa sauti za lugha ambacho kina sifa pambanuzi kuweza kutofautisha na vipande vingine vya aina yake.

TUKI (2013) Fonimu sarufi tamshi katika neno ambalo likibadilishwa na tamshi jingine maana ya neno hilo hubadilika au hupotoka katika lugha hiyo. Mfano: neno sabuni na zabuni hapa fonimu zinazotofautisha maana ni /s/ na /z/.

Pia watalamu mbalimbali wanafasili zana ya alofoni, Hartman (1972) anafasili alofoni kuwa ni sauti moja wapo miongoni mwa sauti kadhaa zinazoiwakilisha fonimu moja. Anaendelea kusema kuwa alofoni hutokea katika mazingira mahususi.

TUKI (2013) wanasema kuwa alofoni ni umbo jingine la fonimu ileile; kibadala cha fonimu kinachotokea kutokana na mazingira ya kiisimu bila kubadilisha maana. Mfano [ r ] na [ d ] ni alofoni za [ r ] katika mrefu na ndefu. Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa alofoni ni maumbo tofautitofauti zaidi ya moja yanayowakilisha fonimu moja. Mfano ulimi na ndimi.

Mwingiliano wa Kifonimu.  Bloch (1941) anaeleza kuwa mwingiliano wa kifonimu ni ile hali ambapo sauti moja inaweza kuwekwa katika kundi la fonimu fulani na wakati mwingine katika kundi la fonimu nyingine. Hii inamaanisha kuwa kifonetiki sauti moja inaweza kuonekana katika makundi mawili ya fonimu na kwamba hili ni jambo la kwaida sana katika lugha. Kuna aina mbili za mwingiliano wa fonimu, ambao ni mwingiliano nusu wa kifonimu na mwingiliano kamili wa kifonimu.

Mwingiliano nusu wa kifonimu. Kwa mujibu wa Bloch (1941) akinukuliwa na Massamba, Mwingiliano huu hutokea pale ambapo sauti moja inapotokea katika mazingira fulani ya kifonetiki ikahesabiwa kuwa ni alofoni ya fonimu fulani na sauti hiyo hiyo inapotokea katika mazingira mengine ya kifonetiki ikahesabiwa kuwa ni alofoni ya fonimu nyingine katika mazingira tofauti ya kifonetiki.  Kwa mfano sauti [K] katika mazingira A inakuwa alofoni ya Y na sauti hiyo hiyo [K] katika mazingira B inakuwa ni alofoni ya X. Katika mazingira haya  inakuwa ni sauti ya kundi fulani na ikiwa katika mazingira mengine inakuwa sauti ya kundi jingine la fonimu. Kwa mfano, katika lugha ya Kideni fonimu /t/ na  /d/ huonyesha tabia tofauti zinapotokea kama silabi za mwisho wa neno. Katika lugha hiyo /t/ ikitokea mwishoni mwa neno hutamkwa /d/, kwa mfano neno /hat/ linatamkwa /had/  “kofia”; lakini /d/ itokeapo mwishoni mwa neno hutamkwa  /ծ/, kwa mfano, neno /had/ hutamkwa [haծ] “chukia”. Lakini katika Kideni hicho hicho neno lenye maana ya “paa la nyumba” ni /tag/ na neno lenye maana ya “siku” ni /dag/. Hii maana yake ni kwamba fonimu zote mbili, yaani /t/ na /d/ zinapotokea mwanzoni silabi hazibadili maumbo yake lakini zinapotokea mwishoni hubadili maumbo yake. Hapa ni wazi kwamba kuna matokeo mawili ya sauti [d]; kuna [d] ambayo ni alofoni ya fonimu [t] na kuna [d] ambayo ni alofoni ya fonimu /d/. Mfano katika  lugha ya Kiswahili
Udogo                 ndogo
Udugu                 ndugu
Ulimi                   ndimi
Katika maneno haya tunaona pia kwamba kuna matokeo mawili tofauti ya sauti [d]. Wakati mwingine sauti [d] inajitokeza kama alofoni ya fonimu [d]  na wakati mwingine sauti hiyohiyo inajitokeza kama alofoni ya fonimu /l/ hujitokeza kama [d] inapokuwa imeandamiwa na konsonanti /n/.

Aina ya pili ni mwingiliano kamili wa kifonimu. Massamba ( 2012) anafafanua kuwa Mwingiliano huu  ni hali inayojitokeza wakati ambapo kunakuwa na mfuatano wa utokeaji wa sauti, katika mazingira yaleyale ya kifonetiki kisha sauti hiyo mara ikahesabiwa kuwa alofoni ya sauti fulani ya /A/ na mara ikahesabiwa kuwa alofoni ya sauti fulani ya /B/. Anaendelea kusema kuwa zingatia kwamba wakati katika mwingiliano nusu wa kifonimu mazingira ya kifonetiki huwa tofauti, katika mwingiliano kamili wa kifonimu mazingira ya kifonetiki huwa ni yale yale. Mfano, sauti /t/ na  /d/ kutoka katika lugha ya Kingereza cha Marekani baadhi ya wasemaji huzitamka kama kipigo cha ufizi /d/, katika maneno kama vile butter, betting, kitty, akiyakinzanishana na budden, bedding na kiddy. Katika mifano yote hii  fonimu /t/ na /d/ hutamkwa kwa namna moja, yaani /betting/- [beDiƞ] na /bedding/ - [beDiƞ]. Kwa hiyo kipigo cha ufizi [D] ni alofoni ya /t/ na ni alofoni ya /d/ katika mazingira yale yale.

Ujozipekee wa fonimu. Bloch (kaishatajwa) akinukuliwa na Massamba anasema Upekeejozi unamaanisha kuwa kila mkururo wa sauti pekee zinazoshabihiana huwakilisha mkururo wa fonimu pekee na kila mkururo wa fonimu pekee huwakilisha pia mkururo wa sauti pekee zinazoshabihiana. Hii ina maana kwamba sauti haziwezi kuingiliana kwani kila fonimu ina sifa zake pekee za kifonetiki ambazo kamwe haziwezi kuingiliana. Mfano irabu [o] na [ u]

[0] + irabu, + nyuma, + nusu juu, + mviringo.
 Irabu [u] ina sifa ya + irabu, + nyuma, + juu + mviringo

Hivyo katika sauti hizo tunaona kuwa sifa za kipekee uko katika mkao wa ulimi wakati wa utamkaji sauti [o] ulimi huwa nusu juu lakini [u] huwa juu.
Msambao kamilishani wa utokeaji wa alofoni. Massamba (2012) ni hali mbapo sauti mbili au zaidi hutokea katika mazingira ambayo kwayo sauti moja ikishatokea katika mazingira hayo basi ile au zile nyingine haziwezi kutokea hapohapo. Kwamfano, tuchukulie kwamba kuna sauti A na B, sauti A ikitokea mwanzoni au katikati basi sauti B haiwezi kutokea mwanzoni au katikati. Hyman (1975)  anaeleza kuwa kila sauti huwa na mazingira yake maalumu ambayo hayawezi
kakaliwa na sauti nyingine mfano katika lugha ya Kiingereza kuna sauti /Pʰ/  na /P/  isiyo na mpumuo ambapo tunaelezwa wazi kuwa sauti [Pʰ] utokea mwanzoni mwa neno tu kwamfano mneno /pin/, /pen/ na /put/. Kwa upande mwingine /P/ isiyo na mpumuo hutokea sehemu yoyote ya neno isipokuwa mwanzoni. /Pʰ/ na /P/ isiyokuwa na mpumuo ni alofoni za fonimu /p/, ambazo kila moja hutokea katika mazingira maalumu

Kwa kuhitimisha, fonolojia huwa na malengo mbalimbali, kutambua na kuolozesha sauti, kuchunguza mfuatano wa sauti, kuchunguza michakato ya kifonolojia inayotokana na sauti, na pia kuchunguza ruwaza za kiimbo.








MAREJELEO
Bloch, B. (1941). Phonemic  Overlapping. In American Speech 16 : 278 – 84. ( reprinted in Joos,
                              M.  1957 pp 93 – 96).
Fudge, E. C (1973). Phonology. Penguin Books.
Hyman (1975). Phonology: Theory and Analysis. Themsoy Learning. Amazon.
Massamba, D. P. B (2012). Misingi ya Fonolojia. Dar – es - Salaam: TATAKI
Mgullu, J. R (1990). Mtalaa wa Isimu. Longhorn. Nairobi.

TUKI (2013). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny